15  MADINA YAMPOKEA

673
Sasa hapa ikhiwani
Tumkumbuke Manani
Kwa mapenzi na Imani
Muumba wetu Jaliya

674
Baa'da dhiqi a'dhimu
Mateso mengi magumu
Ya kuteswa Isilamu
Muangaza waingiya

675
Kutokea Ans'ari
Kunus'uru wakakiri
Na Mtume kuhajiri
Ndio mwanzo waanziya

676
Ndio kusimama Dini
Ikaingia Imani
Kuenea A'rabuni
Na duniya yote piya

677
Ni Mola wetu Muweza
Haya yote kutengeza
Kutangaza muangaza
Kwa juhudi ya Nabiya

678
Siku kumi zikifika
Tangu Mtume kutoka
Mji wake huko Maka
Mwishowe aqurubiya

679
Wakakoga wakapanga
Kujisafisha michanga
Na uchafu wa kutanga
Kutanga na kukimbiya

680
Wakavaa abyadhi
Mtume anazo ridhi
Ndizo nguo zenye hadhi
Na zinazo mwelekeya

681
Huku mjini Madina
Ndugu zetu Waumina
Wana hamu kumuona
Mtume wamngojeya

682
Hata siku ile ile
Ya kuzawa Mteule
Akafika mji ule
Lakini hakuingiya

683
Alitua viungani
Ni qaribu na mjini
Maili mbili thineni
Hapo paitwa Qubaa

684
Alikaa apumuwa
Kipenzi chetu Rasuwa
Siku nne zilikuwa
Hata alipo tuliya

685
Kwa furah'a ya a'jabu
Kapokelewa H'abibu
Wanamwambia: Qaribu
Kwa nyimbo wampokeya

686
Watoto na kina mama
Kwa tungo na kwa magoma
Wampokea Hashima
Ni mno wafurahiya

687
Wakayapiga madufu
Kumpigia Sharifu
Na qas'ida za kus'ifu
Njema walo mtungiya

688
Basi wengine waona
Hata kupita sinina
Kwamba hiyo ndiyo Suna
Mtume kairidhiya

689
Kila mtu amtaka:
Kwangu mimi Bwana shuka
Ngamia atapo fika
Kajibu atashukiya

690
Huyu ngamia katumwa
Alinena hayo Tumwa
Hah'itaji kusukumwa
Ajua pa kufikiya

691
Kufika kwenye baiti
Ya mja mwenye bahati
Ngamia kapiga goti
Nyumba hiyo tawambiya

692
Kwa Bwana Abu Ayubu
Kashuka hapo H'abibu
Ni mmoja wa S'ah'abu
S'ahaba zake Nabiya

693
Akaketi Mukhtari
Qiasi saba shuhuri
Kwa Khalidi mashuhuri
Nyumbaye kuingojeya

694 Ngamia alipo keti
Palijengwa msikiti
Na hapo pia baiti
Ya Mtume kuhamiya

695
Na hebu hapa qalili
Turejee kwake A'li
Alo achwa kwa ajili
Amana kurejezeya

696
Alirejeza amana
Alo kuwa nazo Bwana
Kwisha hapo yeye tena
Mlimani alikweya

697
Akapanda akanadi
Yupo yeyote wah'edi
Alo mpa Muh'amadi
Naaje tamqidhiya

698
Zingatia ewe mja
Kama watafuta hoja
Kwenda mbali huna haja
Haya yat'osha kifaya

699
Wapi haya umeona
Mfano wa wetu Bwana
Kwenda rejeza amana
Kwa wale Majahiliya

700
A'dui walo chukuwa
Vyote vyao vilo kuwa
Wakawa warudishiwa
Amana walo mwachiya

701
Akamwacha wake ndugu
Wa kumwonea uchungu
Pekee na wake Mngu
Kurudisha alo pewa

702
Haya si wewe na mimi
Haya hufanya Mtumi
Hapa nisite usemi
Tupate kuendeleya

703
A'liy kwisha katoka
Kawacha mji wa Maka
Wa miguu kaushika
Madina kaelekeya

704
Akenda usiku wake
Mchana apumzike
Kujificha jua lake
Na a'dui Jahiliya

705
Akafika taa'bani
Kumuona hutamani
Majarah'a miguuni
Na kavimba mno ghaya

706
Tumwa kumuona nduye
Wacha amhurumiye
Tena amkumbatiye
Na dua' kumwombeya

707
Kampuliza madonda
Hapo hapo ikakonda
Miguu kama hajenda
Machofu yakapoteya

708
Na baa'dae mjini
Tumwa kwisha tamakani
Kawapanga Waumini
Wageni na wafikiwa

709
Kila mtu wake ndugu
Wa kupendana kiungu
Kwa matamu na machungu
Na ikhilas'i ya niya

710
Hao wote Ans'ari
Wawafanya Wahajiri
Kwa ndani na kwa dhahiri
Ni ndugu wa kuzaliwa

711
Kila mtu mkimbizi
Kapata ndugu mkazi
Na Simba wake Mwenyezi
Kamchukua Nabiya

712
Alimwambia Amini:
Wewe ndugu duniani
Na hata kesho Peponi
Siwezi kukuachiya

MAFUNZO:

Hebu natuwaze na kuzingatia vipi huwa pale mtu yupo katika kudhulumiwa na anaandaa kukimbia mateso, na mipango ya kuuliwa, wakati huo huo akafikiri kuwarudishia watu amana yao, na ilhali yeye na watu wake wote wamepokonywa kila kitu. Mafunzo kama haya na mifano kama hiyo ndiyo iliyo wafanya wengi walio dhulumiwa Zanzibar kuwafanyia hisani wale wale walio dhulumu. Malipo ni kwa Mwenyezi Mungu.