489
Maqureshi waliwaza
H'ija itapo chomoza
Na Mah'aji kujijaza
Khat'ari itazidiya
490
Khat'ari yake Amini
Kutangaza yake Dini
Kwa hawa watu wageni
Itatanda A'rabiya
491
Wakalita lao bunge
Mipango
Qabula ya kutokeya
492
Na humo hawakutani
Wa chini arubai'ni
Wa myaka hiyo yaqini
A'qili zisha tuliya
493
Wakazileta fikira
Za kila njia na s'ura
Mara hili, hili mara
Wawaza wakiwazua
494
Alitongoa fulani
Natuwatishe wageni
Kwamba hili ni kuhani
Hupoteza watu njiya
495
Walidi bin Mughira
Mwenye rai zilo bora
Hakubali ya kijura
Kabisa kuyasikiya
496
Akanena: Tuyapime
Yenye s'ura tuyaseme
Huyu mdai Utume
Kuhani hakwelekeya
497
Habanii kikuhani
Qauliye mbayani
Ni nani ataamini
Hayo tukimzuliya
498
Hapo mwengine kafiri
Katoa yake shauri:
Mimi naona uzuri
Kichaa kusingiziya
499
Walidi hakukubali
Kufwata hiyo qauli:
Hapana yote dalili
Ya wazimu kumwingiya
500
A'qili yake timamu
Wallahi hana wazimu
Na anaye mshutumu
Ni yeye kaingiliwa
501
Mambo yakawa ni kawi
Walinenalo haliwi
Tunene: Basi mchawi
Mwengine kajisemeya
502
Hayo pia hakuridhi
Walidi mtaa'radhi
Na wangapenda baa'dhi
Hapo walo hudhuriya
503
Ni mazingaombwe gani
Aliyo leta Amini
Hata tuweze kubuni
Uchawi kumtusiya
504
Waliqaribia h'adi
Kushindwa na Muh'amadi
Wakamwambia Walidi:
Twambie twakungojeya
505
Sisi kukwondolea mbeko
Hilo jambo kwetu mwiko
Twambie fikira zako
Mwenye rai zilo tuwa
506
Walidi hapo kanena:
Tuzue lenye maa'na
Ambalo linafanana
Na kweli laelekeya
507
Tuwambie maqaumi:
Huyu mdai Utumi
Ni mtamu wa ulimi
Mzuri wa kutongoa
508
Akitamka qauli
Huzivuruga a'qili
La urongo huwa kweli
Na kichwa huwa mkiya
509
Msimwache kutamka
Neno lake mkashika
H'ata ikiwa ataka
Khat'ari kumsikiya
510
Wote walio kutana
Wakawa wamepatana
Kufwata aliyo nena
Walidi alo wambiya
511
H'ata siku ikifika
Kila njia wakaweka
Mtu watu kuwashika
Haya kuwaelezeya:
512
Jamani nawambiani
Kuna kiumbe mjini
Amezua yake Dini
Na yetu aiumbua
513
Ni mtamu wa kusema
Lakini si mtu mwema
Msirogwe kusimama
Na anga kulinganiya
514
Lau kama ni mkweli
Tungeli kuwa awali
Diniye kuikubali
Kwa maana twamjua
515
Akitaka wasemeza
Ni bora kumfukuza
Hivyo shari mwaiviza
Isije kuwafikiya
516
Mah'aji wakiwas'ili
Katoka wetu Rasuli
Akenda kuwaqabili
Dini kuwakhubiriya
517
Lakini yalo mkuta
Ni mengi mno matata
Watu wote wamsuta
Hawataki msikiya
518
Hujiziba masikio
Hujigubika maguo
Ikawa ni mizomeo
Na mayowe kupigiya
519
Ni haya si mara moja
Kila msimu wa H'ija
Huzuka hivi viroja
Na mengi ya kuzidiya
520
Na mkubwa wa adhabu
Ni huyo Abu Lahabu
Humuandama H'abibu
Kila anapo endeya
521
Hufwata kumkashifu
Mtume wetu Sharifu
Kwa ulimiwe mchafu
Mwana wa kuangamiya
522
Hata myaka ikijiri
Mwaka wa hadi a'shari
Aliona Mukhtari
Wageni akawendeya
523
Ni wageni wa Madina
Watua wanda wa Mina
Mtume akiwaona
Kaanza wakhubiriya
524
Kawaeleza ya Dini
Akasoma Qur'ani
Na wote wakaamini
Na hapo washuhudiya
525
Nao wote watu sita
Mtume wakamfwata
Waa'hidi kutafuta
Wenzao kuwandamiya
526
Waa'hidi wawezao
Kuongoza wenzi wao
Wajue lilio ndio
Waongoke kwa hidaya
527
Kupita myezi miwili
Si haba walo kubali
Kumfuwata Rasuli
Kwa yale walo sikiya
528
Wakautuma ujumbe
Kwa Mtume umuombe
Mpini watie jembe
Kazi wapate anziya
529
Wamtaka Mua'dhamu
Ampeleke mwalimu
Awafunze Usilamu
Kila nyumba kupitiya
530
Akawatuma wawili
S'ah'aba zake wa kweli
Kuongoza ya Jalali
Njia isiyo khat'iya
531
Qiasi kufika mwaka
Mji wote waongoka
Ni wengi walo itika
Wachache walo saliya
532
Na h'ata siku za H'ija
Ujumbe nao ukaja
Hii mara afuwaja
H'isabu tawatajiya
533
Khamsa wa sabii'ni
Na wote walo amini
Na wawili niswani
Kati ya wao rijaa
534
Wakapeana mia'di
Huko nje ya biladi
Siku yao ya kurudi
Usiku ukiingiya
535
Ilipo kaza laili
Mtume aliwas'ili
Huko nyuma ya jabali
Na wao wamngojeya
536
Akaweka asikari
A'li na Abubakari
Waangalie hadhari
Pasiwe wa kusikiya
537
Kwisha kuamkiana
Hapo Mtume kanena
Kuwaidhi Waumina
Nas'aha kawatoleya
538
Kawaeleza ya Dini
Akasoma Qur'ani
Khitilafu kabaini
Za Dini na jahiliya
539
Na tena akauliza
Kama wao wataweza
Ulinzi kuutengeza
Kwa watao waendeya
540
Kasema Bin Maa'ruri:
Sisi sote tu tayari
Wakazuka Ans'ari
Kumua'hidi Nabiya
541
Ulipo kwisha usemi
Ni A'basi wake a'mi
Alosema: Langu mimi
Ninalo la kuwambiya
542
Kwenu nyinyi nat'ulubu
Mtaziweza h'arubu
Maa'dui Waa'rabu
Watapo washambuliya?
543
Mkiwa mtamtupa
Mwenetu mwacheni hapa
Tena hao wakaapa
Wakifa wafe pamoya
544
A'basi wakati huo
Ukafiri anga nao
Ni uchungu alo nao
Wa mwana ndio kajiya
MAFUNZO:
Kikulacho kinguoni mwako, chambilecho Waswahili. Wa kwanza kumpinga Mtume s.a.w. alikuwa ami yake Abu Lahab. Lakini vile vile ni ami zake wengine walio muunga mkono hata kabla ya kuwa Waislamu. Kama Hamza na Abu T'alib na Abbas. Na hapa tunaona vipi kwa utaratibu na kuvumilia na kuishika kamba bila ya kuiachia Uislamu ulijengeka kidogo kidogo. Huu Uislamu ulio fika hivi leo, hata inakisiwa na Umoja wa Mataifa kuwa katika mwaka 2000 katika kila watu mia duniani, khamsini watakuwa ni Waislamu, Uislamu huu haukusimama mara moja. Ukiona kinaelea kimeundwa. Mwenye kupigania Haqi ya Mwenyezi Mungu asivunjike moyo. Ajue njia ya Ushindi ina miba na mizonge mingi.