Dibaji

ya Sheikh Ali Muhsin Al Barwani

Mambo mawili ndiyo yaliyo nipelekea kutunga utenzi huu juu ya maisha ya Mtume Muhammad s.a.w.

Kwanza: kuleta mukhtasari wa hadithi tamu na yenye mafunzo makubwa kama alivyoieleza marehemu Sheikh Abdulla Saleh Al Farsy - aliye kuwa Kadhi Mkuu wa Kenya, na kabla yake alikuwa wa Zanzibar - katika kitabu chake, Maisha ya Nabii Muhammad. Mukhtasari huo kwa kuwa ni kwa utenzi utaweza kuhifadhika na kuimbwa wanapo kutanika watu.

Pili: kutaka kushirikiana, kwa njia ya kiroho na kishairi, na misukosuko isiyo kuwa na mfano aliyo pambana nayo Mtume s.a.w. na Sahaba zake kiasi ya karne 14 zilizo pita, mpaka wakaweza kusimamisha mpango na mwenendo wa kila namna na sura usio na mithali duniani.    Mimi nimehisi pamoja na mtoto, Muhammad, huzuni za upweke kuzaliwa na kumkuta baba kesha kufa, na baada ya miaka michache mama naye akakhitariwa.    Nimeuona, katika utungo huu, wasiwasi wa kuhamishwa mara kwa huyu mara kwa huyu, na kuwaona mmoja baada ya mmoja wa hao walinzi wake wanaifariki dunia.    Pamoja nae, Mtume s.a.w., nimepata pepesi za vituko vilivyo msibu alipo kuwa pekee katika pango la Hira akibebeshwa na Malaika Jibril mzigo wa kuuwokoa ulimwengu.    Pamoja naye nilisherehekea furaha kubwa ya kupata kuaminiwa na vipenzi vyake ambao walikuwa wanamjua undani wake kabisa. Hao ndio Waislamu wa kwanza: Khadija, mkewe; Ali, binami yake; Baraka, mama aliyemlea tangu utoto; Zaid, mwanawe wa kumlea; na Abubakar, rafiki yake wa chanda na pete.

Nimemiminika machozi nilipo kuwa natunga beti za T'aif, alipo aziriwa, na kupopolewa mawe na madongo yeye na mwenzie Zaid, na huku wanachururika madamu tangu utosini mpaka nyayoni, na huku wahuni wakiwazomea.    Huzuni ilioje niliyo kuwa nayo huku nikitunga beti juu ya mateso aliyo yapata Mtume s.a.w. na jamaa zake na sahaba zake walipo tolewa mji na kulazimika kuishi majangwani na hawana chakula  ila majani ya porini.    Yote hayo ni katika kutimiza waajibu wa kazi yake kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu.    Yalimpata hayo pamoja na kubeba mizigo ya kawaida ya binaadamu yeyote.    Aliishi Mtume Muhammad s.a.w. akaona wanawe wote, mmoja baada ya mmoja, wanakufa mbele ya macho yake. Ni mmoja tu, Fatma, ndiye aliye ishi baada yake, naye haikupita miezi 6 ila naye kafariki.

Miezi kadhaa wa kadhaa kabla ya kufikiri kukamata kalamu kutunga utenzi huu niliota ndoto nimo katika hijra, nahama Makka nikiendea Madina. Wenzangu safarini humo ni Sayyidna Uthman aliye kusanya Qur'ani kuwa Msahafu, na Ibn Hisham, maarufu aliye andika maisha ya Mtume s.a.w. yanayo itwa Assiratun Nabawiya.    Ilikuwa hiyo safari ya furaha kwa sababu tulikuwa tunatumai kukutana na Mtume s.a.w. huko Madina.    Labda ndoto hii ilikuwa ni dalili kuwa nitakuja tunga utenzi huu wa maisha ya Mtume s.a.w. na kutarjimu Al Muntakhab katika tafsiri ya Qur'ani Tukufu. Asaa haya yakanikurubisha katika macho ya Bwana wetu s.a.w.

Beti za vita vya Uhud zilinipa taabu kubwa kuzitunga; Mtume s.a.w. kapigwa na kapondwa pondwa kwa mawe na mishale hata akadhaniwa  amekwisha kufa.    Masahaba wake, na ami yake khasa, Hamza, amekatwa katwa.    Haya nilkuwa ninayaona kama kwamba nipo hapo hapo. Lakini mafunzo yaliyo patikana kwa kushindwa huko si haba kwa hao walio okoka wa zama hizo, na hata kwetu sisi wa leo kama tutasoma na kuzingatia yaliyo pita.

Tena ikaja furaha ya furaha; kufunguliwa mji wa Makka.    Baada ya miaka ya mzozano usio sita usiku wala mchana, kupigana na kila ovu,  Makka Takatifu, Ummul Quraa, Mama wa miji, ilifungua milango yake aingie maridhawa Bwana wa mabwana, ambaye mpaka hapo alikuwa akionekana kuwa ni mfukuzwa asiye takikana kuikanyaga ardhi ya Makka.    Muhammad anaingia kwa ushindi kapanda ngamia pamoja na mtoto mweusi, wa mama Muafrika na baba Mwaarabu, Usama mwana wa Zaid ambaye zamani naye alikuwa mtumwa! Hapo hapo Mtume kamtaka Bilali r.a. apande juu ya Al Kaaba aadhini. Huyo naye ni Muafrika mwengine.    Hayo yote ni kama kuyamathili mafunzo ya kimsingi ya hii Dini mpya aliyo kuja nayo Muhammad. Na hapo akaitangaza kwa kauli yake:

" Enyi Maqureshi! Mwenyezi Mungu amekwisha kukuondosheeni jeuri za kijinga na kujitapa kwa ajili ya nasaba. Watu wote wanatokana na Adam, na Adam kaumbwa kwa udongo. Hana fadhila Mwaarabu juu ya asiye kuwa Mwaarabu,  wala mwekundu juu ya mweusi, wala mweupe juu ya mwekundu."

Wote hao walio mtenda kila ovu yeye na watu wake, aliwasamehe, wakawa huru.    Ukarimu ulioje huu! Fadhila ipi ilio kuu kuliko hii?

Kutoka kilele cha furaha kuu ya kushinda huko tukaangukia kizia kilicho tanda ulipo karibia msiba mkuu alipo kuwa Mtume s.a.w. anataka kuwaacha mkono Sahaba zake walio kuwa wakimpenda kuliko roho zao.    Nimeshiriki mimi katika khofu na huzuni hiyo.    Alipo kata roho na mimi ndani ya nafsi yangu nilihisi mgutuko, na machozi yakamwagika bila kizuizi na kilio cha kwikwi kilinitoka, kama kwamba kifo hicho kimetokea leo mbele ya macho yangu. Duni ya mwanamume na mwanamke katika Madina siku hiyo hakuacha kufanya hivyo na zaidi. Maliwaza yetu ni kumsoma na kumsoma tena na tena Bwana huyu - si kila mwaka mara moja, wala si kila siku saba, bali kila siku na kila wakati - na kujaribu kumuiga kwa mwendo wake na tabia zake.

Ali Muhsin Al Barwani
P.O. Box 10679
Dubai, U.A.E.
11 Ramadhan 1417
19 Januari 1997