213
Bwana Mungu alifunza
Watu gani wa kuanza
Isije kuwa ni chonza
Wengine kuwaanziya
214
Aanzie ikhwani
Na wapenzi na wendani
Wa rikale na wa chini
Si watu ajinabiya
215
Kaambiwa Bi Khadija
Hakusita mara moja
K awashinda wote waja
Kums'adiqi Nabiya
216
Bibi huyu mtukufu
Kaongoza uwongofu
Tukafuata uluufu
Na sote twamwandamiya
217
Ameanza kwa baraka
Baraka isiyo shaka
Dini hii kutukuka
Bi Khadija kaanziya
218
Tumeona Isilamu
Wametushinda h'uramu
Kumwitika Mua'dhamu
Ni wao watanguliya
219
Ndio hivyo hii Dini
Hutukuza niswani
Tangu hapa duniani
Na Akhera kuingiya
220
Ndio wao wa kulindwa
Ndio wao wa kupendwa
Ndio wao wa kutendwa
Kwa huruma na muruwa
221
Siku ile wakis'ali
Bi Khadija na Rasuli
Kawaona Bwana A'li
Akabaki ashangaa
222
Kanena: Mwafanya nini?
I'bada hii ni gani?
Sijaonapo zamani
Nijuvye nipate juwa
223
Na huyo Sidi A'lii
Bado mtoto s'abii
Myaka kumi hapitii
Bin A'mi wa Nabiya
224
Mtume akabaini:
Ni i'bada ya Manani
Katufunza hii Dini
Tufwate nakuus'iya
225
Kijana akadhukuri
Nenda baba kushauri
Na yeye atapo kiri
Nitakuja kufwatiya
226
Mtume hakuyapenda
Hayo mtoto kutenda
Haneni mwenye kuunda
H'adi mambo kutimiya
227
Akamwambia: Fikiri
Kata mwenyewe shauri
Ukiona ndiyo kheri
Ni mwenyewe a'zimiya
228
Usiku katika kiza
Mtoto alikiwaza
Akaona muangaza
Wamuonyesha ya Njiya
229
Akaona kwa yaqini
Kuwa hii ndiyo Dini
Kakaye kamuamini
Kuwa kweli ni Nabiya
230
Qiasi kupambazuka
Mbee za Tumwa kafika
Uso wake unawaka
Kwa nuru ilo mwingiya
231
Akamwambia Amini:
Nashuhudia Manani
Na wewe nakuamini
Wewe kweli ni Rasuwa
232
Basi huyu Bwana A'li
Ni Isilamu wa pili
Kwa vijana ni awali
Ni yeye katanguliya
233
Mngu kampa wajihi
Uso kuwa mshabahi
Kumwelekea Ilahi
Tangu utoto s'abiya
234
Uso wake hapo tangu
Umetukuzwa na Mngu
Hakuijua miungu
Ya watu wa jahiliya
235
Ndugu huyu etwa Simba
Asiye jua ruu'ba
Ndiye mwingi wa mah'aba
Kwa Isilamu jamiya
236
Ndiye huyu ni Imamu
Na Mlango wa I'limu
Ni ndugu wa Mua'dhamu
Mkonowe wa kuliya
237
Siku alio kubali
Kusilimu Bwana A'li
Alisilimu wa pili
Mtume alo mleya
238
Wa kulelewa waladi
Nyumbani kwa Muh'amadi
Jinale etwa Zaidi
Na mkewe kafwatiya
239
Mkewe etwa Baraka
Mlezi wa Rasulaka
Baraka Muafirika
Yuko mbele nakwambiya
240
Zingatia utukufu
Kuupata uwongofu
Siku hiyo ya sharafu
Ni siku ya kuanziya
241
Si ajabu hapo basi
Kuvikwa njema libasi
Wote walio weusi
Kutukuzwa na Nabiya
242
Baraka ndiye mamaye
Na Zaidi ni mwanaye
Akamwoza dadaye
Mwanamke Qureshiya
243
Mtume wetu kanena:
Qabila hapana tena
Kuja mtu kujivuna
Na watu kuwaoneya
244
Hapana aliye bora
Kwa ngozi yake kung'ara
Rangi zetu si ishara
Kutukuka kwa Jaliya
245
Mtu yake ni a'mali
Aipendayo Jalali
Kufaulu na kufeli
Mwenyewe kujitendeya
246
Na mambo hayo kujiri
Bwana wetu Bubakari
Alikuwa kasafiri
Yamani ndio kendeya
247
Siku tatu zilipita
Tangu Utume kupata
Hakusita kuja fwata
Mara akiwas'iliya
248
Alipo pata khabari
Kwa mwenyewe Mukhtari
Hapo hapo alikiri
Na hapo kashuhudiya
249
Huyu ni wake rafiqi
Abubakari S'adiqi
Mtetea kila h'aqi
Mwenye s'afi yake niya
250
Tangu wao utotoni
Bubakari na Amini
Walikuwa ni wendani
Waso kuwa na mithaa
251
Hapana wa kuwashinda
Kwa mapenzi ya kupenda
Mfano pete na chanda
Daima wako pamoya
252
Walio silimu naye
Ni mtukufu mamaye
Na pamoja na mwenziye
Mkewe na wana piya
253
Wengine walo amini
A'thumani wa A'fani
Mzalendo Liwat'ani
Kati ya Bani Umeya
254
S'ifa zake ni tukufu
Mwendo wake ni mwongofu
Watu wote huzisifu
Rai zake na t'abiya
255
Alitoa yake mali
Ovyo bila ya kujali
Kwa ajili ya Rasuli
Na Mola wake Jaliya
256
Watumwa na waungwana
Walio mfuata Bwana
Sitoweza kuwanena
Kwa majina moya moya
257
Walikuwa si qalili
Wabora wenye a'qili
Lakini hao juhali
Ni wengi wa kupitiya
258
Kwa hivyo walo amini
Walifanya chini chini
Kutangaza yao Dini
Na huku wakikhofiya
259
Kila mtu Muumini
Hukhubiri kwa wendani
Au sema ikhiwani
Ambao wamsikiya
260
Na wakifanya i'bada
Hutoka nje bai'da
Walikitenda kwa shida
Hawakuwa na h'uriya
261
Walipo gundulikana
Kwamba huko wakutana
Wakaacha hapo tena
Majangwani kujendeya
262
Ikawa tena dharuri
Nyumbani kujisitiri
Ikawa kisirisiri
Wakutanika jamiya
263
Ndugu hao Isilamu
Walio shika khat'amu
Nyumbani kwa Arqamu
Ndiko wakikutaniya
264
Huingia mbali mbali
Kwa vikundi ni muh'ali
Wasiwaone juhali
Wakaja washambuliya
265
Muda wa myaka mitatu
Wakijificha kwa watu
Hapana alo thubutu
Nje kujitangaziya
266
Jambo kuu ukiwaza
Ifwate hii ruwaza
Usiwe kulieneza
Ila kwa mbinu na njiya
MAFUNZO:
Tunaona, basi, kuwa Dini hii ya
Islamu tangu mwanzo ni Dini ya watu wote, wanaume na wanawake, watoto na watu
wazima, matajiri na masikini, watu wa kabila zote. Tangu siku ya kwanza
walikuwamo Waafrika. Kwa Muafrika hii ndiyo Dini yake ya jadi.