163
Mtume tangu udogo
Akichukia urongo
Mas'anamu ya udongo
Huwaje kusujudiya
164
Vitendo vy a kikafiri
Vikimuudhi kathiri
Na kila akifikiri
Huzidi kuvichukiya
165
Akiona uqatili
Watendavyo majahili
Kuwazika at'ifali
Watoto kuwafukiya
166
Akiona majeuri
Watenda watu qahari
Hushindwa na kus'ubiri
Na kuweza vumiliya
167
Akiona na ulevi
Na unyang'anyi na wivi
Hunena huwaje hivi
Watu wakajitendeya
168
Akiona h'asharati
Wanaume na banati
Humkauka s'auti
Qauli humpoteya
169
Na u'mri ukizidi
Bwana wetu Muh'amadi
Chuki yake yashitadi
Kuchukia maa's'iya
170
Akionea huruma
Mpotofu wake umma
Akaungana na chama
Cha dhuluma kuzuiya
171
Chama hichi ni cha
kheri
Kazua A'mi Zuberi
Akangia Mukhtari
Na mno kafurahiya
172
Lakini hakikut'osha
Watu wake kuamsha
Maovu kuyakomesha
Wanyonge kupiganiya
173
Na mambo yakimzidi
Hutoka nje H'amadi
Huacha mji bai'di
Pekee hujitokeya
174
Hwenda huko majangwani
Kangia ndani pangoni
Kimwelekea Manani
Kuwaza na kus'aliya
175
Mambo akiyadabiri
Hawezi kuyas'awiri
Atendeje Mukhtari
Na mambo yamuemeya
176
Akiwa hivyo Amini
U'mri arubaini
Na mwezi wa Ramadhani
Vituko vyamtukiya
177
Kamuona hapo mbele
Kasimama mtu pale
Atamka kwa kelele:
Soma alivyo mwambiya
178
Sijui soma kajibu
Mtu akaja qaribu
Akambana H'abibu
Mayowe ampigiya
179
Kawa hivyo mara tatu
Atendavyo huyo mtu
Amshika Bwana wetu
Ni kama amkemeya
180
Tena hapo katamka
Aya zisiyo na shaka
Iqra Bismi Rabbika
Mtume akafwatiya
181
Tas'awari haya basi
Tusiwe na wasiwasi
Tuyajue sote nasi
Yafaa kuzingatiya
182
Jambo lake la awali
Alilo tumwa Rasuli
Si S'aumu si Kus'ali
Si Zaka kujitoleya
183
Hakuambiwa Kuh'iji
Watumwa kuwafariji
Hakwambiwa kunywa maji
Na tembo kulisusiya
184
Hakuus'iwa kwa mama
Na wana kuwatazama
Aliambiwa: Kusoma
Ndilo alilo anziya
185
Qauli yake awali
Alo itoa Jalali
Mja kwanza kuratili
Kusoma ni kuanziya
186
Mwenyezi Mungu Mwalimu
Kajipa bora isimu
Ni Mfunzi
kwa qalamu
Kupinga ujahiliya
187
Muu'jiza wa kusoma
Ni a'jabu ya daima
Washinda ile ya zama
Zamani zilo pitiya
188
Fimbo kuja kuwa nyoka
Na moto ukazimika
Na watu wakafufuka
Ni h'adithi twasikiya
189
Lakini ya kuyaona
Si maneno ya kunena
Ni hayo ya wetu Bwana
Milele twayangaliya
190
Muu'jiza wa qalamu
Ndio huu wa kudumu
Qur'ani ilo timu
Daima itasaliya
191
Enzi mpya imefika
Ya i'limu kuinuka
Hii Ishara h'aqiqa
Tuone na kusikiya
192
Mtume kwisha kwitika
Mtu yule katoweka
Endako au kutoka
Mtume kwamuemeya
193
Akaondoka Sharifu
Na moyo wajaa khofu
Kizengea takhafifu
Nyumbani akarejeya
194
Bi Khadija kutazama
Akadhani ana homa
Akamfunika vyema
Mumewe alo mjiya
195
Akawa awaweseka
Hajui ano tamka
Hata joto likishuka
Mtume kasimuliya
196
Bibi huyu mbas'iri
Kupata yote khabari
Kamtuza Mukhtari
Akamwambia: Tuliya
197
Lolote lenye madhara
Sidhani litakudara
Hujapata hata mara
Maovu kututendeya
198
Tangu wako utotoni
Wajulikana Amini
Wanyonge na masikini
Daima wahurumiya
199
Ni yaqini Maulaya
Hatokutenda vibaya
Tauliza yote haya
Kwa ndu yangu tamwendeya
200
Ndugu yangu Bunu A'mu
Waraqa mtaa'lamu
Anazo jua i'limu
Za vitabu samawiya
201
Waraqa ni Mnas'ara
Masih'i mwenye imara
Akasema: Aje mara
Nataka kumsikiya
202
Muh'amadi akafika
Kaeleza yalo zuka
Kaambiwa: Malaika
Ndiye aliye kujiya
203
Ni Roho Mtakatifu
Huwajia watukufu
Kawajia wa salafu
Na wewe umefwatiya
204
Kamjia Nabii Musa
Na pia Nabii I'sa
Na wewe ni hivi sasa
Ndiwe alo kutokeya
205
Sasa wewe Mukhtari
Ni Mtume jibashiri
Mola wetu kakhiari
Uongoze watu Njiya
206
Natamani aniweke
Mola wangu nikwitike
Dini yako niishike
Kwa mkono wa kuliya
207
Mtume wetu wa shani
Kajaa hapo Imani
Akaa'zimu pangoni
Atakwenda kurejeya
208
Alitamani Rasuli
Tena Molawe Jalali
Amtume Jibrili
Apate kumsikiya
209
Apate pata maneno
Ya utamu mwingi mno
Yaso andikwa kwa wino
Ya Mola kumshukiya
210
Siku chache si kathiri
Ikashuka Muddathiri
Kaambiwa as'ubiri
Kwa dhiqi zitomjiya
211
Kaambiwa abashiri
Kua'budiwa Qahari
Jinale alikabiri
Na watu kuwelezeya
212
Naye Mbashiri bora
Hakuruka kwa papara
Aliirai bus'ara
Na njia za kupitiya
MAFUNZO:
Mwenyezi Mungu humpa utukufu
amtakaye, lakini utukufu ni jukumu vile vile. Na mtu
hupewa huo utukufu akiwa ni mwenye kustahiki, naye
akatambua jukumu lilio juu yake. Tunaona hapo vipi Bwana wetu Muhammad s.a.w.
alivyo uchukua utukufu wa Unabii, na mzigo ulio
ambatana nao. Na kadhaalika Makhalifa walio kuwa waongofu.
Ama hao ambao walio pewa utukufu wakaona wastarehe nao utukufu, wakaghafilika na jukumu linalo ambatana na utukufu na uwongozi, wamefeli
na wamefedheheka. Pia hapa tunajifunza vipi sisi Waislamu inatupasa kuwatukuza
wake zetu. Mke mwema ni kama huyo Bi Khadija alivyo kuwa kwa
mumewe, Mtume s.a.w. Na kama alivyo kuwa Mwana Fatma binti Rasuli Llahi kwa
mumewe Sayyidna Ali, Mwenyezi Mungu, awape amani na radhi zake. Wazungu wana
usemi: Nyuma ya kila mwanamume mkubwa yupo mwanamke mkubwa.