10  UPINZANI UNAZIDI

393
Wafwasi wake Rasuli
Hao ni watu qalili
Kwa i'dadi ni dhalili
Kwa moyo washinda piya

394
Kwa hayo yaliyo zuka
Kwa makafiri wa Maka
Chuki yao ilifoka
Na khofu ikawingiya

395
Wakaita mkutano
Watafuta mapatano
Walikate moja neno
La kuondoa udhiya

396
Na hapo wakakhut'ubu:
Sikiza Abu T'alibu
Hili kwako twat'ulubu
Twataka uturidhiya

397
Sisi twaona ni bora
Tukupe huyu U'mara
Ni kijana wa imara
Mzuri kumwangaliya

398
Nawe utupe mwanao
Tumtende tutakao
Yaondoke maudhio
Kwakowe na sote piya

399
Utupe tumqatili
Ajidaiye Rasuli
Wewe upate badali
U'mara awe fidiya

400
Abu T'alibu kanena:
Mambo haya sijaona
Nimtunze wenu mwana
Kwa kila s'ura na njiya!

401
Wangu mimi nikupeni
Mumwondoe duniani!
Watu nyinyi watu gani
Msoweza zingatiya?

402
Siradhi tena siradhi
Liliwele ni faradhi
Mtakayo sitoridhi
Wala sito yaridhiya

403
Wana wote wa Hashimu
Na nduzao mah'ashumu
Walijiunga qaumu
Kwa haya yalo tokeya

404
Maqureshi wakakata
Watu hao kuwakata
Wasusiwe katakata
Pasiwe pa kupitiya

405
Wasiwe na la kusema
Ikawapasa kuhama
Kwani wote hao umma
Wamekwisha wagomeya

406
Wakaondoka mjini
Kwenda huko mabondeni
Wakawa wala majani
Chakula kimewishiya

407
Wachache kati ya waja
Wenye mbinu na viroja
Hupeleka mahitaja
Kwa kuwa wahurumiya

408
Na hao ziliwas'ibu
Dhiqi nyingi za h'arubu
Shida nyingi na taabu
Hapana pa kupitiya

409
Myaka mitatu kupita
Ye beluwa na matata
Wazuka wa ithibata
Kuvunja waqus'udiya

410
Watano wana h'alali
Walichoka na kudhili
Waliona ujahili
Kudhili Maqureshiya

411
Walaa'ni mkataba
Ulo tundikwa Kaa'ba:
Vipi sisi tunashiba
Wenzetu wafa na njaa

412
Na hapo wakisutana
Katokea muungwana
A'mi yake Sayidana
Qureshi kawatokeya

413
Abu T'alibu kasema:
Sikizeni enyi jama
Ninenalo kama jema
Naomba kunitikiya

414
Mwanangu kanikhubiri
Kama ni kweli khabari
Tusahau yalo jiri
Mtuache kurejeya

415
Kama yeye ni kidhabu
Mtapata mat'ulubu
Nitakupeni H'abibu
Aifariqi duniya

416
Wakanena Maqureshi:
Kanena nini mzushi?
Sisi hatuna ubishi
Yako tumeyaridhiya

417
Anadai Mursali:
Waraqa ni maakuli
Waliwa kila pahali
Ila jina la Jaliya

418
Anadai Muh'amadi
Ni mchwa alo fisidi
Ila jina la Wadudi
Ni hilo limesaliya

419
Kama kweli alo nena
Na hayo mkayaona
Hapana sababu tena
Ya sisi kutususiya

420
Lakini kama mrongo
Chukueni yake shingo
Mlipate lenu lengo
Mlilo liqus'udiya

421
Makafiri wakakiri
Kwa furaha na sururi
Wanena: Leo Bashiri
Mkononi kaingiya

422
Leo mzushi kafika
Na leo tutamshika
Madai yatakatika
Kuudai Unabiya

423
Wakatoka kwa vishindo
Wamekaza wao mwendo
Ni huo wao mtindo
La shari kuliwaniya

424
Kaaba wakidukhuli
Wakaona ni ya kweli
Yake Mtume qauli
Ni kweli alo wambiya

425
Waraqa wote waliwa
Ni kweli wabunguliwa
Ila jina la Moliwa
Lake Mwenyewe Jaliya

426
Kuuona muu'jiza
A'jabu yawashangaza
Hawana walilo weza
Ila H'aqi kuridhiya

427
Na mkubwa wa kupinga
Lile Baba la Ujinga
Lilishiwa na uganga
Waraqa kupasuliwa

428
Ikawa hapana budi
Walo gomewa warudi
Na mambo yake Wadudi
Mazito kuyaelewa

429
Qiasi kuwafariji
Akamtwaa Mpaji
Mja wake muh'itaji
A'mi ya wetu Nabiya

430
Siku ya tatu kupita
Bi Khadija akamwita
Naye nana akafwata
Mis'iba ikaeneya

431
Kuondoka nguzo mbili
Ilikuwa ni thaqili
Kwa Mtume na ahali
Na walio mfwatiya

432
Ni ya Molawe mapenzi
Mwaka huu wa majonzi
Kumwondolea walinzi
H'abibi wetu Nabiya

433
Basi kero za kufari
Zikazidi kukithiri
Ikawa huleta shari
Bukratan wa a'shiya

434
Miraji alipo rudi
Bwana wetu Muh'amadi
Mambo tena yashitadi
Kila ovu kumweteya

435
Miraji waikanusha
Anenalo walibisha
Ushahidi wa kut'osha
Uchawi wasingiziya

436
Baa'dhi walegalega
Wakaingiwa na woga
Na wengine wavuruga
Mambo yakaa vibaya

437
Lakini wake rafiqi
Abubakari S'adiqi
Hapo hapo kas'adiqi
Khabari kuisikiya

438
Akanena: Twaamini
Anenayo ya mbinguni
Seuze ya hapa chini
Haya mambo ya duniya

439
Kawajibu wadadisi
Hayo mambo ni myepesi
Mimi sina wasiwasi
Namuamini Nabiya

440
Kwa hiyo yake Imani
Akapewa na mwendani
Jina liso nuqus'ani
S'IDIQI lilo timiya

441
Katika zao suali
Makafiri majahili
Kumuuliza Rasuli
Walitaka kusikiya

442
Walitaka awambiye
Kati hiyo safariye
Nani kakutana naye
Yu njiani arejeya

443
Waliona ni muh'ali
Alivyo dai Rasuli
Kusafiri kwa laili
Safari ya siku miya

444
Na yeye akawajibu
Kila kitu babu-babu
Wakasema: Ukis'ibu
Sote tutakwandamiya

445
Misafara kiwas'ili
Wakatoa tafs'ili
Sawa sawa na qauli
Aliyo sema Nabiya

446
Wadawaa mafedhuli
Waiona sasa kweli
Lakini hawakubali
La H'aqi kulifwatiya

447
Yule kafiri shadidi
Anaye itwa Walidi
Akaona hana budi
Uchawi kumzuliya

448
Ni uchawi na uganga
Wamzuliya wajinga
Wataonapi muwanga
Na macho yamepoteya

449
Kaamini Muumini
Mkanya kazidi kani
Karudi kwake nyumbani
Na chuki yamzidiya

450
Mii'raji ni chungio
Wachekechwa walo sio
Watwaliwe walo ndio
Kumnus'uru Nabiya

451
Huo ndio mtih'ani
Waupasi Waumini
Kwani Mtume mwakani
Madina atahamiya

 452
Huko hendi mwenye shaka
Jalali anawataka
Imani walo ishika
Diniye kuiwaniya


 MAFUNZO:

Neno Fitna la Kiarabu lina maana ya mateso, na pia maana ya mtihani, au majaribio, na pia maana ya chokochoko, kufitini. Basi hayo mateso yalipo zidi yalikuwa ni mitihani kwa wenye Imani. Kadhaalika mtihani mkubwa walipewa Waislamu kumuamini Mtume s.a.w. kwa hadithi yake ya Miiraji na Israi. Na ilikuwa pia kwake yeye kumzidishia kuthibitika juu ya Ujumbe wake kwa kuona khasa malipo yatakayo wapata wema na wabaya, na kila siri za Mwenyezi Mungu alizo oneshwa na Mwenyezi Mungu. Hayo yote yamekuja mwaka mmoja tu kabla ya kuja amri ya kuhamia Madina. Kwani huko Madina ndiko kutako kuwa na kazi muhimu na kubwa kabisa ya kusimamisha Uislamu kama ni Dola. Na huko ndiko atakapo pata uadui wa wote. Na kweli ndiyo yaliyo tokea. Huko haukuwa uadui wa Maqureshi wa Makka tu, bali wa Waarabu wote, na Mayahudi, na Waajemi, na Warumi. Kwa hivyo walitakikana wabakie Waumini wa kweli kweli, walio pasi katika mitihani ya mateso, na mitihani ya Imani.