341
Sasa tawapa khabari
Za huyo Bwana U'mari
Alikuwa ni kafiri
Qatili kupindukiya
342
Alikuwa mwenye nguvu
Hukusa watu ziovu
Alikuwa kwa mabavu
Hapana wa kumwingiya
343
Na h'adi aliudhika
Mambo yalivyo chafuka
Dini mpya ilo zuka
Ni mno kaichukiya
344
Alikuwa na a'qili
Lakini hakukubali
Kusikiliza la kweli
Hakutaka kusikiya
345
Hasira ilikithiri
Alipo pata khabari
Isilamu wahajiri
Wenda nchi H'abushiya
346
Akaona uvunjifu
Kwa watuwe watukufu
Kuingia khitilafu
Na wengine kukimbiya
347
Yeye takata mzizi
Akomeshe upuuzi
Huo ulio eneya
348
Akainoa h'adidi
Kumchinjia H'amadi
Akampanda jawadi
Maovu kaqus'udiya
349
Na huku amea'zimu
Akamkuta Nua'imu
Huyo bwana kasilimu
Lakini hujifichiya
350
Akiipata khabari
Kaona akifu shari
Akamwambia U'mari:
U'mari nakukhofiya
351
Unadhani watu wake
Watamwacha peke yake
Wataka watu wacheke
A'ibu ikikujiya?
352
Angalia uendako
Sitengeze kwa wenzako
Ukaacha huko kwako
Hali kunateketeya
353
Kwani kwangu kuna nini?
Dadiyo ameamini
Na shemejiyo yaqini
Saidi amefwatiya
354
U'mari hakujijua
Wala hakujitambua
Kwa chuki ya kupasua
Moyoni ilo mwingiya
355
Akaona afulize
Ende nyumbani kwa nduze
La kweli wamueleze
Ajue la kutendeya
356
Akifika mlangoni
Asikia Qur'ani
Akajua kwa yaqini
Ni kweli alo sikiya
357
Kufika Bin Khat'abu
Walikisoma Kitabu
Na mwalimu ni Khababu
Upesi kajifichiya
358
Akija ingia ndani
Shemeji katupwa chini
Mkono uko kooni
Na Fat'uma kaumiya
359
Na dada katakalamu
Na huku atoja damu:
Ni kweli tumesilimu
Tenda utalo tendeya
360
U'mari kamwacha mume
Apumue na aheme
Kanena: Nipe nisome
Mlio kijisomeya
361
Kutupa yake nadhari
Maneno kayakariri
Aliona kama nuri
Ambayo hakudhaniya
362
Aliona muu'jiza
Ambao wamshangaza
Akaapa kwa Muweza:
Amini hatungi haya
363
Hawezi bini Adamu
Kama haya kunudhumu
Sijaonapo utamu
Mithili ya hizi Aya
364
Hapo mwalimu katoka
Na maneno katamka:
Jana Tumwa akitaka
Na mimi kimsikiya
365
Aliomba Mukhtaru:
Rabi Mola unus'uru
Wisilamu kwa U'maru
Ni wewe natarajiy
366
Na hapo Bin Khat'abu
Aliitoa jawabu
Kumuambia Khababu
Nayo ni hii sikiya:
367
Sasa mimi nas'adiqi
Muh'amadi ni wa h'aqi
Nionesheni t'ariqi
Niende kushuhudiya
368
Kunena hayo U'mari
Maovu yawa mazuri
Na hayo yaliyo jiri
Kana kwamba hayakuwa
369
Kalekezwa mah'ashumu
Nyumba yake Arqamu
Was'alipo Isilamu
Na huko wakutaniya
370
Alipo fika U'mari
Wkaona: Hiyo shari
Anakuja tua'ziri
Na balaa tuleteya
371
H'amza alia'zimu:
Nitamtoa wazimu
Jeuri akizuu'mu
Naliwe litalo kuwa
372
Mtume kamkataza
Kwani yeye anaweza
Kwa nguoze kamkaza
Na huku amkemeya:
373
U'mari wataka nini?
Hutwachi na yetu Dini?
Watufwatia nyumbani?
Utakuja angamiya
374
U'mari yake qauli
Sikiza wangu Rasuli
Mimi sijii qitali
Mimi naja shuhudiya
375
Mtume alikabiri
Kumdhukuru
Jabari
Walo baqi wakariri
Mayowe
kote yeneya
376
Ilikuwa ni sururi
Kwa Isilamu h'aqiri
Kwani nguvu za U'mari
Maa'rufu kote piya
377
Yeye si mtu wa kucha
Wala hajui kuficha
Aliapa hatoacha
H'aqi kuitangaziya
378
Kaondoka hapo hapo
Akapita ajuapo
Kwenye watu waketipo
Yalo jiri kuwambiya
379
Kanena bila muh'ali:
Nimemfwata Rasuli
Ndiye Mtume wa kweli
Na Mngu wetu Mmoya
380
Hii ni Dini ya H'aqi
Musitaqimu T'ariqi
Siutaki unafiqi
La kweli taliteteya
381
Makafiri wakazuka
Hapo hapo wambaka
Ikawa ni pata shika
Kila mtu avamiya
382
Yeye ni mtu hodari
Ni mtesi na jabari
Utadhani ni namiri
Majibwa yamkemeya
383
Lakini ni wengi wape
H'ata ingawa mapepe
Yakikithiri matope
Hulishinda jiwe moya
384
Kapigana kwa Imani
H'ata kawa taa'bani
Kabaki aketi chini
Maneno kiwatupiya
385
Haya yote kumfika
Na yeye hakut'osheka
Mtume kenda mtaka:
Ya nini kujifichiya
386
Tuonyeshe Dini yetu
Waijue wote watu
Ni nani wa kuthubutu
Kwa yetu kutuzuiya?
387
Sisi kweli twaifwata
Tusiogope matata
Lolote likitupata
Ni H'aqi twashikiliya
388
Akaona Mua'dhamu
Waridhika Isilamu
Akaongoza qaumu
H'aramuni kwelekeya
389
Wafika Msikitini
Na makafiri pomoni
Wakas'ali Waumini
Na huku wawangaliya
390
Hapo ni kwanza kuweza
Wanyonge kujitokeza
Kumua'budu Muweza
Mbele ya watu jamiya
391
Kiwango kimesha fika
Cha kweli nje kutoka
Hayakuwa kwa haraka
Haya yaliyo tokeya
392
Na mimi tawapa neno
Msikie mlo pano
Huu ni mwaka wa tano
Tangu kuja Unabiya
MAFUNZO:
Zingatia ilichukua miaka mitano ya kueneza Uislamu kisirisiri kwa unyonge walio kuwa nao Waumini. Ni majaaliwa ya kupata kusilimu mtu shujaa na mkali kama Sayyidna Umar r.a. ndipo wakaweza kujidhihirisha wazi kwa watu wote. Jambo muhimu lolote lafaa kuanziwa kwa mbinu zake, kisirisiri, mpaka itakapo fika wakati wa kulitangaza. Ubingwa ni kujua lini kuficha, na lini kutangaza.