1141
Kupita myaka miwili
Alia'zimu Rasuli
Kwenda Maka kukamili
Kazi aliyo ijiya
1142
Kwani sasa A'rabuni
Watu wote waamini
Isilamu
Umati Muh'amadiya
1143
H'ata nje ya biladi
Wamwitika Muh'amadi
S'ultani wa makundi
Maliki wa H'abushiya
1144
Huyo naye Mfalume
Alimfwata Mtume
Na kwa huyu mwanamume
Dini kwetu yatujiya
1145
Dini ilo takasika
Watu wengi waishika
Wa Bara la Afrika
Tangu siku ya kwanziya
1146
Hii ndiyo Dini yetu
Ndiyo Dini ya kiutu
Tuombee na wenzetu
Hao walio poteya
1147
Na Mola tawaokowa
Na kweli wataijuwa
Linapo dhihiri juwa
Nyota zote hufifiya
1148
Alimtuma Mwenyezi
Mtume wake a'zizi
Ende akaweke wazi
Machache yalo baqiya
1149
Apate kukhitimisha
Kwani zama zimekwisha
Pasiwe kubabaisha
Na uzushi kutokeya
1150
Ikitangaa khabari
Kwamba sasa Mukhtari
Kwenda H'ija yut'ayari
Umati wamjiliya
1151
Si umati ulo kuja
Afwaja afwaja
Niya ya wote ni moja
Kumpenda Maulaya
1152
Bara yote ya A'rabu
Wamwitikia H'abibu
Hawakujia h'arubu
I'bada ndiyo wajiya
1153
Ni i'bada ya kuh'iji
Aitakayo Mpaji
Wajawe kuwafariji
Weshe dhiqi na udhiya
1154
Ni i'bada yao moja
Yakusanya wote waja
Pasiwepo mwenye hoja
Chokochoko kuitiya
1155
Yakumbusha Isilamu
Kwa nguo za ih'iramu
Kuwa ni moja qaumu
Kwa usawa watimiya
1156
Na A'rafa wakifika
Mtume aliwataka
Pasiwe wa kutamka
Ataka wakhut'ubiya
1157
Zingatieni wenzangu
Umati huu wa Mungu
Ulisahau matungu
Zamani yalo pitiya
1158
Wasahau vita vyao
Wasamehe maoneo
Wanajua hii leo
Wao wote ni wamoya
1159
Walo kuwa Makafiri
Walo kuwa Wahajiri
Walo kuwa Ans'ari
Ni S'ahaba wa Nabiya
1160
Nao wote Isilamu
Wafwasi wa Mua'dhamu
Na wapenzi mah'ashumu
Wa Muh'amadi Rasuwa
1161
Zitazame zao s'ura
Kwa mng'aro zinang'ara
Nguo zao ni ishara
Us'afi wa yao niya
1162
Ya kwanza yake qauli
Alo isema Rasuli
Kakataza kuqatili
Bila njia ya sharia'
1163
Roho ya mja tukufu
Haifai kutilifu
Kama Siku Takatifu
Ya I'di ya Udhih'iya
1164
Mali ya mtu h'aramu
Yafaa kuyah'ishimu
Cha mwenzio kwako sumu
Ila akikuridhiya
1165
Mkumbuke wake zenu
Wana h'aqi juu yenu
Watumishi ni ndu zenu
Yapasa wahurumiya
1166
Na muwalishe mlacho
Muwavishe mvaacho
Kiemewa mtakacho
Wachieni yao njiya
1167
Na riba sasa h'aramu
Alitamka Hashimu
Majivuno kashutumu
Ya siku za Jahiliya
1168
Na akanena Amini:
Majivuno ya zamani
Nayaponda miguuni
Na mengi aliwambiya
1169
Alisema Bwana wangu:
Kitabu cha Bwana Mungu
Na huu Mwenendo wangu
Ni hivyo nawaachiya
1170
Mkivifwata viwili
Hamtokwenda bat'ili
Kanena hayo Rasuli
Na wote wamsikiya
1171
Na baa'da yangu mimi
Hakuna tena Mtumi
Huo ni wake usemi
Wa Muh'amadi Nabiya
1172
Akimaliza qauli
Aliadhini Bilali
Akas'alisha Rasuli
Na wote wakafwatiya
1173
Wakiitoa salamu
Kateremsha Karimu
Kwa mpenziwe Hashimu
Aya nitawatajiya
1174
Ni Aya ambayo kwamba
Tangu dunia kuumbwa
Hapana walio kwamba
Wote walo tanguliya
1175
Leo hiyo timilifu
Siku hiyo ni tukufu
Ijumaa' takatifu
Na I'di ya Udhih'iya
1176
Kwa h'aqiqa ni kutimu
Mafunzo yake Rah'imu
Kwa Utume takhatimu
Kwa huyo alo timiya
1177
Ni kama Mungu asema:
Muh'amadi mekutuma
Kwa ulimwengu mzima
H'ata mwisho wa duniya
1178
Umeletewa Kitabu
Kilo shuka taratibu
Kitalindwa na a'ibu
Milele kitabaqiya
1179
Na wewe Mtume wangu
Wat'osha kwa ulimwengu
Akomesha Bwana Mungu
Na muhuri autiya
1180
Amtuma Mursali
Kwa dalili za a'qili
Na Chuo kiso badili
Daima kitasaliya
1181
Baa'da ya kukamili
Dini ya Mola Jalali
Hatuh'itaji wa pili
Utume akajitiya
1182
Ipo hapo h'aja gani
Baa'da yake Amini
Na Chuo cha Qur'ani
Kuzuka tena Nabiya?
1183
Jua linapo zagaa
Vitu vyote hushangaa
Hata nyota zinon'gaa
Hutahayari kwa haya
1184
Kwisha Mtume kusema
Mbele yake atazama
Bakari ameinama
Machozi yamemweneya
1185
Mtume akauliza:
Ni nini kinakuliza?
Hebu nami nieleza
Natamani kusikiya
1186
Akamjibu Bakari:
Nina yaqini Qahari
Qaribu takukhitari
Wakati waqurubiya
1187
Kakuleta Rah'amani
Utufunze sisi Dini
Ne leo anabaini
Kaziyo imetimiya
1186
Ni huo ms'iba wangu
Ewe Mtume wa Mungu
Moyoni nina matungu
Kwa kuwa watukimbiya
MAFUNZO:
Hata ingeli kuwa mwenyewe Mtume Muhammad s.a.w. hakusema:
"Hapana Nabii baada yangu", akili yatosha kutuambia kuwa haiwezi tena
kuwapo Nabii baada yake, kwani Yeye ndiye pekee aliye kuwa ni
Mtume wa mataifa yote. Hayo yalithibiti naye yu hai. Katika
wafwasi wake wa mwanzo walikuwamo Waarabu, Wazungu,
Waafrika na Waasia. Ni fakhari kwa Watu Weusi kuwa
siku ya pili ya kupewa Utume katika walio mkubali Mtume s.a.w. ni Bibi Baraka,
mwanamke mweusi. Shahidi wa kwanza kufa kwa ajili ya
Dini yake katika Uislamu, ni Bibi Sumayya, mwanamke mweusi, na akafuatiwa na
mumewe Yaasir, mtu wa Yaman. Muadhini wa mwanzo ni
Sayyidna Bilal, naye ni mweusi. Hao walikuwa Arabuni.
Lakini hata nje ya Arabuni ni Mfalme wa Uhabeshi
katika walio silimu na mwenyewe Mtume Muhammad s.a.w. yu hai. Kutokana na Masahaba walio kwenda Uhabeshi katika Uhamiaji wa kwanza,
Uislamu ukawa umefika Afrika, tena Afrika Mashariki.
Katika khutba yake ya kuaga, Mtume s.a.w. anahimiza kuangalia watumishi,
kuangalia wake zetu, na kuhishimu
Amri bin Al A'ss, aliye kuwa Liwali wa
Misri alitaka kutanua msikiti, na pakawa hapana nafasi ila ivunjwe nyumba ya
mwanamke wa Kikristo. Alitaka kuinunua, mwanamke kakataa.
Alitaka amjengee nyengine, mwanamke kakataa.
Akaivunja, na akamwekea fidia yake. Mwanamke katoka
Misri mpaka Madina kwa Sayyidna Umar r.a. kumshitakia.
Sayyidna Umar akamuamrisha Liwali aje Madina. Amri bin
Al A'ss alijitetea kwa kusema kuwa ni dharura msikiti
utanuliwe kwa kuzidi Waislamu, na fedha zake huyo mwanamke zipo. Hukumu ya
Sayyidna Umar r.a. ni kusema: "Vunja msikiti na
umjengee huyo mwanamke nyumba yake pale pale ilipo kuwapo, vile vile