121
Kufika kumi na mbili
U'mri wake Rasuli
Mtume alikubali
Kwenda Shamu kutembeya
122
Alifwatana na a'mi
Kwendea nchi ya Shami
Kama a'da ya qaumi
Qureshi wano zoweya
123
Ulikuwa mwendo wao
Na ndio uchumi wao
Watu wote wawezao
Riziqi kwenda zengeya
124
Joto linapo shitadi
Ni Shamu hapana budi
Na kipupwe kikizidi
Kusini waelekeya
125
Wakifika mipakani
Wamkuta Nas'arani
Qasisi mwanachuoni
Jinale nitawambiya
126
Bahira huyo Nas'ari
Kanena: Kuna khat'ari
Nakwambia tahadhari
Vitabu vinanambiya
127
Mwanao ni mtukufu
Mteule wa Lat'ifu
Moyo wangu una khofu
Yahudi kuja muuwa
128
Ni bora urudi naye
Au mpe ende naye
Yeyote umwaminiye
Maka aliko tokeya
129
Na yeye Abu T'alibu
Akamtwaa H'abibu
Akawaaga s'ahibu
Nyumbani wakarejeya
130
Mwanafunzi wa padiri
Alikuja kuikiri
Dini yake Mukhtari
Padiri kamuus'iya
131
Aliacha Unas'ara
Kiona Nuru yang'ara
Kaona zote ishara
Bahira alo mwambiya
132
Ndiye Huyo Salmani
Muajemi wa Irani
Ni S'ahaba mwenye kani
Diniye kupiganiya
133
Muungwana alo bora
Kupita khamustaa'shara
Kaingia bia'shara
Kuuza na kununua
134
Hali yeye masikini
Wote walimuamini
Wakamuita Amini
S'ifaze zikaeneya
135
Akasikia tajiri
Mwanamke mashuhuri
Kamtaka asafiri
Yamani kusafiriya
136
Amuuzie bidhaa'
Qalili ziso khadaa'
Akaona manufaa'
Faida zikazidiya
137
Huyo bibi mah'ashumu
Faida kaona tamu
Kamtaka ende Shamu
Na mali kamwongezeya
138
Akampa mtumishi
Mtoto kama tarishi
Maisara asoghishi
Wa kwitwa kuitikiya
139
Na huko alipo fika
Mapadiri wamtaka
Tarishi akawitika
S'ifaze kawelezeya
140
Waliyo taka kujuwa
S'ifaze wetu Rasuwa
Na h'ali bado hajawa
Mtume wala Nabiya
141
Na hayo kwisha ambiwa
Mapadiri watambuwa
H'amadi tateuliwa
Kijana wewe sikiya
142
Dalili zake twaona
Mteuliwa wa Bwana
Vitabu vyetu vyanena
Ni huyu twamngojeya
143
Mambo yote ya a'jabu
Yalo zuka kwa H'abibu
Maisara kakhutubu
Bibiye akamwambiya
144
Maisara kaeleza
Bibiye akasikiza
Mambo hayo akatuza
Moyoni yakamwingiya
145
Na bibi yamuathiri
Walonena mapadiri
Na faida kukithiri
Bibiya kafurahiya
146
Bibi huyu mtukufu
Akaona ni sharafu
Kuolewa na mwongofu
Apate mtumikiya
147
Na huyo Bibi Khadija
Mtukufu wa wambeja
Hakukiona kiroja
Mahari yeye kutoa
148
Kamtuma shoga yake
Muhamadi amtake
Ampose kwa babake
Na yeye ataridhiya
149
Muh'amadi alipenda
Jambo hilo kulitenda
Mwenyewe yangemshinda
Mahari kujipatiya
150
Wazee kote kuwili
Wafurah'ia mawili
Kupata mke Rasuli
Na Khadija kuolewa
151
Waliketi kwa vizuri
Kwa furah'a na sururi
Robo qarini kujiri
Pasi chuki na udhiya
152
Na Bibi huyu mkweli
Alimzaa Batuli
Fat'uma biti Rasuli
Ndiye Bibi wetu piya
153
Wa kwanza wa kusilimu
Katika wote h'uramu
Wa kwanza wa binadamu
Kums'adiqi Nabiya
154
Watoto wake Rasuli
Wametoka tumbo hili
Ila mmoja t'ifuli
Kwa Mariya Qibt'iya
155
Watukufu wa nasaba
Walikuwa wote saba
Yakapita ya ms'iba
Kufa mbee ya Rasuwa
156
Ni jaa'la ya Jalali
Yalo mpata Rasuli
Kufiliwa na i'yali
Na huku awangaliya
157
Alo baqi baa'daye
Ni Bi Fat'uma pekeye
Ni kutokana na yeye
Wakazaliwa dhuriya
158
Ni yeye Biti Amini
Alo tupa ithineni
Hasani wal Huseini
Mashahidi wa duniya
159
Fat'uma na Bi Khadija
Watukufu wa wambeja
Ni kweli yashinda hoja
Haya ninayo kwambiya
160
Watukufu kama hao
Wametukuza wenzao
Wanawake wengineo
Wote walio baqiya
161
Mtume wetu kasema:
Chini ya nyayo za mama
Pepo yenu mtachuma
Ndivyo alivyo twambiya
162
Na tena kwetu muh'ali
Pepo kuwa ni halali
Ila tuwe na ahali
Mema tunawatendeya
MAFUNZO:
Utoto wake na ujana wake Muhammad s.a.w. ni wa kupigiwa mfano. Hata
kabla ya kupewa Utume alionyesha kwa wote walio kaa
naye kuwa huyu kijana si mtu wa kawaida. Mwendo wake wote ulikuwa ni sawa kabisa. Chambilecho Waswahili: Siku njema huonekana asubuhi.
Wenziwe walio kuwa wanamjua vyema walimpanga jina: Assadiq-Al-Amin, yaani
Mkweli Muaminifu.
Basi vijana na watoto yawapasa wajaribu kumuiga
Mtume Muhammad s.a.w. tangu alivyo kuwa utotoni kwake na ujanani kwake.