22   UGOMBOZI WA MAKA

1077
Mtume kajitahidi
Kutekeleza a'hadi
Lakini wale fisadi
Walishindwa jizuiya

1078
Maqureshi watu shari
Pamwe na Bani Bakiri
Usiku kisirisiri
Wauwa Bani Khuzaa'

1079
Na kulipo pambazuka
Bani Khuzaa' wafika
Kwa Mtume atamka
Wao malenga sikiya

1080
Kakumbusha kwa shai'ri
Ya zamani walo kiri
Itakapo zuka shari
Waje kuwasaidiya

1081
Maqureshi wamekuja
Mji wao kuufuja
Wameuwa afwaja
Mali mengi yapoteya

 1082
Alijibu Muh'amadi
Iandaliwe Jihadi
Kutimiliza a'hadi
A'hadi walo itoa

1083
Walitoka Isilamu
Elfu kumi qaumu
Na wote wamea'zimu
Maka kwenda igomboa

1084
Zingatia tas'awari
Ewe mja wa nadhari
Tangu Tumwa kuhajiri
Mjiwe kuukimbiya

1085
Dhiqi alizo zipata
Mai'sha yake matata
Kila endapo ni vita
A'dui wamfwatiya

1086
Pa kupumua hanako
Kila pahali endako
Aambiwa: Huku siko
Kwa mawe wampopoa

1087
Wakumbuka Muh'amadi
Pamwe na wake Zaidi
T'aifu walipo rudi
Madamu yawaeneya

1088
Na huku kwao nyumbani
Wanaambiwa: Tokeni
Msingie as'ilani
Mtafute pa kwendeya

1089
Pale walipo fukuzwa
Bondeni watokomezwa
Wasile wala kuozwa
Wapate kuteketeya

1090
Kwa muda myaka mitatu
Walipo tengwa na watu
Wasipewe h'ata kitu
Majani wakajiliya

1091
Watuwe wabeuliwa
Watuwe waa'dhibiwa
Watuwe wanauliwa
Mazito wavumiliya

1092
Kulipozidi kutisha
Watuwe kawatorosha
Na wao walipo kwisha
Mwenyewe akakimbiya

1093
Na huko uhamishoni
Wawafwata maluu'ni
Na mjini makhaini
Wachimba wakichocheya

1094
Siku hizo zimepita
Za unyonge na ukata
Za kulazimishwa vita
Wachache wa kuwaniya

1095
Leo hii Mtukufu
Ana umati uluufu
Na wote ni wat'iifu
Anenalo wangojeya

1096
Zamani walo mpiga
Aweza kuwavuruga
Zamani walo mpinga
Aweza kuwavamiya

1097
Walio kimtukana
Hawanalo la kunena
Walio wakijivuna
Kwa leo wanyenyekeya

1098
Sasa yuko milangoni
Hapo nje ya mjini
Na nduguze Waumini
Wote ni kitu kimoya

1099
Kawambia wake umma:
Leo hapa twasimama
Na tuyapige makhema
Na kesho tutaingiya

1100
Maqureshi walo Maka
Nyoyo zao zashituka
Waona nyoto zawaka
Zimetanda kote piya

1101
Waona leo ni leo
Na hapana mengineo
Hii siku ya kilio
Hapana ato saliya

1102
Wakikumbuka maa's'i
Wakazidi wasiwasi
Wajua kuna qis'as'i
Na hicho kitawajiya

1103
Walakini Bwana wetu
Hana uchungu na mtu
Hakutaka fanya kitu
Maovu kuyalipiya

1104
Aliitoa amri
Kwa wote Majamadari:
Msiifanye jeuri
Yeyote kunigusiya

 1105
Sitaki mtu kuguswa
Sitaki mtu kupigwa
Sitaki mtu kufyonywa
Ujuba sitoridhiya

1106
Mtume aliyagawa
Majeshi yake kwa sawa
Sehemu nne zikawa
Kila pembe kuingiya

1107
Yeye kangia mjini
Kutoka kaskazini
Walipanda ithineni
Juu ya wake ngamiya

1108
Aliye panda mwenziwe
Ni Usama kijanawe
Ni mtoto wa mwanawe
Mwanawe wa kumleya

1109
Ni mtoto wa Zaidi
Kijana cha Muh'amadi
Aliye kuwa uledi
Nyumbani akakuliya

1110
Kama huu utukufu
Uko wapi tuushufu
Mbora wa Masharifu
Kumtukuza s'abiya?

 1111
Na baa'dae Rasuli
Kamfanya Jenerali
Chini yake maqubeli
Warabu wamfwatiya

1112
Aliamuru Mtumi
Awaqabili Warumi
Walo toka kule Shami
Wataka tushambuliya

1113
Naye h'ali ni kijana
Kumi na nane sinina
Nyuma yake waungwana
Usama atanguliya

1114
Tunapewa taa'luma
Kwamba huu wetu Umma
Wa ulimwengu mzima
Na Dini ni ya duniya

1115
Ndiyo Dini ya mapendo
Ndiyo Dini ya mwenendo
Ndiyo Dini ya vitendo
Si maneno kutumiya

1116
Na hapo wetu Rasuli
Pamwe na wake t'ifuli
Juu ya wake ibili
Mjini wakaingiya

1117
Na tena naye Sharifu
Akimaliza kut'ufu
Akanena kwa lut'ufu
Umati kakhut'ubiya

1118
Kamshukuru Rabana
Kuiondoa laa'na
Ya Qureshi kujivuna
Jeuri za Jahiliya

1119
Majivuno ya nasabu
Aliyakanya H'abibu
Si mbora Mua'rabu
Na mwengine naye piya

1120
Mweupe hana ukwasi
Kwa kumshinda mweusi
Sote bila wasiwasi
Ni wa Adamu dhuriya

1121
Na Adamu ni mchanga
Basi huo si ujinga
Kujivuna na kuringa
Udongo ulo anziya?

1122
Na tena hapo Amini
Alisoma Qur'ani
Aya inayo baini
Wote watu ni sawiya

1123
Tumwa tena kauliza:
Ni nini mnalo waza
Kulitenda naliweza?
Qureshi mtanambiya

1124
Wakajibu Makafiri:
Twataraji kwako kheri
Wewe ndugu Mukhtari
Na babiyo naye piya

1125
Mtume tena kasema
Kama Yusufu wa zama:
Hapana kwenu lawama
Ndu zangu Maqureshiya

1126
Tuyasahau ya kale
Tuyasahau milele
Tuyatazame ya mbele
Mola tawaghufiriya

1127
Na tena basi Rasuli
Kamuamuru Bilali:
Adhini tupate s'ali
Na Kaa'ba hiyo kweya

1128
Qureshi wakitazama
Walimuona Usama
Kijana msiriama
Amepanda na Nabiya

1129
Wakitupa macho tena
Bilali wanamuona
Anaitoa adhana
Na watu alinganiya

1130
Wakajua hapo hapo
Ya kale leo hayapo
Mja hulipwa malipo
Kwa analo jitendeya

1131
Hapana tena ugozi
Umekwisha ubaguzi
Hii Dini ya Mwenyezi
Usawa sawa sawiya

1132
Na wengi hapo qaumu
Kuuona ukarimu
Hapo hapo wasilimu
Wachache walibaqiya

1133
Walio baqi Kufari
Hawakutendwa qahari
Kwa ya wenyewe khiari
Wakaja kushuhudiya

1134
Alo kuwa maluu'ni
H'ata akala maini
Ya a'mi yake Amini
Bi Hindi naye kangiya

1135
Kaambiwa na Sharifu:
Mimi dada nakua'fu
Wa zamani upotofu
Umekwisha twondokeya

1136
Naye bibi akataja:
Na hapa nilipo kuja
Kati ya jamii waja
Ni wewe kikuchukiya

1137
Na hivi sasa natoka
Ninakwambia h'aqiqa
Sinaye kumchunuka
Kamawe ewe Nabiya

1138
Ninakupenda yaqini
Kwa dhati yangu moyoni
Akamjibu Amini
Inshalla utazidiya

1139
Ni kwa wema na upole
Alo tenda Mteule
Kawavuta watu wale
Na wote wamwitikiya

1140
Akisha kutengeneza
Na mambo yote kutuza
Njia yake kageuza
Madina akarejeya

MAFUNZO:

Tunajifunza hapa kuwa ahadi ni ahadi. Ukifungana na mtu lazima utekeleze maagano yenu. Na hapana khitilafu ikiwa uliye fungamana naye ni Muumini mwenzio au ni kafiri. Mtume s.a.w. amefanya mapatano ya kusaidiana kwa hali na mali na makafiri Bani Khuzaa ambao ni washirikina. Na kwa ajili yao akatoka kwenda kwa azma ya kupigana na Maqureshi wa kabila yake, kwa ajili ya kutekeleza ahadi. Uislamu unatutaka tupiganie uhuru wa watu wote, pasiwepo maonevu. Hiyo ni amri ya Mwenyezi Mungu kama ilivyo simuliwa katika Qur'ani: "Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nyumba za wat'awa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi." (22.40)
Kutenganisha Dini na siasa sio mwendo wa Mtume Muhammad s.a.w. Lakini siasa ifuate uwongozi wa Dini, sio Dini kufuata siasa.