11   YALOMPATA T'AIFU 

453
Sasa kidogo twasita
Tuyatatue matata
Tutazame yalo pita
Mtume alipo fiwa

454
Alipo fiwa Mtumi
Na mlinzi wake a'mi
Na mbora wa h'urami
Bi Khadija maridhiya

455
Alitoka Muh'amadi
Kafwatana na Zaidi
Alo kuwa ni waladi
Kijana wa kumleya

456
Wende mji wa T'aifu
Mji wa Bani Thaqifu
Ulomlea Sharifu
Kwa H'alima Saa'diya

457
Ili ende akhubiri
Awape njema khabari
Ya Dini yake Ghafari
Wapate nao hidaya

458
Kaonana na mababa
Kaeleza mat'ilaba
Aliyo pata si haba
Mazito kuvumiliya

459
Akarudi kwa wadogo
Wakamwambia: Mrongo
Wampopoa madongo
Na mawe yamfwatiya

460
Wahuni wote mjini
Wampopoa Amini
Pamwe na wake mwendani
Na huku wamzomeya

461
Madamu yachururika
Mwili wote wapasuka
Wakichoka wawashika
Wamwambia: Tokomeya

562
Walipo choka watwana
Kuwatesa waungwana
Wakapata hapo tena
Kutua na kupumua

463
Pana kivuli cha mti
Wakatua wakaketi
Wenye shamba kwa bahati
Huruma wawaoneya

464
Hao watu Maqureshi
Nao h'ali ni wabishi
Walituma mtumishi
Chakula kuwagawiya

465
Mtumishi kasaili
Akamjibu Rasuli
Hapo hapo filh'ali
Mtumwa kashuhudiya

466
Mabwana wakaudhika
Kwa hayo yaliyo zuka
Na Mtume kaondoka
Jibrili kamjiya

467
Jibrili ashauri:
Nitoe yao jeuri
Walio kutenda shari?
Sasa wataangamiya

468
Muh'amadi kakataa
Kanena: Hao
a'saa
Wakaona unang'aa
Muanga wakafwatiya

469
Hawa sasa hawajui
Ndio hivyo wawa
wawi
Na zuri hawatambui
Ndio waona wabaya

470
Wao na wao
ghulamu
Watapo kuja fahamu
Kitu gani Isilamu
Ni wao watateteya

471
Mwalimu kataa'jabu
Kwa hii yake jawabu
Kanena: Kweli
Wahabu
Sifa alo kusifiya

472
Mwenyezi alivyo sema
Kitabuni tunasoma
Wewe
Tumwa wa Reh'ema
Kwa viumbe vyote piya

473
Sasa Tumwa akifika
Huko karibu na Maka
Khabari ikamfika
Hana ruhusa kwingiya

474
Hana ruhusa kurudi
Mjini kwake kwa jadi
Aambiwa Muh'amadi
Mzalendo mzaliya

475
Na nini yake lawama?

Kwa kuwa ataka mema
Na kuondoa dhuluma
Na H'aqi apiganiya

476
Na haya tuyaonao
H'ata duniya ya leo
Wale wema watendao
Ndio wanao umiya

477
Wanafukuzwa makwao
Wanyang'anywa kila chao
Wauliwa watu wao
Na wao wavumiliya

478
Kila aliye qatili
Atalipwa na Jalali
Kila aliye dhalili
Malipwa yamngojeya

479
Aliwaomba wajomba
Na Suheli kamuomba
Hunyonya hata la mbwa
La mama ukikoseya

480
Kama a'da ya Warabu
Mtume kenda t'ulubu
Na akapata jawabu
Kukataliwa h'imaya

481
Mut'i'mu kamtaka
Aliye pinga waraqa
Na yeye akamwitika
Akamwambia: Ingiya

482
Mut'i'mu akanadi:
Namlinda Muh'amadi
Naye sasa yuwarudi
Nanyi mtamwangaliya

483
Akaingia mjini
Naye anayo amani
Kama ya a'mi zamani
Qabula hajajifiya

484
Akabaki hii h'ali
Kwa muda myaka miwili
Akikhubiri Rasuli
Dini bila ya udhiya

485
Mii'raji kuja kuwa
Mut'i'mu kachukiwa
H'imaya akayondowa
Maudhi yakarejeya

486
Lakini wetu Rasuli
Fikira hakubadili
Daima yake qauli
Kwa wema humtajiya

487
Japo kuwa Mut'i'mu
Hakuwa Muisilamu
Walakini Mua'dhamu
Wemawe hukumbukiya

488
Yakimfika mauti
Alis'ifiwa kwa beti
Na H'asani wa Thabiti
Kwa amri ya Nabiya

MAFUNZO:

Tunaona kila ambapo mtu wa kawaida anatarajiwa awe na hamaki, na bughdha, aapize, alipize kisasi, Mwongozi wa kweli huonyesha subira, na huruma na usamehevu. Na Mtume s.a.w. ni rahimu hata katika shida.