S'IFA ZA MTUME s.a.w.

 57
Na s'ifa zake Sharifu
Ni mkweli na lat'ifu
Na tena muaminifu
Tangu utoto s'abiya

58
Watu mbali na jirani
Wakamuita Amini
Kwa kuwa wamuamini
Kijana cha Hashimiya

59
Ali mwingi wa huruma
Kwa faqiri na yatima
Ali mwingi wa h'ishima
Kwa watu wote jamiya

60
Ali mzuri wa shani
Akipendeza jamani
Kamaye sijui nani
H'abibi wetu Nabiya

61
Alikuwa mwenye heba
Mtukufu wa nasaba
Ali mwingi wa mah'aba
Kwa viumbe vyote piya

62
Hakumkhofu jeuri
Kwa mnyonge ni h'aqiri
Kivunja ovu kwa zuri
Ndivyo alivyo zoeya

63
Alikipenda utani
Lakini kwa wasit'ani
Hakuwa na
nuqus'ani
Sifaze zimetimiya

64
Kwa wazazi mt'ii'fu
Kwa wanyumbaye lat'ifu
Kwa watoto ni raufu
Kwa Mola anyenyekeya

65
Katukuza kila kazi
Hakujifanya a'zizi
Alichunga hata mbuzi
Kwa hima kiwangaliya

66
Ni mja wa s'ifa hizi
Alo tumwa na Mwenyezi
Aondoe uchafuzi
Ulo enea duniya

67
Akafunza Tawh'idi
Lam Yalid Walam Yuuladi
Umma wetu ni
wah'edi
Kama alivyo Jaliya

68
Hakuridhia kabisa
Kutukanwa
Bwana I'sa
Kwani hayo yali visa
Wazushi wamzuliya

69
Akamueka pahali
Patukufu pa h'alali
Kuwa yeye ni Rasuli
Masih'i tena Nabiya

70
Kavunja ushirikina
Kuwa Mungu ana mwana
Ujinga tena hapana
I'limu isha eneya

71
Wapime wenye a'qili
Walijue jambo hili
Wasifwate ujahili
Wa walio tanguliya

72
Kwani Mtume kanena
Kuwambia Waumina
Wende hata huko China
I'limu kuizengeya

73
Katufunza sote watu
Tuseme na Mola wetu
Kuhani hawezi kitu
Lolote kututendeya

74
Katuumba sote Rabi
S'afi bila ya madhambi
Hatukurithi kwa bibi
Na babu hakutwachiya

75
Hiyo Dhambi ya As'ili
A'qili haikubali
Na ukitaka dalili
Soma vyema Bibliya

76
Kila mtu utendalo
Utakuja lipwa lilo
Kama jema ni jemalo
Na maovu nayo piya

77
Kawapa watu uh'uru
Wenyewe wajinus'uru
Hapana wa kuwadhuru
Wakimt'ii Jaliya

 78
Hapana wa kumkhofu
Ila Mwenyewe Raufu
Hapana la utukufu
Ila kucha kuzidiya

79
Ubaguzi kaukanya
Madhalimu kawaonya
Na ulevi kaufanya
Ni mama wa maa's'iya

80
Mikazo ya Kiyahudi
Kakataza Muh'amadi
Kwani Dini ya Wadudi
Nyepesi katuambiya

81
Ni Dini ya ulimwengu
Ya waja wa Bwana Mungu
Si Mwarabu si Mzungu
Ila ni watu jamiya

82
Ni Dini ya Qur'ani
Maneno yake Manani
Kitabu kiso kifani
Mwanzoe hata kwishiya

83
Kitabu kisobadili
H'ata kwa moja qauli
Tangu siku ya azali
Hata mwisho wa duniya

84
Kitabu cha miu'jiza
Cha Mola wetu Muweza
Walo soma kwa kutuza
Nee'ma zimewajiya

 85
Twakuomba Rah'amani
Tusomeshe Qur'ani
Na tumfwate Amini
Shafii' wa watu piya

86
Twakuomba Bwana Mungu
Uzikate zetu pingu
Utwondolee matungu
Tupate yetu huriya

87
Utupe kila la kheri
Twondolee kila shari
Ya siri na ya dhahiri
Hata tusiyo yajua

88
Mwango huu twakhitimu
Tums'alie Hashimu
Na S'ahabaze kiramu
Na Aali zake jimiya  
 

MAFUNZO:

 Ni hakika isiyo katalika kuwa Mwenyezi Mungu amempamba Mtume wake Muhammad s.a.w. kwa umbo jema kabisa, na tabia njema kabisa. Hakika hizo ni lazima zitajwe na kutajwa tena, ili ipate kuwadhihirikia watu katika nyoyo zao na akili zao, hata iwe kama kwamba wanamwona, na wanaishi naye. Ni hapo tu ndipo tunapo ingiwa na shauku ya kumfuata mtu huyu wa ajabu, na kutamani kumuiga kwa kila alivyo tenda, na alivyo kuwa. Na hapo ndipo wanaadamu tutapo ongokewa ulimwenguni na Akhera.