609
Tena Tumwa na mwendani
Wakaingia pangoni
Huko nje majangwani
Na huku wakikimbiya
610
Maa'dui wanafwata
Waja wingi wa matata
Mbioni wamtafuta
Mpenzi wa Maulaya
611
Wakiongozwa na nyayo
Wakinena: Huyo huyo
Wakazidi pata moyo
Pangoni zikilekeya
612
Wana khofu walo ndani
Khasa S'idiqi wa
Thani
Alimwambia Amini:
Tu pweke ewe Nabiya
613
Akajibu wetu Bwana:
Yupo nasi Maulana
Yeye nasi twashikana
Milele atwangaliya
614
Na kweli hapo tazama
Makafiri wasimama
Kwani waona h'amama
Njiwa hapo katagiya
615
Nyoyo zao zikadunda
Wasijue la kutenda
Buibui ametanda
Na mti umechipuwa
616
Wakaona ni muh'ali
Kwingia watu wawili
Na njiwa asimuh'uli
Buibui naye piya
617
Na hao watu wawili
Walipanga na ahali
Maziwa na maakuli
Na khabari kuweteya
618
Binti Abubakari
Hutengeneza t'ayari
Chakula ama khabari
Kakaye huzizengeya
619
Na Bwana wetu A'miri
Mtu wa Bwana Bakari
Jioni na ufajiri
Mbuzi huko hukamiya
620
Kifika siku ya tatu
Walitoka hao watu
Wakaongozwa na mtu
Bedui wa A'rabiya
621
Bakari na Muh'amadi
Na wawili mazidadi
A'miri mwenye juhudi
Bedui mwongoza njiya
622
Wakatoka watu hao
Watambaa na mwambao
Wakhofu a'dui zao
Walio kiwazengeya
623
Wakapitia Qudaidi
Kwa Mamiye Maa'badi
Katamani Muh'amadi
Aonje chembe maziwa
624
Na hapo wamsalimu
Bi kikongwe mkarimu
Wamwambia wana hamu
Maziwa kuwauziya
625
Na mama kasikitika:
Sinacho mnacho taka
Viwele vimekauka
Kwa jua kukithiriya
626
Na lau kwamba ninayo
Nisingefanya uchoyo
Mngekunywa mtakayo
Msinipe pesa moya
627
Mtume wetu mpenzi
Kaonyeshwa na Mlinzi
Kibuzi kama kibanzi
Kibandani chasinziya
628
Ukurutu wampamba
Kimekonda na chembamba
Kikenda chayumba yumba
Viwele vimejinyweya
629
Basi Mtume kasema:
Niruhusu kumkama
Bahati nitatazama
Hwende tukafanikiwa
630
Na tena hapo Amini
Kamshika h'ayawani
Kamwomba Rah'amani
Kwa jinale kaanziya
631
Pasi muda kumuhuli
Yakajaa mabakuli
Kwa baraka ya Rasuli
Alo pewa na Jaliya
632
Akampa mwenyejiwe
Akawapa na wenziwe
La tano kanywa mwenyewe
Na la sita lazidiya
633
La sita lilio zidi
Ni la Baba akirudi
Ajabu yake shadidi
Maziwa kuyakutiya
634
Mama haya mambo vipi?
Maziwa wapata wapi?
Akampa kwa ufupi
Qis'a kilicho tokeya
635
Kamweleza huyo babu
S'ifa za wetu H'abibu
Huyo bwana akajibu:
Ni huyo nilo sikiya
636
Ni mgomvi wa Qureshi
Apingwao kwa ubishi
Ni Mtume aso ghishi
Huyo ni kweli Nabiya
637
Laiti ningemkuta
Kabisa nisingesita
Hapo hapo ngemfwata
Kokote ano kwendeya
638
Na kama alivyo nena
Mzee na wake nana
Mwishowe waja Madina
Wajia kushuhudiya
639
Sasa hapa tugeuze
Yalivyo tuyaeleze
Mambo yasitutatize
Tusijue yetu njiya
640
Tumwa alipo toroka
Makafiri waalika:
Yeyote akimshika
Zawadi ngamia miya
641
Mashujaa' wazatiti
Kuiwania bahati
Yu hai au maiti
Mkononi kumtiya
642
Walijivika libasi
Za vita viso qiasi
Wakawapanda farasi
Na kote wakaeneya
643
Siku tatu zikifika
Tangu pangoni kutoka
Kawafwatia Suraqa
Wa vitimbi na udhiya
644
Aliambiwa walipo
Akatoka papo hapo
Kwa mbio kama upepo
Ili awakate njiya
645
Na popote hajafika
Farasi akaanguka
Akajizoa Suraqa
Naye akaendeleya
646
Na haya yalims'ibu
Mara tatu kwa h'isabu
Alipo fika qaribu
Farasi kadidimiya
647
Suraqa kayayatika
Msamah'a akataka
Na Mtume kamwitika
Mchanga ukamwachiya
648
Suraqa tena kanena:
Nisikize wangu Bwana
Mimi ninajua sana
Diniyo itaeneya
649
Naomba kwako baruwa
Kwa lolote litokuwa
Inilinde na beluwa
Kwa watu wako Nabiya
650
Mimi hapa naa'hidi
Kwa Mola wangu Wahedi
Sitonena na junudi
Hadi mkiwas'iliya
651
Baruwa akaipata
Bila ya shida kupita
Kwani yaliyo mpata
Yalimkifu kifaya
652
Qiasi ya kuwas'ili
Suraqa wamsaili
Kafiri Abu Jahali
Kamshika kila njiya
653
Mwishowe katakalamu:
Yalo nipata a'dhimu
Na mimi nimesilimu
Na wewe nakuus'iya
654
Kanena Abu Jahali:
Ama we ndiwe jahili
Ndio kwanza filh'ali
Wajua huyu Nabiya?
655
Mimi zamani najuwa
Na la kweli natambuwa
Lakini wangu u'luwa
Haunachi kuridhiya
656
Hawa wana wa Hashimu
Washinde zote qaumu?
Kwani sisi Makhazumu
Sisi nao si sawiya?
657
Shujaa' nasi tunao
Ukarimu kama wao
Utume ushuke kwao
Tutampatapi Nabiya?
658
Kwa hivyo sitokubali
Kumwita yeye Rasuli
Tampinga kiqatili
Na haya nakuapiya
659
Basi huo uh'asidi
Wambana hana budi
Hamuoni Muh'amadi
Reh'ema ya watu piya
660
Kugura wetu Rasuwa
Ni mwezi alo zaliwa
Watuwe aliwatowa
Muh'aramu kuingiya
661
Na mwezi wa Muh'aramu
Watufunza Isilamu
Alo tenda Mua'dhamu
Tuifwate yake njiya
662
Madhila tusiyakiri
Tukiona yakithiri
Ni bora tukasafiri
Pumzi kwenda zengeya
663
Ila kama tunaweza
Maovu kuyageuza
Hapo Mola ahimiza
Dhuluma kuipinduwa
664
Mwenye kuacha wat'ani
Kulinda yake Imani
Hutukuzwa na Manani
Na yeye hunus'uriwa
665
Na ikiwa twahajiri
Tusitupe yetu a'ri
Tukumbuke hiyo shari
Lazima tuje ing'owa
666
Aliye kwenda Madina
Na Maka karudi tena
Madhalimu wakaona
Na huku wanyenyekeya
667
Na mwezi huu wa shani
Tukumbuke ikhwani
Aliuliwa Huseni
Kipenzi chake Nabiya
668
Imamu wa mashahidi
Kipenzi cha Muh'amadi
Kauliwa kwa jihadi
Kwa H'aqi kupiganiya
669
Katuwekea ruwaza
Maamuma kuigiza
Khat'uaze kufwatiza
Muhanga kujitoleya
670
Kujitolea muhanga
Ili dhuluma kupinga
Akhera kuna muanga
Na milele kusaliya
671
Twakuombawe Wahabu
Twongoze njia tus'ibu
Aliyo pita H'abibu
Na H'useni nayo piya
672
Maimamu watukufu
Waongozi waongofu
Wazazi wa Masharifu
Wabora walo timiya
MAFUNZO:
Tunaona vipi Imani ya Mtume s.a.w. ya kuamini kuwa Mwenyezi Mungu
daima yu pamoja naye, haikumwondoka hata dakika moja. Imani hiyo ya dhati ndiyo
iliyo mpa nguvu kukabiliana na kila pingamizi, na kila khatari kwa moyo wa
ushujaa na utulivu. Ndani pangoni, yeye na sahibu yake Sayyidna Abubakar r.a.
peke yao alikuwa anajua vilivyo kuwa Mwenyezi Mungu hakumtupa. Hakuyayatika na
kusema, kama alivyo zuliwa Mtume mwengine kutamka alipo kuwa katika hali kama
hiyo, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umenitupa?" Bali aliyo yasema
ni kumpoza rafiki yake kwa kumwambia: "Usihuzunike!
Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi!"
Kuhama, kwa Waislamu kulitokea mwezi wa Mfungo Nne, Muh'arram. Ajabu iliopo
miongoni wanao pinga kusherehekewa kuzaliwa kwa Mtume s.a.w. katika Mfungo
sita, wapo wanao sherehekea kuhama kwa Waislamu kwenda Madina katika mwezi wa
Muh'arram, kwa kuwa ni mwanzo wa mwaka. Na hakika iliyoko ni kuwa mwenyewe
Mtume s.a.w. kafika Madina taarikh 12 Mfungo Sita, siku ile ile aliyo zaliwa.
Ingeli kuwa bora kuisherehekea siku hiyo kwa kuzaliwa na kuhamia. Ama Muh'arram
ni mwezi wa msiba kwa kuuliwa kiqatili mjukuu wake Mtume s.a.w. Sayyidna
Husein.
Tuzingatie vile vile hapa kama Sayyidna Ali alivyo jitolea kuwa badala ya Mtume
auliwe na makafiri, Sayyidna Abubakar ndiye aliye jitolea kuwa na Mtume, mguu
kwa mguu, mpaka pangoni, mpaka Madina, kwa shida zote, na khatari zote, na
shaqawa zote. Masahaba hawa na kama hawa ndio walio usimamisha Uislamu. Yafaa
tuwatukuze wote, kwani kila mmoja ana sehemu yake katika kuipigania hii Dini
takatifu.