Naanza
yangu qauli
Kwa jina lake Jalali
Alomleta Rasuli
Kuiongoa duniya
Reh'ema
zake A'zizi
Zishuke kwa Mwokozi
Kipenzi chake Mwenyezi
Na Aali zake jamiya
Na S'ahaba zake bora
Wenye nyoyo za imara
Walo kwetu ni ishara
Tukisha Mola h'imidi
Na kus'alia H'amadi
Tutaje ya Maulidi
Ya maisha ya Nabiya
Ulimwengu uli kiza
Hauoni muwangaza
Kila jema wapuuza
Maovu wakakamiya
Fikira zilichafuka
Na nyoyo zilitibuka
Ya kweli yalifichika
Urongo ukaeneya
Ulitoweka muruwa
Wabora wajishauwa
H'ata Mola azuliwa
Kuzaliwa na Mariya
Mapadiri na kuhani
Walijijenga yaqini
Ni nani huyo ni nani
Muweza wa kuzuiya
Walijipa utukufu
Reh'ema kuzis'arifu
(Ewe mja mpungufu)
Na dhambi kughufiriya
Nako huko A'rabuni
Kufuru yatia kani
Ndiyo nyumba ya Shet'ani
Ndiko aliko hamiya
Kaa'ba yake Karimu
Alojenga Burahimu
Ikajazwa masanamu
Zaidi thalatha miya
Na kiza kilipo kaza
Alitengeza Muweza
Kuuleta mwangaza
Kwa kuzaliwa Nabiya
Na mwaka tawambiani
Alo zaliwa Amini
Mia tano sabii'ni
Na moja wa shamsiya
Ni mwezi Mfungo Sita
Qarini zilizo pita
Ulimwengu ulipata
Mtume kumpokeya
Mwezi huu mtukufu
Alizaliwa Sharifu
Mjiwe mtakatifu
Maka nchi H'ijaziya
Kazaliwa Muungwana
Na mamiye Bi Amina
Na babiye wetu
Bwana
Alisha mtanguliya
Akatunzwa na babuye
Na khalafu na a'miye
Na walo mlea yeye
Baraka na Saa'diya
Na huyo Mwana Baraka
Ni mama Muafirika
Na Saa'diya pulika
Ni H'alima A'rabiya
Tunalo jifunza katika mlango huu ni kuwa upotovu ukizidi mno ndio huja uwongofu. Waingereza husema: "The darkest hours are just before dawn". Saa za kiza kabisa ni zile za karibu mno na alfajiri. Ndio Muhammad s.a.w. kazaliwa kwa wakati wake. Nasi tutaraji faraji dhiki zinapo shtadi.