713
Alipoona H'abibu
Ni mji wote qaribu
Kati ya wale Warabu
Wamekwisha shuhudiya
714
Kawataka Mayahudi
Waache
Wamrejee Wadudi
Waifwate bora njiya
715
Waache mambo machafu
Yalo watia upofu
Wajifanye manadhifu
Watakase
716
Waingiwe na Imani
Mtume wamuamini
Wamwelekee Manani
Bwana wa wote jamiya
717
Wazitupe khitilafu
Na kila uharibifu
Waifwate ins'afu
Kweli ilo washukiya
718
Kwani kweli waijuwa
Musa alivyo ambiwa
Mtume tateuliwa
Kwa ndu zao A'rabiya
719
Zinatoa ithibati
Zaburi na Taurati
Msitie lenu kati
Na mengine kubaniya
720
Wachache kati ya hao
Khasa hao u'lamao
Wanyooka nyoyo zao
Kusilimu waridhiya
721
Lakini walo kathiri
Walizidi ukafiri
Wafanya wazi na siri
Kumpindua Nabiya
722
Juu ya kuwa Madina
Watu wengi Waumina
Msidhani kuwa tena
Yalikwisha ya udhiya
723
Kwani Shet'ani watuwe
Yafaa haya tujuwe
Hawamwachi apumuwe
Muongozi wa duniya
724
Mangapi wakiyatenda
Ya fisadi na ya inda
Hata lau ninapenda
Siwezi yote wambiya
725
Lakini tayadhukuri
Machache mukhtas'ari
Kama kuwapa nadhari
Mfano yalo tokeya
726
Walikuja watukufu
Wa qabila maa'rufu
Wakamtaka Sharifu
Walimu kuwaidhiya
727
Walidai wana hamu
Watu wao kusilimu
Ili wapate walimu
Wa kuwaonyesha njiya
728
Na Mtume akatowa
Watu sita wano juwa
Na hao wageukiwa
Kwa kamba wawafungiya
729
Kwa kamba wawatatiza
Wende Maka kuwauza
Maqureshi wataweza
Kuwauwa maridhawa
730
Wane walio kataa
Wawauwa kwa fadhaa'
Na wawili walo saa
Maka walis'ulibiwa
731
Hilo jambo la karaha
Kwao ni kuu furah'a
Kuuwa kwao mzaha
Na mateso wachezeya
732
Bwana A'mri kasilimu
Kwa mwenyewe Mua'dhamu
Kasema: Nipe walimu
Nami hapa tasaliya
733
Nipe watu sabii'ni
Wakafunze watu Dini
Tawandikia nyumbani
Kwa wema kuwapokeya
734
Tumwa wetu Muh'amadi
Kheri kamba inazidi
Kumbe wale mashahidi
Si watu wa kubaqiya
735
Aliye pata baruwa
Kinyume alo ambiwa
Akaamuru kuuwa
Kama kuku nakwambiya
736
Walichinjwa hao wote
Pasisalie yeyote
Qiasi kutema mate
Hapana ndudu mmoya
737
Mara ngapi Makafiri
Viunga wavikhasiri
Bilh'adidi-wa-nari
Kuudhi na kuoneya
738
Binti yake Rasuli
Wamtesa Majahili
Kwa fumo achomwa mwili
Pamwe na wake ngamiya
739
Ngamia alo mbeba
Kamtupa Zainaba
Mja mzito na mimba
Na mwishowe kajifiya
740
Na yeye yuwatoroka
Akimbia huko Maka
Babaye anamtaka
Madina akimbiliya
741
Na hao walio tenda
Si wahuni si manunda
Waungwana wa kushinda
Mabwana wa Qureshiya
742
Mara ngapi wazuu'mu
Makafiri kusilimu
Kumbe kuu yao hamu
Wakamuuwe Nabiya
743
Pengine hujia shari
Hugeuka kuwa kheri
Ni kama hii khabari
Ambayo tawelezeya
744
Siku moja huko Maka
Makafiri waso shaka
Waketi wasikitika
Isilamu kwendeleya
745
U'meri akabaini
Laitani si madeni
Na watoto wa nyumbani
Zamani ngejitoleya
746
Ningelikwenda Madina
Muh'amadi kamuona
Kamuuwa nami tena
Haidhuru kuuliwa
747
Na mwenzake kamjibu:
Nenda katende wajibu
Yote uliyo t'ulubu
Mimi nitakuqidhiya
748
Alinena S'afwani:
Enenda wangu mwendani
Kamwondoe duniani
Ano jidai Nabiya
749
Haja zako tazitimu
Tawatazama ghulamu
Deni zako tasilimu
Zote nitakulipiya
750
Akajituta U'meri
Madina akadhihiri
Lakini wetu U'mari
Shaka ikamzidiya
751
Madina akawas'ili
Na upangawe mkali
Na wenye sumu qatili
Maovu kaqus'udiya
752
Kufika msikitini
Kataka ingia ndani
Ana haja na Amini
U'mari kamzuiya
753
Kwanza ampe khabari
Tumwa wake Mukhtari
Inakujia khat'ari
Na mimi nakukhofiya
754
Muh'amadi kamwambiya:
Mwachieni kuingiya
Yupo nasi Maulaya
a
mimi namngojeya
755
Lakini naye U'mari
Mja mwingi wa hadhari
Akamshika hodari
Yeye naye waingiya
756
Mtume akamtaka:
Haja gani unataka?
U'meri akaropoka:
Mwanangu nimemjiya
757
Nimekuju kut'ulubu
Mwana wangu mah'abubu
Alo tekwa kwa h'arubu
Mekuja kumkombowa
758
Ni nini ulilo panga
Hata kwingia kwa panga?
Kauliza wa Muwanga
Mtume wetu Nabiya
759
Kwingia msikitini
Na upanga mkononi
Haya mambo tangu lini
Kwa anaye aridhiya?
760
U'meri akabaini:
Nilikuwa ghaflani
Kanena tena Amini
La kweli utanambiya
761
A'hadi mlo peana
Na hata mkapatana
Pamoja na S'afwana
Na mliyo azimiya
762
U'meri kababaika
Mtume yakimtoka
Mambo yote yalo zuka
Ni kama kahudhuriya
763
Mambo yote babu-babu
Kayaeleza H'abibu
U'meri kataa'jabu
Na hapo kaangukiya
764
Ikamtoka qauli:
Nashuhudia kikweli
Kwamba wewe ni Rasuli
Na Mngu wetu Mmoya
765
Tangu hapo huyo Bwana
Akawa na Sayidana
Ni watu wano pendana
Na Isilamu jamiya
766
Ni hayo na yalo fana
Yawapata zetu bwana
Walio kuwa Madina
Wamemfwata Nabiya
MAFUNZO:
Tuone na tusistaajabu tukiona nasi tukitokea kuhama nchi kwa ajili ya
dhulma na mateso, na kukimbilia nchi nyengine, tukaona wale madhaalimu tulio
wakimbia wakatufatia huko huko uhamishoni kwa ajili ya kuendeleza madhila yao,
na fitna zao. Huo ndio mwendo wa makafiri na wanaafiqi, ambao wamefanya dhulma
ndio biashara yao. Tunakumbuka vipi kiongozi wa dhulma alivyo kuwa akijitapa
kwa kusema kwa kutishia: "Mkono wangu mrefu unafika hata huko
waliko." Yaani mkono wake ulio jaa damu anaweza kuwauwa hao walio ondoka
popote walipo kimbilia. Lakini:
Akushutao mama sihutuke
Yupi awezao kukwetea lake
Watu wana yao Mungu ana yake
Anaye dai kuwa mkono wake mrefu, siku yake ikifika hutambua kuwa hata kujikuna
hawezi.