19
Qaribu Tumwa kuzawa
Babuye alitongowa
Mwanangu mali chukuwa
Shamu nenda kutembeya
20
Ukafanye bia'shara
Na upatapo tijara
Itakuwa ndio bora
Kwa mwana akizaliwa
21
Tutaifanya karamu
Tumshukuru Karimu
Ukimzaa Hashimu
Ni baraka ya dhuriya
22
Na kumbe hiyo ajali
Na baba yake Rasuli
Wangojana huko mbali
Ajali yamngojeya
23
Alipo kuwa njiani
Anarejea wat'ani
Aliitwa na Manani
Na yeye kamwitikiya
24
Alitawafu Madina
Kana kwamba ni kunena:
Namtangulia mwana
Apate pa kufikiya
25
Mwana wangu mtukufu
Yapasa nimsharifu
Atapo kuja tawafu
Nipate kumpokeya
26
Na hivyo yalivyo jiri
Katawafu Mukhtari
Madina Lianwari
Ndiko aliko jifiya
27
Alipo zawa Hashima
Alikuwa ni yatima
Amina ni wake mama
Ndiye aliye saliya
28
Na babuye ni shaibu
Bwana Abdul Mutt'alibu
Furaha yake a'jabu
Kijana akimjiya
29
Mzee kajikongoja
Mpaka nyumba ya H'ija
Wah'ijapo wote waja
Na mwana kajibebeya
30
Kangia naye Kaa'ba
Akatoa mat'ilaba
Kaomba Mola kwa h'uba
Kumuombea s'abiya
31
Kaomba kwa mashai'ri
Laini kama h'ariri
Akimwombea s'aghiri
Mtoto alo mjiya
32
Baa'da kupita juma
Aliandaa walima
Akawaalika umma
Kula na kufurah'iya
33
Hiyo basi ni awali
Maulidi ya Rasuli
Ishike hii qauli
Ishike ishikiliya
34
Maulidi si uzushi
Na tuuwache ubishi
Ni Suna ya Maqureshi
Na Mtume karidhiya
35
Aanzae suna njema
Ujira wake ni mwema
Hadi Siku ya Qiyama
Mtume katuambiya
36
Na ovu mwenye kuzuwa
Ataipata beluwa
Si kwa kuwa hayakuwa
Bali shari katwachiya
37
Hebu soma Qur'ani
Utaona yabaini
Waambiwa Waumini
Mtume
kums'aliya
38
Na Mtume kums'ifu
Ni amri takatifu
Kaanza Mola Lat'ifu
Na sisi tunafwatiya
39
Na Mola wetu Muweza
Katuwekea Ruwaza
Tupate kumuigiza
Mwenye bora ya t'abiya
40
Na pia katuus'iya
Mtume kums'aliya
Na tena kusalimiya
Waumini sote piya
41
Moletu alo tukuka
Amenena bila shaka
Wa Rafaa'na
laka dhikraka
Na akumbukwe Nabiya
42
Basi haya Maulidi
Kataka Mola Wadudi
Na sisi hatuna budi
Moletu kumwitikiya
43
Wacha nyoyo zifurah'i
Tusilete ikrahi
Kwa nee'ma ya Ilahi
Aliyo tujaa'liya
44
Na kama wataka sifu
Mpezio mtukufu
Kwa nini sipige dufu
Na rika za kutimiya
45
Na hiyo tena ni Suna
Ya S'ahaba wa Madina
Wakimpokea Bwana
Alipo wafikiliya
46
Lakini nasema basi
Tusikiuke qiyasi
Tukayaleta maa's'i
Katika kufurah'iya
47
Tufurah'i kwa h'ishima
Hili sio lelemama
Wala si kama ni ngoma
Maulidi ya Nabiya
48
Na uwe mnyenyekevu
Tenda mambo kwa wekevu
Usifanye upotovu
Ukaipotea njiya
49
Kwa maneno na vitendo
Na kuufwata mwenendo
Na tuonyeshe mapendo
Kwa Bwana wetu Rasuwa
50
Kama kweli twampenda
Mwenyezi alo tuunda
Yatubidi kuyatenda
Alo tufunza Nabiya
51
Tusiwe tuso a'qili
Tukaifanya thaqili
Hii Dini ya Rasuli
H'ata ikatuemeya
52
Hii Dini ni nyepesi
Na haina wasiwasi
Mambo yake ni qiasi
Na sote twashuhudiya
53
Tusiitie vikwazo
Kwa kuzua kwa mawazo
Tukaileta mizozo
Isiyo na as'iliya
54
Ni nani
mkanya mema
Tulo pewa ni nee'ma
Jamani hivyo si vyema
Vizuri kuvibaniya
55
Maulidi si h'aramu
Kumsifu Mua'dhamu
Wala kufanya karamu
Na watu wakajiliya
56
Wakala walo amini
Pamwe na wao wageni
Fuqara na masikini
Wamshukuru Jaliya
Tunajifunza katika mlango huu kwamba hapana
njia ya kusema kuwa kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume s.a.w. ni Bida', Uzushi,
kwa maana ya kuwa inakwenda kinyume na Dini ya Kiislamu. Bali ikiwa ni jambo
lilio anzishwa basi litakuwa katika Sunnatan Hasanah. Wataalamu wa kutegemewa
sio wenye kukusanya ilimu tu, bali wale ambao pia wanatumia akili zao na
wanatambua lilio bora kulifanya kwa wakati wake na pahala pake. Sherehe za
Maulidi ni njia kubwa ya kueneza kwa watu wa kila namna wamjue Mtume s.a.w. na
mwendo wake ili wapate kumfuata.