8   MATESO

267
Siku moja Mursali
Kaambiwa na Jalali
Upinzani usibali
Watangaziye duniya

268
Tangaza nilo amuru
Alimwambia Ghafuru
Siku hiyo ndiyo Nuru
Izagae kote piya

269
Tumwa naye simuhuli
Hapo hapo kaa'jili
Akalendea jabali
La S'afaa kalikweya

270
Akaweta waungwana
Wakaja wanasongana
Akawambia: Nanena
Na nyinyi mnasikiya

271
Akauliza: Qureshi
Mtaufanya ubishi
Nikinena kuna jeshi
Nyumani linatujiya?

272
Wakanena: Twakubali
Akajibu Mursali:
Vipi hivyo kuwa kweli?
Ni nani ashambuliya?

273
Mnajua tangu kale
Hapana yeyote yule
Awezae kuja mbele
Maka kuja twingiliya

274
Huu mji mtukufu
Hakunaye mpotofu
Akajipaka uchafu
H'arubu kutuleteya

275
Wakajibu: Twaamini
Ukinenawe Amini
Twajua tangu zamani
Urongo hujatwambiya

276
Tena hapo katongowa
Kipenzi chetu Rasuwa:
Niaminini ya kuwa
Ndi Mtume wa Jaliya

277
Nimetumwa kuwajuza
Na Mola wetu Muweza
Mas'anamu kupuuza
Mngu wenu ni Mmoya

278
Haya yangu ms'adiqi
Mfwate Dini ya Haqi
Na kubwa la washiriki
Likazuka lavamiy

279
Ni huyo Abu Lahabu
Ndilo makhuluqu tabu
Liso mjua Wahabu
Kafiri lilo bobeya

280
Hili kubwa la Kufari
Ni a'miye Mukhtari
Ndiye mchimvi wa shari
Kumchimbia Nabiya

281
Likamtusi A'zizi
Likamwita: Mpuuzi
S'ubira yake Mwenyezi
Mbora kuvumiliya

282 Akamtaka S'aburi
Mtumewe as'ubiri
Na hilo tatiwa nari
Litakuja angamiya

283
Vituko vyake a'jabu
Huyo Abu Lahabu
Kamkutisha a'dhabu
Sayidi wetu Nabiya

284
Akitesa Isilamu
Akiona ni utamu
Kuwadhili binadamu
Kwa kufwata njema Njiya

285
Na mkubwa wa Juhali
Mwengine Abu Jahali
Huyo khabithi qatili
Ameshinda watu piya

286
Na wako na wengineo
Walio pita upeo
Ole wao Ole wao
Kwa walio tutendeya

287
Hao wakuu wa Nari
Walikaa kudabiri
Wakutishe kila shari
Dini mpya ilo ngiya

288
Wawezao kums'ibu
Wampe nyingi a'dhabu
H'ata mwisho atatubu
Kufuruni tarejeya

289
Mwenye nguvu na u'luwa
Wafanye kumbeuwa
Atakaye kununuwa
Wakatae muuziya

290
Bwana wetu Bubakari
Dini ilipo dhihiri
Alikwenda kukhubiri
Msikitini kangiya

291
Majahili wambaka
Ikawa ni pata shika
Wamkutisha mashaka
Chini wamkanyagiya

292
Kutoka hapo tiati
Akabebwa kitikiti
Si yu hai si maiti
H'ali naye kazimiya

293
Na Bwana wetu Bilali
Muadhini wa Rasuli
Yalo mpata muh'ali
Kuweza yasimuliya

294
Yule mwana wa Khelefu
Kamtesa mtukufu
Akabaki kama mfu
Mateso kumzidiya

295
Akatatizwa makamba
Wabururwa huo mwamba
Na watoto wamuimba
Na huku wamzomeya

296
Huwekwa kutwa juani
Bila ya nguo mwilini
Na mjiwe kifuani
Wa moto wambabua

297
Aambiwa na Kafiri:
Rejea kwetu ukiri
Jawabu ni kukariri:
Ah'adu ndiye Mmoya

298
Aambiwa: Takuuwa
Ah'adu anatongowa
Mpaka akamwopowa
Abubakari sikiya

299
Katika Waafirika
Bilali ametukuka
H'adhi yake imefika
Kwa walimwengu jamiya

300
Kwani mwenyewe Amini
Kamfanya Muadhini
Wa
kwanza wa Waumini
S'alati kulinganiya

301
Na wengine Isilamu
A'dhabu yao a'dhimu
Kuelezea vigumu
Yaliyo kiwafikiya

302
Kwa moto walo uliwa
Na macho kutofolewa
Matumbo kupasuliwa
Na huku wavumiliya

303
Mateso kiwa thaqili
Hwenda hurusha a'qili
Lakini hawakubali
Kufuruni kurejeya

304
Babiye Bwana A'mari
Kababuliwa kwa nari
Na mamiye wakhiari
Kwa madonda kuuliwa

305
A'mari akabaqiya
Mamiye katanguliya
Wa kwanza kushuhudiya
Umati Muh'amadiya

306
Kama qabila wataka
Ni Mama Muafirika
Yamani Mume katoka
Na Mama etwa  Sumaya

307
Alo muuwa qatili
Ni huyo Abu Jahali
Akawa ndiye awali
Wa Peponi kuingiya

308
Nimekupeni mithali
Si mingi bali qalili
Mifano ya uqatili
Walio wakitendewa

309
Hao watu Mashahidi
Kwa Dini yao shadidi
Ikawa hapana budi
Kufari kuzingatiya

310
Ikawapasa wawaze
Mbinu gani wageuze
Ili wapate waweze
Hii Dini kuzuwiya

311
Wakaizua shauri
Wamwendee Mukhtari
Wamsemeze vizuri
Aache wake udhiya

312
Na wa kwenda nena naye
Wamchagua mzee
Na jinale niwambie
U'tuba bin Rabia'

313
Akaambiwa Mtume:
Nisikize mwanamume
Haya mambo uyahame
Nimekuja kukwambiya

314
Umekuja tufitini
Kila mtu na mwendani
Twabaki hatujuani
Kwa Dini uliyo zua

315
Watu wetu wagombana
Baba hamjui mwana
H'ishima tena hapana
Sababu wewe wajuwa

316
Sasa wewe ukhiari
Unataka utajiri?
Tutafanya tadibiri
Mali mengi kukweteya

317
Kama wataka tawala
Hilo jambo ni sahala
Ni sasa bila muhula
Sisi ni wako raiya

318
Unataka uraisi
Hilo ni jambo jepesi
Watu wote hata sisi
Tutakuja kwitikiya

319
Kama haja mwanamke
Tafadhali mtamke
Yeyote usishituke
Tutakuja kuleteya

320
Kama unayo maradhi
Mwanangu niwie radhi
Tutafanya la faradhi
Mganga atakujiya

321
Na huyo wako shet'ani
Alo kwingia kichwani
Wachawi wanachuoni
Waweza kumchomoa

322
Myungu yetu ya kijadi
Uiache Muh'amadi
Watuudhi mno h'adi
Unapo ishambuliya

323
Mtume akamjibu:
Nisikize ewe babu
Hayo yote sit'ulubu
Na wala sikuwaziya

324
Mimi langu jambo moja
Na kwa hilo nimekuja
Niwafunze wote waja
La h'aqi kuandamiya

325
Nimekuja kufikiza
Dini ya Mola Muweza
Na sitaraji majaza
Ila kwa Mola Jaliya

326
Mimi kweli nitakalo
Ni jepesi jambo hilo
Mnachie nitendalo
Ujumbe kutimiziya

327
Kushindwa walipo ona
Wakaondoka mabwana
Wakenda kwa muungwana
Mzee wake Nabiya

328
Na huyo Abu T'alibu
Ni a'mi yake H'abibu
Wakenda kumt'ulubu
Amsemeze Rasuwa

329
Na aache wako mwana
Myungu yetu kuikana
Au twache kuyafanya
Tunayo yaqus'udiya

330
Kupita siku i'dadi
Waona mambo kuzidi
Azidisha Muh'amadi
Diniye kutangaziya

331
Kwa Mzee wakarudi
Wakanena: Huna budi
Umzuie waladi
Au vita twanadiya

332
Tutakupiga na wewe
Na alio pamwe nawe
Atanena na mwanawe
Ni hayo alo wambiya

333
Haya mambo ni mazito
Wala qatt'u si matoto
Aliona kama moto
Moyoni unamwingiya

334
Akamwambia Rasuli:
Usinipe uthaqili
Niso weza kuhimili
Mwanangu nikachukua

335
Tena hapo Mukhtari
Machozi yataka jiri
Waweza kutas'awari
Kuh'isi kwake Nabiya

336
Akamwambia: Babangu
Haya mambo siyo yangu
Nda Mwenyewe Bwana Mungu
Mimi ninatumikiya

337
Kama watu wakushinda
Na huwezi kunilinda
Hapana la kulitenda
Ila basi kwendeleya

338
Na Wallahi ninaapa
Lau kama wangenipa
Jua mwezi hapa hapa
Siliachi nilo jiya

339
Siliachi jambo hili
Ila apende Jalali
Akajibu Babe A'li:
Mwanangu nakuachiya

340
Mwanangu nino kupenda
Tenda utalo litenda
Sitoacha kukulinda
Wallahi nakuapiya  

MAFUNZO:

Katika sifa kubwa ambayo mwanaadamu yafaa awe nayo ni SUBIRA. Subira huvuta kheri. Kuteswa, kunyanyaswa, kuuliwa, kufungwa, kupokonywa chako - yote hayo ndio mambo ya dharura ya kumpata kila anaye pigania haqi. Yalimpata Mtume Muhammad s.a.w. Na yaliwapata Mitume wote, na yamewapata wote walio tetea haqi.  Lakini mwishoe HAQI ndiyo itakayo kuja shinda.