24   KWA KHERI

1189
Aliyo khofu Bakari
Ni hivyo yalivyo jiri
Alitawafu Bashiri
Robo mwaka ukisiya

1190
Kurudi kutoka Maka
H'aliye yadhoo'fika
Kila siku inashuka
H'ata mwisho yamwemeya

1191
Maradhi aliyo mpa
Molawe yalimtupa
Ndiye Yeye wa kutupa
Ndiye Yeye wa kutwaa

1192
Hivyo hivyo ni mgonjwa
Na yeye hujikongoja
Kuzitenda zake h'aja
Za utu na Unabiya

1193
Mzigo wawa thaqili
Aliamuru Rasuli:
Bubukari naas'ali
As'alishe namwambiya

1194
Na siku moja jioni
Ajikongoja Amini
Afika msikitini
Watu wesha jis'aliya

1195
Kwisha s'ali kaeleza
Kwamba Molake Muweza
Mtu alimuuliza:
Waikhiari duniya?

1196
Na mtu hakuqas'iri
Akamjibu Ghafari:
Kuja kwako nakhiari
Ulimwengu nasusiya

1197
Bubakari kafahamu
Madhumuni ya Hashimu
Akaona ni vigumu
Kilio kukizuiya

1198
Akasema kwa uchungu:
Ewe Mtume wa Mungu
Roh'o yangu na wenzangu
Kwako wewe ni fidiya

1199
Tena Mtume kanena:
Wema wake huyu bwana
Washinda ajmai'na
Kwa mali na nafsiya

1200
Enyi wangu Wahajiri
Watunzeni Ans'ari
Vyangu vipenzi khiyari
Ni kwao twakimbiliya

1201
Awatendao h'isani
Huyo mema mlipeni
Na pia msameh'eni
Awatendao mabaya

1202
Tena hapo akarudi
Bwana wetu Muh'amadi
Hakutoka ila h'adi
Siku aliyo zaliwa

1203
Ni siku ya Maulidi
Alifika masjidi
Na watu wai'taqidi
Kaziye atarejeya

1204
Kwisha S'ala kumaliza
Abaqi azungumza
H'adi jua kuchomoza
Na saa zikapitiya

1205
Katika aliyo nena:
Usoni kuna fitina
Na zikisha zipo tena
Na mengi aliwambiya

1206
Ya mwisho yake qauli:
Ya h'aramu na h'alali
Kabisa sikubadili
Kitabu chavyo twambiya

1207
Sinalo la kuongeza
Sinalo la kupunguza
Mwengine akigeuza
Huyo amenizuliya

1208
Alipo rudi nyumbani
Kawa tena taa'bani
Akamwita Rah'amani
Na yeye kamwitikiya

1209
H'ali huku atawafu
Anena wetu Sharifu
Kwa Rafiqi Mtukufu
Hivi sasa namwendeya

1210
Na walio mzunguka
Wakeze wat'ahirika
Naye A'li hakutoka
Kimuuguza Nabiya

1211
Ni yeye na Bi Fat'uma
Kwa upole na huruma
Mtume wamtazama
H'ata mwisho kajifiya

1212
Watu wote wadawaa
Watu wote washangaa
Kuliingia fazaa'
Madina yote jamiya

1213
Bwana A'li hajiwezi
Apigwa na bumbuwazi
Wengine kama wa juzi
Wamekwisha ng'ang'anaa

1214
Shujaa' Bwana U'maru
A'qili zilimduru
H'ata mwisho akufuru
Akanya kufa Nabiya

1215
Aliufuta upanga
Anena: Nitamtwanga
Yeyote ataye pinga
Haya ninaho wambiya

1216
Alinena: Ni muh'ali
Kutawafu Mursali
Na Usilamu ungali
Bado kwenea duniya

1217
Bubakari kiwas'ili
Nyumbani akadukhuli
Kamfunua Rasuli
Usoni kamnoneya

1218
Uso wake una nuri
Wanukia kwa u't'uri
Amuona ni mzuri
Kama walivyo zoeya

1219
Kanena: Sisi shahidi
Kwamba wewe Muh'amadi
Alo kutuma Wadudi
Yote umetimiziya

1220
Na amana ya Karimu
Na h'aqi za wanadamu
Zote hizo ni timamu
Na sisi twashuhudiya

1221
Amani za Mola wetu
Na pia na Rah'amatu
Zishuke kwako mwenzetu
Bukrata wa a'shiya

1222
Alipo toka nyumbani
Kafuza msikitini
Akapanda mimbarini
Na watu kakhut'ubiya

1223
Aliwambia rijali:
Amwabudie Rasuli
Ninawambia la kweli
Muh'amadi kapitiya

1224
Lakini mwenye nadhari
Kumua'budu Qahari
Na zingapita dahari
Moletu atabaqiya  

1225
Akasoma Qur'ani
Aya inayo baini
Kutawafu kwa Amini
Na hii nawasomeya

1226
Na nyinyi jama pimeni
Kitabu hichi ni gani
Kila kitu mbayani
Hapana kilo saliya?

1227
Hapo wote wakajuwa
Kwamba kweli yalo kuwa
Kipenzi chao Rasuwa
Amekwisha tanguliya

1228
Ni Mitume wote wale
Wa zamani zile kale
Hawakuishi milele
Wote walisha jifiya

1229
U'mari kajua kweli
Zikamtua a'qili
Karegea wote mwili
Hawezi kujiinua

1230
Na mama yetu Baraka
Alia asikitika
Anena: Zimekatika
H'adithi za samawiya

1231
Na wapi tutayapata
Kama haya yalo pita?
Mwenyezi Mngu kakata
Aliyo akimwambiya

1232
Huu ms'iba thaqili
Uso kuwa na mithali
Kufa wetu Mursali
Shafii' wa watu piya

1233
Liliwele hali budi
Kutawafu Muh'amadi
Ni kwake Yeye Wadudi
Ndiko aliko kwendeya

1234
Huko sote twakutana
Inshalla tutaonana
Tumuone Sayidana
Kipenzi chetu Nabiya

1235
Na huko tatuongoza
Mbee za Mola Muweza
Tupate yetu majaza
Akhera kama duniya

1236
Sasa hapa twakhitimu
Tums'alie Hashimu
Na S'ahaba mah'ashumu
Na ali zake jamiya

1237
Atuwezeshe Muweza
Kufwata hiyo Ruwaza
Mtume alo maliza
Risala ilo timiya

1238
Wa kwanza wa utukufu
Na kwisha ndio kuqifu
Baa'da yake Sharifu
Hatuh'itaji nabiya

1239
Wano dai nawaseme
Wanaodai ufalume
Wanodai na utume
Si kama waufikiya

1240
Adaivyo ni mzushi
Kudai kwake ubishi
Nao ubishi hawishi
Ndio a'da ya duniya

MAFUNZO:

Mauti ni faradhi. Kila kitu kitateketea ila Mwenyewe Muweza. Mtume Muhammad s.a.w. Mpenzi wetu, Mwongozi wetu amekufa. Lakini ni kiwiliwili chake kilicho kufa. Mafunzo yake yako milele, hayafi. Katwachia Qur'ani na Mwenendo wake. Waajibu wetu tumsome mtu huyu wa ajabu. Kumjua mtu huyu ni mafunzo kwa kila mwanaadamu. Kwake yeye tunapata uwongozi ambao hatuwezi kuupata popote penginepo.