767
Udugu wa Waumina
Walio kuwa Madina
Mfano wake hapana
Tangu kuumbwa duniya
768
Na sote tunamaizi
Kwamba wale wakimbizi
Walikuwa hawawezi
Lolote kujitendeya
769
Walipo acha makwao
Walitupa kila chao
Wabaqi na nguo zao
Mwilini walizo jiya
770
Walikuja kwa Lillahi
Si kuyajia ya jahi
Wakabeba makruhi
Kuitafuta h'uriya
771
Kwa uh'uru wa i'bada
Wakubali kila shida
Wakimbia zile inda
Za wale Majahiliya
772
Na huku Ma-Ans'ari
Kwa kila jema na kheri
Wakawapa Wahajiri
Vitu vyote bisawiya
773
Wakawapa
Kila kitu pande mbili
Na wenye wake wawili
Na hao wawagawiya
774
Walikuwa na usawa
Usawa uso na towa
Huwezi kumtambuwa
Faqiri na aghaniya
775
Mwenendo huu mtamu
Wanga nao Isilamu
Mgeni kumkirimu
H'ishima kumfanyia
776
Twashukuru hata leo
Ni wengi tuwaonao
Kamayo wayatendao
Lillahi wajitoleya
777
Lakini wako qalili
Wavunjao jina hili
Wasahau ya as'ili
Dini ilivyo anziya
778
Yafaa tujisemeze
Mazuri tujizoeze
Maovu tusokomeze
Tuache mbovu t'abiya
779
Ni s'ifa ya Isilamu
Kukithiri ukarimu
Kwa mnyonge urah'imu
Mgeni kumpokeya
780
Khas'a huyo mkimbizi
Ndiye mgeni a'zizi
Apendwaye na Mwenyezi
Ni Suna yake Nabiya
781
Atazamwe kwa huruma
Alo kimbia dhuluma
Ana mengi yamuuma
Huwezi kuyaqisiya
782
Tukumbuke si muhali
Mambo kwenda kubadili
Mwenye leo leso mbili
Kesho moja kuzengeya
783
Tuujue ukosefu
Si wa mtu maa'rufu
Kila mtu maus'ufu
Kupata na kukoseya
784
Si a'jabu wewe leo
Wachezea chako cheo
Kesho uko kwa mwenzio
Riziqi wairondeya
785
Sasa hapa tayanena
Yaliyo kuwa Madina
Watu wote jamii'na
Mtume wamwitikiya
786
Hata hao Mayahudi
Wakawa hawana budi
Kumwendea Muh'amadi
Wakiwa nayo qadhiya
787
Akawa yeye h'akimu
Pasiwe wa kudhulumu
Kafiri na Isilamu
Hukumu
788
Na hayo kayasomeni
Isemavyo Qur'ani:
Sihukumu nuqus'ani
Kwa mtu kumchukiya
789
Lakini wale wabishi
Majeuri Maqureshi
Wakaona hayat'oshi
Isilamu kukimbiya
790
Watoka huko waliko
Kuwaletea vituko
Na mingi misukosuko
Mekwisha waelezeya
791
Wakatoka kwao Maka
Na Madina wakafika
Mateka wakiwashika
Na kuharibu mimeya
792
Wakizitia fitina
Huko nje ya Madina
Maqabila mengi tena
Wakawa wayachocheya
793
Ikawa Waisilamu
Hawana la tabasamu
Kwani ni wengi qaumu
Ambao wawachukiya
794
Tena Mwenyezi Qahari
Akaona ni khat'ari
Watu wake mahaqiri
Watakuja angamiya
795
Ni nani wa kutangaza
Huu mwenge wa mwangaza
Likisha ingia
Hawa wakaangamiya?
796
Huu Utume wa mwisho
Sileti mwengine kesho
Itakuwa sikitisho
Na ms'iba wa duniya
797
Sioni kuwa wekevu
Bali huo upotovu
Kutoa la pili shavu
Ni nani atasikiya?
798
Huu wakati wa kweli
Wa Muh'amadi Rasuli
Jambo lilio muh'ali
Si Mie wa kuwambiya
799
Akaona aweleze
Wasimame wajikaze
Watu wake wajiweze
Haqi kuipiganiya
800
Ruhusa akaitoa
Ya mja kujigomboa
Dhuluma kuiondoa
Na nguvu kuzitumiya
801
Akaamuru Wadudi
Kumwambia Muh'amadi:
Sasa pigana Jihadi
Na anaye kuoneya
802
Mtu anaye jilinda
Mtu huyo nampenda
Akishindwa akishinda
Peponi nitamtiya
803
Lakini mwenye kuanza
Uchokozi kufanza
Mtu huyo tamtanza
Kwa kuwa amevamiya
804
Walo fukuzwa mijini
Bila kitu nuqus'ani
Ila kuwa Waumini
Ni h'aqi kujiteteya
805
Walo pokwa vitu vyao
Wakachinjwa watu wao
Watendeje watu hao?
Jawabu naingojeya
806
Na wengine mah'aqiri
Wasoweza kusafiri
Wafanyiwa ujeuri
Hawawezi kukimbiya
807
Hao watu madhulumu
Basi kwao si h'aramu
Kupigana na qaumu
Walio leta udhiya
808
Lakini wakikubali
Kuacha hichi qitali
Hima hima simuhuli
Suluh'u kukubaliya
809
Dini jambo la khiari
Halih'itaji qahari
Lakini usis'ubiri
Dhuluma ikaeneya
810
Dhuluma kama mtoto
Ichanatwe kwa ufito
Ikiona uchonoto
A'qili zitatuliya
MAFUNZO:
Haikuwa wepesi kwa Mtume s.a.w. kuingia vitani kwa ajili ya kujilinda
na kwa ajili ya kuilinda Haqi. Lakini ilipo kuwa ni lazima, hakusita ila
alifanya kwa kila alilo weza kuipinga dhulma kwa kutumia nguvu. Kwa muda wa
miaka kumi na nne alistahamili kila maonevu, na kila madhila. Katukanwa,
kafukuzwa, kauliwa watu wake, kanyang'anywa kila chake, na mwisho katolewa
kwao. Naye kastahamili yote. Ni mwisho tena ilipo kuwa hapana hila ila
kujitetea, ndio akapewa ruhusa na Mwenyezi Mungu apigane na ajilinde kwa ajili
ya kuipinga dhulma.