20   VITA VYA HANDAKI

951
Sasa hivi naturudi
Huko Madina biladi
Tutazame Mayahudi
Vitendo vyao na niya

952
Mtume wetu karimu
Daima awah'ishimu
Akiwaita isimu
Ya h'ishima na muruwa

953
Aliwaita H'abibu
Enyi Watu wa Kitabu
Hakuwapa chembe tabu
Kufwata yao shariya

954
Na mno kasisitiza
Kwa wema kuwasemeza
Ni mno akikataza
Kuwatendea udhiya

955
Lakini yao fadhila
Ni kufanya kila h'ila
Kumchimba Mursala
Maovu wanuiliya

956
Walipoona Uh'udi
Alishindwa Muh'amadi
Wakaona Mayahudi
Wakati umeadiya

957
Sasa huu ni wakati
Wa kutengeza umati
Wapange wajizatiti
Kumvuruga Nabiya

958
Wakatoka watu wao
Watukufu wenye vyeo
Ni khamsa kubarao
Maqureshi wawendeya

959
Wakasema waa'dhamu:
Tuna mpango mtamu
Kuwasaga Isilamu
Kufumba na kufumbua

960
Sasa wao taa'bani
Tujiunge ikhwani
Tukusanye na wendani
Tuwasage mara moya

961
Tafuteni as'ih'abu
Na sisi tutat'ulubu
Na wengine Waa'rabu
Tuwe sote tu pamoya

962
Na sisi tulio ndani
Ni mchwa wa chini chini
Twaupekecha wat'ani
Siku yetu twangojeya

963
Tunao wetu rafiki
Wawaita wanafiqi
Sisi tunawas'adiqi
Kwa letu watusikiya

964
Na siku itapo fika
Na majeshi yakashuka
Sisi hapo tutazuka
Kwa ndani kushambuliya

965
Maqureshi wakasema:
Hilo ni shauri jema
Tutafanya hima hima
Hilo mlilo lijiya

966
Wakapeana mia'di
Ya kukutana junudi
Wakatoka Mayahudi
Wakashika yao njiya

967
Wakafika majangwani
Kwao Bani A't'afani
Na wao kuwarubuni
Njama zao kuingiya

968
Tena hao maqubeli
Hawakutoa qibali
Mpaka kwa mengi mali
Baa'dhi waliridhiya

969
Alipo pata khabari
Bwana wetu Mukhtari
Watuwe kawashauri
Kwa hayo yalo tokeya

970
Wakapigwa mshangao
Zaemewa bongo zao
Kazuka mmoja wao
Muajemi nawambiya

971
Huyo Bwana Salmani
Alikuwa Nas'rani
Na khalafu kaamini
Kubai'thiwa Nabiya

972
Mwanafunzi wa Bahira
Aliye toa bishara
Ni s'ah'aba wa bus'ara
Mtume kamsikiya

973
Kanena huyo rafiki:
Natulichimbe handaki
Na hilo halipitiki
Hawawezi kutujiya

974
Hii ni rai jadidi
Haijui Muh'amadi
Furaha yake shadidi
Mambo yalipo mweleya

975
Hilo shimo likachimbwa
Na huku nyimbo zaimbwa
Na huku Mungu aombwa
Nus'ura kuwaleteya

976
Huku hali wanachimba
Wakakutana na mwamba
Mtume wakamuomba:
Ni jiwe latuemeya

977
Mtume kateremka
Na mtarimbo kashika
Kapiga pakametuka
Kusini kuelekeya

978
Mtume akatamka
Yamani yatuitika
Karibuni bila shaka
Na hayo ninawambiya

979
Mara nyingine kagonga
Pakachomoza muanga
Kaona hata mjinga
Kaskazi waendeya

980
Tumwa tena ka
kabiri

Akanena: Nabashiri
Kaskazi ya Nasari
Itakuja twandamiya

981
Mara ya tatu kupiga
Jiwe akalivuruga
Nuru pale akimega
Shariqi yachomozeya

982
Na Mtume kakariri
Ile yake takbiri
Kanena bila kiburi:
Ajemi yashuhudiya

983
Na hayo mambo yazuka
Kama Tumwa kutamka
Nchi hizo zawitika
Wito wa Muhamadiya

984
Kwa mpango huo huo
Alo nena mwenye cheo
Ndiye huyo anenao
Akinena neno huwa

985
Kuchimba wakimaliza
Wamshukuru Muweza
Wabaki wajitengeza
A'dui kumngojeya

986
Hata kwisha Ramadhani
Waona vumbi angani
Wakitazama kusini
Wageni wawajiliya

987
Ni arbaa'ta alaafu
Maqureshi watukufu
Lakini ni wapotofu
Waja mji kuvamiya

988
Hapo hapo wawas'ili
A't'afana Majahili
Lajipanga jeshi hili
Kaskazi shariqiya

989
Na hao watu matata
Wafika elfu sita
S'afu zao zilikuta
Zile za Maqureshiya

990
Ni hao elfu kumi
Waja msaga Mtumi
Ambaye wake qaumi
Elfu tatu kwishiya

991
Tena bado huku ndani
Wapo watu makhaini
Mayahudi maluu'ni
Walo zua yote haya

992
Wangojea siku yao
Ndiyo hii hii leo
Waqidhi muradi wao
Hawa wana wa hizaya

993
Maa'dui wakifika
Nyoyo zao zashituka
Shimo lilivyo zunguka
Hapana pa kupenyeya

994
Ikawa watazamana
Isilamu na watwana
Wabaki wapopoana
Mishale ya kutupiya

995
Mmoja mja mashaka
Alijaribu kuruka
Shingoye ikavunjika
Shimoni katumbukiya

996
Kati ya hao junudi
Kuna shujaa' shadidi
Etwa A'mru Abdu Wudi
Na mwanawe naye piya

997
Ni hao watu wawili
Na Mwana Abu Jahali
Waliruka shimo hili
Na huko wakachupiya

998
Walipima wakaqisi
Wakaruka kwa farasi
Waja waso wasiwasi
Vita wamevizoweya

999
A'mru akajinaki:
Ni nani wakunilaqi
Au nambe hamtaki
Papano kunitokeya

1000
Bwa A'li kainuka
Mtume kenda mtaka
A'mru kumuitika
Kwa anayo waitiya

1001
Mtume kamkataza
Watu wote wanyamaza
A'mru akaongeza
Kuringa na kupaniya

1002
Akazidisha maneno
Hata mwisho yawa mno
A'li asiye kifano
Hakuweza jizuiya

1003
Akanena Bwana A'li:
Ewe wa Mngu Rasuli
Nakuomba jambo hili
Na Mtume kamwachiya

1004
Walipo qabiliana
Na nyuso zikaonana
Bwana A'li alinena:
A'mru wanisikiya?

1005
Kumbuka yako qauli
Kwamba hutakwi mawili
Ila moja wakubali
Kwa hilo waitikiya?

1006
Aliponena: Naamu
Kasema wetu Imamu:
Nakutaka usilimu
Umkubali Nabiya

1007
A'mru akabaini:
Siitaki yenu dini
Basi haya shuka chini
Bwana A'li kamwambiya

1008
A'mru hapo kanena:
Kukuuwa ewe mwana
Sitamani mimi tena
Mwengine namzengeya

1009
Kajibu nduye Amini:
Kukuuwa natamani
Teremka hapa chini
Au nambe wakhofiya?

1010
A'mru kakasirika
Na farasi kamshuka
Na mapovu yamfoka
Kijana amwangaliya

1011
Wakawa wakitegana
Na huku
waoteana
Na mwishowe Sayidana
Dharuba kasukumiya

1012
Dharuba hiyo ni kavu
Kampiga mshupavu
Akamkata ubavu
Maiti ametuliya

1013
Hapo
nduye Muh'amadi
Akampanda jawadi
Kumfwatia waladi
Wa yule alo jifiya

1014
Dakika haikupita
Kichwa chake kakikata
A'liy ajua vita
Jamani ninawambiya

1015
Mwana wa Abu Jahali
Kapachukia pahali
Akaona ni h'alali
Mwanamume kukimbiya

1016
Apate kuwa mwepesi
Juu ya wake farasi
Silaha kaona basi
Vumbini kazitupiya

1017
Baa'da ya hayo kwisha
Hapakuwa mshawasha
Makafiri yawat'osha
Waliyo yaangaliya

1018
Zikapita juma tatu
Za kuketi wale watu
Kuwazingia wenzetu
Hapana pa kuingiya

1019
Wakaanza kugombana
Na wenyewe kusutana
Na Mola wetu Rabana
Kimbunga kaweleteya

1020
Ule usiku wa kiza
Upepo kaupuliza
Mwenyezi Mungu Muweza
Wabaki wawayawaya

1021
Hapana kilichokaa
Kila kitu kinapaa
Watu wote washangaa
Kwa fujo lilo tokeya

1022
Kanadi Bu Sufiyani
Nakwenda zangu nyumbani
Nawambia ikhwani
Hapana la kukaliya

1023
Na kulipo pambazuka
Isilamu kuamka
Waona pames'afika
A'dui amepoteya

1024
Mtume akabashiri
Mji huu Munawari
Hautaona khat'ari
Kafiri kuuleteya

MAFUNZO:

Tunaona kuwa Uislamu ulisimamishwa na watu mbali mbali, wa Bara zote. Huyu mtu wa Asia, Muajemi Salman Al Farisy, ambaye Mtume s.a.w. jinsi ya kumpenda kwake hata alisema: Salman minna ahli-l-beit, "Salman ni katika ukoo wetu." Yeye aliuokoa Uislamu katika uchanga wake kwa kuzua hikima ya kuchimba handaki kuilinda Madina na Waislamu wachache. Na pia tunaona ushujaa wa ajabu wa Imam Ali (karama Llahu wajhahu), hali naye kijana wa kiasi labda miaka 24 kwenda pambana na mijabari hiyo ya kikafiri wajuzi wa vita peke yake. Huu si ushujaa tu, bali ni Imani ya moyo aliyo kuwa nayo huyu nduguye Mtume s.a.w. Mtu huyu ndiye aliye itoa roho yake kwa kulalia kitanda cha Mtume, akajifunika shuka ya Mtume, ili achinjwe yeye badala ya Mtume, pale Mtume alipo kimbia Makka! Watu kama hao ndio alio kuwa nao Muhammad s.a.w. Ndio maana Uislamu ukasimama tangu mwanzo, na ukapata nguvu za kutufikia sisi hii leo.