DUA'
FIMBO YA MNYONGE

A'bdalla Buyi            Baba kamwambiya
Mwana wa A'liyi        Mwanangu sikiya
Mambo yakidhii        Tweka la miyaa

1241
Ninaanza kwa isimu
Jinalo nalih'ishimu
Arrah'manu Rrah'imu
Mja wako nakujiya

1242
Ninayo khofu Ghafuru
Nisije nikakufuru
Mwenyewe nikajidhuru
Kwa haya nino kwambiya

1243
Sijui kama ni vyema
Kwako Wewe kulalama
Wayajua nino sema
Na yote nino dhaniya

1244
Kama yafaa kuomba
Kwa Bwana ulo niumba
Na tena ukanipamba
Kwa ninayo hitajiya

1245
Basi haya nikiwaza
Ninaona kingi kiza
Na mengi yanishangaza
Vigumu kuzingatiya

1246
Lakini hizi qauli
Fikira za kijahili
Sikuiona dalili
Vitabu kuniambiya

1247
Mwenyewe ulio nena
Tukuombe Subuh'ana
Kwa Bora yako Majina
Nawe utatwitikiya

1248
Iliyo kuja niponza
Ni Sura yako ya kwanza
Kwa hiyo nikajifunza
Kuifwata hiyo njiya

1249
Basi Mola niwezeshe
Njia njema nionyeshe
Njia ovu niepushe
Nakuomba Maulaya

1250
Nije mfwata H'abibu
Pendo lako linis'ibu
Hilo kwako nat'ulubu
Ewe Mwingi wa a'tiya

1251
Tuwakuombawe Rabana
Tukuzie wetu wana
Na tuwe tunapendana
Na ahali na dhuriya

1252
Ya Rabi Mola Muweza
Twokowe tulo jisoza
Tuonyeshe muangaza
Tuache ya maa's'iya

1253
Katika zetu biladi
Utwondoshee fisadi
Itupe mbali bai'di
Wenetu wanaumiya

1254
Wenetu uwaokowe
Bwana twakuomba Wewe
Wah'ifadhi wasilewe
Na ghururi za duniya

1255
Twakuomba Allahuma
Kwa mapenzi na h'ishima
Wawezeshe kusimama
Na Wewe kukwelekeya

1256
Ya Rabi Rabi Rabana
Twakuomba Subuh'ana
Ukata uwe hapana
Kwa walimwengu jamiya

1257
Pasiwepo ukosefu
Katika zetu s'ufufu
Na dhiqi tusizishufu
Kila tukiangaliya

1258
Twakuombawe Jalali
Tunee'meshe h'alali
Ya h'aramu yawe mbali
Yasiwe yaqurubiya

1259
Tusiwe twamh'itaji
Ila pekeyo Mpaji
Ya Rabi tupe faraji
Kwa dhiqi ilo twingiya

1260
Twakuombawe Manani
Twakuomba tua'wini
Iwe Kun-fayakuni
Ya Rabi tufarijiya

1261
Tuhurumie Rah'imu
Wajao tunasaqimu
Nyoyo zetu zina hamu
Ya Rabi tupe a'fiya

1262
Kwa kila lilo thaqili
Tunaomba tasihili
H'ata likiwa jabali
Waweza kutwondoleya

1263
Karimu Mola Jalali
Twepushe na udhalili
Na woga na ubakhili
Tusikutane pamoya

1264
Tuenezee ya kheri
Nyoyo zingie sururi
Uwahizi majabari
Wapate kila hizaya

1265
Rah'imu Bwana Wadudi
Wareh'emu Mashahidi
Wa hizi zetu biladi
Na wa ulimwengu piya

1266
Walo kufa madhulumu
Bwana wetu wakirimu
Thawabu ziwe u'mumu
Na kwa walio baqiya

1267
Allahuma Mauletu
Tuokowe na wenzetu
Tuwe myongoni mwa watu
Kwako walo jitoleya

1268
Waongoe aquwamu
Wafuate Isilamu
Wampende Mua'dhamu
Sayidi wetu Nabiya

1269
Tuzidishie Imani
Ya kumfwata Amini
Na wenzetu ikhiwani
Rabi uwape hidaya

1270
Twakuomba Mwenye e'zi
I'limu ziweke wazi
Pasiwepo pingamizi
Kupinga na kuzuwiya

1271
Ututoke ujahili
Tutende njema a'mali
Uipendayo Jalali
Kwa Akhera na duniya

1272
Na ukija mtih'ani
Uwe kwetu ahweni
Tua'wini tua'wini
Bwanetu tusaidiya

1273
Allahuma tawfiqi
Tunawirie t'ariqi
Qauliyo tus'adiqi
Tufwate uno twambiya

1274
Tuwe waja wa mithali
Tushike yako Sabili
Kwa qauli na a'mali
Na Imani kutimiya

1275
Ya Rabi tuwafiqie
Twaomba tuitikie
Dini yako ienee
Pasi pembe kusaliya

1276
Ya Rabi tujaa'lie
Unenayo tusikie
Na uwezo ututie
Kutenda tuno us'iya

1277
Twakuombawe Lat'ifu
Ututwae kwa lut'ufu
Utwepushe taklifu
Tusije tukaemewa

1278
Tuishike yako kamba
Bwana wetu twakuomba
Tusiwe twayumba yumba
Khat'arini tukangiya

1279
Allahuma wetu Rabi
Tus'afishie qulubi
Ziwe kama wa H'abibi
Kipenzi chako Nabiya

1280
Utwondolee h'asadi
Ya Rabi shari bai'di
Twakuombawe Wadudi
Bwana wetu tusikiya

1281
Twakuombawe Maliki
Tubai'dishe na chuki
Tujaze h'uba isaki
Tukipendana jamiya

1282
Twakuombawe wa Haqi
Tulinde na unafiqi
Ya Rabba lkhalaiqi
Wajao twanyenyekeya

1283
Ya Rabi tupe s'ubira
Twende mwendo ulo bora
Tupe nyoyo za imara
Tuweze kuvumiliya

1284
Ya Rabi tupe Imani
Kurudi tusitamani
Tukiingia njia
Tusiwe wa kurejeya

1285
Tusikhofu makhaluqi
Ktika vita vya h'aqi
Na Diniyo tuithiqi
Tupinge kila khat'iya

1286
Woga tuutupe nyuma
Si utu wala h'ishima
Tusiikhofu dhuluma
Kupinga na kuyondoa

1287
Utupe nguvu Karimu
Za kumshinda dhalimu
Atesao madhulumu
Tuweze mshindiliya

1288
Tusimamishe a'dili
Kwa jeuri tusidhili
Tujue Mola Jalali
Daima watwangaliya

1289
Twakuomba Allahuma
Watumwao twalalama
Twitikie hima hima
Waona twaangukiya

1290
Ya Allahu Maulana
Twakuomba Rah'mana
Tusiwe tunajiona
Na watu kuwaoneya

1291
Twakuomba Rah'mani
Tuzidishie imani
Pasiwepo hata nani
Kukosa wa kumleya

1292
Ututie na huruma
Wawele kuwatazama
Na watoto mayatima
Tuwe twaangaliya

1293
Twakuomba Mwenye shani
Utupe wema wageni
Na tungiapo njiani
Watu wakitupokeya

1294
Bwana utufarijie
Na balaa twondolee
Kila jema tuletee
Twakuomba twitikiya

1295
Twakuomba Allahuma
Tuwe Kweli twaisema
Kwa h'aqi tunasimama
Na h'aqi twapiganiya

1296
Iwepo Kweli usoni
Kweli iwe kisogoni
Iwe Kweli ubavuni
Pande zote yaeneya

1297
Rabi Wadudi Rah'imu
Walinde wanaadamu
Kafiri na Isilamu
Wafwate yako Hidaya

1298
Mola wetu utuhidi
Tumfwate Muh'amadi
Kama Khulafa Rashidi
Vile walo mpokeya

1299
Rabi eneza Imani
Izagae duniani
Itukuzwe Ramadhani
Shariqi na gharibiya

1300
Na nguzo zisio shaka
Kama Kus'ali na Zaka
Na kwenda Kuhiji Maka
Zishikwe na watu piya

1301
Ya Allahu Subuh'ana
Tua'wini Waumina
Zote faradhi na suna
Rabi tusahilishiya

1302
Utubaqishe Wadudi
Na tuzile nyingi I'di
Sisi na wetu uladi
Kwa furah'a na h'uriya

1303
Allahuma taqabali
Tuzitendazo a'mali
Utufanyie sahali
Kila tunalo lingiya

1304
Ya Rabi Mola wa waja
Tuunge tuwe wamoja
Uwahidi wano fuja
Waache yao mabaya

1305
Uzing'oe tafauti
Kati ya wetu umati
Uzibwage na tiyati
Twakuombawe Jaliya

1306
Wazuke wana wat'ani
Wananchi Waumini
Watutoe taabuni
Na balaa na udhiya

1307
Wafungue madhulumu
Walo fungwa na dhalimu
Na zikome zao ghamu
Ya Rabi wafarijiya

1308
Ya Rabi wetu wa shani
Wafungue kifungoni
Yakome ya kisirani
Wapate yao h'uriya

1309
Ya udhalimu yahame
Upesi kama umeme
Yalo pita tuyaseme
Kana kwamba hayakuwa

1310
Nasi tuwe waungwana
Wasite kutukukana
Wanyanyasi na watwana
Waso mjua Rasuwa

1311
Na wazushi walo zuwa
Uwongo usio kuwa
Wewe Bwana wawajuwa
Uwape yao hizaya

1312
Wamezua makidhabu
Niya yao kuharibu
Kuficha zao a'ibu
Ni mengi wasingiziya

1313
Wakashifu makhaini
Barazani wabaini
Tuwajue wao nani
Na watu kuwazomeya

1314
Waficha nifaqi yao
Kuwatusi bora wao
Wanadhani Mola wao
Waweza kumkimbiya

1315
Mola Wewe wawangoja
Kuwaonyesha viroja
Wataishiwa na hoja
Mbee zako Maulaya

1316
Wayajua yalo ghibu
Ya mbali kwako qaribu
Jaza ya mema thawabu
Na dhambi kwa maa's'iya

1317
Rabi ondoa mateso
Zifunuke zetu nyuso
Yasite yawe na mwiso
Ya karaha na beluwa

1318
Walo pokwa vya h'alali
Bwana uwape badali
Izidi shinda awali
Wawe radhi maridhiya

1319
Zivuke zetu biladi
Watoweke mafisadi
Pasiwe wa kutaa'di
Makwetu kutwingiliya

1320
Waje zishika khat'amu
Wajuao kuh'ishimu
Waso dhili binadamu
Na h'aqi watumikiya

1321
Tureh'emee wazazi
Na pia nao walezi
Na wote wetu a'zizi
Ndu zetu na wana piya

1322
Na mashekhe na walimu
Mola wetu warah'amu
Na jamii' Isilamu
Ghafuru waghufiriya

1323
Na s'alatu zilo timu
Zishuke kwa Mua'dhamu
Na S'ahabaze kiramu
Na aali zake jamiya

1324
Sasa hapa natufunge
Dua' fimbo ya mnyonge
Yauwa nyoka na nge
Mkongwe akongojeya