811
Siku moja yawas'ili
Khabari kwake Rasuli
Kwamba wako Majahili
Madina waqurubiya
812
Unapita msafara
Una mengi mali bora
Itakuwa ni bus'ara
Kutoka kuuzuwiya
813
Kwani hao Makafiri
Ni sana wawakhasiri
Isilamu mah'aqiri
Kwa roho na mali piya
814
Na mali wakiyapata
Ndio huzidi matata
Hujitengeza kwa vita
Na nguvu kuwazidiya
815
Mkubwa tawambiani
Ndiye Abu Sufyani
Alo kuja viungani
Kunyang'anya na kuuwa
816
Na watuwe shujaa'ni
Hawazidi rubai'ni
Kangia khofu moyoni
Madina kuqurubiya
817
Akaipata timamu
Kwa jasusi maa'lumu
Mia tatu Isilamu
Wa njiani wamjiya
818
Upesi akapeleka
Ujumbe ufike Maka
Waje hima kwa haraka
Mali yao yapoteya
819
Qureshi wambiwa nini
Hilo jambo watamani
Kuwasaga Waumini
Na huyo wao Nabiya
820
Hapo hapo waliqifu
Waungwana watukufu
Si chini moja elifu
Wa t'ayari kuvamiya
821
Walijivika libasi
Wakatandika farasi
Ngamia waso qiasi
Na panga na rumh'iya
822
Kila kitu watengeza
Wanawake wa kucheza
Warembo kutumbuiza
Wapate kusherehekeya
823
Walikuwa na yaqini
Kushinda ni yao shani
Mia tatu kitu gani
Mbee zao Qureshiya
824
Huku nyuma Mukhtari
Hana chembe ya khabari
Hajui kuna khat'ari
Huko inawaongojeya
825
Kupata kwake khabari
Ni qaribu ya Badiri
Na hapo akashauri:
Ni lipi kushambuliya?
826
Watu wake Muh'amadi
Ni mia tatu junudi
Kumi na tatu zaidi
Ndio walio zidiya
827
Wengi wao wenda chini
Farasi wao thineni
Silaha zao ni duni
Wanyonge kiwangaliya
828
Tena hao Isilamu
Walikipanda kwa zamu
Wachangia bahaimu
Watatu kila ngamiya
829
Kwa hivyo hapo awali
Waliona afadhali
Kunyang'anya yale mali
Nyumbani kukimbiliya
830
Mtume yake shauri
Wapigane na Kufari
Waiqabili khat'ari
Kuliko kuikimbiya
831
Ni rai yake Rasuli
Kukimbia ni muh'ali
Kwani wale Majahili
Madina watafwatiya
832
Jambo liso kimbilika
Na huwezi liepuka
Bora nje ukatoka
Likute nusu ya njiya
833
Kwa hii yake shauri
Aliungwa na U'mari
Na pia Abu Bakari
Na wengine nawambiya
834
Wamuunga Muh'amadi
Maa'rufu Miqidadi
Na pia Bwana Sai'di
Huyo mwisho Madaniya
835
Hapo katoa amri
Kuwendea Makafiri
Walio kuja kwa shari
Msafara kuwachiya
836
Walipo fika Badiri
Na hapo wasitaqiri
Penye visima t'ahiri
Maji wakayazingiya
837
Walipo kuja Qureshi
Pamoja na lao jeshi
Mas'ah'aba kwa ubishi
Maji wawazuiliya
838
Mtume kawakataza
Kunyima na kuchokoza
Aliwaacha kujaza
Viriba na kujinyweya
839
Na ndio hapo H'akimu
H'akimu bin H'izamu
Akaona ni vigumu
Vita hivi kuvingiya
840
Huu wema wa Mtume
Aliona ni kinyume
Na inda ya wanaume
Walo kuja shambuliya
841
Akenda kumsemeza
Mkubwa mwenye kuweza
Na yeye akaweleza
Qureshi akawambiya:
842
Jamani tusiwauwe
Hawa wenzetu wenyewe
Kila mtu na mwenziwe
Kati yao nasi piya
843
Tuwaache Waarabu
Wasio khusu nasabu
Wawingie kwa h'arubu
Bila sisi kujitiya
844
Mimi naona turudi
Tusimpige H'amadi
Na kama hapana budi
Laumu Bin Rabia'
845
Semeni mimi ni mwoga
Sipendi damu kumwaga
Karuka Baba Ujinga
Abu Jahali sikiya
846
Abu Jahali kanena:
Huyu ni mwongo sana
Khofu yake wake mwana
Alo mfwata Nabiya
847
Akhofu asiuliwe
Hakhofii wenginewe
Nasema natuwauwe
Ukome tena udhiya
848
Sisi nyuma haturudi
Sisi sote ni junudi
Tumsage Muh'amadi
Na wanao mfwatiya
849
Na tukisha natucheze
Mabibi watumbuize
Na vigoma vicharaze
Kwa tatu mtawaliya
850
Tena hapo Makafiri
Wafwata hiyo shauri
Wote t'ayari kwa shari
Hawana la kusikiya
851
Wakatoka wabarizi
Mashujaa wenye e'zi
Wakali wa kirumbizi
Cha panga za A'rabiya
852
Wa kwanza alotokea
Ni yule Bin Rabia'
Na nduye kamfwatia
Wa tatu nitakwambiya
853
Wa tatu ndiye Walidi
Wa U'tba wake waladi
Hao watatu asadi
Ndio walo jitoleya
854
Na hayo kama kunena:
Abu Jahali waona?
Mwenye kukhofia mwana
Mwanangu nimemtoa
855
Memtoa na ndu yangu
Na pia nafusi yangu
Yatazame ya uchungu
Kama haya yazidiya
856
Wakitoka Makafiri
Wakatoka Ans'ari
Mashujaa' mahodari
T'ayari wamepaniya
857
Maqureshi majeuri
Wakanena: Hatukiri
Tunataka akhiyari
Maqureshi nao piya
858
Maqureshi wakanadi:
Sikiliza Muh'amadi
Utuletee junudi
Kama sisi bisawiya
859
Tunataka kuuwana
Na ndu zetu waungwana
Wawe nasi twalingana
Wabora wa kuzaliwa
860
Mtume akawatowa
Wa baba yake ukhuwa
H'amza mwenye u'luwa
Na U'bedi naye piya
861
H'amza ni wake a'mi
U'bedi ni bunu-a'mi
Na A'lii simsemi
Kwani nyote mwamjua
862
Watoka hawa watatu
Kila mtu ana mtu
Ni nani wa kuthubutu
Kati yao kujitiya
863
Hazikupita dakika
Na H'amza msifika
Mtuwe alimfyeka
Akafariqi duniya
864
Bwana A'li Haidari
Na yeye hakuqas'iri
Alitengeza safari
Walidi kampakiya
865
Lakini Bwana U'beda
Ilikuwa kwake shida
Upanga ulipo kwenda
Upanga ukamjiya
866
Dharuba zikapishana
Wawili wakauwana
U'tuba yule mungwana
Papale akajifiya
867
Bwana U'bedi mwanati
Yalimtwaa mauti
Yu njiani katikati
Madina akirejeya
868
Mambo hayo yakizuka
Makafiri washituka
Wakaona ni mzuka
Mwanzo mui kuanziya
869
Hawana la maliwaza
Mtu mume hujikaza
Hivyo hivyo wajisoza
Na khofu imewangiya
870
Kikaingiwa qitali
Vita vilivyo vikali
Na huku wetu Rasuli
Molake kamwelekeya
871
Kamuomba Rah'amani:
Waokoe Waumini
Waeneze yako Dini
Usite wote udhiya
872
Akaomba Mukhtari:
Bwana hawa Makafiri
Wamekuja kwa jeuri
Maovu waqus'udiya
873
Waja wako ni qalili
Wataka wawaqatili
Naomba kwako Jalali
Nus'ura ulo nambiya
874
Ikifika adhuhuri
Afunuliwa Bashiri:
Kushinda kuko t'ayari
Mchanga huu mwagiya
875
Mtume kateka gao
Karusha nyusoni mwao
Vikome vitimbi vyao
Na huku kinuwiziya
876
Kwa kitendo chake hicho
Kafiri wajaa kicho
Halikusalia jicho
Mchanga lisilo ngiya
877
Mchanga huo mkali
Utadhani pilipili
Ukamaliza qitali
Kwa muda wa mara moya
878
Ilikuwa hekaheka
Makafiri waanguka
Na wengine ni mateka
Kwa kamba wawafungiya
879
Wauwawa sabii'ni
Na sabii'ni pinguni
Na wengine majabani
Mbioni walikimbiya
880
Na watuwe Mukhtari
Ni wanane Ans'ari
Na sita kwa Wahajiri
Ndio walio poteya
881
Ni nguvu zake Muweza
Alo tenda muu'jiza
Mia tatu kuwaweza
Elfu Maqureshiya
882
Elfu shujaa' wema
Wenya kupanda wanyama
Na mavazi yao chuma
Na mabibi kuwimbiya
883
Hawa watu makhabithi
Wakashindwa na thuluthi
Wala si kama h'adithi
Ni kweli yalo tokeya
884
Kwisha wapata mateka
Mtume alitamka
Mas'ahaba kawataka
Rai zao kumwambiya
885
Akanena Bubakari
Mimi ni yangu shauri
Uwaache Mukhtari
Wakiitoa fidiya
886
Waache wajikombowe
Kwani hawa wako wewe
Hivi pengine Molawe
Awaonyeshe ya Njiya
887
Kanena Bwana U'mari
Mimi sioni vizuri
Kuwaacha Makafiri
Bure tukawachiliya
888
Hawa watu ni waovu
Wametutenda viovu
Wengi wetu ni majivu
Kwa hawa Majahiliya
889
Hawa watu wauwaji
Wametufukuza mji
Tulidhania hawaji
Huku tulo kimbiliya
890
Lakini watu matata
Na huku wametufata
Wakitupiga kwa vita
Kwa shari washambuliya
891
Naona natuwauwe
Kila mtu na mtuwe
Amrisha sasa wewe
Na sisi tutafwatiya
892
Mtume katakalamu:
Abu Bakari rah'imu
Kama Baba Burahimu
Na I'sa mwana Mariya
893
Na U'mari mshabahu
Ni kama Nabii Nuh'u
A'laihimu S'alla Llahu
Na Musa kamlandiya
894
Kamaliza Mteule:
Tuwafwate watu wale
Walio kuwa wapole
Ni bora kuhurumiya
895
Walo kuwa wajiweza
Fidia aliwatoza
Masikini katengeza
Bure kawaachiliya
896
Walo jua kuandika
Mtume aliwataka
Kufunza kumi kifika
Huwapa
897
Kawataka Isilamu
Walo kiweza qiyamu
Mateka wawakirimu
Mpaka kugombolewa
898
Waliqimiwa vizuri
H'ata wale Makafiri
Nyoyo zao zikakiri
Na Dini wakaingiya
899
Waona jambo a'dhimu
Watendavyo Isilamu
Mateka kuwakirimu
Kushinda zao dhuriya
900
Kati
A'basi a'miye Bwana
Na mwengine sayidana
A'qili nduye Nabiya
901
Na babu zake Imamu
Imamu wa Isilamu
Mkuu mwenye maqamu
Imamu wa Shafii'ya
902
Ndio zema haziozi
Wanena wetu wazazi
Zema hutia mizizi
Ni khazina ya dhuriya
MAFUNZO:
Ukipigana kazana;
ukishindwa usivunjike moyo; ukishinda rehemu. Mwendo huo tunauona daima kwa Mtume
Muhammad s.a.w. na khasa katika Vita vya Badri, Vita vya Uh'ud, na katika
kuikomboa Makka. Tunaona pia kuwa wingi si hoja, hoja ni Imani
na uwongozi mwema.