1. Harufi hizi na mfano wa hizi ndizo zikakusanyika
kuifanya Qur'ani kuwa ni muujiza ulio washinda watu kuiga mfano wake, ijapo
kuwa hizo harufi ndizo wanazo zitamka. Basi mwenye kuitilia shaka hii Qur'ani
kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu au la, basi na alete mfano wake. Na hatoweza.
Rudi kwenye Sura
2. Maneno haya niliyo kufunulia ni Aya za Kitabu chenye kuweka wazi
hukumu zote ziliomo ndani yake.
Rudi kwenye Sura
3. Ewe Nabii! Hebu jionee huruma nafsi yako. Usijikere kwa kuhuzunukia
inadi ya watu wako, na kuto amini kwao.
Rudi kwenye Sura
4. Sisi tunaweza kuwaletea muujiza wa kuwalazimisha Imani,
wat'ii kwa unyenyekevu amri yake, na yatimie unayo yatarajia. Lakini hatuwaletei,
kwa sababu mwendo wetu ni kuwaongoza watu waamini bila ya kuwalazimisha,
ili isikosekane hikima ya kujaribiwa kwa mitihani, na yanayo kuja baada
yake ya thawabu na adhabu.
Rudi kwenye Sura
5. Wala Mwenyezi Mungu hawaletei watu wako kwa ufunuo wake ya kuwakumbusha
Dini ya Haki kuwa ni rehema kwao, ila wao huzua upya upinzani na ukafiri
kuukataa. Kwani njia ya uwongofu imekwisha zibwa mbele yao.
Rudi kwenye Sura
6. Hawa hakika wamekadhibisha Haki uliyo ileta, na wakaifanyia maskhara.
Lakini wewe wasubirie. Wataona matokeo ya maskhara yao ya kuangamiza.
Rudi kwenye Sura
7. Hivyo hao wanatenda watendavyo katika ukafiri wao na kukadhibisha
kwao wala hawaangalii baadhi ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu katika hii hii
ardhi? Lau kuwa wanaangalia kwa kuzingatia wangeli ongoka. Hebu wazingatie
hii mimea ya kila namna yenye manufaa tunayo itoa Sisi kwenye ardhi, na
wala hawezi hayo isipo kuwa Mungu Mmoja Muweza.
Rudi kwenye Sura
8. Hakika katika kutoka kwa hii mimea ni dalili kubwa ya kuwepo Muumba
Muweza. Lakini wengi wa watu si wenye kuamini.
Rudi kwenye Sura
9. Hakika Mwenye kumiliki mambo yako, na Mwenye kukulinda, ndiye
atakaye waadhibu hao wanao kadhibisha, na ndiye Mwenye kuwafadhili Waumini
kwa rehema.
Rudi kwenye Sura
10. Ewe Muhammad! Watajie watu wako kisa cha Musa pale Mola wako
Mlezi alipo mwita: Ewe Musa! Nenda kwa Utume kwa watu walio dhulumu nafsi
zao kwa ukafiri, na wakawadhulumu Wana wa Israili kwa kuwafanya watumwa
na kuwauwa watoto wao wanaume.
Rudi kwenye Sura
11. Nenda kwa kaumu ya Firauni; kwani hao wamepita mipaka katika
dhulma yao. Ama ajabu ya watu hawa! Hawaogopi nini litalo wafika kwa vitendo
vyao hivi, wakatahadhari?
Rudi kwenye Sura
12. Musa akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi nina khofu wasije kuukataa
ujumbe wangu kwa kiburi na inda.
Rudi kwenye Sura
13. Na mimi nimejaa dhiki kwa kuwa wataniambia mwongo, na ulimi wangu
si mkunjufu wa kuweza kuhojiana nao kama ninavyo penda. Basi mtume
Jibril ende kwa ndugu yangu aje kuniunga mkono katika hii kazi yangu.
Rudi kwenye Sura
14. Na watu hawa wana kisasi juu yangu. Kwani mimi nilimuuwa mtu
katika wao. Basi nina khofu watakuja niuwa kwa kisasi kabla sijatimiza
kazi yangu. Hayo yananizidisha khofu.
Rudi kwenye Sura
15. Mwenyezi Mungu akamwambia: Hawatokuuwa. Na kwa mintarafu ya Haruni
nimekukubalia ombi lako. Basi nendeni nanyi mmejizatiti na miujiza yetu.
Mimi niko pamoja nanyi kwa ulinzi. Nayasikia yanayo jiri baina yenu na
Firauni. Nyinyi mtapata ushindi, na kuungwa mkono.
Rudi kwenye Sura
16. Muelekeeni Firauni na mwambieni: Sisi ni Watume wawili tumetumwa
na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Rudi kwenye Sura
17. Anakwambia Mola Mlezi wa walimwengu wote: Waachilie huru Wana
wa Israili, wende nasi.
Rudi kwenye Sura
18. Firauni akamwambia Musa kwa kumsimbulia, naye alimtambua walipo
ingia na wakakadimisha Ujumbe wao, kwani alilelewa mle mle katika kasri
lake: Hatukukulea sisi ulipo kuwa mtoto? Na ukaishi chini ya ulezi wetu
kwa miaka mingi katika umri wako?
Rudi kwenye Sura
19. Na ukatenda makosa yako ya jinaya maovu kumuuwa mtu katika kaumu
yangu, na ukazikanusha neema zangu nilizo kufanyia, hukuwahifadhi raia
zangu, ukaushambulia ungu wetu kwa kudai kuwa wewe ati ni Mtume wa Mola
Mlezi wa walimwengu wote.
Rudi kwenye Sura
20. Musa akasema: Niliyafanya uliyo yataja kwa kutojua yanayo faa
kutambulikana kwa akili nayo ni jambo la kuuwa. Basi hapana masimbulizi
juu yangu.
Rudi kwenye Sura
21. Nikakukimbieni nilipo khofu kuwa mtakuja niuwa kwa jinaya hii
ambayo sikuukusudia. Mola wangu Mlezi akanitunukia fahamu na ilimu, kwa
fadhila zake na neema zake, na akanifanya mmoja katika Mitume.
Rudi kwenye Sura
22. Musa akaashiria sifa katika sifa ovu kabisa za Firauni, nayo
ni kuwa kawafanya watumwa Wana wa Israili, na akiwauwa watoto wao wanaume.
Na akakataa kukuita kule kulelewa kwake katika jumba la Firauni kuwa ni
neema, kwani yaliyo sabibisha hayo ni yale aliyo kwisha yataja, ndio yeye
alitupwa mtoni aokoke asiuliwe. Akaishia kwenye jumba la Firauni. Na lau
kuwa si hivyo basi angeli lelewa na wazazi wake.
Rudi kwenye Sura
23. Firauni akasema: Na nini hizo sifa za Mola Mlezi wa walimwengu
wote ambaye unakithiri kumtaja, na wewe unadai kuwa ni Mtume wake, na hali
sisi hatujui lolote khabari zake?
Rudi kwenye Sura
24. Musa akasema: Yeye huyo ndiye Mwenye kuzimiliki mbingu na ardhi
na kila kilio baina yao. Ikiwa nyinyi mna yakini ya ukweli wa jawabu hii
basi mtanafiika, na mtaongoka, na mtajua kuwa ufalme wa Firauni wa kujidai
haufui dafu mbele ya Ufalme wake Mwenyezi Mungu. Kwani ufalme wa Firauni
haupindukii hata eneo moja katika hii dunia.
Rudi kwenye Sura
25. Firauni kuonyesha mastaajabu kwa wale walio mzunguka kwa kuwa
Musa katika jawabu yake alipo mtaja Mola wake Mlezi na akadhukuru Ufalme
wake hakuugusia hata kidogo ufalme wa Firauni, alisema: Mwayasikiaje maneno
ya Musa?
Rudi kwenye Sura
26. Musa akiendelea na usemi wake bila ya kujali hasira za Firauni
na uchafu wa maneno yake, akasema: Ndiye huyo Mola Mlezi wa walimwengu
wote, aliye kuumbeni nyinyi na baba zenu walio tangulia. Na miongoni mwa
hao walikuwako walio dai ungu kama unavyo dai wewe. Na wao wameteketea.
Na wewe utateketea, na hayo unayo yadai yatapotelea mbali. Kwani Mungu
wa kweli hafi.
Rudi kwenye Sura
27. Firauni akwaambia watu wake yale yanayo mtibuwa roho na kumghadhibisha,
akautaja Utume wa Musa ni kwao wao, wala si kwake yeye, na akambandikiza
wazimu, kwa kuwa ati akiulizwa kitu hujibu kingine, na anamsifu Mola Mlezi
kwa sifa za kiajabu ajabu. Na kwa hivyo Firauni anawahimiza wamkadhibishe.
Rudi kwenye Sura
28. Musa akasema: Ikiwa nyinyi mna akili, basi uaminini Ujumbe wangu.
Kwani kuchomoza jua na kuchwa kwake kwa mpango madhubuti ni dalili wazi
ya Mwenye kuumba. Kwa hivyo basi ni nyinyi ndio mnastahiki kuambiwa wendawazimu.
Rudi kwenye Sura
29. Firauni akamwambia Musa: Ukimfuata mungu yeyote badala yangu
mimi, utakuwa mmoja katika wanao ijua hali yao mbaya katika magereza yangu.
Na yeye Firauni kaangukia kitisho hichi baada ya kushindwa kuondoa athari
za kazi za Muumbaji.
Rudi kwenye Sura
30. Musa akasema kwa upole kwa kutumai asaa akaamini: Utanitia gerezani
hata nikikuletea ushahidi mkubwa wa ukweli wa haya niyasemayo?
Rudi kwenye Sura
31. Firauni akasema: Ulete ushahidi utao onyesha Unabii wako kama
wewe kweli unasema kweli katika wito wako. Kasema hayo kwa tamaa ya kuwa
huenda akapata kipengee cha udhaifu katika hoja zake.
Rudi kwenye Sura
32. Musa akaitupa fimbo yake mbele yao. Ikageuka nyoka kweli kweli,
si kitu cha uwongo cha uchawi kinacho fanana na nyoka.
Rudi kwenye Sura
33. Musa akautoa mkono wake kutoka mfukoni mwake. Hiyo ni Ishara
ya pili. Nao ukawa mweupe, bila ya maradhi, hata wakashangaa watazamaji
kwa kumetuka kwake.
Rudi kwenye Sura
34. Firauni akawaambia watu wake: Hakika Musa ni mchawi bingwa katika
uchawi wake. Kasema hayo kwa kuchelea watu wake wasiifuate Haki waliyo
iona kwa Musa.
Rudi kwenye Sura
35. Tena Firauni akasema: Mchawi huyu anataka kunifanyia kahari apate
kukutoeni katika hii nchi yenu. Na haya ni uchochezi dhidi ya Musa, kwani
katika la dhiki mno katika hayo yaliyo dhiki ni mtu kuiacha nchi yake,
na khasa ikiwa kwa kahari. Naye akataka mawazo ya wale walio kuwa wanamuabudu.
Kasahau ungu wake kwa nguvu za Ishara za Musa.
Rudi kwenye Sura
36. Watu wake wakamwambia: Akhirisha kukata shauri yao hawa, na uwatume
askari wende wawakusanye wachawi katika raia zako. Kwani uchawi hupingwa
kwa uchawi.
Rudi kwenye Sura
37. Watakuletea wengi, na wote wamebobea kwa uchawi, na wamemshinda
Musa kwa ufundi na ustadi. Wamekusudia kwa haya kumpunguzia dukuduku lake
Firauni.
Rudi kwenye Sura
38. Wakakusanywa wachawi kutoka kila upande wa nchi. Wakawekewa wakati
wa mchana siku ya Sikukuu kukutana na Musa.
Rudi kwenye Sura
39. Na watu wakahimizana kuhudhuria siku hiyo waone ramsa wakiambizana:
Mtakusanyika? Yaani ndio: Mkusanyike!
Rudi kwenye Sura
40. Wakatangaza matarajio yao ya kushinda wachawi, ili wapate kuthibiti
katika dini yao, na pia ndio kampeni ya nguvu na juhudi apate kushindwa
Musa.
Rudi kwenye Sura
41. Walipo kuja wachawi kwa Firauni walimwambia: Je! Tutapata kwako
ujira mkubwa pindi tukishinda?
Rudi kwenye Sura
42. Firauni akasema: Naam, mtapata mnacho kisema. Na juu ya huo ujira
mkubwa mtakuwa watu wa karibu kwangu, watu wa cheo na madaraka.
Rudi kwenye Sura
43. Ulipo fika wakati ulio wekwa katika siku iliyo pangwa Musa aliwaambia
wachawi: Tupeni huo uchawi mnao taka kuutupa.
Rudi kwenye Sura
44. Wakazitupa kamba zao na fimbo zao, na watu wakazugwa wakaona
kama ni nyoka wanakwenda. Wakaapa kwa utukufu wa Firauni na nguvu zake
hapana shaka hawa leo watashinda
Rudi kwenye Sura
45. Musa tena akatupa fimbo yake. Mara ikawa joka kubwa likaingia
kuvimeza vile walivyo vizua kwa uchawi, navyo ni kamba na fimbo, wakidanganya
kuwa ni nyoka wanao kwenda.
Rudi kwenye Sura
46. Wachawi wakaanguka wakasujudu kumsujudia Mwenyezi Mungu, walipo
yakinika kuwa mambo ya Musa si uchawi.
Rudi kwenye Sura
47. Wakasema ili kutia mkazo kule kusujudu kwao kwa kauli yao: Tunamuamini
Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Rudi kwenye Sura
48. Na wakabainisha kuwa hakika Mola Mlezi wa walimwengu wote walio
muamini ndiye: Mola Mlezi wa Musa na Harun.
Rudi kwenye Sura
49. Firauni kwa kukasarika kuwa wale wachawi wamemuamini Musa bila
ya yeye kuwapa ruhusa, aliwatishia ya kwamba yeye ndiye mwalimu wao aliye
wafunza fani za uchawi, na watakuja jua adhabu itakayo wateremkia. Akawaambia:
Nitakata mikono yenu na miguu yenu mbali mbali, nitakata wa kulia huu kwa
wa kushoto huu, na kinyume cha hayo. Na nyote nitakutundikeni juu ya misalaba.
Rudi kwenye Sura
50. Wachawi wakasema: Hapana la kutudhuru sisi kwa adhabu unazo tutishia,
kwani sisi ni wenye kurejea kwenye malipo ya Mola wetu Mlezi. Na Yeye ndiye
mbora wa kulipa na mbora wa kuadhibu.
Rudi kwenye Sura
51. Hakika sisi tunataraji Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu
tuliyo yafanya zamani, kwa kuwa sisi ndio wa mwanzo wa Waumini katika kaumu
yako.
Rudi kwenye Sura
52. Na Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Musa a.s. atoke usiku usiku pamoja
na Waumini miongoni mwa Wana wa Israili, ilipo kuwa tena haiwi kumsubirisha
Musa. Mpango ukawa wa makundi mawili kwamba atangulie Musa na kaumu yake,
na Firauni afuatie na kaumu yake, mpaka waingie katika maingilio ya njia
ya baharini, na Mwenyezi Mungu awateketeze.
Rudi kwenye Sura
53. Firauni akawatuma askari wake katika miji ya mamlaka yake, wawakusanye
wenye maguvu katika kaumu yake, alipo jua kuwa Musa kesha toka na Wana
wa Israili, ili awazuie lile walilo kusudia.
Rudi kwenye Sura
54. Firauni akasema: Hakika hawa Wana wa Israili walio kimbia na
Musa ni taifa dogo kwa nguvu zao. Idadi yao ni chache. Anasema hayo kutia
mori katika nyoyo za askari wake.
Rudi kwenye Sura
55. Na wao juu ya hivyo, wanatutibua roho kwa kuvunja amri yetu na
kutoka bila ya idhini yetu.
Rudi kwenye Sura
56. Na sisi ni wengi. Miongoni mwa ada zetu ni kuchukua hadhari,
na kuwa macho, na kupania.
Rudi kwenye Sura
57. Tukawatoa Firauni na askari wake kwenye nchi yao iliyo fanana
na mabustani yapitiwayo na mito kati yao, wakaangamia kwa kujitenga kwao
na Haki, na kuchochewa kutaka kumfuatia Musa, kama ilivyo kuja katika Aya
tatu zilizo tangulia.
Rudi kwenye Sura
58. Tukawatoa, kadhaalika, kwenye khazina za dhahabu na fedha, na
majumba waliyo kuwa wakiyakalia, wakineemeka kwa uzuri wake na ubora wa
starehe zake.
Rudi kwenye Sura
59. Ni kutoka kama huku kwa ajabu tulivyo kueleza ndivyo tulivyo
watoa, na tukawapa ufalme huo na kila namna ya neema zilizo kuwamo
Wana wa Israili, baada ya kuwa masikini hawana mbele wala nyuma.
Rudi kwenye Sura
60. Firauni na watu wake wakakaza mwendo ili wapate kuwawahi Wana
wa Israili. Wakawakuta wakati wa kuchomoza jua.
Rudi kwenye Sura
61. Walipo onana makundi mawili, watu wa Musa walisema: Hakika Firauni
na watu wake watatupata. Basi tutaangamia.
Rudi kwenye Sura
62. Musa akasema: Hakika mimi ninao uangalizi wa Mwenyezi Mungu unao
nifuata kwa kunihifadhi. Na Yeye ataniongoza kwenye Njia ya uwokovu. Amesema
hayo ili awatuze kuwa watasalimika, na iwe mbali na mawazo yao fikra ya
kutisha kwamba watakuja patikana.
Rudi kwenye Sura
63. Tukamuamrisha Musa kwa wahyi, ufunuo, aipige bahari kwa fimbo
yake. Ikapasuka bahari njia kumi na mbili kwa mujibu wa idadi ya mataifa
ya Wana wa Israili. Kila njia katika hizo njia ilikuwa na kizuizi cha maji
yaliyo nyanyuka kama mlima ulio simama imara.
Rudi kwenye Sura
64. Tukawajongeza Firauni na kaumu yake mpaka wakaingia kwenye zile
njia nyuma ya Musa na kaumu yake.
Rudi kwenye Sura
65. Tukamwokoa Musa na walio kuwa pamoja naye kwa hifadhi ya bahari
nayo imeshikamana, mpaka wakamalizika kuvuka.
Rudi kwenye Sura
66. Kisha tukamzamisha Firauni pamoja na walio kuwa pamoja naye kwa
kuwafudikiza kwa maji pale walipo wafuata.
Rudi kwenye Sura
67. Hakika katika vituko hivi vya ajabu vya kiungu pana funzo la
kuzingatia kwa atakaye kunafiika. Lakini watu wengi si wenye kusadiki.
Rudi kwenye Sura
68. Hakika Muumba wako na Mlezi wako ndiye huyo Mwenye nguvu katika
kuwaadhibu wanao kanusha, Mwenye kuwaneemesha kwa rehema Waumini.
Rudi kwenye Sura
69. Ewe Mtume! Na wasomee makafiri hadithi ya Ibrahim , Alayhi Ssalaam.
Rudi kwenye Sura
70. Alipo mwambia baba yake: Mnaabudu kitu gani hichi, ambacho hakifai
kuabudiwa? Anakusudia kwa hayo kuyakebehi masanamu.
Rudi kwenye Sura
71. Wakasema kujibu kwa njia ya kujitapa: Tunaabudu masanamu, nasi
tunadumu daima dawamu tukiyaabudu, kwa kuyaadhimisha na kuyatukuza!
Rudi kwenye Sura
72. Ibrahim akasema: Kwani yanasikia madua yenu? Au yanakuitikieni
mnapo yaomba? Kwa hayo anakusudia kuwanabihisha upotovu wa mwendo wao.
Rudi kwenye Sura
73. Au yanakuleteeni manufaa mnapo yat'ii? Au yanakupatilizeni kwa
madhara mkiyaasi?
Rudi kwenye Sura
74. Wakasema: Hawafanyi lolote katika hayo. Lakini sisi tumewakuta
baba zetu wakiyaabudu mfano wa ibada yetu. Basi sisi tukawafwata
kwa waliyo kuwa wakiyafanya.
Rudi kwenye Sura
75. Ibrahim akasema kwa kuwasusuika: Je! Mlifikiri hata mkalijua
jambo lolote lilio kupelekeeni kudumu na kuyaabudu hayo masanamu?
Rudi kwenye Sura
76. Nyinyi na baba zenu wa zamani - ati haya yanastahiki kuabudiwa
au la? Lau mngeli zingatia mngeli jua kuwa hakika nyinyi mko katika upotovu
ulio wazi.
Rudi kwenye Sura
77. Kwani hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni maaadui
kwangu mimi na kwenu. Basi mimi siwaabudu hao. Lakini ninaye muabudu na
najijongeza kwake ni Muumba wa walimwengu wote, na Mwenye kumiliki mambo
yao, na Mwenye kuwalinda.
Rudi kwenye Sura
78. Ambae ndiye aliye nizua kabla sijawa chochote akaniumba kwa bora
ya umbo, na akanitunukia uwongofu wa kunifikishia kwenye mafanikio yangu
ya duniani na Akhera.
Rudi kwenye Sura
79. Na Yeye ndiye aliye nineemesha kwa vyakula na vinywaji, na akaniwezesha
kuvipata na kunafiika kwavyo, ili kuhifadhi uhai wangu.
Rudi kwenye Sura
80. Na yakinishukia maradhi ni Yeye ndiye anaye niponesha, kwa kunisahilishia
sababu za kupona na kuniwezesha kuzipata.
Rudi kwenye Sura
81. Na Yeye ndiye atanifisha ikifika ajali yangu, na tena atanihuisha
mara nyengine kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura
82. Na Yeye ndiye ninaye mtumai kunighufiria na kuyasemehe makosa
yangu madogo madogo ya kujikwaa duniani, utapo fika wakati wa hisabu.
Rudi kwenye Sura
83. Ibrahim a.s. akasema kwa kuomba: Mola wangu Mlezi! Nitunukie
ukamilifu wa ilimu na vitendo, ili nipate kustahili kuubeba Ujumbe wako
na hukummu kwa waja wako, na niwezeshe niungane pamoja na kundi la watendao
wema.
Rudi kwenye Sura
84. Na nijaalie nipate sifa nzuri na kumbusho jema kwa kaumu zitazo
kuja baada yangu, mabaki yake yasalie mpaka Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
85. Na nijaalie katika waja wako ulio watunukia neema za Peponi,
kuwa ni malipo kwa sababu ya Imani yao kukuamini Wewe, na ibada yao kukuabudu
Wewe.
Rudi kwenye Sura
86. Na mjaalie baba yangu astahili msamaha kwa kumwezesha kuwa Muislamu.
Na yeye alikuwa kamuahidi kusilimu siku alio achana naye, kwani yeye huyo
baba alikuwa ameitupa kando njia ya uwongofu na uwongozi.
Rudi kwenye Sura
87. Wala usinitie aibu au hizaya mbele ya watu, Siku watapo tolewa
makaburini kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura
88. Siku ambayo hapana mtu ataye nafiika kwa mali ayatoe, au kwa
wana wamsaidie.
Rudi kwenye Sura
89. Isipo kuwa aliye kuwa Muumini, na akamkabili Mwenyezi Mungu na
moyo ulio mzima, hauna maradhi ya ukafiri, na unaafiki, na riya (kujionesha).
Rudi kwenye Sura
90. Na Pepo itajongezwa, na itakaribishwa pahala pa watu wema. Basi
wataiendea wale walio jikinga na ukafiri na maasi, na wakaikubali Imani
na ut'iifu duniani.
Rudi kwenye Sura
91. Na Moto utaletwa mbele ya walio iacha Dini ya Haki, mpaka ndimi
zake zikaribie kuwanyakua, nao watakuwa majutoni.
Rudi kwenye Sura
92. Wakaambiwa kwa kuwatahayarisha: Iko wapi hiyo miungu yenu mliyo
kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu?
Rudi kwenye Sura
93. Badala ya Mwenyezi Mungu, na mnadai kuwa ati ndio itakuombeeni
hii leo? Je! Inakufaeni kitu kwa kukunusuruni, au hata inajifaa wenyewe
kujisaidia? Hapana lolote. Kwani wao na miungu yao ni kuni za Moto.
Rudi kwenye Sura
94. Watatumbukizwa katika Jahannamu kifudifudi, wakipinduliwa pinduliwa
mpaka waishie ndani kabisa shimoni, wao na walio wapoteza na wakawatia
katika madhambi na upotovu.
Rudi kwenye Sura
95. Na pamoja nao watakuwapo wasaidizi wa Ibilisi walio kuwa wakiwapambia
shari na madhambi, au wale watu na majini walio wakiwafuata katika maasi.
Rudi kwenye Sura
96. Watasema huku wakiungama makosa yao, na huku wanagombana na miungu
yao waliyo kuwa wakiiabudu:
Rudi kwenye Sura
97. Wallahi! Hakika sisi tulikuwa katika dunia yetu tumepotea kweli,
na wajinga wa kutupwa, na tumeiacha Haki ambayo haina kificho ndani yake.
Rudi kwenye Sura
98. Pale tulipo kufanyeni nyinyi tulio kuabuduni badala ya Mwenyezi
Mungu kuwa ati ni sawa sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote katika kustahiki
kuabudiwa, juu ya kuwa hamjiwezi wala hamfai kwa lolote.
Rudi kwenye Sura
99. Wala hapana walio tutia katika hilaki hii ila wakosefu walio
tupotoa tukaiwacha Njia Iliyo Nyooka.
Rudi kwenye Sura
100. Basi hapana wa kuombwa akaja kutuvua na adhabu hii kama tulivyo
dhania pale kwanza.
Rudi kwenye Sura
101. Wala hapana rafiki wa kuwaonea uchungu kwa hali yao, licha
ya kuwaokoa.
Rudi kwenye Sura
102. Basi hapo ndio wanajitamania nafsi zao lau wangeli rejea duniani
wapate kuwa Waumini ili waokoke.
Rudi kwenye Sura
103. Na hakika katika khabari za Ibrahim zilizo tajwa yapo mawaidha
na mazingatio kwa mwenye kutaka mawaidha na akazingatia. Na wala si wengi
katika watu wako wanao somewa khabari hizi wenye kuitikia wito wako.
Rudi kwenye Sura
104. Na hakika hapana shaka Mola wako Mlezi ni Muweza wa kuwaadhibu
wanao kadhibisha, naye ni Mfadhili wa watu wema kwa neema nyingi.
Rudi kwenye Sura
105. Na Mwenyezi Mungu ametaja khabari za Nuhu kwa kauli yake: Kaumu
ya Nuhu iliukanusha Utume wake, wakamrudishia mwenyewe. Kwa kitendo hicho
ikawa wamewakadhibisha Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wito wao
ni mmoja katika asli yake na lengo lake.
Rudi kwenye Sura
106. Waliukanusha Utume huu pale alipo waambia ndugu yao Nuhu - ndugu
kwa makhusiano ya nasaba si kwa Dini - akiwahadharisha: Hamumchi Mwenyezi
Mungu, mkaacha kuabudu wenginewe?
Rudi kwenye Sura
107. Hakika mimi ni Mtume, nimetumwa kwenu nikuongoeni kwenye Njia
ya wongofu, na ni muaminifu wa kufikisha huu Ujumbe.
Rudi kwenye Sura
108. Basi mkhofuni Mwenyezi Mungu, na fuateni amri yangu katika hayo
ninayo kuitieni kwayo ya kumuamini Mwenyezi Mungu wa pekee na kumt'ii.
Rudi kwenye Sura
109. Na wala sitaki kwenu ujira kwa ajili ya ninayo kupeni ya nasaha
na wito. Na sina malipo ila kwa Mwenye kuwaumba viumbe wote, Aliye miliki
mambo yao.
Rudi kwenye Sura
110. Basi tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na fuateni ninayo
kuamrisheni.
Rudi kwenye Sura
111. Watu wa Nuhu, huku wakiukataa wito wake, walisema: Hatutokuwa
na imani nawe maadamu wanakufuata watu duni kabisa, wasio kuwa na hadhi
wala mali.
Rudi kwenye Sura
112. Nuhu akasema: Kitu gani cha kunijuvya uchache wa hadhi yao na
mali yao? Nikitakacho mimi kwao ni Imani yao bila ya kutafuta kuzijua kazi
zao.
Rudi kwenye Sura
113. Hapana wa kuwalipa kwa vitendo vyao na kazi zao ila Mola wangu
Mlezi; kwani Yeye ndiye anaye yajua vyema ya undani wao. Kama nyinyi
ni watu watambuzi mngeli tambua hayo.
Rudi kwenye Sura
114. Wala mimi siye wa kuwafukuza watu wanao uamini wito wangu vyovyote
itavyo kuwa hali yao ya ufakiri au utajiri, kwa sababu ati ya kukubalieni
nyinyi kwa mtakalo ili ndio mpate kuniamini.
Rudi kwenye Sura
115. Mimi si chochote ila ni Mtume niliye toka kwa Mwenyezi Mungu
kuwaonya walio wajibikiwa kwa onyo lilio wazi, kwa ushahidi wa kutenganisha
baina ya kweli na uwongo, bila ya farka yoyote baina ya mtukufu na mnyonge.
Basi vipi itanifalia mimi kuwafukuza Waumini kwa sababu ya ufakiri wao?
Rudi kwenye Sura
116. Wakasema: Ewe Nuhu! Ikiwa hutoacha huu wito wako basi jua yakini
tutakupopoa mawe. Yaani wanakusudia kwa haya kumtishia kumuuwa.
Rudi kwenye Sura
117. Nuhu kuonyesha kushikilia watu wake kuukadhibisha wito wake,
alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikanusha! Kuthibitisha
kuwa wanastahiki maapizo yake.
Rudi kwenye Sura
118. Basi tuhukumie baina yangu na wao, kwa hukumu ya kuwaangamiza
wanao pinga Upweke wako, na wakamkadhibisha Mtume wako! Na niokoe mimi
na Waumini walio pamoja nami na adhabu ya uasi wao.
Rudi kwenye Sura
119. Ndio hivyo tukamwokoa yeye pamoja na walio amini katika safina
iliyo pakia pomoni wao hao pamoja na mahitaji yao, kwa kuitikia dua yake.
Rudi kwenye Sura
120. Baada ya kuokoka kwa Nuhu na walio amini, Mwenyezi Mungu aliwazamisha
walio baki katika kaumu ya Nuhu walio kuwa hawakuamini.
Rudi kwenye Sura
121. Hakika katika yaliyo simuliwa na Qur'ani juu ya khabari za Nuhu
ni hoja ya kuthibitisha ukweli wa Mitume na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na
katika watu walio somewa hadithi hizi si wengi walio amini.
Rudi kwenye Sura
122. Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu za kumuadhibu
kila jabari mwenye inda, Mwenye kuwaneemesha wachamngu kwa kila namna ya
fadhila.
Rudi kwenye Sura
123. Kabila ya A'di ilimkanusha Mtume wao Hud a.s. Na kwa hivyo wakawa
ndio wamewakadhibisha Mitume wote, kwa kuwa wito wao ni mmoja katika asli
yake na lengo lake.
Rudi kwenye Sura
124. Alipo waambia ndugu yao Hud: Hamumwogopi Mwenyezi Mungu, mkamsafia
ibada?
Rudi kwenye Sura
125. Hakika mimi nimetumwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili nikuongoeni
mfuate uwongozi, na ni mwenye kuulinda ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Naufikisha
ujumbe huo kama alivyo niamrisha Mola wangu Mlezi.
Rudi kwenye Sura
126. Basi ifuateni amri ya Mwenyezi Mungu. Na ikhofuni adhabu
yake. Na t'iini ninayo kuamrisheni yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
127. Wala kwa hii nasaha yangu na uwongozi wangu sitaki kwenu ujira.
Sina malipo isipo kuwa kwa Muumba wa viumbe vyote.
Rudi kwenye Sura
128. Je! Mnasimamisha juu ya kila pahala palipo nyanyuka katika nchi
jengo refu kwa ajili ya kujifakhirisha, na mnakutana humo kwa mambo ya
upuuzi na fisadi? Mwenyezi Mungu Subhanahu anataka kwa haya kuwazindua
watende yatakayo wanufaisha, na anawatahayarisha kwa kuacha kwao Imani
na vitendo vyema.
Rudi kwenye Sura
129. Na mnajenga majumba ya fakhari na imara, na mahodhi ya maji,
kwa kutaraji kuishi milele katika dunia hii, kama kwamba hamtakufa.
Rudi kwenye Sura
130. Na mnapo ingia kutesa, mnapita kiasi katika uasi na uvamizi
wa jeuri, mnauwa, na mnapiga kwa chuki bila ya huruma.
Rudi kwenye Sura
131. Mwogopeni Mwenyezi Mungu katika kutumia nguvu, Na fuateni amri
yangu katika ninayo kuitieni. Kwani hayo hakika ndiyo yatakayo kukufaeni
na ndiyo yatakayo dumu zaidi.
Rudi kwenye Sura
132. Na tahadharini na ghadhabu za Mwenyezi Mungu aliye kukunjulieni
neema zake, kwa mnayo yajua yaliyo mbele yenu ya vipawa vyake vya namna
mbali mbali.
Rudi kwenye Sura
133. Kama alivyo kupeni mifugo kama ngamia, na ng'ombe, na kondoo,
na mbuzi, na wana wenye nguvu, wakukulindieni mifugo yenu, na kukusaidieni
katika shida za maisha.
Rudi kwenye Sura
134. Na mabustani yenye matunda, na chemchem zenye kutiririka maji
mnayo yahitajia.
Rudi kwenye Sura
135. Mimi nina khofu asije Mwenyezi Mungu akakuteremshieni adhabu
kali hapa duniani, na Akhera akakutieni katika Moto wa Jahannamu kwa sababu
ya ujabari wenu na starehe alizo kustarehesheni Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
136. Wakasema kwa kumkejeli: Ni sawa kwetu, ukitupa waadhi na kutuonya
au ukawa si katika wenye kutoa waadhi.
Rudi kwenye Sura
137. Haya uliyo tuletea si lolote ila ni uwongo na upotovu wa watu
wa zamani. Wao wamezoea kuzua kama hivyo. Kwa hivyo sisi hatutaacha tuliyo
kuwa nayo.
Rudi kwenye Sura
138. Wala sisi hatutaadhibiwa kwa vitendo tuvitendavyo.
Rudi kwenye Sura
139. Basi wakaendelea kushikilia kumkanusha. Mwenyezi Mungu akawafanyia
haraka kuwateketeza. Hakika katika hayo aliyo wateremshia Mwenyezi Mungu
kina A'di kwa kuwa ni malipo kwa ukanushi wao, ni hoja inayo juulisha ukamilifu
wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na si wengi katika wanao somewa khabari za
A'adi walio Waumini.
Rudi kwenye Sura
140. Na Mola wako Mlezi ndiye Mtenda nguvu wa kuwashinda hao majabari,
Mwenye kuwarehemu Waumini.
Rudi kwenye Sura
141. Kabila ya Thamud ilimkanusha Saleh katika Ujumbe wake na wito
wake, na kwa hivyo ikawa wamewakanusha Mitume wote, kwa kuwa asli ya Ujumbe
ni moja, na lengo ni moja.
Rudi kwenye Sura
142. Ewe Mtume! Watajie watu wako, wakati ule kina Thamud walipo
ambiwa na ndugu yao kwa uzao na uwananchi, si kwa dini, Saleh: Hamumwogopi
Mwenyezi Mungu, mkamuaabudu Yeye tu?
Rudi kwenye Sura
143. Hakika mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu kwenu kwa mambo yenye
kheri yenu na mafanikio yenu. Na mimi ni mwenye kuuhifadhi Ujumbe huu kama
nilivyo upokea kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
144. Kwa hivyo tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na nifuateni
kwa haya ninayo kuitieni kwayo kutokana na amri zake.
Rudi kwenye Sura
145. Wala sitaki kwenu ujira wowote kwa hii nasaha yangu na uwongozi
wangu. Ujira wangu uko kwa Mwenye kumiliki walimwengu wote.
Rudi kwenye Sura
146. Lilio wazuia ni kule kuamini kwao kwamba ati wataselelea katika
zile starehe, watasalimika na adhabu, na kutoweka, na mauti,
Rudi kwenye Sura
147. Katika mabustani ya matunda, na chemchem zenye kutoa maji matamu,
Rudi kwenye Sura
148. Na konde zilizo wiva, na mitende ambayo mazao yake yamedhihiri
mapevu na laini.
Rudi kwenye Sura
149. Na mnachonga milimani majumba kwa ufundi na ustadi katika hayo
mnayo yaunda.
Rudi kwenye Sura
150. Basi iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kuto mshukuru kwenu
kwa neema zake; na pokeeni nasiha yangu na muitende.
Rudi kwenye Sura
151. Wala msiit'ii amri ya walio pindukia mipaka kwa ushirikina na
kufuata pumbao na matamanio.
Rudi kwenye Sura
152. Ambao wanapitisha maisha yao katika ardhi kwa uharibifu, wala
hawafanyi ya maslaha ya kutengeneza nchi.
Rudi kwenye Sura
153. Wakasema: Wewe si chochote isipo kuwa miongoni mwa walio rogwa
kikweli mpaka zikapotea akili zao. Na katika jawabu hii mna ukali na usafihi.
Rudi kwenye Sura
154. Wewe si chochote ila ni mmoja unaye fanana na sisi kwa ubinaadamu,
basi yawaje uwe bora kuliko sisi kwa Unabii na Utume? Na ukiwa wewe ni
mkweli katika madai yako basi lete muujiza wa kuonyesha uthibitisho wa
Utume wako.
Rudi kwenye Sura
155. Saleh akawaambia - alipo pewa na Mwenyezi Mungu ngamia jike
kuwa ni muujiza wake: Huyu hapa ngamia jike wa Mwenyezi Mungu, amekutoleeni
kuwa ni Ishara. Yeye ana sehemu yake ya maji katika siku moja; siku hiyo
msinywe nyinyi. Na nyinyi mna sehemu yenu siku nyengine. Kunyweni siku
hiyo.
Rudi kwenye Sura
156. Wala msimletee madhara yoyote huyu ngamia, msije mkahiliki kwa
adhabu kubwa.
Rudi kwenye Sura
157. Wakamchinja ngamia, kinyume na walivyo wafikiana na Saleh. Kwa
hivyo wakastahiki kuwashukia adhabu, wakawa ni wenye kujuta kwa kitendo
chao hicho.
Rudi kwenye Sura
158. Basi ikawateketeza adhabu aliyo waahidi Saleh, wala majuto hayakuwakinga
na adhabu ya ukosefu wao. Hakika katika kusimulia kisa chao pana dalili
ya kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu kuwateketeza makafiri na kuwaokoa
Waumini. Na si wengi katika watu wako wenye kuamini.
Rudi kwenye Sura
159. Na hakika bila ya shaka aliye kuumba ndiye Yeye Muweza wa kuwateketeza
wapinzani, na Mfadhili wa kuwaokoa wachamngu.
Rudi kwenye Sura
160. Alipo waita Lut'i watu wake wamuabudu Mwenyezi Mungu pekee,
na waache ushirikina, waliwakanusha Mitume wote.
Rudi kwenye Sura
161. Ewe Mtume! Watajie watu wako pale Lut'i alipo waambia watu wake,
naye ni ndugu yao na shemeji yao:
Rudi kwenye Sura
162. Hakika mimi nimetumwa kwenu na Mwenyezi Mungu nikuleteeni Dini
ya Haki. Nami ni muaminifu wa kuifikisha Dini hii.
Rudi kwenye Sura
163. Basi tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na ifuateni amri
yangu kwa ninayo kuitieni.
Rudi kwenye Sura
164. Wala mimi sitaki kwenu ujira kwa uwongofu na uwongozi ninao
kuitieni. Sina ujira ila kwa Mwenye kumiliki viumbe vyote na Mlezi wao.
Rudi kwenye Sura
165. Lut'i alisema: Nyinyi mnastarehea kuwaingilia wanaume mkaacha
wanawake? Kwa hayo anakusudia kuyakanya yale waliyo yazoea ya vitendo vichafu.
"Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?" Yaani kazi ya liwat'i,
ambayo tangu asli yake ni ukosefu muovu, unao chusha hata kuusikia, kinyume
na maumbile, unao mteremsha mwanaadamu chini kabisa. Na lau kuwa unaenea
basi huharibu sunna ya kuoa, nayo ni sunna ya maumbile, hata uzazi ukatike
na ulimwengu usite kuendelea.
Na kwa liwat'i huenea maradhi kama yanavyo enea kwa uzinzi
kama tego, kisonono, donda ndugu, maradhi ya ngozi kama ukurutu, na hutokea
ishara za kudhoofika nyama za nyuma hata ikawa mtu hawezi kujizuia kutokwa
na choo ovyo. Na nyuma kwake mtu huchanua kukawa kama mdomo wa tarumbeta.
Na huko nyuma hujaa vijidudu vya maradhi na hivyo humuambukiza mwenye kumuingilia
na yeye hivyo vijidudu vikenda mletea maradhi mengine ya njia za mkojo.
Na huenda huyo mwenye kufanywa mambo hayo akawa mpumbavu hafai kitu, ikiwa
kaanza tangu utotoni. Na huenda akajidai kuonesha ujanadume mwingi kuliko
kiasi kwa kutaka kuficha upungufu wake wa uume. (Karibuni imedhihiri kuwa
maradhi ya khatari kabisa ya AIDS [Ukimwi] yameenea zaidi sana kwa watendao
kitendo hichi na watumiao madawa ya ulevi, ijapo kuwa na wazinzi nao hupata!).
Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ameukemea ukosefu huu katika
Aya kadhaa wa kadhaa, na akabainisha hikima ya Mwenye kuhukumu kwa kuharimisha
huku, kwa kusema: " Je! Katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?
Na mnaacha alicho kuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli
nyinyi ni watu mnao ruka mipaka!"
Rudi kwenye Sura
166. Na mnaacha aliyo kuumbieni Mwenyezi Mungu ya kustarehe na wake
zenu walio halali yenu? Ama hakika nyinyi ni watu mlio pindukia mipaka
ya udhalimu katika kufanya maasi.
Rudi kwenye Sura
167. Walikasirika kwa kule kuwakataza na kuwakemea kwa sababu ya
jambo ovu na wakasema: Kama hukuacha kutukebehi tutakutoa mji kwa izara
kubwa.
Rudi kwenye Sura
168. Lut'i akasema: Hakika mimi nakichukia mno hichi kitendo chenu,
wala sitoacha kabisa kukipinga na kukikebehi.
Rudi kwenye Sura
169. Na akamwomba Mola wake Mlezi amwokoe yeye na ahali zake na wayatendayo
wale wajinga, baada ya kwisha kata tamaa kuwa hawamsikilizi.
Rudi kwenye Sura
170. Mwenyezi Mungu akamuitikia ombi lake, akamwokoa yeye na wale
walio fuata wito wake, kwa kuwatoa wote majumbani mwao wakati wa kuteremka
adhabu kuwashukia wenye kukanusha.
Rudi kwenye Sura
171. Ila mkewe kizee aliye baki, na hakutoka nao. Yeye akaangamia
kwa kufuru zake na ukhaini wake, kwa kuwaunga mkono wakosefu.
Rudi kwenye Sura
172. Kisha Mwenyezi Mungu akawahiliki makafiri watendao uovu kwa
hilaki kali na mbaya.
Rudi kwenye Sura
173. Na Mwenyezi Mungu aliwateremshia wale watu wapotovu mawe kutoka
mbinguni, yakawateketeza. Na ilikuwa mvua ya kutisha kwa wingi wake na
namna yake. Basi mvua ovu ya walio kwisha onywa ni mvua hiyo, kwani iliteremka
kwa uangamizi mkubwa mno!
Rudi kwenye Sura
174. Hakika adhabu ile iliyo wateremkia watu wale hapana shaka ni
hoja yenye kuonyesha utimilivu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Wala si wengi
katika watu wako wenye kusadiki hayo.
Rudi kwenye Sura
175. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye kushinda
kila kitu, Mwenye kusifika kwa rehema iliyo kamilika. Huwapa adhabu watendao
dhambi, na huwalipa wema Waumini.
Rudi kwenye Sura
176. Hichi kisa cha Shuaibu pamoja na Watu wa Al Aykat, Machakani,
nao ni msitu wenye miti mizuri, karibu na Madian. Kikundi cha watu waliteremkia
hapo na wakakaa. Mwenyezi Mungu akawapelekea Shuaibu kama alivyo wapelekea
watu wa Madian. Wakamkadhibisha katika wito wake. Na kwa hivi wakawa wamekanusha
risala za Mitume wote.
Rudi kwenye Sura
177. Ewe Muhammad! Watajie watu wako pale Shuaibu alipo waambia watu
wa Machakani: Je! Hamumkhofu Mwenyezi Mungu mkamuamini? Wakaingia kumkadhibisha.
Rudi kwenye Sura
178. Hakika mimi nimetumwa na Mola Mlezi wa walimwengu wote nikuongoeni
na nikuongozeni. Nami ni muaminifu wa kuufikisha ujumbe wake kwenu.
Rudi kwenye Sura
179. Basi tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na nit'iini kwa
kufuata amri za Mwenyezi Mungu, na kuziokoa nafsi zenu na madhambi.
Rudi kwenye Sura
180. Na mimi kwa hivi kukuongozeni na kukufunzeni sikutakini ujira
wowote. Mimi sina malipo kaamili kwa sababu ya kazi yangu ila kutokana
na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
Rudi kwenye Sura
181. Shuaibu akawaamrisha kutimiza vipimo kwa ukamilifu wanapo pima,
kwani ilikuwa ada yao kupunguza kwa pishi na mizani, kupunguza haki za
watu kwa kuwapunja na kuwapimia kasoro.
Rudi kwenye Sura
182. Na wapimieni watu kwa mizani ya sawa sawa, ili wachukue haki
yao kwa uadilifu ulio nyooka.
Rudi kwenye Sura
183. Wala msiwapunguzie watu haki zao, wala msipite katika nchi mkifisidi
kwa kuuwa, na uharamia, na kufanya madhambi, na kufuata pumbao.
Rudi kwenye Sura
184. Na tahadharini na adhabu ya Mwenyezi Mungu aliye kuumbeni, na
akaumba kaumu zenye nguvu na takaburi zilizo tangulia.
Rudi kwenye Sura
185. Wakasema: Wewe si chochote ila ni mtu aliye sibiwa na uchawi
mkali na ikapotea akili yake.
Rudi kwenye Sura
186. Na wewe si chochote ila ni mmoja wetu sawa na sisi kwa utu.
Basi vipi ujipe ubora kuliko sisi kwa Utume? Nasi tunaamini kuwa wewe ni
mwongo wa kubobea.
Rudi kwenye Sura
187. Basi hebu tuangushie vipande vya adhabu kutoka mbinguni ikiwa
ni katika wasemao kweli kwa huu ujumbe wako! Na chini ya shauri hii
kwa hakika pana kila namna ya ubishi.
Rudi kwenye Sura
188. Shuaibu akasema: Mola wangu Mlezi ni Mjuzi, upeo wa kujua, wa
maasi yote myatendayo, na adhabu mnayo stahiki. Yeye atakuteremshieni hayo
kwa wakati wake alio ukadiria. Na huu ndio hadi ya mwisho wa kumwachilia
Mwenyezi Mungu kila kitu, na kuwatisha hao makafiri.
Rudi kwenye Sura
189. Lakini wao waliendelea kumkadhibisha. Mwenyezi Mungu akawapatiliza
kwa adhabu ya joto kuu mno. Wakawa wanatapa tapa hawana pa kukimbilia.
Walipo pata kiwingu cha kuwapa kivuli kukinga mwako wa jua walijikusanya
chini yake. Mwenyezi Mungu akawateremshia moto, ukawateketeza wote katika
siku ya kitisho kikubwa mno.
Rudi kwenye Sura
190. Hakika adhabu iliyo wateremkia watu wa Machakani kuwa ni malipo
ya uasi wao, ni dalili ya ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Na hawakuwa
wengi wa watu wako wenye kusadiki.
Rudi kwenye Sura
191. Na hakika Mola wako Mlezi hapana shaka ndiye Yeye aliye tengeka
kwa Nguvu na Ushindi, Mwenye kuwaneemesha Waumini kwa rehema nyingi.
Rudi kwenye Sura
192. Na hakika hii Qur'ani iliyo tajwa ndani yake visa vya kweli
imeteremshwa kutoka kwa Mwenye kuumba walimwengu wote, Mwenye kumiliki
mambo yao, na Mlezi wao. Basi khabari zake ni za kweli. Na hukumu yake
inatimizwa mpaka Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
193. Ameiteremsha Roho muaminifu, naye ni Jibril a.s.,
Rudi kwenye Sura
194. Juu ya moyo wako ulio tulia kuihifadhi na kuifahamu, na idhibitike
katika moyo wako iwe madhubuti isisahaulike, ili upate kuwaonya wakhalifu
kwa adhabu ziliomo ndani yake.
Rudi kwenye Sura
195. Jibril amekuteremshia kwa lugha ya Kiarabu, yenye maana wazi,
yenye hoja zilizo dhaahiri kwa wanayo hitajia ya kutengeneza mambo yao
ya dunia na Dini.
Rudi kwenye Sura
196. Na hakika kuitaja Qur'ani na kueleza kuwa inatoka kwa Mwenyezi
Mungu kumteremshia Muhammad s.a.w. yametajwa katika Vitabu vya Manabii
walio tangulia.
Rudi kwenye Sura
197. Je! Hawa wenye inda wanaikataa Qur'ani na hali wao wanayo hoja
inayo onyesha ukweli wa Muhammad s.a.w., nayo ni ilimu ya wanazuoni
wa Wana wa Issraili juu ya Qur'ani kama ilivyo katika vitabu vyao?
Rudi kwenye Sura
198. Na lau tungeli mteremshia mtu asiye kuwa Mwaarabu, anaye weza
kusema Kiarabu lakini si kwa ufasihi, wasingeli waza kumtuhumu kuwa kaizua.
Rudi kwenye Sura
199. Na angeli wasomea baraabara kinyume na ada bado wangeli mkanusha,
na wakapatia kisababu kwa ukafiri wao.
Rudi kwenye Sura
200. Sisi tumekutia huko kukanusha katika nyoyo za wakosefu;
na tumekuthibitisha kama tulivyo kuthibitisha katika nyoyo za wenye sifa
kama zao.
Rudi kwenye Sura
201. Basi hapana njia ya wao kuacha tabia yao ya ukafiri mpaka wateseke
kwa hiyo adhabu kali walio ahidiwa.
Rudi kwenye Sura
202. Itawateremkia adhabu kwa ghafla bila ya kuitaraji, wala wao
hawajui kama inakuja.
Rudi kwenye Sura
203. Watasema itapo teremka hiyo adhabu: Je, tutapewa muhula? Haya
ni kwa majuto kwa kupitiwa na Imani na kutaka waakhirishiwe adhabu. Lakini
hawajibiwi.
Rudi kwenye Sura
204. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Watu wa Makka wameghurika na
kuchelewesha kwangu kuwaadhibu, basi ndio wanaihimiza? Anakusudia
Subhanahu Aliye takasika kuzisafihi akili zao kwa sababu ya kuhimiza kwao
adhabu juu ya kuwaonya na kuwatisha.
Rudi kwenye Sura
205. Je, umefikiri ukajua, kama Sisi tuliwastarehesha kwa uhai
kwa muda wa miaka mingi pamoja na maisha mema?
Rudi kwenye Sura
206. Kisha ikawateremkia adhabu iliyo ahidiwa.
Rudi kwenye Sura
207. Kustarehe kwao kwa umri mrefu na maisha mema hakutowakinga hata
chembe na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwani adhabu ya Mwenyezi Mungu itakuja
tu, kama si leo kesho. Wala hapana kheri katika neema ambayo khatima yake
ni adhabu.
Rudi kwenye Sura
208. Na mwendo wetu kwa kaumu zote ni kuwa hatuuteketezi umma ila
baada ya kuwatumia Mitume wa kuwaonya kwa kufuata hoja,
Rudi kwenye Sura
209. Wakumbuke na wazingatie. Wala si shani yetu kudhulumu hata tuuadhibu
umma kabla ya kuwaletea Mtume.
Rudi kwenye Sura
210. Qur'ani inakataa waliyo yasema makafiri wa Makka ya kwamba Muhammad
anafuata majini, nao ndio wanampa Qur'ani. Qur'ani inasema: Mashetani
hawakuiteremsha hii Qur'ani.
Rudi kwenye Sura
211. Wala haiwafalii wao kuiteremsha, na hawawezi kufanya hivyo.
Rudi kwenye Sura
212. Kwani hao hakika wanazuiwa wasiisikie Qur'ani pale inapo funuliwa
kwa Muhammad s.a.w.
Rudi kwenye Sura
213. Basi wewe muelekee Mwenyezi Mungu ukiendelea na usafi wako wa
ibada, wala usishughulike na fisadi za madai ya washirikina na mwendo wao
muovu. Na hivi kutakiwa Mtume s.a.w. awe na ikhlasi ya namna hii ni wito
kwa jamii ya watu waliomo katika umma wake.
Rudi kwenye Sura
214. Watie khofu ya adhabu ya shirki na maasi walio karibu nawe katika
jamaa zako.
Rudi kwenye Sura
215. Na kuwa mpole kwa wanao itikia wito wako wa Imani.
Rudi kwenye Sura
216. Pindi wakikuasi na wasikufuate basi jitenge nao, na jitenge
na vitendo vyao vya ushirikina na maasi yote.
Rudi kwenye Sura
217. Na tegemeza mambo yako kwa Mwenye nguvu, Mwenye uweza wa kuwatenda
nguvu adui zako kwa utukufu wake, na kukunusuru wewe na kumnusuru kila
mwenye kufanya a'mali yake kwa usafi wa niya.
Rudi kwenye Sura
218. Ambaye anakuona pale unapo simama kwa ibada za usiku na vitendo
vyote vya kheri.
Rudi kwenye Sura
219. Na anaona mwendo wako kati ya wanao sali, kwa kusimama, na kukaa,
na kurukuu na kusujudu, pale unapo waongoza katika Sala.
Rudi kwenye Sura
220. Hakika Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kusikia dua zako na dhikri
zako, ndiye Mjuzi wa kujua niya yako na vitendo vyako. Ni kama kwamba Subhanahu
anamwambia: Usichukue taklifu kubwa bila ya kiasi katika mashaka ya ibada,
kwani uyatendayo yote nayaona na nayasikia Mimi.
Rudi kwenye Sura
221. Washirikina walisema: Mashetani ndio wanamsomea Qur'ani Muhammad.
Qur'ani ikawajibu: Nikupeni khabari watu gani Mashetani ndio wanawateremkia,
na wakawashawishi?
Rudi kwenye Sura
222. Wanamteremkia kila mwenye kubeba dhambi za namna mbaya kabisa
za uwongo, na madhambi ya kuchusha kabisa. Nao ni hao makohani mafisadi
ambao tabia zao na tabia za Mashetani ni jinsi moja na zimewafikiana.
Rudi kwenye Sura
223. Hao hutega masikio yao kwa Mashetani, na kwao wakapata mambo
ya dhana dhana tu. Na wengi wao ni waongo, na huzidisha tena juu ya kauli
walizo zipata kwa Mashetani.
Rudi kwenye Sura
224. Makafiri wanasema: Hii Qur'ani ni mashairi, na Muhammad ni mtungaji
mashairi. Mwenyezi Mungu ameyavunja haya kwa kuthibitisha kuwa hakika Qur'ani
imejaa hikima na hukumu. Mpango wake unapingana na mpango wa mashairi ambao
unategemea juu ya kweli na uwongo. Na amebainisha kwamba hali ya Muhammad
s.a.w. inapingana na hali ya watungaji mashairi. Yeye anasema kwa hikima,
wao wanasema kwa udanganyifu. Na hii ndiyo hali ya wengi katika watungaji
mashairi.
Rudi kwenye Sura
225. Kwani huwaoni vile wanavyo tangatanga katika mabonde ya maneno
wala hawaongoki kwenye Haki?
Rudi kwenye Sura
226. Na kwamba wao husema kwa ndimi zao wasio yaambatisha na vitendo
vyao?
Rudi kwenye Sura
227. Lakini walio hidika kwa hidaya ya Mwenyezi Mungu, na wakatenda
mema mpaka zikatua katika nafsi zao sifa bora, na wakamkumbuka Mwenyezi
Mungu kwa wingi mpaka ikathibiti khofu katika nyoyo zao, hawa basi huyafanya
mashairi kama dawa ilio sibu kwa ugonjwa wake. Na hupambana kwa ajili ya
kuiwania Dini yao na kusimamisha Haki, inapo kuwa Haki inafanyiwa jeuri.
Na walio dhulumu nafsi zao kwa shirki na kumkejeli Mtume kwa mashairi,
watatafuta wapi pa kuikimbia shari na hilaki wanayo iendea.
Rudi kwenye Sura