1. Nabii Muhammad (s.a.w.) katolewa Makka na kalazimishwa
kuihama kwa sababu ya vitimbi vya mapagani, washirikina, na kwa kuazimia
kwao kumuuwa, ili Waislamu wapate kuwa na dola yao. Naye akenda kukaa Madina
kwenye amani na manusura. Huko ikawa hapana budi ila kuwania kujilinda
na uvamizi wa maadui, wasije wenye Imani wakapata mateso. Vikatokea hivyo
Vita vya Badri. Waumini wakapata ushindi ulio wazi na ngawira nyingi waliziteka.
Ikatokea khitilafu kidogo na suala katika shauri la ugawaji wa hizo ngawira.
Ndio hivyo Mwenyezi Mungu anasema: Wanakuuliza khabari ya ngawira, zende
wapi? Apewe nani? Ni za nani? Zigawanywe vipi? Ewe Nabii! Waambie: Hizo
ngawira ni za Mwenyezi Mungu kwanza. Na Mtume, kwa amri ya Mola wake Mlezi,
ndiye mwenye madaraka ya kuzigawa. Basi wacheni kukhitalifiana kwa ajili
ya hayo. Na uwe mtindo wenu ni kumkhofu Mwenyezi Mungu na kumt'ii. Na tengenezeni
yaliyo baina yenu, na mfanye mapenzi na uadilifu ndio makhusiano baina
yenu. Kwani hakika hizi ndizo sifa za watu wa Imani.
Rudi kwenye Sura
2. Ama hakika Waumini wa haki na kweli daima wanakuwa na khofu na
ut'iifu kwa Mwenyezi Mungu. Akitajwa Allah Subhanahu, Mwenyezi Mungu Aliye
takasika, nyoyo zao hufazaika, na zikajaa khofu. Kwa hivyo kila wakisomewa
Aya za Qur'ani Imani yao inazidi kuwa imara, na wao huzidi unyenyekevu
na ujuzi, na wala hawamtegemei yeyote ila Mwenyezi Mungu aliye waumba,
na ndiye anaye walinda na kuwaendeleza.
Rudi kwenye Sura
3. Na hao Waumini walio wa kweli katika Imani, wanashika Sala kwa
kutimiza nguzo zake, na kukamilisha unyenyekevu na ut'iifu, ili wawe daima
katika kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na wanatoa katika mali aliyo waruzuku
Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la, kwa ajili ya Jihadi, na mambo yote
ya kheri, na kuwasaidia wanyonge.
Rudi kwenye Sura
4. Hakika hawa wanao sifika kwa sifa hizi ndio khasa wanao sifika
kwa Imani kwa haki na kweli. Na malipo yao ni kupata vyeo vya ngazi ya
juu kwa Mwenyezi Mungu. Yeye Allah Subhanahu ndiye ataye wapa radhi zake,
na maghafira wanapo teleza, na duniani atawapa riziki njema, na Akhera
neema ya daima.
Rudi kwenye Sura
5. Ushindi, bila ya shaka, upo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Na funguo
za mambo yote ziko kwake. Na hali ya Waumini katika kukhitalifiana kwao
katika mambo ya ngawira ni kama hali yao pale alipo kuamrisha Mwenyezi
Mungu utoke ukapigane na washirikina katika Badri, nayo ni Haki iliyo thibiti.
Kwani miongoni mwa Waumini kulikuwapo na kikundi kilicho chukia vita kweli
kweli.
Rudi kwenye Sura
6. Wanajadiliana nawe hao wa kikundi hicho, na wanajaribu kutilia
nguvu kauli yao katika jambo la haki, nalo ni kutoka kwa ajili ya Jihadi.
Na kumbe wao walikuwa na wenzao walio toka kwenda kupokonya mali ya Makureshi
yaliyo kuwa yanakwenda Sham, na wasiyapate. Kikundi hichi kikakhiari kurejea
baada ya kuona wamenusurika, kwa kujuvywa na Mtume, na kwamba makafiri
wanawaogopa, na kwa kuwa hadi wakivichukia vita, na kuwa hawajui litalo
wapata. Na walipo kuwa wakiviendea vita walikuwa kama wanao sukumwa kwenda
kufa, na wao wanaona kitacho wauwa, na yanawapata mateso yake.
Rudi kwenye Sura
7. Enyi Waumini! Kumbukeni ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwenu
kwamba atakupeni ushindi juu ya moja katika makundi mawili, hilo lenye
silaha na nguvu. Na hali nyinyi mnapendelea kupambana na hilo kundi jengine
lenye mali na watu tu. Na hilo ni msafara wa Abu Sufyan. Nanyi mkakhiari
mali yasiyo kuwa na wapiganaji. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka kuithibitisha
Haki kwa mapendo yake na uwezo wake na kwa maneno yake yaliyo kwisha tangazwa,
na ili aung'oe kabisa ukafiri katika Bara Arabu kwa ushindi wa Waumini.
Aya hizi tukufu zinatoa sura ya yanayo pita katika nafsi wakati
wa vita, nako ni kutamani kukutana na maadui wachache na kuchukia kukutana
na wengi, na kupenda kuteka mali na ngawira; na ilhali Mwenyezi Mungu Mtukufu
anataka kuitukuza Dini na ishinde Haki na wang'oke makafiri.
Rudi kwenye Sura
8. Ili athibitishe Haki, na auondoe upotovu, hata wakichukia makafiri
ambao wamedhulumu Haki ya Mwenyezi Mungu na Haki ya Waumini na Haki ya
nafsi zao wenyewe.
Rudi kwenye Sura
9. Na enyi Waumini! Kumbukeni nanyi mnagawana ngawira na mnakhitalifiana,
mlipo omba uwokovu na msaada, na mkaandikiwa kuwa hapana la kukuepusheni
na vita. Mwenyezi Mungu alikuitikieni maombi yenu, akakuungeni mkono kwa
kukuleteeni (Malaika) Roho zilizo safi nyingi zinazo fika elfu zinazo fuatana,
zikija moja baada ya moja.
Walipo jua wapiganaji Waumini kuwa hapana njia ya kuepukana na vita
wakaomba msaada kwa Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu Mtukufu akawaitikia,
na akawaunga mkono kwa Malaika elfu walio fuatana. Yaani alianza kwa kupeleka
msaada kwa vikosi vilivyo fuatana ili iwe wepesi kwa kila kikosi kuelekea
pahala pake katika vita pasiwepo kukaa bure au kupigana makumbo. Na ifikapo
misaada ya majeshi ya vita roho hufurahi na moyo huingia nguvu. Na hayo
ndiyo aliyo yakusudia Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kauli yake: "Na Mwenyezi
Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe." Na
ushindi daima unatokana na Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
10. Wala Mwenyezi Mungu Mtukufu hakujaalia huko kukuungeni mkono
kwa (Malaika) hizo Roho safi ila ni kuwa ni kukupeni khabari njema, kama
bishara kwenu kuwa mtashinda, mpate kutua nyoyo na msonge mbele. Na Mwenyezi
Mungu anakusaidieni, na wala ushindi hauji ila kwa msaada wa Mwenyezi Mungu,
Mwenye nguvu, Mwenye kushinda, ambaye anaye panga mambo kwa pahala pake
kwa mujibu wa ujuzi wake usio pitikiwa na chochote.
Rudi kwenye Sura
11. Enyi Waumini! Kumbukeni wakati mlipo ingiwa khofu kwa upungufu
wa maji, na kuwaogopa maadui. Mwenyezi Mungu alikupeni utulivu, kwa kukuleteeni
usingizi, mkalala mkatua. Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni mkajisafishia,
na mkauondoa wasiwasi wa Shetani, na nyoyo zenu zikawa imara kwa msaada
wa Rahmani na pia ardhi ikashikamana kwa hayo maji, na miguu yenu ikaweza
kukanyaga bila ya kudidimia katika mchanga.
Aya hii inaashiria fadhila ya Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya
wapiganaji Waumini kwa kupatikana hali ya amani kwa kupumzika kwa usingizi,
na kuteremka mvua kwa kujitahirisha na kukoga, na kushikamana mchanga kwa
kuwepo maji, basi nyayo zikasimama imara. Inajuulikana kuwa mchanga laini
unawaletea taabu wapiganaji na unakuwa pingamizi katika kwenda huku na
huko ambako ni katika dharura za vita muhimu. Na aya ya pili inaeleza maneno
ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaambia Malaika wawathibitishe Waumini na watie
khofu katika nyoyo za makafiri. Na ni maarufu kuwa khofu ikiwatawala askari
katika midani huwaletea kuemewa. Na katika Aya hii tukufu panaashiriwa
pahali pa kupiga napo ni juu ya shingo na kuvikata vidole vinavyo kamata
silaha mkononi.
Rudi kwenye Sura
12. Enyi Waumini! Kumbukeni pale Mwenyezi Mungu alipo wafunulia wale
wenye Roho zilio t'ahirika, yaani Malaika, watie ndani ya nyoyo zenu kuwa
Mimi ni pamoja nanyi, nakuungeni mkono, na ninakusaidieni, kwa kuwaambia:
Zitieni nguvu nyoyo za walio amini, wait'ii Haki na wapigane katika Njia
ya Mwenyezi Mungu. Na Mimi nitaifanya khofu izitawale nyoyo za washirikina,
nao watakuogopeni. Nanyi enyi Waumini! Wapigeni vichwani mwao vilio juu
ya shingo zao, na kateni vidole vyao vinavyo kamata panga.
Rudi kwenye Sura
13. Ukawa ushindi na kuungwa mkono nyinyi, na kwao ni kitisho na
fazaa, kwani wao walikuwa upande mmoja, na Mwenyezi Mungu na Mtume wake
walikuwa upande mwengine, kwa kuwa wao walimpinga Mwenyezi Mungu
na Mtume wake. Basi ndio Mwenyezi Mungu anawateremshia adhabu chungu. Na
adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.
Rudi kwenye Sura
14. Enyi Waumini! Hivyo ndio vita, basi vionjeni, na muwe na yakini
kuwa mtapata nusura na kuungwa mkono. Na wanao pinga Ishara za Mwenyezi
Mungu watapata adhabu nyengine Siku ya Kiyama, nayo ni adhabu ya Moto.
Rudi kwenye Sura
15. Enyi mlio isadiki Haki na mkait'ii! Mkikutana na wale walio kufuru
katika uwanja wa vita nao wanakujieni kwa wingi wao, msiwakimbie mkazipa
mgongo panga zao.
Rudi kwenye Sura
16. Na asiye wakaabili uso kwa uso, basi Mwenyezi Mungu amekasirika
naye, na marejeo yake ni Motoni. Na huo ndio mwisho muovu kweli. Na mwenye
kuacha kuwakaabili kwa kuwa ni hila na mbinu za vita, au kaacha kikosi
kwenda jiunga na kikosi kingine cha Waumini apate kuwa na nguvu zaidi za
mpambano, huyo hana dhambi.
Rudi kwenye Sura
17. Na nyinyi Waumini, pale mnapo washinda, na mkawauwa mlio wauwa
katika wao, basi hakika si nyinyi mlio wauwa kwa nguvu zenu, lakini ni
Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliye kupeni ushindi na kuweza kuwauwa, kwa
msaada wake kwenu na kutia khofu katika nyoyo zao. Na wewe Mtume, pale
ulipo warushia mchanga na kokoto nyusoni mwao kuwafazaisha, si wewe ulio
rusha, lakini ni Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliye rusha, na wao wakafazaika.
Na hayo Mwenyezi Mungu ameyafanya kuwaneemesha Waumini kwa neema njema.
Katika hayo pana majaribio ya nguvu kwao, ili ionekane ikhlasi yao, na
kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua mambo yao, Mwenye kusikia maneno
yao, na Mwenye kujua mambo ya maadui zao na kauli zao pia.
Rudi kwenye Sura
18. Huo ndio ushindi mkubwa, na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye
kudhoofisha kila hila za makafiri.
Rudi kwenye Sura
19. Ikiwa nyinyi washirikina mlikuwa mkining'inia mapazia ya Al Kaaba
na huku mnaomba yapambanuliwe baina yenu na Waumini ijuulikane haki ipo
wapi, basi sasa imekwisha kujieni hukumu ya kupambanua, na ushindi si wenu,
bali ni wa Waumini. Na nyinyi mkirejea tena kufanya uadui Nasi tutakushindeni
tena. Wala kukusanyika kwenu kwa ajili ya madhambi hakutakufaeni kitu!
Hata ikiwa idadi yenu kubwa vipi! Kwani hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja
na wanao isaidiki Haki na wanaikubali.
Rudi kwenye Sura
20. Enyi mlio isadiki Haki, na mkaifuata! Hakika mmejua ushindi umepatikana
kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na kumt'ii Mtume wake. Basi endeleeni kumt'ii
Mwenyezi Mungu na Mtume. Wala msiupuuze wito wa Mtume anao itia Haki, nanyi
mnamsikia na mnafahamu ayasemayo.
Rudi kwenye Sura
21. Wala msiwe kama wanaafiki wanao sema: Tumeisikia Haki na tumefahamu.
Lakini hawaifuati wala hawaiamini. Basi wamekuwa kama wasio sikia.
Rudi kwenye Sura
22. Hao washirikina na wanaafiki ni kama wanyama waovu kabisa walio
sibiwa na uziwi, kwa hivyo hawasikii; na wakasibiwa na ububu, kwa
hivyo hawasemi. Basi wao ni viziwi kwa Haki, na hivyo hawasikii, wala hawaitamki
na hawaielewi!!
Rudi kwenye Sura
23. Na Mwenyezi Mungu kwa ilimu yake ya tangu na tangu lau angeli
ona ndani yao kuwa, katika hali yao hivi sasa, itakuja patikana kheri
yoyote kwao hao kwa nafsi zao, na kwa watu, na kwa Haki, basi angeli wafanya
wasikie kusikia kwa kuongoka hata Haki ikaingia akilini mwao. Na hata wangeli
isikia na wakaifahamu Haki basi bado wasingeli ifuata. Na mapuuza hayawaachi
kwa kuzidiwa na pumbao.
Rudi kwenye Sura
24. Enyi mlio isadiki Haki na mkaifuata! Muitikieni Mwenyezi Mungu
kwa kufikisha anayo kuamrisheni. Na muitikieni Mtume katika vile anavyo
fikisha anayo yaamrisha Mwenyezi Mungu, pale anapo kuiteni Mtume kufuata
amri za Mwenyezi Mungu ambazo zitakuleteeni uzima wa miili yenu, na roho
zenu, na akili zenu, na nyoyo zenu. Na mjue kwa yakini kuwa Mwenyezi Mungu
ni Mwenya kuangalia nyoyo zenu. Huzielekeza atakavyo. Basi Yeye huingilia
baina yenu na nyoyo zenu zinapo ingiliwa na matamanio, Yeye basi
hukuokoeni nayo ikiwa nyinyi wenyewe mnajielekeza kwenye Njia iliyo nyooka.
Na nyinyi nyote mtakusanywa kwake Siku ya Kiyama, na huko ndiko malipo
yatakuwa.
Rudi kwenye Sura
25. Na jikingeni na Dhambi kubwa ya kufisidi jamii yenu, kama vile
kuacha kwenda kwenye Jihadi, na kufarikiana mkagawana mapande mapande,
na kama kuacha kuamrisha mema na kukataza maovu. Kwani Fitna hiyo, Dhambi
hiyo, haiwapati wale walio dhulumu peke yao, bali inawapata wote. Na mjue
kuwa bila ya shaka kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali hapa duniani na
Akhera pia.
Rudi kwenye Sura
26. Na hebu kumbukeni, enyi Waumini, katika hali ya kuwa mna nguvu,
pale mlipo kuwa wachache na wanyonge. Maadui walikudhilini kwa unyonge
wenu, nanyi mlishikwa na khofu wasije maadui zenu kukunyakueni. Basi tena
mkahama kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na makaazi yenu yakawa Yathrib (Madina).
Na mkapata manusura kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na tawfiki yake, na akakuruzukuni
ngawira njema kutaraji mtashukuru kwa neema hii, na muendelee katika Njia
ya Jihadi kulinyanyua Neno la Haki.
Rudi kwenye Sura
27. Enyi mlio isadiki Haki mkaifuata! Haikufaliini kumkhini Mwenyezi
Mungu na Mtume wake kwa kufanya urafiki na maadui wa Haki, na kukhuni katika
ngawira, au kwa kuacha kwenda kwenye Jihadi. Wala msikhuni amana mnazo
pewa nanyi mnajua amri na makatazo yake.
Rudi kwenye Sura
28. Enyi Waumini, wenye kusadiki! Jueni kuwa fitna ya nafsi zenu
inatokana na kupita mpaka katika mapenzi yenu kwa watoto wenu na mali yenu.
Basi isiwe kupenda kwenu kuyapenda mali na wenenu yakazidi kuliko mapenzi
ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hayo yatakuharibieni mambo yenu. Na jueni kuwa
malipo ya Mwenyezi Mungu yanakutosheni kuliko mali na watoto.
Rudi kwenye Sura
29. Enyi mlio isadiki Haki na mkaifuata! Mkizinyenyekea amri
za Mwenyezi Mungu kwa siri na dhaahiri, Mwenyezi Mungu atakujaalieni katika
nafsi zenu uwezo wa kupambanua baina ya Haki na upotovu, na atakutunukieni
ushindi wa kutenga baina yenu na maadui zenu, na atakusitirieni maovu yenu
yaondoke, naye akusameheni. Na Yeye Subhanahu daima ni Mwenye fadhila kubwa.
Rudi kwenye Sura
30. Na kumbuka ewe Nabii, neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yako,
pale washirikina walipo panga njama kukutia nguvuni - ama wakufunge, au
wakuuwe, au wakutoe mji! Hakika walikupangia mipango miovu! Na Mwenyezi
Mungu Mtukufu alikupangia utokane na shari yao. Na mpango wa Mwenyezi Mungu
ndio wa kheri, na una nguvu zaidi, na ndio wenye kushinda.
Rudi kwenye Sura
31. Na ewe Nabii! Kumbuka inda ya washirikina ulipo kuwa ukiwasomea
Aya za Qur'ani Tukufu, nazo ni Ishara zetu. Ujahili wao na ghururi yao
iliyo pita kiasi iliwapelekea kusema: Tungeli taka kusema kama isemavyo
hii Qur'ani tungeli sema; kwani humu hamna chochote ila visa walivyo viandika
watu wa kale!
Rudi kwenye Sura
32. Na kumbuka, ewe Nabii, vipi walivyo kuwa wanakupinga na kumpinga
Mwenyezi Mungu hata kwa inda yao wakasema kumwambia Mwenyezi Mungu, Mola
wao Mlezi: Ikiwa haya unayo kuja nayo ni mambo madhbuti, basi zijaalie
mbingu zitunyeshee mawe, au tuletee adhabu yoyote iliyo kali yenye uchungu!
Rudi kwenye Sura
33. Si katika hikima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaadhibu katika
dunia kwa adhabu kali na hali wewe upo miongoni mwao unaitia Haki, nawe
unataraji asaa wataitikia. Wala si mtindo wa Mwenyezi Mungu kuwaadhibu
wenye kuasi nao wangali wanamuomba maghfira na wamo kuyavua yale waliyo
nayo.
Rudi kwenye Sura
34. Hakika hali yao iliyo sasa inaruhusu kuwaadhibu, kwani wanawazuia
watu wasiutumie Msikiti ambao Mwenyezi Mungu ameutukuza kwa kuharimisha
vita karibu yake. Lakini Mwenyezi Mungu anawaakhirisha kwa alivyo wakadiria
katika ujuzi wake kuwa wengi wao watakuja amini. Wao wakati huu wa sasa
sio walinzi wa kuunusuru huo Msikiti Mtukufu, bali wao wameunajisi kwa
kutia ibada ya masanamu ndani yake. Ama wa kuunusuru hakika ni Waumini,
wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu. Lakini wengi katika washirikina hawaijui
Dini, wala hawajui cheo cha Nyumba hiyo Tukufu.
Rudi kwenye Sura
35. Na maombi yao kwenye Nyumba hii Tukufu (Al Kaaba) si chochote
ila ni kupiga myunzi na makofi. Ilivyo kuwa hiyo ndiyo hali yenu, basi
wacha mauti yakupateni, na yaonjeni katika uwanja wa vita, upate kubaidika
ushirikina kutokana na Al Kaaba. Na kuuliwa huko kwenu ni kwa sababu ya
ukafiri wenu.
Rudi kwenye Sura
36. Hakika hao wanao zipinga Ishara za Mwenyezi Mungu na wanamshirikisha
na miungu mingine, hutoa mali yao ili wawazuie watu wasiifuate Imani ya
Haki! Nao wataendelea kutoa hayo mali, kisha hayo mali, kwa kuwapotea bure
bila ya pato walitakalo, yatawaletea majuto na machungu. Na katika uwanja
wa mpambano watashindwa hapa duniani, na kisha watakusanywa wote katika
Jahannam, wakibaki na ukafiri wao.
Rudi kwenye Sura
37. Kwa kushindwa makafiri duniani na kuadhibiwa Motoni Akhera Mwenyezi
Mungu anapambanua aliye khabithi wa roho na vitendo na maneno, awe mbali
na aliye mwema wa roho yake na moyo wake. Na awafanye wale waovu makhabithi
wapandane wenyewe kwa wenyewe, huyu juu ya huyu, na awatie Motoni Siku
ya Kiyama. Na hao washirikina mafisadi ndio wenye kukhasiri peke yao, duniani
na Akhera.
Rudi kwenye Sura
38. Hakika juu ya vitisho hivi, mlango wa matarajio ungali wazi.
Basi ewe Nabii wa rehema! Waambie hawa wapinzani kuwa wakikoma, wakaacha
inadi yao na ushirikina wao, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atawasamehe
vile vitendo vyao vilivyo kwisha pita. Na wakiendelea na upotovu wao, na
wakarudia tena kukupigeni vita, basi mwendo wa Haki kwa walio tangulia
umethibiti utakuwa ule ule, nao ni kuwa Haki lazima iushinde upotovu, pindi
ikiwa wale watu wa Haki wakishika ut'iifu na njia za ushindi.
Rudi kwenye Sura
39. Na endeleeni kuwapiga vita washirikina mpaka waache kuharibu
itikadi za Waumini kwa kuwatesa na kuwaudhi. Wakiacha ukafiri na kuwaudhi
Waumini, na wakamsafia Dini Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuvijua vitendo vyao, na atawalipa kwavyo.
Rudi kwenye Sura
40. Na wakiendelea na kupuuza kwao na kuwaudhi Waumini, basi enyi
Waumini, jueni ya kuwa nyinyi mko katika ulinzi wa Mwenyezi Mungu, na huo
ndio ulinzi wenye kupendeza na wenye nguvu kabisa. Na Yeye ndiye Mwenye
kukunusuruni, na nusura yake ndio yenye nguvu zaidi na bora zaidi.
Rudi kwenye Sura
41. Na enyi Waislamu! Jueni kuwa katika mali ya makafiri mliyo yateka,
hukumu yake ni kugawiwa mafungu matano. Fungu moja ni la Mwenyezi Mungu
na Mtume, na jamaa zake Mtume, na mayatima, nao ni watoto wadogo wa Waislamu
waliofiwa na baba zao nao ni mafakiri; na masikini, nao ni wale Waislamu
wenye haja; na msafiri, naye ni mwenye kukatikiwa safari yake ya halali.
Na yaliyo khusishwa katika hiyo sehemu moja katika tano kuwa ni ya Mwenyezi
Mungu na Mtume hukhusishwa kwa maslaha ya umma kama anavyo pasisha Mtume
katika uhai wake, au, baada ya kufa kwake, Imam. Na yaliyo baki katika
ile Khumsi watapewa walio kwisha tajwa. Ama sehemu nne nyengine katika
ghanima (ngawira), na Aya ikanyamaza kimya juu yake, ni za wale walio pigana.
Basi jueni hayo, na myajue ikiwa mmemuamini Mwenyezi Mungu kweli, na mmeziamini
Ishara tulizo mteremshia mja wetu, Muhammad, za kumthibitisha na kumsaidia,
siku ya Mpambanuo, tulipo pambanua baina ya ukafiri na Imani, nayo ndiyo
siku lilipo kutana kundi lenu na kundi la makafiri katika Badri. Na Mwenyezi
Mungu Mwenye kudra kubwa juu ya kila kitu aliwapa ushindi Waumini juu ya
uchache wao, kuwashinda makafiri juu ya wingi wao.
Rudi kwenye Sura
42. Na kumbukeni mlipo kuwa bondeni ng'ambo hii ya karibu na Madina,
na wao makafiri wako ng'ambo ile ya mbali, na msafara wenye bidhaa mlio
kuwa mnautaka uko karibu zaidi nanyi upande wa baharini. Na lau kuwa
mmepeana miadi ya kukutana kwa kupigana basi msinge wafikiana hivyo. Lakini
Mwenyezi Mungu kapanga mkutane bila ya miadi, na bila ya kutaka wao, ili
apate kutekeleza jambo ambalo katika ujuzi wake limekwisha thibiti litokee
tu, wala hapana jenginelo. Jambo lenyewe ni kuwa vitokee vita vitavyo pelekea
nyinyi mshinde na wao washindwe. Ipate kuondoka shaka - wateketee wa kuteketea
kwa hoja wazi ya kuonekana, nako ni kushindwa makafiri juu ya wingi wao;
na wahuike Waumini kwa hoja iliyo wazi, nako ni kushinda kulio toka kwa
Mwenyezi Mungu kuwapa Waumini wachache. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusikia na kujua. Haimfichikii kauli wala niya yoyote ya pande zote mbili.
Rudi kwenye Sura
43. Na kumbuka, ewe Mtume! Pale Mwenyezi Mungu alipo kufadhili kwa
kukuonyesha usingizini ndoto ya kuwa hilo jeshi la maadui ni dogo, ili
akutulizeni nyoyo muamini kuwa mtawashinda, kwa hivyo muwe imara kuwakaabili.
Na lau angeli kuacheni muwaone wengi, bila ya kukuthibitisheni kwa ndoto
hiyo, mngeli waogopa, na mkasita sita kupigana nao, na mngeli emewa, na
mkazozana msonge mbele au mrudi. Lakini Mwenyezi Mungu amekuvueni
na hayo, na akakuokoeni na matokeo yake, kwani hakika Yeye ni Mwenye kuyajua
vyema yaliyomo ndani ya vifua vya watu.
Rudi kwenye Sura
44. Na kumbuka, ewe Mtume! Alipo kuonyeshemi Mwenyezi Mungu
kuwa maadui zenu mnapo kutatana nao ni wachache katika macho yenu, kama
alivyo waonyesha wao kuwa nyinyi ni wachache, na kwa kuwa tangu hapo wao
wana ghururi ndani ya nafsi zao kuwa ni wengi, ili kila mmoja wenu awanie
kupigana na mwenzie, na kwa hivyo yatimie aliyo kwisha yaamrisha Mwenyezi
Mungu. Na ilikuwa hapana budi hayo yatimie. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio
hurejea mambo yote ya ulimwengu. Halitendeki jambo ila alilo kwisha
lihukumia na kuzitengeneza sababu zake.
Rudi kwenye Sura
45. Enyi mlio amini! Mkikutana na kikosi cha wapiganaji katika adui
zenu, basi kuweni imara, wala msiwakimbie. Na mkumbukeni Mwenyezi Mungu
kwa kufuata uwezo wake, na ahadi yake ya kuwasaidia Waumini, mkikithirisha
kumkumbuka na kumtaja pamoja na kuwa imara na kusubiri. Mkifanya hivyo
ndio matarajio yenu ya kupata mafanikio yatapo timia.
Rudi kwenye Sura
46. Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika mambo mlio amrishwa
na mlio katazwa. Na wacheni kuzozana na kukhitalifiana. Hayo ndiyo yanayo
pelekea kupoteza nguvu na kushindwa. Na vumilieni mkipata shida za vita.
Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanao vumilia wakasubiri kwa kuwapa
msaada na kuwaunga mkono, na kuwalipa malipo mema.
Rudi kwenye Sura
47. Wala msiwe kama wale walio toka kwenye majumba yao, nao wana
ghururi (udanganyifu) kwa nguvu na neema walizo nazo, wakijifakhari na
kujionyesha mbele za watu, wakitaka wasifiwe kwa ushujaa na ushindi, na
wao huku wanapinga watu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanaupinga Uislamu.
Na Mwenyezi Mungu amevizunguka vitendo vyao kwa ujuzi na uwezo. Na Yeye
atakuja walipa duniani na Akhera.
Rudi kwenye Sura
48. Na kumbukeni, enyi Waislamu! Pale Shetani alipo kuja kuwazaini
hawa washirikina kwa kuwaonyesha kuwa wayatendayo ni mazuri kwa uchochezi
wake, akiwaambia: Hapana mtu ye yote anaye weza kuwashinda. Na akawahakikishia
kuwa yeye atawalinda, na kuwanusuru! Yalipo kutana makundi mawili katika
vita, vitimbi vyake na uchochezi wake ukavunjika. Akarejea nyuma, na akajitoa
nao, akaogopa Mwenyezi Mungu asimuangamize. Na Mwenyezi Mungu ni Mkali
wa kuadhibu.
Rudi kwenye Sura
49. Na kumbuka ewe Mtume! Walipo sema wanaafiki miongoni mwa makafiri
na wale wenye Imani dhaifu walipo kuoneni mmesimama imara: Hawa Waislamu
wameghurika kweli na dini yao! Na hakika mwenye kumwakilisha Mwenyezi Mungu
jambo lake, na akamuamini Yeye, na akamtegemea Yeye, basi hapana shaka
kuwa Mwenyezi Mungu atamkifia amwondolee hamu yake, na atamnusuru na maadui
zake. Kwani hakika Mwenyezi Mungu madaraka yake yana nguvu, naye ni Mwenye
hikima katika mipango yake.
Rudi kwenye Sura
50. Na lau kuwa unaona, ewe Mtume, kile kitisho kikubwa, kinacho
wateremkia hawa makafiri, wakati ule Malaika wanapo wafisha na kuwang'oa
roho zao, nao wakiwapiga mbele na nyuma, na wakiwaambia: Onjeni adhabu
ya Moto kwa sababu ya vitendo vyenu viovu!!
Rudi kwenye Sura
51. Na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja wake kwa
kuwaadhibu kwa madhambi waliyo yatenda. Bali huo ni uadilifu, kwa sababu
hawawi sawa muovu na mwema. Basi kuadhibiwa kwake ni kwa vitendo viovu
alivyo vitenda mwenyewe.
Rudi kwenye Sura
52. Hakika ada ya hawa washirikina, na shani yao katika ukafiri,
ni kama shani ya Mafirauni na majabari wote walio baki walio kuwa kabla
yao. Walizipinga Ishara za Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu aliwaadhibu
kwa madhambi yao. Wala Yeye si mwenye kuwadhulumu. Hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwenye nguvu katika kutekeleza hukumu yake, na Mkali wa kumlipa anaye
stahiki adhabu.
Rudi kwenye Sura
53. Na huu ni uadilifu katika kulipa, kwa sababu Mwenyezi Mungu hakika
haibadilishi neema anayo waneemesha watu, kama vile neema ya amani, kutononoka,
na afya, mpaka wao wenyewe waigeuze hali yao na sababu zake! Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuyasikia wayasemayo, na Mwenye kuyajua wayatendayo.
Rudi kwenye Sura
54. Kama ilivyo kuwa ada yao na mtindo wao hawa katika kuzikanusha
Ishara za Mwenyezi Mungu na neema zake ni kama mtindo wa watu wa Firauni
na walio watangulia, hali kadhaalika ada yao na shani yao katika kuendelea
kuwakadhibisha Mitume wake, na dalili za Unabii wao, ni kama ada ya watu
wa Firauni na walio kabla yao. Basi wamefanana hao katika kukanusha Ishara,
na kuupinga Utume wa Mitume, na kuwakadhibisha, na kuendelea juu ya mwendo
huo vile vile. Na kila mmoja Mwenyezi Mungu amemtia mkononi kwa dhambi
zake -wale kwa midharuba, na vimbunga, na kadhaalika; na watu wa Firauni
kwa kuwazamisha. Na wote walikuwa ni madhaalimu wa nafsi zao. Kwa hivyo
walistahiki adhabu iliyo wafika.
Rudi kwenye Sura
55. Hakika katika vyote vilio enea juu ya uso wa ardhi walio
waovu mno mbele ya Mwenyezi Mungu katika hukumu yake na uadilifu wake,
ni makafiri walio kakamia juu ya ukafiri wao,
Rudi kwenye Sura
56. Nao ni wale ulio fungamana nao kwa mikataba, nao wakawa
hawaachi kuivunja kila mara; na watu hao ni Mayahudi ambao hawachelei utukufu
wa Mwenyezi Mungu, wala hawakhofu kupatilizwa naye, wala adhabu yake.
Rudi kwenye Sura
57. Basi ewe Mtume! Ukiwakuta hawa wavunjao mapatano, na ukasadifiana
nao katika vita nawe umeshinda, basi watishe baraabara kwa kuwapa
adhabu ya kuwatia uchungu na kuwaogopesha wale walio nyuma yao, upate kuwafarikisha
walio baki. Mateso haya ndiyo ya kuwakumbusha uovu wa kuvunja mapatano,
na kuwazuia wenginewe wasitende kama hayo.
Katika Aya tukufu hizi tunahadharishwa na wale wanao toa ahadi na
kisha wakazivunja. Hawa yafaa wapewe adhabu ya kutia mfano kwao na kwa
walio nyuma yao. Na katika Aya hii unabainishwa umuhimu wa kuvuruga askari
wa adui walio nyuma. Hizi ni mbinu za vita za kisasa, kwani kuzua vurugo
katika askari wa nyuma hutosha kuleta fujo na kupelekea jeshi kutawanya
askari wake kulinda mgongo wake, na kwa hivyo zinavunjika nguvu zake.
Juu ya hivyo katika sehemu za nyuma katika midani ndio huwapo mambo
yaliyo khusu idara ya jeshi ambayo juu yake ndio jeshi linategemea kwa
msaada. Ukileta vurugu hapa hupelekea kukosekana nidhamu yote ya jeshi,
na kwa hivyo ndio huleta kuemewa na kushindwa.
Rudi kwenye Sura
58. Na ukiona alama za hao watu kutaka kuleta khiana kuvunja maagano
yaliyo baina yako na wao, ikate njia yao wasiweze kukukhuni, kwa kuwatangazia
wewe kuvunja hayo mapatano, mpaka walijue jambo lako, na wasiweze kukukhuni.
Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi makhaini, wala haridhii kuwa nyinyi msifike
kwa sifa yao.
Rudi kwenye Sura
59. Wala wasidhani walio kufuru kuwa wamekwisha tangulia na wameiepuka
adhabu ya kukhuni kwao na kwenda kinyume! Wao kabisa hawatamshinda Mwenyezi
Mungu asiwazunguke na kuwatia nguvuni, bali Yeye peke yake ni Muweza, na
atawalipa kwa nguvu zake na uadilifu wake.
Rudi kwenye Sura
60. Enyi Umma wa Kiislamu! Tayarisheni kila muwezavyo nguvu za vita
za namna zote kwa ajili ya kujizatiti kwa ajili ya kupigana, na wekeni
askari walinzi na farasi wao mipakani na kando kando ya nchi, ili
kwa hivi mjitayarishe na ulinzi mwatie kiwewe adui za Mwenyezi Mungu na
adui zenu miongoni mwa hao makafiri ambao wamo kungojea likupateni jambo.
Na pia mpate kuwatishia wenginewe ambao nyinyi hamwajui
hivi sasa, lakini Mwenyezi Mungu anawajua, kwani hapana jambo
linalo jificha kwake. Na kila mnacho kitoa kwa kuzitayarisha nguvu zenu
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi Yeye atakulipeni malipo ya kutosha, bila
ya kupunguka hata chembe katika mnayo stahiki katika fadhila ya Mola wenu
Mlezi
Katika Aya hii tukufu pana kuhimizwa na kuamrishwa kujitayarisha
kwa ajili ya kupambana na adui. Kwani vita, zamani na sasa, ni jambo la
khatari na muhimu kabisa. Juu yake inategemea kheri na shari, kufa kupona
kwa umati na umati. Basi yapasa kujitayarisha, kujizatiti, na kujitengeneza
kwa jiha mbali mbali za vifaa na silaha na zana. Kuingia vitani bila
ya kujipatia zana zote na kujitayarisha ni kutafuta kushindwa. Na tunaona
hivi sasa madola yanavyo jiandaa wakati wa amani na vita, na yanavyo jenga
siasa zao na mipango yao na wanavyo kusanya uwezekano wao wote ili wapate
ushindi katika vita. Na vita sasa havimsazi mtu. Wanashiriki katika vita
wanajeshi na raia. Kwa hivyo ndio inapasa zaidi kujitengeneza kila mmoja
wao kwa matengenezo ya kuwakusanya na kuwaweka tayari wote ili upatikane
ushindi.
Rudi kwenye Sura
61. Maadui wakielekea kutaka amani na kuacha uadui wao, basi nawe
ewe Mtume, elekea kwenye amani. Kwani vita sio lengo, bali wewe unakusudia
kujilinda tu na uadui wao na upinzani wao kupinga wito wako. Basi kubali
amani, na umtegemee Mwenyezi Mungu, wala usikhofu vitimbi vyao na njama
zao! Yeye Subhanahu ni Mwenye kuzisikia njama zao, ni Mwenye kuijua mipango
yao. Hapana kinacho fichikana kwake.
Huu ni msingi mkuu katika misingi ya Uislamu, Dini ya Salama. Na
leo tunasikia kila dola duniani ina nadi Usalama, na kwa hivyo ukaundwa
Umoja wa Mataifa.
Rudi kwenye Sura
62. Ikiwa hao maadui wanataka kukukhadaa na kukufanyia ujanja kwa
hivyo kuonyesha kuwa wanataka amani, basi Mwenyezi Mungu anakutosheleza
kukulinda na vitimbi vyao kwa kila upande. Kwani Yeye alikwisha tangulia
kukuunga mkono kwa kukupa ushindi pale alipo kutengenezea sababu zilizo
onekana na za siri za kutia imara nyoyo za Waumini katika Wahajiri, wahamiaji
walio toka Makka, na Ansari, wasaidizi wa Madina.
* Rudi kwenye Sura
63. Na Mwenyezi Mungu akawaweka pamoja kwa mapenzi baada ya
mtafaruku na uadui, hata wakawa marafiki mbele yako, wakizisabilia roho
zao na mali yao kwa ajili ya wito wako. Na wewe hata ungeli toa mali yote
na vitu vyote vya nafuu viliomo duniani kwa ajili ya kuwaunga pamoja huku,
usinge weza kuyapata hayo. Kwa sababu nyoyo zimo katika mkono wa Mwenyezi
Mungu, na Yeye ndiye aliye waunganisha, kwa kuwaongoa kwenye Imani na mapenzi
na udugu. Hakika Yeye Mtukufu ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda. Anawapangia
waja wake kwa mujibu wa manufaa yao.
Rudi kwenye Sura
64. Ewe Nabii! Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kukudhamini
wewe na wenye kukufuata miongoni mwa Waumini katika kila jambo lenye maana
kwenu.
Rudi kwenye Sura
65. Ewe Nabii! Wahimize Waumini wende vitani kwa ajili ya kulinyanyua
Neno la Mwenyezi Mungu, na wapendezeshe kwa yatayo wafwatia katika kheri
ya dunia na Akhera watayo ipata, ili nafsi zao ziingie nguvu. Nayo ikiwa
wapo kati yenu watu ishirini walio shikamana na Imani na subira na ut'iifu,
basi watawashinda makafiri mia mbili. Hayo ni kwa sababu wao ni watu wasio
fahamu ukweli wa mambo, kwani hawana Imani, wala subira, wala tamaa ya
kupata thawabu.
Rudi kwenye Sura
66. Ilivyo kuwa ni waajibu wenu enyi Waumini, kusubiri mnapo kutana
na maadui zenu katika hali ya kuwa mna nguvu, ijapo kuwa wamekuzidini mara
kumi, sasa Mwenyezi Mungu amekuruhusini katika hali isiyo kuwa ya nguvu,
kuwa mvumilie ikiwa adui kakuzidini mara mbili basi. Hayo ni kwa kukujua
kwake kuwa hamna nguvu nyingi, kwa hivyo mmefanyiwa wepesi na mmesahilishiwa,
baada ya kuwa heba ya Uislamu imeingia katika nafsi za makafiri. Kwa hivyo
mkiwa nyinyi ni wapiganaji mia wenye kusubiri mnaweza kuwashinda makafiri
mia mbili. Na mkiwa elfu moja mtawashinda elfu mbili, kwa Mwenyezi Mungu
kupenda na kusaidia. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri kwa
nusura yake na kuunga mkono kwake.
Rudi kwenye Sura
67. Haimfalii Nabii yeyote kukamata mateka, au kuchukua fidia, au
kutoa bure msamaha, mpaka ashinde, na maadui waone wameshindwa, na wawe
wamepata pigo kubwa hata kuwa hawawezi tena kupigana katika nchi.
Lakini, nyinyi jamaa wa Kiislamu, mmefanya haraka katika Vita vya Badri
kukamata mateka kabla hamjatamakani mkawa imara katika nchi. Mnatafuta
manufaa ya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera, kwa kutukuzwa Neno
la Haki, na lisikushughulisheni la dunia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu,
Mwenye kushinda. Hukupangieni mambo yenu kwa mujibu wa faida yenu.
Rudi kwenye Sura
68. Ingeli kuwa hapana hukumu iliyo kwisha tangulia kutoka kwa Mwenyezi
Mungu ya kumsamehe mwenye kujitahidi japo kuwa amekosa, basi ingeli kupateni
adhabu kubwa kwa papara mliyo ifanya.
Rudi kwenye Sura
69. Basi sasa tumieni mlicho kipata katika fidia kwa kuwa ni halali
kwenu, wala si uchumi muovu. Na mcheni Mwenyezi Mungu katika mambo yenu
yote. Hakika Mwenyezi Mungu ni mkubwa wa kusamehe na kumrehemu amtakaye
katika waja wake pindi akirejea.
Rudi kwenye Sura
70. Ewe Nabii! Waambie hao mateka walio angukia mikononi mwenu: Ikiwa
katika nyoyo zenu ipo kheri anayo ijua Mwenyezi Mungu, Yeye atakulipeni
yaliyo bora zaidi kuliko hicho walicho kichukua Waumini, na atakusameheni
ushirikina wenu na madhambi mliyo kuwa nayo. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi
wa maghfira na rehema kwa mwenye kutubia madhambi yake.
Rudi kwenye Sura
71. Na pindi wakitaka kukukhuni, kwa vile baadhi yao walivyo onyesha
kumili kwenye Uislamu, pamoja na nyoyo zao kupenda kukufanyia khiana makusudi,
wewe usivunjike moyo. Mwenyezi Mungu atakupa uwezo juu yao. Kama hapo kwanza
walipo mkhini Mwenyezi Mungu kwa kumfanyia wenzi na washirika wa kuwaabudu,
na wakaikufuru neema yake, na Yeye aliwaweza kwa kukupa ushindi juu yao
katika Badri, juu ya kuwa jeshi lako ni dogo na lao ni kubwa. Na Mwenyezi
Mungu Mwenye nguvu, Mwenye ushindi, Muendeshaji kwa hikima yake, aliwathibitisha
wakawa na nguvu waja wake Waumini kwa nusura yake.
Rudi kwenye Sura
72. Hakika walio isadiki Haki na wakaikubali hukumu yake, wakahama
Makka, wakapigana Jihadi kwa mali yao na roho zao, na wale walio wapa makaazi
wakimbizi ugenini, wakamsaidia Mtume wa Mwenyezi Mungu, wanapigana vita
na wale wanao wapiga vita. Wanamfanyia uadui anao wafanyia uadui. Wao kwa
wao wanasaidia kuunga mkono Haki, na kutukuza Neno la Mwenyezi Mungu. Na
wale wasio hama, haijathibiti kupata ulinzi na msaada wa Waumini, mpaka
wahajiri. Lakini wakikutakeni muwanusuru na wanao wakandamiza katika Dini,
basi wanusuruni. Wakikutakeni muwasaidie dhidi ya watu ambao mna mapatano
nao, na wala hawakuvunja mapatano hayo, basi msiwakubalie. Na Mwenyezi
Mungu anayaona myatendayo, hana kinacho fichika kwake. Basi simameni kwenye
mipaka yake msije mkatumbukia katika adhabu yake.
Rudi kwenye Sura
73. Na walio kufuru wao ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Na wao husaidiana
kwa mambo ya upotovu, na wanaungana mkono kukufanyieni nyinyi uadui. Basi
nyinyi msifanye nao urafiki. Mkikhaalifu, yaani mkenda kinyume na haya
mkawafanya ni wenzenu itaingia fitna katika safu zenu, na utakuwa uharibifu
mkubwa katika nchi.
Rudi kwenye Sura
74. Na walio amini, na wakahajiri, na wakapigana Jihadi katika Njia
ya Mwenyezi Mungu, na walio wapa makaazi, na wakaisaidia Haki na Neno la
Mwenyezi Mungu - hao ndio walio na Imani ya kweli. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu
atawasamehe, na watapata riziki kubwa duniani na Akhera.
Rudi kwenye Sura
75. Na walio amini baada ya wale wa mwanzo, na mwishoe wakahama nao,
na wakapigana Jihadi pamoja na walio tangulia, basi hao ni katika nyinyi,
kwa mkusanyo wa Muhaajirina (Walio hama Makka) na Ansari (walio msaidia
Mtume, watu wa Madina). Hao wanastahiki ulinzi na haki kama ziliopo baina
ya nyinyi kwa nyinyi. Na walio kuwa wame nasibiana katika Waumini
- juu ya urafiki wa Imani -wana urafiki zaidi wa kuwa ni jamaa. Basi hao
wanazidiana katika mapenzi, na mali, na kusaidiana, na kuungana mkono.
Na Mwenyezi Mungu ameyabainisha hayo katika Kitabu chake. Naye ni Mwenye
kujua kila kitu.
Rudi kwenye Sura