1. Alif Lam Mym 'Saad. (A.L.M.S'.) Hizi ni harufi za
kutamkwa ambazo zinaanzia baadhi ya Sura za Makka, kwa ajili ya kuwazindua
Washirikina kuwa hakika hii Qur'ani Tukufu imeundwa kwa harufi zile zile
wanazo zitamka wao. Na juu ya hivyo wao wanaemewa hawawezi kuleta mfano
wake. Kadhaalika harufi hizi zinapo somwa huwazindua wao wasikilize,
kwa kuwa walikuwa wananasihiwa na wakubwa zao kuwa wasiisikilize Qur'ani.
Rudi kwenye Sura
2. (Ewe Nabii!) Umeteremshiwa wewe Qur'ani ili uwaonye hao wanao
kanya wapate kuamini, na uwakumbushe Waumini wapate kuzidi Imani yao. Basi
usiingie dhiki katika kifua chako unapo ifikilisha kwa kukhofu kuwa utakanushwa.
Rudi kwenye Sura
3. (Enyi Watu!) Fuateni aliyo kufunulieni Mola wenu Mlezi, wala msiwafuate
marafiki au walinzi wengineo badala yake Yeye, mkawa mnawaitikia wao na
mkiwaomba msaada! Itakuwa kama hamkuwaidhika ikiwa mtaiacha Dini ya Mwenyezi
Mungu na muifuate nyengineyo, hali ya kuwa yapo mengi ya kuzingatia katika
haya mliyo funuliwa.
Rudi kwenye Sura
4. Kwani Sisi tumekwisha iteketeza miji kadhaa wa kadhaa, kwa sababu
watu wao walikuwa wakiwaabudu wasio kuwa Mwenyezi Mungu, na kwa kuwa katika
mwendo wao hawakufuata Njia yake. Ikawajia adhabu yetu wakati wao wameghafilika
na wametuwa usiku nao wamelala, kama yalivyo wapata kaumu ya Lut'; au wakatekezwa
mchana nao wamepumzika wakati wa kujinyoosha, kama yalivyo wapata kaumu
ya Shua'ib.
Rudi kwenye Sura
5. Basi wakaungama kwa madhambi yao yaliyo waletea msiba wao. Hakuwa
hata mmoja katika wao walipo ona adhabu ila alisema, na wakati huo kusema
huko hakufai kitu: Hakika sisi tulikuwa tumejidhulumu nafsi zetu kwa maasiya,
wala Mwenyezi Mungu hakutudhulumu kwa kutupa adhabu.
Rudi kwenye Sura
6. Na Siku ya Kiyama hisabu ya Mwenyezi Mungu itachungua kila kitu
kwa uadilifu. Tutawauliza watu tulio watumia Mitume: Je, Ujumbe umewafikilia?
Na wamewajibu nini hao Wajumbe tulio watuma? Na tutawauliza Mitume pia:
Je, mmefikisha yaliyo teremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi? Na hao
kaumu zenu wamekujibuni nini?
Rudi kwenye Sura
7. Na tutawapa wote khabari ya kweli yote yaliyo kuwa kwao, kwa sababu
hakika Sisi tumewadhibitia kila kitu chao, kwani Sisi hatukuwa mbali nao,
wala hatukuwa hatujui waliyo kuwa wakiyafanya.
Rudi kwenye Sura
8. Na Siku tutapo wauliza na kuwaeleza, vipimo vya vitendo vyao kwa
ajili ya kulipwa vitakuwa vipimo vya uadilifu. Wale ambao mema yao yatazidi
kuliko maovu yao watakuwa ndio wenye kufuzu, tutakao walinda na Moto na
tutawatia Peponi.
Rudi kwenye Sura
9. Na wale ambao maovu yao yatakithiri kuliko mema yao, hao ndio
watakuwa khasarani, kwa kuwa wameziuza nafsi zao kwa Shetani, wakaacha
kuzingatia Ishara zetu kwa ukafiri na inda.
Rudi kwenye Sura
10. Nasi tumekuwekeni katika ardhi, na tukakupeni nguvu za kuiamirisha
mkajipatia manufaa ndani yake, na tukakusahilishieni njia za kupatia maisha.
Juu ya neema hizi zote, kumekuwa kuchache mno kumshukuru kwenu Mwenyezi
Mungu. Nanyi mtakuja pata malipo ya hayo myatendayo!
Rudi kwenye Sura
11. Na katika khabari za wale wa mwanzo pana mazingatio na mawaidha,
yanayo dhihirisha kuwa Shetani anajaribu akuondoleeni neema kwa kusahau
kwenu amri za Mwenyezi Mungu. Sisi tumemuumba baba yenu Adam, na tukampa
Sura. Kisha tukawaambia Malaika: Mtukuzeni! Wakamtukuza kwa kut'ii amri
ya Mola wao Mlezi, ila Iblisi hakut'ii.
Rudi kwenye Sura
12. Mwenyezi Mungu kwa kuudhika naye kwa uasi wake alimwambia: Nini
kilicho kuzuia usimtukuze Adam, na hali Mimi nimekuamrisha ufanye hivyo?
Iblisi akajibu kwa inda na kiburi: Mimi bora kuliko Adam. Umeniumba kwa
moto, na yeye umemuumba kwa udongo. Na moto ni mtukufu zaidi kuliko udongo.
Rudi kwenye Sura
13. Mwenyezi Mungu alimlipa kwa inda yake na kiburi chake kwa kumfukuza
katika makao ya utukufu wake, na akamwambia: Teremka kutoka hapo baada
ya kuwa katika pahala pa juu. Haikufalii ukapandwa kichwa na ukaasi humo!
Toka huko, nawe umehukumiwa hizaya na udhalili!
Rudi kwenye Sura
14. Iblisi akamwambia Mwenyezi Mungu: Nipe muhula, unibakishe mpaka
Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
15. Mwenyezi Mungu akamjibu: Wewe utakuwa katika walio bakishwa wa
mwisho.
Rudi kwenye Sura
16. Kwa kumchukia Adam na kumhusudu alisema: Kwa sababu ya kunihukumia
kupotoka na kupotea, nakuapia nitawapoteza wana wa Adam wasiifuate Njia
yako Iliyo Nyooka, kwa kutumia kila hila zinazo mkinika.
Rudi kwenye Sura
17. Na ninaapa, nitawatokelea mbele yao, na nyuma yao, na kuliani
kwao, na kushotoni kwao, na kila upande ninao weza, nikitafuta kila kipengee
cha kughafilika kwao au udhaifu wao, nipate kuwapotosha, hata wasiwe wengi
wao wanao kuamini Wewe, kwa kuto shukuru neema yako.
Rudi kwenye Sura
18. Mwenyezi Mungu akazidi kuudhika, akamwambia: Toka kwenye makao
ya ukarimu wangu, wewe ulio hizika kwa kiburi chako na uasi wako, na khatima
yako ni kuhiliki tu! Na ninaapa nitaijaza Jahannamu kwa wewe na hao wana
wa Adam watao kufuata nyote pamoja!
Rudi kwenye Sura
19. Na ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika makao ya ukarimu wangu,
nayo ndiyo hiyo Bustani, mneemeke humo, mkila kila chakula mpendacho, isipo
kuwa mti huu. Msiukaribie! Msije mkawa wenye kujidhulumu nafsi zenu kwa
adhabu itayo kupateni kwa kuvunja amri.
Rudi kwenye Sura
20. Shetani akawazaini waivunje amri ya Mwenyezi Mungu, ziwavuke
nguo zilizo wasitiri zikashifike tupu zao. Akawaambia: Mola wenu Mlezi
hakukukatazeni mti huu ila ni kwa kuwa hataki muwe Malaika, au msije mkawa
mnaishi milele, na neema yenu haikatiki daima katika makao haya!
Rudi kwenye Sura
21. Naye akawaapia kuwa ati yeye ni katika wanao wapa nasaha njema,
na akakariri kiapo chake.
Rudi kwenye Sura
22. Basi akawachochea kwa udanganyifu mpaka wakenda kula ule mti.
Walipo uonja tupu zao zikafichuka, wakaingia wanakusanya majani ya miti
kujisitiri tupu zao. Mola wao Mlezi akawakaripia, na akawatanabahisha makosa
yao kwa kuwambia: Mimi sikukukatazeni mti ule, na nikakwambieni kuwa Shetani
ni adui yenu wa dhaahiri, hakutakieni kheri?
Rudi kwenye Sura
23. Adam na mkewe wakasema nao wamejuta wananyenyekea: Ewe Mola wetu
Mlezi! Tumejidhulumu nafsi zetu kwa kuvunja amri yako, kuliko pelekea kuondoka
kwa neema. Na ikiwa hutusamehe ukhalifu wetu, ukaturehemu kwa fadhila yako,
hapana shaka tutakuwa katika wenye kukhasiri.
Rudi kwenye Sura
24. Mwenyezi Mungu akawaambia wao na pia na Shetani: Teremkeni nyote
nyinyi, mtakuwa maadui nyinyi kwa nyinyi. Makao yenu na starehe yenu kwa
muda mpaka ifike ajali yenu, yatakuwa katika ardhi.
Rudi kwenye Sura
25. Katika ardhi mnazaliwa, na mnaishi, na humo mnakufa na kuzikwa.
Na kutoka huko mtatolewa wakati wa kufufuliwa.
Rudi kwenye Sura
26. Enyi Binaadamu! Sisi tumekuneemesheni. Tumekuumbieni nguo kusitiri
tupu zenu, na vitu vya pambo. Lakini ut'iifu ndio nguo bora ya kukukingeni
na adhabu. Neema hizo ni katika Ishara zenye kuonyesha uwezo wa Mwenyezi
Mungu, na rehema yake, ili watu waukumbuke utukufu wake. Yeye tu ndiye
anaye stahiki Ungu. Na kisa hichi ni katika nyendo za Mwenyezi Mungu
za uumbaji wake, zinazo bainisha nini malipo ya kuvunja amri ya Mwenyezi
Mungu, ili watu wakumbuke, na wafanye pupa kumt'ii Allah na kumshukuru.
Rudi kwenye Sura
27. Enyi wanaadamu! Msimuitikie Shetani na upotovu wake, mkatoka
kwenye neema hizi, ambazo hazidumu ila kwa kushukuru na kut'ii, kama walivyo
muitikia wazazi wenu, Adam na mkewe, akawatoa Shetani kwenye neema na ukarimu,
na akawavua nguo zao zikaonekana tupu zao. Basi yeye Shetani na wasaidizi
wake wanakujieni kwa namna msio watambua, wala hamuhisi mipango yao na
vitimbi vyao! Lakini Shetani hana madaraka juu ya Waumini. Sisi tumemfanya
yeye na wasaidizi wake kuwa ni marafiki wa wale wasio amini Imani ya kweli
yenye kulazimikana na ut'iifu ulio timia.
Rudi kwenye Sura
28. Na wakanushao wakitenda jambo ovu la mwisho, kama shirki, na
kut'ufu kwenye Al Ka'aba nao wako uchi, na mengineyo, basi wao hutoa udhuru
kwa kusema: Sisi tumewakuta baba zetu wakenda mwendo huu huu, na sisi tunawafuata
wao; na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hivi na ameturidhia kwa kuwa ametukiria!
Waambie ewe Nabii kuwapinga kwa uzushi wao: Hakika Mwenyezi Mungu hakuamrisha
mambo haya maovu! Je, mnamnasibishia Mwenyezi Mungu mambo msiyo kuwa nayo
tegemeo lolote mnalo jua lina dalili ya ukweli wa kumnasibisha nalo Subhanahu?
Rudi kwenye Sura
29. Wabainishie aliyo yaamrisha Mwenyezi Mungu, useme: Mola Mlezi
wangu ameamrisha uadilifu usio ingiliwa na uchafu. Na amekuamrisheni mumkhusishe
Yeye tu kwa ibada kila wakati na kila pahala, na muwe wenye kumsafia niya
katika hayo. Na nyote nyinyi baada ya kufa ni wenye kurejea kwake.
Na kama alivyo anza kukuumbeni kwa wepesi, na mlikuwa hammiliki kitu chochote,
basi kadhaalika mtarejea kwake kwa wepesi na hali mmeziacha nyuma ya migongo
yenu neema zote mlizo nazo.
Rudi kwenye Sura
30. Siku ya Kiyama watu watakuwa makundi mawili:- Kundi moja lilio
pata tawfiqi ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa lilichagua Njia ya Haki, likaamini
na likatenda vitendo vyema. Na kundi jengine limehukumiwa upotovu, kwa
sababu lilikhiari njia ya baat'ili, nayo ni ukafiri na uasi! Na hao walio
potea waliwafanya mashetani ndio rafiki zao badala ya Mwenyezi Mungu, wakawafuata,
nao wanadhani kuwa wao wamewafikiwa kwa kudanganyika kwao na khadaa za
mashetani!
Rudi kwenye Sura
31. Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu, nalo ni nguo hizi "maaddiy"
za kuonekana, za kusitiri utupu, na nguo za "adabiy" zisizo onekana, bali
ni za maana, nazo ni Taqwa, Uchamngu, katika kila pahala pa Sala, na kila
wakati mnapo fanya ibada. Na jistarehesheni kwa kula na kunywa bila ya
kufanya israfu au ubadhirifu, yaani kutumia kwa fujo, katika hayo. Basi
msitumie vitu vilivyo harimishwa, wala msipite kiasi cha kiakili katika
huko kujistarehesha. Hakika Mwenyezi Mungu hana radhi na wanao tumia kwa
fujo.
Rudi kwenye Sura
32. Ewe Muhammad! Waambie kwa kuupinga ule uzushi wao kumzulia Mwenyezi
Mungu juu ya kuhalalisha na kuharimisha: Nani aliye harimisha pambo la
Mwenyezi Mungu alilo waumbia waja wake? Na nani aliye harimisha riziki
iliyo halali na nzuri? Waambie: Hivi vitu vizuri ni neema inayo toka kwa
Mwenyezi Mungu. Isingeli faa wastarehe navyo duniani ila wale walio amini,
kwa sababu wao wanatimiza haki yao kwa shukrani na ut'iifu. Lakini rehema
ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu, imewakusanya pia makafiri na wakhalifu katika
dunia. Na Siku ya Kiama neema hizi zitakuwa za Waumini peke yao, wala hapana
mwenginewe ataye shirikiana nao katika hayo. Na Sisi tunazieleza Aya, Ishara,
zinazo onyesha hukumu kwa mpango huu ulio wazi kwa ajili ya watu wanao
fahamu kwamba hakika Mwenyezi Mungu peke yake, Mwenye kumiliki kila kitu,
ndiye Mwenye uwezo wa kuhalalisha na kuharimisha.
Rudi kwenye Sura
33. Ewe Muhammad! Sema: Hakika Mola wangu Mlezi ameharimisha mambo
yaliyo zidi kwa ubaya, kama uzinzi; sawa sawa ukifanywa kwa siri au kwa
dhaahiri. Pia ameharimisha kila maasi ya namna yoyote, na dhulma isiyo
na njia ya haki. Na ameharimisha kumshirikisha na chochote kisicho kuwa
na hoja madhubuti, au dalili ya kweli. Na pia kumzulia uwongo Subhanahu,
Aliye takasika, katika kuhalalisha na kuharimisha, na mengineyo.
Rudi kwenye Sura
34. Na kila umma una ukomo wake maalumu. Na hapana uwezo wowote wa
kuupeleka mbele mwisho huo au kuuakhirisha muda wake hata ukiwa mdogo vipi.
Rudi kwenye Sura
35. Enyi wanaadamu! Wakikujieni Mitume kutokana na hiyo jinsi yenu
ya kibinaadamu kukufikishieni Ishara zangu zilizo funuliwa nyinyi mnakuwa
makundi mawili. Kwa wale wenye kuamini na wakatenda mema kwa usafi wa niya,
hapana khofu, wala wao hawatahuzunika katika dunia yao na Akhera yao.
Rudi kwenye Sura
36. Na wale wanao zikanusha hizo Ishara na wakapandwa na kiburi wasizifuate
wala wasiongoke kwazo, basi hao ni watu wa Motoni. Humo wataadhibiwa daima
milele katika adhabu.
Rudi kwenye Sura
37. Hapana wakubwa wa dhulma kuliko hao wanao mzulia Mwenyezi Mungu
uwongo, kwa kumnasibisha na mshirika na mwana, na kuzua kuhalalisha na
kuharimisha na mengineyo, pasina hoja. Au wanao kanusha Aya, Ishara, za
Mwenyezi Mungu zilizo funuliwa katika Vitabu vyake na zinazo onekana katika
ulimwengu wake. Hao wanapata hapa duniani sehemu ya aliyo waandikia Mwenyezi
Mungu katika riziki, au uhai, au adhabu. Mpaka akiwajia Malaika wa Mauti
kuzipokea roho zao, hapo huwaambia kwa kuwasuta: Iko wapi hiyo miungu yenu
mliyo kuwa mkiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu ije kukukingeni na mauti?
Nao wajibu: Wametukataa, wametuacha na wametukimbia. Na wajishuhudie wenyewe
wakikiri kuwa hakika walikuwa makafiri.
Rudi kwenye Sura
38. Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atawaambia hawa makafiri: Ingieni
Motoni pamoja na kaumu nyengine za kikafiri miongoni mwa watu na majini,
walio kwisha kutangulieni. Kila umma ukiingia Motoni huwalaani umma mwingine
ulio kufuru mfano wao, na ambao waliwafanya ndio wa kuwafuata. Mpaka
wakisha ingia kwa kufuatana wote wakakusanyika, wale walio fuata watawashutumu
wale walio kuwa waongozi kwa kusema: Ewe Mola wetu Mlezi! Hao walitupoteza
tulipo wafuata, kwa kuwa walitutangulia au kwa kuwa walikuwa ndio wakitutawala.
Basi wakatugeuza kwenye Njia ya Haki tusiifuate. Basi wao wape adhabu mara
mbili, wabebe malipo ya uasi wao na uasi wetu! Mwenyezi Mungu atawajibu:
Kila mmoja wenu atapata adhabu mara mbili ambayo hapana ataye iepuka katika
makundi yenu mawili. Wanao fuata watapata adhabu marudufu kwa ukafiri wao
na upotovu wao, na kufuata kwao bila ya kuzingatia na kufikiri. Na wale
walio fuatwa watapata adhabu marudufu kwa ukafiri wao na upotovu, na pia
kwa kuwakufurisha na kuwapotoa wengineo. Lakini nyinyi hamjui kiasi gani
itakuwa adhabu ya kila mmoja wenu.
Rudi kwenye Sura
39. Na hapa tena watasema wale walio fuatwa kuwaambia walio fuata:
Kutuiga kwenu sisi katika ukafiri na uasi hakukufanyeni nyinyi muwe bora
kuliko sisi hata mstahiki kupunguziwa adhabu! Basi Mwenyezi Mungu atawaambia
wote: Onjeni adhabu mlio jiletea wenyewe kwa kuwa mlikuwa mkizua ukafiri
na uasi!
Rudi kwenye Sura
40. Hakika wale walio kanusha Ishara zetu zilizo teremshwa katika
Vitabu, na ziliopo katika ulimwengu, na wakapanda kiburi kukataa kuhidika
kwa Ishara hizo, na wala wasitubu, nawakate tamaa kupokelewa a'mali zao
na kupata rehema ya Mwenyezi Mungu, na kuingia Peponi, kama alivyo kata
tamaa ngamia kupita katika tundu ya sindano. Na kwa mfano huu ndio tutawaadhibu
hao wenye kiburi katika kila umma.
Rudi kwenye Sura
41. Huko katika Jahannamu kitanda chao ni moto, na shuka ya kujifunika
ni moto. Na kwa mfano huu tutawaadhibu wanao zidhulumu nafsi zao kwa ukafiri
na upotovu.
Rudi kwenye Sura
42. Na wenye kuamini na wakatenda vitendo vyema ambavyo hatumlazimishi
ila kwa kiasi anavyo weza mtu, hao ndio watu wa Peponi. Watastarehe humo
daima dawamu!
Rudi kwenye Sura
43. Na tutazitoa chuki zote ziliomo katika nyoyo zao. Basi watakuwa
katika Janna, Pepo, ndugu wenye kupendana, ikipita mito ya maji matamu
mbele yao. Watasema kufurahia neema watayo ipata: Alhamdulillahi,
yaani Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye tuonyesha Njia ya
kufikia neema hizi, na akatuwezesha kuifuata. Na ingeli kuwa hakutuhidi,
kutuongoa, Mwenyezi Mungu kwa kutupelekea Mitume na akatupa tawfiq, tusingeweza
sisi wenyewe kufikia uwongofu. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi wametujia
na wahyi wa Haki! Hapo tena Mwenyezi Mungu atawaambia: Hakika hii Pepo
ni zawadi mmepewa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mmepewa kwa fadhila yangu
bila ya kuwa nyinyi kutoa kitu, kama urithi. Na takrima hii mlio pata ni
sababu ya vitendo vyenu vyema duniani.
Rudi kwenye Sura
44. Watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni kwa kuwaambia: Sisi
tumekwisha ona thawabu alizo tuahidi Mola Mlezi wetu kuwa ni kweli. Je,
nyinyi hiyo adhabu aliyo kuahidini Mola Mlezi wenu mmeiona kuwa ni kweli?
Nao watajibu: Naam, Ndiyo! Basi mtangazaji atawatangazia watu wa Peponi
na watu wa Motoni: Laana, yaani kunyimwa na kufukuzwa kwenye rehema ya
Mwenyezi Mungu, ndio malipo ya wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa ukafiri
na upotovu.
Rudi kwenye Sura
45. Hawa madhaalimu ndio wanao wazuia watu wasende kwenye Njia ya
Mwenyezi Mungu wa Haki, nayo ndiyo Imani na kutenda mema; na wanaweka vikwazo,
na shakashaka, ili hiyo Njia yende upogo iwapoteze watu wasiweze kuifuata.
Na hao wanaikanusha Akhera hawaiogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
46. Na baina ya watu wa Peponi na watu wa Motoni patakuwa na pazia
kuzuia kufikia kwenye Mnyanyuko - na hapo ni pahala palipo nyanyuka palipo
juu. Watu katika bora ya Waumini na watukufu wao, watakuwa wanawaangalia
khalaiki wote hao, na wanawajua wema na waovu kwa alama zinazo onyesha
ut'iifu wao na uasi wao. Wataitwa watu wema kabla ya kuingia Peponi, na
hali wao wanataraji kuingia humo, watawabashiria kwa Imani na utulivu na
kuingia Peponi.
Rudi kwenye Sura
47. Macho ya hao Waumini yakigeukia upande wa watu wa Motoni baada
ya wito huo, watasema kwa kitisho watacho kioni cha Moto: Ewe Mola wetu
Mlezi! Usitutie pamoja na hawa madhaalimu walio dhulumu nafsi zao, wakadhulumu
Haki, na wakawadhulumu watu!
Rudi kwenye Sura
48. Na wale watu wa daraja za juu katika Pepo, nao ni Manabii, na
Mas'iddiqina, watawaita walio kuwa wakiwajua kwa sifa zao katika watu wa
Motoni, wakisema kwa kuwalaumu: Huko kujumuika kwenu kwa wingi, hakukufaini
chochote, wala huko kupanda kiburi kuikataa Haki kwa kutegemea ujamaa wenu
na utajiri wenu. Na hivi sasa mnawaona hawa, nini hali yao na nini hali
yenu.
Rudi kwenye Sura
49. Hao wanyonge mlio kuwa mkiwadharau, na mkaapa kuwa hayumkini
Mwenyezi Mungu awateremshie rehema, kama kwamba nyinyi ndio mnao ishika
rehema yake, wao wamekwisha ingia Peponi! Na Mola wao Mlezi atawaambia:
Ingieni humo kwa amani. Hapana khofu juu yenu kwa jambo lolote litalo kupateni,
wala hamtahuzunika kwa jambo mlilo likosa.
Rudi kwenye Sura
50. Na watu wa Motoni watawanadia watu wa Peponi kwa kuwaambia: Hebu
twachilieni maji kidogo yatumiminikie sisi, au tugaieni kitu katika vyakula
na mavazi na starehe nyengine alizo kupeni Mwenyezi Mungu Mtukufu!
Nao watu wa Peponi watawajibu: Sisi hatuwezi kufanya hayo, kwa sababu Mwenyezi
Mungu amezuia vyote hivyo wasipate watu wapinzani, walio mkanusha Yeye
na neema zake katika dunia.
Rudi kwenye Sura
51. Hawa makafiri ndio ambao hawakufanya juhudi kutafuta Dini ya
Haki, lakini ikawa dini yao ni kufuata pumbao na matamanio, ndio pumbao
la kujipumbazia na upuuzi wa kuchezea, na maisha ya dunia na anasa zake
zikawakhadaa, wakadhania hayo tu ndiyo maisha, na wakasahau kukutana nasi!
Basi Siku ya Kiyama Sisi tutawasahau. Na wao hawato istarehea Pepo, na
watauonja Moto, kwa sababu ya sahau yao kuisahau Siku ya Kiyama, na kuzikanusha
Ishara zenye kubainika wazi, zinazo thibitisha Haki.
Rudi kwenye Sura
52. Na hakika kwa ajili ya kubainisha Haki tuliwapa Kitabu, na tukakipambanua.
Kitabu hicho kimekusanya ilimu nyingi, na ndani yake zimo hoja za Tawhid,
Upweke wa Mwenyezi Mungu, na Ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu;
na pia zimo sharia zake, maelezo ya Njia Iliyo Nyooka, na uwongofu wa kuifikilia.
Na pia yamo ndani ya Kitabu hichi mambo ambayo, lau watu wakiyafuata watapata
rehema. Na wala hawanufaiki kwacho ila wale ambao ni shani yao kuinyenyekea
Haki na kuiamini.
Rudi kwenye Sura
53. Hakika wao hawaiamini hii Qur'ani, na wala hawangojei ila matokeo
ambayo Mwenyezi Mungu ameyabainisha kuwa yatawapata wanayo
ikataa! Na Siku yatapofika hayo matokeo, nayo ni Siku ya Kiyama, walio
ziacha amri zake na maelezo yake, na wakaghafilika kuwa ni waajibu kuiamini,
na hali wakiungama madhambi yao, watasema: Hakika walikuja Mitume kutoka
kwa Muumba wetu na Mlezi wetu, wakituitia Haki waliyo tumwa kuileta, nasi
tukaikataa! Nao wataulizwa: Je, mnao waombezi wakakuombeeni? Nao hawatowapata!
Au, je, watarudishwa tena duniani watende mema? Hawatajibiwa! Wamepoteza
vitendo vyao kwa kukhadaika na dunia, na umewapotea ule uzushi wa uwongo
wa kudai kuna mungu asiye kuwa Allah, Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
54. Hakika Mola Mlezi wenu ambaye Mitume wake wanakuiteni mwende
kwenye Haki, na kuiamini Siku ya Mwisho na Malipo, ndiye Muumba ulimwengu,
naye ndiye aliye uanza. Kaumba mbingu na ardhi kwa viwango sita, vinavyo
shabihiana na siku sita, katika siku za dunia. Kisha akatawala juu ya Ufalme
ulio kamilika. Naye ndiye anaye ufanya usiku uufunike mchana kwa kiza chake,
na usiku unafuatia mchana kwa upesi na mpango na kufuatana kusikosita,
kama anavyo taka Yeye. Naye Mwenyezi Mungu Subhana ameliumba jua, na mwezi,
na nyota. Na vyote hivyo vinamnyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu, vinakwenda
kwa amri yake. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye kuumba na Mwenye amri ya
kuitikiwa. Baraka za Mwenye kuanzisha ulimwengu na viliomo ndani yake zimetukuka.
Aya hii tukufu imekusanya maana tatu:
* Ya kwanza ni kuwa mbingu na ardhi ameziumba Mwenyezi Mungu Mtukufu
mnamo siku sita. Na hizi siku sio muradi wake hizi tuzionazo sasa, na tunazo
zihisabu. Bali muradi wake ni kubadilika hali, baina ya giza totoro, na
giza-giza la alfajiri, na mpambazuko wa asubuhi, na mchana, na adhuhuri,
na jioni. Na haya yamekusanya hali sita zinazo badilika. Na giza-giza la
magharibi linakitangulia kiza cha usiku.
Na hizo hali sita au vipindi sita, ambavyo vimeitwa "siku"
ndivyo wanavyo vitaja wanachuoni wa sayansi, navyo ni: Kipindi cha "Ether",
kilicho elezwa katika Surat Ad-dukhan ya 44 ya kuwa ni moshi. Kisha kutokana
na hiyo "Ether" yakatokea majua, ambayo moja lake ni hili jua letu. Kisha
kutokana na jua zikawa sayari, na miongoni mwa sayari hizo ni hii dunia
yetu. Tena katika ardhi zikawamo maadini mbali mbali. Tena ndio kikawa
kipindi cha Ardhi, na baadae ukatokea uhai juu yake.
* Maana ya pili ya Aya hii ni kuwa kila kiliomo ulimwenguni kimo
chini ya ufalme wa Mwenyezi Mungu peke yake, wala hapana ufalme usipo kuwa
wake Yeye. Na nguvu zozote anazo pewa mtu hatoweza kuuendesha ulimwengu
atakavyo. Ukomo wa uwezo wake ni kunufaika na vilivyo umbwa na akajua baadhi
ya siri ziliomo ulimwenguni ambazo zilikuwa zimefichika. Kwa hivyo Mwenyezi
Mungu pekee ndiye aliye tuwa na kutawala juu ya A'rshi iliyo juu ya vyote
vilivyo umbwa, na kwamba nyota na vitu vyote haviendi ila kwa amri yake
peke yake.
* Maana ya tatu ni kuwa kupishana usiku na mchana kumetokea baada
ya kwisha umbwa ardhi na mbingu. Basi hizo ni hali zenye kukhusika na asli
ya uumbaji wa dunia, na makhusiano ya baina mbingu na ardhi na kuzunguka
kwao na Mwenyewe Subhana Mwenye kuumiliki ufalme na utukufu na ukarimu.
Rudi kwenye Sura
55. Ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu, ndiye aliye umba
kila kitu peke yake, basi muombeni Yeye tu kwa kumuabudu na kwa mengineyo,
mkimtangazia hayo maombi, kwa udhalilifu na kunyenyekea, kwa dhaahiri au
bila ya kudhihirisha. Wala msipite mipaka kwa kumshirikisha na wenginewe,
au kwa kumdhulumu yeyote. Kwani hakika Mwenyezi Mungu, hawapendi wanao
ruka mipaka, na wafanyao uadui.
Rudi kwenye Sura
56. Wala msifanye fisadi katika nchi njema kwa kueneza maasi na dhulma
na uvamizi. Na muombeni Yeye Subhanahu, Aliye takasika, kwa kuiogopa adhabu
yake, na kwa kutumai thawabu zake. Na hakika rehema yake ipo karibu kwa
kila mwenye kufanya mema. Na hayo ni hakika.
Rudi kwenye Sura
57. Na Mwenyezi Mungu, Aliye takasika, Aliye tukuka, peke yake, ndiye
anaye zipeleka pepo kubashiria rehema yake, kwa mvua ambazo kwa sababu
yake ndio makulima humea, na konde humwagiwa maji. Hizo pepo hubeba mawingu
ambayo nayo yamebeba maji. Tunayachunga mpaka yafike kwenye nchi isiyo
kuwa na mimea, ambayo ni kama maiti asiye na uhai, yakamiminika maji, na
tena Mwenyezi Mungu husabibisha kumea namna kwa namna ya mazao na matunda.
Na mfano kama huu wa kuihuisha ardhi kwa mimea, ndivyo tunawafanya maiti
wakawa wahai. Haya ni kwa ajili mpate kuikumbuka kudra ya Mwenyezi Mungu,
na mpate kuamini kuwa kupo kufufuliwa.
Rudi kwenye Sura
58. Na ardhi njema yenye rutba nzuri huzalisha mimea inayo
kua kwa nguvu, kwa idhini ya Mola Mlezi. Na ardhi mbaya haitoi ila mimea
michache, isiyo na faida, ambayo huwa ndio sababu ya dhiki ya huyo mkulima.
Rudi kwenye Sura
59. Washirikina wakafanya inda, na wakaikanusha Haki ilipo wajia
kwa hoja za kukata zisio pingika. Lakini huo ndio mtindo wa makafiri kwa
Manabii wao tangu zamani. Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake alio tokana
nao. Naye akawakumbusha kuwa yeye ni mmoja wao: Enyi watu wangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake. Kwani nyinyi hamna Mungu asiye kuwa huyu.
Na mjue kuwa kutakuwapo kufufuliwa na kuhisabiwa Siku ya Kiyama. Na hiyo
ni Siku adhimu. Mimi nakukhofieni Siku hiyo msije mkapata adhabu kali kweli.
Rudi kwenye Sura
60. Wakasema wale wahishimiwa wao, watu wa mbele mbele na uwongozi
katika wao, wakiujibu ule wito wake wa Tawhidi na Siku ya Akhera: Hakika
sisi tunakuona wewe uko mbali kabisa na hiyo haki.
Rudi kwenye Sura
61. Nuhu akawaambia kukataa yale waliyo msingizia: Mimi sina upotofu
kama mnavyo dai. Lakini mimi ni Mtume niliye toka kwa Muumba wa viumbe
vyote, basi hayumkini awe mbali na haki.
Rudi kwenye Sura
62. Na mimi katika huu wito wa Haki mshike Tawhidi na kuamini Siku
ya Mwisho, nafikisha Ujumbe aliyo nituma Mwenyezi Mungu, nao mfuate hukumu
za Mwenyezi Mungu ambazo ndizo zinazo msilihi mwanaadamu. Na mimi nakupeni
nasaha ya kweli itokayo kwenye moyo wangu ulio safi. Na Mwenyezi Mungu
amenifunza mambo ambayo nyinyi hamyajui.
Rudi kwenye Sura
63. Mnanizulia kuwa nimepotea na kuwa nipo mbali na Haki? Na mnastaajabu
kukujieni kumbusho kutokana na Mwenyezi Mungu aliye kuumbeni kwa ulimi
wa mtu aliye kuja kwenu kukuonyeni adhabu pindi mkikanusha, na akakuiteni
mwende kuufuata uwongofu, na kutengeza nyoyo, na kujiepusha na ghadhabu
ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kutaraji muwe katika rehema ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu duniani na Akhera? Haifai kuwa mnastaajabu na mnakanusha
juu ya kuwepo hoja zenye kuthibitisha Utume huu.
Rudi kwenye Sura
64. Lakini wao juu ya hoja hizo zilizo wazi wengi wao hawakuamini,
bali walimkanusha. Kwa hivyo tukawateremshia adhabu ya kuwazamisha katika
maji, na tukawaokoa wale walio amini katika jahazi alilo liunda kwa kuongozwa
nasi. Na wakazama wale walio kanusha juu ya kuwapo hoja zilizo wazi, nao
wakafanya inda wakawa hawaioni Haki kwa kuwa walipofuka wasiione.
Rudi kwenye Sura
65. Kama tulivyo mtuma Nuhu kwa kaumu yake kuwalingania Tawhidi,
kadhaalika tuliwatumia kina 'Aad Nabii Hud,(1) naye ni mmoja wao, makhusiano
yake nao ni kama ndugu kwa ndugu. Akawaambia: Enyi watu wangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu peke yake, nanyi hamna Mungu asiye kuwa Yeye. Na hii ndiyo
njia ya kujikinga na shari na adhabu. Nayo ndiyo Njia Iliyo Nyooka. Basi
je, mtaifuata njia mjikinge na shari na upotovu?
(1) 'Aad ni katika kabila yenye nguvu katika matumbo ya taifa la
Sam, na ni katika mat'abaka ya kwanza katika Waarabu wa jangwani. Ama makaazi
yao yalikuwa katika Al-ah'qaaf iliyo tajwa katika Kitabu kitukufu katika
Sura ya Al-ah'qaaf Aya 21.
Wamewafikiana wanachuoni wa Kiislamu wa kutegemewa kuwa hiyo Ah'qaaf
ipo katika nchi ya Yaman, ijapo kuwa wamekhitalifiana kidogo wapi khasa
pahala penyewe. Kwa mujibu wa Yaaqut Al-h'amawy ni bonde baina ya Oman
na nchi ya Mahara. Na kwa mujibu wa Is-haaq akimnukulu Ibn Abbas na Ibn
Khaldun ni sehemu ya mchanga baina ya Oman na Hadhramaut. Kwa mujibu wa
Qutaada ni sehemu ya mchanga karibu na bahari katika Shajar katika nchi
ya Yaman. Na yafaa kutaja kuwa nchi ya 'Aad kwa mujibu wa baadhi ya Wamagharibi
wa zamani ipo pande za juu za Hijaz katika jimbo la Husmaa, na karibu na
makaazi ya Thamud. Vyo vyote ilivyo si mbali kuwa hao kaumu ya 'Aad walisafiri
wakahamia jimbo hili wakati mmoja wapo.
Rudi kwenye Sura
66. Wakasema wenye uwongozi na umbele mbele katika kaumu yake: Sisi
tunakuona umepungukiwa na akili, kwa kutuitia wito huu; na tunaitakidi
kuwa wewe ni mwongo.
Rudi kwenye Sura
67. Akasema: Enyi watu wangu! Katika wito huu sina upungufu wa akili
hata chembe, wala mimi si mwongo. Lakini mimi nimekuja na uwongofu, na
mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, naye Yeye ndiye Mola Mlezi wa viumbe
vyote.
Rudi kwenye Sura
68. Katika haya ninayo kwambieni mimi nafikisha amri na makatazo
ya Mola Mlezi wangu, na hayo ndio Ujumbe wake kwenu. Na mimi nakupeni nasaha
ya dhati, kwa niya safi kabisa. Na mimi ni muaminifu katika ninayo kwambieni,
wala mimi si miongoni ya watu waongo.
Rudi kwenye Sura
69. Tena Hud akawaambia: Hivyo mmestaajabu mno, na mkaona mageni
kukujieni ukumbusho wa Haki kwa ulimi wa mtu aliye mmoja wenu, kukuonyeni?
Mkiendelea na haya mliyo nayo matokeo yake yatakuwa ni mabaya mno. Na hakika
jambo hilo si la kustaajabiwa. Kisha Hud akawatajia yaliyo wasibu walio
kanusha katika watu walio watangulia, na akawakumbusha neema za Mwenyezi
Mngu juu yao. Akasema: Kumbukeni Mwenyezi Mungu alivyo kufanyeni ndio warithi
wa nchi baada ya kaumu ya Nuhu alio waangamiza kwa kumkadhibisha Nuhu,
na Mwenyezi Mungu akakuzidishieni nyinyi nguvu za mwili na nguvu za utawala.
Na neema hizo zinatakikana zilete Imani. Basi zikumbukeni neema zake ili
mpate kufuzu.
Rudi kwenye Sura
70. Lakini wao juu ya wito mzuri huu walisema kwa kuona mageni: Hivyo
wewe umetujia kututaka tumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja peke yake, na tuache
masanamu waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu? Na hapana shaka sisi hatutofanya
hayo, nawe tuletee hiyo adhabu unayo tutishia, kama wewe kweli ni katika
wasema kweli!
Rudi kwenye Sura
71. Hakika kwa hii inadi yenu mmestahiki adhabu ya Mwenyezi Mungu
ikuteremkieni, na ghadhabu yake ikufikieni! Nyinyi mnabisha kwa ajili ya
masanamu ambayo mliyo yaita kuwa ni miungu nyinyi na baba zenu, na wala
si chochote ila ni majina tu walio pewa, na wala Mwenyezi Mungu hakuleta
hoja ya kuonyesha ungu wao. Hayo hayana nguvu za muumbaji inayo kuruhusuni
kuyaabudu! Na ikiwa mtashikilia ukaidi huu basi ingojeeni adhabu ya Mwenyezi
Mungu, nami pamoja nanyi, sote tungoje nini kitakushukieni.
Rudi kwenye Sura
72. Basi Sisi tukamwokoa A'ad na walio amini pamoja naye kwa rehema
yetu, na tukawateremshia makafiri cha kuwateketeza, na hapana chao kilicho
bakia wala hapana athari yao, na wala hawakuingia katika kundi la Waumini.
Rudi kwenye Sura
73. Na tuliwapelekea kina Thamud (1) ndugu yao Saleh, ambaye ni mwenzi
wao kwa nasaba na uwananchi. Na wito wake ulikuwa kama wito wa Mitume walio
kuwa kabla yake na baada yake. Akawaambia: Msafishieni ibada Mwenyezi Mungu
peke yake, na wala hapana Mungu isipo kuwa Yeye. Na hoja ya Utume wangu
imekwisha kukujilieni kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Nayo ni huyo ngamia mwenye
sifa za pekee. Katika huyo ngamia pana hoja. Yeye ni ngamia wa Mwenyezi
Mungu, muacheni ale atakapo katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru
isije kukupateni adhabu chungu.
(1) Thamud ni kabila ya Kiarabu iliyo kuwa Al Hijr, baina ya Hijaz
na Sham karibu na Wadi Alquraa
Rudi kwenye Sura
74. Na kumbukeni kuwa Mwenyezi Mungu amekujaalieni ndio wa kurithi
nchi ya A'ad, na akakupeni katika hiyo nchi makaazi mema, mkijenga majumba
ya fakhari katika nyanda zake. Na mkichonga milima mkifanya majumba. Basi
kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu, alivyo kuwekeni kwa makini katika
nchi, wala msifanye maovu katika nchi, mkawa wenye kufisidi na kuharibu
baada ya kukaa kwa makini kama huku.
Rudi kwenye Sura
75. Wale wenye kiburi katika watu wa mbele-mbele na uwongozi waliwasemeza
wanyonge kwa kuwalaumu na kuwadhalilisha: Hivyo nyinyi mnaitakidi kuwa
kweli Saleh ametumwa na Mola Mlezi wake? Watu wa Haki wakawajibu: Sisi
tunaitakidi na tunakubali aliyo tumwa kwetu.
Rudi kwenye Sura
76. Wakasema wenye kiburi: Sisi tunapinga na tunayakataa hayo mnayo
yaamini nyinyi, na hayo anayo itia Saleh ya kuwa Mungu ni mmoja.
Rudi kwenye Sura
77. Inda ya wenye kiburi ikakakamia, na wakampinga Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, na wakamchinja Ngamia. Walivuka mpaka katika kiburi chao,
wakaitupilia mbali amri ya Mola wao Mlezi, na wakasema kwa upinzani: Ewe
Saleh! Tuletee hiyo adhabu uliyo tuahidi ikiwa kweli wewe ni miongoni ya
alio watuma Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
78. Tetemeko la nguvu lilikuja kuwanyakua, na kulipo
pambazuka wakawa wote wamekwisha jifia majumbani mwao
wamejifudikiza kifudifudi.
Rudi kwenye Sura
79. Na kabla ya kuwateremkia adhabu hiyo ndugu yao Saleh aliwaachilia
mbali (kwa kukata tamaa nao), akawaambia: Enyi watu wangu! Mimi nimekufikishieni
amri na makatazo ya Mola Mlezi wangu. Na nimekusafieni nasaha yangu, lakini
nyinyi kwa ushindani wenu na ushupavu wenu, mmekuwa hamumpendi anaye kunasihini!
Rudi kwenye Sura
80. Na hakika tulimtuma Nabii wa Mwenyezi Mungu, Lut', kwa kaumu
yake; awaite wafuate Tawhidi, yaani ibada ya Mwenyezi Mungu mmoja. Na awazindue
juu ya waajibu wa kuachana na makosa maovu kabisa waliyo kuwa wakiyafanya.
Aliwaambia: Nyinyi mnakwenda kufanya jambo lilio pita mpaka kwa ubaya wake,
kinyume na maumbile? Mmezua uchafu huo ambao unapingana na khulka, na ambao
hapana watu walio kutangulieni walio fanya hayo!
Rudi kwenye Sura
81. Na jambo hilo ni kuwa mnawaendea wanaume kwa kuwatamani, na mnawawacha
wanawake! Nyinyi kwa jambo hili inakuwa mnafanya fujo, na mmetoka nje ya
maumbile, na mmefanya kitendo asicho fanya hata mnyama.
Rudi kwenye Sura
82. Na haikuwa jawabu ya watu wake kwa kukatazwa hichi kitendo kiovu
kisicho kuwa na mfano, ila ni kusema: Watoeni Lut' na jamaa zake na wafuasi
wake katika mji wenu! Nayo ni kwa kuwa wao wanajitahirisha na wanajitenga
na hichi kitendo ambacho akili na maumbile yanakiona ni kibaya, na wao
hao watu wanakioni kizuri!
Rudi kwenye Sura
83. Amri ya kuadhibiwa ilikwisha thibiti. Basi Sisi tukamwokoa Lut'
na watu wake, isipo kuwa mkewe, kwani yeye alikuwa katika hao walio potea.
Rudi kwenye Sura
84. Basi tuliwateremshia mvua ya mawe ya kuteketeza, na ardhi ikatandazwa
kwa mitetemeko ya chini yao! Basi ewe Nabii! Angalia vipi ulikuwa mwisho
wa wakosefu.
Rudi kwenye Sura
85. Na kwa watu wa Madyana tulimtuma ndugu yao, Shua'ib. Akasema:
Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake. Kwani nyinyi hamna
mungu isipo kuwa Yeye. Hoja zilizo wazi za kuthibitisha Haki inayo toka
kwa Mola Mlezi wenu juu ya Utume wangu kwenu zimekwisha kujieni. Na umekujieni
Ujumbe wa Mola wenu Mlezi kwamba mtengeneze kwa uadilifu maingiliano yenu
nyinyi kwa nyinyi. Basi timizeni vipimo na mizani mnapo uziana, wala msipunguze
haki za watu, wala msiiharibu nchi nzuri, kwa kufisidi mapando na kadhaalika,
na kuwatenga jamaa na kuondoa mapenzi. Kwani hayo ni bora kwenu mkiwa mnamuamini
Mwenyezi Mungu Mtukufu, na mnaamini Haki iliyo wazi.
Rudi kwenye Sura
86. Wala msikae katika kupinga kila njia za Haki na uwongofu na a'mali
njema, mkiwatishia wapitao, na kwa hivyo mkawazuia watafutao kheri wasiifikie.
Nao hao ndio watu wa Imani wanao muamini Mwenyezi Mungu, nanyi mnaitaka
njia iliyo potoka! Na kumbukeni mlivyo kuwa ni watu wachache, Mwenyezi
Mungu akakufanyeni mkawa wengi kwa kwenda sawa kutaka uzazi na mali. Na
zingatieni nini ulikuwa mwisho wa waharibifu walio kuwa kabla yenu.
Rudi kwenye Sura
87. Ikiwa kipo kikundi kati yenu kilicho amini Haki niliyo kuja nayo,
na kikundi kingine hakikuamini, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete
hukumu yake baina ya pande mbili hizo. Naye ndiye Mbora wa mahakimu.
Rudi kwenye Sura
88. Hii ni khabari ya Shua'ib katika wito wake kuwalingania kaumu
yake. Ama hao kaumu yake walikuwa wamemili juu ya upotovu. Na wale wakubwa
wao walio takabari waliukataa wito, na wakaona ni uvunjifu kuifuata Haki.
Wakamkabili Shua'ib kumwambia dhamiri yao kwa kusema: Hakika hapana vingine
ila tukutoe wewe na hao walio amini pamoja nawe katika mji wetu. Na tutakufukuzeni,
wala hamtasalimika na adhabu hii ila mkirejea katika hii dini yetu mliyo
iacha. Shua'ib a.s. akawajibu kwa kusema: Turejee katika mila yenu na hali
sisi tunaichukia kwa uharibifu wake? Hayawi hayo abadan!
Rudi kwenye Sura
89. Akaendelea zaidi kuwavunja tamaa yao ya kuwarejeza kwenye mila
yao kama walivyo taka. Akasema: Tutakuwa tunamzulia uwongo Mwenyezi Mungu
tukiwa katika mila yenu baada ya Mwenyezi Mungu kesha tuhidi kwenye Njia
Iliyo Nyooka. Na haifai sisi kuwa katika mila yenu kwa khiari yetu na kutaka
kwetu, ila akipenda Mwenyezi Mungu turejee katika mila yenu. Na hayo hayawi!
Kwa sababu Mola Mlezi wetu anatujua vyema, na Yeye hataki turejee kwenye
upotovu wenu. Yeye aliye tukuka shani yake amekienea kila kitu kwa ujuzi
wake. Anatuongoa kwa upole wake na hikima yake kwenye jambo litalo tuhifadhia
Imani yetu. Kwa Yeye peke yake ndio tumesalimisha mambo yetu, na huku tunashikilia
yale aliyo tuwajibisha tuyashike. Ewe Mola Mlezi wetu! Tutenge sisi na
hao kaumu yetu kwa Haki, kama ilivyo kuwa mwendo wako unavyo amua baina
ya wenye kufuata Haki na wakatenda mema, na wale wapotovu waharibifu. Na
Wewe kwa kuwa ujuzi wako na uwezo ulivyo enea ndiye Muadilifu na Muweza
kuliko mahakimu wote.
Rudi kwenye Sura
90. Hapo basi wale watu walikata tamaa ya kuwafanya Shua'ib na walio
kuwa naye wawafuate wao. Na wakajua kuwa hakika hao walikuwa wamethibiti
katika Dini yao. Kadhaalika waliogopa wasizidi kuwa wengi wale walio hidika
pamoja na Shua'ib kwa kudhihiri nguvu zake na kuthibiti kwake juu ya wito
wake. Kwa hivyo wale waheshimiwa wa kikafiri wakawaelekea wafwasi wao wakiwatisha
kwa kusema: Wallahi! Mkimfuata Shua'ib mkakubali wito wake, basi hapana
shaka nyinyi utakutokeni utukufu wenu na utajiri wenu kwa kufuata dini
potovu wasio kuwa wakiifuata wazee wenu.
Rudi kwenye Sura
91. Basi hapo kauli ya kuteremka adhabu ikawa imethibiti. Wakasibiwa
kwa tetemeko lilio tikisa nyoyo zao, wakawa katika majumba yao wamesinukia
kifudifudi hawana tena uhai.
Rudi kwenye Sura
92. Hii ndio shani ya Mwenyezi Mungu na hao walio mkanusha Shua'ib,
na wakamtishia, na wakamwonya kuwa watamfukuza katika mji wao, na wakafanya
kila kitu kuupinga wito wake. Wamehiliki wao na ukahiliki mji wao, ikawa
kama kwamba humo hawakuwahi kuishi wale walio mkadhibisha Shua'ib na wakadai
kuwa ati atakaye mfuata atakuwa amekhasiri, na wakatilia nguvu madai hayo.
Na lililo kuwa ni kuwa wao ndio walio poteza neema yao ya dunia na Akhera.
Rudi kwenye Sura
93. Shua'ib alipo ona hilaki ya kuvuruga iliyo wateremkia wale watu,
basi aliwaachilia mbali, na akasema kujivua nafsi yake asiwe mkosa pamoja
nao: Mimi nimekufikishieni ujumbe wa Mola wenu Mlezi unao pelekea mpate
wema nyinyi, lau kuwa mngeli ufuata. Na mimi nimefanya ukomo wa uwezo wangu
katika kukunasihini, na kukuwaidhini kwa mambo ya kukuokoeni na adhabu
ya Mwenyezi Mungu. Basi vipi tena niwasikitikie mno watu makafiri? Hayawi
hayo baada ya kuwa mimi nimekwisha jiudhuru kwao, na nikatumia juhudi yangu
kwa ajili ya kutaka kuwahidi na kuwaokoa, na wao wakakhiari kufuata yale
yale ya kuwahiliki.
Rudi kwenye Sura
94. Na Sisi hatukumpeleka Nabii yeyote kwenye mji akawalingania watu
wake wafuate Dini ya Mwenyezi Mungu iliyo sawa, na wao wakakataa kuukubali
huo wito, ila tuliwapatiliza kwa ufakiri na maradhi, ili wapate kuwa wanyonge
na wamwombe Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu, na kumsafia niya wapate kuondokewa
na balaa na wamuitikie Mtume wake.
Rudi kwenye Sura
95. Basi tena ilivyo kuwa hawakufanya hayo, bali wakaendelea na ukafiri
wao na inadi yao, tukawapa mtihani wa kuwapa neema badala ya dhiki ili
kuwapururia tu. Tukawapa kutononoka, na nafasi nzuri, na siha na afya,
mpaka wakawa wengi, na mali yao yakazidi, wakasema kwa ujinga wao: Hayo
yaliyo wapata baba zetu ya mahna, na balaa, na starehe na neema - hayo
yote ndio shani ya ulimwengu. Shida na neema huwajia watu kwa zamu. Hawakuzindukana
wakajua kuwa haya ni malipo ya kufru zao wakajizuia! Na kwa hivyo wakawa
hawaujui mwendo wa Mwenyezi Mungu, iliyo tukuka shani yake, katika sababu
za matengenezo na uharibifu wa binaadamu, na nini linalo leta neema na
nini linalo leta dhiki! Matokeo ya hayo ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwapatiliza
kwa kuwaletea adhabu ya kuteketeza kwa ghafla, na wao bila ya kujua nini
litawafika.
Rudi kwenye Sura
96. Na lau kuwa watu wa hiyo miji wangeliamini walio kuja nayo Mitume,
na wakatenda walio wausia, na wakajitenga na aliyo yaharimisha Mwenyezi
Mungu, tungeli wapa baraka nyingi zitokazo mbinguni na kwenye ardhi, kama
mvua, na mimea, na matunda, na wanyama, na riziki, na amani na kusalimika
na misiba. Lakini wao wakapinga na wakawakadhibisha Mitume. Basi
tukawapatiliza kwa adhabu nao wamelala, kwa sababu ya ukafiri na maasi
waliyo yazua. Basi huko kushikwa waliko shikwa kwa adhabu ni matokeo ya
lazima kuwa kwa ajili ya maovu waliyo yachuma, na yawe kuwa ni somo kwa
walio kama wao ikiwa wanayatia akilini!
Rudi kwenye Sura
97. Je, watu wa hii miji walio letewa wito wa Manabii wao na wasiwaamini,
wamejiaminisha kuwa adhabu yetu haitawafika nao wamezama katika usingizi
wao?
Rudi kwenye Sura
98. Je, watu hawa wameghafilika na wamejiaminisha kuwa adhabu haitawajia
mchana kweupe na jua linawaka, nao wameshughulikia mambo yasiyo na faida
nao?
Rudi kwenye Sura
99. Je, hawaujui mwendo wa Mwenyezi Mungu anavyo kwenda nao wanao
kanusha, hata wakajitumainisha kuwa haitowafikia adhabu usiku au mchana?
Naye, huipeleka kwa mpango wake wasio uona watu. Hakika hawawi wajinga
wa mpango na mwendo wa Mwenyezi Mungu katika kuadhibu ila wale wanao kanusha,
wenye kuzikhasiri nafsi zao kwa kutozinduka katika mambo yaliyo khusu kufanikiwa
kwao.
Rudi kwenye Sura
100. Je, hawaujui mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa kaumu zilizo kwisha
pita kabla yao, na kuwa shani yetu kwao ni kama ilivyo kuwa kwa walio watangulia?
Na kwamba wao lazima wafuate tuyatakayo. Tukitaka kuwaadhibu kwa sababu
ya madhambi yao tutawapatiliza kama tulivyo wapatiliza walio kama wao.
Nasi tunatia muhuri nyoyo zao kwa kuwa zimeharibika bila ya kiasi, mpaka
ikafika ukomo kuwa hazipokei tena uwongofu. Kwa muhuri huo imekuwa hawasikii
hikima wala nasiha, kwa msikio wa kufahamu na kuwaidhika.
Rudi kwenye Sura
101. Hiyo ni miji iliyo dumu karne nyingi, na imepitiwa na muda mrefu
katika taarikhi yao. Tunakusimulia hivi sasa baadhi ya khabari zao zenye
somo la kuzingatiwa. Na watu wa miji hiyo walifikiwa na Mitume wao kwa
Ishara zilizo wazi zenye kuonyesha ukweli wa wito wao. Lakini haikuwa shani
yao kuamini baada ya kuja hizo Ishara zilizo wazi, kwa sababu ya mtindo
wao wa kuwakanusha wasemao kweli. Basi wakawakadhibisha Mitume wao, wala
hawakuongoka! Basi ni hivyo Mwenyezi Mungu huweka kizuizi juu ya nyoyo
na akili za makafiri, ikafichika kwao Njia ya Haki, na wakajitenga nayo.
Rudi kwenye Sura
102. Wala hatukuwakuta wengi wa watu hao kuwa ni wenye kutimiza ahadi
kwa Imani tulio wausia kwa ndimi za Mitume, na yanayo tambuliwa na akili
na nadhari nzuri. Na mwendo ulio thibiti kwao ni vile kuselelea katika
upotofu na kwenda kinyume na kila ahadi.
Rudi kwenye Sura
103. Tena baada ya Mitume hao tulimtuma Musa a.s. Naye akaja na dalili
zenye kuonyesha ukweli wa anayo yafikisha kutokana nasi kumpelekea Firauni
na kaumu yake. Musa akaufikisha wito wa Mola wake Mlezi, na akawaonyesha
Ishara ya Mwenyezi Mungu. Nao wakadhulumu nafsi zao na watu wao kwa kuzikataa
kwa kiburi na upinzani tu! Basi wakastahiki adhabu kali kutokana na Mwenyezi
Mungu, na hivyo ukawa mwisho wa mambo yao! Basi ewe Nabii! Angalia vyema
mwisho wa mafisadi katika ardhi.
Rudi kwenye Sura
104. Musa akasema: Ewe Firauni! Hakika mimi nimetumwa kutoka kwa
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, Mwenye mamlaka juu ya mambo
yao yote, ili nikufikishieni wito wake, na nikuiteni muifuate Sharia yake.
Rudi kwenye Sura
105. Na mimi pupa yangu ni kumsemea kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na nimekujieni na Ishara yenye shani kubwa, yenye hoja iliyo dhaahiri katika
kubainisha Haki niliyo kuja nayo. Basi waachilie waje nami Wana wa Israili,
na uwatoe kwenye utumwa wa kahari yako, wende nami kwenye nchi nyengine
isiyo kuwa yako, na huko wapate kumuabudu Mola Mlezi wao na wako.
Rudi kwenye Sura
106. Firauni akamwambia Musa: Ikiwa umekuja na Ishara (muujiza) kutokana
na huyo aliye kutuma, basi nionyeshe kama wewe ni katika watu wakweli wanalo
lishika neno la haki.
Rudi kwenye Sura
107. Kiasi ya Musa kuitupa fimbo aliyo kuwa nayo mkononi mwake wa
kulia mbele ya Firauni, mara hiyo fimbo ikawa nyoka khasa dhaahiri, anakwenda
mbio huku na huku, kwa nguvu zinazo onyesha kuwa ana uhai timamu.
Rudi kwenye Sura
108. Akautoa mkono wake kutoka mfukoni mwake,
na hapo hapo ukawa mweupe safi kabisa ukimeremeta katika macho ya wanao
angalia!
Rudi kwenye Sura
109. Musa alipo ionyesha Ishara ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, zilitibuka
roho za wapambe wa Firauni na waheshimiwa wa kaumu yake, wakasema katika
kujipendekeza kwa Firauni na kumtetea: Hakika huyu ni bingwa katika ilimu
ya uchawi, wala hii si Ishara itokayo kwa Mwenyezi Mungu!!
Rudi kwenye Sura
110. Na yeye ameelekeza lengo lake akupokonyeni ufalme wenu,
na akutoeni katika nchi yenu kwa uchawi wake na yatayo tokea hapo kwa kuwavutia
watu wamili na wamfuate. Basi tazameni, mnaamrisha njia gani ya kutokana
naye huyu?
Rudi kwenye Sura
111. Wakasema: Akhirisha kukata shauri juu yake na nduguye huyu anaye
msaidia katika wito wake, na watume watu katika askari wako wende katika
miji ya ufalme wako wawakusanye walio mafundi katika ilimu ya uchawi.
Rudi kwenye Sura
112. Wakuletee kila mwanachuoni wa ilimu
za uchawi. Na wao watakufichulia nini khasa hakika ya aliyo kuja nayo Musa,
asije akafitinika yeyote.
Rudi kwenye Sura
113. Basi wakaja kwa Firauni wachawi walio kusanywa na askari wake.
Nao wakasema: Hapana shaka nasi tutapata malipo makubwa yanayo lingana
na hili linalo takikana kwetu, ikiwa sisi tutamshinda Musa.
Rudi kwenye Sura
114. Haraka haraka Firauni akawajibu kwa walitakalo: Naam! Hapana
shaka mtapata malipo makubwa. Na hapana shaka juu ya hayo nyinyi mtakuwa
watu wenye cheo kwangu.
Rudi kwenye Sura
115. Kisha wachawi wakamgeukia Musa, baada ya Firauni kuwaahidi alivyo
waahidi, na wao wakaonyesha wana imani na nafsi zao na kujitayarisha kwao
kwa uchawi wao katika uwanja wa mapambano. Wakamwabia: Ama utupe ulicho
nacho kwanza, au sisi tuwe wenye kutupa tulicho nacho.
Rudi kwenye Sura
116. Musa akwajibu jawabu ya mwenye imani ya kushinda, akionyesha
kutowabali: Tupeni nyinyi kwanza hicho mnacho tupa. Walipo tupa kila mmoja
wao, navyo ni kamba na fimbo, macho ya watu yalizugwa, na ikawapitikia
kuwa walicho kifanya kile ni hakika kweli. Na hali haikuwa ila ni kiini
macho tu. Mambo yale yaliwatisha watu, na nyoyo zao zikaingia khofu na
kitisho. Kwani wachawi wale waliwaletea watu uchawi unao onekana ni mkubwa,
na athari yake katika macho yao ni kubwa!
Rudi kwenye Sura
117. Mwenyezi Mungu akaitoa amri yake kumpelekea Musa: Tupa fimbo
yako. Sasa umekwisha fika wakati wake. Akaitupa kama alivyo amrishwa. Mara
hiyo fimbo ikaingia kuvimeza vile vizushi vyao walivyo zua na kubuni!
Rudi kwenye Sura
118. Basi Haki ikathibiti na kudhihiri upande wa Musa a.s. na
ukabwatika udanganyifu wa wachawi.
Rudi kwenye Sura
119. Firauni na waheshimiwa wake wakashindwa katika ule mkutano mkubwa,
na wakawa madhalili mbele ya watu wote kwa masaibu yaliyo wapata, nayo
ni kuvunjika moyo na kukata tamaa.
Rudi kwenye Sura
120. Haya ni mambo yaliyo wafika Firauni na waheshimiwa wake. Ama
wale wachawi Haki iliangaza kwao, na wakaanguka kwa kumsujudia Mwenyezi
Mungu nao wanainyenyekea Haki.
Rudi kwenye Sura
121. Huku wakisema hao wachawi walio tubia: Tumemuamini Muumba
wa viumbe vyote, Mwenye kumiliki na kuendesha mambo yao yote.
Rudi kwenye Sura
122. Hakika huyo ndiye Mungu anaye
itakidiwa na kuaminiwa na Musa na Haarun.
Rudi kwenye Sura
123. Jambo hili lilimtisha Firauni na ikafoka ghadhabu yake, akasema:
Hivyo nyinyi mmemuamini na kumsadiki Mola Mlezi wa Musa na Haarun
kabla sijakupeni ruhusa mimi? Hakika hapa pana kijambo mmekizua nyinyi
na Musa na Haarun kwa kuwafikiana. Na haya si chochote ila ni vitimbi mlivyo
vipanga katika mji wa Misri mpate kuwatoa wenyewe kwa hila yenu. Basi ngojeni,
mtaiona adhabu itayo kushukieni kuwa ndio jaza yenu kwa kumfuata
Musa na Haarun, na ndio adabu yenu kwa hivi vitimbi vyenu na khadaa!
Rudi kwenye Sura
124. Na ninakuapieni kuwa nitakuteseni vikali, na nitakukateni mikono
yenu na miguu yenu mbali mbali, nitakata mkono wa upande mmoja na mguu
wa upande wa pili, kisha nitakutundikeni misalabani, kila mmoja wenu,
nanyi mmo katika hali hiyo, ili muwe ni zingatio kwa anaye jifikiria kutufanyia
vitimbi, au kutaka kuufanyia uasi utawala wetu!
Rudi kwenye Sura
125. Nao hawakuibali kauli yake wala vitisho vyake, kwa kuwa Imani
ilikwisha saki ndani ya nyoyo zao. Wakamwambia: Hakika sisi ni wenye kurejea
kwa Mola wetu Mlezi. Kwa hivyo tunaneemeka katika rehema yake na bora ya
malipo yake.
Rudi kwenye Sura
126. Na wewe hutuchukii na kutuadhibu ila kwa kuwa tumemsadiki Musa,
na tumezikubali zilipo tujia Ishara za Mola wetu Mlezi zilio wazi, zenye
kuonyesha Haki! Kisha wakamuelekea Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu, wakisema:
Ewe Mola Mlezi wetu! Tumiminie subira kubwa, itupe nguvu kuhimili shida
zote; na utufishe katika Uislamu bila ya kuteseka kwa anayo tuahidi Firauni.
Rudi kwenye Sura
127. Baada ya Firauni na watu wake kuona waliyo yaona, katika vile
kudhihiri mambo ya Musa na nguvu za ushindi wake, na wachawi wakamuamini,
walisema wakuu wa kaumu yake: Unamuacha Musa na watu wake wawe huru katika
amani, ili mwisho wao wawafisidi kaumu yako dhidi yako katika nchi ya Misri
kwa kuwatia katika dini yao, na wakuache wewe na miungu yako bila ya wao
kujali? Hapo watu wa Misri watakuona wewe na hiyo miungu kuwa mmeshindwa.
Firauni akasema kuwajibu: Tutawawauwa watoto wao wa kiume wa watu hawa,
kila anaye zaliwa; na tutawabakisha wa kike wawe hai, ili wasiwe na nguvu,
kama tulivyo fanya zamani. Na sisi tuko juu yao kwa kuwashinda na
kwa utawala, na kuwafanyia kahari.
Rudi kwenye Sura
128. Na hapo Musa aliona kama dalili za huzuni katika watu wake,
basi akawatia nguvu katika azma yao. Akawambia: Mtakeni Mwenyezi Mungu
msaada na kukuungeni mkono. Na kuweni imara, wala msifazaike. Kwani ardhi
yote imo katika nguvu za uwezo wa Mwenyezi Mungu na ufalme wake.
Humrithisha amtakaye katika waja wake, wala si ya Firauni. Na mwisho mwema
wataupata wale wanao mcha Mwenyezi Mungu kwa kushikamana naye na kuzikamata
hukumu zake.
Rudi kwenye Sura
129. Wakasema wale watu kwa huzuni na unyonge: Sisi tulipata
maudhi zamani kutoka kwa Firauni kabla hujatujia, na hivi sasa tena baada
ya kuja kwako. Musa akawafungulia mlango wa matarajio mema kwa kuwaambia:
Hakika linalo tarajiwa kwa fadhila za Mola wenu Mlezi ni kumteketeza adui
yenu, aliye kufanyeni watumwa na akakuteseni kwa dhulma yake, na akujaalieni
nyinyi ndio wa kuimiliki ardhi aliyo kuahidini. Yeye Subhanahu, Aliye takasika,
anayajua mnayo yatenda baada ya kukuwekeni huku. Je, mtaishukuru neema
au mtaikufuru? Na mtatenda mema katika nchi au mtafanya fisadi? Hayo ili
apate kukulipeni duniani na Akhera kwa mujibu wa mtendayo.
Rudi kwenye Sura
130. Na hakika Sisi tuliwaadhibu Firauni na watu wake kwa ukame,
na dhiki ya maisha, na upungufu wa matunda na mazao na miti, kwa kutaraji
kuwa watazindukana wautambue unyonge wao, na kushindwa ufalme wao wa jeuri
mbele ya nguvu za Mwenyezi Mungu, wapate kuwaidhika na waache kuwadhulumu
Wana wa Israili, na wauitikie wito wa Musa a.s. Kwani mtindo wa shida ni
kuzuia kujidanganya, na kutengeza tabia, na kuzielekeza nafsi ziikubali
Haki, na kumridhi Mola Mlezi wa viumbe vyote, na kumnyenyekea Yeye tu,
si mwenginewe.
Rudi kwenye Sura
131. Lakini tabia ya Firauni na wasaidizi wake ni kuto thibiti juu
ya Haki. Wepesi kurejea kwenye khiana na uasi. Hao ni watu wa kigeugeu!
Ikiwajia kutononoka na neema - na mara nyingi huwa hivyo - wao wakisema:
Sisi tunastahiki haya tuliyo nayo kuwapita watu wengineo! Na likiwasibu
la kuwaudhi, kama ukame, au tauni, au msiba wa miili au riziki, wakiona
yamewapata hayo kwa ukorofi wa Musa na walio pamoja naye. Na wanaghafilika
kuwa dhulma zao, na fisadi zao ndizo zilizo pelekea kuja hayo yanayo wapata!
Basi na watanabahi, na wajue kuwa ujuzi wa ukorofi wao uko kwa Mwenyezi
Mungu. Yeye ndiye anaye wapatiliza kwa sababu ya vitendo vyao viovu. Yeye
ndiye anaye wapelekea hayo yanao waudhi, wala si Musa na alio nao. Lakini
wengi wao hawaijui Hakika ambayo haina shaka.
Rudi kwenye Sura
132. Na kwa hii fikra mbovu waliyo nayo wakaendelea na upinzani.
Walisema walipo ona miujiza ya Musa: Wewe hata ukituletea kila namna ya
Ishara zinazo onyesha ukweli wa wito wako, ili kutuachisha dini yetu, na
tusiwafanye watumwa watu wako, sisi hatukusadiki wala hatukufuati.
Rudi kwenye Sura
133. Basi Mwenyezi Mungu aliwateremshia masaibu na balaa zaidi,
kama tufani lilio funika mwahala mwao, na nzige walio kula kila mmea na
mti ulio bakia, na chawa, yaani vijidudu vinavyo haribu matunda na kuteketeza
wanyama na mimea. na vyura vilivyo enea vikafanya maisha yao dhiki, na
vikachafua kila pahala, na damu iliyo sabibisha maradhi mengi, kama kupasuka
mishipa ya damu katika mwili, na damu inayo najisisha kila pahala ikasabibisha
presha, au kupasuka ikaleta kiharusi na kupooza, na kutokwa na mkojo wa
damu kwa sababu ya kichocho na mfano wake, au ikawa inachanganyika na maji
yao wanayo hitajia kunywa au kupikia. Mwenyezi Mungu aliwapatiliza na Ishara
hizi zote zilio wazi! Nao wasiathirike, nyoyo zao zikabaki kuwa ngumu,
na wenye kutakabari hawataki Imani wala kurejea kwenye Haki. Walikuwa watu
walio bobea kwenye madhambi na ukosefu, kama ilivyo ada yao.
Rudi kwenye Sura
134. Katika kuzidi kigeugeu chao kama zinavyo badilika sababu, walikuwa
kila ikiwashukia namna yoyote ya adhabu wakisema kwa shida na machungu
yanayo wapata: Ewe Musa! Tuombee kwa Mola Mlezi wako, kwa vile alivyo
kuahidi kuwa ukimwomba atakupa miujiza na atakuitikia dua, atuondolee adhabu
hii. Na sisi tunakuapia kuwa ukituondolea basi bila ya shaka tutakuitikia
na tutawaachilia wende nawe Wana wa Israili kama ulivyo taka!
Rudi kwenye Sura
135. Tulipo waondolea adhabu kila mara kwa muda wao mpaka mwisho
wake ukisha huivunja ahadi yao, na huenda kinyume na kiapo chao, na hurejea
yale yale waliyo kuwa nayo. Kwao wao hayo majaribio ya kuwaachisha maovu
hayakuleta faida!
Rudi kwenye Sura
136. Tuliwateremshia nakama yetu. Tukawazamisha baharini kwa sababu
ya kushikilia kwao kukanusha Ishara zetu, na hadi ya kutoyabali mafunzo
ya Imani na ut'iifu yaliyomo katika hizo Ishara.
Rudi kwenye Sura
137. Tukawapa watu ambao walikuwa wakidharauliwa katika Misri, nao
ni Wana wa Israili, ardhi alio ipa baraka Mwenyezi Mungu kwa kuifanya ina
rutba na kheri nyingi, tangu mashariki mpaka magharibi yake. Neno jema
la Mwenyezi Mungu likatekelezwa kwa ukamilifu, na pia ahadi yake ya ushindi
kwa Wana wa Israili, kwa sababu ya kuvumilia kwao dhiki. Na tukayateketeza
majumba ya fakhari, na kila majenzi, na chanja za mimea ya kutambaa, na
bustani, na pandio za mizabibu, waliyo kuwa wakisimamisha na kujenga akina
Firauni na watu wake! Hiyo ndiyo shani ya Mwenyezi Mungu, na ametimiza
kweli ahadi yake kwa Wana wa Israili.
Rudi kwenye Sura
138. Wana wa Israili wakaivuka bahari kwa uangalizi wetu, na
kuwaunga mkono na kuwafanyia mepesi mambo yao. Baada ya kwisha vuka waliwakuta
kaumu wameshika ibada ya masanamu. Walipoona hivi yale waliyo kuwa wameyazoea
kuwaona Wamisri wakiabudu masanamu yaliwaghilibu, wakamtaka Musa awafanyie
nao masanamu wayaabudu, kama ilivyo kuwa wale kaumu wana masanamu yao wanayo
yaabudu! Hapo hapo Musa a.s. aliwatahayarisha na kuwakanya, akasema: Hakika
nyinyi ni watu wapumbavu, msio na akili! Hamjui ibada ya Haki, wala hamumjui
Mungu anaye stahiki kuabudiwa!
Rudi kwenye Sura
139. Hawa mnao waona wanaabudu masanamu, hapana shaka haya walio
nayo ni yenye kuangamia, na hii dini waliyo nayo ni potovu , bure bilashi.
Na a'mali zao ni zenye kupotea, wala hazibaki.
Rudi kwenye Sura
140. Je, nikutafutieni wa kuabudiwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu Mola
Mlezi wa viumbe vyote, na Yeye ndiye aliye kupeni fadhila, na akakupeni
neema asio pata kupewa mwengine asiye kuwa nyinyi katika zama zenu?
Rudi kwenye Sura
141. Kumbukeni alipo kuvueni Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa uangalizi
wake na watu wa Firauni, walio kuwa wakikuadhibuni ukomo wa adhabu, wakikudhalilisheni
muwatumikie katika kazi ngumu, wala hawakukuoneeni huruma kama wanyama,
wakiuwa wavulana wenu na wakiwabakisha wasichana ili mzidi kudhoofika kwa
wingi wa wanawake! Na katika adhabu za Firauni zilizo kushukieni, na kukuvueni
nazo, pana mtihani mkubwa wa Mola wenu Mlezi, wala hapana mfano wake.
Rudi kwenye Sura
142. Tulimuahidi Musa tutazungumza naye na tutampa Taurati baada
ya kutimia masiku (wingi wa "usiku") thalathini ya yeye kuabudu. Na tukauongeza
muda huo kwa masiku kumi, kutimiza ibada. Yakawa masiku arubaini. Musa
akamwambia nduguye Haarun alipo kuwa anakwenda kuzungumza na Mwenyezi Mungu:
Kuwa badala yangu kwa hawa watu wangu. Na watengenezee mambo yao yanayo
hitajia kutengenezwa. Na tahadhari na kufuata njia ya mafisadi. (Angalia:
Kwa Kiswahili safi, "Masiku" ni wingi wa "Usiku". Ama wingi wa "Siku" ni
"Siku" vile vile kama ilivyo katika aghlabu ya maneno mengine yanayo anzia
"S", kama Saa, Sanda, Sahani, Sabuni, Safari, Sufuria n.k.)
Rudi kwenye Sura
143. Na alipo kuja Musa kuzungumza nasi, na Mola Mlezi wake akanena
naye kwa maneno ambayo siyo kama kusema kwetu, Musa alisema: Ewe Mola Mlezi
wangu! Nionyeshe dhati yako na unidhihirikie, nipate kukutazama nizidi
utukufu. Mwenyezi Mungu akasema: Huwezi kuniona. Kisha Subhanahu, Aliye
takasika alitaka kumkinaisha kuwa hawezi kumwona, akamwambia: Walakini
utazame huo mlima ambao una nguvu kuliko wewe. Ukithibiti pahala ulipo
wakati wa kudhihiri kwangu, basi utaniona nikijidhihirisha kwako. Basi
Mola wake Mlezi alipo jionyesha kwa huo mlima kwa njia inayo wafikiana
naye Mtukufu, mlima ulivurugika ukawa sawa sawa na ardhi. Musa akaanguka,
kazimia kwa kitisho alicho kiona. Alipo zindukana kutokana na kuzimia kwake
alisema: Nakutakasa mtakaso mkuu na kuonekana kwako duniani! Hakika mimi
ninatubu kwako kuja kukutaka kitu bila ya ruhusa yako. Na mimi ni wa mwanzo
katika zama zangu wa wanao amini utukufu wako na ubora wako.
Rudi kwenye Sura
144. Mwenyezi Mungu alipo mzuilia Musa asimwone, akaingia kumhisabia
neema zake ili amliwaze kwa vile kumkatalia, akamwambia: Ewe Musa! Mimi
nimekufadhilisha, na nimekuteua kuliko watu wote wa zama zako, ili ufikishe
vitabu vya Taurati, na kwa kusema nawe bila ya kuwapo mtu kati. Basi yashike
hayo niliyo kukufadhili, na unishukuru kama wafanyavyo wenye kushukuru,
wanao kadiri neema.
Rudi kwenye Sura
145. Na tulimbainishia Musa katika zile mbao za Taurati kila kitu
kilicho khusu mawaidha na hukumu zilizo elezwa mbali mbali, wanazo hitajia
watu duniani na Akhera. Na tukamwambia: Zishike hizi mbao baraabara
na kwa kuazimia. Na waamrishe watu wako washike yaliyo bora humo, kama
kusamehe badala ya kulipiza kisasi, na kuachilia badala ya kungojea, na
kulegeza badala ya kukaza. Enyi kaumu ya Musa! Nitakuonyesheni katika vitabu
vyenu makaazi ya wale wanao asi amri za Mwenyezi Mungu, na watavyo angamia,
ili mpate kuzingatia. Basi msende kinyume yakakusibuni yalio wasibu hao
waasi.
Rudi kwenye Sura
146. Hao walio majeuri na wakapanda kiburi katika ardhi wakakataa
kukubali yaliyo sawa bila ya haki, nitawazuia wasiweze kuzizingatia dalili
za uwezo wangu ziliomo katika nafsi za watu na jiha zote. Watu hawa
hata wakiona kila Ishara inayo thibitisha ukweli wa Mitume wetu hawaisadiki.
Na wakiiona njia ya uwongofu hawaipiti, na wakiiona njia ya upotofu ndio
wanaipita! Hayo yanatokea kwao kwa sababu wamezikanusha Ishara zetu zilio
teremshwa, na wameghafilika na kuongoka kwazo.
Rudi kwenye Sura
147. Na walio zikanusha Ishara zetu zilio teremshwa juu ya Mitume
wetu kwa ajili ya uwongofu, na wakakanusha kukutana nasi Siku ya Kiyama,
wakakataa kufufuliwa na kulipwa, vitendo vyao walivyo kuwa wakitarajia
viwafae vitapotelea mbali. Hawatokuta ila malipo ya kufru na maasi waliyo
endelea nayo kuyatenda.
Rudi kwenye Sura
148. Na baada ya Musa kwenda kwenye mlima kusema na Mola Mlezi wake,
kaumu yake walichukua vyombo vyao vya kujipamba wakatengeneza Sura ya ndama,
asiye na akili wala hatambui kitu. Lakini akitoa sauti mfano wa sauti ya
ng'ombe, kwa namna walivyo muunda na ukipita upepo ndani yake. Na aliye
waundia ni Saamiriyu (Msamaria). Naye akawaamrisha wamuabudu! Upumbavu
gani huu wa akili zao! Hivyo wao walipo mfanya ndiye mungu wakamuabudu,
hawakuona kuwa hawasemezi, wala hawezi kuwaongoa wafuate njia iliyo sawa?
Hakika hawa wamejidhulumu nafsi zao kwa kitendo hichi kiovu.
Rudi kwenye Sura
149. Walipo tambua kuteleza kwao, na makaso yao, wakababaika, na
wakajuta majuto makubwa kwa kumfanya ndama ndiye mungu. Makosa yao yakabainika
wazi, wakasema: Wallahi! Ikiwa Mola wetu Mlezi hakutusamehe hakika tutakuwa
miongoni walio khasiri khasara iliyo dhaahiri; kwa vile kuabudu kisicho
faa kuabudiwa.
Rudi kwenye Sura
150. Na Musa alipo rejea kutoka kuzungumza na Mola Mlezi wake kuja
kwa watu wake, naye kakasirika nao kwa vile walivyo muabudu ndama, na amehuzunika
kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewatia mtihanini - kwani Mwenyezi Mungu alikwisha
mpa khabari ya yale kabla hajarejea - aliwaambia: Kitendo gani kiovu hichi
mlicho kitenda baada ya kuondoka kwangu! Mmetangulia kwa kumuabudu ndama
msifuate amri ya Mola wenu Mlezi kuwa mningojee, na mkawa hamkuishika ahadi
yangu mpaka nikakuleteeni Taurati? Akaziweka zile mbao, na akamuelekea
nduguye kwa huzuni kubwa kwa yale aliyo yaona kwa kaumu yake. Akaingia
kumvuta ndugu yake kwa kichwa akimbururia kwake kwa wingi wa ghadhabu.
Haya ni kuwa alidhani kuwa amefanya taksiri hakuwazuia kufanya walio yafanya!
Haarun akasema: Ewe mwana wa mama yangu! (1) Hakika hawa watu walipo fanya
waliyo yafanya walinidharau na wakanishinda nguvu. Na wakakaribia kuniuwa
kwa kuwa niliwakataza wasimuabudu ndama. Basi usiwafurahishe maadui kwa
kunitesa mimi, wala usiitakidi kuwa mimi ni mmoja wa wenye kudhulumu, kwani
mimi ni mbali nao na dhulma yao.
(1) Haarun amemwita Musa kwa kumnasibisha na mama yao, ijapo kuwa
hao walikuwa ndugu khalisa, wa baba na mama, kwa sababu huyo mama alikuwa
Muumini. Kumtaja yeye ni kuzidi kukumbusha mapenzi.
Rudi kwenye Sura
151. Musa alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nisamehe kwa haya niliyo
mfanyia ndugu yangu kabla sijayajua mambo. Na msamehe ndugu yangu ikiwa
kakosea katika kushika pahala pangu kwa vizuri. Na tuingize katika eneo
la rehema yako, kwani Wewe ndiwe Mwenye rehema nyingi kushinda wote wenye
kurehemu.
Rudi kwenye Sura
152. Hakika wale walio endelea kumfanya ndama kuwa mungu, kama Msamaria
na wenziwe, itawafika ghadhabu kubwa kutoka kwa Mola wao Mlezi huko Akhera,
na uvunjifu mkubwa katika maisha ya duniani. Na mfano wa malipo hayo ndio
tunamlipa kila mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo, na akaabudu kinginecho.
Rudi kwenye Sura
153. Na wale walio tenda vitendo vibaya vya ukafiri na kuabudu ndama
na maasi mengineyo, kisha wakarejea kwa Mwenyezi Mungu baada ya kutenda
hayo, na wakamsadiki, basi hakika Mola wako Mlezi baada ya toba yao, ni
Mwenye kuwasitiri, na kuwasamehe kwa hayo waliyo kuwa nayo.
Rudi kwenye Sura
154. Na Musa zilipo muondoka ghadhabu kwa kutoa udhuru nduguye, akazirejea
zile mbao alizo ziweka chini akazichukua. Na kwenye hizo mbao umeandikwa
uwongofu, na uwongozi, na njia za kupata rehema, kwa wale wanao iogopa
ghadhabu ya Mola wao Mlezi.
Rudi kwenye Sura
155. Kisha Mwenyezi Mungu alimuamrisha awalete baadhi ya jamaa katika
kaumu yake wawatakie radhi walio muabudu ndama, na akawapa miadi. Musa
akawateuwa katika kaumu yake watu sabiini katika wasio muabudu ndama, nao
wakawa wanawawakilisha kaumu yao. Akenda nao mpaka kwenye mlima. Na huko
wakamwomba Mwenyezi Mungu awaondolee balaa, na akubali toba ya walio muabudu
ndama kati yao. Ikawachukua zilzala (tetemeko) kubwa pahala hapo, wakazimia
kwa sababu yake. Na hayo kwa kuwa hawakuwaacha kaumu yao walipo abudu ndama,
wala hawakuamrisha mema, wala hawakuwakanya maovu! Musa alipoona yale alisema:
Ewe Mola wangu Mlezi! Lau ungeli penda kuwaangamiza ungeli waangamiza kabla
hawajaja hapa kwenye miadi, na ukaniangamiza na mimi pia, ili waone hayo
Wana wa Israili wasinituhumu kuwa mimi nimewauwa. Basi ewe Mola Mlezi wangu!
Usituhiliki kwa walio yafanya wajinga kati yetu. Kwani hii balaa ya kuabudu
ndama haikuwa ila ni majaribio yaliyo toka kwako. Wewe unampoteza unaye
taka apotee katika hao wanao ishika njia ya shari, na unawahidi unaye taka
ahidike. Wewe ndiye mwenye kusema: Nitawaandikia wenye kujikinga na ukafiri
na maasi katika kaumu yako, na akatoa Zaka iliyo faridhiwa, na Mwenye kusamehe
madhambi.
Rudi kwenye Sura
156. Na tukadirie hapa duniani maisha mema, na tupate tawfiqi tuweze
kut'ii, na Akhera tupate malipo mazuri, na maghfira, na rehema, kwa kuwa
sisi hakika tumekwisha rejea kwako na tunatubu kwako. Mola Mlezi wao akawaambia:
Adhabu yangu namfikishia nimtakaye katika wasio tubu, na rehema yangu imeenea
juu ya kila kitu, na nitawaandikia khasa wale wanao jikinga na ukafiri
na maasi katika kaumu yako, na wanao toa Zaka zilio lazimishwa, na
wanao sadiki Vitabu vyote vilivyo teremka.
Rudi kwenye Sura
157. Na nawakusudia khasa wanao mfuata Mtume Muhammad, ambaye haandiki
wala hasomi, na ambaye wanakuta sifa zake zimeandikwa katika vitabu vyao
vya Taurati na Injili. Yeye anawaamrisha kila kheri na anawakataza kila
shari. Na anawahalalishia vitu ambavyo tabia inaviona ni vizuri, na anawaharimishia
vitu ambavyo tabia inavichukia kwa kuwa vina madhara, kama damu na mzoga.
Na anawaondolea mizigo mizito na mikazo iliyo kuwa ikiwabana. Basi wanao
usadiki Utume wake, na wakamsaidia, na wakamuunga mkono, na wakamnusuru
na maadui zake, na wakaifuata Qur'ani aliyo teremshiwa pamoja naye kama
nuru ya uwongofu, hao basi ndio wenye kufuzu, sio wenginewe ambao hawakumuamini.
Rudi kwenye Sura
158. Ewe Nabii! Waambie watu: Hakika mimi nimetumwa kutoka kwa Mwenyezi
Mungu kwenu nyinyi nyote, bila ya farka baina ya Mwaarabu na asiye kuwa
Mwaarabu, baina ya mweusi na mweupe. Na Mwenyezi Mungu aliye nituma ni
Yeye peke yake ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Huipitisha amri
yake kwa mujibu wa hikima yake. Na hufanya mbinguni na duniani kama anavyo
penda. Wala hapana wa kuabudiwa kwa haki ila Yeye. Na Yeye ndiye Mwenye
uwezo wa kuhuisha na kufisha, wala hapana mwenginewe. Basi muaminini Yeye
na Mtume wake, huyu Nabii asiye soma wala kuandika. Naye huyu anamuamini
Mwenyezi Mungu ambaye anaye kuiteni mumuamini. Na anaamini Vitabu vyake
vilivyo teremshwa. Basi mfuateni katika kila afanyalo na asemalo mpate
kuongoka na kuongozeka.
Rudi kwenye Sura
159. Na katika kaumu ya Musa wako jamaa walio bakia na Dini iliyo
sawa. Wakiwahidi watu kwa Haki aliyo kuja nayo Musa kutoka kwa Mola wake
Mlezi, na wakifanya uadilifu pale wanapo pitisha hukumu.
Rudi kwenye Sura
160. Mwenyezi Mungu amezitaja neema zake juu ya kaumu ya Musa. Akafahamisha
kuwa aliwafanya makundi thinaashara, na akawafanya mataifa, na kila taifa
likawa na mpango wao, ili kuzuia uhasidi na kukhitalifiana. Na walipo taka
watu wake maji jangwani, alimfunulia Musa alipige jiwe kwa fimbo yake.
Akalipiga, zikatibuka kutoka kwenye hilo jiwe chemchem kumi na mbili kwa
idadi ya kabila zao. Kila kabila kati yao ilijua pahala pake makhsusi pa
kunywa. Basi haikuwa huyu kumuingilia huyu. Na akajaalia kiwingu
chende kuwapa kivuli chake katika jangwa, kuwakinga na mwako wa jua. Akawateremshia
Manna, nacho ni chakula kwa Sura kinafanana na mvua ya barafu, na tamu
kama asali. Na akateremsha Salwa, naye ni ndege aliye nona. Na akawaambia:
Kuleni hivi vinono tulivyo kuruzukuni katika tulivyo kuteremshieni. Lakini
walijudhulumu nafsi zao, na wakazikufuru neema hizo, kwa kuzikataa na kutaka
nyenginezo. Na Sisi hatukupata madhara kwa udhalimu wao, lakini upungufu
wamepata wao.
Rudi kwenye Sura
161. Ewe Nabii! Wakumbushe hao waliopo miongoni mwao katika zama
zako - ili iwe ni onyo kwa vile walivyo tenda walio watangulia -
wakumbushe kauli yetu tulio waambia hao walio watangulia kwa ulimi wa Musa:
Kaeni katika mji wa Baitul Muqaddas (Yerusalemu) baada ya kutoka jangwani.
Na kuleni kheri zake kokote humo mtakako, na semeni: Tunakuomba ewe Mola
Mlezi wetu, utufutie makosa yetu. Na muingie kwenye lango la mji kwa kuinamisha
vichwa kama kurukuu kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Mkifanya hivyo tutakufutieni
dhambi zenu, na tutazidisha thawabu za watendao mema.
Rudi kwenye Sura
162. Lakini waliikhalifu amri ya Mola wao Mlezi, wakasema kwa udhalimu
maneno sio walio ambiwa, kwa kusudi ya kumkejeli Musa. Basi tukawateremshia
adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya kuendelea kwao na udhalimu na kukiuka
mpaka.
Rudi kwenye Sura
163. Na waulize Mayahudi, kwa kuyachukia walio yafanya wenzao walio
watangulia, khabari ya kijiji, nacho ni Elat, kilicho kuwa karibu na bahari.
Wakaazi wake walivunja amri ya Mwenyezi Mungu ya kupiga marfuku kuvua samaki
siku ya Jumaamosi, kuwa hiyo ni siku ya ibada tu kwao. Na siku hiyo samaki
walikuwa wakiwajia vururu juu ya maji. Na siku isiyo kuwa Jumaamosi
samaki walikuwa hawaji. Huo ni mtihani wa Mwenyezi Mungu! Na kwa mfano
wa mtihani huo, au majaribio hayo yaliyo tajwa, ndio tunawajaribu kwa majaribio
mengine kwa sababu ya upotovu wao unao endelea, ili adhihiri mwema na mbaya.
Rudi kwenye Sura
164. Na wakumbushe pia hao Mayahudi pale kikundi cha watu wema katika
wenzao walio tangulia, ambao hawakutenda mabaya waliyo yatenda wengineo,
walipo waambia wanao wapa mawaidha wale waovu: Kwa sababu gani mnawapa
nasaha watu ambao Mwenyezi Mungu atawahiliki, au atawaadhibu adhabu kali
Akhera, kwa sababu ya madhambi wanayo yatenda? Wakasema: Tunawapa mawaidha
ili tupate udhuru kwa Mola wako Mlezi, tusiwe tumefanya taksiri, na kutaraji
huenda wakamchamngu.
Rudi kwenye Sura
165. Walipo yaacha mawaidha waliyo pewa, tukawaokoa na adhabu wale
ambao walikuwa wakikataza vitendo viovu, na tukwashika walio dhulumu na
wakavuka mipaka na wakakhalifu kwa kuwapa adhabu kali, nayo ni udhalili
na shakawa, kwa sababu ya kuendelea kwao kutokana na ut'iifu wa Mwenyezi
Mungu, Mola Mlezi wao.
Rudi kwenye Sura
166. Walipo zidi kuwa wagumu, na wakaendelea kutobali waliyo katazwa,
wala adhabu kali isiwaachishe uovu, tukawafanya kama manyani kwa kuzigeuza
nyoyo zao, na kuwaondolea uwezo wa kuifahamu Haki, wakawa mbali na kila
kheri.
Rudi kwenye Sura
167. Na wakumbushe pia hao Mayahudi pale alipo wajuvya Mola Mlezi
wako wenzao walio watangulia kwa ndimi za Manabii wao: Mwenyezi Mungu atawasalitisha
Mayahudi mpaka Siku ya Kiyama adhabu mbaya kabisa kwa sababu ya dhulma
yao na upotovu wao. Kwani Mola wako Mlezi ni Mwepesi wa kuwaadhibu watu
makafiri, kwani adhabu yake itakuja tu bila ya shaka yoyote. Na kila kijacho
kipo karibu, (chambilecho Waarabu). Na Yeye Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
na Mwenye kurehemu kwa anaye rejea kwake akatubu.
Rudi kwenye Sura
168. Na Sisi tumewagawa makundi makundi duniani. Wamo kati yao walio
wema. Na hao ndio walio amini wakenda mwendo ulio sawa. Na wapo miongoni
mwao watu wasio sifika kwa wema. Na wote tumewafanyia mitihani kwa kuwapa
neema na kuwapa nakama, ili watubu, waache waliyo katazwa.
Rudi kwenye Sura
169. Baada ya hao tulio kwisha wataja na tukawagawa sehemu mbili,
walifuatia waovu wakairithi Taurati kutokana na walio watangulia. Lakini
hao hawakufanya yalio amrishwa humo. Kwani wao walishika starehe ya dunia
badala ya Neno la Haki. Wakijiambia nafsi zao: Mwenyezi Mungu atatusamehe
kwa tunayo yatenda! Wakitaraji maghfira, na ilhali kuwa yakiwajia kama
yale waliyo yashika watayashika vile vile. Basi wao wamekuwa wameshikilia
kuendelea na madhambi pamoja na kutaka kwao msamaha. Tena basi Mwenyezi
Mungu anawatahayarisha kwa vile kutaka maghfira na huku wanaendelea na
yao, akasema: Sisi tulichukua kwao ahadi katika Taurati - nao wameyasoma
yaliomo humo - kuwa waseme kweli; nao wakasema uwongo! Na hakika neema
za nyumba ya Akhera za wanao jikinga na maasi ni bora kuliko starehe za
duniani! Basi je, mtaendelea na uasi wenu, wala hayaingii akilini mwenu
kuwa neema hizo ni bora kwenu? Na mnakhiari badala yake hizo starehe za
dunia?
Rudi kwenye Sura
170. Na wanao ikamata baraabara Taurati,
na wakashika Sala zilizo faridhiwa kwao, hakika Sisi hatutaupoteza ujira
wao kwa sababu ya kutengeneza kwao na kutenda kwao mema.
Rudi kwenye Sura
171. Mwenyezi Mungu ameijibu kauli ya Mayahudi walipo sema kwamba
Wana wa Israili hawakupata kwenda kinyume na Haki. Alisema: Ewe Nabii!
Wakumbushe pale tulipo unyanyua mlima juu ya Wana wa Israili ukawa kama
kiwingu, na wakafazaika kwa kuwa walidhani utawaangukia. Nasi tukawaambia
wakati ule ulipo nyanyuliwa na wao wamo katika khofu: Yashikeni ya uwongofu
tuliyo kupeni katika Taurati kwa nguvu na kuazimia ut'iifu. Na kumbukeni
yaliyomo ndani yake ili mpate kuzingatia na zitengenee nafsi zenu kwa kuchamngu.
Rudi kwenye Sura
172. Hapa Mwenyezi Mungu amebainisha hidaya ya wanaadamu kwa kusimamisha
dalili katika viumbe, baada ya kwisha bainisha kwa njia za Mitume na Vitabu.
Alisema: Ewe Nabii! Waambie watu pale Mola wako Mlezi alipo watoa kutoka
migongo ya wanaadamu na watoto wao na wanao zaliwa karne baada ya karne,
kisha akwasimamishia dalili za Ungu wake, na akawapa akili na nadhari
ya kuwawezesha kuzijua, na kwa hizo akili na nadhari waweze kutambua
Tawhidi na Rubuubiya, yaani kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja Pekee na ni Mola
Mlezi wa viumbe vyote, hata wakawa hao wanaadamu kama walio ulizwa: Je,
Mimi siye Mola wenu Mlezi? Nao wakajibu: Kwani, Wewe ndiye Mola Mlezi wetu.
Tunajishuhudia hayo juu ya nafsi zetu...Haya ni kwa kuwa kumkini kwao kupata
kujua hizo hoja na dalili, na kutamakani kwao katika hayo imekuwa kama
kwamba ni kukiri na kuungama. Na Sisi tumefanya haya ili msije kusema Siku
ya Kiyama: Hakika sisi tulikuwa tumeghafilika na hiyo Tawhidi, na tulikuwa
hatuijui.
Katika Aya hii inaonyesha kuwa watoto asili yake wanatoka kwenye
uti wa mgongo. Na ilimu ya kisasa imethibitisha kuwa kokwa za khaswa zinakuwa
katika sehemu ya mgongo chini ya mafigo. Na zinakaa hapa mpaka katika miezi
ya mwisho ya mimba ndio huteremka pale pahali pake pa kawaida panapo onekana.
Na pengine hata hivyo huchelewa kuteremka hata baada ya mtoto kuzaliwa.
Kadhaalika mayai ya mwanamke yanafanyika chini ya figo khasa, kisha ndio
huteremka pahala pake karibu na tumbo la uzazi.
Rudi kwenye Sura
173. Au mtasema: Walishiriki baba zetu kabla yetu, na sisi ni dhuriya
zao tumewafuata tu. Basi ewe Mola Mlezi wetu! Unatushika utuhiliki kwa
walio yafanya wapotovu miongoni mwa baba zetu, kwa kujenga misingi ya ushirikina
tulio endelea nao? Basi hamna hoja.
Rudi kwenye Sura
174. Kwa mfano wa maelezo wazi yenye hikima tunawabainishia wanaadamu
dalili za kuwepo Mwenyezi Mungu, ili warejee waache ukhalifu wao na kuwafuata
wapotovu.
Rudi kwenye Sura
175. Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa wanao kadhibisha kwa Aya zake
alizomteremshia Mtume wake. Akasema: Ewe Nabii! Wasomee kaumu yako khabari
za mtu mmoja katika Wana wa Israili. Tulimpa ilimu ya kuzijua Ishara tulizo
wateremshia Mitume wetu. Yeye huyo akazipuuza, wala asizishughulikie. Basi
Shetani akamfuata kwa khatua zake, na akamtawala kwa upotovu wake, akawa
katika kundi la walio potea.
Rudi kwenye Sura
176. Na lau tungeli taka kumnyanyua afike daraja za watu wema, tungeli
mnyanyua kwa kumwezesha kuyatenda maamrisho ya hizo Aya.. Lakini yeye alishikamana
na dunia, na hakuweza kunyanyuka kwendea uwingu wa uwongofu. Akafuata matamanio
yake. Akawa hali yake daima yumo katika dhiki, na kushughulika kwake ni
kwa dunia, na tafakuri zake duniani ni kutaka kuipata hiyo dunia basi.
Hali yake ni kama hali ya mbwa anapo kuwa katika hali ovu kabisa, anavyo
kuwa daima anapumua na kutoa limi lake nje, ukimkemea au ukimwacha. Hudorora
ulimi wake kwa kuvuta pumzi kwa shida! Kadhaalika mwenye kuipenda
dunia hudumu daima katika kuwania starehe zake na matamanio yake! Hakika
hizo ndizo sifa zinazo mueleza huyo mwenye kuziacha Aya zetu, na ndio sifa
ya wote wanao zikadhibisha Aya zetu zilio teremka. Basi wasimulie
kisa chake hichi, huenda wakafikiri na wakaamini.
Rudi kwenye Sura
177. Ni mbaya kweli hali ya hao wanao zipinga
Ishara zetu, na kwa huku kukengeuka kwao na kuacha Haki hakumdhulumu mtu
ila nafsi zao tu.
Rudi kwenye Sura
178. Na yule ambaye Mwenyezi Mungu amemwezesha kufuata njia ya haki
huyo basi ndie aliye ongoka kweli, mwenye kupata furaha ya kote kuwili
duniani na Akhera. Na mwenye kukosa uwezesho huo kwa sababu ya kumilikiwa
na pumbao lake basi watu hao ndio walio khasiri.
Rudi kwenye Sura
179. Na tumewaumbia wengi katika majini na watu marejeo yao ni Motoni
Siku ya Kiyama. Kwani hao wana nyoyo zisio funguka ikaingia Haki ndani
yake. Wana macho yasiyo angalia dalili za kudra. Wana masikio yasiyo sikia
Aya na mawaidha kwa sikio la kuzingatia na kuwaidhika! Hao ni kama wanyama
kwa kutonafiika kwa neema ya akili za kuzingatia walizo neemeshwa na Mwenyezi
Mungu. Bali hao ni wapotovu zaidi kuliko wanyama, kwani wanyama hutaka
cha kuwafaa na hukimbia cha kuwadhuru. Lakini hawa watu hata hawatambui
hayo. Hao ndio walio fikia ukomo wa kughafilika.
Rudi kwenye Sura
180. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye Majina yenye kuonyesha
sifa za ukamilifu. Basi mtumilieni hayo mnapo muomba, au mnapo mwita au
kumtaja. Na waepukeni hao wanao mili katika hayo yasiyo elekeana
na dhati ya utukufu wake. Hao watakuja lipwa malipo ya vitendo vyao.
Rudi kwenye Sura
181. Na katika tulio wajaalia waingie Peponi wapo wanao waita wengineo
kwenye Haki kwa kuipenda Haki, na kwa Haki tu wanafanya uadilifu katika
hukumu zao.
Rudi kwenye Sura
182. Na wale walio zikanusha Ishara (Aya) zetu zilio teremshwa tutawapururia
pole pole, na tutawawacha mpaka wafike ukomo watapo fika. Na hayo ni kwa
kuwapururia neema juu yao, juu ya kushughulika kwao katika maasi, mpaka
maangamizo yawazukie nao wameghafilika wakitaladhadhi na starehe zao.
Rudi kwenye Sura
183. Nitawakunjulia maisha, bila ya kuyapuuza maovu yao. Na mipango
yangu niliyo wapangia ni ya nguvu na mikali juu yao, inalingana na madhambi
yao yaliyo zidi kwa kupita kiasi.
Rudi kwenye Sura
184. Wao wameanza kwa kukadhibisha, wala hawakuzingatia yale anayo
waitia kwayo Mtume, na hoja anazo zitoa. Bali wakamsingizia kuwa ni mwendaazimu,
na hali hana wazimu chochote. Yeye huyu ni mwenye kuwaonya wasifikiwe na
adhabu ya ushirikina wao. Na onyo lake liwazi, la dhaahiri.
Rudi kwenye Sura
185. Wamemwambia Muhammad mwongo kwa Tawhidi anayo waitia, wala hawakutazama
kwa kuzingatia na kutafuta dalili za ufalme mtukufu wa Mwenyezi Mungu ulioko
katika mbingu na ardhi na viliomo ndani yao, zinazo onyesha ukamilifu wa
uwezo wa huyu Mwenye kuunda, na zinazo onyesha Umoja wake wa pekee. Wala
hawakufikiri kuwa ajali yao imekwisha karibia, au huenda ikawa imekaribia,
wapate kufanya haraka kutupia nadhari na kuitafuta Haki kabla ya kuzuka
ajali. Ikiwa basi watu hawa hawaamini maneno ya Qur'ani watakuja amini
maneno gani baada yake
Rudi kwenye Sura
186. Aliye andikiwa na Mwenyezi Mungu kupotea kwa uwovu wa uchaguzi
wake mwenyewe, basi hapana mtu wa kumhidi. Na Yeye Subhana, Aliye takasika,
anawaacha watu kama hao wakihangaika wala hawaitambui njia.
Rudi kwenye Sura
187. Ewe Muhammad! Mayahudi wanakuuliza khabari ya Saa itakayo malizikia
dunia. Itakuwa wakati gani, kujuulikana khasa? Waambie: Ujuzi wa wakati
wake uko kwa Mwenyewe Mola wangu Mlezi peke yake. Haujui wakati wake mtu
yeyote isipo kuwa Yeye. Itapo tokea kitisho chake kitakuwa kikuu kwa walioko
mbinguni na ardhini! Wao wanakuuliza suala hili kama kwamba wewe una pupa
ya kuijua! Basi wakaririe jawabu, na uwambie kwa kutia mkazo: Hakika kuijua
hiyo Saa kuko kwa Mwenyezi Mungu, lakini aghlabu ya watu hawatambui hakika
ya wasiyo yaona au wanayo yaona!
Rudi kwenye Sura
188. Waambie: Mimi siimilikii nafsi yangu kujiletea nafuu, wala kujikinga
na madhara, ila Mwenyezi Mungu akipenda hayo. Hapo ndio hunipa mamlaka.
Na lau kuwa mimi najua yale yaliyo fichikana kwangu, kama mnavyo dhani,
basi ningeli kithirisha kila kheri, kwa kuwa ninajua sababu zake. Na ninge
ilinda nafsi yangu na kila ovu, kwa kuyaepuka yanayo leta madhara. Mimi
si chochote ila ni mwonyaji wa adhabu, na mbashiri wa thawabu, kwa kaumu
wanayo iamini Haki na wanait'ii.
Rudi kwenye Sura
189. Yeye ndiye Allah, Mwenyezi Mungu, aliye kuumbeni hapo mwanzo
kwa nafsi moja. Na akajaalia katika nafsi ile ile mwenzie, na vizazi vyao
vikaendelea kuwepo. Nanyi mlikuwa mume na mke. Basi alipo muingilia akachukua
mzigo mwepesi, nayo ndio mimba changa, inapo kuwa kama pande la damu na
pande la nyama. Mimba ikiwa nzito katika tumbo lake huyo mke, mume na mke
humwomba Mola wao Mlezi wakisema: Wallahi, ukitupa mwana mzima asiye na
ila katika umbo lake, tutakushukuru kwa neema yako.
Rudi kwenye Sura
190. Akisha wapa wakitakacho, huwafanya masanamu ndio washirika wa
Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ile zawadi yake ya ukarimu, kwa kuyatambikia
kama kwamba ndio wanayashukuru. Na Mwenyezi Mungu pekee ndiye anaye stahiki
kushukuriwa. Yeye ametukuka, hawezi kuwa kama hiyo miungu yao ya kishirikina.
Rudi kwenye Sura
191. Jee, inawafalia kumshirikisha Mwenyezi Mungu na masanamu yasio
weza kuumba kitu, bali hayo yameumbwa na Mwenyezi Mungu?
Rudi kwenye Sura
192. Wala hayawezi kuwasaidia hao wanayo yaabudu, wala hayajisaidii
wenyewe akitokea mtu kuyashambulia.
Rudi kwenye Sura
193. Na nyinyi mnao yaabudu masanamu! Mkiyaomba hayo masanamu yakuongozeni
mpate mnacho kipenda hayakuitikieni hayo myatakayo! Ni sawa sawa kwenu
kuwa hapana faida ya kuwaomba au mkinyamaza. Hali yao haibadiliki vyo vyote
vile.
Rudi kwenye Sura
194. Hakika hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, na mkataraji
nafuu kwao, wao wenyewe wanamnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa hukumu ya maumbile
yao. Kwani Yeye Mwenyezi Mungu amewafanya wafuate amri yake mfano wenu
nyinyi. Kama nyinyi mnasema kweli katika madai yenu kuwa hao wanaweza lolote,
basi watakeni, na wao wakutimilizieni.
Rudi kwenye Sura
195. Bali haya masanamu ni duni kuliko nyinyi kwa kuumbwa na kuwa!
Kwani wao wana miguu ya kuendea? Au wana mikono ya kukinga madhara yasikupateni
au yasiwapate wenyewe? Au wana macho ya kuonea? Au masikio ya kusikia hayo
mnayo yataka wakakupeni? Hawana chochote katika hayo! Vipi basi mnawashirikisha
hao na Mwenyezi Mungu? Na ikiwa nyinyi mnadhani kuwa hio miungu ya uwongo
inaweza kunidhuru mimi au mtu yeyote, basi iiteni, na mfanye njama
zenu pamoja nao kama mtakavyo, bila ya kunipa muhula wala kungoja.
Hao hakika hawawezi kitu! Basi msiningojee, na wala mimi siwabali.
Rudi kwenye Sura
196. Hakika msaidizi wangu wa kuninusuru nanyi ni Yeye Mwenyezi Mungu.
Ulinzi wangu uko kwake. Naye ndiye aliye niteremshia Qur'ani. Na Yeye peke
yake ndiye anaye wanusuru waja wake walio wema.
Rudi kwenye Sura
197. Na hayo masanamu mnayo taka kwao msaada, badala ya Mwenyezi
Mungu, hayawezi kukusaidieni nyinyi, wala kujisaidia wenyewe.
Rudi kwenye Sura
198. Na ukiwataka uwongofu katika yaliyo na kheri nanyi hawalisikii
ombi lenu, licha ya kukuongozeni! Unawaona wanavyo kukabili kama kwamba
wanakutazama, na kumbe wao kwa hakika hawaoni kitu!
Rudi kwenye Sura
199. Ewe Nabii! Waachilie mbali hao majaahili, na endelea katika
njia ya Da'wa (Wito). Na wachukulie watu kwa lilio wepesi kwao. Na waamrishe
kila jambo linalo pendeza na kuingia akilini.
Rudi kwenye Sura
200. Na Shetani akikuchochea kwa wasiwasi ili apate kukuachisha ulio
amrishwa, kama vile kukasirika kwa kukushikilia kwao mambo ya shari, basi
omba ulinzi wa Mwenyezi Mungu akuepushe naye huyo Shetani. Kwani Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusikia na kujua kila linalo tokea.
Rudi kwenye Sura
201. Hakika wale wamchao Mola wao Mlezi, na wakaweka baina yao na
maasi kinga cha kuzuia uchochezi wa Shetani unao wapitia kuwaachisha yaliyo
waajibu wao, hukumbuka uadui wa Shetani na vitimbi vyake. Kwa hivyo hao
wanaiona Haki, basi ndio wanarejea.
Rudi kwenye Sura
202. Na ndugu zao mashetani, nao ni hao makafiri, mashetani huwazidisha
upotovu kwa kuwajaza wasiwasi. Tena hawa makafiri hawaachi upotovu wao
wakazingatia.
Rudi kwenye Sura
203. Na usipo waletea makafiri Ishara wanayo itaka kwa inadi na ukafiri,
husema: Kwa nini hukuitaka? (au hukuizua? Makusudio yao ni kuwa Mtume s.a.w.
akizibuni Aya zote.) Waambie: Mimi sifuati ila Qur'ani ninayo funuliwa
kwa wahyi kutoka kwa Mola wangu Mlezi. Na waambie: Hii Qur'ani ni hoja
zinazo toka kwa Mola Mlezi wenu kukuonyesheni njia za Haki. Nayo ina uwongofu,
na rehema, kwa Waumini, kwa sababu wao wanaifuata kwa vitendo.
Rudi kwenye Sura
204. Enyi Waumini! Mkisomewa Qur'ani isikilizeni kwa masikio yenu,
mpate kuzingatia mawaidha yake, na msikilize vizuri mpate kuipata rehema.
Rudi kwenye Sura
205. Na mtaje Mola wako Mlezi ndani ya nafsi yako, upate kuhisi kuwa
upo karibu na Mwenyezi Mungu, kwa kumnyenyekea na kumkhofu, bila ya kupiga
makelele, bali juu kidogo kuliko kwa siri, na chini ya kudhihirisha kwa
maneno. Na umtaje na umkumbuke asubuhi na jioni, ili uanzie mchana wako
kwa kumkumbuka Mola wako Mlezi, na ukhitimishie kwayo vile vile. Na wakati
wako wote usighafilike na kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
206. Hao walio karibu na Mola wako Mlezi kwa utukufu na takrimu hawatakabari
wakaacha kumuabudu. Na wanamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisio faa kwake.
Na wanamnyenyekea Yeye.
Rudi kwenye Sura