1. Anaye stahiki sifa njema ni Mwenyezi Mungu peke yake.
Yeye ndiye aliye zifanya mbingu na ardhi zikawa bila ya kuwapo ruwaza ya
kuigia mfano wake. Naye ndiye aliye wajaalia Malaika kuwa ni wajumbe kuwatuma
kwa viumbe vyake. Wao hao wana mbawa za idadi mbali mbali, mbili-mbili,
tatu-tatu, na nne-nne. Yeye huzidisha katika kuumba kwake kama atakavyo
kuzidisha. Hashindwi na kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ana uweza mkubwa juu
ya kila kitu.
Rudi kwenye Sura
2. Mwenyezi Mungu akipeleka rehema kwa watu, rehema yoyote ile iwayo,
ikiwa ni mvua, au neema, au amani, au hikima - hapana mtu yeyote awezaye
kuwazuilia na kuwanyima. Na chochote katika hivyo akikizuilia Yeye basi
hapana mmoja awezaye kukifungulia isipo kuwa Yeye Mwenyewe. Na Yeye ndiye
Mwenye kushinda ambaye hashindwi. Mwenye hikima asiye kosea.
Rudi kwenye Sura
3. Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu, kwa
kuzishukuru na kutimiza haki yake. Na mkiri hayo yaliyo tokea ndani ya
nafsi zenu, ya kwamba hapana muumba isipo kuwa Mwenyezi Mungu ambaye anakuruzukuni
kutoka mbinguni kwa zinavyo viteremsha, na kutoka kwenye ardhi kwa vinavyo
toka humo, ambavyo vinakuleteeni uhai wenu. Hapana mungu isipo kuwa Yeye
anaye waruzuku waja wake. Basi yawaje mnavyo geuzwa mkaacha Tawhidi ya
Muumba wenu na Mwenye kukuruzukuni mkaendea kumshirikisha katika ibada
yake?
Rudi kwenye Sura
4. Na hao makafiri wa kaumu yako wakikukadhabisha kwa uwongofu ulio
waletea, basi wewe wastahamilie. Kwani Mitume wa kabla yako walikwisha
kadhibishwa vile vile, na wakavumilia kwa walivyo kadhibishwa mpaka wakashinda.
Na mambo yote yatarejea kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Rudi kwenye Sura
5. Enyi watu! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu, juu ya mambo ya kufufuliwa,
na malipo, na ushindi, ni haki ya kweli. Basi msiache dunia ikakukhadaini
na Akhera. Wala Shetani akakukhadaini mkaacha kuwafuata Mitume, na akakupeni
tamaa kuwa mtasamehewa na hali huku mnaendelea na maasi.
Rudi kwenye Sura
6. Hakika Shetani ni adui yenu wa kale, msikhadaike kwa ahadi zake.
Nanyi mchukulieni kuwa ni adui yenu. Kwani hakika yeye anawaita wafwasi
wake wapate kuwa watu wa Moto uwakao kwa nguvu, na wala hawaitii kwa jenginelo.
Rudi kwenye Sura
7. Wanao mkufuru Mwenyezi Mungu na Mitume wake watapata adhabu kali.
Na wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wakatenda mema watapewa
kutokana na Mwenyezi Mungu kusamehewa madhambi yao, na ujira mkubwa kwa
vitendo vyao.
Rudi kwenye Sura
8. Wamekuwa hawatambui? Je! Yule ambaye Shetani kampambia vitendo
vyake viovu na mwenyewe akaona ni vizuri, ni kama aliye hidika kwa uwongofu
wa Mwenyezi Mungu na akaliona jema kuwa ni jema, na uovu akauona kuwa ni
uovu? Kwani hakika Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye katika wanao
khiari njia ya upotovu, wakaiona ndiyo njia ya kuifuata. Na humhidi amtakaye
miongoni mwa walio ikhiari njia ya hidaya kuwa ndiyo njia ya kuifuata.
Basi usiihiliki nafsi yako kwa kuwasikitikia wapotovu na kuwaonea huruma.
Hakika Mwenyezi Mungu anajua uovu wautendao, naye atawalipa kwa hayo.
Rudi kwenye Sura
9. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anaye zituma pepo ziyatimue
mawingu yaliyo rindika kwa mvuke wa maji. Tena tukayasukuma hayo mawingu
mpaka kwenye nchi yenye ukame, tukaihuisha ardhi yake baada ya kuwa ilikuwa
imekufa. Kama tunavyo itoa mimea katika ardhi, basi hali kadhaalika tutawatoa
maiti makaburini Siku ya Kiyama.
Rejea maoni ya ki-ilimu juu ya Aya 57 katika Surat Al Aa'raaf.
Rudi kwenye Sura
10. Mwenye kutaka utukufu na nguvu na akazitafute kwa kumt'ii Mwenyezi
Mungu. Kwani Yeye ndiye Mwenye nguvu zote. Kumwendea Yeye ndio linapanda
neno jema. Na Mwenyezi Mungu huinyanyua a'mali njema na akaipokea. Na wale
wanao wapangia Waumini vitimbi vya kuwadhuru watapata adhabu iliyo kali.
Na hizo njama zao zitafisidika, hazito leta hayo waliyo yakusudia, wala
hazileti natija yoyote.
Rudi kwenye Sura
11. Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na udongo. Kwani ndivyo
hivyo alivyo muumba baba yenu Adam. Kisha akakuumbeni kutokana na tone
ya manii, nayo ni maji yanayo miminwa katika tumbo la uzazi, nayo pia ni
katika chakula kinacho toka kwenye udongo. Kisha akakufanyeni waume na
wake. Wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai ila kwa ujuzi wa Mwenyezi
Mungu Mtukufu. Wala hauongezwi umri wa mtu yeyote, wala haupunguzwi ila
husajiliwa katika Kitabu. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni sahali, mepesi.
Rudi kwenye Sura
12. Na haziwi sawa bahari mbili katika ujuzi wetu na makadirio yetu,
ijapo kuwa zinashirikiana katika baadhi ya manufaa yao. Haya maji matamu
yanakata kiu kwa uzuri wake, na utamu wake, na wepesi wake kuyanywa. Na
haya mengine ni maji ya chumvi, uchumvi wake mkali. Na kutokana na namna
zote mbili mnakula nyama mpya (fresh, haikuchacha) nayo ni samaki mnao
wavua. Na mnatoa kutoka maji ya chumvi mapambo mnayo yavaa, kama lulu na
marijani. Na wewe, mwenye kutazama, unaona vipi vyombo vya baharini vinavyo
kwenda, vikipasua maji kwa mwendo wake, ili mkatafute baadhi ya fadhila
za Mwenyezi Mungu kwa kufanya biashara, na ili asaa mpate kumshukuru Mola
wenu Mlezi kwa neema hizi.
Na katika Ishara za Mwenyezi Mungu ambazo anawaitia watu wazizingatie
na ambazo amewaneemesha fadhila zake ni mwendo wa marikebu na kukata kwake
maji baharini kwa mujibu wa kawaida zake alizo ziwekea katika tabia za
maumbile, nazo ni hizo sharia za vitu kuelea, (The law of boayancy). Ni
maarufu kuwa baadhi ya mapambo yanapatikana kutoka maji ya chumvi, na baadhi
ya watu labda wanaona haiwi maji matamu kutoa mapambo vile vile. Lakini
ilimu na mambo yalivyo yamethibitisha kinyume cha hivyo. Ama lulu kama
zinavyo patikana katika maji ya chumvi, basi vile vile zinapatikana kwenye
namna fulani nyengine za chaza wa mitoni. Hupatikana lulu katika maji matamu
katika Uingereza, Scotland, Wales. Czechoslovakia na Japan.. n.k. mbali
na lulu za baharini maarufu. Na pia vinaingia katika vinavyo patikana katika
maji matamu maadini thamini ngumu kama almasi, zinazo patikana katika udongo
unao tupwa na mito. Hupatikana pia Yaakuti, katika mito ya Mojok karibu
na Andalas katika Burma ya juu. Ama katika Siam (Thailand) na Sri Lanka
hupatikana Yaakuti katika mito. Na katika mawe ambayo yashabihiana na ya
ghali na hutumiwa kwa pambo ni Topaz. Na hupatikana pia kwenye mito
mwahali mwingi katika Brazil na Urusi (Ural na Siberia) Fluro-sylicate
of aluminium. Aghlabu hiyo huwa ya manjano au rangi ya kahawia. Circom
ni jiwe thamini linavutia. Sifa zake zinakaribia za Almasi. Namna zake
nyingi hupatikana kwenye mito. (Kadhaalika dhahabu, ambayo inaitwa Alluvial
gold yaani dhahabu ya mtoni, hupatikana nchi nyingi, mojawapo ni Zaire.)
Rudi kwenye Sura
13. Yeye huuingiza usiku katika mchana, na mchana katika usiku. Matokeo
yake ni kuwa saa zao hurefuka na hufupika kwa mujibu wa mipango ya hikima
miaka nenda miaka rudi. Na Yeye amelifanya jua na mwezi kutumika kwa manufaa
yenu. Kila kimojapo kinakwenda kwa muda maalumu utao ishia kwake. Huyo
mwenye shani kuu ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye kuyapanga mambo yenu. Ufalme
ni wake Yeye peke yake. Na hao wengineo mnao waomba kuwa ni miungu mnao
waabudu hawawezi kumiliki hata ugozi mwembamba ule wa kokwa ya tende. Basi
inakuwaje wastahili kuabudiwa?
Aya hii tukufu inaonyesha kuwa jua lina muda utakao kwisha baadae.
Na huenda kuwa huo ndio utao kuwa Mwisho kwa mujibu wasemavyo wataalamu
wa ilimu ya Falaki (Astronomy) kwamba jua linaunguza kuni zake za Dharra
(Nuclear fuel) nayo ni Hydrogen inayo geuka kuwa Helium. Huenda kuwa
ukisha muda wa jua ndio Msiba Mkuu wa Ulimwengu wote.
Rudi kwenye Sura
14. Mkiwaomba hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawasikii
maombi yenu. Na hata ingeli kuwa wanasikia wasingeli kujibuni kitu chochote
kwa hayo myatakayo. Na Siku ya Kiyama watakuja kukataa huo ushirikina wenu
kuwashirikisha na Mwenyezi Mungu. Wala hapana wa kukupeni khabari za hali
za Akhera kuliko huyo Mwenye kuzijua vyema kwa ujuzi wa ndani kabisa.
Rudi kwenye Sura
15. Enyi watu! Nyinyi ndio mnao mhitajia Mwenyezi Mungu kwa kila
kitu. Na Yeye Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kujitosha, hawahitajii
viumbe vyake. Na Yeye ndiye Mwenye kustahiki kusifiwa kwa kila hali
Rudi kwenye Sura
16. Mwenyezi Mungu akitaka kukuteketezeni, basi atakuteketezeni kwa
utimilivu wa uweza wake. Na alete uumbaji mpya utao ridhiana na hikima
yake.
Rudi kwenye Sura
17. Wala kukuhilikini nyinyi na kuwaleta wenginewe si muhali kwa
Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
18. Wala nafsi yenye dhambi haitobeba dhambi za mwenginewe. Na mtu
aliye kuwa taabani kwa mzigo wake wa madhambi, akimwomba mwenginewe amchukulie,
huyo mwengine hatomchukulia hata kidogo, hata angeli kuwa ni jamaa yake.
Haya ni kwa kuwa kila mtu kashughulika na yake. Na ewe Nabii! Usihuzunike
kwa inadi ya watu wako. Kwani hakika maonyo yako yanawafaa wale ambao wanamkhofu
Mola wao Mlezi peke yao katika siri, na wakashika Sala kwa mujibu inavyo
faa. Na mwenye kujisafisha na uchafu wa madhambi, basi anajisafisha kwa
faida ya nafsi yake. Na marejeo yote mwishoni ni kwa Mwenyezi Mungu, na
Yeye atamtendea kila mtu kwa anavyo stahiki.
Rejea maoni ya ki-ilimu juu ya Aya 7 Surat Azzumar: Na mbebaji habebi
mzigo wa mwengine.
Rudi kwenye Sura
19,20,21. Hawawezi kulingana wakawa sawa:- asiye hidika kuifuata
Haki kwa ujinga wake na mwenye kufuata Njia ya uwongofu kwa ujuzi wake;
wala uwongo na kweli; wala kivuli na upepo umoto
Rudi kwenye Sura
22. Wala hawawezi kuwa sawa walio hai kwa kukubali Imani, na maiti ambao
hawahisi kitu na nyoyo zao zimefungika na kuweza kusikia yaliyo kweli. Hakika Mwenyezi Mungu humhidi amtakaye asikie hoja kwa sikio la kukubali. Wala wewe, ewe Nabii, si mwenye kuwasikilizisha walio kufa kwa inadi yao na ukafiri wao, kama ilivyo kuwa huwasikilizishi walio makaburini.
Rudi kwenye Sura
23. Wewe huna jukumu ila la kufikisha Ujumbe na kuonya tu.
Rudi kwenye Sura
24. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma wewe uwafikishie watu wote
hii Dini ya Haki, ukiwabashiria Pepo wenye kuamini, na ukiwaonya kwa adhabu
ya Moto wanao ikataa hii Dini. Na hapana kaumu yoyote katika kaumu zilizo
pita ila walijiwa na mtu kutokana na Mwenyezi Mungu wa kuwahadharisha na
adhabu yake.
Rudi kwenye Sura
25. Na ikiwa kaumu yako wanakukadhibisha wewe basi walio kuwa kabla
yao waliwakadhibisha Mitume wao vile vile. Na wao waliwaletea miujiza iliyo
wazi, na Maandiko ya Mola Mlezi na Kitabu chenye nuru kwa ajili ya
kuwaongoza Njia ya kuokoka duniani na Akhera.
Rudi kwenye Sura
26. Kisha nikawashika walio kufuru kwa mshiko mkali. Basi hebu angalia
kulikuwaje kuchukia kwangu kwa vitendo vyao, na ghadhabu yangu juu yao!
Rudi kwenye Sura
27. Ewe mwenye akili! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu anayateremsha maji
kutoka mbinguni, na kwa maji hayo anatoa mazao yanayo khitalifiana rangi
zake? Mengine ni mekundu na manjano, na matamu na machungu, mazuri na mabaya.
Na katika milima, ipo milima yenye njia na mistari myeupe na myekundu,
yenye kukhitalifiana pia kwa kukoza na kufifia.
Ya kustaajabisha kitaalamu katika Aya hii tukufu sio tu kwa kukhitalifiana
rangi mbali mbali katika milima, ambazo zinatokana na hizo sehemu za maadini
zilizo fanya majabali, kama vile chuma huonyesha rangi yake nyekundu, na
manganese na makaa ya mawe huonekana kwa rangi nyeusi, au shaba ambayo
hudhihirisha rangi ya kijani n.k. Lakini ya kustaajabisha khasa ni kuunganisha
baina ya kutoa matunda ya namna mbali mbali na hali miti yake inanyweshwa
maji yale yale, na kuumbwa milima myekundu, na myeupe, na myeusi,
na yote yana asli moja kwa kuundwa kwake. Wataalamu wa ilimu za t'abaka
za ardhi, Jiolojia, wanaita Magma. Na hii Magma moja inapo chomoza pahala
mbali mbali katika ardhi, na penye vina mbali mbali (kwenda chini) katika
ardhi kutoka juu basi hupatikana khitilafu katika muundo wake na hukusanyika
kwa kurindika kuwa ni milima yenye maadini ya rangi mbali mbali. Na huu
basi mwendo wa Mwenyezi Mungu ni mmoja. Kwani hakika asli ni moja, na matawi
ndiyo yanakhitalifiana kwa kuonekana. Na katika haya yanapatikana manufaa
na faida kwa binaadamu.
Rudi kwenye Sura
28. Na miongoni mwa watu na wanyama, na mifugo, yaani ngamia, ng'ombe,
kondoo na mbuzi, kadhaalika zipo khitilafu katika sura, ukubwa na rangi.
Na hawazingatii huu muumbo wa ajabu na wakamwogopa aliye umba ila wanazuoni
ambao wanatambua siri ya uumbaji wake. Hakika Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda
anaogopwa na Waumini, naye ni Mwingi wa kuwafutia madhambi yao wanao rejea
kwake.
Baada ya kueleza kukhitalifiana matunda, na milima, na watu, na
wanyama, na mifugo, inaashiriwa kuwa juu ya khitilafu hizi zinazo onekana
baina ya hali hizi zote, upo umoja wa asli. Kwani hayo matunda yanatokana
na maji yale yale. Na milima inatokana na Magma moja. Kadhaalika khitilafu
za rangi, na watu, na wanyama, na mifugo, hazidhihiri katika tone za manii
ambavyo vyote hivyo vimetoka mwanzo wake. Na lau hizo tone zingeli chunguzwa
kwa darubini ya Maikroskopu kisingeli onekana kitu cha kuonyesha hizo khitilafu
zitazo kuwa. Kwani hizo ni siri zilioko ndani yake katika zinazo itwa Genes
(Jiinz). Na labda haya pia yanaonyesha kuwa sifa za kurithi ziliomo katika
asli ya mimea, na wanyama, na binaadamu, zinalindwa katika maumbile yake,
na hazigeuki kwa tabia ya pahala au chakula.
Rudi kwenye Sura
29. Hakika wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kwa kukizingatia
na kukitenda, na wakashika Sala kwa mujibu itakikanavyo na wakatoa kwa
siri na kwa kuonekana baadhi ya alicho waruzuku Mwenyezi Mungu, wanataraji
kwa hayo kufanya na Mwenyezi Mungu biashara isiyo anguka faida yake.
Rudi kwenye Sura
30. Ili Mwenyezi Mungu awalipe ujira wao, na awazidishie juu yake
kutokana na fadhila yake kwa anavyo waongezea mema yao na kuwafutia maovu
yao. Yeye ni Msamehevu, Mwingi wa kufutia makosa ya kujikwaa, Mwenye kushukuru,
Mwingi wa kushukuru kwa ut'iifu wa waja.
Rudi kwenye Sura
31. Na tuliyo kuletea Wahyi wewe katika hii Qur'ani ni Haki tupu
isiyo kuwa na shaka yoyote. Tumeiteremsha kuthibitisha Vitabu vilivyo teremshwa
kwa Mitume walio kuwa kabla yako, kwa kuwa vyote ni asli moja. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mkunjufu wa kujua na kuona kwa waja wake.
Rudi kwenye Sura
32. Tena tumekifanya Kitabu hichi ni mirathi ya kurithiwa na waja
wetu tulio wateuwa. Basi kati yao yupo aliye jidhulumu nafsi yake kwa kuzidi
maovu yake kuliko mema yake; na yupo wa kiasi, hakupita mpaka katika maovu
yake na wala hakukithirisha mema yake; na miongoni mwao yupo aliye washinda
wenginewe kwa kufanya mambo ya kheri, kwa kusahilishiwa na Mwenyezi Mungu.
Huko kushinda katika mambo ya kheri ndio kufuzu kukubwa mbele ya Mwenyezi
Mungu.
Rudi kwenye Sura
33. Malipo yao Akhera ni Mabustani ya daima watayo yaingia. Humo
watajipamba kwa vikuku vya dhahabu na lulu. Na nguo zao za Peponi ni hariri.
Rudi kwenye Sura
34. Na watasema wakisha ingia: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu aliye
tuondolea ya kutuhuzunisha. Hakika Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa maghfira,
Mwingi wa shukra.
Rudi kwenye Sura
35. Aliye tuweka kwenye Nyumba ya neema ya milele kwa fadhila zake
hatupi taabu humo, wala hatuletei machofu.
Rudi kwenye Sura
36. Na walio kufuru malipo yao waliyo ahidiwa ni Moto wa Jahannamu
watakao uingia. Mwenyezi Mungu hatawahukumia mauti wakafa, wala hawatapunguziwa
chembe ya adhabu wakapumzika. Ni kama hivyo tunavyo mlipa kila mwenye kuendelea
katika ukafiri na akaushikilia.
Rudi kwenye Sura
37. Na humo watapiga makelele kuomba msaada wakisema: Mola wetu Mlezi!
Tutoe humu Motoni, tupate kutenda mema siyo yale tuliyo kuwa tukiyatenda
duniani. Atawaambia: Hatukukupeni fursa ya kufanya a'mali, tukaufanya
mrefu umri wenu kwa muda unao mkinika mtu ndani yake kuzingatia kwa mwenye
kuzingatia? Na akukujieni Mtume akakuhadharisheni na adhabu hii. Basi onjeni
katika Jahannamu malipo ya udhalimu wenu. Kwani mwenye kudhulumu hapati
wa kumnusuru wala kumsaidia.
Rudi kwenye Sura
38. Hakika Mwenyezi Mungu anajua vyema kila kilicho fichikana katika
mbingu na ardhi. Hapana chenye kufichikana kwake. Na lau ange kukubalieni
akakurudisheni duniani mngeli rejea yale yale aliyo kukatazeni. Hakika
Yeye Mtukufu anavijua vyema vishawishi na vivutio viliomo ndani ya vifua.
Rudi kwenye Sura
39. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kufanyeni baadhi yenu wawafuatie wengine
katika kuiamirisha dunia na kuifanya itoe matunda yake. Na Yeye ni Mwenye
kustahiki kushukuriwa si kukufuriwa. Basi mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu
dhambi za kufuru yake zitakuwa juu yake mwenyewe. Na makafiri hawatopata
ziada yoyote kwa Mola wao Mlezi isipo kuwa chuki na kukasirika. Wala makafiri
hawatazidi ila kupata khasara tu.
Rudi kwenye Sura
40. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Hebu nambieni, mmeiona hali ya
hawa miungu wenu wa kishirikina mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu?
Hebu nambieni, sehemu gani katika ardhi waliyo iumba wao? Hebu wanao ushirika
wowote na Mwenyezi Mungu katika kuziumba mbingu? Sisi hatukuwapa kitabu
cha ushirikina wakawa wao wanatoa hoja kutoka humo. Lakini wenye kudhulumu
hawaahidiani wenyewe kwa wenyewe kwa uombezi wa miungu yao ya kumshirikisha
na Mwenyezi Mungu ila kwa uwongo na kupambia pambia kuso mdanganya mtu
ila aliye kuwa akili yake ni dhaifu.
Rudi kwenye Sura
41. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye zuia mpango wa mbingu na ardhi
usivurugike, na ndiye anaye zihifadhi mbingu na ardhi zisiondoke. Na lau
akizijaalia kuondoka hapana wa kuweza kuzihifadhi hizo isipo kuwa Mwenyezi
Mungu Mwenyewe. Hakika Yeye ni Mpole, hafanyi papara kuwaadhibu wakhalifu.
Yeye ni Msamehevu wa madhambi ya wenye kurejea kwake wakatubu.
Aya hii tukufu inathibitisha kwamba Mwenyezi Mungu Subhanahu wa
Taa'la peke yake ndiye Muumba mbingu na ardhi. Yeye ndiye Mwenye kuzishika
zisiondoke. Kwani hivi vitu viliomo mbinguni vya karibu na mbali vinavyo
onekana katika qubba la mbingu vimeshikamana kwa mujibu wa mpango maalumu
wa namna ya pekee alio uumba Mwenyezi Mungu Aliye takasika na Kutukuka.
Na Yeye ndiye aliye viwekea mvutano usio katika kwa kupita zama na vizazi,
na ndiye anaye vihifadhi visikosee mizani yao. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu
wa Taala ndiye Mwenye uweza huu, wala hapana mwenginewe.
Rudi kwenye Sura
42. Na makafiri waliapa kwa jina la Mwenyezi Mungu mwisho wa juhudi
yao kutilia nguvu kiapo chao, ya kwamba bila ya shaka akiwajia Mtume kuwaonya
basi wao hapana shaka watakuwa miongoni mwa mataifa walio ongoka zaidi
kuliko hao wenginewe walio wakadhibisha Mitume wao. Lakini alipo wajia
Mtume kutokana na wao wenyewe, akiwaonya, hakuwazidishia kwa kuwaonya kwake
na kuwanasihi, isipo kuwa kuikimbia Haki.
Rudi kwenye Sura
43. Wameikimbia Haki kwa kupandwa na kiburi katika nchi, na kuona
ari kumnyenyeka Mtume na Dini aliyo kuja nayo. Wakapanga njama za vitimbi
viovu. Na ni Shetani ndiye aliye waongoza hata wakaiacha Dini na wakaingia
kumpiga vita Mtume. Na wala madhara ya vitimbivi viovu hayampati mtu ila
yule yule aliye vipanga. Basi watu hao wanangojea nini isipo kuwa
sunna ya Mwenyezi Mungu iliyo wasibu wale walio watangulia? Basi
hutoipata njia ya Mwenyezi Mungu anavyo yafanyia mataifa ibadilike,
kama wanavyo tumai hawa wapangaji vitimbi yawe kinyume na walio watangulia.
Na kabisa hutopata mwendo wa Mwenyezi Mungu ubadilishe njia ulio elekea.
Rudi kwenye Sura
44. Je! hao hukaa na wakakanya tu ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa washirikina,
bila ya wao kusafiri katika ulimwengu wakaangalia kwa macho yao athari
za maangamizo yaliyo wateremkia walio kuwa kabla yao kwa sababu ya kuwakadhibisha
kwao Mitume? Na kabla ya wao yalikuwako mataifa yaliyo kuwa na nguvu kushinda
wao. Nguvu zao hazikuweza kuzuia adhabu ya Mwenyezi Mungu. Kwani Yeye hashindwi
na chochote kilioko mbinguni wala katika ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye ilimu
kubwa kabisa, Mwenye uweza mkubwa kabisa.
Rudi kwenye Sura
45. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli kuwa anawaadhibu watu duniani,
basi hapana shaka adhabu yake ingeli enea. Na asingeli muacha juu ya mgongo
wa ardhi hata mnyama mmoja, kwa kuwa wote wametenda madhambi. Lakini anaakhirisha
kuwaadhibu mpaka siku maalumu, nayo ni Siku ya Kiyama. Basi ukifika muda
wao walio wekewa atawalipa kwa uangalizi kaamili. Kwani Yeye ni Mwenye
kuviona vitendo vya waja wake; hafichikiwi na kitu chochote katika hivyo.
Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua kushinda wote.
Rudi kwenye Sura