1. Sifa zote nzuri ni haki ya Mwenyezi Mungu, ambaye
ndiye Mwenye kuumba, na Mwenye kumiliki, na Mwenye kupanga vyote vilioko
mbinguni, na vilioko katika ardhi. Na Yeye peke yake ndiye Mwenye sifa
Akhera, kwa kutamalaki kwake kuliko enea. Naye ndiye Mwenye hikima asiye
kosa, Mwenye khabari zote, hapana asicho kijua siri yake.
Rudi kwenye Sura
2. Anajua kila kinacho ingia katika sehemu za ardhi, kama maji, na
khazina, na vilio zikwa, na sehemu za maiti; na kila kinacho toka, kama
wanyama, na mimea, na maadeni, na maji ya visima, na chemchem. Na anajua
vinavyo teremka kutoka mbinguni, kama Malaika, na Vitabu wanavyo vipokea
Manabii, na mvua, na radi; na anajua vinavyo panda ndani yake na kwendea
huko, kama Malaika, na a'mali za ibada, na roho. Na Yeye ni Mwingi wa rehema,
Mkubwa wa kusamehe.
Rudi kwenye Sura
3. Na wenye kukufuru wakasema: Haitujii Saa iliyo ahidiwa kuwa ni
ya kufufuliwa na kukusanywa watu. Waambie ewe Mtume! Hapana shaka
itakujieni, nami naapa kwa Mola wangu Mlezi, Mwenye kujua ya siri, ambaye
hapana chenye kughibu na ujuzi wake hata ingawa kiasi ya chembe tu, si
katika mbingu wala katika ardhi. Wala kilicho kidogo kuliko chembe, wala
kikubwa kuliko hivyo hakikosi kuandikwa katika Kitabu kilicho timia, chenye
kubainisha kila kitu.
Dharra , tuliyo ifasiri "Chembe", na kisayansi ni Atom kwa
hakika katika lugha ya Kiarabu ni kitu kidogo sana, kama sisimizi
mdogo, au chembe ya vumbi. Na uzito wa Dharra maana yake ni uzani
wake. Na Aya inaonyesha kuwa kipo kilicho kuwa ni kidogo kuliko Dharra.
Na yafaa kutaja hapa kuwa sayansi za sasa zimethibitisha kuwa Dharra, yaani
Atom, imegawika katika sehemu ndogo zaidi nazo ni Nucleus na Electrons.
Na haya haya hayakuthibitika ila katika karne ya ishirini ya kuzaliwa Nabii
Isa.
Rudi kwenye Sura
4. Ili Mwenyezi Mungu awathibitishe walio amini na wakatenda mema
kwa ajili ya nafsi zao na kwa ajili ya watu wengine. Hao Waumini
watendaji watapata kwa Mwenyezi Mungu msamaha wa kuwafutia madhambi yao,
na riziki kunjufu isiyo na masimbulizi ndani yake.
Rudi kwenye Sura
5. Na hao walio zishughulisha nafsi zao kuipiga vita Qur'ani kutaka
kuishinda amri ya Mwenyezi Mungu katika kumsaidia Mtume wake, hao watapata
adhabu katika adhabu za mwisho wa ubaya na uchungu.
Rudi kwenye Sura
6. Na walio neemeshwa na Mwenyezi Mungu kwa kupewa ujuzi kuwa Qur'ani
ulio teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi, yenye ndani yake mambo ya itikadi
na uwongofu, ni Haki isiyo kuwa na shaka yoyote, wanajua kuwa hiyo ndiyo
yenye kuwaongoa watu kwendea Njia ya Mwenyezi Mungu, Mwenye kushinda kila
kitu, Mwenye kustahiki kila sifa njema.
Rudi kwenye Sura
7. Na makafiri waliambiana wenyewe kwa wenyewe, kwa kufanyia kejeli
kufufuliwa: Je! Tukuonyesheni mtu ataye kuambieni kwamba mtapo kwisha kufa,
na viwiliwili vyenu vikagawika mapande mapande kuwa ati mtafufuliwa
tena kwa umbo jipya?
Rudi kwenye Sura
8. Mtu huyu amemzulia uwongo Mwenyezi Mungu kwa kumnasibishia kuwa
atawafufua wafu, au mtu huyu ana wazimu ndio anasema asiyo yajua? Siyo
hayo wayasemayo. Bali ukweli wa mambo ni kuwa hao wasio iamini Akhera wataingia
katika adhabu na upotovu wa kupotelea mbali na Haki.
Rudi kwenye Sura
9. Je! Wamepofuka, hata hawaaoni yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma
yao ya mbinguni na katika ardhi wakaujua uweza wetu wa kutenda tuyatakayo?
Tukitaka ardhi iwameze, tutawazamisha. Au tungeli taka viwaangukie vipande
vya mbingu tuwasage sage tungeli wateremshia. Hakika katika tuliyo yataja
zipo dalili kwa kila mja mwenye kurejea kwa Mola wake Mlezi katika kila
jambo lake.
Rudi kwenye Sura
10. Wallahi! Kwa hakika tulimpa Daudi fadhila kutoka kwetu kwa kumpa
hikima na Kitabu. Na tulisema: Enyi milima! Karirini pamoja naye Tasbihi
kumtakasa Mwenyezi Mungu, pale anapo sabihi yeye. Na Sisi tuliwafanya
ndege pia wamtumikie, nao wawe wakikariri kumtakasa Mwenyezi Mungu. Na
tukakifanya chuma kiwe laini kwake aunde kwa sura atakayo.
Daudi, a.s. ni mmoja wa Manabii wa Wana wa Israili, na mmoja wa
wafalme wao. Aliishi katika zama za baina ya mwaka 1010 na 970 K.K. (yaani
kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s.)
Rudi kwenye Sura
11. Tulimfunulia kumwambia aunde nguo za chuma pana za kujilinda
katika vita na maadui. Naye azifume kwa hikima na ustadi katika kuviunga
viungo vyake. Na tukamwambia yeye na watu wake: Tendeni yatakayo kuleteeni
kheri na maslaha. Hakika Mimi nayaona vyema yote myatendayo, hapana kinacho
niporonyoka nisikione.
Rudi kwenye Sura
12. Na Suleiman tukamfanyia upepo umtumikie. Mwendo wake wakati wa
asubuhi mmoja ni sawa na safari ya dasturi inayo chukua mwezi mzima. Na
mwendo wake wakati wa jioni moja ni kama safari ya kuchukua mwezi. Na tukamyayushia
maadeni ya shaba ikawa inatiririka kwa wingi moja kwa moja. Na tukawafanya
majini wawe wakimtumikia mbele yake kwa amri ya Mola wake Mlezi. Na yeyote
katika majini aliye wacha kut'ii amri ya Suleiman basi tulimwonjesha adhabu
ya Moto unao waka kwa nguvu.
Rudi kwenye Sura
13. Hao majini wakifanya atakacho Suleiman, kama misikiti kwa ajili
ya ibada, na masanamu, na madeste au mabakuli makubwa kama mahodhi ya maji,
na vyombo vya kupikia, yaani masufuria, makubwa yaliyo kaa pale pale
penye mafya yake hayaondoki kwa kuwa ni makubwa mno. Na tukawaambia watu
wa Daudi: Tendeni kazi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu vilivyo. Na ni wachache
miongoni mwa waja wangu ambao wanakumbuka neema zangu wakawa wananishukuru
kwa wingi.
Rudi kwenye Sura
14. Tulipo mhukumia Suleiman mauti, hapana aliye waonyesha majini
kuwa kesha kufa ila kinyama cha ardhi kilicho ila fimbo yake aliyo kuwa
akiiegemea. Alipo anguka majini wakajua kuwa lau kuwa wangeli jua ya ghaibu
wasingeli endelea na ile adhabu ya mashaka ya kuwadhalilisha.
Rudi kwenye Sura
15. Ninaapa: Hakika katika watu wa Sabaa katika makaazi yao ya Yaman
palikuwa na Ishara ya uweza wetu. Zilikuwako bustani mbili zilizo zunguka
nchi yao, kulia na kushoto. Wakaambiwa: Kuleni katika riziki ya Mola wenu
Mlezi, na mshukuru neema zake kwa kuzitumilia inavyo faa. Huu mji wenu
ni mji mzuri, una vivuli na matunda. Na Mola wenu Mlezi ni Mwingi wa maghfira
kwa anaye mshukuru.
Rudi kwenye Sura
16. Lakini wao waliacha kushukuru neema, na wakawa maisha yao ya
kiburi. Tukawafungulia mafuriko ya nguvu yaliyo tokea baada ya kupasuka
kuta za mahodhi, yakateketeza mabustani yao. Tukawabadilishia badala ya
bustani zao mbili zile zenye matunda mazuri, zikawa nyengine mbili zenye
matunda machungu, na miti isiyo kuwa na matunda, na mikunazi kidogo isiyo
toa hamu.
Hili liitwalo "Hodhi" la maji ya mvua kubwa au "Hodhi la Ma`arib"
ni kubwa kuliko mahodhi yote ya Yaman. Hodhi hili linaweza kubadilisha
ardhi kavu ya kiasi ya maili 300 ya mraba ikawa yenye rutba na mashamba.
Na dalili ya hayo ni hizo bustani mbili zilizo tajwa. Wanazuoni wa taarikh
(historia) wanakhitalifiana katika ujenzi wa hilo hodhi kuu. Vile
vile zipo kauli mbali mbali kukhusu kubomoka kwake.
Rudi kwenye Sura
17. Hayo ndiyo malipo tuliyo walipa kwa kufuru zao kuzikufuru neema
na kuto zishukuru. Na kwani Sisi tunamuadhibu kwa adhabu hii kali yeyote
yule ila aliye kuwa mwingi wa kumkufuru Mwenyezi Mungu na fadhila zake?
Rudi kwenye Sura
18. Na tulifanya baina ya maskani yao ya Yaman na baina ya miji mingine
iliyo barikiwa miji mingineyo pia iliyo karibiana inaonana. Na tukafanya
makhusiano baina yao ni kiasi maalumu cha mwendo usio kuwa wa taabu. Na
tukawaambia: Nendeni humo usiku na mchana nanyi mko katika amani.
Rudi kwenye Sura
19. Kwa kutakabari kwa neema, na raha, na amani, walisema: Tuwekee
mbali masafa ya safari zetu, tusisadifu kukuta miji iliyo amirishwa ya
katikati mpaka tufike huko twendako! Mwenyezi Mungu akazifanya ziwe mbali
hizo safari zao. Na wakawa wao wamejidhulumu nafsi zao kwa uasi wao. Tukawafanya
hao ni masimulizi ya watu, na tukawatenganisha mtengano mkubwa. Hakika
katika yaliyo wapata hao yapo mawaidha kwa kila mwenye kusubiri kwa balaa,
mwenye kushukuru kwa apewacho.
Rudi kwenye Sura
20. Na bila ya shaka Iblisi amehakikisha dhana yake juu yao. Nao
wakamfuata yeye isipo kuwa wachache miongoni mwa Waumini.
Rudi kwenye Sura
21. Na wala Iblisi hakuwa na nguvu za kuwafanya wamt'ii na kumnyenyekea;
lakini Mwenyezi Mungu kawafanyia mtihani apate kuwadhihirisha wepi wanao
isadiki Akhera, na wepi wana shaka nayo. Ewe Nabii! Mola wako Mlezi ni
Mwenye kuchungua kila kitu, Mwenye kusimamia kila kitu.
Rudi kwenye Sura
22. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Waombeni hao mnao dai kwa uwongo
kwamba ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu, wakuleteeni manufaa au wakuondoleeni
madhara. Hawakujibuni kitu. Kwani hao hawamiliki hata kiasi ya chembe ya
kitu katika mbingu wala katika ardhi. Wala wao hawana ushirika wowote na
Mwenyezi Mungu katika kuumba au kumiliki. Wala hapana yeyote katika hao
miungu ya uwongo anaye msaidia Mwenyezi Mungu katika kupanga mambo ya viumbe
vyake.
Rudi kwenye Sura
23. Wala maombezi kwa Mwenyezi Mungu hayawafai ila wenye kustahili
makamo ya kuombewa. Mpaka itapo ondoka khofu katika nyoyo zao kwa kutolewa
ruhusa ya kuombewa, hapo watakuwa wakiambiana kwa furaha: Mola wenu Mlezi
kakwambieni nini? Na wengine watajibu kwamba alilo sema ni kauli ya haki,
kwa kutoa ruhusa kuombewa aliye mridhi. Na Yeye peke yake, ndiye Mwenye
Utukufu na Ukubwa. Na Yeye ndiye anaye ruhusu na kumkatalia amtakaye.
Rudi kwenye Sura
24. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Nani anaye kuleteeni riziki kutoka
mbinguni na kwenye ardhi? Watapo kuwa hawajibu kwa inda tu, waambie: Mwenyezi
Mungu peke yake ndiye anaye kuruzukuni kutoka kote kuwili. Je! Ni
sisi Waumini au nyinyi washirikina ndio walio katika moja ya hali mbili,
ya uwongofu au upotofu ulio wazi?
Rudi kwenye Sura
25. Ewe Nabii! Waambie: Nyinyi hamuulizwi khabari ya madhambi tuliyo
yafanya sisi; wala sisi hatuulizwi khabari ya vitendo vyenu.
Rudi kwenye Sura
26. Waambie: Mola wetu Mlezi atatukusanya Siku ya Kiyama, kisha atatuhukumu
kwa haki. Na Yeye Subhanahu ndiye Hakimu wa kila shauri, Mwenye kujua kwa
hakika yetu sisi na yenu nyinyi.
Rudi kwenye Sura
27. Waambie: Nionyesheni hao mlio waunganisha na Mwenyezi Mungu kwa
kustahiki kuabudiwa, mnao dai kuwa ni miungu wa shirika na Yeye. Yeye hana
mshirika, bali Yeye ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye
hikima katika kupanga kwake na kuendesha kwake.
Rudi kwenye Sura
28. Na Sisi hatukukutuma ewe Muhammad, ila kwa watu wote. Uwe ni
mwenye kuwabashiria Waumini kuwa watapata kheri, na mwenye kuwaonya makafiri
kuwa watapata shari. Lakini aghlabu ya watu hawaujui ukweli wako, wala
kuwa Utume wako ni wa kwa watu wote. (Haya ni kwa sababu hapana Mtume aliye
kuja kwa watu wote ila huyu Nabii Muhammad s.a.w. Nabii Musa alikuja kwa
Wana wa Israili kuwatoa Misri. Nabii Isa, Yesu Kristo, pia kaja kwa Wana
wa Israili tu, kama isemavyo Qur'ani 3.49, na Injili ya Mathayo 10.5-6
Yesu alipo sema: "Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa
nyumba ya Israeli." Na 15.24 alipo sema: "Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea
wa nyumba ya Israeli." Na Injili ya Yohana 17.9)
Rudi kwenye Sura
29. Na makafiri wanasema kwa kuifanya haiwi hiyo Siku iliyo ahidiwa
kwa ajili ya malipo: Lini itakuwa ahadi hii tuingie Motoni, na nyinyi muingie
Peponi, kama nyinyi ni wakweli kwa hiyo ahadi yenu?
Rudi kwenye Sura
30. Ewe Nabii! Waambie: Miadi yenu ni Siku kubwa mno; ikifika hamto
chelewa hata kwa saa moja, wala hamto tangulia.
Rudi kwenye Sura
31. Na walio kufuru wanasema: Hatuisadiki Qur'ani hii wala hivyo
Vitabu vilivyo tangulia kabla yake kwa hayo vinavyo amrisha na kulingania.
Na lau ungeli ona - ewe mwenye kuweza kuona - wakati wanapo simamishwa
madhaalimu mbele ya Muumba wao, Mwenye kumiliki amri yao, ungeliona maajabu
katika msimamo wao, pale wanapo jibizana maneno wao kwa wao. Walio wanyonge
wakiwaambia walio tukuka juu yao: Ingeli kuwa si nyinyi, kwa kutusaliti
na kutamalaki, hapana shaka tungeli kuwa Waumini.
Rudi kwenye Sura
32. Walio takabari na wakajiona ni wakubwa, watawaambia wanyonge,
kwa kuyapinga maneno yao: Kwani sisi tulikuzuieni msiongoke ulipo kufikieni
uwongofu? Tumekuzuieni sisi au nyinyi wenyewe ndio mmekhiari upotofu kuliko
uwongofu.
Rudi kwenye Sura
33. Na wanyonge nao watawaambia walio takabari: Bali vitimbi vyenu
na uchochezi wenu kutuchochea usiku na mchana ndio umetutumbukiza katika
hilaki, pale mlipo kuwa mkitutaka tumkufuru Mwenyezi Mungu, na tumfanyie
miungu mingine ya kumshirikisha. Na pande zote mbili zikaficha majuto yao
walipo iona adhabu inawashukia. Wakajua kuwa hapana faida ya kuonyesha
majuto. Na tukayaweka makongwa, (nira), juu ya shingo za wasio amini. Je!
Watu hawa wanastahiki chochote ila malipo kwa yale waliyo kuwa wakiyatenda?
Rudi kwenye Sura
34. Na sisi hatukumtuma Mtume yeyote kwenda kwenye mji kuwaita watu
wake wafuate Haki ila wale wanao jidekeza kwa starehe zao katika
ule mji husema: Hakika sisi tunayakanusha hayo mliyo kuja nayo.
Rudi kwenye Sura
35. Na husema kwa kujipa: Sisi tuna mali mengi zaidi na watoto. Wala
hatutaadhibiwa Akhera.
Rudi kwenye Sura
36. Ewe Nabii! Waambie: Hakika aliye niumba humkunjulia riziki amtakaye,
katika wanao muasi na wanao mt'ii. Na humdhikisha amtakaye. Wala hiyo si
dalili ya kuwa Yeye yuradhi na mtu au anamchukia. Lakini watu wengi hawajui
haya.
Rudi kwenye Sura
37. Wala mali yenu wala watoto wenu sio jambo la kukurubisheni kwetu
mkawa karibu. Lakini ambaye Imani yake imethibiti, na akawa anatenda mema,
basi watu kama hao ndio watapata thawabu mara mbili kwa waliyo yatenda.
Na Peponi watakuwa ni watu wa juu na wenye amani.
Rudi kwenye Sura
38. Na hao ambao wana fanya juhudi kuzipinga Ishara zetu, wakifanya
kila hila kuzivunja na kuwazuia Manabii wetu wasifikishe Ujumbe wake, hao,
basi watakuwa katika adhabu, wamehudhurishwa na wala hawataepuka.
Rudi kwenye Sura
39. Ewe Nabii! Sema: Hakika Mola wangu Mlezi anamkunjulia riziki
amtakaye katika waja wake, na humdhikisha amtakaye. Na chochote mtacho
kitoa Yeye atakilipa. Na Yeye Aliye takasika ni Mbora wa wenye kuruzuku.
Rudi kwenye Sura
40. Na taja, ewe Nabii, siku Mwenyezi Mungu atapo wakusanya wote,
na kisha Subhanahu awaambie Malaika mbele ya wale walio kuwa wakiwaabudu:
Je! Hawa walikuabuduni nyinyi khasa badala yangu mimi?
Rudi kwenye Sura
41. Malaika watasema: Sisi tunakutakasa kabisa na kuwa Wewe una mshirika
wowote. Wewe ndiye tulio shikamana nawe kwa mapenzi na ut'iifu, sio
wao. Hao wameghurika katika madai yao kuwa wanatuabudu sisi. Bali walikuwa
wanafuata nyayo za mashetani walio wapambia ushirikina. Wengi wao wakiwasadiki
hao.
Rudi kwenye Sura
42. Basi Siku ya Mkusanyo hapana atakaye weza kumletea mwenzie manufaa
wala kumkinga na madhara. Na tutawaambia walio jidhulumu nafsi zao: Ionjeni
adhabu ya Moto ambayo mlio kuwa duniani mkiikanusha.
Rudi kwenye Sura
43. Na makafiri walipo somewa Aya zetu zilio wazi dalili zake kuonyesha
Haki, makafiri walisema: Huyu si chochote ila ni mtu anaye taka kukuzuilieni
msiwaabudu walio kuwa wakiwaabudu baba zenu. Na pia walisema: Hii
Qur'ani si chochote ila ni uwongo ulio tungwa tu. Na walio ikataa Qur'ani
ilipo wajia walisema: Hii si chochote ila ni uchawi ulio wazi.
Rudi kwenye Sura
44. Na Mwenyezi Mungu hakuwateremshia Waarabu Vitabu vya mbinguni
wavisome; wala hutukupata kuwapelekea Mwonyaji kabla yako wa kuwahadharisha
na matokeo ya ukafiri wao.
Rudi kwenye Sura
45. Na kaumu zilizo tangulia ziliwakadhibisha Manabii wao. Na hawa
washirikina wa kaumu yako hawajafikia hata sehemu moja katika kumi za nguvu
na umadhubuti tulio wapa hao walio tangulia. Wakawakanusha Mitume wangu.
Basi ilikuwaje ghadhabu yangu juu yao jinsi nilivyo wakasirikia!
Rudi kwenye Sura
46. Waambie: Mimi nakuamrisheni jambo moja tu - Msimame kwa ikhlasi
ya kumtakasia Mwenyezi Mungu muache kufuata mitindo yenu ya zamani - katika
kuchungua kwa kumsafia niya Mwenyezi Mungu, mkigawika wawili-wawili, au
mmoja-mmoja, muangalie kwa uadilifu na insafu. Kisha mfikiri khabari ya
huyu mwenzenu, Muhammad, ambaye mmeishi naye na mnajua kuwa akili yake
ni timamu. Huyu hana wazimu kwa kuliingia jambo hili. Yeye huyu si chochote
ila ni Mwonyaji kwenu, anakuhadharisheni msije mkapata adhabu kali inayo
kukabilini mbele yenu.
Rudi kwenye Sura
47. Waambie makafiri: Ujira wowote nilio kutakeni juu ya kufikisha
Ujumbe ni kwa maslaha yenu. (Yaani nyinyi mwongoke na mpate malipo
kwa Mwenyezi Mungu.) Sina ujira ninao utaraji mimi ila kwa Mwenyezi Mungu.
Naye ni Mwenye kuangalia na kuchungua kila kitu.
Rudi kwenye Sura
48. Waambie: Hakika Mola wangu Mlezi huitupa Haki juu ya baat'ili
(uwongo) ikauondoa. Na Yeye ndiye Mwenye kuijua vyema ghaibu; hapana siri
inayo fichikana kwake.
Rudi kwenye Sura
49. Waambie: Uislamu umedhihiri, wala uwongo hauwezi kuwa ndio njia
ya kuipinga Haki. Na hizo mbinu za zamani hazirejei tena.
Rudi kwenye Sura
50. Waambie: Nikiiacha Haki basi madhara ya hayo yataniangukia mwenyewe.
Na nikiongoka basi nimeongozwa na Mola wangu Mlezi. Yeye ni Mwenye kusikia
kauli yangu na kauli yenu. Yupo karibu nami, na karibu yenu.
Rudi kwenye Sura
51. Na lau kuwa utaona, ewe mwenye kuona, pale watapo fazaika makafiri
kweli itapo dhihiri, basi hawatakuwa na pa kukimbilia. Na watachukuliwa
wapelekwe kwenye Moto kutoka pahala karibu.
Rudi kwenye Sura
52. Na watasema, watapo iona adhabu: Tunaiamini Haki! Na vipi wao
waipate Imani kwa wepesi huo kutoka pahala mbali na dunia ambayo wakati
wake umekwisha pita?
Rudi kwenye Sura
53. Na ilhali wao walikwisha ikataa Haki kabla ya Siku hii, na wakavurumiza
kwa dhana ya uwongo kutoka mahala palipo mbali na ukweli.
Rudi kwenye Sura
54. Patawekewa kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani ya Imani
ya kuwafaa, kama walivyo fanyiwa wenzao wa kabla yao walipo amini baada
ya kwisha wakati wake. Kwa sababu wote hao wote walikuwa katika kuifanyia
Haki shaka inayo pelekea kutuhumiwa.
Rudi kwenye Sura