1. Ewe Nabii endelea hivyo hivyo, kama ulivyo, kumcha
Mwenyezi Mungu, wala usiyakubali mawazo ya makafiri na wanaafiki. Kwa hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa kuvijua, ni Mwenye
hikima katika kauli yake na vitendo vyake.
Rudi kwenye Sura
2. Na fuata wahyi unao teremka juu yako kutokana na Mola wako Mlezi.
Hakika Mwenyezi Mungu anaye kufunulia kwa wahyi anazo khabari hata za mambo
madogo madogo unayo yatenda wewe, na wanayo yatenda makafiri na wanaafiki.
Rudi kwenye Sura
3. Na wewe mwachilie mambo yako yote Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi
Mungu anatosha kabisa kuwa ni mtegemewa wa kila jambo.
Rudi kwenye Sura
4. Mwenyezi Mungu hakumjaalia mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani
ya mwili wake; wala hakumfanya mke wa yeyote katika nyinyi kuwa ni mama
yake, pale anapo sema ati: Wewe kwangu mimi kama mgongo wa mama yangu!
Wala hakuwafanya watoto mnao wapanga kuwa ni wenenu, kuwa hakika ni wana
wenu kwa nasaba. Hayo ya kuwafanya watoto wa kupanga kuwa ni wenenu,
ni kauli inayo toka kwenye vinywa vyenu, wala hayana ukweli. Hapana hukumu
yoyote inayo tokana na hayo. Na Mwenyezi Mungu anasema jambo lilio thibiti
la hakika. Na anakuongozeni mlifikie. Na Yeye peke yake Subhanahu ndiye
anaye ongoa watu kwenye Njia iliyo sawa.
Rudi kwenye Sura
5. Wanasibishieni hawa watoto kwa baba zao khasa. Hayo ndiyo ya uadilifu
zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Ikiwa hamwajui baba zao walio nasibiana
nao khasa, basi hao ni ndugu zenu katika Dini na rafiki zenu wa kuwanusuru.
Wala nyinyi hamna dhambi ikiwa mmewanasibisha na watu wasio kuwa baba zao
kwa kukosea. Lakini inakuwa dhambi kwa mlio kusudia kwa nyoyo zenu baada
ya kwisha jua yaliyo. Na Mwenyezi Mungu anakusameheni kwa kukosea kwenu,
na anaikubali toba yenu kwa makosa mliyo kusudia.
Rudi kwenye Sura
6. Nabii Muhammad ni mwenye kustahiki zaidi urafiki kwa Waumini,
na ana huruma zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Basi yawapasa wao wampende
na wamt'ii. Na wake zake ni Mama zao kwa kuwatukuza na kuwahishimu, na
kuwa ni haramu juu yao kuwaoa baada yake. Na jamaa walio khusiana ni karibu
zaidi kuliko Waumini wenginewe na Wahajiri, walio hama Makka, kwa kurithiana
wao kwa wao kama ilivyo wajibika katika Qur'ani. Lakini inafaa kumfanyia
wema mlio fanya urafiki naye katika Dini asiye kuwa jamaa yenu, kwa
kuwapa wema na mapenzi au hata kumuandikia mali katika wasia. Hayo
ya kurithiana jamaa walio khusiana yamethibiti katika Kitabu cha Qur'ani
wala hayawezi kubadilishwa.
Rudi kwenye Sura
7. Na kumbusha pale tulipo fanya agano na Manabii wote walio tangulia
kuwa watafikisha ujumbe na wito kulingania Dini iliyo sawa, na wewe, na
Nuhu, na Ibrahim, na Musa, na Isa bin Maryamu; na tukachukua kwao
agano lenye shani kubwa.
Rudi kwenye Sura
8. Ili Mwenyezi Mungu awaulize Manabii Siku ya Kiyama juu ya waliyo
waambia kaumu zao. Na Yeye amewaandalia wenye kuwakataa Mitume adhabu yenye
kutia uchungu.
Rudi kwenye Sura
9. Enyi mlio amini zikumbukeni neema na fadhila za Mwenyezi Mungu
zilio juu yenu, pale yalipo kujieni makundi katika Siku ya Handaki. Tukawapelekea
upepo mkali wa kimbunga ubaridi, na Malaika ambao nyinyi hamwaoni. Kikawaingia
kiwewe katika nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu alikuwa Mwenye kuviona vitendo
vyenu, na ukweli wa niya zenu. Basi akaingia kukulindeni.
Rudi kwenye Sura
10. Walipo kujieni kutoka upande wa juu ya bonde, na kutoka chini,
na macho yakakodoka, na nyoyo zikapanda mpaka kwenye koo, kwa kufazaika
na kubabaika. Na nyinyi katika wakati ule wa shida kubwa kila namna ya
dhana zilikujieni juu ya ahadi ya Mwenyezi Mungu.
Si makusudio ya maneno haya kuwa maadui walikuja kutoka kila upande.
Tukiangalia ufafanuzi wa tukio hili inadhihirika kuwa makusudio ni kuwa
walio kuja kutoka upande wa juu ya Waislamu, ni kabila ya Ghat'fan na walio
wafuata katika wakaazi wa Najdi, kwani wao walikuja pande za juu
ya Bara Arabu upande wa mashariki. Na inatudhihirikia kuwa walio kuja upande
wa chini ya Waumini ni Makureshi, kwa sababu wao walikuja kutoka upande
wa chini ya Bara Arabu upande wa magharibi.
Rudi kwenye Sura
11. Katika wakati ule Waumini walifanyiwa mtihani juu ya kusubiri
kwao juu ya Imani. Wakatikisika kwa khofu kwa mtikiso mkubwa.
Rudi kwenye Sura
12. Na kumbuka shaka iliyo waingia wanaafiki na wagonjwa wa nyoyo
walipo sema: Ahadi aliyo tupa Mwenyezi Mungu na Mtume ni ahadi ya uwongo,
imekusudiwa kutudanganya tu.
Rudi kwenye Sura
13. Na kumbuka walipo sema kikundi cha wanaafiki na ambao wanao rega
rega: Enyi watu wa (Yathrib, yaani) Madina! Hapana maana kubakia hapa nyinyi
katika vita hivi vya kushindwa. Rudini mwende makwenu. Na kundi jingine
kati yao walimtaka ruhusa Mtume warejee Madina, na wakasema: Hakika nyumba
zetu hazina ulinzi. Hatuna budi kurejea tukazilinde. Wala nyumba zao hazikuwa
khatarini kabisa kama walivyo sema. Hawakutaka ila kukimbia vita tu, kwa
udhuru wa uwongo.
Rudi kwenye Sura
14. Lau kuwa makundi ya majeshi ya maadui wangeli waingilia Madina
kwa kila upande, na wakawataka watangaze kuwa wameuwacha Uislamu na wawapige
vita Waislamu bila ya shaka wangeli wakubalia yale waliyo takiwa, na wala
wasingeli sita ila muda mfupi tu.
Rudi kwenye Sura
15. Na hakika hawa wenye kukimbia kutoka midani ya vita walikwisha
muahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kuwa watasimama imara katika vita pamoja
na Mtume, na wala hawatakimbia. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa
kwa yule mwenye kuitoa, na yampasa aitimize.
Rudi kwenye Sura
16. Waambie: Kukimbia hakukufaeni kitu ikiwa ndio mnayakimbia mauti
au kuuwawa, maadamu ajali yenu imekwisha fika. Na ikiwa haijafika, basi
hamtobaki mkistarehe katika dunia ila kwa muda wa umri wenu, nao ni mchache.
Rudi kwenye Sura
17. Waambie hawa wanao babaika: Nani atakaye kulindeni na Mwenyezi
Mungu akitaka kukuleteeni shari, au atakaye kuzuieni msipate kheri, akitaka
Yeye kukurehemuni? Wala hawatapata badala ya Mwenyezi Mungu yeyote wa kuwalinda
au kuwaokoa.
Rudi kwenye Sura
18. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua wanao zuilia miongoni mwenu, na
wanao waambia ndugu zao: Unganeni nasi! Wala hawaingii katika vita vinapo
shitadi ila kidogo tu.
Rudi kwenye Sura
19. Wana pupa juu yenu kwa kuonekana dhaahiri inapo kuwa hapana khofu.
Na ikija khofu ya adui au ya Mtume s.a.w. utawaona wanakuangalia na macho
yao yanawazunguka hawajitambui, kama hali ya mwenye kuzimia wakati wa sumbuko
la kukaribia mauti. Na khofu ikiondoka wanapita mpaka kukutukaneni na kukushutumuni
kwa ndimi za kukata. Hao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao hawakuamini
kwa nyoyo zao, ijapo kuwa wametangaza kuwa ni Waislamu. Basi Mwenyezi Mungu
amezibat'ilisha a'mali zao kwa ukafiri wao walio dhamiria. Na kubat'ilisha
huko ni jambo jepesi kwa Mwenyezi Mungu.
Aya hii tukufu inaashiria ukweli wa kisayansi ambao ulikuwa
haukujuulikana namna yake wakati wa kuteremka Qur'ani Tukufu. Ukweli huo
ni kuwa jicho wakati wa kukurubia mauti au wakati wa khofu huzunguka. Na
katika sababu za hayo ni kuwa kwa shida ya khofu utambuzi hutoweka, ikawa
mtu hajitambui. Vituo vya navo zisio tambua katika ubongo hupoteza mizani
yake, basi huwa huyo mwenye khofu kama mfano wa mwenye kuzimia kwa kukaribia
kufa, jicho lake huzunguka na mboni ya jicho hupanuka, na hubaki katika
hali ya kukodoa macho mpaka kufa.
Rudi kwenye Sura
20. Wanadhani hawa wanaafiki kwamba majeshi ya makafiri yaliyo ungana
bado yapo mahali pao wanaizinga Madina. Na hayo makundi ya maadui yakirejea
tena, watatamani hao woga laiti wangeli kuwa wanaishi pamoja na mabedui
huko majangwani wakidondoa khabari zenu. Na lau wakibaki kwenye kambi zao,
na wasikimbie, na majeshi mawili yakapambana, basi hata hivyo wasinge pigana
pamoja nanyi ila kidogo tu, kama kujionyesha na watajwe kuwa nao walikuwamo.
Rudi kwenye Sura
21. Hakika nyinyi mna kiigizo kizuri kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu,
kwa mwenye kutaraji rehema ya Mwenyezi Mungu, na neema za Siku ya Mwisho,
na akamkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi katika khofu na kutumai,
na katika shida, na katika neema.
Rudi kwenye Sura
22. Na Waumini walipo yaona makundi ya washirikina walisema: Haya
ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake zamani. Kwani walituahidi
tutapata shida, na kisha tutapata ushindi. Mwenyezi Mungu na Mtume wake
wamesema kweli. Taabu hizi basi, hazikuwazidishia ila nguvu za kumuamini
Mwenyezi Mungu, na uzuri wa kuinyenyekea kwao hukumu yake.
Rudi kwenye Sura
23. Miongoni mwa hawa Waumini wapo watu walio muahidi Mwenyezi Mungu
kuwa watasimama imara na Mtume katika vita. Nao wakatimiza ahadi yao. Miongoni
mwao wapo walio pata utukufu wa kufa mashahidi, na wengine wamebakia wahai
wakingojea nao kupata utukufu huo. Wala hawakuigeuza ahadi ya Mwenyezi
Mungu waliyo jikatia juu ya nafsi yao, wala hawakugeuza chochote katika
hayo.
Rudi kwenye Sura
24. Ili Mwenyezi Mungu apate kuwalipa Waumini walio wakweli kwa sababu
ya ukweli wao katika Imani yao na kutimiza kwao ahadi waliyo itoa. Na awaadhibu
wanaafiki - pindi akitaka - au amwezeshe aliye elekea, kufikia toba. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe kwa kukubali toba, Mwenye kurehemu kwa
kusamehe maasi.
Rudi kwenye Sura
25. Mwenyezi Mungu akawarudisha nyuma makafiri walio jiunga makundi
kumpiga Mtume na nyoyo zao zimejaa chuki. Hawakupata kheri yoyote kwa ushindi
wala ngawira. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini wasipate mashaka,
kwa kuwapatiliza wale makafiri kwa upepo na Malaika. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwenye uweza wa kutimiliza alitakalo, ni Mwenye nguvu hapana wa kumshinda.
Rudi kwenye Sura
26. Na Mwenyezi Mungu aliwateremsha walio wasaidia makundi ya maadui
katika Watu wa Kitabu, nao ni Mayahudi wa Bani Quraidha, kutokana na ngome
zao walipo kuwa wakijilinda ndani yake. Na akaingiza katika nyoyo zao kitisho.
Wengine mkawa mnawawauwa, nao ni wanaume, na wengine mnawachukua mateka,
nao ni wanawake na watoto.
Rudi kwenye Sura
27. Na akakurithisheni ardhi zao, na nyumba zao, na mali zao, na
ardhi ambazo nyayo zenu hazijapata kuzikanyaga kabla yake. Na Mwenyezi
Mungu Subhanahu ni Muweza wa kutimiza kila alitakalo.
Rudi kwenye Sura
28. Ewe Nabii! Waambie wake zako kwa kuwanasihi: Ikiwa mnataka maisha
ya duniani na starehe zake, basi jongeeni nitakupeni cha kupunguza upweke
wa talaka, itakuwa ni tunza yenu. Na nitakupeni talaka isiyo na uovu ndani
yake.
Rudi kwenye Sura
29. Na ikiwa mnakhiari mapenzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
neema za nyumba ya Akhera, na mnaridhi maisha magumu mlio nayo hivi sasa,
basi hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia mfano wenu nyinyi miongoni mwa
wanawake walio wema kwa vitendo vyao, ujira ambao haukadiriki.
Rudi kwenye Sura
30. Enyi wake wa Nabii! Miongoni mwenu mwenye kufanya makosa yaliyo
dhaahiri ubaya wake, basi juu ya adhabu yake zinaongezwa adhabu mbili,
ili iwe adhabu tatu kwa kulinganisha na mwenziwe. Na kuongeza huko
kwa Mwenyezi Mungu ni kwepesi.
Rudi kwenye Sura
31. Na katika nyinyi mwenye kudumu juu ya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, na akatenda mema, Mwenyezi Mungu atampa ujira mara mbili.
Na tumemuandalia kwa Akhera riziki ya kipimo kizuri.
Rudi kwenye Sura
32. Enyi wake wa Mtume! Nyinyi si kama wanawake wengine kwa fadhila
na utukufu. Kama mnataka uchamngu, basi msizungumze kwa maneno ya kuregeza
sauti, hata ambaye ana uharibifu katika moyo wake akaingia tamaa.
Kusema kwenu kuwe kama kawaida sio kujitia.
Rudi kwenye Sura
33. Na kaeni nyumbani kwenu, wala msitoke ila kwa haja. Wala msidhihirishe
uzuri wenu na mapambo yenu kwa wanaume pale mnapo toka, kama walivyo kuwa
wakifanya watu wa ujahili wa zamani. Na timizeni Sala kwa ukamilifu, na
toeni Zaka, na fuateni amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi
Mungu anataka, kwa yote anayo kuamrisheni na kukukatazeni, mpate utukufu
na hishima, ili muondokewe na madhambi na maasia, enyi Ahli Baiti Nnabii,
Watu wa Nyumba ya Nabii, na akusafisheni kwa usafi usio kuwa na shaka.
Rudi kwenye Sura
34. Na hifadhini yanayo somwa katika nyumba zenu ya Qur'ani aliyo
iteremsha Mwenyezi Mungu, na hikima zilio sawa za Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua mambo yalio zama ndani kabisa na
ya hakika yake. Basi tahadharini na kwenda kinyume naye na kumuasi Mtume
wake.
Rudi kwenye Sura
35. Hakika wenye kut'ii miongoni mwa wanaume na wanawake, na wenye
kumsadiki Mwenyezi Mungu na Mtume wanaume na wanawake, na wenye kusimama
kwa ut'iifu wanaume na wanawake, na walio wa kweli katika kauli zao na
vitendo vyao katika wanaume na wanawake, na wenye kusubiri katika kubeba
mashaka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wanaume na wanawake, na wanyenyekevu
kwa Mwenyezi Mungu wanaume na wanawake, na wenye kuzihifadhi tupu zao kwa
yasiyo kuwa halali wanaume na wanawake, na wenye kumdhukuru Mwenyezi Mungu
kwa wingi katika nyoyo zao na ndimi zao wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu
amewaandalia kuwasamehe madhambi yao, na kuwalipa malipo makubwa kwa vitendo
vyao.
Rudi kwenye Sura
36. Haimjuzii Muumini, mwanamume au mwanamke, kuwa na khiari katika
jambo lolote baada ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake wakisha lihukumia. Na
mwenye kwenda kinyume na alivyo hukumu Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi
amejitenga mbali na njia iliyo sawa kwa umbali ulio dhaahiri.
Rudi kwenye Sura
37. Na kumbuka pale ulipo mwambia Zaid bin Haritha, ambaye Mwenyezi
Mungu amemneemesha kwa kumwongoa kwenye Uislamu, na wewe ukamneemesha kwa
kumlea na kumkomboa utumwani: Shikamana na mkeo, Zainab binti Jahsh, na
umche Mwenyezi Mungu, na vumilia kukaa naye. Na wewe ulikuwa unaficha nafsini
mwako ambayo Mwenyezi Mungu atakuja yadhihirisha, yaani kuwa yeye atampa
t'alaka na wewe utakuja muwoa. Nawe ukakhofu watu wasije kukulaumu. Na
Mwenyezi Mungu ndiye anaye stahiki umkhofu, ijapo kuwa hayo ni mashaka
juu yako. Basi Zaid alipo kwisha haja naye, na akampa t'alaka kujiondolea
dhiki ya kuishi naye, tukakuoza wewe, ili iwe ni chanzo cha kuvunja ada
iliyo mbovu. Baada ya hayo hapana ubaya tena kwa Waislamu kuwaoa walio
kuwa wake za walio kuwa wamewapanga utoto, baada ya kwisha wat'aliki. Na
amri ya Mwenyezi Mungu aitakayo ni lazima iwe bila ya pingamizi.
Rudi kwenye Sura
38. Nabii hana makosa kutenda kitendo alicho muamrisha Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu ameweka mwendo huo kwa Manabii walio tangulia, kuwa wasipige
marfuku alicho wahalalishia na akawakunjulia. Na amri ya Mwenyezi
Mungu ni kupitisha alicho pitisha, na hukumu iliyo thibiti.
Rudi kwenye Sura
39. Manabii hao ndio walio wafikishia watu ujumbe wa Mwenyezi Mungu
kama tulivyo wateremshia. Nao wanamkhofu Yeye, wala hawamkhofu yeyote asiye
kuwa Yeye. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Yeye ndiye Muangalizi Mwenye
kuhisabu.
Rudi kwenye Sura
40. Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu hata iwe ni haramu
kwake kumwoa mt'alaka wake. Lakini yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na
ni Mwenye kukhitimisha Manabii wote. Juu yake ni kufikilisha ujumbe kama
alivyo muamrisha Mola wake Mlezi, bila ya kumchelea yeyote. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.
Rudi kwenye Sura
41,42. Enyi ambao mmeamini! Msifuni Mwenyezi Mungu kwa namna mbali
mbali za sifa, na mfanye hayo kwa wingi. Na mtakaseni na kila kisicho kuwa
laiki naye mwanzo wa mchana na mwisho wake.
Rudi kwenye Sura
43. Na Yeye ndiye aliye kuahidini kukupeni rehema yake na upole wake.
Na Malaika wake wanakuombeeni maghfira na uwongofu, ili Mwenyezi Mungu
akutoeni kwenye giza la ukafiri na upotovu, mwendee kwenye nuru na ut'iifu.
Na Mwenyezi Mungu hakika ni Mkuu wa kuwarehemu Waumini.
Rudi kwenye Sura
44. Maamkio yao siku watakapo kutana naye ni: Amani na Salama kwao.
Na amewatengezea kwa vitendo vyao ujira wa ukarimu utakao waonyesha
fadhila zake.
Rudi kwenye Sura
45. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma kwa watu wote uwapelekee ujumbe
wa Uislamu. Ushuhudie Haki, na uwabashirie Waumini kwamba watapata kheri
na thawabu, na uwaonye makafiri kuwa watapata mwisho muovu.
Rudi kwenye Sura
46. Na umetumwa uwe ni mwenye kuwaita viumbe vyote vimwendee Mwenyezi
Mungu kwa amri yake. Na uwe ni taa ya uwongofu kuwaongoa kwa nuru yake
waliopo katika kiza cha shaka.
Rudi kwenye Sura
47. Na wabashirie Waumini kwamba watapata kheri kubwa ya kuzidi katika
dunia na Akhera.
Rudi kwenye Sura
48. Na wala usiwafuate makafiri na wanaafiki, wala usijishughulishe
na maudhi yao. Na mfanye Mwenyezi Mungu ndiye Wakili wako wa kumtegemea
kukulinda na madhara yao na shari zao. Na Mwenyezi Mungu anakutosha kabisa
kuwa ndiye Mtegemewa wa kukukifia na kukukinaisha.
Rudi kwenye Sura
49. Enyi mlio amini! Mkifunga ndoa na wanawake Waumini, kisha mkawat'aliki
kabla ya hamjawaingilia, basi haiwalazimu eda wao mkawa mnaihisabu. Basi
wapeni kitu katika mali kwa kuwapoza. Na mwatoe majumbani kwenu bila ya
kuwaletea madhara yoyote.
Rudi kwenye Sura
50. Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari.
Na tumekuhalishia wajakazi ulio wamiliki mkono wako wa kulia, katika alio
kuneemeshea Mwenyezi Mungu. Na tumekuhalalishia kuwaoa mabinti ami zako,
na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa
dada, yaani ndugu wa kike, wa mama yako, walio hama nawe. Na tumekuhalalishia
mwanamke Muumini akijitolea nafsi yake bila ya mahari, nawe ikawa unataka
kumwoa na umempenda. Kujitolea huku ni kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine.
Kwao haifai hivyo. Tunajua hukumu tulizo wafaridhia Waumini kwa wake zao
na wajakazi wao, na tuliyo kuruhusu wewe, si wao, ili isiwe dhiki juu yako
kwa tuliyo kuhukumia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe madhambi ya
waja wake, Mwenye kuwarehemu kwa ukunjufu.
Rudi kwenye Sura
51. Unaweza kumuakhirisha umtakaye katika kugawa zamu, na ukamjongeza
umtakaye. Na kumtaka uliye muakhirisha zamu yake hapana lawama juu yako.
Hivyo kuachiliwa utakavyo wewe yakaribia zaidi kupelekea furaha yao na
baada ya kuwahuzunikia, na wao wote wawe radhi kwa ulio wapa. Na Mwenyezi
Mungu anayajua yaliomo ndani ya nyoyo zenu, ya kuudhika au kuridhika kwa
aliyo kufanyieni sharia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua yaliomo vifuani,
Mpole hafanyi papara kuadhibu.
Rudi kwenye Sura
52. Hawakuhalalikii wanawake wengine baada ya hawa, wala kuwapa t'alaka
kwa ajili ya kuwabadilisha kwa wengine uwatakao, hata wakikupendeza kwa
uzuri wao. Lakini Mwenyezi Mungu amekuhalalishia wajakazi ulio wamiliki
kwa mkono wako. Na Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu, na anakihifadhi.
Rudi kwenye Sura
53. Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila kwa idhini yake
kwa ajili ya kwenda kula chakula, bila ya kwenda kungoja wakati mpaka kitapo
kuwa tayari. Lakini Mtume akikuiteni, basi ingieni. Na mkisha kula ondokeni.
Wala msikae baada yake mkijizoeza mazungumzo nyinyi kwa nyinyi. Kwani hakika
kuingia bila ya idhini yake, na kukaa muda mrefu baada ya kwisha kula,
kunamuudhi Nabii, naye anakustahini hawezi kukutakeni mtoke. Lakini Mwenyezi
Mungu Mtukufu hana la kumzuia asiitangaze haki kama wanavyo zuilikana
viumbe. Na mtakapo wauliza wake za Nabii s.a.w. haja yoyote, basi waulizeni
nyuma ya mapazia. Hivyo ni usafi bora kwa nyoyo zenu na nyoyo zao zisiingiwe
na uchochezi wa Shetani. Na haikufaliini nyinyi kumuudhi Mtume wa Mwenyezi
Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake milele, kwa sababu ya hishima yake
na yao. Hakika jambo hilo ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu.
Yanarejea maelezo ya ki-ilimu juu ya Aya mbili 58, na 59 za
Surat An-nur, katika yaliyo khusu adabu za kuzuru.
Rudi kwenye Sura
54. Mkidhihirisha walau kidogo katika mambo yanayo muudhi, au mkikificha
katika vifua vyenu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
Rudi kwenye Sura
55. Hapana dhambi kwa wakeze Nabii wakitojificha kwa baba zao, au
watoto wao, au ndugu zao, au watoto wa ndugu zao wa kiume, au watoto wa
ndugu zao wa kike, au wanawake Waumini wenginewe, au watumwa walio wamiliki,
kwa sababu ya shida ya kuwahitajia kwa matumishi. Nanyi wanawake, mcheni
Mwenyezi Mungu katika mambo aliyo kuamrisheni, wala msipindukie mipaka
yake. Kwani Yeye hakika anajua kila kitu, hapana kilicho fichikana kwake.
Rudi kwenye Sura
56. Hakika Mwenyezi Mungu anamrehemu Nabii wake na yu radhi naye.
Na Malaika wanamwombea yeye. Enyi mlio amini! Msalieni na mumsalimu kwa
salamu.
Rudi kwenye Sura
57. Hakika wanao muudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kuwapinga
na kuchochea watu wawakatae, Mwenyezi Mungu amewafukuza kwenye rehema yake
duniani na Akhera; na amewaandalia adhabu itayo wavunja kiburi chao.
Rudi kwenye Sura
58. Na wanao waudhi Waumini wanaume na wanawake kwa maneno au vitendo,
bila ya wao kufanya makosa yoyote, hao basi wamebeba migongoni mwao mzigo
wa ule uwongo wao, na inakuwa wametenda dhambi iliyo dhaahiri ubaya wake.
Rudi kwenye Sura
59. Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake wa Waumini,
wateremshe nguo zao juu ya miili yao. Na wakivaa namna hii ni afadhali
na wanaelekea zaidi kujuulikana na kwa hivyo wasipate kuudhiwa. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kumrehemu mwenye kuacha madhambi yake.
Rudi kwenye Sura
60. Ninaapa! Ikiwa hawataacha hao wanaafiki, na wenye maradhi katika
nyoyo zao, na wanao eneza khabari za uwongo katika Madina, hapana shaka
nitakusalitisha juu yao, kisha hawatabakia kuwa karibu yako ila kwa muda
mchache tu.
Rudi kwenye Sura
61. Hao wanastahiki laana na kufukuzwa. Kila watapo patikana wakamatwe
na wauliwe moja kwa moja.
Rudi kwenye Sura
62. Mwendo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu tangu zamani, kwa walio kuwa
wakiwafanyia unaafiki Manabii na Mitume, na wakiasi, ni kuwa huuwawa kila
wanapo kutikana. Wala mwendo wa Mwenyezi Mungu haugeuki.
Rudi kwenye Sura
63. Watu wanakuuliza lini itasimama Saa ya Kiyama. Waambie hao: Hakika
ujuzi wa wakati wake uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na nini kitakujuvya?
Pengine wakati wa kusimama Saa ya kiyama upo karibu.
Rudi kwenye Sura
64. Hakika Mwenyezi Mungu amewafukuza makafiri kwenye rehema yake,
na amewatengenezea Moto mkali mno.
Rudi kwenye Sura
65. Hawatatoka humo kabisa. Hawatampata wa kuchukua dhamana ya kuwahami,
wala wa kuwatetea.
Rudi kwenye Sura
66. Siku zitakapo geuka nyuso zao Motoni kutoka hali hii kwendea
hali hiyo, wakisema kwa majuto: Laiti kuwa sisi tulimt'ii Mwenyezi Mungu
na tungeli mt'ii Mtume!
Rudi kwenye Sura
67. Na watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwafuata maraisi
wetu, na wakubwa wetu katika kukukataa Wewe na Mtume wako. Na wao ndio
wakatutenganisha mbali na Njia Iliyo Nyooka.
Rudi kwenye Sura
68. Mola wetu Mlezi! Wajaalie adhabu yao iwe mardufu, na uwafukuze
kwenye rehema yako kabisa kwa kadri ya madhambi yao na makosa yao.
Rudi kwenye Sura
69. Enyi mlio amini! Msimuudhi Nabii kwa namna yoyote ya udhia, kama
wale walio muudhi Musa katika kaumu yake. Na Mwenyezi Mungu akamtoa makosani
na akamsafisha na hayo waliyo mzulia. Na Musa mbele ya Mwenyezi Mungu alikuwa
ni bwana mwenye hadhi.
Rudi kwenye Sura
70. Enyi mlio amini! Iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu mkimuasi,
na semeni maneno yalio simama sawa yasio kwenda upogo.
Rudi kwenye Sura
71. Apate kukuwezesheni kutenda mema, na azifute dhambi zenu. Na
mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo amepata kufuzu kukubwa
kwa kuepuka adhabu, na kupata thawabu.
Rudi kwenye Sura
72. Sisi kwa hakika tulizitaka mbingu na ardhi na milima zichukue
dhamana, nazo zikakataa kuichukua, na wakaiogopa. Lakini mwanaadamu aliichukua.
Hakika yeye amekuwa ni mkubwa wa kujidhulumu nafsi yake kwa kutojua jukumu
la kuchukua huko.
Rudi kwenye Sura
73. Ili Mwenyezi Mungu awaadhibu wanaafiki wanaume, na wanaafiki
wanawake, na washirikina wanaume, na washirikina wanawake; na Mwenyezi
Mungu apate kukubali toba za Waumini wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwingi wa rehema.
Rudi kwenye Sura