1. Harufi hizi zimeanzia baadhi ya Sura kuashiria kuwa
Qur'ani ni muujiza ulio tungwa na harufi kama harufi wanazo zitumia Waarabu
katika maneno yao. Na juu ya hayo wao wameshindwa kuleta mfano wake. Na
pia ni kwa ajili ya kuzindua watu wasikilize na watege sikio. Na washirikina
walikuwa wamewafikiana kuwa wawe wanaropokwa maneno ya upuuzi tu ikisomwa
Qur'ani wala wasiisikilize.
Rudi kwenye Sura
2. Hizi Aya tukufu ni Aya za Qur'ani iliyo kusanya hikima na ukweli.
Rudi kwenye Sura
3. Hizi Aya ni Uwongofu ulio kamilika, na Rehema iliyo kusanya kwa
wenye kutenda mema.
Rudi kwenye Sura
4. Hao ndio wanao timiza Sala kwa njia ya ukamilifu kabisa, na wanawapa
Zaka wanao istahiki; na wao wanayaamini maisha ya Akhera kwa imani yenye
nguvu kabisa.
Rudi kwenye Sura
5. Hao Waumini wanao tenda vyema vitendo vyao, wametua kwenye Uwongofu
ulio wajia kutokana na Mola wao Mlezi. Na hao tu - si wengineo - ndio wenye
kufuzu kikweli.
Rudi kwenye Sura
6. Na miongoni mwa watu wapo ambao hununua maneno ya uwongo
wawasimulie watu wapate kuwatenga na Uislamu na Qur'ani kwa kutojua dhambi
zilio juu yao, na wanaifanyia maskhara Dini ya Mwenyezi Mungu na Ufunuo
wake. Watendayo hayo watapata adhabu ya kuwatia unyonge na kuwadhalilisha.
Rudi kwenye Sura
7. Na mpotovu kama huyu akisomewa Aya za Mwenyezi Mungu huzipuuza
kwa kiburi. Hali yake kwa haya ni hali ya ambaye hasikii, kama kwamba ana
uziwi katika masikio yake. Basi mwonye kuwa hakika Mwenyezi Mungu amemuandalia
adhabu yenye machungu makali.
Rudi kwenye Sura
8. Hakika walio amini na wakatenda vitendo vyema watapata Bustani
zenye neema.
Rudi kwenye Sura
9. Watabaki humo daima dawamu; Mwenyezi Mungu amewaahidi ahadi isiyo
vunjika. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mshindi wa kila kitu, Mwenye hikima katika
maneno yake na vitendo vyake.
Rudi kwenye Sura
10. Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu zisio na nguzo za nyinyi kuziona.
Na juu ya ardhi ameweka milima iliyo simama imara, ili ardhi isikutingisheni.
Na humo katika ardhi ametawanya kila namna ya wanyama wanao tambaa na kwenda.
Na tumeteremsha maji kutoka mbinguni, na tukaotesha mimea ya kila namna
nzuri yenye manufaa katika ardhi.
Rejea uangalie maelezo ya kisayansi juu ya Aya 2, Sura ya Ar-Raa'd.
Rudi kwenye Sura
11. Hivi viumbe vya Mwenyezi Mungu vipo mbele yenu, basi hebu nionyesheni
walicho umba hao mnao wafanya ni miungu badala yake Yeye hata wawe ni washirika
wake! Bali madhaalimu - kwa ushirikina wao - wamo katika upotovu ulio wazi.
Rudi kwenye Sura
12. Na hakika tulimpa Luqman hikima, na ilimu, na kauli ya kusibu.
Tulimwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema aliyo kupa. Na mwenye kushukuru
basi hakika huyo anaitafutia kheri nafsi yake. Na mwenye kuzikufuru neema,
akazikataa, na asishukuru kwa ajili yake, basi kwa hakika Mwenyezi
Mungu si mwenye kuihitaji shukra yake, na Yeye Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kustahiki sifa zote njema, na ingawa pasiwepo hata mmoja wa kumsifu.
Rudi kwenye Sura
13. Taja pale Luqman alipo mwambia mwanawe: Ewe mwanangu! Usimshirikishe
Mwenyezi Mungu na yeyote. Hakika kumshirikisha Mwenyezi Mungu ni dhulma
kubwa, kuwaweka sawa Mwenye kustahiki na asiye stahiki.
Waarabu walikuwa wanawajua watu wawili kwa jina hili. Mmoja wapo
ni Luqman bin A'adi. Nao walikuwa wakimtukuza cheo kwa werevu wake, uraisi,
ujuzi, ufasihi na ujanja. Na walikithiri sana kumtaja na kumpigia
mithali, kama inavyo onekana katika vitabu vya Kiarabu vingi.
Ama mwengine ni huyo anaye itwa Luqman Alhakim, (Mwenye hikima),
aliye kuwa mashuhuri kwa hikima yake na mifano yake, na ambaye Sura hii
ya Qur'ani imeitwa kwa jina lake. Na hikima zake zilikuwa zimeenea kwa
Waarabu. Ibn Hisham amesimulia kwamba Suwaid bin Ass'amit alifika Makka.
Naye alikuwa mtu mtukufu kwa watu wake. Mtume s.a.w. akamtaka asilimu.
Suwaid akasema: Huenda labda uliyo nayo wewe ndiyo kama niliyo nayo mimi.
Mtume s.a.w. akasema: Nini ulicho nacho? Akasema: Majalla ya Luqman. Mtume
s.a.w. akasema: Nisomee. Akamsomea. Tena akasema: Hakika haya maneno mazuri.
Na niliyo nayo mimi ni bora zaidi, nayo ni Qur'ani aliyo niteremshia Mwenyezi
Mungu, nayo ni Uwongofu na Nuru. Mtume s.a.w. akamsomea Qur'ani na akamtaka
asilimu.
Na pia Imam Malik ametaja kwa wingi hikima za Luqman katika kitabu
chake, Al Muwatt'a. Na baadhi ya vitabu vya Tafsiri ya Qur'ani na Adab
(maandishi ya ufasihi wa lugha) vimetaja namna mbali mbali katika hikima
hizo.
Kisha baadae ikakusanywa mithali kwa visa katika kitabu chenye jina
la Mithali za Luqman. Lakini kwa sababu ya udhaifu wa mpango wake, na wingi
wa makosa ya nahau na sarfu, na kuwa kutopokewa kitabu cha jina hili katika
vitabu vya Waarabu wa kale, yatilia nguvu kuwa hichi kimezuliwa tu katika
zama za mwisho.
Na maoni yanayo gongana juu ya uhakika wa Luqman Al-hakim: ni kuwa
yeye ni Mnubi katika watu wa Abla au Uhabeshi, au mtu mweusi wa Sudan ya
Misri, au ni Muibrani. Na wengi walio mtaja wanakubaliana kuwa hakuwa Nabii.
Wachache tu ndio wanasema kuwa alikuwa Nabii. Na tunalo weza kutambua katika
yaliyo tajwa ni kuwa hakuwa Mwaarabu, kwa sababu wote wamewafikiana kwa
hayo. Na kwamba alikuwa ni mtu mwenye hikima, na hakuwa Nabii, na kwamba
ameingiza miongoni mwa Waarabu hikima mpya zikawa zinatajwa mara nyingi
kama ilivyo onekana baadae katika vitabu.
Rudi kwenye Sura
14. Na tumemuamrisha mtu awafanyie wema wazazi wake, na mama
yake ampe fungu kubwa zaidi. Kwani yeye alimbeba katika mimba kwa udhaifu
unao zidi kila siku kidogo kidogo. Na tena kamnyonyesha muda wa miaka miwili
ndipo alipo muachisha ziwa. Na tumemuusia: Mshukuru Mwenyezi Mungu
na wazazi wako. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo kwa ajili ya hisabu na
malipo.
Rudi kwenye Sura
15. Na ikiwa wazazi wako wakikushikilia kwa juhudi umshirikishe Mwenyezi
Mungu na vitu usivyo vijua kuwa vinastahiki kuabudiwa, basi usiwakubalie.
Lakini endelea na kusuhubiana nao duniani kwa wema na ihsani. Na fuata
njia ya wanao rejea kwangu kwa Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja,
na Ikhlasi, usafi wa niya na vitendo. Kisha nyote mtarejea kwangu, na nitakupeni
khabari ya mliyo kuwa mkiyatenda, ya kheri na shari, ili nipate kukulipeni
kwayo.
Rudi kwenye Sura
16. Ewe mwanangu! Hakika wema au ubaya kwa mtu, hata ukiwa, mathalan,
kwa udogo wake kama chembe ya khardali, iliyoko pahali palipo fichikana
kabisa, kama ndani ya jabali, au ndani ya mbingu, au chini ya ardhi, Mwenyezi
Mungu ataufichua na autolee hisabu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo
fichika, hakifichikani kitu hata kidogo kwake, ni Mwenye khabari ya kujua
hakika ya kila kitu.
Rudi kwenye Sura
17. Ewe mwanangu! Zihifadhi Sala, na amrisha kila wema, na kataza
kila baya, na stahamili kwa shida zinazo kusibu. Hakika anayo usia Mwenyezi
Mungu ni katika mambo ambayo yanahitajia kufanyiwa hima na kuyashikilia.
Rudi kwenye Sura
18. Wala usiwageuzie watu uso wako kwa takaburi, wala usitembee
katika nchi kwa kujiona na majivuno. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila
mwenye kuringa na kujiona.
Rudi kwenye Sura
19. Na nenda mwendo wa wastani, si mbio mbio mno wala taratibu mno.
Na teremsha sauti yako. Kwani hapana sauti mbaya kama sauti ya punda. Inaanzia
kwa mngurumo unao ghasi, na inaishia kwa ukenje unao kera.
Rudi kwenye Sura
20. Mmeona kwamba Mwenyezi Mungu amekudhalilishieni viliomo mbinguni
kama jua, na mwezi, na nyota na vyenginevyo; na viliomo katika ardhi, kama
mito, na matunda, na wanyama. Naye amekutimizieni neema zake zilio dhaahiri
na zilio sitirika, msizo ziona. Na miongoni mwa watu, wapo wanao jadiliana
juu ya dhati ya Mwenyezi Mungu na sifa zake bila ya dalili wala uwongozi
ulio pokewa kutokana na Nabii au Wahyi (ufunuo) wenye kumurika kwa mwangaza
njia ya Haki.
Rudi kwenye Sura
21. Na pindi wakiambiwa: Fuateni Haki na Uwongofu alio uteremsha
Mwenyezi Mungu, wao husema: Bali sisi tunafuata tuliyo wakuta nao baba
zetu. Je! Wanawafuata hao, ijapo kuwa Shetani ndio anawaitia wende kwenye
upotovu utakao waingizia Motoni?
Rudi kwenye Sura
22. Na mwenye kumuelekea Mwenyezi Mungu kwa moyo wake na uso wake,
na akamwakilisha Yeye mambo yake yote, naye akawa ni mwenye kutenda vitendo
vyema, basi amefungamana na sababu za nguvu kabisa za kumfikisha kwenye
radhi ya Mwenyezi Mungu. Na kwake Yeye, Subhanahu, ndio marejeo ya mambo
yote.
Rudi kwenye Sura
23. Na asiye mtakasia Mwenyezi Mungu dhati yake na nafsi yake, basi
usikuhuzunishe upinzani wake na mapuuza yake. Kwetu Sisi peke yetu ndio
marejeo yao Siku ya Kiyama. Hapo tutawaonyesha vitendo vyao. Kwani Sisi
tumezunguka kwa kuvijua viliomo ndani ya nafsi zao, seuze vitendo vyao
vya dhaahiri.
Rudi kwenye Sura
24. Tunawastarehesha kwa muda mchache katika dunia yao, kisha tutawalazimisha
kwenda kwenye adhabu kali isiyo stahimilika.
Rudi kwenye Sura
25. Ewe Nabii! Nakuapia ya kuwa ukiwauliza: Nani aliye umba mbingu
na ardhi? Hapana shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Sifa njema zote
ni za Mwenyezi Mungu, aliye ziweka dalili za Upweke wake hata zikaubomoa
ushirikina wao wa kumshirikisha na wenginewe katika ibada. Na lakini wengi
wao hawajui ya kuwa kwa kukiri kwao huku, basi wamesimamisha hoja ya kuwapinga
wenyewe kwa ubovu wa itikadi yao.
Rudi kwenye Sura
26. Viliomo katika mbingu na ardhi ni vya Mwenyezi Mungu, kwa kuviumba,
na kuvikadiria, na kuvipanga. Basi vipi wao wanaacha kumuabudu Yeye? Na
Mwenyezi Mungu Aliye takasika si mhitaji wa viumbe vyake wala ibada yao.
Yeye ni Msifiwa kwa dhati yake. Ni mwenye kustahiki kusifiwa na waja wake.
Rudi kwenye Sura
27. Na lau kuwa miti yote ya duniani ikageuka kalamu, na maji yote
ya baharini kwa wingi wake yakageuka wino, kuandikia maneno ya Mwenyezi
Mungu, basi zingeli kwisha kalamu na wino ukamalizika kabla ya kumalizika
maneno ya Mwenyezi Mungu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu,
hashindwi na chochote, Mwenye hikima hakimfutu kitu katika ujuzi wake na
hikima yake. Basi hayeshi maneno yake na hikima yake.
Rudi kwenye Sura
28. Kukuumbeni nyinyi hapo mwanzo na kukufufueni baada ya kufa, mbele
ya uweza wa Mwenyezi Mungu si chochote ila ni kama kumuumba na kumfufua
mtu mmoja tu. Hakika Mwenyezi Mungu anaisikia kauli ya washirikina wanapo
sema ati: Hakuna kufufuliwa. Naye ni Mwenye kuviona vitendo vyao, naye
atawalipa kwavyo.
Rudi kwenye Sura
29. Je! Huangalii, ewe mwenye jukumu, kwa maangalio ya mwenye kuzingatia,
ya kwamba hakika Mwenyezi Mungu huupunguza wakati wa usiku kwa kadri ya
anavyo uongeza mchana? Na anaupunguza mchana kwa kadri ya anavyo uzidisha
usiku? Naye amedhalilisha jua na mwezi kwa ajili ya maslaha yenu, na amefanya
hayo yafuate mpango wa peke yao. Basi kila moja katika hayo huenda katika
njia maalumu ya mbinguni wala haigeuki. Na mwendo huo unaendelea mpaka
Siku ya Kiyama. Na hakika Yeye, Subhanahu, anazo khabari za yote myatendayo,
na ni Mwenye kukulipeni kwayo.
Rudi kwenye Sura
30. Hayo yaliyo tajwa ni katika ajabu za uundaji wa Mwenyezi Mungu
na uweza wake, kwa sababu muundaji wake ni Mungu aliye thibiti Ungu wake,
Mwenye kustahiki peke yake kuabudiwa, na kwamba miungu yote mnayo iabudu
badala yake ni miungu ya uwongo. Na hakika Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye
Mtukufu wa shani, Mkubwa wa utawala.
Rudi kwenye Sura
31. Ewe mtu! Huzitazami marikebu, vyombo vinavyo kwenda baharini
kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, vikichukua ndani yake bidhaa za kukupeni
manufaa, ili Mwenyezi Mungu akuonyesheni baadhi ya maajabu ya uundaji wake,
na dalili za uweza wake? Hakika katika hayo zimo Ishara kwa kila mwenye
kuvumilia mitihani yake, mwenye kuzishukuru kwa neema zake.
Rudi kwenye Sura
32. Hawa makafiri wanao mkataa Mwenyezi Mungu wakipanda marikebu,
na bahari ikawachafukia, na mawimbi yakaja juu mpaka wakaona yatawafunika,
na wakawa yakini watazama bila ya muhali, humkimbilia Mwenyezi Mungu, wakimwomba
kwa ikhlasi na unyenyekevu, awaokoe. Basi akisha waokoa wakafika nchi kavu
wapo kati yao wachache wanao kumbuka ahadi yao, na wakenda mwendo wa sawa.
Na wapo kati yao, nao ndio wengi, walio sahau fadhila za Mola wao Mlezi,
na wakaendelea na kumkataa. Na wala hakatai fadhila za Mola wake Mlezi
na hisani yake ila kila mtu aliye mwingi wa ukhaini, aliye pita mpaka kumkanya
Mola wake Mlezi.
Rudi kwenye Sura
33. Enyi watu! Fanyeni aliyo kuamrisheni Mola wenu Mlezi, na wacheni
aliyo kukatazeni. Na tahadharini na adhabu yake ya Siku ya Kiyama, Siku
ambayo kwamba mzazi hatamfaa mwanawe kwa lolote, wala mwana hatamfaa mzazi
wake kwa lolote. Hakika Siku hii ndiyo aliyo iahidi Mwenyezi Mungu. Na
ahadi yake ni ya kweli, hayendi kinyume. Basi yasikupumbazeni mapambo ya
dunia na uzuri wake, mkaacha kujitayarisha kwa ajili ya Siku hiyo. Wala
msikhadaike na uchochezi wa Shetani, ukakuachisheni kumuelekea Mwenyezi
Mungu na kumt'ii.
Rudi kwenye Sura
34. Hakika ujuzi wa Saa ya Kiyama uko kwa Mwenyezi Mungu umethibiti.
Basi hapana anaye ijua isipo kuwa Yeye tu. Na Yeye huteremsha mvua kwa
wakati wake alio uweka. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi,
kama wanaume, au wanawake, hivyo viliomo vimetimia au havikutimia
mimba. Wala hapana mtu ajuaye, mwema na muovu, atapata nini kesho, kama
kheri au shari. Wala hapana mtu ajuaye pahala gani duniani itamfika ajali
yake ya kufa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye timia ujuzi wake na
kuwa na khabari ya kila kitu. Wala hapana yeyote awezae kujua siri yake.
Rudi kwenye Sura