1. Sura hii imeanzia kwa Aya hii ili kufahamisha kwamba
Qur'ani imetungwa kwa hizi hizi harufi wanazo zitamka Waarabu kwa
wepesi na kwa uwazi. Lakini wanao kanya wameshindwa kuleta mfano wake.
Nazo vile vile zinawazindua watu wasikilize na wanyamaze, na ziwapelekee
kuusadiki Utume wa Muhammad s.a.w.
Rudi kwenye Sura
2,3. Waajemi waliwashinda Warumi katika nchi ya karibu na Arabuni,
nayo ni mipakani mwa Shamu. Nao Warumi baada ya kushindwa kwao watakuja
washinda Waajemi...
Rudi kwenye Sura
4,5... kabla ya kupita miaka tisa. Na washirikina walifurahi kwa
kushinda Waajemi, na wakawaambia Waislamu: Tutakushindeni kama Uajemi ilivyo
ushinda Urumi ambayo ni katika Watu wa Kitabu. Lakini Mwenyezi Mungu alitimiza
ahadi yake, Warumi wakawashinda Waajemi kwa muda ule ule alio utaja. Ikawa
ile ni Ishara ya ukweli wa Muhammad s.a.w. katika wito wake, na ukweli
wa aliyo yaleta. Ni ya Mwenyezi Mungu amri na hukumu kabla ya kila kitu
na baada ya kila kitu. Na siku ya Warumi kuwashinda Waajemi watafurahi
Waumini kwa ajili ya ushindi wa Mwenyezi Mungu anao mpa amtakaye. Na Yeye
ndiye Mwenye kuwashinda maadui zake, Mwenye kuwarehemu vipenzi vyake.
Maoni ya wataalamu juu ya Aya 1-4:
Katika Aya hizi tukufu ipo ishara ya vituko viwili. Cha kwanza kilikwisha
tokea khasa. Na cha pili kilikuwa bado hakijatokea, na hayo
ni kutoa khabari ya ghaibu. (Na imetajwa kuwa yatatokea mnamo miaka michache,
ambayo maana yake ni mitatu mpaka tisa.)
Na maelezo ya tukio la mwanzo ni kuwa Waajemi na Warumi walipambana
kwa vita katika nchi ya Shamu katika enzi za Khasro Abrawiz, au Khasro
wa Pili, Mfalme wa Uajemi, maarufu kwa Waarabu kwa jina la Kisra,
na Heraklius Mdogo, Mfalme wa Wafalme wa Kirumi, ambaye kwa Waarabu ni
maarufu kwa jina la Heraklu. Katika mwaka 614 Uajemi iliiteka Antiokia,
mji mkubwa kabisa katika jimbo la Mashariki katika Ufalme wa Rumi, na baadae
ikatekwa Dimishqi (Damask), na ukazingwa mji wa Baitul Muqaddas (Yerusalemu)
mpaka ukasalimu amri. Wakauunguza, wakawaingilia wakaazi wake kuwachinja.
Moto huo uliteketeza Kanisa la Kiyama. Wavamizi hao waliuchukua Msalaba
wakaupeleka kwenye jiji lao. Nyoyo za Wakristo zilihuzunika sana kwa msiba
huu wa kutisha. Ilivyo kuwa kushindwa huku kuliwaletea furaha washirikina
wa Makka na wakawa wanawafanyia tashtiti Waislamu kwa kuwa Warumi ni Watu
wa Kitabu kama watu wa Muhammad s.a.w., na Waajemi kama washirikina si
Watu wa Kitabu, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye tukuka alimteremshia
Muhammad Aya hizi zilizo wazi ili ambashirie kuwa Watu wa Kitabu watakuja
shinda, nao Waumini watafurahi. Na kushindwa kwa washirikina na uovu wa
khatima yao kuliwekewa kiwango cha miaka michache.
Na ufafanuzi wa tukio la pili ni kuwa Heraklu, Kaisari wa Rumi,
ambaye jeshi lake lilishindwa, hakukata tamaa kuwa atashinda. Akawa anajiandaa
kwa ajili ya mpambano utakao futa ari ya kushindwa. Mpaka mwaka wa 622
wa kuzaliwa Nabii Isa a.s. , yaani mwaka wa kwanza wa Hijra Waajemi wakalazimika
kuingia vita katika nchi ya Arminia. Huko Warumi wakashinda. Na ikawa hapo
ndio chanzo cha ushindi mara nyingi wa Rumi kuishinda Uajemi. Ndio hivi
Watu wa Kitabu wakawashinda washirikina, na ukweli wa bishara ya Qur'ani
ukathibiti.
Na tena kituko cha tatu kinafahamika kwa maana kutokana na Aya hizi
tukufu, nacho kikaleta furaha kwa Waislamu. Nacho ni kushinda kwao kuwashinda
washirikina Makureshi katika Vita vya Badri vilivyo tokea siku ya Ijumaa,
17 Ramadhani mwaka wa pili wa Hijra, yaani mwaka 623 wa kuzaliwa Nabii
Isa a.s.
Rudi kwenye Sura
6. Mwenyezi Mungu ameagana na Waumini kwa agano la kweli. Na Mwenyezi
Mungu havunji agano lake. Lakini makafiri, wanao kataa, si ada yao kujua
mambo hakika yalivyo.
Rudi kwenye Sura
7. Wanajua mambo na njia za kuamirisha na kustarehe na mapambo yake,
na hali wao wamepita mpaka katika ujinga na kughafilika kujitengenezea
Akhera yao.
Rudi kwenye Sura
8. Yamefutwa macho yao na nyoyo zao, na hivyo hawajifikirii mambo
yaliyo khusiana na roho zao wakaujua mwisho wao. Mwenyezi Mungu hakuziumba
mbingu na ardhi na nyota na vinginevyo viliomo baina yao ila kwa kweli
kweli, si mchezo, na kwa wakati ulio wekewa kiwango chake maalumu kitakacho
kwisha. Na hakika wengi wa watu wanakataa kuwa watakuja kukutana na Mwenyezi
Mungu, na kwamba itakuwapo Saa ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
9. Wao wameshikilia kukaa katika nchi zao tu, wala hawendi kote kote
duniani wapate kushuhudia ulikuwaje mwisho wa walio kufuru wa kabla yao.
Hao walikuwa na nguvu zaidi kuliko hawa makafiri wa sasa, na wakaugeuza
uso wa ardhi wapate kutoa humo viliomo ndani yake, kama maji, na maadeni,
na makulima. Na wakaiamirisha ardhi zaidi kuliko walivyo amirisha hawa.
Na Mitume wa Mwenyezi Mungu wakawajia na miujiza iliyo wazi, na wao wakaikataa.
Mwenyezi Mungu akawatia mkononi, kwani Yeye hawalipi bila ya makosa, wala
hawashiki kabla ya kuwakumbusha na kuwapa muhula. Lakini watu hawakuwa
wanadhulumu ila nafsi zao tu.
Rudi kwenye Sura
10. Tena mwisho wa hao watu walio tenda hadi ya uovu ni kuzikataa
Ishara za Mwenyezi Mungu, na wakawa wanazidharau khasa.
Rudi kwenye Sura
11. Mwenyezi Mungu, aliye takasika na kutukuka, huanzisha uumbaji
wa binaadamu tangu mwanzo. Kisha hurejea tena kuwaumba baada ya kwisha
kufa kwao. Tena hao wote wanarejea kwake Yeye peke yake kwa ajili ya hisabu
na malipo.
Rudi kwenye Sura
12. Na kikifika Kiyama makafiri watakata tamaa ya kuweza kujitetea
nafsi zao.
Rudi kwenye Sura
13. Na wala hawapatikani waombezi kutokana na hao walio waabudu badala
ya Mwenyezi Mungu na kwa sababu yao wakawa ni makafiri duniani.
Rudi kwenye Sura
14. Na itapo simama Saa, yaani Siku ya Kiyama, kila kikundi kitaendea
kwenye ajali yake ya milele.
Rudi kwenye Sura
15. Ama walio amini, na wakaambatisha Imani yao na vitendo vyema,
basi hao watakuwa katika Bustani yenye miti na mauwa, watafurahi na wataneemeka.
Rudi kwenye Sura
16. Ama wale walio kufuru, na wakazikataa Ishara zetu na mkutano
wa kufufuliwa na kuhisabiwa, basi hao watakuwa wanaishi katika adhabu,
wala hawatoki humo.
Rudi kwenye Sura
17. Basi mtakaseni Mwenyezi Mungu na kila ambacho hakimuelekei kwa
utukufu wake na ukamilifu wake. Na muabuduni Yeye mnapo ingia jioni na
mnapo ingia asubuhi.
Rudi kwenye Sura
18. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye kustahiki kuhimidiwa
na kusifiwa na kushukuriwa na walioko katika mbingu na katika ardhi. Basi
mhimidini na mumuabudu wakati wa alasiri na mnapo ingia adhuhuri.
Rudi kwenye Sura
19. Yeye hutoa kiumbe kihai kutokana na kitu kisicho kuwa na uhai.
Na hukitoa kitu kisicho kuwa na uhai kutokana na kitu chenye uhai. Na huihuisha
ardhi kwa mimea baada ya kuwa ni kavu tupu. Na mfano wa anavyo fanya hivi
basi ndivyo hivyo Mwenyezi Mungu atakutoeni makaburini mwenu.
Rudi kwenye Sura
20. Na katika dalili za kuonyesha ukamilifu wa uweza wake ni kuwa
ameumba asili yenu kutokana na udongo usio kuwa na uhai. Kisha nyinyi mmekuwa
watu mlio tawanyika katika ardhi kwa ajili ya kutafuta kitacho kuleteeni
kubaki kwenu.
Rudi kwenye Sura
21. Na katika dalili za rehema yake ni kuwa kakuumbieni, enyi wanaume,
wake wa jinsi yenu mkae nao kwa uzuri na kituo. Na amekujaalieni baina
yenu na wao mapenzi na kuoneana huruma. Hakika katika haya bila ya shaka
zipo dalili kwa watu wanao ufikiria uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Rudi kwenye Sura
22. Na katika dalili za kuonyesha uweza wake na hikima yake ni uumbaji
wa mbingu na ardhi kwa mpango huu wa namna peke yake wenye kupendeza, na
kukhitalifiana ndimi zenu katika lugha mbali mbali na lafdhi mbali mbali,
na kutafautiana rangi zenu katika weusi na weupe na nyenginezo. Hakika
katika haya bila ya shaka zipo dalili zinazo wanufaisha watu wenye ujuzi
na kufahamu.
Rudi kwenye Sura
23. Na katika Ishara zake zenye kuonyesha ukamilifu wa uweza wake
ni kuwa amekupeni sababu za mapumziko kwa kulala kwenu. na akakusahilishieni
kutafuta riziki usiku na mchana kutokana na fadhila zake kunjufu. Hakika
katika haya bila ya shaka zipo dalili kwa watu wanao nafiika kwa wanayo
yasikia.
Rudi kwenye Sura
24. Na katika Ishara zake ni kuwa anakuonyesheni umeme katika mawingu,
muone khofu kwa radi na tamaa ya kupata mvua ya kuteremka kutoka mbinguni
ili ardhi ihuike baada ya kuyabisika. Hakika katika hayo bila ya shaka
zipo dalili kwa watu wanao zingatia mambo wakayafahamu kama ifaavyo.
Rudi kwenye Sura
25. Na katika dalili za ukamilifu wa uweza wake, na hikima yake,
na ukunjufu wa rehema yake, ni kuwa mbingu na ardhi zimesimama kwa amri
ya Mwenyezi Mungu, kama muonavyo, kwa mujibu wa hukumu za ufundi na ustadi
wa kupanga. Kisha akikuiteni kwa ajili ya kukufufueni mtatoka makaburini
mbio mbio kuitikia wito wake.
Rudi kwenye Sura
26. Na ni vyake Mwenyezi Mungu Subhanahu vyote viliomo katika mbingu
na ardhi, kwa kuviumba, na kuvimiliki, na kunyenyekea. Vyote ni vyenye
kumt'ii Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
27. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu aliye umba viumbe vyote bila ya ruwaza,
kisha atavirudisha tena baada ya mauti. Na kurudisha kwake ni jambo jepesi
zaidi kuliko kuvizua mwanzo, kwa mujibu wa nadhari ya vipimo vyenu na itikadi
yenu, kwamba kukirudisha kitu ni sahala kuliko kukizua. Na Mwenyezi Mungu
ana sifa ya kutangulia ya shani ya namna ya pekee katika uweza ulio kamilika,
na hikima iliyo timia, katika mbingu na ardhi. Na Yeye ni Mwenye kushinda
katika ufalme wake, Mwenye hikima katika vitendo vyake na kukadiria kwake.
Rudi kwenye Sura
28. Mwenyezi Mungu amekupigieni mfano unao tokana na nafsi zenu -
na Mwenyezi Mungu Mtukufu Mwenye kutukuka amempigia mfano huo huyo aliye
wafanya viumbe ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Mfano wenyewe ni: Kwani
nyinyi mnawafanya watumwa wenu washirika katika mali na vyenginevyo tulivyo
kupeni? Basi, je! Nyinyi na wao ni sawasawa katika hayo, mnawaogopa hao
watumwa wenu, na hamfanyi kitu kwa mnavyo miliki bila ya ruhusa yao, kama
wanavyo ogopana waungwana wao kwa wao? Ikiwa nyinyi hamyatii akilini haya
wala hamyafanyi, basi imekuwaje hata mnavifanya baadhi ya alivyo vimiliki
Mwenyezi Mungu kuwa ni washirika wake? Kwa ufafanuzi kama huu tunawabainishia
Aya watu ambao wanazingatia mifano inayo pigwa.
Rudi kwenye Sura
29. Bali walio kufuru wanafuata pumbao zao bila ya kujua matokeo
ya kufuru zao. Basi hapana yeyote aliye achiliwa na Mwenyezi Mungu kupotoka,
atakaye ongoka. Wala hapana ataye waombea, na akawalinda na adhabu.
Rudi kwenye Sura
30. Basi elekeza uso wako, na uelekee kwenye Dini mbali na upotovu
wao. Na shikamana na maumbile ya Mwenyezi Mungu aliyo waumbia watu. Nayo
ni kuwa wao ni wenye kuikubali Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja,
wala si wenye kuikataa. Na haitakikani kuigeuza khulka hii. Huko ndio kuumbwa
juu ya Tawhidi, nayo ndiyo Dini Iliyo Nyooka sawasawa. Lakini washirikina
hawaujui ukweli huo.
Rudi kwenye Sura
31. Kuweni wenye kurejea kwake kwa kutubu! Na tendeni aliyo kuamrisheni,
na acheni aliyo kukatazeni. Na hifadhini Sala, wala msiwe katika wenye
kumuabudu mwenginewe pamoja na Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
32. Katika walio igawanya dini yao, wakawa makundi mbali mbali, kila
kikundi kinawania upande wake, na kila fungu miongoni mwao linafurahia
kwa waliyo nayo, wanajidhania kuwa wao tu ndio wako katika haki.
Rudi kwenye Sura
33. Na watu yakiwapata madhara, ya ugonjwa au shida yoyote, humkimbilia
Mwenyezi Mungu, na wakamwomba nao wamerejea kwake, wakitaka waondolewe
hiyo shida. Kisha akiwaonjesha kuondokewa na hiyo shida, na akawapa sehemu
ya fadhila yake, baadhi yao hukimbilia mbio kwendea kumshirikisha Mola
wao Mlezi.
Rudi kwenye Sura
34. Upate kuwa mwisho wa mambo yao kuzikanya neema za Mwenyezi Mungu
alizo wapa. Basi enyi makafiri mnao kataa! Stareheni kama mpendavyo. Mtakuja
ujua mwisho wenu.
Rudi kwenye Sura
35. Kwani tuliwaacha katika upotovu wao, wala hatukuwazindua na ndoto
zao, bali tukawateremshia hoja ya kushuhudia kwa yale walio kuwa wakiyashirikisha
na Mwenyezi Mungu?
Rudi kwenye Sura
36. Na tukiwaonjesha watu neema huifurahia kwa furaha ya kuwatia
kiburi. Na ikiwapata shida kwa madhambi waliyo yachuma wenyewe huwa wepesi
wa kukata tamaa na Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema.
Rudi kwenye Sura
37. Je! Wameingiwa na ujinga hata hawajui nini kinacho fikisha kwenye
Imani? Wala hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye,
na humdhikisha amtakaye, kwa mujibu inavyo wafikiana na hikima yake? Hakika
katika hayo zipo dalili wazi kwa watu wanao iamini Haki.
Rudi kwenye Sura
38. Na ilivyo kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye anaye kunjua riziki
na akaidhikisha, basi mpe aliye jamaa haki yake kwa ajili ya hisani na
kuunga udugu. Na mhitaji na aliye katikiwa safari yake wape pia haki zao
kutokana na Zaka na Sadaka. Hayo ndiyo ya kheri kwa wenye kutaka radhi
ya Mwenyezi Mungu, na wanataka thawabu zake. Na hao ndio wenye kufuzu kuipata
neema ya milele.
Rudi kwenye Sura
39. Na mnacho toa, enyi wala riba, katika mali ili yakuzidieni kutokana
na mali yao, basi kwa Mwenyezi Mungu hakizidi wala hakiingii baraka. Na
mnacho toa sadaka kwa kutafuta wajihi wa Mwenyezi Mungu, bila ya riya,
kujionyesha tu, wala tamaa ya kulipwa - basi hao ndio watakao pewa malipo
mema marudufu.
Rudi kwenye Sura
40. Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Aliye takasika, ndiye aliye kuumbeni.
Kisha akakupeni cha kukupeni maisha. Kisha ndiye anaye kufisheni; na kisha
atakufufueni kutoka makaburini kwenu. Je! Yupo yeyote katika hao miungu
wa kishirikina mnao dai, na mkawaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, mwenye
kutenda hayo, ya kuumba, na kuruzuku, na kufisha, na kufufua, au kitendo
chochote? Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mshirikisha
naye.
Rudi kwenye Sura
41. Kumetokea moto, na ukame, na kila maafa, na kuharibika biashara,
na mafuriko, kwa sababu ya uovu na madhambi, ili Mwenyezi Mungu awaadhibu
watu duniani kwa baadhi ya vitendo vyao, huenda labda wakatubia maasi yao.
Rudi kwenye Sura
42. Ewe Nabii! Waambie washirikina: Nendeni pande mbali mbali za
dunia, muangalie vipi waliishia walio kutangulieni? Mtaona kuwa Mwenyezi
Mungu aliwaangamiza na akayaharibu majumba yao, kwa sababu wengi walikuwa
washirikina kama nyinyi.
Rudi kwenye Sura
43. Na uelekeze sawa sawa uso wako kwenye Dini iliyo kamilika kunyooka
kwake, kabla haijafika Siku ambayo hapana mtu atakaye weza kuirejesha
kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo watu watagawanyika, na hali zao zitakhitalifiana.
Rudi kwenye Sura
44. Mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu, basi itampata mwenyewe laana
ya ukafiri wake. Na wenye kuamini na wakatenda mema basi ni kwa ajili ya
nafsi zao tu, wanajitengenezea njia nzuri iliyo nyooka.
Rudi kwenye Sura
45. Kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu huwalipa walio amini na wakatenda
mema kwa yale waliyo yatanguliza. Na tena huwazidishia malipo yao kwa kuwafadhili.
Kwani Yeye anawapenda hao na anawachukia walio kufuru na wakazikanya neema
zake.
Rudi kwenye Sura
46. Na katika dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu na rehema yake ni
kuwa Yeye huzipeleka pepo za kubashiria mvua kwa sababu ya kumwagia mashambani
na kunyweshea wanyama na watu. Na ili akupeni katika kukumimieni hisani
zake manufaa yanayo tokana na mvua, na ili zipate kwenda marikebu za majini
kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kudra yake, na ili mtafute riziki kwa fadhila
yake kwa biashara na kutumia viliomo nchi kavu na baharini, na ili mpate
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa ut'iifu wenu na kumuabudu Yeye tu.
Rudi kwenye Sura
47. Na kabla yako hakika tulikwisha watuma Mitume kwa kaumu zao.
Na kila Mtume alikuja na hoja zilizo wazi, zenye kuonyesha ukweli wake.
Kaumu yake ikamkadhibisha. Nasi, basi, tukawaangamiza wale walio fanya
madhambi na wakaasi. Na Mwenyezi Mungu amejilazimisha nafsi yake kuwanusuru
waja wake Waumini.
Rudi kwenye Sura
48. Mwenyezi Mungu, Subhanahu Wataa'la, Aliye takasika na akatukuka,
ndiye anaye zituma pepo ambazo kwa nguvu zake zikayasukuma mawingu. Na
Mwenyezi Mungu akayatandaza mbinguni kama atakavyo hapa na kule, kwa uchache
au wingi. Na akayafanya mapande mapande. Basi nawe ndio unaona mvua inatoka
kwenye mawingu. Na Mwenyezi Mungu anapo iteremsha mvua kwa waja wake awatakao,
hao huwa wepesi kukunjuka roho na kufurahi.
Rejea kwenye maelezo ya Aya ya 43 ya Sura An-Nur.
Rudi kwenye Sura
49. Nao hakika kabla ya kunyweshewa na mvua hiyo walikuwa wamekwisha
kata tamaa na wamedawaa.
Rudi kwenye Sura
50. Basi iangalie mvua, muangalio wa kufikiri na kuzingatia, vipi
Mwenyezi Mungu anavyo ihuisha ardhi baada ya kuwa imetulia kama maiti.
Hakika aliye ihuisha ardhi baada ya kufa kwake bila ya shaka ni Muweza
wa kuwahuisha watu. Na Yeye ni mtimilivu wa uweza, hashindwi na kitu.
Rudi kwenye Sura
51. Nami ninaapa! Lau kuwa tukiwapelekea upepo wa kudhuru mimea,
nao wakauona umekuwa manjano kwa sababu yake, hapana shaka wataendelea
hata baada ya kuwa manjano, wakizikanya neema, na wakimkataa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
52. Basi wewe usihuzunike kwa inadi yao na kuto kukuitikia. Kwani
wewe huwezi kuwafanya maiti wausikie wito wako; wala kuwafanya viziwi wakusikie
unapo wanadia, wakizidi uziwi wao kwa wanavyo kukimbia kwa mapuuza.
Rudi kwenye Sura
53. Na watu hawa ni kama vipofu, kwa vile nyoyo zao zimefungika hawafuati
uwongofu. Na wewe huwezi kuwaongoa vipofu, na ukawazuia wasifanye ukafiri
wao. Ama hakika wewe unaweza kuwafanya wakusikie msikio wa kufahamu na
kukubali wale ambao nyoyo zao zimejitayarisha kupokea Imani. Basi hao wanaifuata
Haki inapo dhihiri.
Rudi kwenye Sura
54. Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni kutokana na tone la manii,
mkawa dhaifu, hamna nguvu. Kisha akakujaalieni baada ya unyonge huo mkawa
na nguvu. Akakukuzeni hata mkawa watu wazima. Kisha akakufanyeni
baada ya nguvu hizi mkawa na udhaifu wa uzee na ukongwe. Yeye huumba atakavyo.
Na Yeye ndiye Mjuzi wa kupanga uumbaji wake, Muweza wa kuleta atakacho.
Rudi kwenye Sura
55. Na Siku itapo fika Saa ya Kiyama makafiri wataapa kwamba hawakukaa
duniani au makaburini mwao isipo kuwa kwa muda wa saa moja tu. Na mfano
wa mwendo kama huo ndivyo Mashetani walikuwa wakiwaendesha duniani, kuwaachisha
Haki na kuwapeleka kwenye upotovu.
Rudi kwenye Sura
56. Na walio pewa ujuzi na Mwenyezi Mungu, nao ni Manabii, na Malaika,
na Waumini, watasema: Bila ya shaka nyinyi mlikwisha kaa katika hukumu
ya Mwenyezi Mungu na amri yake mpaka Siku ya kufufuliwa. Basi hii ndiyo
Siku ya kufufuliwa mlio ikanya. Na lakini nyinyi duniani mlikuwa hamjui
kama hii ni Haki, kwa ujinga wenu na mapuuza yenu.
Rudi kwenye Sura
57. Basi Siku hiyo watafufuliwa watu. Hakutowafaa kitu makafiri
kutoa udhuru wao kwa kukanya kwao na kuwakadhibisha kwao Mitume wao. Wala
hatawataka mtu yeyote wafanye jambo la kumridhi Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa
wao wamekwisha dharaulika mbele yake, na wamefukuzwa kutokana na rehema
yake.
Rudi kwenye Sura
58. Na kwa ajili ya uwongofu wa watu, tumebainisha katika Qur'ani
hii kila mfano wa kuwaongoza kwenye Njia ya Uwongofu. Na wewe ukiwaletea
kila muujiza bila ya shaka makafiri, kwa kupita hadi inda yao na ugumu
wa nyoyo zao, watasema: Wewe na hao wanao kufuata si chochote
ila ni waongo tu katika huo wito wenu.
Rudi kwenye Sura
59. Na muhuri kama huu umepigwa juu ya nyoyo za hao wasio ijua Tawhidi
miongoni mwa majaahili.
Rudi kwenye Sura
60. Ewe Nabii, yavumilie maudhi yao. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu
kukupa ushindi juu ya maadui wako, na kushinda kwa Uislamu juu ya dini
zote, ni kweli isiyo geuka kabisa. Wala wasio muamini Mwenyezi Mungu na
Mtume wake wasikuletee dhiki na ukaiacha subira.
Rudi kwenye Sura