1. Alif Lam Mim - Hizi ni harufi za kutamkwa na zikasikilizana,
zilizo letwa ili kubainisha kwamba hii Qur'ani yenye kuwaemea watu kuiiga
imetungwa kwa harufi hizi hizi mnazo ziweza kuzitamka vizuri. Na pia ni
kwa ajili ya kuwazindua wasikilizaji na wapate kuiangalia Haki.
Rudi kwenye Sura
2. Hivyo watu wanadhani kwamba wataachiliwa tu hivi hivi kwa sababu
ya kutamka kwao shahada mbili basi, bila ya kujaribiwa kwa mitihani na
shida ili utambulikane ukweli wa Imani yao? La, sivyo hivyo! Bali hapana
budi kutiwa mithanini.
Rudi kwenye Sura
3. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu alikwisha zijaribu kaumu zilizo
tangulia kwa kuwapa shida na namna mbali mbali za neema na mitihani,
ili yapate kuonekana yale ambayo Yeye anayajua tangu mwanzo, na awatengue
baina ya walio kuwa wakweli katika Imani yao, na waongo.
Rudi kwenye Sura
4. Wanadhani wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu na wanamuasi kwamba
watatuponyoka katika kukimbia kwao kuikimbia adhabu ya Mwenyezi Mungu na
malipo yake? Kuhukumu kwao huku ni kuovu mno!
Rudi kwenye Sura
5. Mwenye kuamini kufufuliwa, na akawa anataraji malipo ya Mwenyezi
Mungu, na anaikhofu adhabu yake, basi huyo Imani yake ni ya kweli. Basi
na aingie kwenye vitendo vyema. Kwani Siku iIliyo ahidiwa itakuja tu, hapana
hivi wala hivi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maneno ya waja, ni
Mwenye kuvijua vitendo vyao. Na atamlipa kila mmoja kwa anavyo stahiki.
Rudi kwenye Sura
6. Na mwenye kuwania jihadi kwa sababu ya kutukuza Neno la Mwenyezi
Mungu, na akapambana na nafsi yake ivumilie juu ya ut'iifu, basi malipo
ya jihadi yake yatamrudia mwenyewe. Na hakika Mwenyezi Mungu aliye takasika
si mhitaji wa ut'iifu wa walimwengu.
Rudi kwenye Sura
7. Na wale walio sifika kwa Imani na wakatenda mema hapana shaka
tutawaondolea makosa yao, na tutawasamehe, na tutawalipa bora ya malipo
kwa vitendo vyao vyema.
Rudi kwenye Sura
8. Na Mwenyezi Mungu amemuamrisha mwanaadamu afanye ukomo wa uwezo
wake kuwafanyia wema wazazi wake na kuwat'ii. Na wakikushikilia kumfanyia
shirki Mwenyezi Mungu - na hayo hayakubaliki katika ilimu wala akili -
basi usiwat'ii. Na marejeo ya viumbe vyote ni kwa Mwenyezi Mungu, na Yeye
atawaeleza waliyo yatenda duniani, na atawalipa kwayo.
Rudi kwenye Sura
9. Na walio msadiki Mwenyezi Mungu na Ujumbe wake, na wakatenda mema,
basi hao hapana shaka Mwenyezi Mungu atawaingiza pamoja na walio wema,
wapate malipo yao na wayastarehee.
Rudi kwenye Sura
10. Na miongoni mwa watu yupo ambaye husema kwa ulimi wake: Tumeamini.
Na akipata dhiki yoyote kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hukereka na akafitinika
hata katika dini yake. Wala haifikirii adhabu ya Mwenyezi Mungu ya Siku
ya Kiyama. Yeye huyo huwa kama kwamba anafanya mateso ya wanaadamu kuwa
sawa na adhabu ya Mwenyezi Mungu ya Akhera. Mwenyezi Mungu akiwanusuru
Waumini, akawapa ushindi kuwashinda maadui zao na wakapata ngawira, watu
hao wanao dhihirisha imani huja wakawaambia Waislamu: Sisi ni wenzenu katika
Imani. Basi hebu tupeni nasi fungu letu la ngawira. Wasidhani watu hawa
kwamba mambo yao yamefichikana kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu
anayajua yaliomo vifuani mwa watu, ikiwa unaafiki au Imani.
Rudi kwenye Sura
11. Na hapana shaka Mwenyezi Mungu atawadhihirishia watu yale ambayo
Yeye anayajua tangu hapo. Atawatenga mbali mbali baina ya Waumini na wanaafiki.
Na kila mmoja atamlipa kwa alilo litenda.
Rudi kwenye Sura
12. Waongozi wa shirki walikuwa wakiwaambia wale walio ingia katika
Uislamu kwa usafi wa niya: Kueni kama mlivyo kuwa katika dini yetu. Na
fuateni tunayo fuata sisi. Na ikiwa kama huko kutakuwapo kufufuliwa na
kuhisabiwa ambako nyinyi mnakuogopa, basi sisi tutakubebeeni madhambi yenu.
Hapana mtu atakayembebea mwenzie dhambi zake. Hakika hao makafiri ni waongo
tu katika hiyo ahadi yao.
Rudi kwenye Sura
13. Basi makafiri wataibeba wenyewe mizigo yao mizito, na juu ya
hiyo watabeba mfano wa mizigo ya wale walio wapoteza na wakawazuia wasiifuate
Haki. Na hapana shaka yoyote watahisabiwa Siku ya Kiyama kwa walio kuwa
wakiyazua ya uwongo duniani, na watapewa adhabu kwa hayo.
Rudi kwenye Sura
14. Na Mwenyezi Mungu alimtuma Nuhu ende kwa watu wake awaite wafuate
Tawhidi, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Akakaa nao miaka mia tisa na khamsini
akiwalingania. Nao hawakumuitikia. Mwenyezi Mungu akawazamisha kwa kuwapelekea
tufani (kimbunga), nao ni wenye kujidhulumu nafsi zao kwa ukafiri.
Rudi kwenye Sura
15. Mwenyezi Mungu akamtimilizia Nuhu ahadi yake, na akamwokoa yeye
na Waumini walio panda naye jahazi. Na akakifanya kisa chao ni funzo kwa
walio kuja baadae.
Rudi kwenye Sura
16. Na kumbuka, ewe Mtume, kisa cha Ibrahim, pale alipo wataka watu
wake wamuamini Mwenyezi Mungu Mmoja na wamt'ii Yeye, na akawanabihisha
kwamba kuamini ni bora kwao kuliko kukanusha, ikiwa wao wana ujuzi na akili.
Rudi kwenye Sura
17. Akawaambia: Nyinyi hamuabudu badala ya Mwenyezi Mungu ila vinyago
na masanamu mnayo yaunda kwa mikono yenu. Na mnazua uwongo na mnayaita
kuwa miungu. Na haya masanamu mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu hayakufaini
wala hayakudhuruni, wala hayawezi kukupatieni riziki. Basi tafuteni riziki
kwa Mwenyezi Mungu peke yake, na muabuduni Yeye tu, na mshukuruni Yeye
tu kwa neema zake. Kwani kwake Yeye ndio marejeo yenu nyote, naye atakulipeni
kwa mujibu wa vitendo vyenu.
Rudi kwenye Sura
18. Na mkishikilia kunikadhibisha mimi basi hamtanidhuru kitu. Kwani
bila ya shaka nimekwisha kwambieni kwamba Mitume wa kabla yangu walikanushwa
na kaumu zao, na hawakuwadhuru kitu, bali walijidhuru wenyewe nafsi zao,
pale Mwenyezi Mungu alipo waangamiza kwa sababu ya kukadhibisha kwao. Basi
Mjumbe hana jukumu lolote ila kufikisha Ujumbe wake kwa kaumu yake kwa
uwazi.
Rudi kwenye Sura
19. Hakika wamekwisha ona na wamejua kwamba hakika Mwenyezi Mungu
ndiye aliye anzisha uumbaji, na akisha akaurudisha tena. Basi vipi ikawa
wanakanusha kufufuliwa Siku ya Akhera kwa ajili ya hisabu na malipo? Hakika
kurejesha tena kwa Mwenyezi Mungu ni jambo jepesi zaidi.
Rudi kwenye Sura
20. Ewe Mtume! Waambie hawa wanao kanusha: Tembeeni katika ardhi,
na zingatieni vilivyo vitu mbali mbali alivyo viumba Mwenyezi Mungu. Na
angalieni mabaki ya waliyo kuwa kabla yenu, baada ya kwisha kufa kwao na
majumba yao waliyo yaacha. Na jueni ya kuwa Mwenyezi Mungu kwa kudra yake
atayarejesha yote hayo mwishoe kwa kufufua, nako ndiko huko kuumba umbo
la baadaye. Hali kadhaalika shani yenu. Hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu
ni Mwenye kutimia uwezo wake juu ya kila kitu.
"Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji;
kisha Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Muweza juu ya kila kitu." Aya hii tukufu inawahimiza wachunguzi
wende katika dunia wapate kuvumbua vipi ulianza uumbaji wa vitu, tangu
wanyama, na mimea mpaka visio kuwa na uhai. Kwani mabaki ya uumbaji wa
mwanzo yamehifadhiwa baina ya tabaka za ardhi na juu yake. Na kwa hivyo
ardhi ni daftari lilio sajiliwa ndani yake taarikhi yote ya uumbaji, tangu
mwanzo wake mpaka hivi sasa.
Rudi kwenye Sura
21. Mwenyezi Mungu atawaadhibu awatakaye baada ya uumbaji mwingine,
na hao ndio wale wenye kukanusha hayo. Na atawarehemu awatakaye, nao ndio
Waumini wenye kuyakubali hayo. Na kwake Yeye peke yake ndio marejeo ya
viumbe vyote kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura
22. Enyi mnao kadhibisha! Nyinyi hamtaweza kuishinda kudra ya Mwenyezi
Mungu; sawa sawa mkiwa katika ardhi au katika mbingu. Bali hiyo kudra yake
imekuzungukeni nyinyi. Wala nyinyi hamna mlinzi wa kukulindeni na Mwenyezi
Mungu, wala msaidizi wa kukuzuilieni adhabu yake.
Rudi kwenye Sura
23. Na wale wanao zikataa dalili za Mwenyezi Mungu zinazo thibitisha
upweke wake, na wakawakadhibisha Mitume wake na Vitabu vyake, na wakakanusha
kufufuliwa na kuhisabiwa - watu hao hawana tamaa ya kupata rehema ya Mwenyezi
Mungu. Na watu hawa watapata adhabu kali yenye kutia uchungu.
Rudi kwenye Sura
24. Na pale Ibrahim alipo waamrisha watu wake wamuabudu Mwenyezi
Mungu na waache ile ibada ya masanamu waliyo kuwa nayo, hawakuwa na jawabu
yoyote ya kumjibu ila kukakamia katika ukafiri, na kuambizana wenyewe kwa
wenyewe: Muuweni, au mchomeni moto! Basi wakamtupa motoni. Lakini Mwenyezi
Mungu akaufanya moto uwe baridi na wenye salama kwake. Na akamwokoa nao.
Hakika kwa kubwatika vitimbi vyao na kuokoka kwake zipo dalili zilizo wazi
kwa watu wanao isadiki Tawhidi (upweke) wa Mwenyezi Mungu na kudra yake.
Rudi kwenye Sura
25. Ibrahim akawaambia watu wake: Kwa nini mnaabudu miungu ya uwongo,
na wala hamkatazani, kwa sababu ya mapenzi ya madhambi mliyo yakhiari katika
maisha yenu ya dunia? Kisha hali itabadilika Siku ya Kiyama. Huko waongozi
watawakataa wafuasi wao. Na wafwasi watawalaani waongozi wao. Na marejeo
ya wote ni Motoni. Wala hamtakuwa na msaidizi wa kukuzuilieni msiingie
humo.
Rudi kwenye Sura
26. Na alikuwa katika wa mwanzo wa kuitikia wito wa Ibrahim, ni Lut'i.
Akasadiki, na kabla yake alikuwa kesha kuwa mwenye kushika Tawhid. Na Ibrahim
akasema kwa kut'ii amri ya Mwenyezi Mungu: Mimi ninahama kwendea upande
aliyo niamrisha Mola wangu Mlezi nihamie, na nikakae na huko niwaitie watu
wamfuate Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu wa kuweza kunilinda
na maadui zangu, Mwenye hikima ambaye haniamrishi ila lilio la kheri.
Rudi kwenye Sura
27. Na Mwenyezi Mungu akamtunukia Ibrahim kwa kumpa mwana, naye ni
Is-haq, na kumpa mjukuu, naye ni Yaa'qub. Na akamfanyia ukarimu kwa kumjaalia
Unabii katika dhuriya zake, na kuwateremshia Vitabu vya mbinguni, na kwa
kumlipa bora ya malipo katika dunia, naye huko Akhera kuwa ni miongoni
mwa bora ya watu wema.
Rudi kwenye Sura
28. Na ewe Mtume! Kumbuka pale tulipo mtuma Lut'i kwa kaumu yake,
akawataka waishike Tawhidi ya Mwenyezi Mungu na ut'iifu wake. Na akawakataza
kitendo kichafu walicho kuwa wakikitenda, ambacho hajapata kukitenda yeyote
katika viumbe vya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
29. Hakika hayo myatendayo ni maovu na yanahilikisha. Kwani
nyinyi mnawafanya mambo machafu wanaume, na mnaikata njia ya uzazi; na
khatima ya hayo ni kutoweka kabisa. Na katika mikutano yenu mnatenda maovu
bila ya kumkhofu Mwenyezi Mungu wala kuoneana haya baina yenu. Wala watu
wake hawakumsikia, wala hawakuwa na jawabu ya kumpa ila kumfanyia maskhara
tu. Na wakamtaka alete upesi hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu aliyo watishia
kwayo, ikiwa yeye ni mkweli kwa hayo ayasemayo.
Rudi kwenye Sura
30. Basi Lut'i akamtaka msaada Mwenyezi Mungu kupambana nao, na akamwomba
amnusuru juu ya watu wake wenye kufanya fisadi katika nchi.
Rudi kwenye Sura
31. Na walipo kuja Malaika wa Mwenyezi Mungu kwa Ibrahim, a.s. kwa
kumbashiria, walisema kwamba wameamrishwa kuwaangamiza watu wa mji huo
kwa sababu ya kufisidi kwao na kujidhulumu kwao wenyewe kwa ushirikina
na kutenda uchafu.
Rudi kwenye Sura
32. Ibrahim a.s. akawaambia Malaika: Hakika katika huo mji yumo Lut'i.
Basi vipi mtawaangamiza hao naye yumo kati yao. Malaika wakamjibu kwamba
wao wanajua nani waliomo humo, na kwamba wao kwa hakika watamwokoa Lut'i
na ahali zake wasipate adhabu, isipo kuwa mkewe. Yeye huyo atakuwa miongoni
mwa watao angamizwa kwa sababu ya ukafiri wake na uovu wake.
Rudi kwenye Sura
33. Walipo ondoka wale Malaika walio tumwa kumuendea Lut'i naye
akawaona, alihuzunika kwa kuwakhofia uadui wa watu wake, na akaemewa asiwe
na hila ya kuweza kuwalindai. Wao, basi, wakampoza na wakamwambia: Kabisa
usiukhofu uadui wa kaumu yako juu yetu, wala usihuzunike kwa ajili yetu.
Kwani sisi hakika tumekuja kuwaangamiza watu wa mji huu, na tutakuokoa
wewe na ahali zako. Lakini mkeo atakuwa pamoja na wenye kuangamia.
Rudi kwenye Sura
34. Malaika wakasema: Hakika sisi tumetumwa kutimiliza amri ya Mwenyezi
Mungu kwa kuwateremshia watu wa mji huu adhabu itokayo mbinguni kwa sababu
ya uchafu wao na ukafiri wao.
Rudi kwenye Sura
35. Na Mwenyezi Mungu akauteketeza mji huu, na akaacha humo mabaki
yaliyo wazi, ili yawe ni dalili ya kuonyesha aliyo wafanyia Mwenyezi Mungu,
na funzo kwa mwenye kuzingatia.
Rudi kwenye Sura
36. Na Mwenyezi Mungu aliwapelekea watu wa Madyana Mtume kutokana
nao wenyewe, naye ni Shuaibu. Akawaita waishike Tawhidi ya Mwenyezi Mungu,
na wamuabudu Yeye tu, na waiogope Siku ya Mwisho, na watende vitendo ambavyo
kwavyo watumai kupata malipo mema kwa Mwenyezi Mungu, na akawakataza kukimbilia
kutenda ufisadi katika nchi.
Rudi kwenye Sura
37. Wakamkanusha na wakamuasi. Basi Mwenyezi Mungu akawaangamiza
kwa tetemeko kubwa mno lilio wavunjia majumba yao. Wakawa humo wameanguka
maiti.
Rudi kwenye Sura
38. Na ewe Mtume! Watajie hawa walio danganyikiwa kw mali zao na
madaraka yao vifo vya A'di na Thamudi pale tulipo waangamiza. Na
yapo yamebakia mabaki ya majumba yao yenye kuonyesha utajiri wao. Na sababu
ya kuangamizwa huko ni kwa kuwa Shetani aliwazaini, aliwapambia vitendo
vyao viovu, nao wakamfuata. Basi akawaachisha Njia ya Haki ambayo walikuwa
wakiijua kwa kufunzwa na Mitume.
Rudi kwenye Sura
39. Na ewe Mtume! Watajie hawa walio ghurika kwa mali yao na madaraka
yao, kifo cha Qaruni na Firauni na Hamana na yaliyo wapata katika ada ya
Mwenyezi Mungu kuwahiliki wakanushao. Na Mwenyezi Mungu aliwatumia
Musa naye akawa na miujiza iliyo wazi ya kuthibitisha ukweli wake. Lakini
wao walimkadhibisha, na wakakataa kumuitikia kwa kiburi chao tu. Na wala
wao hawakuweza kuishinda kudra ya Mwenyezi Mungu kwa kuikimbia adhabu yake.
Rudi kwenye Sura
40. Kila kaumu katika kaumu zote zilizo wakadhibisha Mitume wao Mwenyezi
Mungu ameziangamiza kwa sababu ya kufuru zao walizo zifanya na maasi yao.
Baadhi ya kaumu hizo Mwenyezi Mungu alizihiliki kwa upepo wa kimbunga ulio
wapopoa kwa mawe. Na baadhi yao waliangamia kwa ukelele wenye kuvuma
wenye kuhiliki. Na baadhi yao Mwenyezi Mungu aliwadidimiza katika ardhi.
Na baadhi yao aliwazamisha majini. Wala adhabu hizi hazikuwa ni kudhulumiwa
na Mwenyezi Mungu, bali sababu yake ni kwa kufuru yao wenyewe na kutenda
maasi kwao.
Rudi kwenye Sura
41. Shani ya hao waongo wenye kumfanya urafiki asiye kuwa Mwenyezi
Mungu na kumtegemea asiye faa kutegemewa, ni kama shani ya buibui mwenye
kuifanya nyumba ya kumlinda, na hali nyumba yake ndiyo nyumba isiyo faa
kabisa kutumika kwa ulinzi. Na lau kuwa hawa waongo ni watu wa ujuzi
na utambuzi wasinge fanya hayo.
"Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano
wa buibui alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote
ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.":
Nyumba za buibui anazo jenga kwa ajili ya maskani yake na kwa ajili
ya kukamatia mateka wake zimeundwa kwa wembamba mno, kwani hizo ni nyuzi
zilizo kuwa hadi ya mwisho wa wembamba, zinashinda wembamba wa hariri.
Na kwa hivyo mfumo wake umekuwa ni wa mwisho wa udhaifu kuliko nyumba zote
walizo jijengea wanyama kuwa ni makaazi yao.
Rudi kwenye Sura
42. Hakika Mwenyezi Mungu, Subhanahu, anajua vyema upotovu wa kuwaabudu
hiyo miungu ya uwongo. Na Yeye Subhanahu ndiye Mwenye kushinda kila kitu,
Mwenye hikima katika kuendesha na kuweka sharia.
Rudi kwenye Sura
43. Na mazingatio haya na mifano hii, Mwenyezi Mungu anawatajia watu
ili wawaidhike na wazingatie. Na hawazingatii haya ila wenye akili ambao
wanapima.
Rudi kwenye Sura
44. Mbali na aliyo yataja Mwenyezi Mungu ya visa na mifano na ishara
ipo Ishara moja iliyo wazi kabisa, nayo ni uumbaji wa mbingu na ardhi kwa
uwezo na hikima, na kipimo kilicho kamilika, kwa maslaha ya watu. Na katika
haya zipo dalili za kweli kwa wenye kuiamini Haki.
Rudi kwenye Sura
45. Ewe Nabii! Soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, wala usiwashughulikie.
Na timiza Sala kwa inavyo stahiki. Kwani Sala pamoja na ikhlasi, kwa dhati
yake humwachisha, mwenye kuishika, madhambi makubwa na kila maovu yanayo
katazwa na Sharia. Na bila ya shaka, kumcha Mwenyezi Mungu, na kumhudhurisha
kwa kumkumbuka katika Sala na kwengineko kuna athari kubwa zaidi na thawabu
nyingi zaidi. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda, yakiwa ya kheri
au shari. Naye atakulipeni kwayo.
Rudi kwenye Sura
46. Wala msijadiliane na wanao kukhalifuni katika Mayahudi na Wakristo
ila kwa njia yenye uwongofu kabisa, na laini kabisa, na inayo pelekea zaidi
kukubalika. Isipo kuwa wale walio pita mpaka katika ubishi, basi hao hapana
ubaya mkiwakabili kwa mkazo. Na waambieni mnao jadiliana nao: Sisi tumeiamini
Qur'ani tulio teremshiwa sisi, na Taurati na Injili mlizo teremshiwa nyinyi.
Na tunaye muabudu sisi, na mnaye muabudu nyinyi, ni mmoja. Na sisi tunamnyenyekea
Yeye peke yake.
Rudi kwenye Sura
47. Na kama tulivyo wateremshia vitabu Mitume wa kabla yako, tumekuteremshia
wewe hii Qur'ani. Basi wale tulio wapa Kitabu (Biblia) kabla ya Qur'ani,
na wakaizingatia na wakaifuata, wanaiamini hii Qur'ani. Na miongoni mwa
hawa Waarabu (washirikina) wapo wanao iamini. Na hapana wanao zikataa Ishara
zetu - baada ya kudhihiri kwake na kuondoka kila shaka juu yake - ila walio
shikilia ukafiri.
Rudi kwenye Sura
48. Wala wewe hukuwa ukisoma kitabu chochote kabla ya Qur'ani. Wala
hukuwa ukiandika kwa mkono wako wa kulia. Na lau kuwa wewe ni katika ya
wanao soma na kuandika wangetilia shaka watu wapotovu kuwa hiyo Qur'ani
haitoki kwa Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
49. Kitabu hichi si cha kutiliwa shaka, bali hizi ni Ishara zilizo
wazi zilizo hifadhiwa katika vifua vya watu ambao Mwenyezi Mungu amewapa
ilimu. Na hazikatai Ishara zetu, baada ya kuzijua, ila wenye kuidhulumu
Haki na wakazidhulumu nafsi zao.
Rudi kwenye Sura
50. Na makafiri katika majadiliano yao na ukaidi wao walisema: Mbona
hakuteremshiwa miujiza ya kuiona kwa macho kama iliyo wateremkia Mitume
wa kabla yake? Waambie: Miujiza yote iko kwa Mwenyezi Mungu. Huiteremsha
anapo taka. Ama mimi nimetumwa kuonya kwa uwazi, sio kuleta hayo
mtakayo.
Rudi kwenye Sura
51. Wanataka Ishara hizo, nao haiwatoshi wao kuwa Sisi
tumekuteremshia hichi Kitabu wanacho somewa? Na huu ndio Muujiza wa kudumu
milele na zingapita zama. Hakika kwa kuteremka Kitabu hichi juu yako bila
ya shaka ni rehema kwao na kwa vizazi vyote vijavyo baada yao, na ni kumbusho
la daima dawamu lenye manufaa kwa watu ambao shani yao ni kuamini wanapo
onyeshwa wazi Njia ya Uwongofu.
Rudi kwenye Sura
52. Sema: Yanitosha mimi na yakutosheni nyinyi ya kwamba Mwenyezi
Mungu ndiye Shahidi kuwa mimi nimefikisha niliyo tumwa kwenu. Na
hayo ndiyo chanzo cha mambo yangu na mambo yenu. Wala hakifichiki kwake
chochote cha mbinguni na duniani. Na walio muabudu asiye kuwa Mwenyezi
Mungu, na wakamkataa Mwenyezi Mungu na wasimkhusishe Yeye tu kwa ibada,
hao ndio walio nunua ukafiri kwa Imani, na wakasibiwa na khasara iliyo
wazi.
Rudi kwenye Sura
53. Na makafiri wanakufanyia ushindani ya kuwa kama unaweza basi
waletee kwa haraka hiyo adhabu ulio waonya kuwa itawapata. Na lau
kuwa wakati maalumu haukuwekwa kwa mujibu wa hikima yetu, tungeli waletea
kwa haraka hiyo adhabu wanayo ihimiza. Ninaapa itawatokea kwa ghafla, na
hali wao hawana khabari.
Rudi kwenye Sura
54. Wanakutaka waletewe upesi adhabu, nayo itawajia tu, hapana hivi
wala hivi. Na hakika, Jahannamu imewazunguka makafiri kwa yakini.
Rudi kwenye Sura
55. Siku itapo wafunika adhabu kutoka juu, licha ya kutoka chini,
na Malaika aliye wakilishwa kuwaadhibu atapo sema: Onjeni jazaa ya hayo
maovu mliyo kuwa mkiyatenda!
Rudi kwenye Sura
56. (Mwenyezi Mungu anasema:) Enyi waja wangu mlio niamini Mimi na
Mtume wangu! Hakika ardhi yangu ni kunjufu kwa atakaye kukimbia kutoka
katika nchi za shirki. Kimbieni mje kwangu mpate kunisafia Mimi ibada.
Rudi kwenye Sura
57. Kila nafsi itaonja uchungu wa mauti bila ya shaka yoyote. Kisha
mtarejea kwetu, na mtakuja lipwa kwa hayo mliyo yatanguliza, ikiwa ya kheri
au ya shari.
Rudi kwenye Sura
58,59. Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Vitabu vyake na Mitume
wake, na wakatenda vitendo vyema, tunaapa kwamba bila ya shaka tutawaweka
katika makaazi ya starehe kwenye maghorofa yapitayo mito chini yake. Neema
zake haziwakatikii. Ni nzuri mno jazaa hii kuwa ni ujira wa wenye kutenda,
wenye kusubiri kwa yanayo wapata kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wanapo acha
nchi zao na watu wao na mali yao, nao wakimtegemea Mwenyezi Mungu peke
yake katika hali zao zote.
Rudi kwenye Sura
60. Na wanyama wengi wanao ishi nanyi katika ardhi ambao, kwa unyonge
wao, hawawezi kubeba riziki yao na wakaihamisha kwa ajili ya kuila au kuiweka
akiba. Ni Mwenyezi Mungu ndiye ambaye anawatengezea sababu za kuwaruzku
na kuwaweka hai. Na Yeye anakutengenezeeni nyinyi sababu za riziki zenu
na maisha yenu. Na Yeye ni Mwenye kumiliki kila alicho kiumba kwa kusikia
na kukijua.
Rudi kwenye Sura
61. Na ninaapa ukiwauliza washirikina: Nani aliye ziumba mbingu na
ardhi, na akalit'iisha jua na mwezi, na akayafanya hayo yawanufaishe watu?
Hapana shaka watasema: Kaviumba hivyo Mwenyezi Mungu. Wala hawamtaji mwenginewe.
Basi inakuwaje wanaacha kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja Mtukufu, baada ya
kukiri kwao huku?
Rudi kwenye Sura
62. Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humdhikishia amtakaye,
kwa mujibu wa inavyo wafikiana na ujuzi wake kwa ajili ya maslaha. Kwani
hakika Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa ujuzi wake.
Rudi kwenye Sura
63. Ninaapa, lau kuwa utawauliza: Nani anaye teremsha maji kutoka
mbinguni, na akaihuisha ardhi kwa mimea baada ya kuwa na ukame? Hapana
shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi, kuwa wanaikubali
Haki. Lakini wengi wao hawafahamu kuwa wenyewe wanajitia katika migongano
ya maneno.
Rudi kwenye Sura
64. Na haya maisha ya duniani si chochote ila ni starehe ya muda
wenye ukomo. Wanapumbazika walio ghafilika kama wanavyo pumbazika watoto
wadogo, na wanacheza kwa muda fulani na kisha wanatawanyika. Na hakika
makaazi ya Akhera ndio makaazi ya maisha ya kweli, yaliyo kamilika, yenye
kudumu. Na kweli hizi ni zenye kuthibiti, wangeli zitambua hawa lau kuwa
ni watu wa kutambua vilivyo.
Rudi kwenye Sura
65. Hao kwa walivyo sifika kwa ushirikina, wakipanda vyombo vya baharini,
na wakapata kidogo katika vitisho vyake, humuelekea Mwenyezi Mungu kwa
kumwomba kwa ikhlasi ili awaondolee madhara. Na akisha waokoa akawafikisha
nchi kavu mara hukimbilia kurejea kwenye ushirikina.
Rudi kwenye Sura
66. Ili wapate kuzikanya neema tulizo wapa, na wapate kunafiika kwa
yale yanayo ridhiana na pumbao lao katika maisha haya. Basi watakuja yajua
matokeo ya ukafiri pale watapo iona adhabu iliyo chungu.
Rudi kwenye Sura
67. Makafiri wa Makka wameingia upofu, hawazioni neema za Mwenyezi
Mungu alizo wamiminia, wala hawaoni kwamba hakika Sisi tumeufanya mji wao
kuwa umehifadhika, haushambuliwi wala hauvamiwi, mtakatifu; watu wake hawatekwi
nyara, wala ndani yake havitokei vita. Na hali kote jirani zao watu wananyakuliwa!
Hawa wamepofuka hawazioni neema hizi, basi wanasadiki yasiyo na asli yoyote,
na wanamkanusha Muhammad na yote aliyo yaleta!
Rudi kwenye Sura
68. Na hapana aliye dhulumu zaidi kuliko yule anaye msingizia Mwenyezi
Mungu jambo ambalo hakulitolea sharia, au akaikadhibisha Dini ya Haki inapo
mfikilia. Hakika katika Jahannam ndiko kwenye makaazi ya watu hawa madhaalimu,
makafiri.
Rudi kwenye Sura
69. Na wale walio fanya ukomo wa juhudi zao, na wakastahamili mashaka
kwa sababu ya kuinusuru Dini yetu, hapana shaka tutawazidishia kuwaongoa
kuendea kheri na Haki. Na hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka yu pamoja
na wale wanao fanya vizuri vitendo vyao; atawasaidia na atawanusuru. Na
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi kuliko wote.
Rudi kwenye Sura