1. T'aa Siin, (T' na S) harufi mbili za kutamkwa, ni
harufi za alifbete, ndizo zimeanzia Sura hii, ili kunabihisha siri ya muujiza
wa Qur'ani pamoja na kuashiria kuwa imeundwa kwa jinsi ya harufi hizi hizi
mnazo zitumia katika kusema, na pia kuzindua akili ziisikilize hii Qur'ani
inapo somwa.
Hizi Aya zilizo teremka kwa kusomwa, na ni Kitabu chenye kubainisha
mambo yaliyo kuja ndani yake.
Rudi kwenye Sura
2. Na hii Qur'ani ni Uwongofu wa kuwaahidi Waumini waifuate njia
ya kheri, na kufuzu duniani na Akhera, na inawabashiria kuwa watapata malipo
mazuri.
Rudi kwenye Sura
3. Waumini hao ndio wanao ishika Sala kwa unyenyekevu na kutimiliza
nguzo, na wanatoa Zaka kwa nyakati zake, nao wana yakini ya maisha ya baadaye
Akhera, na yatayo kuwa huko ya adhabu na thawabu.
Rudi kwenye Sura
4. Hakika wale ambao hawaiamini Akhera, Sisi tumewapambia vitendo
vyao kwa kuwaumbia matamanio ndani yake. Kwa hivyo wao wanababaika humo
katika upotovu wao.
Rudi kwenye Sura
5. Hao ndio watapata adhabu mbaya kabisa, na Akhera ndio watakuwa
khasarani kushinda wote.
Rudi kwenye Sura
6. Ewe Nabii! Wewe unapokea Qur'ani hii unayo teremshiwa kutokana
na Yeye ambaye hapana anaye mkaribia kwa hikima yake, naye anajua kila
kitu.
Rudi kwenye Sura
7. Kumbuka pale Musa alipo mwambia mkewe na walio pamoja naye na
yeye ndio anarejea Misri: Mimi nimeona moto. Nitakwenda kuleteeni khabari
ya njia, au nitapata kijinga cha moto, kitacho kufaeni kwa kuota moto kwa
hii baridi.
Rudi kwenye Sura
8. Alipo fika huko paliitwa: Wamebarikiwa waliomo katika moto huu
na walioko pembezoni mwake, yaani karibu yake. Nao ni Malaika na Musa.
Na Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote ametakasika na kila kisicho
kuwa laiki naye.
Rudi kwenye Sura
9. Ewe Musa! Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mwenye kustahiki kuabudiwa
pekee, Mwenye kushinda kila kitu, Mwenye kuweka kila kitu pahala pake.
Rudi kwenye Sura
10. Na katika njia ya kufikisha wito wako, tupa fimbo yako na utaiona
inatikisika kama kijoka jepesi kinakwenda mbio. Yeye akarudi nyuma, wala
hakurejea baada ya kurudi nyuma. Mwenyezi Mungu Mtukufu akamtuza kwa kauli
yake: Usiogope. Mbele yangu hawaogopi. Mitume ninapo sema nao.
Kisa cha Musa kimetajwa zaidi ya mara moja katika Qur'ani.
Pengine hutolewa yasiyo tajwa penginepo. Na kila sehemu ina mnasaba wake.
Katika sehemu hii makusudio ni kuondoa yale mastaajabu ya kuwa Nabii Muhammad
s.a.w. kapata Ufunuoa (Wahyi) vile vile.
Rudi kwenye Sura
11. Lakini mwenye kutenda asicho ruhusiwa, na kisha akaleta wema
baada ya kuteleza kwake, basi Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mkubwa wa kurehemu.
Rudi kwenye Sura
12. Na utie mkono wako katika mfuko wa nguo zako, utatoka mweupe
wala si kwa balanga. Hayo ni katika Ishara tisa (1) za kumpelekea Firauni
na kaumu yake. Hakika hao walikuwa watu walio tokana na amri ya Mwenyezi
Mungu, ni makafiri.
(1) Hizo Ishara tisa ni:- Kupasuka bahari, T'ufani (Kimbunga), Nzige,
Chawa, Vyura, Damu, Ukame, Fimbo, Kutoka mkono mweupe bila ya maradhi.
Rudi kwenye Sura
13. Ilipo kuja miujiza hii kwa uwazi na dhaahiri wakasema: Huu ni
uchawi wazi!
Rudi kwenye Sura
14. Wakaikadhibisha miujiza wakikataa kuwa inaonyesha dalili ya Utume.
Na hakika yakini ilikwisha waingia katika nyoyo zao, lakini hawakusalimu
amri kwa kuwa walikwisha tangaza kufuata upotovu na kushika uasi. Basi
ewe Nabii! Hebu angalia vipi yalikuwa matokeo ya walio shikilia ufisadi,
wakaikanya miujiza nayo iko wazi.
Rudi kwenye Sura
15. Hizo ndizo jeuri za Firauni kwa sababu ya ufalme wake. Hebu sasa
angalia utawala muadilifu, utawala wa hukumu, utawala wa unabii wa Daudi
na mwanawe, Sulaiman, Mwenyezi Mungu awape amani. Sisi tuliwapa ilimu nyingi
za sharia na mazoezi ya kuhukumu. Wakasimamisha uadilifu, na wakamhimidi
Mwenyezi Mungu aliye wapa fadhila kushinda wengi katika waja wake wenye
kusadiki, na kuifuata Haki.
Rudi kwenye Sura
16. Ufalme na hukumu ukatoka kwa Daudi ukenda kwa mwanawe, Sulaiman;
naye akasema: Enyi watu! Sisi tumefunzwa lugha ya ndege, na tumepewa mengi
tunayo yahitajia katika utawala wetu. Hakika neema hizi ni fadhila iliyo
wazi aliyo tukhusisha sisi Mwenyezi Mungu,
"Na Sulaiman alimrithi Daudi, na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa
usemi wa ndege, na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhaahiri."
Sulaiman a.s. ni mwana wa Daudi, naye ni Nabii na Mfalme kama yeye. Aliishi
mnamo mwaka 974 mpaka 937 K.K. (yaani Kabla ya Kuzaliwa Nabii Isa). Mwenyezi
Mungu alimjaalia kumjuvya kufahamu maneno ya ndege. Uchunguzi wa kisasa
umeonyesha kwamba kila namna ya ndege wana njia zao za kufahamiana wao
kwa wao. Katika njia hizo ni kwa kugusa, na sauti, na ishara.
Rudi kwenye Sura
17. Na Sulaiman alikusanya majeshi yake ya majini, watu, na ndege,
kwenye uwanja mmoja. Na wao wakawa jeshi moja lenye nidhamu kwa vile kudhibitiwa
wa mwanzo mpaka mwisho.
Rudi kwenye Sura
18. Hata walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, mdudu chungu
mmoja akasema: Enyi wadudu chungu! Ingieni vishimoni mwenu, asije Sulaiman
na askari wake wakakuuweni na wao wala hawahisi kuwa nyinyi mpo.
"Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu
chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni
Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua." Inafahamikana wazi katika
Aya hii kuwa wadudu chungu wanaishi kwa makundi, yaani wana umoja, na moja
katika sifa zao ni kuwa macho na kutahadhari. Na inajuulikana tangu zamani
kuwa wadudu chungu wana sifa kadhaa wa kadhaa makhsusi ambazo zinaonyesha
kuwa wana umoja wenye nidhamu madhubuti katika hukumu, na wana kiasi kikubwa
cha akili, na werevu, na nguvu za kukumbuka, na kupenda kazi na kukakamia,
na juhudi isiyo jua kunyong'onyea wala kukata tamaa. Kama wanavyo juulikana
kuwa wana wingi wa hila za kuendesha kazi zao. Na dalili ya hayo ni kuwa
jamaa wa wadudu chungu ni peke yao baada ya binaadamu ndio wanao
zika maiti wao. Na makundi mbali mbali yao yanashughulikia kukutana pahala
pamoja kwa nyakati maalumu. Kwa ajili ya hayo zimewekwa siku makhsusi za
kusimamisha soko wanapo kusanyika makundi yote kwa kubadilishana bidhaa
na kujuana. Na makundi haya yanapo kutana hutokea mazungumzo kwa hima kubwa,
na huulizana masuala yaliyo khusiana na mambo yao. Katika yanayo onekana
yaliyo fungamana na mikusanyiko hiyo ni kuzuka mashauri yaliyo khusu umma
wao, kama kutengeneza barabara ndefu, kwa subira na kukakamia kunako staajabisha.
Wala makundi haya hayatosheki na kufanya kazi mchana tu, bali huendeleza
kazi zao katika masiku ya mbaamwezi; ama masiku ya kiza hubaki mwahala
mwao. Na jamaa wa makundi haya wana njia za pekee za kukusanya na kubeba
na kuhifadhi vifaa vyao vya kula. Akishindwa mdudu kuchukua chakula alicho
kikusanya kwa mdomo wake hukisukuma kwa miguu yake ya nyuma, na akakinyanyua
kwa mikono yake. Na katika mtindo wao ni kuzing'ong'ona mbegu, na kuzipasua
baadhi ya nafaka kabla ya kuzirindika ili zisije kuchipua. Na mbegu kubwa
kubwa huzigawa vipande vipande ili iwe wepesi kuziingiza katika ghala zao.
Na pindi zikiroana kwa mvua huzitoa zipate upepo na jua zikauke.
Rudi kwenye Sura
19. Sulaiman akatabasamu akicheka kwa ile kauli ya mdudu chungu yenye
kushughulikia maslaha yao, na akahisi neema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyo
juu yake. Akasema: Ewe Uliye niumba! Nijaalie niwe na shukrani kwako kwa
neema ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na niwezeshe nitende vitendo
vyema unavyo viridhia, na unitie kwenye rehema yako iliyo timia.
Rudi kwenye Sura
20. Akalikagua jeshi lake la ndege asimwone Hud-hud. Akastaajabu,
akasema: Mbona simwoni Hud-hud! Yupo hapa na mimi simwoni, au ameghibu
hayupo miongoni mwetu?
Rudi kwenye Sura
21. Wallahi! Nitampatisha adhabu kali ya kumshikisha adabu, au nitamchinja
ikiwa kosa lake ni kubwa! Ila aniletee hoja madhubuti ya kumtoa makosani
kwa kuto kuwepo mbele yangu.
Rudi kwenye Sura
22. Na Hud-hud alikuwa kakaa si pahala mbali kwa muda usio kuwa mrefu.
Kisha akamjia Sulaiman, akamwambia: Nimejua jambo ulilo kuwa wewe hujalijua,
na nimekujia kutoka nchi ya Sabai na khabari muhimu sana, nayo ni ya kweli
kwa yakini.
"Basi hakukaa mbali, na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na
ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za yakini. Hakika
mimi nimemkuta mwanamke anawatawala, naye amepewa kila kitu, na anacho
kiti cha enzi kikubwa.Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala
ya Mwenyezi Mungu; na Shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia Njia.
Kwa hivyo hawakuongoka." Hizi ndizo Aya khasa zilizo khusu Ufalme wa Sabai.
Na hii Sabai ni moja katika falme za kusini ya Arabuni, inayo itwa Yaman,
na ambayo zamani ilikuwa ni maarufu kwa jina la "Arabia Iliyo Neemeka".
Na jina hili la mwisho linaonyesha maendeleo yake na utajiri wake. Kwani
kwa hakika ilikuwa nchi hiyo ina ustaarabu wa juu tangu miaka elfu mbili
kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s. Ikitegemea makulima, kwa sababu ya rutuba
ya ardhi yake, na uzuri wa hali yake ya hewa. Na pia ikitegemea biashara
kwa kuwa ipo kati baina ya Bara Hindi, na Uhabeshi, na Somalia, na Sham,
na Iraq. Na kwa hakika mahodhi yaliyo jengwa kuwekea maji na kuyatumia,
na maarufu yao yote ni Hodhi Maa'rib (Tazama Aya 16 Surat Sabai) na miji
iliyo jengewa ngome, na makasri, na mahekalu, yanashuhudia mpaka hii leo
maendeleo ya kijamii ya utajiri ulio kuwako katika nchi hii.
Na hakika nakshi walizo zinakishi watawala wao, na baina ya nakshi
hizo zipo kanuni za kuendesha mambo ya ujenzi na mengineyo, yanaonyesha
kwa kila dalili ukomo wa ustaarabu ulio nawiri walio ufikilia. Na huu ufalme
wa Sabai ambao ulifikilia kilele cha kustawi kwake katika siku za Sulaiman
a.s. kiasi ya karne kumi kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s. ulikuwa ni ufalme
kama wa kabla yake, yaani watoto wakiwarithi baba zao. Na kwa hivyo alikuwa
akihukumu wakati wa Sulaiman a.s. Malkia. Wataalamu wa taarikhi wamekhitalifiana
juu ya jina la Malkia huyo. Waarabu wakimwita Balqiis; akisaidiwa na wazee
wahishimiwa kama ni Baraza la Mashauri lake. (Tazama Aya 28-33 katika Surat
An-naml.) Wala haikuthibitisha taarikh (historia) kuwa Ufalme wa Sabai
ulikuwa dola ya kuteka nchi, bali ulikuwa ufalme wa biashara, na misafara.
Katika mabaki yake hatuoni kutajwa vita au kuteka nchi isipo kuwa kwa uchache.
Na haya ni kuwa umuhimu wa majeshi yake ulikuwa ni kuhifadhi ngome zake
na kuzihami, na kulinda misafara yake kwa aghlabu. Na wananchi wa Sabai
walikuwa ni mapagani, makafiri, wakiliabudu jua, kama ilivyo kuja katika
Aya tukufu nambari 24 katika Sura hii. Pia wakiabudu mwezi. Na hao ndio
miungu yao muhimu kabisa. Na walikuwa wakiwatolea sadaka na wakifukiza
ubani katika mahekalu yao.
Rudi kwenye Sura
23. Hakika mimi nimewaona watu wa Sabai wanatawaliwa na mwanamke,
na amepewa kila kheri za kidunia, naye ana kiti cha enzi kikubwa kinacho
onyesha dalili ya utukufu wa ufalme na nguvu za madaraka yake.
Rudi kwenye Sura
24. Nimemwona yeye na watu wake wanaabudu jua, wala hawamuabudu Mwenyezi
Mungu. Na Shetani amewazainishia vitendo vyao na wenyewe wakaviona ni vizuri
na hali ni viovu. Kwa hivyo amewapoteza Njia ya Haki, basi hawakuongoka.
Rudi kwenye Sura
25. Hawamsujudii Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambaye ndiye anayafichua
yaliyo fichika katika mbingu na ardhi, na anajua mnayo fanya kwa siri na
kwa dhaahiri.
Rudi kwenye Sura
26. Mwenyezi Mungu, ambaye hapana wa kuabudiwa kwa Haki isipo kuwa
Yeye, ndiye Mwenye madaraka makuu yasio na ukomo juu ya kila kiumbe.
Rudi kwenye Sura
27. Sulaiman akasema kumwambia Hud-hud: Tutaichungua khabari yako
hii tujue kwamba umesema kweli au wewe ni miongoni mwa waongo.
Rudi kwenye Sura
28. Nenda na barua yangu hii umfikishie yeye na kaumu yake. Kisha
jitenge nao ujifiche pahali karibu, uangalie wanarejesheana maneno gani.
Rudi kwenye Sura
29. Barua ikamfikia yule Malkia, naye basi akawakusanya wahishimiwa
wa kaumu yake, na halmashauri wake. Naye akasema: Enyi wahishimiwa! Mimi
hakika imenifikilia barua yenye shani kuu.
Rudi kwenye Sura
30. Kisha akawasomea hiyo barua, nayo imeanzia kwa jina la Mwenyezi
Mungu Mwenye utukufu na neema zote, ambaye daima anawamiminia waja wake
rehema zake.
Rudi kwenye Sura
31. Msifanye kiburi juu yangu, na nijieni nanyi mmet'ii na wanyenyekevu.
Rudi kwenye Sura
32. Akaiambia baraza ya washauri wake: Nibainishieni lifaalo katika
haya mambo muhimu nilio wekewa mbele yangu. Kwani mimi sikati shauri juu
ya jambo lolote mpaka muwe nyinyi mmehudhuria.
Rudi kwenye Sura
33. Wakamwambia nao wametua: Sisi ni watu wenye nguvu za mwili, na
tuna moyo na mashujaa. Hatuogopi vita. Basi angalia wewe jambo unalo taka
kutuamrisha nasi ni wenye kut'ii.
Rudi kwenye Sura
34. Akasema kwa taratibu na kupendelea salama: Hakika watawala wakiingia
katika miji mikubwa pamoja na majeshi yao huifisidi, wakaondoa matengenezo
yake, wakateketeza makulima na roho, na wakawafanya walio watukufu katika
watu wa hiyo miji kuwa ndio madhalili, na huo ndio mtindo wao daima.
Rudi kwenye Sura
35. Na mimi kwa kupendelea salama na uzima nitampelekea zawadi Sulaiman
na kaumu yake, na nitatazama wajumbe watarejea na nini - wataikubali zawadi
au watairudisha?
Rudi kwenye Sura
36. Wajumbe walifika kwa Sayyidina Sulaiman na zawadi zao. Huku anazijua
neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu zilio juu yake, Akawaambia naye ndio anamsemeza
huyo Malkia na watu wake katika mkabala na wajumbe: Hivyo ndio mnanipa
mimi mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ya Unabii, na ufalme, na neema, ni
makubwa zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Bali nyinyi kwa hizi zawadi zenu
na wingi wa mali yenu mnafurahi, sio kama mimi. Kwa sababu nyinyi hamjui
ila yaliyo shikamana na dunia hii tu.
Rudi kwenye Sura
37. Akasema, akimsemeza yule msemaji kwa jina lao: Ewe mjumbe! Rejea
kwao. Wallahi! tutawatokea kwa majeshi wasio yaweza kupambana nayo na kuyakabili.
Na tutawatoa kwenye nchi ya Sabai nao wamepoteza utukufu wao, wamefanywa
watumwa.
Rudi kwenye Sura
38. Sulaiman akawaelekea binaadamu na majini aliyo dhalilishiwa na
Mwenyezi Mungu kumtumikia, akawashitua kwa jambo geni. Akasema: Ni nani
katika nyinyi anaweza kuniletea kiti chake cha enzi kikubwa kabla hawajanijia
nao wamekwisha nyenyekea wanat'ii.
Rudi kwenye Sura
39. Mmoja pandikizi la kijini lilisema: Mimi nitakuletea, na wewe
umekaa katika baraza yako hii, kabla hujaondoka. Na mimi hakika naweza
hayo, na muaminifu katika maneno yangu na vitendo vyangu.
Rudi kwenye Sura
40. Akasema aliye pewa nguvu za kiroho, na ilimu ya Kitabu: Mimi
nitakuletea hicho kiti cha enzi kabla jicho lako halijapepesa. Na akatimiza
aliyo yasema. Sulaiman alipo kiona kiti kile kimetua mbele yake bila ya
mtingisiko, alisema: Haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu aliye niumba
na akanipa kheri zake ili anifanyie mtihani, nitashukuru kwa neema hizi
au sitoi haki yake? Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu basi huyo hakika
amejiondolea nafsi yake mzigo wa waajibu. Na mwenye kuacha kushukuru kwa
neema basi hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi, si mwenye kuhitajia shukrani.
Naye ni Karimu wa kuneemesha.
Rudi kwenye Sura
41. Sulaiman akawaambia watu wake: Kigeuzeni geuzeni hichi kiti cha
enzi kwa baadhi ya mabadiliko ya nje, tupate kuona atakijua kwa kukiendea
au hato kijua na kwa hivyo hato kiendea.
Rudi kwenye Sura
42. Alipo fika jicho lake lilipiga kwenye kiti chake cha enzi. Akaambiwa:
Je! Kiti chako cha enzi ni mfano wa hiki? Akasema kwa vile kilivyo kamilika
kufanana: Kama kwamba ndicho hichi. Na Sulaiman na walio pamoja naye wakasema:
Sisi tulisha pewa ujuzi kumjua Mwenyezi Mungu na uwezo wake na ukweli wa
yaliyo kuja kutoka kwake kama anavyo jua mwanamke huyu. Na sisi tangu hapo
ni watu tulio mfuata Mwenyezi Mungu na tunamsafia Yeye ibada.
Rudi kwenye Sura
43. Na zile ibada za jua na mfano wake zilimzuia yule Malkia kumuabudu
Mwenyezi Mungu. Kwani yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.
Rudi kwenye Sura
44. Baada ya hao akaambiwa: Ingia katika jumba la Sulaiman. Na uwanja
wake wa ndani ulikuwa umesakafiwa kwa kiyoo, na chini yake maji, na samaki
wakiogelea humo. Kupandisha nguo miundi yake ya miguu ikaonekana, kwa kuwa
alidhania ni maji. Sulaiman akamwambia hicho ni kiyoo, basi yakamuathiri
yale madhaahiri ya kilimwengu, na akaona kuwa ufalme wake yeye haufai chochote
mbele ya ufalme wa Nabii Sulaiman. Akasema: Mola Mlezi! Hakika mimi nimeidhulumu
nafsi yangu kwa kughurika na ufalme wangu na ukafiri wangu. Na sasa ninanyenyekea
pamoja na Sulaiman kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye kuumba walimwengu
wote na kuwalea na kuwasimamia.
Rudi kwenye Sura
45. Na tuliwapelekea Thamud ndugu yao Saleh kuwafunza wamuamini Mwenyezi
Mungu pekee. Wao wakakimbilia kugombana na kukhitalifiana. Wakawa makundi
mawili. Moja lenye kuamini, na moja la kikafiri.
Rudi kwenye Sura
46. Saleh akasema nao kuwanasihi: Enyi watu! Mbona mnaihimiza adhabu
mlio ahidiwa kabla ya kutubu? Kwa nini hamwombi msamaha kwa Mola wenu Mlezi,
mkamuamini Yeye kwa kutaraji akurehemuni?
Rudi kwenye Sura
47. Wakasema: Sisi tunakuona wewe na hao walio nawe ni wakorofi,
ndio tukapatilizwa na ukame. Yeye akasema: Sababu za kheri na shari zinazo
kuteremkieni bila ya shaka yoyote zinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Bali nyinyi
ni watu mnao pewa mitihani ya neema na nakama, ili mpate kuamini.
Rudi kwenye Sura
48. Na waongozi wa shari kati yao walikuwa ni tisa, kazi yao ni kufisidi
katika nchi kwa maoni yao na madai yao. Wala haukuwa mtindo wao kutenda
jema lolote.
Rudi kwenye Sura
49. Wale washirikina wakaambizana wenyewe kwa wenyewe: Apishaneni
kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwamba kwa yakini tutamshambulia yeye na ahali
zake, na tutawauwa. Kisha tutamwambia jamaa yao wa damu kwamba sisi hatukayaona
mauwaji yake wala ya ahali zake. Na hakika sisi ni wasema kweli kwa haya
tuliyo yataja.
Rudi kwenye Sura
50. Walipanga kumuuwa Saleh na ahali zake, na Mwenyezi Mungu nyuma
yao kapanga kumwokoa Nabii wake na ahali zake, na kuwateketeza wao, na
hali wao hata hawatambui.
Rudi kwenye Sura
51. Ewe Nabii! Hebu tazama vipi yalikuwa matokeo ya mipango yao na
mipango yetu. Sisi tuliwaangamiza wote hao wao na kaumu yao.
Rudi kwenye Sura
52. Na hebu yatazame mabaki yao. Utakuta nyumba zao zimeanguka, zimevurugika,
kwa sababu ya udhalimu wao na kufru zao, na kumtakia shari Nabii wao. Hakika
kwa walio fanyiwa kina Thamud ipo Ishara kwa watu wanao ujua uwezo wetu
na wakawaidhika.
Rudi kwenye Sura
53. Na Sisi tukakiokoa kikundi kilicho muamini Saleh kutokana na
hilaki hii, na wakawa wanao gopa kuziacha amri zake.
Rudi kwenye Sura
54. Ewe Nabii! Mtaje Lut'i na khabari zake pamoja na kaumu ya watendao
uchafu, pale alipo waambia: Je! Mnafanya dhambi hizi ambazo zimepita hadi
ya uchafu na kinyume na maumbile, na hali nyinyi mnaona na mnaangalia uovu
wa haya mliyo yashikilia?
Rudi kwenye Sura
55. Hivyo inaelekea katika nadhari ya akili zenu na maumbile kuwaingilia
wanaume kwa matamanio yenu, na mkwawacha wanawake? Ama kweli nyinyi mmesibiwa
na upumbavu na ujinga wa kufudikiza, hata imekuwa hamwezi tena kuteuwa
baina ya kiovu na chema.
Rudi kwenye Sura
56. Haikuwa jawabu ya watu wake alipo wakataza ila ni kusema: Mtoleeni
mbali Lut'i na wafwasi wake katika mji huu. Kwani wao wanajitakasa hawataki
kushirikiana nasi katika haya tuyatendayo.
Rudi kwenye Sura
57. Basi Sisi tukamwokoa yeye na ahali zake na ile adhabu walio pelekewa
wale watu, isipo kuwa mkewe. Mwenyezi Mungu alimkadiria awe na walio baki
nyuma ili apate kuangamia kwa adhabu pamoja na makafiri.
Rudi kwenye Sura
58. Na Sisi tukawanyeshea mvua hao mafisadi, mvua ya adhabu na nakama.
Ilikuwa mvua ya kuwahiliki walio onywa kuwa watapata adhabu chungu, na
wala wasisikie.
Rudi kwenye Sura
59. Ewe Mtume! Sema: Hakika mimi namhimidi Mwenyezi Mungu na namsifu
Yeye peke yake. Na namwomba Mwenyezi Mungu salama na maamkio kwa
waja wake alio wateuwa kwa kuwapa Ujumbe wake. Na ewe Mtume! Waambie washirikina:
Je! Kumuamini Mwenyezi Mungu Mmoja, Aliye Mpweke, ni bora kwa mwenye
kuamini, au kuabudu masanamu mnayo mshirikisha naye, nayo hayawezi kukudhuruni
wala kukufaeni?
Rudi kwenye Sura
60. Bali, ewe Mtume, waulize: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi
na viliomo ndani yake, na akakuteremshieni kutoka mbinguni mvua yenye manufaa,
na kwa hiyo akakuotesheeni bustani nzuri zenye kupendeza. Msingeli weza
nyinyi kuiotesha miti yake ya namna mbali mbali, na rangi mbali mbali,
na matunda mbali mbali! Mipango hii iliyo umana sawa katika uumbaji inathibitisha
kuwa hapana mungu pamoja na Mwenyezi Mungu. Lakini makafiri ni watu walio
potoka wakaiacha Haki na Imani, na wameelekea kwenye upotovu na ushirikina.
Rudi kwenye Sura
61. Bali waulize, ewe Mtume: Nani aliye itengeneza ardhi hata ikafaa
kukaliwa na watu wakatulia humo, na akaumba mito kati yake, na juu yake
akaumba milima kuizuilia isiyumbe yumbe, na akayatenganisha maji matamu
na maji ya chumvi hata yasichanganyike? Hapana mungu pamoja na Mwenyezi
Mungu. Yeye ndiye Mwenye kuumba peke yake. Lakini wengi wa watu hawanafiiki
na ujuzi wa Haki kama ilivyo. Wamekuwa kama kwamba hawajui kitu.
Rudi kwenye Sura
62. Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye muitikia aliye shikwa na
shida katika maombi yake, pale anapo shikwa na shida, akamtegemea Mwenyezi
Mungu kwa unyonge na unyenyekevu, naye akamwondolea huyo mtu karaha iliyo
msibu, na akakufanyeni warithi wa walio kutangulieni katika nchi? Hapana
mungu pamoja na Mwenyezi Mungu wa kukupeni neema zote hizi. Lakini nyinyi
makafiri, ni kuchache kabisa kuwaidhika kwenu.
Rudi kwenye Sura
63. Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye waongoza katika nyendo za
katika giza la usiku katika safari za nchi kavu na baharini? Na nani
anaye zipeleka pepo zinazo bashiria mvua, nayo ni rehema itokayo kwa Mwenyezi
Mungu? Je! Yupo mungu pamoja na Mwenyezi Mungu anaye fanya hayo? Mwenyezi
Mungu Subhanahu ametakasika kuwa na mshirika.
Rudi kwenye Sura
64. Bali waulize, ewe Mtume: Nani anaye anzisha uumbaji tangu mwanzo,
na kisha baada ya kupotea kwake akaurejesha kama ulivyo kuwa? Na nani anaye
kuteremshieni riziki kutoka mbinguni, na akaitoa kwenye ardhi? Hakuna mungu
pamoja na Mwenyezi Mungu atendaye hayo. Sema, ewe Mtume, kuwatahayarisha
na kuwakanya: Kama nyinyi mnaye mungu asiye kuwa Mwenyezi Mungu basi tupeni
hoja ya hayo, ikiwa mnadai kuwa nyinyi ni wasema kweli. Na wala hayataweza
kuwa hayo kwenu.
Rudi kwenye Sura
65. Sema, ewe Mtume: Hakika mwenye kutenda yote haya peke yake ndiye
Yeye Subhanahu aliye tengeka peke yake kwa kuyajua mambo ya ghaibu
yalioko mbinguni na duniani. Na Yeye huyo ndiye Mwenyezi Mungu wa pekee.
Wala watu hawajui wakati gani watafufuliwa kutoka makaburini kwao kwa ajili
ya kuhisabiwa na kulipwa.
Rudi kwenye Sura
66. Ujuzi wao wa Akhera umefuatana na ujinga, na huo ukawapelekea
kuitilia shaka. Nao wamekuwa vipofu hawaitambui Haki katika jambo lolote,
kwa sababu upotovu umefisidi fahamu zao.
Rudi kwenye Sura
67. Wakasema makafiri kwa kukanya kufufuliwa: Hivyo sisi tukisha
kuwa mchanga, na ikisha oza miili yetu na ya baba zetu walio tutangulia,
ndio tutarejeshwa tutolewe upya tuwe wahai?
Rudi kwenye Sura
68. Muhammad ametuahidi kuwa tutafufuliwa, kama Mitume walio tangulia
walivyo waahidi baba zetu. Ingeli kuwa hayo ni kweli, basi yangeli kwisha
kuwa. Haya si chochote ila ni uwongo tu wa watu wa kale.
Rudi kwenye Sura
69. Ewe Mtume! Waambie: Tembeeni duniani, na mtazame mabaki ya yaliyo
wapata walio kadhibisha, nayo ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Huenda labda
mkayazingatia haya, na mkaikhofu adhabu ya Akhera.
Rudi kwenye Sura
70. Ewe Mtume! Usiwahuzunukie makafiri wasio kufuata. Kwani kwa hakika
waajibu wako ni kufikisha Ujumbe tu. Wala usiwe na dhiki kifuani mwako
kwa sababu ya hila zao na vitimbi vyao. Kwani hakika Mwenyezi Mungu atakupa
ushindi juu yao.
Rudi kwenye Sura
71. Na makafiri wanafanya ukomo wa juhudi yao kukanusha, na wanaihimiza
adhabu kwa kusema: Lini, basi, itakuwa hiyo adhabu ambayo mnatutishia kuwa
itakuja, ikiwa nyinyi mnasema kweli kuwa adhabu itawashukia wanao kanusha?
Rudi kwenye Sura
72. Ewe Mtume! Sema: Huenda ikakukuteni, na imekukaribieni baadhi
ya adhabu mnayo ihimiza.
Rudi kwenye Sura
73. Na hakika Mwenyezi Mungu Mola wako Mlezi, ewe Mtume, ni Mwenye
neema na hisani kwa watu wote. Na katika rehema zake ni kuakhirisha hiyo
adhabu kwa hao wanao kadhibisha. Lakini watu wengi hawaelewi fadhila za
Mwenyezi Mungu wala hawamshukuru.
Rudi kwenye Sura
74. Ewe Mtume! Hakika Mwenyezi Mungu, Mola wako Mlezi, hapana shaka
anajua kila wanalo lificha na wanalo litangaza, ikiwa maneno au vitendo
viovu. Naye atakuja walipa kwayo.
Rudi kwenye Sura
75. Na hapana kilicho fichikana cha ghaibu, na kiwe kidogo vipi au
duni, mbinguni au katika ardhi ila Mwenyezi Mungu anakijua, na amekidhibiti
katika Kitabu cha Haki kilioko kwake.
Rudi kwenye Sura
76. Hakika Kitabu hiki alicho teremshiwa Muhammad kinawawekea wazi
Wana wa Israili ukweli wa yaliyo kuja katika Taurati, katika mambo ya itikadi
na hukumu na hadithi. Na kinawarudisha kwenye kweli katika mambo waliyo
khitalifiana kwayo.
Rudi kwenye Sura
77. Hakika Kitabu hichi ni Uwongofu wa kuokoa watu wasipotee, na
ni Rehema ya kuwakinga na adhabu wote wenye kukiamini.
Rudi kwenye Sura
78. Ewe Mtume! Hakika Mola wako Mlezi atawapambanua watu wote Siku
ya Kiyama kwa uadilifu wake. Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, basi
hapana wa kuipinga hukumu yake. Yeye ni Mjuzi wa kila kitu, basi mbele
yake kweli haiwezi kuchanganyika na uwongo.
Rudi kwenye Sura
79. Basi, ewe Mtume, mtegemezee mambo yako Mwenyezi Mungu, na shikilia
wito wako kwa kuamini kuwa utashinda tu, kwa sababu wewe uko juu ya Haki
iliyo wazi, na mapuuza ya makafiri kukupuuza wewe hakutakudhuru kitu.
Rudi kwenye Sura
80. Ewe Mtume! Hakika wewe huwezi kuwaongoa hao, kwani hao ni kama
maiti kwa kuto tambua kitu, na kama viziwi kwa kutosikia. Basi hao hawako
tayari kuusikia wito wako kwa vile walivyo shikilia kukupuuza.
Rudi kwenye Sura
81. Na wala huwezi kuwaongoa kwenye Haki wale ambao wamepofuka kuona
kwao na kutambua kwao. Na huwezi kumfanya asikie ila mwenye kukubali kuziamini
Ishara zetu. Hao ndio wenye kut'ii na wenye kuitikia.
Rudi kwenye Sura
82. Na itapo karibia kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu kuileta Saa
ya Kiyama na kuwateremshia makafiri adhabu, Mwenyezi Mungu atawatolea watu
mnyama kwenye ardhi atakaye waambia miongoni mwa atakayo sema: Hakika makafiri
walikuwa hawaiamini miujiza yetu yote, na pia Siku ya Mwisho. Na hayo waliyo
kuwa wakiyakanusha sasa yamekwisha kuwa. Na hichi basi kitisho cha hiyo
Saa na yanayo fuatia!
Hii ndio tafsiri ya Aya hii kwa dhaahiri ya matamko yake. Na zipo
tafsiri mbili nyengine ambazo za hii Aya zinazo weza kuwa: Kwanza ni kuwa
makusudio ya "Dabbah" ni yeyote aendaye "yadibbu", katika watu au
wengineo. Na hapa inachukuliwa kuwa ni watu, watao kuja kabla ya Kiyama.
Na maana yake ni kuwa ikiwateremkia kauli juu yao na adhabu ikathibiti
watakuja makundi ya Waumini wakiwaendea, wakienea kote kote, wakizitikisa
nguzo za ukafiri. Tafsiri ya pili neno hilo "Dabbah" makusudio yake ni
watu waovu, ambao kwa ujinga ni kama wanyama, kama alivyo sema Al As'fahan
katika Muqarrarat yake. Na maana yake ni kuwa ikikaribia Siku ya Kiyama,
uovu na ufisadi utazidi, na Kiyama wanacho kikanusha makafiri ndio kitakuja.
Na hiyo kauli itakuwa, nayo si kauli ya kutamkwa kwa mdomo, lakini kwa
kuwa hali yenyewe itakuwa hivyo ni kama iliyo semwa, kama maoni yaliyo
kwisha tangulia.
Rudi kwenye Sura
83. Na ewe Mtume! Kumbuka siku tutapo wakusanya kutoka kila kundi
la wenye kukadhibisha Ishara zetu, nao ni hao waongozi wanao fuatwa. Basi
hao watachungwa wawe mbele ya kaumu zao kuendea hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura
84. Na pale watakapo simama mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya
hisabu, atasema Subhanahu kuwaambia kwa kuwadhili na kuwabinya: Nyinyi
mlizikadhibisha Ishara zangu zote, na mkazikataa bila ya kuzingatia wala
kufahamu. Na khasa mlikuwa mkitenda nini nanyi hamkuumbwa kwa upuuzi?
Rudi kwenye Sura
85. Na adhabu itawateremkia kwa sababu ya kujidhulumu nafsi zao kwa
ukafiri. Basi watakuwa hawawezi kujilinda wala kutaka udhuru.
Rudi kwenye Sura
86. Bila ya shaka wameshuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameufanya usiku
ili wapate kupumzika, na akaufanya mchana una mwangaza, wapate kushughulikia
kutafuta maisha yao. Hakika katika hayo zipo dalili wazi za Ungu wa Mwenyezi
Mungu, na Upweke wake, kwa watu wanao zingatia wakaamini.
Rudi kwenye Sura
87. Na taja, ewe Mtume, Siku atapo puliza Israfil baragumu
kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na watapo ingiwa kiwewe walioko katika mbingu
na katika ardhi kwa kitisho cha mpulizo huo, isipo kuwa huyo ambaye Mwenyezi
Mungu atamtuliza na akamhifadhi na kitisho. Na viumbe vyote watakuja
kwa Mola wao Mlezi nao ni madhalili.
Rudi kwenye Sura
88. Na unaiona, ewe Mtume, milima na unadhani haitaharaki imetulia
tu, lakini kwa hakika inakwenda mbio kama mawingu. Na haya ni katika uundaji
wa Mwenyezi Mungu aliye umba kila kitu na akakizua. Hakika Yeye, Subhanahu,
ni Mwenye kutimia ujuzi wake kwa yote wayatendayo watu, ya ut'iifu na maasi.
Naye atawalipa kwayo.
"Na unaiona milima unaidhunia imetulia; nayo inakwenda kama mwendo
wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila
kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo." Aya hii inathibitisha
kuwa vitu vyote vinavyo fuata mvutano wa ardhi, kama milima, bahari, na
funiko la anga n.k. vinashirikiana na dunia katika mzunguko wake wa kila
siku juu ya msumari-kati wake, na mzunguko wake wa kila mwaka kulizunguka
jua. Lakini mzunguko huu hauonekani. Ni kama kwenda kwa mawingu
angani.
Wanao tazama wanayaona, lakini hawasikii sauti yao, wala hawayagusi.
Inaonyesha Aya hii tukufu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu aliye tukuka, ameumba
ulimwengu na mipango yake ya kuiendeshea. Naye ni Muweza wa kuifanya hii
dunia imetulia tu haizunguki juu ya msumari-kati wake, au akaifanya kuzunguka
juu ya msumari-kati wake sawa sawa na kuzunguka kwake kulizunguka jua.
Na kwa hivyo ingeli kuwa nusu ya dunia imo kizani totoro kwa muda wa miezi
sita, na kwa muda wa miezi sita ikawa nusu ya pili imo katika mwangaza
moja kwa moja wa mchana. Na haya yangeli pelekea kuharibika mizani ya joto
katika dunia yote. Na kwa hivyo uhai ulioko ungeli toweka duniani. Na Mwenyezi
Mungu, Subhanahu wa Taa'la, ndiye aliye panga mpango huu uliopo kwa rehema
yake na huruma zake kwa waja wake.
Na juu ya kuwa Aristakhoris, mtaalamu wa ilimu ya falaki wa Iskandaria
(Alexandria) katika Misri, aliandika (310-230 K.K.) juu ya kuzunguka dunia
wenyewe kwa wenyewe, maandishi haya ya kisayansi ya kale yalikuwa hayajawafikia
Waarabu wakati wa Mtume Muhammad s.a.w. au kabla yake. Bali wa mwanzo wa
kuashiria mambo haya katika wao alikuwa Albiruni katika mwaka 1000 B.K.
(Baada ya Kuzaliwa Nabii Isa), baada ya kuingia kufasiriwa vitabu vya ilimu
za zamani kwa lugha ya Kiarabu ulio kuweko katika enzi za Banul Abbas.
Basi kutokea haya kwa ulimi wa Mtume Muhammad s.a.w. ambaye aliye kuwa
hajapata ilimu hiyo, ni dalili kuwa haya yalifunuliwa kwake na Mwenyezi
Mungu.
Rudi kwenye Sura
89. Kila mwenye kuleta wema katika dunia, nayo ni Imani na usafi
wa ut'iifu, atapata huko Akhera thawabu kubwa kabisa kwa ajili ya aliyo
yatanguliza. Na wenye mema haya watasalimika na khofu na kufazaika Siku
ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
90. Na kila mwenye kuleta uovu katika dunia - nao ni shirki na maasia
- na akafa na hayo, basi malipo ya kundi hili ni kuwa Mwenyezi Mungu atawasukumiza
juu ya nyuso zao katika Moto, na wataambiwa hapo kwa kuwatahayarisha: Hakika
hii leo hamlipwi ila kwa sababu ya shirki yenu na maasi yenu.
Rudi kwenye Sura
91. Ewe Mtume! Waambie watu: Sikuamrishwa nimuabudu yeyote isipo
kuwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa mji wa Makka aliye utukuza, na akaufanya
mtakatifu wenye amani, usio faa kumwagwa damu ndani yake, wala kuwindwa
wanyama wake, wala kukatwa miti yake. Na vitu vyote viliomo ulimwenguni
ni vya Mwenyezi Mungu kuvimiliki na kuvitawala, na mimi nimeamrishwa niwe
katika wanao mnyenyekea Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
92. Na nimeamrishwa nidumishe kuisoma Qur'ani, kwa ibada, na kuzingatia,
na kuwaitia watu wafuate yaliomo humo. Basi mwenye kuongoka, akaiamini,
na akakufuata wewe, basi kheri ya hayo na malipo yake ni kwa nafsi yake.
Na mwenye kupotea asiifuate Haki, na asikufuate wewe, mwambie: Hakika mimi
ni Mtume, naonya, na nafikisha Ujumbe tu.
Rudi kwenye Sura
93. Na sema, ewe Mtume: Alhamdu Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi
Mungu kwa neema ya Unabii na Uwongofu. Mwenyezi Mungu atakuonyesheni hapa
duniani athari za uwezo wake, na Akhera atakuonyesheni ukweli wa aliyo
kwambieni, na mtayajua vilivyo. Wala Mwenyezi Mungu hashindwi kukuhisabieni
wala haghafiliki na vitendo vyenu.
Rudi kwenye Sura