1. Mambo ya Mwenyezi Mungu yametukuka, na kheri yake
imezidi. Yeye ndiye aliye iteremsha Furqani, yaani Qur'ani,
ya kufarikisha baina ya kweli na uwongo juu ya mja wake, Muhammad
s.a.w., ili awe mwonyaji na mwenye kuifikisha hiyo Qur'ani kwa walimwengu
wote.
Rudi kwenye Sura
2. Yeye Subhanahu ndiye peke yake aliye miliki mbingu na ardhi, aliye
takasika na haja ya kuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika wowote katika
ufalme wake. Na Yeye kaumba kila kitu na akakipima kwa kipimo baraabara
kwa sharia zake ili kiweze kutimiza waajibu wake kwa nidhamu.
"Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana,
wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria
kwa kipimo." Ilimu ya sayansi ya sasa imethibitisha kuwa vitu vyote vinakwenda
kwa mujibu wa hukumu za uumbaji wake, na maendeleo yake namna mbali mbali
kwa kufuata mpango madhubuti ambao hapana mwenye uwezo juu yake ila Muumbaji
mwenye uwezo Mwenye kuanzisha kila kitu. Kwani katika kuwa kwake imebainika
kuwa vitu vyote viumbe vyote na vinga khitalifiana umbo lake na sura yake
kwa hakika vinatokana na madda chache za asli za kuhisabika, na hisabu
ya madda hizo (elements) zinakaribia mia, nazo ni 96 zinazo juulikana mpaka
sasa. Nazo zina khitalifiana kwa sifa zao za maumbile (physically ) na
za Al Kimyaa (Chemically), na pia katika uzito wake wa chembe (Atomic Weight).
Zinaanza kwa madda asli (element) Nambari 1. Nayo ni Hydrogen yenye
Atomic weight 1, na kuishia na element ya nambari 96, Borium, ambayo atomic
weight yake bado haijuulikani. Na element ya mwisho katika sayansi ni Uranium
na atomic weight yake ni 238.57. Na hizi elements hujengeka na kufanyika
Compounds kwa mujibu wa kanuni madhubuti zisio weza kuepukwa. Hali kadhaalika
mimea na wanyama. Kila mmoja wao amegawika katika koo na makundi na namna
(orders, families, species and sub-species) zinazo geuka sifa zake kwa
madaraja ya viumbe vilivyo hai mpaka kuishia viumbe vyenye Khalaya au Cell
moja (unicellular) kama microbes mpaka viumbe vyenye cells nyingi
(multi- cellular) mpaka kufikia binaadamu, naye ndiye aliye kamilika kuliko
wote. Na kila namna ya hizi sifa maalumu zinarithika katika kundi kizazi
baada ya kizazi. Na yote haya yanakwenda kufuata kanuni na mipango iliyo
thibiti madhubuti inayo onyesha kwa uwazi utukufu wa Mwenye kuumba na uwezo
wake. Ametakasika, Subhanahu na ametukuka na hao wanao mshirikisha
naye.
Rudi kwenye Sura
3. Na juu ya yote hayo makafiri wakaacha kumuabudu Yeye, wakenda
kuchukua miungu mingine kuiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, katika masanamu,
na nyota, na watu. Na hao hawanalo waliwezalo kuliumba, bali wao ni viumbe
vya Mwenyezi Mungu. Wala hawawezi kujikinga nafsi zao na madhara, wala
kujiletea kheri. Wala hawawezi kumfisha yeyote wala kumhuisha, wala kuwafufua
maiti kutoka makaburini kwao. Na kila asiye miliki lolote katika hayo basi
hastahiki kuabudiwa. Na mjinga wa kutupwa anaye waabudu. Mwenye kustahiki
kuabudiwa ni yule Mwenye kumiliki haya yote.
Rudi kwenye Sura
4. Makafiri wakaitia ila Qur'ani, wakasema kuwa hiyo ati ni
uwongo kauzua Muhammad mwenyewe, na akamsingizia Mwenyezi Mungu.
Na wakamsaidia baadhi ya jamaa wengine katika Ahli-l-Kitab. Basi hawa makafiri
wamefanya dhulma kwa kauli yao hiyo katika hukumu na kuishambulia Haki,
wakaleta uzushi usio kuwa na ushahidi wowote. Kwani hao wanao waashiria
katika Ahli-l- Kitab lugha yao hata si Kiarabu. Na Qur'an ni kwa lugha
ya Kiarabu fasihi.
Rudi kwenye Sura
5. Wakaisema Qur'ani pia kuwa ati ni uwongo walio andika watu wa
kale katika vitabu vyao, kisha akawataka wao wamuandikie na wamsomee asubuhi
na jioni mpaka ahifadhi na apate kusema naye hayo hayo.
Rudi kwenye Sura
6. Ewe Nabii! Waambie: Hakika Qur'ani ameiteremsha Mwenyezi Mungu
ambaye anazijua siri zilizo fichikana katika mbingu na ardhi. Na
ameziweka katika Qur'ani ya muujiza kuwa ni dalili ya kwamba hiyo ni Ufunuo
wake Subhanahu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira na rehema,
anawasamehe wenye kuasi pindi wakitubu, wala hafanyi haraka kuwaadhibu.
Rudi kwenye Sura
7. Wakamkejeli Muhammad, wakasema: Kitu gani kinacho mtengua huyu
anaye dai kuwa ni Mtume, hata anakula chakula kama tulavyo sisi, na anazururuka
masokoni kutafuta maisha kama watu wengine? Angeli kuwa ni Mtume Mwenyezi
Mungu angeli mtosheleza kwa hayo, na yeye angeli mwomba Mola wake Mlezi
amteremshie Malaika kutoka mbinguni amsaidie katika uwonyaji na kufikisha
Ujumbe, na amsadikishe katika wito wake, tupate sisi kumuamini.
Rudi kwenye Sura
8. Na hebu lau angeli mtaka amtosheleze chakula cha kutosha asihitajie
kuzunguka masokoni, akamtupia khazina kutoka mbinguni ya kutumia, au akamjaalia
na bustani ya kumlisha matunda yake? Na wakubwa wa makafiri walio
jidhulumu nafsi zao kwa ukafiri, wenye kuwapotoa watu wasimuamini Muhammad,
na wenye kufanya hila za kuwaingiza shaka Waumini, walisema: Nyinyi hamumfuati
ila huyu mtu aliye zugwa akili yake, basi anabwabwatika bila ya kuwa na
hakika.
Rudi kwenye Sura
9. Hebu angalia, ewe Nabii! Vipi wanavyo kupigia mifano hawa! Mara
wanakupigia mfano wa mwenye kurogwa, mara nyengine kuwa ati ni mwendawazimu,
mara ya tatu kuwa ni mwongo, na mara yane kuwa unaipokea Qur'ani kutokana
na wasio kuwa Waarabu. Hao kwa hayo hakika wameipotea njia ya haki, na
kuhojiana kulio sawa. Basi hawaitambui njia ya kufikilia yote hayo.
Rudi kwenye Sura
10. Mwenyezi Mungu ametukuka, na izidi kheri yake! Yeye ndiye ambaye
pindi akitaka atakujaalia duniani bora kuliko hayo wanayo pendekeza wao.
Kwa Akhera Yeye amekwisha kujaalia kama alivyo kuahidi, nayo ni mabustani
mengi yapitayo mito pembezoni mwake, na baina ya miti yake, na majumba
ya fakhari madhubuti.
Rudi kwenye Sura
11. Na kwa hakika hawa wamepinga kila Ishara. Kwani wao wamekanusha
kufufuliwa, na Siku ya Kiyama. Nao kwa hivyo wanayatia ila matakwa haya
ili kuwageuza watu washughulikie upotofu wao. Na Sisi tumekwisha
waandalia wanao ikanusha Siku ya Kiyama Moto wenye kuwaka vikali mno.
Rudi kwenye Sura
12. Wakiuona Moto, na huo Moto ukawaona, wataisikia sauti yenye hasira,
yenye hamu kuwateketeza. Na katika hayo ni mfano wa mingurumo inayo toka
kifuani mwa aliye kasirika kuwa ni alama ya ukali alio nao.
Rudi kwenye Sura
13. Na watapo tupwa katika pahali pembamba kwa kulingana na unene
wao, nao wamefungwa pingu mikono yao kwenye shingo zao, watapiga kelele
kuhimiza wateketezwe upesi upesi ili wapate kupumzika na kitisho cha adhabu.
Rudi kwenye Sura
14. Wataambiwa kwa kuwahizi na kuwakejeli: Msitake kuangamia mara
moja tu, bali takeni muangamie mara nyingi. Hamtopata kusalimika na hayo
mliyo nayo. Na hakika namna ya adhabu zao ni nyingi.
Rudi kwenye Sura
15. Ewe Nabii! Waambie makafiri: Je! Marejeo haya waliyo ahidiwa
makafiri ni bora au Pepo yenye kudumu neema zake, na ambayo wameahidiwa
Waumini, wachamngu, kuwa itakuwa yao kama ndio malipo na marejeo ya kwendea
baada ya kufufuliwa na kuhisabiwa?
Rudi kwenye Sura
16. Humo watapata wakitakacho, wataneemeshwa kwa neema za daima,
zisio katika. Na neema hizi ni ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao. Walimwomba
Mola wao Mlezi itimie, naye akawaitikia kwa walilo liomba; kwani ahadi
yake hayendi kinyume.
Rudi kwenye Sura
17. Na taja, kwa ajili ya mawaidha, Siku ambayo Mwenyezi Mungu atawakusanya
washirikina kwa ajili ya hisabu katika Siku ya Kiyama, pamoja na hao ambao
walikuwa wakiwaabudu duniani badala ya Mwenyezi Mungu, kama Yesu (Isa),
Ezra (Uzair) na Malaika. Mwenyezi Mungu atawauliza hao waabudiwa: Je! Ni
nyinyi ndio mlio wapoteza waja wangu, mkawaamrisha wakuabuduni, au wao
wenyewe ndio walio potea Njia kwa khiari yao, wakakuabuduni?
Rudi kwenye Sura
18. Jawabu yao itakuwa: Umetakasika, na Umetukuka! Haikutafalia sisi
kabisa tumtake mlinzi badala yako atunusuru na aangalie mambo yetu. Basi
itakuwaje juu ya haya tumtake yeyote atuabudu sisi badala yako Wewe? Lakini
sababu ya ukafiri wao hawa ni kuwa uliwastarehesha kwa muda mrefu duniani,
wao na baba zao. Hayo yakawapandisha kichwa, wakasahau kukushukuru, na
kukuelekea Wewe tu kwa ibada. Basi wakawa kwa jeuri hiyo na ukafiri huo
wanastahiki kuangamizwa.
Rudi kwenye Sura
19. Wataambiwa wenye kuabudu, washirikina: Wamekukadhibisheni hao
mlio kuwa mkiwaabudu, ambao mkidai kuwa wamekupotezeni. Basi nyinyi leo
mnarejea kwenye adhabu. Hamna hila ya kuepukana nayo; wala hamyapati manusura
ya kukutoeni. Na wajue waja wote kwamba mwenye kudhulumu kwa ukafiri na
uasi kama walivyo fanya hao basi Sisi tutawaadhibu adhabu kali.
Rudi kwenye Sura
20. Na ikiwa washirikina wanakutia ila ewe Nabii, kwa kula kwako
chakula, na kwenda kwako masokoni kwa ajili ya kazi na kuchuma maisha,
basi huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa Mitume wake walio kuja kabla
yako. Hatukumtuma yeyote kati yao ila alikuwa akila chakula, na anakwenda
kwenda masokoni. Na enyi watu! Tumewafanya baadhi yenu wawe ni mitihani
kwa wenginewe. Na mafisadi wanafanya hila kuziba Njia ya Uwongofu na Haki
kwa namna mbali mbali. Basi, enyi Waumini, mtavumilia juu ya Haki yenu,
na mtaishikilia Dini yenu, mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake kwa ushindi?
Subirini! Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuvizunguka vitu vyote, na atamlipa
kila mtu kwa kitendo chake.
Rudi kwenye Sura
21. Na wakasema wanao kataa kufufuliwa na wala hawatumai kuwa yapo
malipo kwa vitendo vyao: Kwa nini hatuteremshiwi Malaika wa kukuunga mkono,
au Mwenyezi Mungu akajionyesha kwetu na akatwambia kwamba kweli Yeye kakutuma?
Kiburi kimewajaa katika nafsi zao, na wamepita mpaka katika udhalimu na
ujabari!
Rudi kwenye Sura
22. Siku ya Kiyama watawaona Malaika kama walivyo tamani, na hayo
yatakuwa ni sababu ya kitisho kwao wala si jambo la kuwafurahisha. Watatafuta
kujilinda nao, kama walivyo kuwa wakitafuta kujilinda na vinavyo watisha
duniani.
Rudi kwenye Sura
23. Na Siku ya Kiyama tutawaletea waliyo yatenda katika mambo ya
kuonyesha wema kwa dhaahiri na hisani katika dunia, na Sisi tutayafanya
yaondokee patupu, na tutawaharimisha thawabu zake, kwa kuwa yamekosa Imani
ambayo ni dharura ipatikane ili vitendo vitiwe maanani.
Rudi kwenye Sura
24. Watu wa Peponi Siku ya Kiyama ndio watao kuwa na utulivu bora,
na mashukio mazuri, na makaazi ya starehe, kwa sababu hii ni
Pepo walio andaliwa Waumini, si Moto walio andaliwa makafiri.
Rudi kwenye Sura
25. Ewe Nabii! Itaje Siku itapo pasuka mbingu na ikafunguka, na yakadhihiri
kati yake mawingu, na Malaika wakashuka khasa kwa yakini.
Rudi kwenye Sura
26. Katika siku hii mali ya watu wenye mali yataharibika, madai yao
wanao jidai yatakatika, na Ufalme wote utabaki ni wa Arrahmani , Mwingi
wa Rehema, peke yake. Na itakuwa siku ya shida ngumu mno kwa makafiri.
Rudi kwenye Sura
27. Siku ya Kiyama mwenye kujidhulumu nafsi yake atajiuma mikono
yake kwa hasira na majuto kwa ukafiri wake na kumwendea kinyume Mtume,
na kwa kutamani atasema: Laiti lau ningeli mfuata Mtume, nikaifuata njia
ya kwendea Peponi, na nikaiepuka njia ya kwendea Motoni!
Rudi kwenye Sura
28. Na atasema kwa kujuta kuwafuata walio mpoteza: Laiti ningeli
kuwa sikumsadiki fulani, ambaye nimemwachia aniongoze.
Rudi kwenye Sura
29. Rafiki huyu amenibaidisha na Ukumbusho, Dhikr, kumkumbuka Mwenyezi
Mungu na kuikumbuka Qur'ani baada ya kwisha kuwa ni nyepesi kwangu. Ndio
hivi Shetani anavyo mkhini binaadamu, na kumtokomeza kwenye hilaki yake.
Rudi kwenye Sura
30. Na Mtume alisema akimshitakia Mwenyezi Mungu kwa taabu anazo
zipata kwa watu wake: Hakika hawa wameiacha Qur'ani na wameihama, na wameshikilia
katika kuipuuza, na kuifanyia inda na uadui.
Rudi kwenye Sura
31. Kama tulivyo wajaalia watu wako, ewe Muhammad, wanavyo kufanyia
uadui na kukukadhibisha, basi kadhaalika tulimjaalia kila Nabii ana maadui
miongoni mwa wakosefu, wanao mfanyia uadui na wanaupinga wito wake. Na
Mwenyezi Mungu atakunusuru, na atakuongoa mpaka uwashinde. Na Yeye anakutosha
kwa uwongofu na kukunusuru.
Rudi kwenye Sura
32. Na makafiri kutaka kuikebehi Qur'ani walisema: Kwa nini haikuteremshwa
kwa mara moja? Na Sisi hakika tumeiteremsha kwa mapande mapande ili moyo
wako uthibiti kwayo kwa raha yako na ili uihifadhi. Na tumeisoma, yaani
tumeigawa kwa Aya, au tumeisoma kwa ulimi wa Jibril, kidogo kidogo kwa
utulivu na upole.
Rudi kwenye Sura
33. Na wala hawakujii na upinzani dhaifu, ila nasi tunakuletea Haki
ya kubainisha, na bora ya maelezo.
Rudi kwenye Sura
34. Na walio ukataa Ujumbe wako watabururwa kupelekwa Motoni kifudifudi
na madhalili. Hao ndio watu wa chini kabisa kwa cheo, na ndio walio zama
mno katika upotovu.
Rudi kwenye Sura
35. Na Mtume s.a.w. anapozwa kwa yaliyo wapata Mitume wa kabla yake.
Hakika Sisi tulimteremshia Musa Taurati, na tukamkalifisha afikishe Ujumbe
wetu, na tukamuunga mkono kwa ndugu yake Harun, awe waziri wake na
msaidizi katika kazi yake.
Rudi kwenye Sura
36. Tukasema: Nenda wewe na nduguyo kwa Firauni na watu wake. Tukamuunga
mkono kwa miujiza inayo onyesha ukweli wake. Hawakumuamini, wakamkadhibisha.
Mwisho wao ukawa tukawateketeza na tukawafutilia mbali!
Rudi kwenye Sura
37. Hali kadhaalika kabla ya Musa tuliwafanyia kaumu ya Nuhu walipo
mkadhibisha, na aliye mkanusha Mtume mmoja basi amewakanusha Mitume wote.
Nao tukawazamisha katika tufani, na tukawafanya wawe ni zingatio kwa watu.
Na tukawajaalia hao na kila mshirikina kupata adhabu chungu Akhera.
Rudi kwenye Sura
38. Na kadhaalika tuliwahiliki A'di na Thamudi na watu wa Rass
(1) walipo wakanusha Mitume wao. Na tuliziangamiza kaumu nyingi baina ya
kaumu ya Nuhu na baina ya A'di, yakawapata malipo ya wenye kudhulumu.
(1) Rass, kama ilivyo elezwa katika Mufradaat ya Raaghib Al-As'fahani,
ni bonde, na akatolea ushahidi ubeti wa shairi: (Nao ni bonde la Rass,
kama mkono kwa mdomo.) Hao watu wa Rass, kama ilivyo kuja katika
Aya tukufu, ni watu walio kuwa wakiabudu masanamu. Mwenyezi Mungu aliwatumia
Shuaib. Basi hao ndio walio pelekewa Mtume Shuaib a.s. Na Mwenyezi Mungu
Aliye takasika amewaeleza hao kaumu ya Shuaib kuwa ni Watu wa Vichakani
(Al-Aykat), napo ni pahali penye miti mingi panasifika kwa neema, na mara
nyengine wanaitwa Watu wa Rass, nalo ni bonde lenye kheri kubwa, kuonesha
neema alizo waneemesha Mwenyezi Mungu. Nao wakazikufuru neema za Mwenyezi
Mungu, wakaabudu masanamu.
Rudi kwenye Sura
39. Na Sisi tumezionya kaumu zote hizi. Tukawakumbusha mawaidha,
na mifano ya kweli yenye manufaa. Lakini hawakuwaidhika. Tukawashika wote
kwa kuwaadhibu, tukawahiliki, na tukayabomoa majumba yao mpaka kifusi.
Rudi kwenye Sura
40. Na hawa Makureshi katika safari zao za kwenda Sham wanapita kwenye
mji wa kaumu Lut'i, tulio unyeshea mvua ya shari na ovu kabisa, nayo ni
mawe ya Motoni. Je! Hawauoni mji huo wakawaidhika kwa yaliyo wafika watu
wake? Hakika wao wanauona huo, lakini si kwa macho ya kuwaidhika na kuzingatia.
Kwani hawaamini ahadi (za Mwenyezi Mungu) wala kufufuliwa. Wala hawataraji
kuwa ipo siku watakuja fufuliwa kwa ajili ya hisabu.
Rudi kwenye Sura
41. Na wakikuona watu hawa hawakuchukulii ila kukufanyia kejeli na
maskhara. Na huambiana wao kwa wao: Ndiye huyu aliye mtuma kwetu Mwenyezi
Mungu awe ni Mtume, na sisi tumfuate twende nyuma yake?
Rudi kwenye Sura
42. Mtu huyu hakika kajaaliwa kuwa na ufasihi mzuri, na hoja za kuvutia
kwa wanao msikia. Na hapana shaka ameweza kuchota katika imani zetu hata
alikaribia kututoa kwa miungu yetu tumfuate mungu wake. Lakini sisi tumesimama
imara juu miungu yetu na dini yetu. (Mwenyezi Mungu anasema:) Tutakuja
wabainishia ukweli wa mambo watapo kuja iona adhabu Siku ya Kiyama, na
watajua nani huyo aliye thibiti katika upotovu na makosa.
Rudi kwenye Sura
43. Ewe Mtume! Umeona upotovu wa mwenye kufuata matamanio yake na
pumbao lake hata akawa anaabudu mawe ambayo hayadhuru wala hayanafiishi?
Na wewe umetumwa uwe mwonyaji na mbashiri, wala hukuwakilishwa kwa imani
yao na uwongofu wao.
Rudi kwenye Sura
44. Na hivyo unadhani kuwa wengi wao wanasikia kwa sikio la kufahamu
au wanaongoka kwa akili zao? Wamesha tupilia mbali kama walivyo amrishwa
na ndoto zao. Wamekuwa kama wanyama wa kufuga, hawanalo linalo washughulisha
ila kula, na kunywa, na kustarehe na maisha ya dunia. Wala hawana fikra
yoyote baada ya hayo. Bali hali yao ni ovu zaidi kuliko ya wanyama, kwani
wanyama huwafuata bwana zao katika yenye kheri nao, na wanayaepuka ya kuwadhuru.
Lakini watu hawa wanajitokomeza wenyewe kwenye mambo ya kuwahiliki.
Rudi kwenye Sura
45. Tumesimamisha dalili za Tawhidi, Upweke wa Mwenyezi Mungu, za
kuwaongoa wenye akili. Hebu kiangalie kivuli. Mwenyezi Mungu amekitandaza
na akakifanya kimetulia mwanzo wa mchana. Kisha tukalipeleka jua likaondoa
pahala pake kwa mwako wake. Likawa jua ni kama ndio linaongoza kivuli.
Bila ya jua, kivuli kisingeli juulikana. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu ange
penda angeli kifanya kivuli kitulie vile vile kimewang'ang'ania watu, na
yakawaharibikia maslaha yao na mambo yao.
" Je! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli.
Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa
ni kiongozi wake." Aya hii inadhihirisha hima ya Muumba na uwezo
wake. Kwani kutandaza kivuli kunaonyesha mzunguko wa dunia na kuinama kwa
msumari-kati (axis) wake. Na lau kuwa ardhi, yaani dunia, ingeli tulia
tu, haitaharaki kulizunguka jua, na pia ikawa haizunguki wenyewe kwa wenyewe
juu ya msumari-kati wake, basi kivuli kingeli tulia, na mwako wa jua ungeli
piga juu ya nusu ya dunia, na nusu ya pili ikabaki ni usiku, moja kwa moja.
Hayo yangeli leta khitilafu kubwa za baridi na joto, na ingeli pelekea
kutoweka uhai kabisa katika dunia. Na kadhaalika ingeli kuwa hii ni hali
ya dunia basi kivuli kingeli tulia. Na haya pia yange tokea ikiwa muda
wa kuzunguka ardhi juu ya msumari-kati wake ndio muda ule ule muda wa kuzunguka
kwake kulizunguka jua, yaani siku moja ikawa sawa na mwaka mzima. Lakini
hapana awezaye kufanya hayo isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Haya licha ya kuwa
kivuli nafsi yake ni neema miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu. Na lau
kuwa Mwenyezi Mungu aliviumba vitu vyote vyapenyeza mwangaza (transparent)
kisingeli kuwapo kivuli, na vitu visingeli pata fursa ya kuwepo ambavyo
vinahitajia vivuli.
Rudi kwenye Sura
46. Na kukiondoa kwetu kivuli ni kwa utaratibu, kwa kipimo. Hakukuwa
kwa mara moja. Na katika hayo yapo manufaa kwa watu.
Rudi kwenye Sura
47. Na katika Ishara za Tawhidi ni kuwa tumeufanya usiku ni sitara
kwa kiza chake, ndani yake wanaingia viumbe ukawazunguka kama inavyo wazunguka
nguo kwa mwenye kuivaa. Na tukawatengenezea malazi, ikawa ni mapumziko
kupumzika na machofu, na kwa mwangaza wa jua wanazinduliwa watu watafute
maisha yao na riziki zao.
Rudi kwenye Sura
48. Na Yeye ndiye aliye zifanya pepo zimtumikie, zikasukuma mawingu,
nayo yakawabashiria watu itakuja mvua, ambayo ni rehema itokayo kwake kuwaendea
wao. Na hakika Sisi tunateremsha kutoka mbinguni maji safi yanayo safisha
kuondoa najisi na uchafu.
"Na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi." Katika Aya
hii tukufu Mwenyezi Mungu anawasimbulia watu kwa kuwateremshia maji yaliyo
safi kutoka mbinguni. Na Aya hii inafahamisha kuwa maji ya mvua katika
asli ya kuumbwa kwake ni maji safi kabisa. Na juu ya kuwa baada yake yanabeba
takataka nyingi katika anga, lakini bado yamo katika daraja ya usafi.
Rudi kwenye Sura
49. Tunaiteremsha mvua kwa sababu makulima yapate kumea na
kukua, na ardhi ipate kufufuka baada ya kufa kwake, na wanyweshwe
watu na wanyama walio umbwa.
Rudi kwenye Sura
50. Na hii Qur'ani tumeibainisha na tumeisarifu, tumeifanya, ili
watu wamkumbuke Mola wao Mlezi, na wawaidhike, na watende kwa mujibu
wake. Lakini wengi wa watu wanakataa isipo kuwa ukafiri na inda tu.
Rudi kwenye Sura
51. Na lau kuwa tumetaka basi tungeli mpeleka mwonyaji kwenye kila
mji. Basi jitahidi na wito wako; na wacha maneno ya makafiri; na tupilia
mbali wanayo yaleta.
Rudi kwenye Sura
52. Na endelea na kulingania kwako kwa Haki, na kufikisha Ujumbe
wa Mola wako Mlezi. Na wao wakiupinga wito wako, na wakawavamia Waumini
basi wapige vita, na kwa hayo pigana Jihadi kubwa.
Rudi kwenye Sura
53. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziendesha bahari mbili, bahari
ya maji matamu na bahari ya maji ya chumvi. Na akafanya njia ya kila moja
inakaribiana na nyengine. Na juu ya hivyo maji yao hayachanganyikani. Hiyo
ni neema na rehema kwa watu.
"Naye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na
hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho."
Yamkini Aya hii inaashiria neema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kwa kuto
changanyika maji ya chumvi yanayo penya kutoka baharini kwenye miamba ya
karibu na mwambao, na maji matamu yanayo penya kutoka bara, yasichanganyike
kwa ukamilifu na hali nayo yanakutana. Matamu yanakuwa yako juu ya maji
chumvi kama kwamba baina yao pana kinga kinacho zuia haya yasiingiane na
haya, na kizuizi kizuiacho, yaani kizuizi chembamba tusicho weza kukiona.
Na haya si tu, bali ipo kanuni madhubuti inayo hukumu makhusiano
haya, na inayo yahukumu kwa maslaha ya wanaadamu wanao kaa katika maeneo
hayo, na maisha yao yanategemea kuwepo hayo maji matamu. Kwani imethibiti
kuwa t'abaka ya maji matamu yalioko juu huzidi unene wake kwa mujibu wa
kuzidi usawa (level) wa bahari kwa mpango maalumu. Hata inakuwa yawezekana
kuhisabu kina cha mwisho cha maji matamu ambayo yamkinika kuyapata. Kwani
hiyo ni sawa sawa na kadri ya khitilafu baina ya usawa (level) wa ardhi
na usawa wa bahari mara arubaini.
Rudi kwenye Sura
54. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba kutokana na manii hawa watu,
na akawajaalia wanaume na wanawake walio khusiana kwa nasaba ya kuzaana
na kwa ushemeji wa kuoana. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza kwa atakayo, kwani
kwa hiyo hiyo manii ameumba namna mbili mbali mbali.
Rudi kwenye Sura
55. Na baada ya Ishara hizi zenye kuonyesha kuwa Mwenyezi Mungu peke
yake ndiye anaye stahiki kuabudiwa, na kwamba hapana mungu isipo kuwa Yeye,
wanatoka kikundi cha watu kuabudu masanamu yasiyo wafaa wala kuwadhuru.
Na hawa kwa kujua kwao haya wanamsaidia Shetani, na yeye anawapoteza. Basi
hao inakuwa wanasaidiana katika kuipinga Haki ambayo Mwenyezi Mungu anawaitia.
Rudi kwenye Sura
56. Na ewe Nabii! Huna jukumu ila kufikisha hayo ulio tumwa basi,
na kuwabashiria Pepo Waumini, na kuwakhofisha makafiri kwa haya watayo
yakuta. Baada ya hayo huna jengine unalo takiwa.
Rudi kwenye Sura
57. Na waambie: Hakika mimi sitafuti kwa huku kukuiteni muufuate
Uislamu ujira wowote wala malipo. Ila nilitakalo ni mwongoke na muifuate
Njia ya Haki mrejee kwa Mola wenu Mlezi.
Rudi kwenye Sura
58. Na katika mambo yako mtegemee Mwenyezi Mungu Aliye Hai, ambaye
hayumkini kufa. Na mtakase na mtukuze kwa kuzisifu neema zake. Na waachilie
mbali walio toka kwenye Njia. Kwani Mwenyezi Mungu anawajua vyema, na atawalipa
kwa dhambi zao.
Rudi kwenye Sura
59. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi na vilio
baina yao kwa siku sita. Naye ametawala juu ya A'rshi, Kiti cha Enzi, cha
Ufalme wote, na madaraka yake yameenea kila kitu. Na Yeye ndiye Mwingi
wa Rehema, Arrahman. Na ukitaka lolote katika sifa zake muulize ajuae atakujibu.
Naye ni Mwenyezi Mungu Mwenye hikima.
"Ambaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku
sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Ulize
khabari zake kwa wamjuaye." Hizo Siku Sita ni usemi wa Mwenyezi Mungu,
Mtukufu Aliye tukuka, kueleza wakati. Na Yeye Mtukufu ndiye Mwenye kujua
zaidi kipimo cha hiyo Siku. Na kwa upande wa kiilimu za sayansi kazi
ya kuumba ulimwengu unahitaji kupita vipindi na viwango mbali mbali. Na
"Mbingu na ardhi na viliomo ndani yake" ni ishara ya vyombo vyote vya mbinguni,
nyota, majua, sayari, miezi, mavumbi, gesi za namna mbali mbali, na nishat'i,
Energy , na vyote hivyo vinavyo fanya ndio ulimwengu wa duniani na
angani. Na kwa kuupanga ulimwengu wote, yaani uumbaji wote, kwa tafsili
ya ukamilifu inayo kusanya kila kitu, ndio inaweka wazi, Utawala
wa Mwenyezi Mungu, Subhanahu juu ya ulimwengu kwa jumla na kwa tafsili.
"Uliza khabari zake kwa ajuaye". Katika kifungu hichi cha Aya hii tukufu
pana uwongozi wa kisayansi kutokana na Mwenyezi Mungu kuonyesha dharura
ya uchunguzi na utafiti wa mambo yanayo onekana ya uumbaji na mipango yake
tuyaangalie ya ndani, ili tujue siri za uweza wa Mwenyezi Mungu katika
kuanzisha huu ulimwengu.
Rudi kwenye Sura
60. Na wakiambiwa hawa makafiri: Mnyenyekeeni Arrahmani, Mwingi wa
Rehema, na mumuabdu, wao husema: Nani huyo Arrahmani? Sisi hatumjui, hata
tumsujudie. Basi tukufuate amri yako tu? Na wanazidi kuwa mbali na kutengeka
na Imani.
Rudi kwenye Sura
61. Ametukuka Arrahman, Mwingi wa Rehema, na zimezidi fadhila zake.
Ameziumba sayari mbinguni na akazijaalia na vituo vyake vya kupitia, na
katika hizo akaumba jua kuwa ni taa yenye mwangaza, na mwezi wenye nuru.
"Ametukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo
taa na mwezi unao ng'ara." Aya hii tukufu inaashiria maana za ki-ilimu
za sayansi zenye kukusanywa katika mpango wa ulimwengu alio uumba Mwenyezi
Mungu, Aliye takasika, Aliye tukuka, na zikazidi fadhila zake. Na sisi
tunashuhudia nyota za mbinguni kwa sura ya makundi ambayo takriban hayageuki
sura na yangapitiliwa na karne, na Buruuj nayo ndio hayo makundi ya nyota,
ni yale yale yanayo pitiwa mbele yake na jua katika mzunguko wake unavyo
dhihiri kuizunguka ardhi. Hizo Buruuj ni kama vituo vya jua katika mzunguko
wake katika mwaka. Na kila tatu katika hizo huwa ni musimu katika misimu
ya mwaka. Nazo kwa kuzitaja moja moja kuanzia msimu wa Rabii' (Spring)
unao kuja baina ya siku za baridi na joto, ni kama ifuatavyo kwa majina
ya Kiarabu na Kizungu: Alh'aml (Aries, or Ram), Ath-thawr (Taurus),
Aljawzaa' (Gemini), Assarat'aan (Cancer), Al Asad (Leo), Assunbulah (Spica),
Al Miizaan (Libra), Al-A'qrab (Scorpion), Al Jadyu (Capricorn), Addalwu
(Aquarius), Alh'uut (Pisces). Na jua ni moja katika nyota zenye nguvu
za kati na kati. Nalo kama nyota zilizo baki lina mwangaza wake mwenyewe
wa dhati kwa vituko vya kichembechembe (atomic reaction) vinavyo tokea
ndani yake. Basi miale ya jua inayo toka kwenye nguvu hizo huangukia juu
ya sayari, na ardhi, na miezi, na vyombo vilio baki vya mbinguni ambavyo
havina mwanga wa nafsi yao. Kwa hivyo navyo hutoa nuru. Basi jua ndio Taa
inayo waka kwa nafsi yake. Ama mwezi unarudisha nuru ya mwanga wa jua kutokana
na uso wake, kama kiyoo. Hakika kwa kusifiwa Jua kuwa ni Taa, na ukasifiwa
mwezi kuwa unatoa nuru, ni ishara ya kuwa Jua ndio chanzo cha nguvu, nishati,
(T'aaqah, Energy) za joto.
Rudi kwenye Sura
62. Mwingi wa Rehema ndiye aliye ufanya usiku na mchana kufuatana,
mmoja nyuma ya mwenzie. Na tumeyapanga haya ili mwenye kutaka akumbuke
mpango huu, na ajue hikima ya Mwenyezi Mungu na uweza wake; au apate kushukuru
kwa neema hii njema.
Rudi kwenye Sura
63. Na waja wa Mwenyezi Mungu ni wale wanao nyenyekea duniani. Wakitembea
katika ardhi wanatembea kwa utulivu na staha. Hali kadhaalika katika mambo
yao yote. Na masafihi katika washirikina wakiwasubu wanawaachilia mbali
na shani yao, na wanawaambia: Hatuna shani nanyi. Letu sisi ni Assalamu
Alaikum!
Rudi kwenye Sura
64. Na wale ambao wanakesha katika ibada na Sala, wakimdhukuru Mwenyezi
Mungu kwa wingi.
Rudi kwenye Sura
65. Na wale ambao khofu yao inashinda matarajio - nao ndio mwendo
wa wachamngu. Basi wanaikhofu adhabu ya Akhera, na hawaachi kumwomba Mwenyezi
Mungu awaepusha na adhabu ya Jahannamu. Kwani adhabu yake ikimteremkia
mkosefu inamganda, wala haimwachi.
Rudi kwenye Sura
66. Na hakika Jahannamu ni kituo kiovu mno kwa mwenye kutua, na makao
maovu kwa mwenye kukaa ndani yake.
Rudi kwenye Sura
67. Na katika alama za waja wa Mwenyezi Mungu ni kuwa wana kiasi
katika kutumia kwao mali, kwa ajili ya nafsi zao na jamaa zao. Wao hawafanyi
ubadhirifu, wala hawabanii matumizi bila ya kiasi. Bali kutoa kwao ni kati
kati baina ya hayo.
Rudi kwenye Sura
68. Na katika sifa zao hao waja wa Mwenyezi Mungu ni kuwa wameisafia
niya Tawhid, na wakatupilia mbali kila athari ya ushirikina katika kumuabudu
Mola wao Mlezi. Na wakajizuia kuuwa nafsi aliyo kataza Mwenyezi Mungu kuuliwa,
ila ikiwa imefanya uadui basi huuliwa kwa haki. Nao hujitenga mbali na
uzinzi, na katika mambo ya starehe hawatendi ila lilio halali tu, ili waepukane
na adhabu ya mambo yanayo angamiza. Kwani anaye tenda katika mambo hayo
atakuta shari na adhabu.
Rudi kwenye Sura
69. Na Siku ya Kiyama atapata adhabu mardufu kuliko hiyo, na atadumu
Motoni kwa udhalili na unyonge.
Rudi kwenye Sura
70. Lakini mwenye kutubu na madhambi haya na akawa mkweli katika
Imani yake, na akafuatiliza hayo kwa ut'iifu na vitendo vyema, hao atawasamehe
kwa rehema yake, na atawajaalia bora ya thawabu badala ya maovu yaliyo
kwisha tangulia. Na hakika shani ya Mwenyezi Mungu ni kurehemu na kusamehe.
Rudi kwenye Sura
71. Na hivyo ndio mambo yetu yendavyo, yaani kuwa mwenye kutubu madhambi,
na akaonyesha matokeo yake katika kukubali ut'iifu na kuepuka maasi, basi
huyo Mwenyezi Mungu huikubalia toba yake. Na kwa hivyo hurejea kwa Mola
wake Mlezi baada ya kumwacha kwake.
Rudi kwenye Sura
72. Na katika khulka za waja wa Mwingi wa Rehema ni kuwa wanajiepusha
na kutoa ushahidi wa uwongo, na wakisadifu kukutana na mtu asiye kuwa na
kauli au kitendo chema hawashirikiani naye katika hayo, na huacha kufuatana
naye.
Rudi kwenye Sura
73. Na katika sifa zao ni kuwa mwenye kuwaidhi akiwapa mawaidha,
na akawasomea Aya za Mwenyezi Mungu, humwelekea kumsikiliza, na nyoyo zao
zikawaidhika, na macho yao hufunuka. Wala hawawi kama wale ambao wanatapatapa
wanapo yasikia, wanapuuza, masikio yao hayapenyi kitu, wala macho yao hayafumbuki.
Rudi kwenye Sura
74. Na wao humwomba Mola wao Mlezi awajaalie wake zao na watoto
wao wawe wa kuwapoza moyo kwa vitendo vya kheri, na awajaalie wawe ni waongozi
katika kheri ili watu wema wawafuate.
Rudi kwenye Sura
75. Hawa wenye kusifiwa kwa sifa hizi tulizo zitaja ndio waja wa
Mwenyezi Mungu wa kweli. Na malipo yao ni makao ya Peponi ya juu, kuwa
ni jazaa ya kusubiri kwao juu ya ut'iifu. Na huko Peponi watakuta maamkio,
na kusalimiwa.
Rudi kwenye Sura
76. Na neema zao za Peponi ni za daima, hazikatiki. Pepo ndio kituo
na makao mema kabisa.
Rudi kwenye Sura
77. Ewe Mtume! Waambie watu: Mwenyezi Mungu hakutakini nyinyi ila
mumuabudu Yeye, na mumwombe Yeye katika mambo yenu, wala msimwombe yeyote
mwenginewe. Na kwa hayo ndio kakuumbeni. Lakini makafiri katika nyinyi
wameyakanusha waliyo kuja nayo Mitume. Basi adhabu yao itawaganda hao,
wala hapana wa kuwaokoa nayo.
Rudi kwenye Sura