1. Sura hii tumeifunua na tumewajibisha hukumu zake,
na tumeteremsha ndani yake dalili zilizo wazi za kuthibitisha uwezo wa
Mwenyezi Mungu na upweke wake, na kwamba Kitabu hichi kinatoka kwake, ili
mpate kuwaidhika.
Rudi kwenye Sura
2. Na miongoni mwa hukumu hizo ni hukumu ya mwanamke na mwanamume
wenye kuzini. Basi kila mmoja wao mpigeni fimbo mia. Wala huruma kwao isikuzuieni
kutimiza hukumu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.
Kwani yanayo takikana na Imani ni kukhiari kumridhi Mwenyezi Mungu kuliko
kuwaridhi watu. Na wahudhurie baadhi ya jamaa Waumini waone hiyo adhabu
inavyo tekelezwa, ili adhabu hiyo iwatishe wenginewe wasitende hivyo.
Rudi kwenye Sura
3. Mwanamume muovu aliye zoea uzinifu hapendi kumwoa ila mchafu
anaye zini au mshirikina. (1). Na mwanamke mchafu ambaye kazi yake
ni uzinifu hapendelei kuolewa ila na mchafu anaye zini;au mshirikina.
Na ndoa namna hii haiwaelekei Waumini, kwa kuwa imeshabihi fiski na kupelekea
kutuhumiwa.
(1) Haya ikiwa haikupita toba. Na tafsiri ya haya ni kuwa inabainishwa
tabia za washirikina au wazinifu kuwa wao hawapendi ila mambo ya ufisadi
tu. Na kwa mujibu wa maoni ya Hambali na Ahli-Dhaahir (na pia Ibadhi) haisihi
ndoa ya mwanamume mzinifu au mwanamke mzinifu kabla ya toba.
Rudi kwenye Sura
4. Na wanao watuhumu wanawake wenye hishima zao wasio na makosa kwa
tuhuma ya uzinzi bila ya kuleta mashahidi wane wa kuthibitisha tuhuma yao,
waadhibuni kwa kuwapiga fimbo thamanini, na wala ushahidi wao usikubaliwe
tena kwa jambo lolote muda wa uhai wao. Basi hawa ndio wanao faa kuitwa
kwa jina la walio toka vibaya kwenye mipaka ya Dini.
Maoni ya Wataalamu juu ya Aya 2-4
" Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika
wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya
Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.
Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini. Mwanamume mzinifu hamwoi
ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi
ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo yameharimishwa kwa Waumini.
Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane,
basi watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na
hao ndio wapotovu." Makosa katika Sharia ya Kiislamu ni mambo yaliyo harimishwa
na Mwenyezi Mungu akayakemea kwa kuyawekea adhabu au izara ya kufedhehesha.
Na maharimishwa hayo ama ni kutenda kilicho katazwa kukitenda, au kuacha
kutenda kilicho amrishwa na Sharia kutendwa. Na sababu ya kuharimishwa
haya yaliyo katazwa ni kuwa hayo ni kupiga vita moja katika maslaha yanayo
kubaliwa katika Uislamu. Na maslaha hayo yanayo kubaliwa ni matano, nayo
ni:
1. Kuhifadhi nafsi. 2. Kuhifadhi Dini.
3. Kuhifadhi akili.
4. Kuhifadhi mali 5. Kuhifadhi hishima.
Kuuwa kwa mfano ni kuipiga vita nafsi. Na kurtadi, kutoka katika
Uislamu, ni kuipiga vita Dini. Na kutumia vinavyo levya ni kuipiga vita
akili. Na wizi ni kuyapiga vita mali. Na uzinzi ni kuipiga vita hishima.
Na wanazuoni wa ilimu ya Fiqhi (Sharia) wameyagawa makosa sehemu
mbali mbali. Lakini sisi yatutosha kwa sababu ya kueleza Aya hizi kugawa
kwa mujibu wa uzito wa adhabu zake, na namna ya kiasi chake. Nayo yamegawika
mafungu matatu:
1. H'udud, yaani Adhabu. 2. Kisasi au Diya 3. Izara, au Fedheha.
Ama H'udud, au Adhabu, ni makosa ambayo yanaonekana kuwa yanaingilia
kuvunja Haki ya Mwenyezi Mungu, au kuwa Haki ya Mwenyezi Mungu ni kubwa
zaidi ndani yake kuliko haki ya binaadamu. Na kwa hivyo ndio Mwenyezi Mungu
akaiwekea MIPAKA ndio maana khasa ya H'udud. Kaiwekea mipaka adhabu yake
katika Qur'ani au katika Sunna za Mtume s.a.w. Ama makosa ya Kisasi na
Diya ni makosa ambayo baadhi kubwa yake yamewakhusu wenyewe waja. Mwenyezi
Mungu amewekea adhabu za baadhi yake katika Qur'ani au katika Sunna za
Mtume s.a.w., na amewaachilia mengine wapime wenyewe wenye madaraka. Mfano
wa hayo makosa ya kumwaga damu, kama kuuwa na kukata viungo, na kujuruhu.
Ama makosa ya Izara, Uislamu umejitosheleza kwa kutaja mwisho wa
ukali na mwisho wa upole katika adhabu zao, na kuachia yaliyo baki wenye
kutawala wahukumie kwa kila kosa kwa mujibu wa hali na zama yanapo tokea
makosa.
Makosa ya H'udud ni saba:
1. Uzinzi. 2. Kuzulia wanawake mahashumu wasio na makosa.
3. Udhalimu. 4. Wizi. 5. Uharamia. 6.Ulevi.
7. Kurtadi. (Kutoka katika Uislamu).
Mwenyezi Mungu ameyawekea mipaka yote makosa hayo na ameyaleta kwa
hisabu yake katika Qur'ani, kama alivyo wekea adhabu zake katika Qur'ani
vile vile, isipo kuwa adhabu ya mwenye kuzini naye amewahi kuoa, yaani
Zaani Muh's'an, ambaye hupigwa mawe, na mlevi na adhabu yake ni fimbo thamanini,
na adhabu ya mwenye kurtadi ambaye jaza yake ni kuuwawa. Hayo yamekuja
katika Sunna.
Na zimezoea hizi kanuni za kuundwa na watu katika kupinga makosa
ya uzinzi kwa adhabu khafifu kama vile kifungo, hata ndio uchafu ukaenea
kati ya watu, na fiski na ukahaba ukazagaa, na hishima zikapotea, na maradhi
yakakithiri, na nasaba za ukoo zikachanganyika. Katika jambo la ajabu ni
kuwa hizi kanuni za kisasa za nchi zinazo ambiwa za kistaarabu ndio zinazo
yalinda makosa haya. Katika kanuni za adhabu za Kifaransa, kwa mfano, wazinzi
wasio oa wala kuolewa hawapati adhabu yoyote maadamu wao wakiwa wamekwisha
fikilia utu uzima. Kwa kuwa ati uhuru wao wa binafsi unataka waachiliwe
wajifanyie wenyewe watakalo. Ama mzinzi mwanamume aliye na mke, au mwanamke
mwenye mume, basi huyo adhabu yake ni kifungo. Lakini mwana sharia wa serikali
haingii kuchunguza ila akipata mashtaka kutokana na mume au mke. Na inaonyesha
kuwa ni haki ya mume tu kuwa hilo kosa limetokea au la, kwani ikiwa yeye
ndiye aliye fikisha mashtaka, basi yeye anaweza kuyafuta pia, na uchunguzi
utasita. Na yeye anaweza kumsamehe mkewe akatoka gerezani kabla ya kutimiza
muda wa kifungo chake ijapo kuwa hukumu ilikuwa ni juu yake huyo mwanamke
mwishoni.
Na wapo baadhi ambao ati wanaushutumu Uislamu kwa ukali wake kushadidia
kwake kuadhibiwa wazinifu. Yaliyo elekea zaidi ni kuwa lau wangeli zingatia
kuwa kama ilivyo kuwa adhabu ni kali, hali kadhaalika umeshadidiwa ushahidi
kwa jambo hili. Kwani ijapo kuwa katika kosa la mauwaji yatosha ushahidi
wa mashahidi wawili waadilifu, katika uzinzi ni lazima wapatikane mashahidi
wane waadilifu walio ona kitendo hicho kwa macho yao, au aungame mkosa!
Hayo, na tunaona kuwa Qur'ani Tukufu imelazimisha kuwa kupigwa hizo
fimo kuwe jahara ili mkosa ajuulikane, na iwe ni onyo kuwakhofisha wenginewe.
Rudi kwenye Sura
5. Lakini mwenye kutubu katika wao akajuta kwa maasi yake, na akaazimia
kuwa mt'iifu na kuonyesha ukweli wa toba yake kwa kwenda kwake mwendo mwema,
basi Mwenyezi Mungu atamsamehe kumuadhibu.
Rudi kwenye Sura
6. Na hao wanao watuhumu wake zao kuwa wamezini na hawana mashahidi
wanao takikana kushuhudia ukweli wa tuhuma yao, basi anatakikana mmoja
wa hao kama anataka isimpate adhabu, ashuhudie kwa Mwenyezi Mungu mara
nne kuwa yeye ni mkweli katika hiyo tuhuma yake.
Rudi kwenye Sura
7. Na mara ya tano aseme kuwa yeye anastahiki kutengwa na rehema
ya Mwenyezi Mungu akiwa ni mwenye kusema uwongo kwa hayo.
Rudi kwenye Sura
8. Baada ya haya mwanamke akinyamaza kimya itampasa kupata adhabu
ya uzinzi. Ili kujikinga na adhabu yampasa ashuhudie kwa Mwenyezi Mungu
mara nne kwamba mumewe ni mwongo kumtuhumu yeye kwa uzinzi.
Rudi kwenye Sura
9. Na ataje katika mara ya tano kuwa yeye mwanamke anastahiki ghadhabu
ya Mwenyezi Mungu imshukie ikiwa mumewe ni mwenye kusema kweli katika tuhuma
yake.
Rudi kwenye Sura
10. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufanyieni fadhila na akakurehemuni,
na kuwa Yeye ni Mwingi wa kukubali toba za waja wake, na Mwenye hikima
katika vitendo vyake vyote, asingeli kufanyieni sharia za hukumu hizi,
na angeli fanya haraka kukuadhibuni duniani kwa maasia.
Rudi kwenye Sura
11. Hakika hao walio zua uwongo ulio potoka na kila uwongofu kumzulia
Aisha, mke wa Nabii s.a.w. walipo mtangazia uzushi, ni kikundi wanao ishi
pamoja nanyi. Msidhani kituko hichi ni shari kwenu, bali ndiyo kheri yenu;
kwa sababu kimewapambanua baina ya wanaafiki na Waumini wa kweli. Na ukadhihiri
ukarimu wa walio wema na wenye kuingiwa na uchungu. Na kila mtu katika
hawa walio tuhumu watapata malipo yao kwa mujibu wa kadri alivyo shiriki
katika uzushi huu. Na mkuu wa kikundi hichi ndiye ataye pata adhabu kubwa
kwa ukubwa wa makosa yake.
Rudi kwenye Sura
12. Ilikuwa inavyo takikana kwa Imani ni kuwa wakati wa kusikia huu
uzushi, ni Waumini wanaume na wanawake wajidhanie nafsi zao kheri ya usafi
na unadhifu, na waseme kwa kupinga: Huu ni uwongo ulio wazi umezuliwa,
kwa kuwa haya yamemkhusu bora ya Mitume na bora ya wanawake walio wa kweli.
Rudi kwenye Sura
13. Je! Hao wazushi walileta mashahidi wane wa kushuhudia hayo waliyo
yasema? Hawakufanya hayo...Na ikiwa hawakufanya basi hao kwa hukumu ya
Mwenyezi Mungu ni waongo.
Rudi kwenye Sura
14. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakukufanyieni fadhila kwa kubainisha
hukumu, na hakukurehemuni duniani kwa kuacha kuleta adhabu kwa haraka,
na Akhera kwa kukusameheni, angeli kuteremshieni adhabu kubwa kwa sababu
ya kujiingiza kwenu katika uzushi huu.
Rudi kwenye Sura
15. Mmezichukua khabari hizo kwa ndimi zenu na mkazieneza kati yenu.
Wala nyinyi hamkujua kuwa hizo ni khabari za kweli, na mkaona jambo hili
ni dogo si la kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu, au sana adhabu yake ni ndogo;
na ilhali ni jambo kubwa kweli la kuadhibiwa adhabu kali na Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
16. Yanayo faa ni kuwa baada ya kusikia maneno haya ya uwongo ni
kuambizana msiyazungumze, kwa sababu si laiki yenu, na mustaajabie kuzuliwa
uwongo muovu wa namna hii wa khatari.
Rudi kwenye Sura
17. Na hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni msirudie tena kufanya
maasi namna hii kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini wa kweli. Kwani sifa za
Imani zinapingana na mwendo huu.
Rudi kwenye Sura
18. Na Mwenyezi Mungu anakuteremshieni Aya zenye kuonyesha hukumu
kwa uwazi dhaahiri. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa Ujuzi, hapana asicho
kijua katika vitendo vyenu. Naye ni Mwenye hikima kwa kila anacho kitungia
sharia na kukiumba. Kwani kila sharia zake na uumbaji wake ni kwa
mujibu wa hikima.
Rudi kwenye Sura
19. Hakika hao wanao penda kutangaza machafu, wakayatangaza
baina ya Waumini watapata adhabu yenye kutia uchungu duniani kwa mateso
yaliyo kwisha pasishwa, na Akhera watatiwa Motoni ikiwa hawato tubu. Na
Mwenyezi Mungu anazijua vyema hali zenu zote, za dhaahiri na zilizo fichikana.
Na nyinyi hamjui anayo yajua Yeye.
Rudi kwenye Sura
20. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake
kwenu, na kuwa Yeye ni Mwingi wa upole, Mkunjufu wa rehema, asingeli kubainishieni
hukumu, na angeli kuleteeni mateso kwa haraka hapa duniani kwa maasi yenu.
Rudi kwenye Sura
21. Enyi mlio amini! Hifadhini nafsi zenu kwa Imani. Wala msimfuate
Shetani anaye kuvutieni kwenda tangaza uchafu na maasi baina yenu. Na mwenye
kumfuata Shetani basi huyo amekwisha a'si, kwani Shetani anaamrisha madhambi
makubwa makubwa na maasi mabaya. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu
juu yenu na rehema yake kwenu kwa kubainisha hukumu na kukubali toba ya
wenye kuasi asinget'ahirika hata mmoja wenu na uchafu wa maasi. Lakini
Mwenyezi Mungu anamsafisha mwenye kumuelekea Yeye kwa kumwezesha kuwa mbali
na maasi, au kwa kumsamehe kwa kutubu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia
kila kauli, Mwenye kujua kila kitu, na atakulipeni kwayo.
Rudi kwenye Sura
22. Wala wasiape wema wenu wenye nafasi kuwa watazuia kuwafanyia
hisani jamaa zao na masikini na walio hama makwao katika Njia ya Mwenyezi
Mungu na wengineo kwa sababu za kibinafsi, kama vile kuwa wamewatendea
uovu fulani. Lakini inatakikana wawasamehe na wayaachilie mbali makosa
yao. Na ikiwa mnapenda Mwenyezi Mungu akusameheni maovu yenu basi wafanyieni
wanao kufanyieni mabaya mfano wa anavyo kufanyieni nyinyi Mola wenu Mlezi.
Na fuateni mwendo wake kwani Yeye ni Mkunjufu wa kusamehe na kurehemu.
Aya hii imeteremka pale Abu Bakar r.a. alipo apa kumkatia
msaada jamaa yake Mist'ah bin Uthaathah hapo alipo ingia Mist'ah katika
uzushi alio zuliwa bibi Aisha r.a.
Rudi kwenye Sura
23. Hakika hao wanao wasingizia wanawake wema walio safi, ambao hawadhaniwi
hayo, bali wao kwa kumshughulikia Mwenyezi Mungu hata wameghafilika na
hayo wanayo singiziwa, Mwenyezi Mungu atawatenga mbali na rehema yake katika
dunia na Akhera, na watapata adhabu kubwa ikiwa hawatotubu.
Rudi kwenye Sura
24. Adhabu hiyo itakuwa Siku ya Kiyama ambapo itakuwa hapana njia
ya kuikataa. Bali waliyo yatenda yatathibiti juu yao, kwa kuwa zitawashuhudia
ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao, kwa madhambi yote waliyo yatenda.
Na hayo ni kwa kudhihiri athari ya vitendo vyao juu ya viungo hivyo, au
kwa kutamkishwa na Mwenyezi Mungu ambaye anatamkisha kila kitu.
Rudi kwenye Sura
25. Siku hiyo Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu iliyo kwisha hukumiwa
wapewe kwa ukamilifu wake bila ya upungufu. Na hapo wataujua kwa ujuzi
wa yakini Ungu wa Mwenyezi Mungu na hukumu za Sharia yake, na ukweli wa
ahadi yake na kitisho chake. Kwani yote hayo yatakuwa wazi hayana kificho.
Rudi kwenye Sura
26. Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake
waovu. Na kadhaalika wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema
ni wa wanawake wema. Basi yamkini vipi kuwepo uwovu katika wema ulio hifadhiwa
nao ni mke wa mwema muaminifu Mtume Mtukufu s.a.w.? Na wema hawa wamehifadhika
na tuhuma wanazo wasingizia hao waovu. Na wao wana maghfira ya Mwenyezi
Mungu kwa vijidhambi vidogo vidogo ambavyo mwanaadamu hakosekani kuwa navyo.
Na watapata ukarimu mkubwa wa kupata neema za Peponi.
Rudi kwenye Sura
27. Enyi mlio amini! Msiingie katika nyumba zisio kuwa zenu
ila baada ya kutaka idhini kwa wakaazi wake na mkaruhusiwa kuingia, na
baada ya kuwatolea salamu wakaazi wake - na salamu ni bora kwenu
kuliko kuingia tu bila ya kutoa salamu. Na Mwenyezi Mungu amekuwekeeni
sharia hii ili mpate kunasihika na muifuate.
Rudi kwenye Sura
28. Na ikiwa katika hizo nyumba hamkumkuta mtu wa kukupeni idhini
basi msiingie mpaka aje wa kukuruhusuni. Na ikiwa hakukuruhusuni na akakutakeni
mrudi nyuma, basi rudini; wala msishikilie kutaka ruhusa ya kuingia. Kwani
kurejea nyuma ni hishima zaidi na usafi zaidi kwa nafsi zenu. Na Mwenyezi
Mungu anazijua vyema hali zenu zote na atakulipeni, basi msende kinyume
na uwongozi wake.
Rudi kwenye Sura
29. Na mkitaka kuingia nyumba za umma zisio kaliwa na watu makhsusi
na ndani yake zipo haja zenu, kama vile maduka, mahoteli, nyumba za ibada,
hapana ubaya kuingia bila ya kutaka ruhusa. Na Mwenyezi Mungu anajua kwa
ujuzi wa timamu kabisa vitendo vyenu vyote vya dhaahiri na vilivyo fichikana.
Basi tahadharini na kwenda kinyume naye.
Rudi kwenye Sura
30. Ewe Nabii! Waambie Waumini katika yanayo pelekea zina na kutilisha
shaka, wasitazame yanayo harimishwa kutazama, nayo ni tupu za wanawake
na sehemu za uzuri wao, na wanaume wahifadhi tupu zao kwa kuzisitiri na
kuto zitumilia kwa njia isiyo ruhusiwa na Sharia. Adabu hiyo ndio ina hishima
zaidi na safi zaidi kwao wasiingie katika maasi na tuhuma. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kujua baraabara yote wayatendayo, na atakuja walipa kwayo.
Rudi kwenye Sura
31. Vile vile ewe Nabii, waambie wanawake Waumini, wanaamrishwa waache
kutazama yaliyo harimishwa, na wazihifadhi tupu zao kwa kuzisitiri na kutoingiliwa
ila kwa njia ya Kisharia. Na wasiwaonyeshe wanaume ya kuwavutia katika
uzuri wa umbo lao na mapambo, kama kifua, mabega, vidani, isipo kuwa yale
tangu hapo yamedhihiri, kama uso na mikono. Na ewe Nabii! Watake hao wanawake
wajisitiri mwahali zilipo funuka nguo, kama shingo na kifua. Na hayo kwa
kuteremshia vitambaa vya kichwani. Na wasiachilie kuonekana uzuri wao ila
kwa waume zao, na jamaa ambao ni haramu kuoana nao milele, kama baba zao,
au baba za waume wao, au watoto wao, au watoto wa waume zao kwa wake wengine,
au kaka zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao. Na mfano wa
hawa ni wanawake wenzao, sawa sawa wakiwa waungwana au wajakazi, na wanaume
wanao ishi nao na hawana tena haja ya wanawake kwa ukongwe. Na kadhaalika
watoto wadogo ambao hawajafikilia miaka ya kutamani. Na pia watake wanawake
wasifanye vituko vya kutaka kuwavutia wanaume kama kugonga miguu chini
ili isikilizane milio ya mitali na kugesi iliyo fichikana ndani ya nguo.
Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, kwa mlivyo iacha amri
ya Mwenyezi Mungu. Na shikamaneni na adabu za Dini mpate kuongokewa katika
dunia na Akhera yenu.
Rudi kwenye Sura
32. Na saidieni katika kujitenga na zina na yanayo pelekea
zina, kwa kuwaoza ambao bado hawajaoana miongoni mwa wanaume wenu na wanawake
wenu, na walio kuwa wanafaa kwa hayo katika watumwa wenu. Na wala umasikini
usiwe sababu ya kuzuilia kuoa. Kwani Mwenyezi Mungu atasahilisha njia za
maisha mazuri kwa mwenye kutaka kuishi maisha safi. Na fadhila za Mwenyezi
Mungu ni kunjufu, na Yeye anajua kabisa niya za watu, na kila lipitalo
katika ulimwengu.
Rudi kwenye Sura
33. Na ambao hawakupata uwezo wa fedha za kuolea basi wafuate mojapo
wa njia nyengine kama saumu na riyadha (1) na kazi za kutumia akili . Kwa
hayo hujikurupusha mpaka Mwenyezi Mungu akawafungulia kwa fadhila zake
zitakazo wawezesha kuoa. Na watumwa ambao wanataka kuandikiana nanyi ili
wapate uhuru wao ni waajibu juu yenu kuwakubalia walitakalo, mkijua kuwa
watatimiza kutekeleza na wanaweza. Na juu yenu kuwasaidia waweze kutimiza
walio andikiana nanyi, na hayo ama ni kwa kuwapunguzia shuruti mlizo andikiana
nao, au kwa kuwapa mali katika mali aliyo kuneemesheni Mwenyezi Mungu,
mkawapa katika Zaka au Sadaka. Na ni haramu juu yenu kuwafanya vijakazi
vyenu njia ya pato la duniani rakhisi kwa kuwafanya makahaba, na mkawalazimisha
kwa hayo. Na vipi mnakwenda kumlazimisha uchafu anaye taka kuwa safi? Na
mwenye kuwalazimisha, basi Mwenyezi Mungu humsamehe mwenye kulazimisha
pindi akitubu kwa dhambi zake za kulazimisha. Kwani hakika Mwenyezi Mungu
ni Mkunjufu wa maghfira na rehema.
(1)Haya yanaelezwa na kauli ya Mtume s.a.w.: "Enyi vijana! mwenye
kuweza kuwoa na aoe kwani hivyo linalindwa jicho, unahifadhiwa utupu. Asiye
weza na afunge, kwani hivyo ni kinga yake."
Rudi kwenye Sura
34. Na Sisi tumekuteremshieni katika Sura hii na nyenginezo Aya zilizo
wazi zenye kubainisha hukumu. Na tumekuteremshieni mifano ya hali mbali
mbali za walio tangulia, na uwongozi, na mawaidha ambayo kwayo watapata
faida wenye kumkhofu Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
35. Mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha Nuru ya katika mbingu na ardhi.
Yeye ndiye Mwenye kunawirisha vyote hivyo kwa nuru yote tunayo iona na
tukenda ndani yake, na ya maana, kama Nuru ya Haki na uadilifu, na ilimu,
na fadhila, na uwongofu, na Imani, na kwa ushahidi na athari kama alivyo
waahidi viumbe vyake, na kwa vyote vinavyo onyesha kuwepo kwa Mwenyezi
Mungu, na vikalingania Imani kumuamini Yeye Subhanahu. Na mfano wa Nuru
yake Tukufu na dalili zake zilizo zagaa kwa uwazi ni kama mfano wa Nuru
ya taa yenye kung'aa kwa ukali kabisa, iliyo wekwa kwenye shubaka la ukutani
ili kuukusanya mwangaza wake na kuzidi kuupa nguvu. Na taa hiyo imevikwa
tungi la kigae safi linameremeta kama inavyo meremeta nyota. Na taa ile
inawaka kwa mafuta ya mti wenye baraka nyingi, ulio pandwa kwenye
udongo mzuri na pahali pazuri. Mti huu ni mzaituni unao mea pahala pa kati
na kati. Basi huo si wa mashariki ukakosa joto la jua wakati wa alasiri,
wala si wa magharibi ukakosa joto la jua wakati wa asubuhi. Bali huo uko
juu ya kilele cha mlima, au katika uwazi wa ardhi unao patisha jua mchana
kutwa. Mafuta ya mti huu yanakaribia kutoa mwanga kwa ubora wa usafi wake
hata ikiwa hayajaguswa na moto wa taa. Mambo haya yote yanazidisha mwangaza
wa hiyo taa juu ya mwangaza wake, na Nuru juu ya Nuru.
Na namna hii ndio zinakuwa dalili zilizo enea katika ulimwengu, za
kuonekana na kupimika kwa akili; ni Ishara zilizo wazi hazitaki kutiliwa
shaka yoyote kwa kuwepo Mwenyezi Mungu, na kuwajibikia Imani kumuamini
Yeye, na Risala za Mitume aliyo waleta. Na Mwenyezi Mungu humwezesha kufikia
Imani amtakaye kwa njia ya dalili hizi ikiwa huyo mtu atajaribu kunafiika
na nuru ya akili yake. Na Mwenyezi Mungu ameleta mifano ya kuweza kuhisiwa
na kuonekana ili iwe wepesi kuelewa mambo ya kiakili. Na Yeye Subhanahu
ni Mkunjufu wa ujuzi, anawajua wenye kuangalia Ishara zake na wenye kuzipuuza
na wakapanda kiburi. Naye atawalipa kwa hayo.
Rudi kwenye Sura
36. Hakika wapo watu wanao mtakasa Mwenyezi Mungu na wanamuabudu
misikitini ambayo Mwenyezi Mungu ameamrisha ijengwe na iamirishwe kwa kudhukuriwa
Mwenyezi Mungu, nao wameshughulikia hayo asubuhi na jioni.
Rudi kwenye Sura
37. Dunia na yaliomo duniani ya kuuza na kununua hayawashughulishi
wakaacha kumdhukuru Mwenyezi Mungu na kumzingatia. Wao wanashika Sala,
na wanatoa Zaka, na huku wakiikhofu Siku ya Kiyama ambapo nyoyo zitakuwa
hazina utulivu kwa sababu ya wasiwasi na hamu, na kungojea matokeo, na
macho yatadahadari kwa mhangaiko na kushtuka kwa vituko vigeni wanavyo
viona, na wingi wa vitisho.
Rudi kwenye Sura
38. Na malipo ya vitendo vyao ni kulipwa sawa sawa kwa ubora wa malipo
kwa vitendo vyao vyema, na watapata fadhila kwa kupewa zaidi kuliko wanavyo
stahiki. Kwani Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa fadhila, humpa amtakaye katika
waja wake wema kipao kikubwa, asichoweza mtu kukihisabu wala wenye kuhisabu
hawawezi kukisia.
Rudi kwenye Sura
39. Na hao walio pinga na wakakanya wanadhani wenyewe kuwa wamefanya
vizuri, na kwamba vitendo vyao vizuri vitawaletea faida Siku ya Kiyama.
Lakini hao wamekosea katika dhana yao hiyo. Kwani mfano wa vitendo vyao
katika upotovu wake na kukosa maana ni kama mmetuko unao tokea unapo angukia
mwako wa jua wakati wa adhuhuri juu ya ardhi tambarare jangwani. Mwenye
kiu hudhania kuwa ni maji. Hata akiyafikia asikute chochote chenye manufaa
kama alivyo dhania. Hali kadhaalika vitendo vya makafiri siku ya malipo
vitakuwa vumbi lilio tawanyika. Na kafiri ataikuta adhabu ya Mwenyezi Mungu
inamngojea kwa utimilivu wake bila ya nuksani. Hakika hisabu ya Mwenyezi
Mungu hapana shaka inakuja. Na Yeye, Aliye takasika, ni Mwepesi katika
kuhisabu kwake, hachelewi wala hakosei.
Rudi kwenye Sura
40. Na huu mfano mwengine wa vitendo vya makafiri. Mfano wake ni
mfano wa giza la bahari kubwa iliyo tanda yenye kina kirefu. Mawimbi yake
yanapigana na kusukumana wenyewe kwa wenyewe. Nayo yamefunikwa na
mawingu mazito meusi hayapitishi mwangaza. Katika giza hili lililo rundikana
msafiri wa baharini hawezi kuuona mkono wake hata akiukurubisha machoni.
Basi anabaki ameduwaa amebabaika hajijui. Na vipi ataona kitu atokane
na butaa hili bila ya kupata Nuru ya kumwongoa katika mwendo wake, na kumwokoa
na kugongana na kuhiliki. Na basi kama hali hiyo hiyo makafiri hawapati
faida katika vitendo vyao, wala hawatoki katika upofu wao na upotovu wao,
wala hawajiokoi nafsi zao, ila kwa Nuru ya Imani. Kwani hana Nuru ya kumwongoa
kwenye Njia Iliyo Nyooka. Basi atakuwa katika walio teketea.
"Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani.
Mwenye kiu huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta
Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu
ni Mwepesi wa kuhisabu." Sarabi si chochote ila mandhari ya mwangaza yanayo
sabibishwa na marejeo (reflection) ya miale inayo toka kwenye vitu vyenye
kutoa mwanga. Na hiyo hurejeshwa tena kutokana na ardhi pana tupu, yaani
uwanda, na kupanda kidogo kidogo mkabala na uso wa ardhi, na joto linapo
panda wakati wa mchana, basi miale hiyo inayo rejea ikifika kwa jicho la
mwenye kuangalia huona vile vitu vimegeuka juu chini kama kwamba kwenye
kiyoo kikubwa kilicho tanda. Na kadhaalika mbingu safi ya rangi ya kibuluu
huonekana kama kwamba ni ziwa la maji juu ya uso wa ardhi. Na vile vitu
vingine kama miti miti na mitende iliyo onekana juu chini inazidi kuonyesha
kama kwamba ni vivuli kwenye maji. Na hii Sarabi huzidi kudhihiri kwa uwazi
kabisa inapo kuwa khitilafu ni kubwa baina ya joto la uso wa ardhi na angani
katika hewa. Na hayo huonekana zaidi majangwani na nyandani na kwenye barabara
za jangwani za lami zilio nyooka. Kwa maelezo hayo inaonekana kuwa Sarabi
ni kiini macho tu.
Maoni ya wataalamu juu ya Aya 40:
" Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu
ya mawimbi, na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono
wake anakaribia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru
hawi na nuru." Aya hii tukufu imekusanya yaliyo muhimu kabisa katika midharuba
ya baharini. Ni maarufu kuwa midharuba ya bahari kuu huwa na mawimbi yanayo
khitalifiana urefu wao na ukubwa wao au mnyanyuko wao, hata inaonekana
kama kwamba hayo mawimbi yanapandana moja juu ya mwenzie, na kwa hivyo
yakaziba mwangaza wa jua kwa vile hiyo midharuba inasabibisha kurundika
kwa mawingu mazito ambayo nayo huuziba mwangaza wa jua, na kwa hivyo husabibisha
giza mtu asiweze kuona kitu juu ya kuwa macho yake mazima. Na ilivyo kuwa
Mtume s.a.w. kazaliwa na kakulia jangwani, kuja maelezo kama haya ya undani
ya ki-ilimu kwa ulimi wake kuwa ni ufunuo ulio tokana na Mwenyezi
Mungu, ni ushahidi kuwa Qur'ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu, na kuwa ni
muujiza wa Mtume huyu mtukufu.
Rudi kwenye Sura
41. Ewe Nabii! Hujui kwa yakini kwamba kwa Mwenyezi Mungu hunyenyekea
kila kiliomo mbinguni na duniani? Na wanamnyenyekea ndege vile vile, nao
wamekunjua mbawa zao? Basi viumbe vyote hivi vinanyenyekea amri ya Mwenyezi
Mungu na mipango yake. Vinamtakasa na washirika na kila lisio na laiki
naye. Na kila kimojawapo kinajua kwa kujaaliwa na Mwenyezi Mungu yaliyo
kiwajibikia katika unyenyekevu na kutakasa na kutimiza wadhifa wa maisha.
Na Mwenyezi Mungu nyuma yao anajua kwa utimilivu wa kujua Sala ya kila
mwenye kusali, na kusabihi kwa mwenye kusabihi, na yote wayafanyayo waja.
Basi huwaje makafiri wakawa hawaamini?
Rudi kwenye Sura
42. Na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kumiliki mbingu na ardhi
na viliomo ndani yao, na ndiye Mwenye madaraka juu yao, na wote watarejea
kwake Siku ya Kiyama kwa ajili ya hisabu na malipo.
Rudi kwenye Sura
43. Ewe Nabii! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyavuta mawingu, kisha
huyakusanya na kuyarindika moja juu ya moja. Utaona mvua inatoka kwenye
mawingu. Na Mwenyezi Mungu huteremsha kutokana na mawingu yaliyo rindikana
yanayo shabihi milima (1) kwa ukubwa wake, vipande vya barafu kama changarawe,
vikawaangukia watu vikawaletea manufaa au madhara, kufuatana na kanuni
zake na matakwa yake, wala asiwateremshie wenginewe kwa mujibu apendavyo
Yeye Subhanahu, Mtendaji, Mwenye kukhitari. Mwangaza wa umeme unao tokea
kwa kugongana mawingu hukaribia kutia upofu kwa ukali wake. Na mambo kama
haya ya kuonekana ni dalili za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu ambao
unao wajibisha kuleta Imani ya kumuamini Yeye. (2)
(1) Hajui kushabihiana baina ya mawingu na milima ila mwenye kupanda
ndege (eropleni) inayo ruka juu ya mawingu, akayaona kutoka huko
juu kama ni milima na vilima. Ilivyo kuwa ndege hizo hazijawa bado zama
za Mtume s.a.w. basi hii inakuwa ni dalili kuwa maneno haya yanatokana
na Mwenyezi Mungu anaye jua ya juu na chini.
(2) "Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu,
kisha huyaambatisha, kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka
kati yake. Na huteremsha kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe,
akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko
wa umeme wake kupofua macho." Aya hii tukufu imeutangulia msafara wa sayansi.
Kwani hii yaeleza daraja za kuundika mawingu yanayo rindikana, na sifa
zake, na yaliyo juulikana hivi karibuni ki-sayansi ya kwamba mawingu ya
mvua huanzia kwa sura ya moja moja kisha yakajumuika yakawa kikundi, ndiyo
hayo mawingu yaliyo rindikana, yaani mawingu yanayo endelea kukua
kwa kuelekea utosini. Hayo hukua kimo chake hata kufikia urefu wa kilomita
15 au 20, na hapo huonekana kama ni milima mikubwa iliyo nyanyuka.
Na yajuulikanayo ki-sayansi ni kuwa mawingu yaliyo rindika yanapitia
daraja tatu, nazo:
Daraja ya kukusanyika na kukua.
Daraja ya kunyesha.
Na mwisho daraja ya kumalizikia.
Kama ilivyo kuwa mawingu hayo - nayo ni peke yao - yenye mvua ya
mawe na inabeba nguvu za umeme (electricity, Kahrabaa) , huweza kuwa
yakashika mfululizo wa umeme na radi, hata huweza ikawa ni miripuko karibu
40 kwa dakika moja, hata mtu anaye tazama akawa hawezi tena kuona kwa ukali
wa mwanga wake. Na haya ndiyo khasa yanayo wapata marubani wa meli na ndege
wakati wa midharuba ya radi.
Rudi kwenye Sura
44. Mwenyezi Mungu huzigeuza hali za usiku na mchana kwa urefu na
ufupi, na kwa kuanzia na kumalizikia, kwa mizunguko ya falaki. Hakika katika
hayo pana mazingatio kwa wenye akili zilio nzima zenye busara, na kwa njia
hiyo wakamuamini Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
45. Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na ndiye aliye anzisha
kila kitu kwa kupenda kwake. Na akaumba kila kilicho hai kutokana na asili
moja ya shirika, nayo ni maji. Na kwa hivyo kila kihai hakiachi kuwa na
maji. Kisha zinawakhitalifisha khitilafu nyengine kwa namna, na uwezo,
na sura, na kadhaalika. Katika wanyama wapo wanao tambaa kwa matumbo yao,
kama samaki, na nyoka. Na wapo wanao kwenda kwa miguu miwili kama wanaadamu
na ndege. Na wapo wanao kwenda kwa miguu mine kama mahayawani wengi wa
kufugwa na wa mwituni. Mwenyezi Mungu huumba apendavyo kwa njia mbali mbali,
kuonyesha uwezo wake na ujuzi wake. Kwani ni
Mwenye kutaka atakacho, na Mwenye kukhitari apendacho. Na Yeye ni Muweza
wa kila kitu.
"Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine
katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili,
na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu." Maji katika Aya hii tukufu ni maji
ya uzazi, yaani vinyama vinavyo toa manii. Na Aya hii si kama imetangulia
msafara wa sayansi katika kubainisha kuzalikana mtu kutokana na tone la
manii, kama ilivyo kuja katika kauli yake Aliye tukuka: "Hebu naajitazame
mtu, ameummbwa kwa kitu gani? Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa kuchupa."
(Sura Att'alaq 5,6), bali imetangulia pia katika kubainisha kwamba kila
kinyama kinacho kwenda kwenye ardhi kimeumbwa kwa njia ya kuzalikana na
vinyama vya manii, na vinga khitalifiana hivyo vinyama vya manii na sifa
zao katika kila namna mnamo hizo namna za vinyama. Katika maana za kisayansi
ambazo zaweza kuwa nazo hii Aya ni kuwa maji ni msingi wa kila kiumbe kilicho
hai. Kwa mfano mwili wa mtu umekusanya 70% ya uzito wake kuwa ni maji.
Yaani mtu mwenye uzito wa kilo 70, kiasi kilo 50 ni maji. Na kabla
ya kuteremka Qur'ani haya hayakuwa yakijuulikana kabisa ya kuwa mtu
ana sehemu hii kubwa ya mwili wake kuwa ni maji.
Na maji ndio chakula cha dharura kabisa kwa mwanaadamu. Kwani hali
mtu yamkini aishi siku 60 bila ya kula chakula chochote, hawezi kuishi
bila ya maji kwa zaidi kuliko siku 3 mpaka 10 mwisho wake.
Na maji ndio msingi wa kufanyika damu, na maji ya limfo, na ya katika
ubongo wa mifupa, vimwagavyo na mwili, kama mkojo, na jasho, na machozi,
na mate, na nyongo, na maziwa, na maji yanayo patikana katika viungo, na
ambayo ndiyo sababu ya ulaini wa mwili. Na yakikosekana 20% ya maji yake
basi mwanaadamu hukabiliwa na mauti.
Na maji huyayusha vyakula vikasahilika kufyonzeka. Na kadhaalika
huyayusha makombo yenye asili ya vilivyo hai au maadini katika mkojo na
jasho. Na kwa namna hii maji yana sehemu kubwa zaidi na muhimu kabisa katika
kuumbwa kwa mwili. Na kwa hivyo yamkini kusema kwamba kila kiumbe kilicho
hai kimeumbwa kutokana na maji.
Rudi kwenye Sura
46. Na hakika Sisi tumeteremsha kwa wahyi Aya zilizo wazi za kubainisha
hukumu na mawaidha, na zinazo piga mifano. Na Mwenyezi Mungu humwezesha
kwenye kheri ampendaye katika waja wake ambao wapo tayari kuziangalia na
kufaidika nazo.
Rudi kwenye Sura
47. Na wanaafiki husema kwa ndimi zao: Tumemuamini Mwenyezi Mungu
na Mtume, na tunazifuata amri zao. Na wanapo tiwa mtihanini kikundi kati
yao hukataa kushirikiana na Waislamu katika kazi ya kheri, kama Jihadi
na nyenginezo, baada ya kauli yao hii. Na watu hawa si Waumini wa kweli,
wala hawastahiki kutumiliwa jina la Waumini kwao.
Rudi kwenye Sura
48. Na katika hali zao ni kuwa wakitakiwa kuhukumiwa mbele ya Mtume
kwa jambo alilo literemsha Mwenyezi Mungu, unaafiki wa baadhi yao hudhihiri,
na wao hukataa kuhukumiwa wakijua kuwa haki ni ya wale makhasimu zao.
Rudi kwenye Sura
49. Ama wakijua kuwa haki iko upande wao basi humjia Mtume mbio mbio
ili awahukumu baina yao na makhasimu zao.
Rudi kwenye Sura
50. Na kwa nini wanasimama msimamo huu katika kushitakiana mbele
ya Mtume? Ni kwa sababu nafsi zao zimesibiwa na maradhi ya upofu, na kwa
hivyo haziridhiki na hukumu yako ya haki? Au ni kwa kuwa wao wanatilia
shaka uadilifu wa Muhammad s.a.w. katika kuhukumu? Si lolote katika hayo
kabisa. Lakini hao ni madhaalimu walio dhulumu nafsi zao na wengineo kwa
sababu ya ukafiri wao na unaafiki wao na kuiacha kwao haki.
Rudi kwenye Sura
51. Hakika kauli ya haki ifaayo kwa Waumini wa kweli wanapo itwa
wahukumiwe kwa mujibu wa yaliyo kuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume
wake, ni kuwa waseme kwa kukubali na kunyenyekea: Tumesikia wito wako,
ewe Muhammad! Na tumeridhia hukumu yako. Na hao ndio watao kuwa watu wa
kufanikiwa katika dunia yao na Akhera yao.
Rudi kwenye Sura
52. Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na kuridhia anayo yaamrisha Mtume
s.a.w. na wakaiogopa dhati ya Mwenyezi Mungu Tukufu, na wakaukumbuka Utukufu
wake, na wakaikhofu ghadhabu yake, hao ndio watakao pata radhi ya
Mwenyezi Mungu na mapenzi yake, na neema za Pepo, na ndio wenye kupata
kheri tupu.
Rudi kwenye Sura
53. Na wanaafiki wanaapa kwa ukomo wa nguvu za viapo vyao, kwamba
wewe, Muhammad, ukiwaamrisha watoke nawe kwenda vitani watakut'ii. Waambie:
Msiape! Kwani mambo yatakikanayo kwenu mnayajua, hapana hata mmoja wenu
asiye yajua. Wala yamini zenu za uwongo haziondoi ujuzi huo. Na hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua baraabara kila linalo tokana nanyi, na Yeye
atakulipeni kwayo.
Rudi kwenye Sura
54. Waambie: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume kwa ut'iifu
wa kweli wenye kuonyesha vitendo vyenu. Wanaafiki wakipuuza wasifuate,
basi juu ya Muhammad ni waajibu wa aliyo twishwa tu na Mwenyezi Mungu,
nayo ni amri ya kufikilisha Ujumbe, wala hakukalifishwa uwongofu wao. Na
nyinyi juu yenu ni hayo aliyo kutwikeni Mwenyezi Mungu nayo ni kufuata
na kut'ii. Na mtapata adhabu ikiwa mtaendelea na uasi. Na mkimt'ii Mtume
mtaongoka kwenye kheri. Na yeye haimpasi ila kufikisha kwa uwazi
- mkit'ii au mkiasi - na yeye kesha fikisha.
Rudi kwenye Sura
55. Mwenyezi Mungu amewaahidi katika nyinyi walio isadiki Haki na
wakaifuata, na wakatenda vitendo vyema, kwa ahadi ya kutia mkazo, ya kwamba
atawafanya makhalifa (wafwatizi, warithi) wa wale walio watangulia wawarithi
katika kuhukumu na utawala katika nchi, kama ilivyo kuwa hali ya walio
watangulia. Na atawasimamishia Uislamu kuwa ndio Dini yao aliyo wapendekezea.
Basi watakuwa na heba na madaraka. Na ataibadilisha hali yao ya khofu
iwe ya amani, wawe wananiabudu Mimi nao wametua. Hawanishirikishi Mimi
na chochote kile katika ibada. Na wenye kukhiari ukafiri baada ya ahadi
hii ya kweli, au wakartadi wakaacha Uislamu, basi hao ndio walio toka nje,
walio asi, wapinzani.
Rudi kwenye Sura
56. Na shikeni Sala kwa ukamilifu wa nguzo katika utulivu na unyenyekevu,
ili ipate kuwa inazuia uchafu na mambo mabaya. Na wapeni Zaka wanao stahiki.
Na mt'iini Mtume kwa yote anayo kuamrisheni, ili mpate kutaraji rehema
ya Mwenyezi Mungu na radhi yake.
Rudi kwenye Sura
57. Ewe Nabii! Usidhani kuwa makafiri wataweza kumkwepa Mwenyezi
Mungu asiwashike kwa madhambi yao, au watu wa Haki wasiwaone pahala popote
pale katika ardhi. Bali Yeye ni Muweza, na marejeo yao Siku ya Kiyama
ni Motoni. Na marejeo maovu kabisa ni marejeo yao.
Rudi kwenye Sura
58. Enyi mlio amini! Yakupaseni muamrishe watumishi wenu na vijana
wenu ambao bado hawajabalighi wasikuingilieni vyumbani mwenu ila baada
ya kutaka idhini katika nyakati tatu, nazo ni kabla ya Sala ya alfajiri
(1) , na pale mnapo punguza nguo zenu wakati wa kupumzika mchana, na baada
ya Sala ya Isha mnapo jitayarisha kulala. Kwani nyakati hizi mtu hubadilisha
mavazi ya kulalia badala ya mavazi ya kutokea, na huonekana sehemu za mwili
ambazo hazifai kuonekana. Wala hapana ubaya kwenu wala kwao kuingia bila
ya ruhusa nyakati nyenginezo, kwa sababu ni jamba la ada watu wa nyumbani
kupitiana kwa maslaha yao. Na kwa uwazi wa namna hii Mwenyezi Mungu
anakubainishieni Aya za Qur'ani ili akuwekeeni wazi hukumu. Na Mwenyezi
Mungu Subhanahu ni Mkunjufu wa ujuzi, Mkubwa wa hikima, anajua
yanayo silihi kwa waja wake, na anawatungia Sharia zinazo wanasibu, na
kwa kadri ya haja yao.
(1)"Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamikiliki mikono
yenu ya kulia na walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla
ya Sala ya alfajiri, na wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada
ya Sala ya isha. Hizi ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya
kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi.
Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya zake, na Mwenyezi Mungu
ni Mjuzi Mwenye hikima." Aya hii tukufu ni moja katika Aya zinazo elekeza
nadhari ya watu wazingatie yaliyo laiki katika jamii za watu khasa ndani
ya ukoo. Nayo kuwa kuchanganyika kwa watumishi na watoto katika aila
yao huenda kukapindukia mipaka ya hishima za maingiano, wakawa wanawaingilia
wenginewe bila ya kutaka idhini katika nyakati maalumu zilizo tajwa katika
Aya. Na kwa kuwa nyakati hizo ni nyakati za faragha na uhuru wa binafsi,
na kuvua nguo nzito nzito, Aya hii imekusudia kuweka Sharia ya kutaka idhini
katika nyakati hizo kutokana na watumishi na vijana ili wasione ambayo
yanahisabiwa kuwa ni siri, ambayo ni kama utupu ambao wapasa kusitiriwa.
Na kwa hivyo wanaelekezwa watu wa ukoo wavae mavazi yanayo kuwa laiki
ya kukabiliana hata wao kwa wao, ili hishima yao ibaki imehifadhika, na
uhuru wao umedhaminika, na adabu zao zimechungika. Na Qur'ani ndio inaayo
faa khasa kutuongoza tufuate mwendo ulio bora na wa juu. (Ikiwa watoto
wa nyumbani haiwafalii kuwaingilia watu katika nyakati hizo za faragha
zilizo tajwa, seuze watu mbali!)
Rudi kwenye Sura
59. Na vijana vyenu wakifikilia umri wa kubalighi inawapasa watake
ruhusa ya kuingia kila nyumba, na kila wakati, kama ilivyo wapasa wenzao
wa kabla yao. Na kwa mfano wa uwazi kama huu Mwenyezi Mungu anakuwekeeni
wazi Aya zake alizo ziteremsha. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mkunjufu
wa ujuzi, Mkubwa wa hikima. Anajua linalo wasilihi waja wake, na anawaatungia
Sharia zinazo wanasibu, na kwa kadri ya haja yao.
Rudi kwenye Sura
60. Na wanawake wakongwe ambao hawatumai kuolewa, hawalaumiwi wakipunguza
baadhi ya nguo zao, kwa sharti wasiwe wanajishauwa kwa kuonyesha uzuri
wa mwili wao ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha usitiriwe. Lakini kujihishimu
kwa kujisitiri kwa ukamilifu ni bora kwao kuliko kujifunua. Na Mwenyezi
Mungu anawasikia wayasemayo, na anayajua makusudio yao, na atawalipa kwa
hayo.
Rudi kwenye Sura
61. Wenye udhuru kama vile vipofu, viguru, wagonjwa hawana lawama,
bali hata nyinyi wazima hamna lawama kula katika nyumba za watoto
wenu, kwani hizo ni nyumba zenu. Wala kula katika nyumba za baba zenu,
na mama zenu, na ndugu zenu wanaume na ndugu zenu wanawake, au nyumba za
ami zenu, au mashangazi zenu, au wajomba zenu, au mama wadogo, dada wa
mama zenu, au nyumba ambazo mmewakilishwa kuzitazama, au nyumba za rafiki
zenu mnao changanyika nao, ikiwa hamna yaliyo harimishwa humo. Na hayo
ikijuulikana kuwa mwenye nyumba ameruhusu yeye au mkewe. Wala hapana ubaya
kula humo pamoja au mbali mbali. Na muingiapo katika nyumba toeni salamu
kwa waliomo ambao hao ni baadhi yenu kwa umoja wa Dini na ujamaa. Kwani
hao ni kama nyinyi. Na maamkio haya ni maamkio yaliyo wekewa Sharia, yenye
baraka na thawabu, na pia ndani yake nyoyo hupoa. Na kwa mfano kama huu
Mwenyezi Mungu anazifafanua Aya kwa ajili yenu mpate kuelewa waadhi na
hukumu ziliomo ndani yake, na mpate kuzifahamu na mzitende.
Rudi kwenye Sura
62. Hakika Waumini wenye kusadiki ni wale ambao wamemuamini Mwenyezi
Mungu na Mtume wake, na wala hawamwachi Mtume peke yake katika jambo muhimu
linalo hitajia wajumuike pamoja kwa ajili yake, kama mfano wa Jihadi. Ila
baada ya kumtaka ruhusa ya kuondoka na wakakubaliwa, hakika wanao kukadiri
wewe, ewe Nabii, kama unavyo stahiki, na wanatambua umuhimu wa huo mkusanyiko
hawaondoki ila baada ya wewe kukubali. Hao ndio wenye kusadiki katika Imani
yao kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Basi wakikutaka ruhusa hawa
kwenda kufanya baadhi ya maslaha yao mpe ruhusa umtakaye katika wao, pindi
ukimwona kuwa ana haja kweli ya kuondoka, na si dharura kwa mkutano kuwapo
yeye. Juu ya hivyo waombee maghfira kwa Mwenyezi Mungu kwa kuondoka kwao,
ambako kwa hakika hakuelekei kabisa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu
wa maghfira na rehema.
Rudi kwenye Sura
63. Fanyeni hima kuhishimu wito wa Mtume kukuiteni kukusanyika kwa
mambo muhimu. Na muitikieni huo wito wake, wala msifanye wito huo kama
mnavyo itana nyinyi kwa nyinyi, kuwa inafaa kupuuza na kuondoka mpendavyo.
Wala msiondoke ila baada ya kutaka ruhusa na mkakubaliwa, na tena iwe katika
mipaka ya ufinyo kabisa, na dharura za shida. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu
anawajua wanao ondoka bila ya idhini wakijificha ficha kati ya watu ili
ati Mtume asiwaone. Na watahadhari wanao kwenda kinyume na amri ya Mwenyezi
Mungu asije Subhanahu akawapatiliza kwa uasi wao wakapata mateso makali
duniani kama ukame na mitetemeko, au akawapa adhabu yenye wingi wa uchungu
aliyo waandalia Akhera, nayo ni ya Motoni.
Rudi kwenye Sura
64. Zindukaneni enyi watu! Mjue kuwa Mwenyezi Mungu peke yake ndiye
Mwenye kumiliki mbingu na ardhi, na viliomo ndani yao. Anayajua mlio nayo,
ukafiri wenu na Uislamu wenu, na uasi wenu, na ut'iifu wenu. Basi msiende
kinyume na amri yake. Na Yeye atawapa khabari watu, watapo rejea kwake
Siku ya Kiyama, kwa yote waliyo yatenda duniani, na atawalipa kwayo. Kwani
Yeye amekizunguka kila kitu kwa ujuzi wake.
Rudi kwenye Sura