1. Kumethibiti kufanikiwa kwa Waumini wanao muamini
Mwenyezi Mungu na waliyo kuja nayo Mitume; na wamefuzu kwa wayatakayo.
Rudi kwenye Sura
2. Hao ambao wameambatisha juu ya Imani yao vitendo vyema. Basi hao
katika Sala zao humuelekea Mwenyezi Mungu kwa nyoyo zenye kumkhofu na kumnyenyekea,
wanahisi unyenyekevu wa mwisho kwake Yeye .
Rudi kwenye Sura
3. Hao wanashughulikia mambo ya maana, wanapuuza vitendo na maneno
yasiyo na kheri ndani yake.
Rudi kwenye Sura
4. Nao wanashikilia kutoa Zaka kuwapa wanao stahiki. Kwa hivyo wanakusanya
ibada ya mwili na ibada ya mali, na baina ya kujisafisha nafsi na kuyasafisha
mali.
"Na ambao wanatoa Zaka,": Huu waajibu wa kutoa Zaka unapelekea kujenga
mashikamano ya umoja baina ya Waislamu, na kutia katika moyo wa kila mtu
kuwa ana jukumu kwa nduguye, anahisi kama anavyo hisi yeye, na anaungulika
kama anavyo ungulika yeye. Kwa hivyo ni waajibu wake kufanya awezavyo kumkinga
na balaa za kilimwengu, na machungu ya ukosefu. Kwa hivyo fakiri au masikini
hatomchukia tajiri, bali wote watahisi kama ni ukoo mmoja unao saidiana
na wenye kushikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu. Wala mwenye deni hakati
tamaa kuweza kulipa deni lake lilio bakia ikiwa hana cha kumalizia hilo
deni. Wala haianguki chini azma ya mujaahidi anaye pigana katika Njia ya
Mwenyezi Mungu kuinusuru Dini yake na kukomboa nchi yake kwa sababu ya
kukosa mali ya kutimizia makusudio yake. Wala msafiri au mgeni mhitaji
aliye mbali na mali yake hakosi wa kumkidhia haja zake kwa kumsaidia mpaka
afike kwake. Na juu ya haya Zaka ilikuwa ni njia moja katika njia
kubwa ulio chukua Uislamu kukombolea mateka na wafungwa na kuondoa utumwa.
Na Uislamu umeongeza kutimiza malengo yake ya kijamii kwa ulimwengu mzima
ikatupilia mbali chuki zinazo chusha za kidini, na ikatoa ruhusa Zaka wapewe
makafiri ikihitajia haja kuwakopesha. Hali kadhaalika hupewa wale wanao
itumikia Zaka, kama kuikusanya na kuigawa. Pia waandishi, na wasafiri,
na wanao khasiri kwa ajili ya kupatanisha wenye kugombana, na wanao wasaidia
Waislamu katika vita. Ama makusudio ya kiuchumi ya Zaka ni kuondoa
ufakiri popote ulipo, na kumsaidia kila mwenye haja kama ilivyo kwisha
tangulia.
Rudi kwenye Sura
5. Nao wanajihifadhi nafsi zao wasiingiane na wanawake.
"Na ambao wanazilinda tupu zao, isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo
wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. Lakini anaye
taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka." Aya hizi zinaambatana
na Aya nyengine ziliomo katika Suratun Nur zilio anzia: "Mzinifu mwanamke
na mzinifu mwanamume, mpigeni kila mmoja wao bakora mia." Hakika Aya hizi
tukufu zilizo tajwa zinaashiria maovu ya katika umma yanayo tokea kwa uzinzi.
Ama katika umma ni kuvurugika nasaba ya watoto isijuulikane, ama katika
siha ni sehemu mbili. KWANZA ni katika mwili, mfano wa kisonono, tego,
AIDS n.k. Kisonono huweza kuzalisha maradhi ya urithi kwa watoto hata huweza
kuleta upofu. Ama tego (Syphilis) huenea katika mishipa ya damu na ya hisiya
na huweza kuishia wazimu, na pia huenea mpaka kwa vizazi, na huenda mtoto
akafa tumboni au akatoka na kilema. Ama maradhi ya AIDS (Ukimwi) hayo ni
maafa yasiyo semeka, Mwenyezi Mungu atulinde nayo. PILI ni kuathirika
mishipa ya hisiya na akili, kwani uzinzi huweza kuathiri dhamiri ya mtu,
na kuadhibika nayo, na hata mwishoe huweza kuingia wazimu.
Rudi kwenye Sura
6. Isipo kuwa kwa njia ya ndoa ya kisharia, au wenye kumiliki masuria.
(1) Hao hawalaumiwi.
(1) Zamani utumwa ulikuwa ni jambo la kawaida, na ilikuwa mtu akiweza
kuchukua katika wajakazi wake akawafanya kuwa ni wakeze. Na Uislamu ulihalalisha
utumwa wa mateka katika vita vilivyo fuata sharia ikiwa maadui nao wanakamata
watumwa, basi ilikuwa ni halali kuwatendea wao hali kadhaalika. Ikiwa maadui
hawawafanyi mateka kuwa ni watumwa basi ilikuwa haiwafalii Waislamu kuwafanya
mateka kuwa ni watumwa.
Rudi kwenye Sura
7. Mwenye kutaka kuingiliana na mwanamke bila ya kupitia njia hizi
mbili, basi huyo amevuka mipaka ya sharia hadi ya kuvuka.
Rudi kwenye Sura
8. Na (hao Waumini) wawe ni wenye kuhifadhi kila walicho pewa kuwa
ni amana, ikiwa mali au neno au kitendo au chenginecho, na watimize kila
ahadi iliyo baina yao na Mwenyezi Mungu au na watu. Wasikhuni amana,
wala wasivunje ahadi.
Rudi kwenye Sura
9. Na wawe wenye kudumisha kutimiza Sala kwa nyakati zake, na kuzitekeleza
kwa nguzo zake na unyenyekevu wake, mpaka yapatikane makusudio yake. Nayo
ni kuachisha uchafu na maovu.
Rudi kwenye Sura
10. Hawa wenye kusifiwa hivi ndio watakao rithi kheri yote na wataipata
Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
11. Hawa ndio Mwenyezi Mungu atawafadhili kwa kuwapa Firdausi, ndio
pahala pa juu kabisa huko Peponi, wastarehe humo peke yao.
Rudi kwenye Sura
12. Yawapasa watu waangalie asli ya kuumbwa kwao; kwani hiyo ni dalili
za kuonyesha uwezo wetu zenye kupelekea kumuamini Mwenyezi Mungu, na kuamini
kufufuliwa. Kwani Sisi tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo.
Rudi kwenye Sura
13. Kisha tukaumba vizazi vyake, navyo ni kuwa tulimfanya mtu kwanza
tone ya mbegu ya uzazi - yaani maji yenye kila sifa ya uhai wa mwanzo.
Tukaiweka kwenye tumbo la uzazi, napo ni pahala pa utulivu palipo lindwa.
Rudi kwenye Sura
14. Kisha tukaifanya hii mbegu ya manii baada ya kuipandisha na yai
la mwanamke kuwa damu. Kisha damu tukaigeuza kuwa kipande cha nyama, kisha
tukafanya mafupa, na mafupa tukayavika nyama. Kisha tukatimiza uumbaji
wake mwishoe baada ya kuipulizia roho kuwa kiumbe kingine mbali ili kuanza
kumjenga. Shani ya Mwenyezi Mungu imetukuka kwa utukufu wake na uwezo wake.
Yeye hana mshabaha wake na yeyote katika kuumba kwake na kutengeza kwake
na kuanzisha kwake.
Rudi kwenye Sura
15. Kisha hakika nyinyi wanaadamu baada ya haya mambo yenu tuliyo
yataja ni wenye kuyaendea mauti bila ya shaka yoyote.
Rudi kwenye Sura
16. Na kisha nyinyi mtafufuliwa Siku ya Kiyama kwa ajili ya kuhisabiwa
na kulipwa jaza yenu.
Rudi kwenye Sura
17. Na hakika Sisi tumeziumba mbingu saba zilizo nyanyuka juu yenu.
Ndani yake vipo viumbe ambavyo hatukughafilika navyo. Tunavihifadhi na
tunaviendesha. Na Sisi kabisa hatughafiliki na viumbe vyetu vyote. Bali
tunavilinda visipotee na kuharibika, na tunavipangia mambo yao yote kwa
hikima.
"Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa wenye
kughafilika na viumbe." Hizo njia saba zilizo tajwa katika hiyo Aya
maana yake ni mbingu saba, na kwamba hizo si mbingu moja, na Mwenyezi Mungu
haghafiliki na mbingu hizo na viumbe viliomo ndani yake.
Rudi kwenye Sura
18. Na Sisi tumeteremsha kutoka mbinguni mvua kwa hikima na kipimo
katika umbo lake na kuteremka kwake. Na kusahilisha kwa ajili ya manufaa
tumeijaalia ikae juu ya uso wa ardhi na ndani yake chini. Na Sisi hakika
ni wenye kuweza kuiondoa wasipate kunafiika nayo. Lakini hatukufanya hayo
kwa kukuoneeni huruma. Basi muaminini Mwenye kuiumba na mumshukuru.
"Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza
katika ardhi. Na hakika Sisi tunaweza kuyaondoa." Aya hii tukufu inaashiria
maana ya kisayansi yenye kukhusu mzunguko wa maji katika ardhi. Yajuulikana
kuwa mvuke unao paa kutoka baharini hupelekea kufanyika mawingu ambayo
ndiyo huteremsha mvua. Na hivyo ndio chanzo cha maji matamu juu ya uso
wa ardhi, na ndio chombo cha msingi cha uhai wa ardhini. Kutokana na mvua
ndio huzuka mito inayo zua uhai katika sehemu kamwe zisio pitikiwa na mvua.
Kisha hiyo mito inamiminika baharini, na khulka inarejea tena kutoka
baharini kwenda angani na kwendea nchi kavu, na kisha kuingia baharini
mara ya pili. Isipo kuwa baadhi ya hayo maji ya mvua yanatulia na yanazama
kuhifadhika katika mahodhi ya chini ya ardhi, yakawekeka kwa muda mrefu.
Mfano wa hayo ni hayo maji yanayo patikana chini ya Jangwa la Magharibi
katika Libya, ambayo yamegunduliwa na watafiti hivi karibuni kutokana na
asli yake ya kale. Na huenda maji kama haya yalio hifadhika chini yakapatwa
na mabadiliko ya joto wanayo yaita wataalamu wa ilimu ya t'abaka za ardhi
(Geology) kuwa ni Mikondo ya Jiolojia, ikenda hiyo na maji mpaka pahala
pengine pakavu, ikaleta uhai baada ya kuwa ni maiti.
Na Aya hii inaonyesha hikima kubwa ya uenezaji wa maji kwa kipimo,
yaani kipimo cha haki na hikima, kwa ajili ya kuleta manufaa na kupinga
madhara. Na tena maana nyengine ya Aya tukufu ni kufahamisha apendavyo
Mwenye Kuumba, Aliye tukuka, navyo ni kujaalia yawepo maji ya kiasi maalumu
katika bahari za ulimwengu kutosha kuwepo mizani ya joto la kufaa katika
sayari hii, na ili isiwepo khitilafu kubwa mno baina ya joto la siku za
joto, na baridi ya siku za baridi, hata ikawa ni muhali kubakia uhai, kama
ilivyo katika sayari nyengine na katika mwezi. Kadhaalika maji ya ardhi
yanateremka kwa kiasi maalumu, hayazidi yakafunika ardhi yote, wala hayatindikii
sana hata yasipatikane hata kidogo kunyweshea baadhi ya nchi kavu.
Rudi kwenye Sura
19. Kwa haya maji tukakuumbieni mabustani ya mitende na mizabibu
yenye matunda mengi kwa ajili yenu, na katika hayo nyinyi mnakula.
Rudi kwenye Sura
20. Na tumekuumbieni mti wa zaituni unao ota katika jimbo la Mlima
wa Sinai. Katika matunda yake yanapatikana mafuta yanayo kufaeni. Na hizo
zaituni ni kitoweo cha chakula kwa wanao kula.
"Na mti utokao katika mlima wa Sinai, unatoa mafuta na kuwa kitoweo
kwa walao." Aya hii tukufu inathibitisha kuwa mti wa zaituni ni miongoni
mwa neema alizo mneemesha Mwenyezi Mungu binaadamu na ambazo baadhi yake
zimetajwa katika Aya zilizo tangulia. Na la kuongeza kwenye Aya hii ni
kuwa mzaituni ni miongoni mwa miti ya mbao inayo ishi muda mrefu sana,
zaidi ya mamia ya miaka. Kwa hivyo hauhitajii juhudi kubwa kwa mtu, bali
huendelea kuzaa wenyewe mfululizo. Kadhaalika una sifa ya kuwa daima kijani,
unapendeza kuutazama.
Uchunguzi wa kisayansi unaonyesha kwamba zaituni ni katika chakula
kizuri. Kwani ndani yake imo Protein nyingi. Vile vile zimo chumvi za Calcium,
chuma na Phospohorous. Na hivi ni muhimu na vya kutegemewa katika chakula
cha binaadamu. Na juu ya hivyo zaituni inayo Vitamin A na Vitamin B. Na
kutokana na tunda lake hutolewa mafuta ya zaituni, ambayo ni mafuta bora
ya mafuta mepesi. Mafuta haya hutumiwa katika chakula. Uchunguzi
wa kitabibu unaongeza kusema kuwa zipo faida nyengine katika mafuta ya
zaituni, nazo ni kuwa zinasaidia kwa jumla katika viungo vya usagaji wa
chakula, na khasa maini. Nayo yanashinda ubora mafuta yote yanayo tokana
na mimea na wanyama, kwa kuwa hayasabibishi maradhi ya mishipa ya damu
kama mafuta mengineyo, na kadhaalika yanalainisha ngozi. Na mafuta ya zaituni
yana matumizi mengine mengi katika sanaa (ufundi), kwani yanatumiwa katika
kufanya sabuni nzuri kabisa, na vitu vinginevyo katika ufanyaji wa vyakula
na vitu vya sanaa.
Rudi kwenye Sura
21. Na nyinyi mnapata kutokana na nyama hoa, nyama wa kufuga, nao
ni ngamia, ng'ombe, kondoo na mbuzi, mambo yanayo onyesha uwezo wetu na
fadhila zetu juu yenu kwa kukuneemesheni. Tunakunywesheni kutoka matumboni
mwao maziwa safi, matamu, mepesi kwa wenye kuyanywa. Na mbali ya maziwa
mnapata manufaa mengine kama nyama, na sufi, na manyoya. Na kutokana na
hao nyinyi mnaishi na mnaruzukiwa.
Rudi kwenye Sura
22. Na juu ya hawa wanyama wa kufuga na marikebu nyinyi mnapanda,
na mnapakia mizigo. Basi Sisi tumekuumbieni njia za usafirishaji na upakizi
nchi kavu na baharini. Na kwa hizo mnapata kuwasiliana nyinyi kwa nyinyi.
Rudi kwenye Sura
23. Na katika visa vya watu wa kale pana mazingatio kwa ajili yenu
mpate kuamini. Basi Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, naye akawaambia:
Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu pekee. Kwani nyinyi hamna anaye
stahiki kuabudiwa asiye kuwa Yeye. Hamwogopi adhabu yake, na kuondoka neema
zake mkimuasi?
Rudi kwenye Sura
24. Wakubwa wa kaumu yake walio kufuru wakiukanya wito wake na wakizuia
watu wasimfuate, walisema: Hapana khitilafu yoyote baina ya Nuhu na nyinyi.
Kwani yeye ni mtu kama nyinyi, lakini anataka kujipa ubora juu yenu kwa
huu wito wake. Na lau kuwa wapo Mitume wanao toka kwa Mwenyezi Mungu kama
anavyo dai yeye, basi ange waletea Malaika. Sisi hatukupata kusikia wito
huu katika taarikhi za baba zetu walio tangulia, wala kutumwa binaadamu
kuwa ni Mtume.
Rudi kwenye Sura
25. Huyu si chochote ila ni mtu mwenye wazimu. Na kwa hivyo wakasema:
Ngojeni, na mstahamilieni mpaka ukashifike wazimu wake, au kufike kuangamia
kwake.
Rudi kwenye Sura
26. Nuhu akamwomba Mola wake Mlezi baada ya kukata tamaa kuamini
kwao, akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ninusuru nao, na watie adabu kwa sababu
ya kuukadhibisha kwao wito wangu!
Rudi kwenye Sura
27. Tukamwambia kwa njia ya ufunuo (wahyi): Unda jahazi, nawe utalindwa
na uangalizi wetu. Shari yao haitokupata, nasi tutakuongoza katika kazi
yako. Na ikifikilia miadi ya kuwaadhibu, na ukaona tanuri inafoka maji
kwa amri yetu, basi waingize katika jahazi katika kila namna ya viumbe
vilivyo hai dume na jike. Na waingize ahali zako, isipo kuwa walio kwisha
thibitika adhabu yao kwa kukosa kwao Imani. Wala usiniombe kuwaokoa wale
walio dhulumu nafsi zao na wakawadhulumu na wengineo kwa ukafiri na uasi.
Kwani Mimi nimewahukumia kuwazamisha kwa sababu ya dhulma yao ya ushirikina
na uasi.
"Tukampa wahyi: Unda jahazi mbele ya macho yetu na uwongozi
wetu! Basi itapo fika amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize ndani
yake wa kila namna dume na jike, na ahali zako, isipo kuwa yule ambaye
katika wao juu yake imekwisha tangulia kauli. Wala usinitajie hao walio
dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa." Hakika haya maelezo ya
Tofani lilio tokea ijapo kuwa ni kwa mukhtasari tu katika hizi Aya tukufu,
kwa mwenye akili ya kuzingatia yana maana na mambo ya hakika mengi ya ki-ilimu
ambayo yanawapitia watu wengi. Na "tanuri" kwa lugha ni jiko la kuchomea
mikate, au pia ni uso wa ardhi na kila chenye kutimbuka maji, na kila penye
mkusanyiko wa maji.
Na si wepesi kusema kwa yakini taarikhi ya hiyo Tofani, kwani zilitokea
tofani nyingi zama za kale, kama katika Babilonia, Bara Hindi na Amerika.
Na zipo baadhi ya hadithi za kienyeji mbali mbali zinazo taja khabari
ya Tofani. Lakini haielekei kuwa hadithi hizo ndio zimekhusu hii
Tofani kubwa au Tofani ya Nuhu. Uchunguzi umethibitisha na pia zimeonekana
tofani nyingi ulimwenguni. Na tofani ya mwisho ya ulimwengu mzima ilikuwa
sababu yake ni kumalizika kipindi cha barafu cha mwisho, na kuyayuka barafu
nyingi ya kaskazini kabisa na kusini kabisa kwa dunia. Na sisi hatujui
kwa yakini lini mizani iligeuka na tanuri ikafurika - yaani uso wa ardhi
- kwa kupanda kwa ghafla kwa hivyo kuyayuka barafu, hata yakapanda juu
maji ya bahari na ya kamwagika maji.
Yafaa kutaja kuwa kuyayuka barafu ya zama za barafu za mwisho kulileta
hali ya hewa yenye mvua nyingi sana katika sehemu za dunia zilio mbali
na huko kaskazini na kusini kabisa kwa ulimwengu, kama vile katika Bahari
ya Kati (Mediterenian).
Vyo vyote vile ilivyo inakubalika kuwa hatuna ushahidi wa kuweza
kusema lini khasa zilikuwa hizo zama za Nuhu na kaumu yake. Yaliyo dhaahiri
kuwa yote hayo ni muujiza wa Mwenyezi Mungu. Na katika miujiza ni kuwa
Nuhu aliwanasihi watu wake na akawaonya na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu akafunua kuwa atawazamisha ikiwa hawakutengenea. Na tena
akamfunulia aunde marikebu. Kisha ikaja amri ya Mwenyezi Mungu, na mizani
ikapinduka, na tanuri ikafurika, ikamiminika mvua kuthibitisha aliyo yasema
Mwenyezi Mungu kumwambia Nuhu ya kwamba Mwenyezi Mungu anajua kuwa hatoamini
mtu katika kaumu yake baada ya wale walio kwisha amini.
Rudi kwenye Sura
28. Na ukisha panda na ukatua wewe na walio pamoja nawe katika jahazi
hiyo basi sema kwa kumshukuru Mola wako Mlezi: Alhamdulillahi! Sifa zote
njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliye tuokoa na shari ya watu makafiri
walio asi.
Rudi kwenye Sura
29. Na useme: Ewe Mola Mlezi! Nijaalie nishuke mashukio yenye baraka,
pahala pazuri pa kukaa wakati wa kuteremka nchi kavu. Na unitunukie amani
hapo. Kwani ni Wewe tu peke yako unaye weza kututeremsha pahala pa kheri
na amani na salama.
Rudi kwenye Sura
30. Hakika katika kisa hichi yapo mazingatio na mawaidha mengi. Na
hakika Sisi tunawajaribu (tunawapa mitihani) waja wetu kwa kheri na shari.
Na ndani ya nafsi zao wana utayarisho wa yote hayo.
Rudi kwenye Sura
31. Tena baada ya kaumu ya Nuhu tukaumba namna ya watu wengine, na
wao ni A'adi.
Rudi kwenye Sura
32. Tukawapelekea Huud. Naye ni katika wao. Tukawaambia kwa ulimi
wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu peke yake. Kwani nyinyi hamna Mungu anaye
stahiki kuabudiwa asiye kuwa Yeye. Ni Yeye peke yake anaye faa mumwogope.
Basi, jee mmeikhofu adhabu yake mkimuasi?
Rudi kwenye Sura
33. Na wakubwa katika kaumu yake walio kufuru na kukadhibisha
kukutana na Mwenyezi Mungu na mambo ya Akheria ya hisabu na malipo, na
tukawapa sehemu kubwa ya starehe na neema, wakasema kwa kukanusha wito
wake, na kuwazuia watu wasimfuate: Hapana khitilafu yo yote baina ya Huud
na nyinyi. Anakula chakula hicho hicho mnacho kila nyinyi. Na anakunywa
vinywaji hivyo hivyo mnavyo vinywa nyinyi. Mfano wa huyu hawezi kuwa Mtume,
kwa sababu hana sifa msizo kuwa nazo nyinyi.
Rudi kwenye Sura
34. Na wakawahadharisha kwa nguvu na mkazo, wakiwaambia: Mkimt'ii
mtu aliye kama nyinyi kwa utu wake, basi nyinyi hakika mtakuwa mmekhasiri
kwa kuwa hamtapata manufaa yo yote mkimfuata.
Rudi kwenye Sura
35. Wakawaambia pia katika kukanya kufufuliwa: Hivyo Huud anakuahidini
kuwa mtafufuliwa kutoka makaburini kwenu baada ya kwisha kufa kwenu, na
mkawa udongo na mafupa yasiyo kuwa na nyama na mishipa?
Rudi kwenye Sura
36. Hayo anayo kuahidini ni ya mbali mno, wala hayatakuwa abadan.
Rudi kwenye Sura
37. Hapana uhai ila mmoja tu. Nao ndio huu uhai wa duniani, ambao
tunauona una mauti na uhai unao tupitia. Kinacho zaliwa kinazaliwa, na
kilicho hai kinakufa. Wala hatutofufuliwa baada ya kwisha kufa kabisa.
Rudi kwenye Sura
38. Huyu si chochote ila ni mtu aliye mzulia Mwenyezi Mungu, na akadai
kwamba Mwenyezi Mungu kamtuma yeye. Na amesema uwongo katika hayo anayo
tuitia. Wala hatutomsadiki abadan.
Rudi kwenye Sura
39. Huud akasema baada ya kwisha kata tamaa kuamini kwao: Ewe Mola
wangu Mlezi! Ninusuru na uwatie adabu, kwa sababu ya kuukadhibisha wito
wangu.
Rudi kwenye Sura
40. Mwenyezi Mungu akamwambia Huud kuzidi kutilia nguvu ahadi yake:
Baada ya muda mchache watakuja juta, kwa waliyo yafanya, itapo wateremkia
adhabu.
Rudi kwenye Sura
41. Ukawachukua ukelele mkali ulio wahilikisha kama walivyo stahiki.
Tukawafanya kwa udhalili na udhaifu kama vijiti na majani ya miti yanayo
chukuliwa na maji ya mvua. Na huko ni kuteketea na kupotelea mbali na rehema
kwa madhaalimu kwa ukafiri wao na uasi wao.
Rudi kwenye Sura
42. Kisha baada yao tukawaumba kaumu nyengine wasio kuwa wao, kama
kaumu ya Saleh na ya Luut'i na ya Shuaib.
Rudi kwenye Sura
43. Kila umma una zama zake maalumu, hazitangulii wala hazikawii.
Rudi kwenye Sura
44. Kisha tukawatuma Mitume wetu wakifuatana, kila mmoja kwa kaumu
yake. Kila akija Mtume kwa kaumu yake waliukadhibisha wito wake. Nasi tukawateketeza
mfululizo, na tukazifanya khabari zao ni hadithi za watu kusimuliana na
kuzistaajabia. Basi hao kaumu wasio isadiki Haki wala hawaifuati wametengeka
mbali na rehema, na wamehiliki.
Rudi kwenye Sura
45. Kisha tukamtuma Musa na nduguye, Haaruni, tukawapa dalili za
kukata kuthibitisha ukweli wa ujumbe wao, na hoja wazi yenye kudhihirisha
kuwa wao ni kweli wametumwa kutoka kwangu.
Rudi kwenye Sura
46. Tuliwatuma wawili hao kwa Firauni na kaumu yake. Wakakataa kuamini
kwa ajili ya takaburi, na wao ni watu walio kuwa wakisifika kwa kiburi,
na majivuno, na ujeuri.
Rudi kwenye Sura
47. Wakasema kwa mastaajabu na kukanya: Je, tuuamini wito wa watu
wawili walio ni wanaadamu kama sisi, na tena watu wao hawa Wana wa Israili
ni wenye kutunyenyekea sisi na kutut'ii kama ni watumwa?
Rudi kwenye Sura
48. Basi waliwafanya waongo katika huo wito wao, na wakawa wenye
kuhiliki kwa kuzamishwa.
Rudi kwenye Sura
49. Na hakika tulimfunulia Musa Taurati apate kuwaongoa watu wake
kwa yaliyomo ndani yake ya uwongozi kwendea hukumu na njia za mafanikio.
Rudi kwenye Sura
50. Na tumemjaalia Isa bin Maryamu na mama yake, kwa vile kuchukua
mimba bila ya kuingiliwa na mtu, na kuzaliwa yeye Isa bila ya baba, kuwa
dalili ya kukata ya uwezo wetu wenye kushinda. Na tukamweka Maryamu
pahala pa kukaa penye ardhi iliyo nyanyuka na kukunjuka panapo faa kukaa,
na pana maji mengi. Na hayo ndiyo yanayo wezesha maisha ya starehe.
Rudi kwenye Sura
51. Tumewaambia Mitume wawafikishie watu wao: Kuleni vyakula vya
kila namna vya halali na vizuri, na stareheni na ishukuruni neema yangu
kwa vitendo vyema. Hakika Mimi ni Mjuzi wa myatendayo na nitakulipeni kwayo.
Rudi kwenye Sura
52. Na tukawaambia wawafikishie watu wao: Hakika hii Dini niliyo
kutumeni muifikishe ni Dini moja kwa mintarafu ya Imani na misingi ya sharia.
Na hakika nyinyi ni umma mmoja katika vizazi vyote. Miongoni mwao wapo
walio ongoka, na wapo walio potoka. Na Mimi ndiye Mola wenu Mlezi niliye
kuamrisheni muifuate, basi iogopeni adhabu yangu pindi mkiasi.
Rudi kwenye Sura
53. Lakini watu walilikata kata hili jambo la Dini yao. Wapo kati
yao walio ongoka, na wapo walio potoka ambao wakafuata matamanio yao, wakafarikiana
kwa sababu hiyo wakawa makundi mbali mbali yenye kufanyiana uadui. Kila
kikundi kinafurahi kwa walio nayo, kwa kudhania kuwa wao tu ndio walio
sibu.
Rudi kwenye Sura
54. Basi, ewe Muhammad, waachilie mbali makafiri na ujinga wao na
kughafilika kwao, maadamu wewe umekwisha wanasihi, mpaka Mwenyezi Mungu
awahukumie adhabu baadae.
Rudi kwenye Sura
55. Hivyo hawa maasi wanadhani ya kwamba pale Sisi tunapo wawacha
wakistarehe na mali na watoto tulio wapa
Rudi kwenye Sura
56. Ndio basi Sisi tumekuwa radhi nao, na kheri zikawamiminikia mbio
mbio na kwa wingi? Hao ni kama wanyama, hawatambui, kwa kuwa hawazitumii
akili zao. Mimi si radhi nao. Na hizi neema ni kuwapururia tu, kuwapa muda.
Rudi kwenye Sura
57. Hakika wale ambao humkhofu Mwenyezi Mungu na humwogopa, na zimejaa
ndani yao khofu ya Mwenyewe Subhanahu,
Rudi kwenye Sura
58. Na wale ambao wanaziamini Ishara za Mola wao Mlezi ziliomo ulimwenguni
na zinazo somwa katika Kitabu kilicho teremshwa,
Rudi kwenye Sura
59. Na wale ambao hawamshirikishi Mwenyezi Mungu na yeyote,
Rudi kwenye Sura
60. Na wale ambao wanatoa katika vile anavyo waruzuku Mwenyezi Mungu,
na wanafanya a'mali yao na hali wao wana khofu wasifanye taksiri, kwa sababu
bila ya shaka wao ni wenye kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa kufufuliwa na
watahisabiwa,
Rudi kwenye Sura
61. Hao wote hukimbilia na a'mali zao kuendea kupata kheri, na wao
ni wenye kuwatangulia wengineo katika kupata huko.
Rudi kwenye Sura
62. Na Sisi hatumlazimishi mtu yeyote ila kwa analo liweza kulifanya,
kwa sababu limo ndani ya makdara yake. Na kila a'mali katika a'mali za
waja zimesajiliwa kwetu katika kitabu, na tutawapa khabari zake kama zilivyo.
Na wao hawatadhulumiwa kwa kuongezewa adhabu wala kupunguziwa thawabu.
Rudi kwenye Sura
63. Lakini makafiri kwa sababu ya inadi yao na chuki zao ni wenye
kughafilika na kufanya kheri, na kujikalifu kufanya liwezekanalo, na kwamba
kuna hisabu ya kuchungua kila kitu. Na mbali na hayo bado wanavyo vitendo
vingine viovu wanavyo dumu navyo.
Rudi kwenye Sura
64. Na Sisi tunapo wapatiliza adhabu matajiri wenye kudeka katika
starehe zao hupiga makelele na wakayayatika kuomba msaada.
Rudi kwenye Sura
65. Basi tunawaambia: Msiyayatike, wala msiombe msaada hivi sasa.
Hamtatoka ndani ya adhabu yangu, wala kuyayatika kwenu hakufai kitu.
Rudi kwenye Sura
66. Hamna udhuru. Kwani Aya zangu zenye kuteremshwa kwa wahyi zilikuwa
mkisomewa, nanyi mkizipuuza kwa mapuuza yenye kugeuza hali zenu, na wala
hamkuzisadiki, wala hamkuzifuata kwa vitendo.
Rudi kwenye Sura
67. Na nyinyi katika mapuuza yenu mlikuwa mnatakabari na mnafanyia
maskhara, mkiutaja huu Wahyi kwa sifa mbaya mnapo kutana katika taanusi
zenu za usiku.
Rudi kwenye Sura
68. Je! Hawa wenye kupuuza wamekuwa wajinga hata hawakuizingatia
Qur'ani wakaijua kwamba hii hakika ni Haki? Au huu wito wa Muhammad kwao
umekuwa ni namna mbali kuliko walio kuja nayo Mitume wengine kwa kaumu
zilizo kwisha tangulia walio ambao baba zao waliwawahi?
Rudi kwenye Sura
69. Au hawamjui Mtume wao Muhammad aliye kulia kati yao katika
tabia zake tukufu ambazo hazijapata kuwa na uwongo, na wao hivi sasa wanaukataa
wito wake kwa dhulma na husda.
Rudi kwenye Sura
70. Au wanasema kuwa huyu ni mwendawazimu? Hasha! Huyu hakika
kawaletea Dini ya Haki, na wengi wao wanaichukia haki, kwani hiyo ni kinyume
na matamanio yao na mapenzi yao, basi kwa hivyo hawamuamini.
Rudi kwenye Sura
71. Ingeli kuwa Haki inafuata matamanio yao ufisadi ungeli enea ulimwenguni,
na hawa za nafsi zingeli pambana wenyewe kwa wenyewe. Lakini Sisi tumewapelekea
Qur'ani ambayo inawakumbusha haki ambayo inapasa wote wajumuike juu yake.
Na juu ya hivyo wao wanayapuuza hayo.
"Na lau kuwa Haki ingeli fuata matamanio yao, basi zingeli
haribika mbingu na ardhi na waliomo ndani. Bali tumewaletea ukumbusho wao,
nao wanajitenga mbali na ukumbusho wao." Hilo neno "Haki" ni tamko
lenye maana kadhaa. Huweza kuwa maana yake ni "Mwenyezi Mungu" Subhanahu
wa Taa'la , mfano wa kauli yake Mtukufu: "Ametukuka Mwenyezi Mungu wa Haki".
Pengine huwa maana yake ni "Qur'ani" , kwa mfano :"Hakika Sisi tumekutuma
kwa Haki". Na huenda kukusudiwa "Dini yote", yaani miongoni mwake
ni Qur'ani na Sunna (Hadithi) Sahihi, mfano wa kauli yake: "Na sema: Imekuja
Haki na uwongo umetoweka". Na iliyo dhaahiri katika tamko la Haki
hapa ni kuwa makusudio yake ni ile maana ya kwanza, yaani "Mwenyezi Mungu"
Aliye takasika na kutukuka. Na kwa hivyo maana iliyo kusudiwa na
Aya ni: Lau kuwa mwenendo wa Mwenyezi Mungu unafuatana na watakayo na wanayo
yapendekeza makafiri mpango usingeli bakia katika hali iliyo simamia
shani ya mpango wa mbingu na ardhi na wa viumbe viliomo ndani yake. Lakini
Mwenyezi Mungu Mwenye hikima kuu na uwezo wa kutenda na ujuzi wake ulio
enea kwa viumbe vyake na hikima yake ikadhamini kwa mpango madhubuti,
na Qur'ani kusema kwa uwazi ya kwamba mbingu zina viumbe, anatuelekeza
tufahamu:
* Kwanza kuwa Kuamini hayo kwa jumla ni yakini, tuache tafsili yake
mpaka apendavyo Mwenyezi Mungu Subhanahu kuidhihirisha kwa kuambatana
na kauli yake: "Tutawaonyesha Ishara zetu angani na katika nafsi zao."
* Pili: Anatuelekeza kwenye utafiti wa kisayansi kama tunaweza "kwani
kufikilia hakika hii inatutilia nguvu Imani yetu. Na Imani ndiyo lengo
muhimu katika kuelekea kwetu kwenye Ishara hizo."
Rudi kwenye Sura
72. Kwani, ewe Nabii! Unawataka ujira kwa huku kufikisha kwako
ujumbe? Hayakuwa hayo! Kwa kuwa ujira hakika ujira wa Mola wako Mlezi ni
bora zaidi kuliko walio nao wao; na Yeye ndiye Mbora wa kutoa.
Rudi kwenye Sura
73. Na hakika wewe, ewe Muhammad, hapana shaka yoyote unawaitia Dini
ambayo ndiyo Njia Iliyo Nyooka yenye kupelekea Uwokovu.
Rudi kwenye Sura
74. Na hakika hao wasio iamini Akhera na yalioko huko ya Pepo au
Moto wanaiacha Njia Iliyo Nyooka inayo mhifadhi mpitaji wakaishika njia
ya ubabaishi na misukosuko na ufisadi.
Rudi kwenye Sura
75. Na lau tungeli warehemu, na tukawaondolea madhara yalio wateremkia
katika miili yao, na ukame katika mali yao, na mfano wa hayo, basi hapana
shaka yoyote wangeli zidi ukafiri, na wakaendelea katika maasi na jeuri.
Rudi kwenye Sura
76. Na Sisi kwa hakika tuliwapa adhabu kama kwa kuwauwa au kuwaletea
njaa. Na wala hawakumnyenyekea Mola wao Mlezi, bali waliendelea na jeuri
zao na kiburi chao kiasi ya kuondoka tu hiyo adhabu.
Rudi kwenye Sura
77. Wanashikilia kupuuza kwao mpaka pale tunapo wapatiliza kwa adhabu
kali ya njaa au mauwaji hapa duniani huwa tena wanababaika na kukata
tamaa, hawaioni njia ya kuvuka.
Rudi kwenye Sura
78. Na yawaje mkamkufuri Mwenyezi Mungu na hali ni Yeye ndiye aliye
kuumbieni usikizi mkaisikia Haki, aliye kupena uwezo wa kuona mkauona ulimwengu
na viliomo ndani yake, na akakupeni akili mzingatie kwayo utukufu wake
mpate kuamini? Hakika nyinyi hamumshukuru Mwenye kuumba vyote hivyo
kwa Imani na ut'iifu ila kwa uchache tu, nao ni uchache mno!
Rudi kwenye Sura
79. Na Yeye ndiye aliye kuumbeni duniani, na kwake Yeye peke yake
ndio mtarejeshwa Siku ya Kiyama kwa ajili ya malipo.
Rudi kwenye Sura
80. Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na kwa amri yake na sharia
zake ndio usiku na mchana zinapitishana. Na kukhitalifiana kwazo kwa urefu
na ufupi, hamzingatii hiyo kuwa ni dalili ya uwezo wake na kupasa
kumuamini Yeye na kuamini kufufuliwa?
"Na Yeye ndiye anaye huisha na kufisha, na yake Yeye
mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je! Hamfahamu?" Aya zenye kutaja usiku
na mchana zimekuja mwahala mwingi katika Qur'ani tukufu, na haya yanaonyesha
kuwa Mwenyezi Mungu wa Haki, Aliye takasika na kutukuka, anawakumbusha
waja wake kwa Ishara hii ya uumbaji; na kwa kuwa yamo maana ya ndani inawapelekea
wenye kufikiri wazidi kuzingatia na kuchungua. Na kukhitalifiana usiku
na mchana kunatokana na pande mbili kubwa:
Kwanza: Kukhitalifiana kwa wakati, urefu na ufupi. Na Pili: Kukhitalifiana
kwa dhaahiri ya tabia na isiyo onekana.
* Kwanza - Khitilafu kwa nyakati:
Mchana ni kipindi cha wakati baina ya kudhihiri ncha ya jua na inapo
potea upeo wa macho, pale linapoonekana kwa jicho kama linagusa uso wa
ardhi. Na ilivyo kuwa kwa hakika pale pahali pake pa kuzama jua sipo hapo
upeo wa macho, bali tunaona tu hivyo kwa kuwa miale inayo tokana na jua
inapinda inapo pita katika matabaka ya anga mpaka inapo fikilia kwenye
jicho la mtazamaji, na yeye akaliona jua kama lipo huko upeo wa macho.
Lilio kweli ni kuwa kuzama huku kuko chini kuliko upeo wa macho kwa
kadri ya dakika 35 kwa kipimo cha mduara.
Na Usiku ni kipindi cha kutimiliza wakati wa mchana mpaka kitimilie
kipindi cha mzunguko wa ardhi juu ya nafsi yake kutoka magharibi kwendea
mashariki. Na baina ya Usiku na Mchana vipo vipindi viwili, navyo vya magharibi
na mapambazuko. Na kipindi cha mchana kinakhitalifiana kwa mujibu wa hali
ya uwazi wa pahala na musimu wa mwaka. Hali kadhaalika kipindi cha usiku
kinakhitalifiana hivyo hivyo kwa kufuatana haya. Na nyakati za Sala
na Saumu zinawekwa kufuatana na matulio ya jua huko upeo wa macho.
* Pili - Khitilafu katika yanayo dhihiri katika tabia:
Na madhaahiri haya ni ya namna nyingi, na yanazalikana kutokana
na michanganyiko ya miale ya jua, inayo onekana na isiyo onekana, na vitu
vilio beba nguvu za umeme pamoja na vifuniko vya anga na nyuso za bahari
na majangwa n.k. Kadhaalika yapo mambo ya kuonekana kama kupatwa kwa jua
na mwezi, na nyota zenye kufanya mikia, nyota za dasturi na nyota ziendazo
na mawingu meupe, na nyota zinazo anguka, na ambazo hufumbwa na ukali wa
anga la jua kuonekana mchana, ilhali usiku huonekana wazi. Na muhimu
kabisa katika yanayo onekana kuwa ni khitilafu baina ya usiku na mchana
ni huu mwangaza wa mchana. Na sababu yake ni kuwa miale inayo toka kwenye
jua inapo piga juu ya funiko la anga, ambalo kwa hakika ni sehemu ndogo
ndogo zenye chembe chembe ndogo mno za vumbi, hizo hurejesha mwangaza na
kuutawanya pande mbali mbali. Ikiwa hali ya anga ni safi, na vile vichembe
chembe vya vumbi ni vidogo sana, na jua liko upeo wa macho, basi rangi
inayo enea zaidi na inayo onekana kwa macho zaidi, inakuwa ya kibuluu.
Ama wakati wa kuchomoza jua au kuchwa basi mbingu huonekana na rangi
ya machungwa yenye kupiga wekundu, na mwangu wa kibuluu unatawanyika. Nz
kwa hivyo mbingu utosini huelekea kuwa kibuluu khafifu.
Na wakati wa kuchwa jua tunaona rangi ya kijani kiasi ya nukta moja
hivi au akali pembezoni mwake. Huu huitwa mmetuko wa kijani, na aghlabu
yake huonekana unapo kuwa baharini, au nyuma ya kilele cha mlima, au hata
kwenye kuta za majumba. Na asli ya kuonekana hivi ni kwa ajili ya kugeuka
na kutawanyika miale ya jua hata ikatoa rangi mbali mbali katika hizo kijani.
Mukhtasari wa haya ni kuwa miale ya jua ina rangi zinazo onekana
na zisizo onekana. Na zinakhitalifiana kwa urefu wa mawimbi yake na kufuata
kwake sifa hiyo. Kwa hivyo ndio tunaona kwa migongano hiyo mwangaza wa
mchana, mazigazi (sarabi), upinde wa mvua, na rangi za aina mbali mbali
zinazo zunguka jua, na mengineyo katika Ishara za mbinguni za ulimwengu
tuuonao. Na linapo potea jua jioni mbingu inaonekana kwa rangi mbali mbali
kwa sababu ya kuparaganyika mwangaza katika matabaka ya anga la juu. Na
kila jua likiteremka unapungua mwangaza wa jioni, na zinapungua zile rangi
zake za tabia, mpaka likifikilia daraja ya duara 18.5 mbingu inakuwa kiza.
Na wataalamu wa nyakati wameweka kuwa huu ndio wakati wa kuambiwa kuwa
usiku umekuwa giza na kwa hivyo ndio wakati wa kuadhinia Sala ya Isha.
Na wakati huo khasa ndio huanza mwangaza wa nyota kama sura ya mnara wa
sukari na tako lake liko upeo wa magharibi. Na hivyo huendelea katika masiku
safi ya siku za baridi mpaka kilele cha ile "cone" au "makhruut'" yaani
sura ya mnara wa sukari kifikie utosini. Na kati kati ya usiku hudhihiri
rangi za kuchomoza jua kidogo kidogo wakati wa mapambazuko kwanza kama
kilele cha ile "cone" au "makhruut'" . Kilele chake hicho huzidi kupanda
, na tako lake hutanuka kwenye upeo wa mashariki mpaka inapo dhihiri alfajiri,
yaani linapo kuwa jua liko chini ya upeo wa macho wa mashariki kwa kadri
ya daraja 18.5 za duara. Na hapo ndio wakati wa kuadhiniwa Sala ya
Alfajiri. Na rangi za mapambazuko huanza kudhihiri kwa taratibu kinyume
na zile za kuchwea jua magharibi. Na imedhihiri karibuni kuwa jua
lina kifuniko chembamba kimetanda angani takriban kimekaribia kufunika
anga lote la ardhi. Kifuniko hichi chembemba ndicho kinacho sabibisha kuleta
rangi mbali mbali za katika anga.
Mambo haya mbali mbali ambayo tumeyataja kama ni mifano isiyo na
ukomo imetuonyesha vipi mbingu inavyo kuwa pindi ikiwa hapana mawingu
wala hapana pepo za mchanga. Kwani hapo tena huwa ni kiza. Na ikiwa mawingu
yamebeba matone ya maji ya mvua basi hayo hupambana na miale ya jua, na
hufanyika kama huo upinde wa mvua katika hali maalumu.
Na ikiwa mawingu yenyewe ni ya namna fulani ambayo yanabeba maji
yaliyo ganda (crystals) "kristali" zenye pande sita, basi maji hayo huingiana
na miale ya jua na hiyo miale huvunjika ndani ya hayo maji (kama mwaangaza
upitavyo katika kigae cha thuraya, "prism") kisha mwangaza huo ukatoka
nje kwa rangi mbali mbali. Na katika hali fulani fulani ndio hutokea rangi
nzuri nzuri kulizunguka jua. Na wakati wa weusi wa usiku utaziona nyota
kama kwamba zipo karibu nasi na kwa hakika hizo ziko mbali kwa masafa makubwa
sana ya kukisiwa kwa miaka na miaka ya mwendo wa mwanga. Vile vile tunaona
katika anga hili nyota na sayari na nyota mkia na vimondo kama kwamba zipo
karibu, utadhani kuwa khitilafu ya masafa imeondoka kabisa. Na haya ndiyo
yanayo tupelekea tutambue maana iliyo fichikana ya kauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu: "Na tumeifanya mbingu kama dari iliyo hifadhiwa; nao wamezipuuza
Ishara zetu." Kama tulivyo kwisha eleza kuwa juu ya miale inayo tokana
na jua kuna miale inayo tokana na vitu vingine vya eneo la jua vyenye nishat'i
ya nguvu, na vyenye kubeba nguvu za umeme. Kadhaalika inatokana na hizo
miale iliyo juu ya zambarau Ultra Violet Rays. Vitu hivi na miale hii inapambana
na matabaka ya anga la juu, na huathirika kwa mvuto wa smaku kuizunguka
dunia. Kwa hivyo hulitibua anga la kaskazini na kusini, na huleta kiza
katika mbingu ya kaskaazini kama kwamba ni pazia kuzuia mianga yenye rangi
nzuri nzuri za kijani zenye kumili kwenye wekundu na kibuluu. Sura
hizi hubaki pengine muda wa saa kadhaa katika mbingu ya kaskazini, na zaidi
waweza kuziona masiku kadhaa wa kadhaa linapo kuwa jua linashitadi. Mapazia
haya si kama unayaona kaskazini tu, bali hata pia katika kati kati
ya dunia.
Na katika mbingu vipo vibebaji nguvu za umeme katika mawingu na
anga ambavyo huzalikana kutokana navyo radi na mimetuko katika anga la
juu. Mambo yote haya yanayo onekana ambayo tunayashuhudia yanatupelekea
tufahama maana ya ndani ya kauli yake Subhanahu wa Taa'la: "Hakika katika
kuumbwa kwa mbingu na ardhi na kukhitalifana usiku na mchana pana Ishara
kwa wenye akili."
Kutokana na yaliyo pita kwa mambo ya dhaahiri ya maumbile inabainikana
kwamba haya yanakuwa kwa sababu ambazo hayumkini mwanaadamu kuingilia
ndani yake. Na hakika ni Mwenyezi Mungu, Aliye tukuka shani yake, ndiye
mwenye kuleta hizo khitilafu za usiku na mchana, wala hawezi binaadamu
kabisa siku yoyote kuweza kugeuza usiku wala mchana. Na Yeye Mwenyezi Mungu
Aliye tukuka shani yake ndiye anaye zifuatanisha usiku na mchana kwa mizani
madhubuti na vipimo baraabara, na anaendesha siku zote mwaka ingia
mwaka toka.
Rudi kwenye Sura
81. Hawakuzingatia hayo, bali waliwafuata wakanushaji walio kwisha
tangulia, wakasema kama walivyo sema hao.
Rudi kwenye Sura
82. Katika kukanusha kwao kufufuliwa, walisema: Hivyo sisi tutafufuliwa
baada ya kwisha geuka mchanga na mifupa?
Rudi kwenye Sura
83. Sisi tuliahidiwa haya, na pia baba zetu waliahidiwa hayo hayo
hapo zamani. Haya si chochote ila ni ahadi za uwongo walizo buni watu wa
zamani.
Rudi kwenye Sura
84.. Ewe Muhammad! Waambie: Ni nani aliye imiliki ardhi na viliomo
ndani yake, tangu watu mpaka viumbe vyote? Kama nyinyi mna ujuzi nijibuni.
Rudi kwenye Sura
85. Watakiri kuwa ardhi ni ya Mwenyezi Mungu. Basi hapo tena waambie:
Hamkumbuki kuwa Mwenye kumiliki hayo ndiye anaye faa kuabudiwa peke yake?
Rudi kwenye Sura
86. Waambie tena: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu saba na Mola Mlezi
wa A'rshi Kuu? (Kiti Kikuu cha Enzi)
Rudi kwenye Sura
87. Watakiri kuwa huyo ni Mwenyezi Mungu. Basi waambie: Je! Hamwogopi
matokeo ya ushirikina wenu na ukafiri wenu na kumuasi kwenu Mwenye
uumbaji huu wote mkubwa?
Rudi kwenye Sura
88. Waambie vile vile: Nani mwenye ufalme wa kila kitu mkononi mwake,
na mwenye madaraka yasio na ukomo katika kila kitu, na ambaye ndiye kwa
uwezo wake analinda kila kitu, wala hayamkiniki yeyote kumlinda yeyote
na adhabu yake? Kama nyinyi mnaijua jawabu, basi nijibuni.
Rudi kwenye Sura
89. Watakiri kuwa hakika huyo ni Mwenyezi Mungu. Waambie:
Basi huwaje mkadanganyika kwa pumbao na kuchochewa na mashetani, na mkaacha
ut'iifu wa Mwenyezi Mungu?
Rudi kwenye Sura
90. Hakika Sisi tumewabainishia Haki kwa ndimi za Mitume, na
wao ni waongo katika kila jambo linalo khitalifu na Haki hii.
Rudi kwenye Sura
91. Mwenyezi Mungu hakumchukua yeyote kuwa ni mwanawe. Yeye ametakasikia
na hayo. Wala hana mshirika. Angeli kuwa na mshirika basi kila mmoja wao
angejipa madaraka ya pekee kwa alivyo viumba, na vikawa ndio milki yake,
na wangeli gombana wenyewe kwa wenyewe kama wanavyo onekana wafalme wanavyo
fanya. Na ulimwengu ungeli fisidika kwa mizozano hiyo. Basi Mwenyezi Mungu
ametakasika na hayo wayasemayo washirikina yanayo kwenda kinyume na Haki.
Rudi kwenye Sura
92. Na Yeye amevizunguka vitu vyote kwa kuvijua. Anajua tusiyo
yaona na tunayo yaona. Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mnasibisha
nayo makafiri kuwa ati ana washirika.
Rudi kwenye Sura
93. Ewe Nabii! Sema: Ukiwateremshia adhabu ulio waahidi hapa duniani
nami nipo pamoja nao,
Rudi kwenye Sura
94. Basi nakuomba usinifanye mwenye kuadhibiwa pamoja na makafiri
waasi.
Rudi kwenye Sura
95. Na Sisi tunaweza kwa utimilivu kukuonyesha adhabu tulio waahidi
ikiwateremkia. Basi wewe tuwa ujue kuwa tutashinda.
Rudi kwenye Sura
96. Wewe endelea na wito wako, na ukabili uovu wao kwa vitendo vilivyo
vizuri kama kusamehe au vyenginevyo. Na Sisi tunajua vyema wanakutaja vipi
wewe, na wanavyo usema kwa ubaya huo wito wako kwa uwovu na uzushi. Na
Sisi tutawalipa kwa hayo.
Rudi kwenye Sura
97. Nawe sema: Ewe Mola Mlezi! Najilinda kwako na wasiwasi wa mashetani
wasiniingilie katika nafsi yangu kwa vitendo visio kupendeza.
Rudi kwenye Sura
98. Na ewe Mola Mlezi! Najilinda kwako wasiwe nami katika kitendo
chochote ili kitendo hicho kiwe kimetakasika, safi, kwa
ajili ya ridhaa yako tukufu.
Rudi kwenye Sura
99. Wanaendelea kuwakanusha mpaka utapo fika wakati wa kufa mmoja
wao hujuta na akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Nirudishe duniani.
Rudi kwenye Sura
100. Ili nipate kufanya a'mali njema katika mali au wakati nilio
acha. Wala ombi lake halitokubaliwa. Kwani haya ni maneno anayasema bila
ya faida, hayakubaliwi. Na pindi akikubaliwa hatotenda kitu. Na juu ya
yote hatorudi kabisa! Kwani mauti ni kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani
mpaka Mwenyezi Mungu atapo wafufua.
Rudi kwenye Sura
101. Ukifika wakati wa kufufuliwa tutawafufua kutoka makaburini
kwao. Na hayo ni kwa mfano wa kupulizwa tarumbeta watafufuka nao wamefarikiana.
Hapana mtu utaomfaa ujamaa wake na fulani. (Ujamaa Kiswahili maana yake
makhusiano ya nasaba, sio usoshalisti.) Wala hapana mtu atae muomba mtu
kitu cha kumfaa. Kwani kila mmoja wao siku hiyo atakuwa kashughulika na
lake.
Rudi kwenye Sura
102. A'mali (Vitendo) ndio mizani ya kupimia. Mwenye Imani nzuri
na vitendo vyema atakuwa na uzito katika mizani ya Mwenyezi Mungu. Hao
ndio walio fuzu.
Rudi kwenye Sura
103. Na asiye kuwa na thawabu au vitendo vyenye uzito mbele ya Mwenyezi
Mungu, hao ndio walio zikhasiri nafsi zao kwa kuziuza kwa Shetani. Nao
wataadhibiwa Motoni, wadumu humo.
Rudi kwenye Sura
104. Moto utawababua nyuso zao, nazo zitakuwa zimekunjana kwa uwovu
wa mwisho wao.
Rudi kwenye Sura
105. Mwenyezi Mungu anawakemea na anawaambia: Aya zangu zilizo kuwa
zinateremshwa zilikuwa mkisomewa duniani, nanyi mkizikadhibisha.
Rudi kwenye Sura
106. Watasema nao wanakiri makosa yao : Ewe Mola wetu Mlezi!
Maasi yetu yalikuwa mengi, ndio yakatupatia mashaka, na tukawa wenye kupotea
tukaiacha njia ya sawa.
Rudi kwenye Sura
107. Na watasema: Mola wetu Mlezi! Tutoe Motoni na uturejeshe duniani.
Basi tukirudi tena kwenye ukafiri na uasi basi tutakuwa kweli ni twenye
kujidhulumu nafsi zetu.
Rudi kwenye Sura
108. Na Mwenyezi Mungu atawaambia kwa kuwadharau na kuwabeza: Kaeni
humo kwa madhila na unyonge, wala msiseme nami kabisa!
Rudi kwenye Sura
109. Mimi sikukudhulumuni, bali nyinyi mmejidhulumu wenyewe. Kwani
Waumini wema katika waja wangu walikuwa wakisema duniani: Ewe Mola wetu
Mlezi! Tumeamini. Basi tughufirie na uturehemu. Na Wewe ndiwe Mbora wa
wanao rehemu.
Rudi kwenye Sura
110. Na nyinyi daima mlikuwa mkiwafanyia maskhara, mpaka maskhara
yenu yakakusahaulisheni kunikumbuka Mimi na kuniabudu Mimi. Basi hamkuamini
wala hamkut'ii. Nanyi mlikuwa mkiwacheka kwa kejeli.
Rudi kwenye Sura
111. Hakika Mimi hii leo nimewalipa wao kwa mafanikio, kwa kuwa waliyavumilia
maskhara yenu na maudhi yenu.
Rudi kwenye Sura
112. Mwenyezi Mungu atawaambia makafiri: Mliishi miaka mingapi huko
duniani?
Rudi kwenye Sura
113. Watasema kwa kuyaona mafupi maisha yao kwa adhabu wanayo ikuta:
Tuliishi muda wa siku moja au baadhi ya siku hivi. Basi waulize wanao weza
kuhisabu, sisi tumeshughulishwa na hii adhabu.
Rudi kwenye Sura
114. Basi Mwenyezi Mungu atawaambia: Hamkuishi duniani ila muda mchache
tu. Na lau ingeli kuwa mnajua malipo ya ukafiri na uasi na kwamba starehe
ya duniani ni chache mngeli amini na mkat'ii.
Rudi kwenye Sura
115. Je! Mlidhani kuwa tulikuumbeni bila ya hikima ndio mkafanya
ufisadi katika ardhi, na mkadhani kuwa hamtafufuliwa mpate kulipwa?
Rudi kwenye Sura
116. Utukufu ni wa Mwenyezi Mungu peke yake. Na Yeye ndiye Mwenye
kumiliki ufalme wote. Hapana Mwenye kuabudiwa kwa Haki isipo kuwa Yeye.
Na Yeye ndiye Mwenye A'rshi Tukufu.
Rudi kwenye Sura
117. Na mwenye kumuabudu mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu
hana ushahidi wa kumfanya huyo astahiki kuabudiwa. Hakika Mwenyezi Mungu
atampa adhabu kwa ushirikina wake bila ya shaka yoyote. Hakika makafiri
hawaongokewi. Bali watao ongokewa ni Waumini.
Rudi kwenye Sura
118. Na sema, ewe Nabii, ukimlingania Mwenyezi Mungu na kumnyenyekea:
Ewe Mola wangu Mlezi! Nisamehe dhambi zangu, na nirehemu. Kwani Wewe ni
Mbora wa wanao rehemu, kwa sababu rehema yako imeenea na ipo karibu kwa
watendao mema.
Rudi kwenye Sura