1. Umewakaribia washirikina wakati wao wa
kuhisabiwa Siku ya Kiyama, nao hali wameghafilika na kitisho chake,
wanapuuza kuiamini.
Rudi kwenye Sura
2. Haiwajii Qur'ani kutokana
na Mola wao Mlezi pale inapoteremka kuwakumbusha
ya kuwanufaisha, ila wao huisikiliza na hali wao wameshughulika na mengine
yasiyo na faida nao, wakicheza kama wachezavyo watoto wadogo.
Rudi kwenye Sura
3. Nyoyo zao zimo katika pumbao, hazizingatii, wameshikilia kuficha
njama zao za kumpinga Nabii na Qur'ani, wakiambizana wenyewe kwa wenyewe:
Huyu Muhammad si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi. Na Mtume hawi ila
Malaika. Basi, je! Mnamsadiki Muhammad na mnahudhuria baraza za uchawi
na hali nyinyi mnaona kuwa hakika huo ni uchawi?
Rudi kwenye Sura
4. Mtume, kwa kuwa Mwenyezi Mungu kamjuulisha waliyo kuwa wakiyasema
kwa siri, aliwaambia: Mola wangu Mlezi anayajua yote yanayo semwa katika
mbingu na katika ardhi, na Yeye ndiye anaye sikia kila linalo sikiwa; na
anajua kila linalo tokea..
Rudi kwenye Sura
5. Bali wao wakasema: Hizi ni mchanganyiko wa ndoto alizo ziota (Muhammad);
bali kazua tu na akamsingizia Mwenyezi Mungu kwa uwongo. Kisha wakaacha
hayo na wakasema: Bali huyu ni mtunga mashairi anaziteka nafsi za wenye
kumsikiliza. Kama kweli, basi na atuletee muujiza khasa wa kuonyesha ukweli
wake, kama walivyo tumwa Manabii wa zamani wakitiwa nguvu kwa miujiza mbali
mbali.
Rudi kwenye Sura
6. Hizo kaumu tulizo ziangamiza baada ya kukadhibisha hiyo
miujiza hazikuamini. Basi, je! Watakuja amini hawa yatapo wajia hayo wayatakayo?
Rudi kwenye Sura
7. Ewe Nabii! Kabla yako wewe hatukuwatumia watu ila watu wa kibinaadamu
vile vile, ambao tuliwafunulia Dini waifikishe kwa watu. Basi, enyi mnao
kataa! Waulizeni wanazuoni wajuao ilimu za Vitabu vilivyo teremka, ikiwa
nyinyi hamyajui hayo.
Rudi kwenye Sura
8. Wala Sisi hatukuwajaalia Mitume kuwa na miili inayo khitalifiana
na miili ya wanaadamu wengine, wakawa wanaishi bila ya chakula, na wakabaki
siku zote, na wala hawakuwa wanaishi daima milele.
Rudi kwenye Sura
9. Kisha tukawatimizia na tukawahakikishia ahadi, na tukawaokoa wao
na pamoja nao tukawaokoa tulio taka kuwaokoa miongoni mwa Waumini. Na makafiri
walio vuka mipaka tuliwaangamiza kwa kukadhibisha kwao na kuukataa Ujumbe
wa Manabii wao.
Rudi kwenye Sura
10. Sisi hakika tumekuteremshieni Kitabu. Ndani yake yamo mawaidha
ya kuwakumbusheni ikiwa mtakisoma na mtayatenda yaliyomo ndani yake. Basi
huwaje mkakipuuza na mkakikataa? Je, inda na upumbavu umefika hadi ya kukufikisheni
hali hii mlio nayo, mkawa hamuelewi lipi lenye manufaa nanyi mkalikimbilia?
Rudi kwenye Sura
11. Na wengi katika watu wa miji tuliyo iteketeza kwa sababu ya ukafiri
wao na kuwakadhibisha Manabii, na baada yao tukasimamisha kaumu nyengine
zenye hali bora na mwisho mwema kuliko hao.
Rudi kwenye Sura
12. Na tulipo taka kuwateketeza, na wakahisi ukali wa adhabu yetu
na uwezo wetu wa kuwateremshia hayo yatakayo wapata, wakafanya haraka kukimbia,
kama wanyama hayawani, ati kutafuta kuokoka!
Rudi kwenye Sura
13. Enyi wapinzani! Msikimbie! Hapana kitu chochote kitacho kulindeni
na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Rudini kwenye zile zile neema na majumba mliyo
kuwa nayo, huenda watumishi wenu na wenzenu watakutakeni msaada na rai
kama ilivyo kuwa ada yenu. Wapi! Hamtoweza!
Rudi kwenye Sura
14. Kwa kuwa hao makafiri wamekwisha sikia wanavyo kejeliwa na wanavyo
itwa kwenda teketezwa na wana yakini nako, basi watasema: Hakika kweli
sisi tulikuwa ni wenye kudhulumu tulipo yaacha yanayo tunafiisha, na tusiziamini
Ishara za Mola wetu Mlezi.
Rudi kwenye Sura
15. Maneno hayo hawaachi kuyakariri na kuyapigia makelele mpaka kwa
adhabu yetu tukawafanya kama mimea iliyo fyekwa, na moto ulio zimika, hawana
tena uhai.
Rudi kwenye Sura
16. Wala hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa mpango
huu wa hikima, na muundo huu wa namna peke yake, kwa mchezo. Bali tumefanya
yote haya kwa hikima ya juu ambayo wanaifahamu wenye kuzingatia.
Rudi kwenye Sura
17. Lau kuwa tunataka kufanya mchezo na pumbao isingeli mkinika kuchukua
ila yaliyo katika ufalme wetu, kwani hapana ufalme ila wetu - ingeli kuwa
Sisi ni wa kufanya hayo. Wala nasi si wenye kufanya hayo, kwa kuwa si laiki
ya haki yetu.
Rudi kwenye Sura
18. Lakini jambo linalo tuelekea Sisi kulifanya ni kuipambanisha
kweli juu ya uwongo ipate kuuondoa. Na nyinyi makafiri mtahiliki kwa sababu
ya kumzulia Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Rudi kwenye Sura
19. Na ni vya Mwenyezi Mungu peke yake vyote viliomo mbinguni na
katika ardhi, kwa kuviumba na kuvimiliki. Basi ni haki Yeye peke yake kuabudiwa.
Na Malaika walio karibishwa kwake hawana kiburi cha kuwazuia kumuabudu
na kumnyenyekea, wala hawaoni machofu na kunyong'onyea kwa ibada ya mchana
na usiku.
Rudi kwenye Sura
20. Wanamtakasa aliye tukuka shani yake na kila lisio muelekea. Kumtakasa
huku hakusiti, bali huo ni mtakaso wa daima, hawana shughuli nyengine ya
kuwashughulisha.
Rudi kwenye Sura
21. Washirikina hawafanyi wafanyavyo walio karibishwa katika
kumsafishia ibada Mwenyezi Mungu, bali wao wamewaabudu wenginewe, na wakafanya
miungu duniani isiyo stahiki kuabudiwa. Na huwaje kwenda kuabudu kitu kisicho
kuwa Mwenyezi Mungu, ambacho hakiwezi kufufua?
Rudi kwenye Sura
22. Lau kuwa mbinguni na duniani kuna miungu isipo kuwa Mwenyezi
Mungu wanao endesha mambo yao, basi ingeli haribika nidhamu iliyo simamishiwa
hizo mbingu na ardhi kwa kuumbwa, na ikafikilia mwisho wa mpango na hikima.
Basi na atakasike Mwenyezi Mungu, Mwenye Ufalme wote, na yote wanayo msingizia
washirikina.
Rudi kwenye Sura
23. Yeye Subhanahu hahojiwi kwa anayo yatenda, kwani ni Yeye pekee
mwenye utukufu na madaraka, Mwenye hikima na ujuzi. Hakosei katika kutenda
chochote. Ni wao ndio watahisabiwa na kuhojiwa kwa wanayo yatenda, kwa
kuwa wao hukosea kwa udhaifu wao na ujinga wao na kughilibiwa na matamanio.
Rudi kwenye Sura
24. Hawaujui waajibu wa Mwenyezi Mungu uliyo juu yao, ndio
maana wakawa na miungu mingine isiyo kuwa Yeye wakaiabudu bila ya kuwa
na ushahidi wowote wa kuingia akilini, wala uthibitisho wa kweli. Ewe Nabii!
Waambie: Leteni uthibitisho wenu kama kweli Mwenyezi Mungu ana mshirika
katika utawala hata akafaa kushirikishwa katika kuabudiwa. Hii Qur'ani
iliyo kuja kuukumbusha umati wangu kwa linalo wajibikia, na hivi Vitabu
vya Manabii wengine vilivyo kuja kukumbusha kaumu za kabla yangu, vyote
hivyo vimesimama juu ya Tawhid, Upweke wa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi
wao hawajui yaliyo kuja ndani ya Vitabu hivyo, kwa sababu hawajishughulishi
kuyazingatia yaliomo humo. Basi wao wamekuwa wenye kuipuuza Imani ya Mwenyezi
Mungu.
Rudi kwenye Sura
25. Ewe Nabii! Sisi hatukumtuma Mtume yeyote kabla yako ila tulimpa
wahyi (ufunuo) awafikishie watu wake kuwa hastahiki kuabudiwa isipo kuwa
Mimi. Basi nisafieni ibada, iwe kwangu tu.
Rudi kwenye Sura
26. Na baadhi ya makafiri wa Kiarabu walisema: Arrahman, Mwenyezi
Mungu Mwingi wa Rehema, ana mwana, kwa yale madai yao kuwa Malaika ni binti
za Mwenyezi Mungu. Ametakasika na kuwa na mwana! Kwani hao Malaika ni waja
wake walio tukuzwa tu kwa kuwakaribisha, na kwa wanavyo muabudu Yeye.
Rudi kwenye Sura
27. Hawamtangulii Mwenyezi Mungu kwa kauli yao wainenayo kabla ya
Yeye kuwapa ruhusa. Na wao hawatendi lolote ila kwa amri yake tu, wala
hawapindukii mipaka ya amri anayo waamrisha.
Rudi kwenye Sura
28. Mwenyezi Mungu anazijua hali zao zote na vitendo vyao vyote,
walivyo vitanguliza na walivyo viakhirisha. Wala hawamwombei mtu kwake
ila kwa aliye ridhia Mwenyezi Mungu. Na wao jinsi ya wingi wa khofu yao
kumwogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kumtukuza Yeye, daima wana hadhari
naye..
Rudi kwenye Sura
29. Na miongoni mwa Malaika atakaye sema: Mimi ni mungu wa kuabudiwa
badala ya Mwenyezi Mungu, huyo tutamlipa kwa kumtia Jahannamu. Mfano wa
malipo hayo tunamlipa kila mwenye kupindukia mipaka ya haki, na wakajidhulumu
nafsi zao kwa kudai Ungu na kuingia katika ushirikina.
Rudi kwenye Sura
30. Wenye kukufuru wamepofuka, na
hawaoni kuwa mbingu na ardhi hapo mwanzo zilikuwa zimeshikamana. Kwa uwezo
wetu tukazibambandua mbali mbali. Na tukajaalia kutokana na maji, ambayo
hayo si kitu hai, kila chenye uhai kutokana na hayo hayo. Basi je! Baada
ya yote haya wangali kupuuza tu, na hawaamini kuwa bila ya shaka yoyote
hapana mungu isipo kuwa Sisi?
"Je! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa
zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho
hai? Basi je, hawaamini?" Aya hii ina maana ya kisayansi yenye kutilia
nguvu nadhariya ya ilimu za kisasa katika kuumbwa sayari na ardhi. Nayo
ni kuwa mbingu na ardhi asili yao zilikuwa zimeshikamana. Na ukweli wa
sayansi zinazo kubaliwa ni kuwa hakika ziliambatana, na sayansi mbali mbali
zinathibitisha hayo. Na zipo nadhariya nyengine kadhaa wa kadhaa ambazo
kwazo zaweza kuelezea dhaahiri ya mambo haya. Lakini bado kuthibiti nadhariya
mojapo kwa njia ya mkato kwa wanazuoni kwa kuwafikiana wote. Kwa kuonyesha
mfano tutaja nadhariya mbili:
Nadhariya ya Kwanza: Imekhusu kuumbwa kwa mfumo wa jua (Solar
System). Kwa mfano imethibiti kuwa mawingu au umande ulio zunguka jua ulianza
kuenea kwenye anga lilio baridi, na chembechembe za gasi zinazo fanya hayo
mawingu au moshi zikakusanyika kwenye chembechembe za vumbi linalo kwenda
kwa kasi kubwa. Kisha chembechembe hizo zikawa zinagongana na zinarindika,
na huku ndani yake zikawamo gasi nzito, na kukazidi kurindika na kujumuika
kwa kupita mamilioni na mamilioni ya makarne mpaka zikafanyika sayari na
mwezi na ardhi kwa umbali unao stahiki. Na yajuulikana kuwa huko kukusanyika
na kurindika huzidisha mbinyo (Pressure), na huo huzidisha joto. Na gamba
la ardhi lilipo ingia kupoa, na wakati zilipo ripuka volkano ardhi ikapata
mvuke wa maji na gasi ya Carbon dioxide ilio tokana na miripuko ya volkano...na
katika iliyo saidia kupatikana Oxygen katika hewa baada ya hapo ni
nishati na nguvu za miyale ya jua kwa njia ya mwanga juu ya mimea na majani
ya mwanzo.
Ama Nadhariya ya Pili: Imekhusiana na uumbaji wa ulimwengu kwa
jumla, ambao kwa mukhtasari unaelezwa na kauli yake Mtukufu: "Zilikuwa
zimeambatana", yaani zimeshikamana na kuwa kitu kimoja. Na hayo ndiyo yaliyo
fikilia mwishoni ilimu za sayansi katika uumbaji wa ulimwengu. Nayo ni
kwamba kabla ya kufikilia sura yake hii ya sasa ulikuwa kama donge lilio
kusanyika lenye kutisha, la mkusanyiko wa chembechembe zenye kuambatana
chini ya mbinyo pressure, hata akili haiwezi kuifikiria. Na hizi sayari
zote na nyota zilioko mbinguni hivi leo tunazo ziita mfumo wa jua solar
system zilikuwa ni mkusanyiko wa donge moja lisilo zidi 1/2 diameter yake
maili milioni tatu. Na neno lake Mwenyezi Mungu: "Tukazibambandua" linafahamisha
ule mripuko mkubwa wa mwanzo wa ki-nuclear ukazalisha uumbaji wa anga na
sayari za namna mbali mbali tunazo ziita kwa pamoja "Mfumo wa Jua" au Solar
System.
"Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai": Aya hii imethibitisha
uhakika wa kisayansi ulio thibitishwa na ncha mbali mbali za ilimu. Imethibitisha
Cytology, sayansi ya "cells", (khalaya), kwamba maji ni muhimu kabisa katika
ujengaji wa "cells" zote za vitu vilivyo hai, ikiwa mimea au wanyama. Na
ilimu ya "Kimyaa", Chemistry kwamba maji ni lazima yapatikane katika
vitendo na mageuko yoyote katika viumbe vilivyo hai. Basi hayo maji ama
yawe ni kiungo, kitu cha kusaidia, au cha kuwamo ndani ya kitendo, au ni
matokeo yake.
Na imethibitisha ilimu ya viungo physiology kwamba maji ni
dharura kwa viungo kufanya kazi yao. Bila ya hayo maji hautodhihiri uhai
katika viungo.
Rudi kwenye Sura
31. Na katika dalili za uweza wetu ni kuwa tumeifanya milima imesimama
imara kwenye ardhi ili isiyumbeyumbe nao watu, na tumefanya humo njia pana,
za kupitia kwa wasaa, ili waweze kuongoza njia humo kwa makusudio yao.
Maoni ya wataalamu juu ya Aya ya 31:
"Na tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe,
na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka." Ilivyo kuwa ndani ya ardhi
kila kitu kimeyayuka, na lau kuwa milima imewekwa tu katika baadhi ya sehemu
za huu mpira wa dunia kama majabali yaliyo nyanyuka juu tu, uzito wao ungeli
sabibisha gamba la dunia liyumbe, au lipindane na kupasuka. Kwa hivyo Mwenyezi
Mungu kwa utukufu wa shani yake ameifanya milima isimame imara kwa
kuwa na mizizi iliyo zama kwenye gamba la ardhi mpaka chini kwenye kina
kirefu kulingana na urefu wake kwendea juu. Kwa hivyo imekuwa hiyo milima
kama vigingi, kama alivyo jaalia eneo la minyanyuka hii na mizizi ni duni
kuliko maeneo ya gamba lilio zunguka. Yote haya ni kwa ajili ya kueneza
sawa uzito wa juu ya gamba kwa pande zote ili pasiwepo kuyumbayumba na
kupasuka. Kwani hakika kuenezwa kwa uzito juu ya uso wa dunia yakaribia
kuwa hakuleti athari kubwa ya kutajika.
Na ilimu za kisasa zimethibitisha kuwa kuenezwa kwa nchi kavu na
maji juu ya ardhi, na kuwepo mfululizo wa milima juu yake ni katika yanayo
hakikisha hali ilivyo ardhi, na imethibitika kuwa chini ya milima mizito
kuna vitu vyepesi kubungunyika, na chini ya maji ya bahari kuu vipo vitu
vizito. Kwa kuenezwa uzani wa namna hiyo mbali mbali katika dunia, na mgawanyo
huu wa milima, makusudio yake ni kusawizisha uzani wa mpira huu wa ardhi.
Na ilivyo nyanyuka milima zikatokea nyanda na mabonde na njia baina ya
milima na mwambao na bahari na minyanyuko, na zikawa njia.
Rudi kwenye Sura
32. Na tumeifanya mbingu kama dari iliyo nyanyuliwa, na tukailinda
isianguke, au visianguke viliomo humo. Na juu ya hayo, wao hawazioni wala
hawaziingatii Ishara zetu zenye kuonyesha uweza wetu na hikima yetu na
rehema yetu.
Maoni ya wataalamu juu ya Aya 32:
"Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa lakini wanazipuuza
Ishara zake. ": Aya hii tukufu imethibitisha kuwa mbingu na vyote viliomo
ndani yake vimehifadhiwa visiwe na ila yoyote, na vimehifadhiwa visidondoke
juu ya ardhi. Na mbingu ni kila kilicho juu yetu, kuanzia kifuniko hichi
cha hewa inayo walinda walioko juu ya ardhi na khatari nyingi za angani
ambazo zinazuia maisha, mfano wa vimondo vya nyota za mkia, na miyale.
Na juu ya ardhi pana kifuniko cha hewa kinacho linda ardhi kwa nguvu za
mvutano, na haifai kukosekana hivyo bila ya maangamizo kabisa. Na juu ya
kifuniko cha hewa ndio kuna hizo sayari za mbinguni, na zipo kwa umbali
mbali mbali kufuatana na nyendo zao tangu mwanzo.
"Na tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa" yaani hizo sayari
na vyote vilio mbinguni vyaonekana kwa nadhari yetu kama kwamba ni dari,
na tunaona vilio juu ya vichwa vyetu kama ni vidogo kuliko vilioko upeo
wa macho. Na hayo ni kiini macho tu, kama tunapo liona jua kubwa wakati
wa kuchomoza na kuchwa kuliko adhuhuri. Na hili qubba la mbingu lina sifa
zake, zinazo khitalifiana kila ukizidi mnyanyuko wa ardhi, kama hizo sayari
za mbinguni kwa mujibu wa jicho linavyo ona katika qubba la mbingu.
Rudi kwenye Sura
33. Na Mwenyezi Mungu ndiye aliye umba usiku na mchana, na jua na
mwezi. Vyote hivyo vinakwenda katika njia zake kama alivyo zijaalia Mwenyezi
Mungu, na zinamtakasa bila ya kupotea.
Maoni ya wataalamu juu ya Aya 33:
"Na Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote
katika anga vinaogelea." Kila sayari ya mbinguni ina mzunguko wake makhsusi
inayo ogelea kuufuata. Na zote hizo hazisiti, na zinakwenda kwa mwendo
wao maalumu katika anga. Na sisi tunaona hayo kwa hakika kwa kutazama mwendo
wa jua na mwezi. Kama kadhaalika mzunguko wa ardhi wake wenyewe ndio unao
leta usiku na mchana kwa zamu, kama kwamba unaogelea.
Rudi kwenye Sura
34. Ewe Nabii! Hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako wewe aishi
milele, hata ikawa hao makafiri wakawa wanakutamania ufe wewe. Vipi wanakutamania
mauti wewe na hali na wao vile vile watakufa kama wewe? Ukifa wewe, je,
ndio wao watabakia kushinda wanaadamu wote?
Rudi kwenye Sura
35. Kila nafsi haina budi kuonja mauti. Na Sisi tunakufanyieni hapa
duniani kama wenye kukupeni mtihani, kwa kukupeni yenye manufaa yenu na
yenye madhara pia, ili abagulike mwenye kushukuru kwa kupewa kheri na kuvumilia
balaa, na yule asiye na fadhila kwa neema aipatayo na anapapatika akipata
misiba. Nanyi mtarejeshwa kwetu, na hapo tutakuhisabieni vitendo vyenu.
Rudi kwenye Sura
36. Na wakikuona, ewe Nabii, wale walio mkataa Mwenyezi Mungu na
ulio kuja nayo wewe, hawakufanyii wewe ila maskhara na kejeli. Huambiana
wao kwa wao: Ndiye huyu anaye watia aibu miungu yenu? Na hali wao hawasadiki
kumdhukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliye waeneza rehema yake!
Rudi kwenye Sura
37. Na ikiwa wao wanataka waletewe adhabu kwa upesi, basi ndio tabia
ya binaadamu kutaka kila jambo kwa haraka. Basi enyi wenye haraka! Nitakuonesheni
neema yangu duniani, na adhabu yangu Akhera. Msijishughulishe kuhimiza
kitu ambacho hakina budi kuwa.
Maoni ya wataalamu juu ya Aya 37:
"Mwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi
msinihimize." Makusudio ya kauli ya "Ishara" ni ishara za maumbile zenye
kuonyesha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na uweza wake. Na ujuzi wa ilimu za
sayansi utavumbua kwa mujibu wa itavyo nyanyuka akili ya binaadamu. Na
hayo ni kwa mujibu wa miadi ilio wekwa kwa wakati wake. Kila ukifika wakati
maalumu Mwenyezi Mungu hudhihirisha Ishara yake, au huwasahilishia wanaadamu
njia za kuzifikilia Ishara hizo.
Rudi kwenye Sura
38. Na makafiri wanao himiza adhabu na huku wanaona haiwi, wanasema:
Lini yatakuwa hayo mnayo tuahidi, enyi Waumini, kama kweli hayo myasemayo?
Rudi kwenye Sura
39. Lau kuwa hao walio mkufuru Mwenyezi Mungu wangeli ijua hali yao
wakati watapo kuwa hawawezi kuuondoa Moto kwenye nyuso zao na migongo yao,
na wala hawampati wa kuwasaidia kuuondoa, wasingeli sema wayasemayo.
Rudi kwenye Sura
40. Kiyama hakiwajii kwa kukitarajia kutokea kwake, bali kitawazukia
kwa ghafla tu kiwababaishe, wasiweze kukirudisha, wala wao hawatapewa muhula
wa kutubia na kutafuta udhuru kwa waliyo kwisha yatenda..
Rudi kwenye Sura
41. Na Mitume wa kabla yako yaliwapata vile vile ya kufanyiwa kejeli
na makafiri katika kaumu zao. Ikawateremkia hao walio wakataa Mitume na
kuwafanyia maskhara adhabu hiyo hiyo ambayo wao waliifanyia maskhara
na kejeli.
Rudi kwenye Sura
42. Ewe Nabii! Waambie: Ni nani anaye kuhifadhini na nakama zake
wakati wa usiku na mchana, na akakurehemuni na kukuneemesheni? Hapana awezae
hayo. Lakini wao wanaipuuza Qur'ani ambayo ndiyo inawakumbusha ya kuwafaa
na kuwalinda na adhabu.
Rudi kwenye Sura
43. Kwani wao wanao miungu wa kuwalinda na adhabu itokayo kwetu?
Hasha! Hiyo miungu yao haiwezi kujilinda wenyewe, licha kumlinda mwenginewe.
Wala hapana yeyote awezae kumlinda yeyote kati yao karibu yake au pamoja
naye pindi tukitaka kumuadhibu na kumteketeza.
Rudi kwenye Sura
44. Sisi hatufanyi haraka kuwaadhibu hawa kwa ukafiri wao, lakini
tunawapururia na kuwastarehesha katika uhai wa dunia, kama tulivyo wastarehesha
baba zao kabla yao, mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je! Wanajitia upofu hawaoni
yanao wazunguka wakaona kuwa Sisi tunaiendea nchi na tukaipunguza ncha
zake kwa ushindi wa Waumini? Ni wao ndio wenye kushinda au Waumini ambao
Mwenyezi Mungu amewaahidi kuwasaidia na kuwaunga mkono?
Maoni ya wataalamu juu ya Aya 44:
"Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza
mipaka yake? Basi je! Hao ni wenye kushinda?": Aya hii ni katika Aya za
miujiza ya kisayansi katika Qur'ani Tukufu. Hii inaonyesha kuwa dunia si
mduwara kaamili. Na wataalamu wa sayansi hawakutamakani kupima masafa ya
dunia baraabara mpaka kiasi ya miaka 250 tu takriban, walipo ingia kikundi
cha mabingwa walio khusika na ilimu ya kupima marefu baina ya daraja mbili
za urefu longitudes. Na hayo kwa pahala mbali mbali duniani. Katika kupima
huku ikadhihiri kuwa nusu ya kati ya dunia kwenye equator inazidi kuliko
nusu ya poles kwa takriban kilomita 21.5. Yaani dunia imepungua katika
ncha zake, yaani katika poles. Na inajuulikana maalumu kuwa sura ya dunia
na masafa yake ndio msingi katika kuchorwa kwa ramani.
Rudi kwenye Sura
45. Ewe Nabii! Sema: Sikuhadharisheni kwa maneno yanayo tokana nami.
Lakini nakuhadharisheni kwa Wahyi (Ufunuo) unao tokana na Mwenyezi Mungu
Mtukufu ulio nijia mimi. Na huo ni wa Haki na kweli. Lakini hao kwa sababu
ya kupuuza kwao kurefu kuipuuza Sauti ya Haki, Mwenyezi Mungu ameyaziba
masikio yao mpaka wakawa kama viziwi. Na kiziwi hasikii Wito anapo hadharishwa
na adhabu!
Rudi kwenye Sura
46. Na kuwa na yakini kuwa nao wakisibiwa hata na chembe ya adhabu
ndogo wanayo ifanyia maskhara, hupiga kelele kwa khofu wakisema: Ole wetu!
Hakika sisi tulikuwa tunajidhulumu nafsi zetu, na tukiwadhulumu wenginewe,
tulipo yakataa tuliyo ambiwa.
Rudi kwenye Sura
47. Na Sisi tunaweka mizani ya kupimiwa kwa uadilifu Siku ya Kiyama.
Basi hadhulumiwi mtu kwa kupunguziwa wema wake au kuongezewa maovu yake.
Hata ikiwa ni kiasi ya uzani wa chembe ndogo hii tutaileta na tutaihisabu.
Na yatosha kuwa ni Sisi ndio wa kuhisabu. Basi hapana atakaye dhulumiwa
kitu.
Maoni ya wataalamu juu ya Aya ya 47:
"Nasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi
nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali
tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu.": Aya hii tukufu inaonyesha
kuwa chembe ya khardali ni hadi ya udogo katika mizani. Imethibitika
kwa majaribio ya sayansi kuwa Kilogram ya chembe za khardali ni chembe
913,000. Kwa hivyo chembe moja ya khardali ni takriban sehemu moja katika
elfu ya gram, yaani ni takriban sawa na Miligram moja. Na huu ni uzito
mdogo kabisa unao juulikana katika mbegu za mimea mpaka sasa. Kwa hivyo
hutumiwa katika kupimiwa vitu vidogo vidogo kabisa.
Rudi kwenye Sura
48. Na Musa na Haaruni tuliwapa Taurati ya kupambanua baina ya kweli
na uwongo, na halali na haramu. Na juu ya hivyo hiyo ni nuru ya kuwaongoa
watu wafuate njia ya kheri na uwongozi mwema, na ni kumbusho la kuwafaa
wachamngu...
Rudi kwenye Sura
49. Ambao wanamkhofu Muumba wao Mwenye kumiliki mambo yao yote, juu
ya kuwa wako mbali na watu, na wala hawamwoni mtu. Nao wamo katika khofu
ya daima kuikhofu Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
50. Na hii Qur'ani ni kumbusho, lenye kheri nyingi. Tumekuteremshieni
kama tulivyo mteremshia Musa. Basi yawaje nyinyi muikatae, na hali nyinyi
ndio mnao stahiki zaidi kuiamini kuliko watu wote!
Rudi kwenye Sura
51. Na hakika Sisi tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu na fikra ya kutafuta
Haki kwa usafi wa niya kabla ya Musa na Haaruni. Na Sisi ni Wenye
kujua vyema hali yake na fadhila zake zilizo mfanya astahiki kuchukua Utume.
Rudi kwenye Sura
52. Ewe Nabii! Kumbuka pale Ibrahim alipo mwambia baba yake na watu
wake kuwaonya juu ya masanamu waliyo kuwa wakishughulikia kuyaabudu: Ni
nini haya masanamu ambayo nyinyi mmeshika kuyaabudu?
Rudi kwenye Sura
53. Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyatukuza na wameshika kuyaabudu.
Nasi tukawafuata.
Rudi kwenye Sura
54. Yeye akasema: Nyinyi na baba zenu kabla yenu, ni wazi kuwa nyote
mko mbali na Haki.
Rudi kwenye Sura
55. Wakasema: Je! Umetujia kwa haya uyasemayo na hakika ya kweli
unayo iamini, au kwa maneno haya wewe ni katika wanao fanya pumbao na mchezo
tu bila ya kuwa na maana yoyote?
Rudi kwenye Sura
56. Akasema: Hapana maskhara katika niyasemayo. Bali Mola wenu Mlezi
anaye stahiki peke yake kutukuzwa na kuogopwa na kuabudiwa ndiye aliye
ziumba mbingu na ardhi, na akazileta bila ya kuwapo mfano wake wa kuigiza.
Basi ni haki yake Yeye tu peke yake kuabudiwa. Na mimi kwa haya niyasemayo
ni katika wenye hakika ambao hunena wanayo yashuhudia na wanayajua.
Rudi kwenye Sura
57. Na akasema moyoni mwake: Naapa kwa Mwenyezi Mungu, nitayafanyia
vitimbi haya masanamu yenu niyavunje pale mtapo ondoka, ili mpate kuona
upotovu wenu.
Rudi kwenye Sura
58. Baada ya kwisha ondoka wale watu, Ibrahim aliyaendea masanamu
akayavunja vipande vipande, isipo kuwa sanamu kubwa. Hilo aliliacha ili
wapate kulirejea waliulize yaliyo isibu miungu yao. Nalo halikujibu kitu.
Kwa hivyo upotovu wa ibada yao ukabainika.
Rudi kwenye Sura
59. Baada ya kwisha ona yaliyo wapata miungu yao wakasema: Nani aliye
itendea haya miungu yetu? Hakika mtu huyu hapana shaka ni katika walio
jidhulumu wenyewe kwa adhabu itayo mpata..
Rudi kwenye Sura
60. Wakasema baadhi yao: Tumemsikia kijana mmoja akiitaja kwa kuisubu;
naye anaitwa Ibrahim.
Rudi kwenye Sura
61. Wakasema wakubwa wao: Nendeni mkamlete, ahukumiwe mbele ya macho
ya watu, na washuhudie aliyo yatenda!
Rudi kwenye Sura
62. Baada ya kwisha mhudhurisha, wakasema: Ni wewe ulio itenda haya
miungu yetu, ewe Ibrahim?
Rudi kwenye Sura
63. Kuwanabihisha upotovu wao, alisema kwa kuwakejeli: Hili kubwa
lao ndilo lililo tenda hayo! Iulizeni hiyo miungu aliyo yatenda huyu, kama
kweli inaweza kujibu suala yenu!
Rudi kwenye Sura
64. Wakazirejea nafsi zao wakiifikiria ile ibada yao kuabudu vitu
visivyo mnufaisha yeyote wala haviwezi kujitetea wenyewe. Wakayaona makosa
yao. Baadhi yao wakasema: Ibrahim si katika walio dhulumu, bali nyinyi
ndio madhaalimu kwa kuabudu vitu visio stahiki kuabudiwa.
Rudi kwenye Sura
65. Kisha wakarejea tena, wakaacha uwongofu, wakarudia upotovu. Wakamwambia
Ibrahim: Hakika wewe umekwisha jua kuwa haya masanamu tunayo yaabudu hayasemi
kitu. Basi vipi unatutaka tuyaulize?
Rudi kwenye Sura
66. Ibrahim akasema: Ikiwa hali yao haya masanamu ni hii, hayawezi
kitu, na nyinyi ndio makhusiano yenu nao ni hivi, basi nyinyi mmekuwa mnaacha
kumuabudu Mwenyezi Mungu, na badala yake mnaabudu vitu visivyo kupeni faida
hata chembe mkiviabudu, wala havikudhuruni kwa lolote mkiviachilia mbali?
Rudi kwenye Sura
67. Aibu yenu! Nyinyi na miungu yenu mmelaanika! Mnaacha fikra zenu
zipotee, na mnapuuza kuzingatia? Bila ya shaka haya masanamu hayafai kuabudiwa!
Rudi kwenye Sura
68. Wakaambiana wenyewe kwa wenyewe: Mchomeni moto mpate kuinusuru
miungu yenu kwa mateso haya, ikiwa nyinyi mnataka kufanya kitu cha kuiunusuru
miungu yenu.
Rudi kwenye Sura
69. Sisi tukaufanya moto ule uwe baridi na salama, hauna madhara
yoyote, kwa Ibrahim.
Rudi kwenye Sura
70. Wao walitaka kumuangamiza, lakini Sisi tukamwokoa, na tukawafanya
wao ndio watu walio khasiri mno.
Rudi kwenye Sura
71. Na tukamwokoa yeye na Luut'i na njama zilizo pangwa, wakaelekea
kwenye nchi tuliyo ijaalia kheri nyingi kwa watu wote, na tukawapeleka
huko Manabii wengi.
Rudi kwenye Sura
72. Na tukampa Ibrahim mtoto Is-haq, na kutokana na Is-haq tukampa
Yaaqubu, zaidi kuliko aliyo taka. Na wote wawili, Is-haq na Yaaqubu tuliwajaalia
kuwa ni watu wema.
Rudi kwenye Sura
73. Na tukawafanya ni Manabii wakiwaendea watu, wakiwaongoa kwenye
kheri kwa mujibu wa tulivyo waamrisha. Na tukawaonyesha vitendo vyema,
na kudumisha Sala kama inavyo faa, na kutoa Zaka. Na wakawa wanatunyenyekea
na kutusafia ibada Sisi tu.
Rudi kwenye Sura
74. Luut'i tukampa kauli ya kukata na madhubuti katika hukumu
na ilimu yenye manufaa. Na tukamwokoa kutokana na mji ambao watu wake wanafanya
kitendo cha namna ya peke yake katika uovu. Hakika hao walikuwa watu walio
shikilia kufanya maovu, walio toka kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu na
tabia iliyo zowewa.
Rudi kwenye Sura
75. Tukampeleka njia ya watu wa rehema yetu. Hakika huyo alikuwa
miongoni mwa watu wema alio wakusanya Mwenyezi Mungu katika rehema yake
na akawakunjulia msaada wake.
Rudi kwenye Sura
76. Na hapa tumtaje Nuhu wa kabla ya Ibrahim na Luut'i, pale alipo
mwomba Mola wake Mlezi aisafishe nchi kwa kuwaondoa waovu. Tukamuitikia
ombi lake, tukamwokoa yeye na wale walio amini katika watu wake, kutokana
na shakawa ya kimbunga kikubwa.
Rudi kwenye Sura
77. Tukamlinda kwa nusura yetu na vitimbi vya kaumu yake walio zikanusha
Ishara zetu zenye kuthibitisha Utume wake. Hakika hao walikuwa watu wa
shari. Basi tukawagharikisha wote!
Rudi kwenye Sura
78. Ewe Nabii! Wataje Daud na Suleiman walipo toa hukumu katika kesi
ya konde, ilio ingiliwa na mbuzi wa watu mbali usiku na wakala mazao yake.
Na Sisi tulikuwa tunaijua hukumu iliyo khusiana na kesi hiyo.
Kisa cha hiyo hukumu: Mbuzi waliingia usiku mmoja katika konde
ya mtu, wasibakishe kitu. Daud akahukumu kuwa wale mbuzi wawe wa mwenye
konde kulipia khasara yake. Suleiman akatoa hukumu nyengine, akasema: Mbuzi
wale wabakie mkononi mwa mwenye konde mpaka itapo mea tena mazao yake,
na avumilie kwa yaliyo mpata. Na baada yake warejesheane.
Rudi kwenye Sura
79. Basi tulimfahamisha Suleiman hiyo fatwa. Na wote wawili tuliwapa
hikima na ilimu ya maisha na mambo yake. Na tulimfanyia Daud pamoja na
milima it'ii na imtakase Mwenyezi Mungu kama alivyo kuwa anamtakasa yeye
Daud na kila lisio kuwa linamwelekea Mwenyezi Mungu. Na kadhaalika tuliwafanya
ndege hivyo hivyo wamsabihi Mwenyezi Mungu pamoja naye. Na tulifanya hayo
kwa uweza wetu usio shindika.
Rudi kwenye Sura
80. Tukamfundisha Daud kufuma nguo za chuma, ili zikulindeni katika
vita vyenu. Basi mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa neema hii aliyo kuneemesheni.
Rudi kwenye Sura
81. Na tulimsahilishia Suleiman upepo unao vuma kwa nguvu umtumikie,
nao huo ulikuwa unakwenda kwa kufuata amri yake mpaka kwenye nchi tuliyo
izidishia kheri yake. Nasi ni wenye kuyajua yote hayo. Halitupotei kubwa
wala dogo.
Rudi kwenye Sura
82. Na tukawafanya mashetani wamtumikie kwa kuzamia chini baharini
kumletea lulu na marijani; na wakifanya kazi nyenginezo, kama kujenga ngome
na majumba ya kifalme. Na Sisi tulikuwa tukiwaangalia katika kazi zao hizo,
basi hapana hata mmoja wao aliye pata shida, wala hawakuvunja amri ya Suleiman.
Rudi kwenye Sura
83. Ewe Nabii! Mtaje Ayyubu, pale alipo mwita Mola wake Mlezi, na
maradhi yalikwisha mdhoofisha, na akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika
nimesibiwa na madhara na yananiuma! Na Wewe ni Mbora wa wanao rehemu..
Rudi kwenye Sura
84. Tukamwitikia kwa aliyo yaomba, tukamwondolea madhara, na
tukampa watoto kwa kadri ya waliyo kwisha kufa. Na tukamwongezea mfano
wa wale, kuwa ni rehema iliyo tokana na fadhila yetu, na pia ni kuwa ni
kumbusho kwa wenginewe wanao tuabudu ili wapate nao kusubiri kama alivyo
subiri yeye, na watumai kupata rehema ya Mwenyezi Mungu kama alivyo tumai
yeye.
Rudi kwenye Sura
85. Ewe Nabii! Watajie watu wako khabari za Ismail, na Idris, na
Dhulkifli. Wote hao ni miongoni wanao subiri wakahimili taklifa na shida.
Rudi kwenye Sura
86. Na tukawajaalia miongoni mwa watu wa kupata rehema yetu. Hakika
hao ni katika waja wetu wema.
Rudi kwenye Sura
87. Ewe Nabii! Taja kisa cha Yunus, aliye mezwa na samaki..Pale alipoona
dhiki kwa vile watu wake walipo puuza wito wake, naye akawahama akenda
mbali nao na huku amewakasirikia. Akadhani ya kuwa Mwenyezi Mungu
amemruhusu kuwahama, na kwamba haitopita hukumu juu yake. Samaki akammeza,
na akaishi katika kiza cha bahari. Akamwita Mola wake Mlezi kwa kumnyenyekea,
na kuungama aliyo kuwa nayo, akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hapana wa kuabudiwa
kwa haki ila Wewe. Ninakutakasa na kila lisio kuelekea Wewe. Ninaungama
kuwa hakika mimi nilikuwa miongoni mwa walio dhulumu nafsi zao kwa kutenda
yasio kupendeza.
Rudi kwenye Sura
88. Tukamwitikia kwa aliyo kuwa akiyaomba, na tukamvua na dhiki aliyo
kuwa nayo. Na mfano wa hivi ndivyo tunavyo waokoa Waumini wanao ungama
makosa yao, na wakatuomba kwa usafi wa moyo.
Rudi kwenye Sura
89. Na kitaje kisa cha Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi baada
ya kwisha ona uweza wake Subhanahu kwa alivyo mtia katika nafsi yake matarajio
ya rehema yake. Alisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Usiniache mpweke bila ya
kuwa na mrithi, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi. Kwani Wewe ndiye utakaye
baki baada ya kumalizika viumbe vyote.
Rudi kwenye Sura
90. Tukamtimizia matumaini yake, na tukamwitikia dua yake, na tukamtunukia
juu ya ukongwe mwanawe, Yahya, tukamfanya mkewe tasa aweze kuzaa. Hakika
wasafi hao Manabii walikuwa wepesi wa kutenda kheri tunayo waitaka waitende,
na wanatuomba kwa kutumai rehema yetu, na kuikhofu adhabu yetu. Na walikuwa
hawamtukuzi mtu wala hawamwogopi mtu isipo kuwa Sisi tu.
Rudi kwenye Sura
91. Pamoja na hawa simulia kisa cha Maryamu aliye ulinda uke wake,
nasi tukamfikishia siri katika siri zetu. Tukamjaalia achukue mimba bila
ya mume, na tukamjaalia mwanawe azaliwe bila ya baba. Akawa yeye na mwanawe
dalili iliyo wazi ya uweza wetu kugeuza sababu na vinavyo sabibishwa. Na
hakika Sisi ni waweza wa kila kitu.
Rudi kwenye Sura
92. Hakika mila hii, nayo ndiyo Uislamu, ndiyo mila iliyo sahihi
inayo kupasini kuilinda, kwa kuwa ni mila moja iliyo shikamana wala haikukhitalifiana
baina ya hukumu zake. Basi nanyi msifarikiene katika mila hii kwa
makundi na vyama. Na Mimi ndiye Muumba wenu, na Mwenye kumiliki mambo yenu
yote. Basi niabuduni Mimi tu, wala msinishirikishe na mwengine.
Rudi kwenye Sura
93. Na juu ya kuwepo uwongozi huu aghlabu ya watu wamegawanyika kwa
mujibu wa matamanio yao, wakafanya mambo yao ya Dini mapande mapande, wakawa
makundi mbali mbali. Na kila kundi litaturejea Sisi tulihisabie vitendo
vyake.
Rudi kwenye Sura
94. Basi mwenye kutenda vitendo vyake vyema, naye ni mwenye kumuamini
Mwenyezi Mungu na Dini yake aliyo iridhia, hatopunguziwa kitu katika juhudi
yake. Bali atalipwa malipo kaamili. Na Sisi ni wenye kuiandika hiyo juhudi
yake. Basi hakitopotea kitu.
Rudi kwenye Sura
95. Na haitakuwa kwa watu wa mji tulio uteketeza kwa sababu ya dhulma
yao kwamba hawatarejea kwetu Siku ya Kiyama, bali hapana budi kuwa watarejea
na tutawahisabia vitendo vyao viovu.
Rudi kwenye Sura
96. Mpaka itapo funguliwa milango ya shari na ufisadi, wakaingia
wana wa Juju na Maajuju wakikimbizana kuteremka milimani na majiani kwa
kufanya vitendo vya fujo na rabsha.
Rudi kwenye Sura
97. Na ikakaribia miadi iliyo haina budi kutimizwa, nayo ni Siku
ya Kiyama, wakawa wale walio kufuru wanakutikana wakikodoa macho yao kwa
wingi wa kitisho, wakipiga makelele kusema: Kitisho gani hichi cha kutuangamiza!
Hakika sisi tulighafilika na Siku hii. Bali tulikuwa ni wenye kujidhulumu
nafsi zetu kwa ukafiri na inda.
Rudi kwenye Sura
98. Wataambiwa makafiri hawa: Nyinyi na hiyo miungu mliyo kuwa mkiiabudu
badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Moto wa Jahannamu. Nyinyi mtaingia
humo muadhibiwe!
Rudi kwenye Sura
99. Lau kama hawa mlio waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni miungu
inayo stahiki kuabudiwa, wasingeli ingia nanyi humo. Na nyote, wenye kuabudu
na kuabudiwa, mtabaki Motoni, wala hamtatoka.
Rudi kwenye Sura
100. Humo watatoa pumzi zitokazo vifuani kwa sauti kama ya mwenye
kukabwa, kwa dhiki watayo pata, na hawatasikia la kuwafurahisha.
Rudi kwenye Sura
101. Hakika wale tulio wakubalia kwa kufuata kwao Haki na vitendo
vya kheri, na tukawaahidi malipo mema, hao watawekwa mbali kabisa na Jahannamu
na adhabu yake.
Rudi kwenye Sura
102. Hawatasikia sauti ya Moto wake unavyo vuma. Nao huko watapata
kila ambacho nafsi inatamani, daima milele.
Rudi kwenye Sura
103. Hawato huzunishwa na Kitisho Kikubwa kinacho wafazaisha makafiri.
Na Malaika watawapokea kwa kuwapongeza kwa kusema: Hii ndiyo Siku yenu
ya neema aliyo kuahidini Mola wenu Mlezi!
Rudi kwenye Sura
104. Siku tutapo zikunja mbingu kama zinavyo kunjwa karatasi katika
kitabu. Na tutawarejeza viumbe kwa ajili ya hisabu na malipo. Wala hatushindwi
kuwarejeza, kwani tuliwaumba mara ya kwanza. Na kama tulivyo waanza tutawarejeza.
Ahadi yetu kwa hayo ni ahadi ya kweli. Daima Sisi tunatenda tunayo yaahidi.
Rudi kwenye Sura
105. Na tulikwisha andika katika Zaburi - nacho ni Kitabu cha Daud
baada ya Taurati - kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema wapate
kuitengeza, na kusahilisha njia za maisha bora humo. ("Bali wenye
upole watairithi nchi"..Zaburi 37.11 "Wenye haki watairithi nchi,
nao watakaa humo milele".. Zaburi 37.29)
Rudi kwenye Sura
106. Hakika katika haya tuliyo yataja, khabari za Manabii pamoja
na kaumu zao, na khabari za Pepo na Moto, yanatosha kuwakumbusha na kuwafanya
wazingatie watu walio tayari kumuabudu Mwenyezi Mungu pekee na hawasalitiki
na mapambo ya dunia.
Rudi kwenye Sura
107. Na hatukukutuma, ewe Nabii, ila uwe ni Rehema kwa walimwengu
wote.
Rudi kwenye Sura
108. Ewe Nabii! Sema: Hakika kiini cha Wahyi aliyo nipa Mwenyezi
Mungu ni kwamba hakika nyinyi hamna Mungu isipo kuwa Yeye. Na yote yaliyo
bakia niliyo funuliwa yanafuata asili hii.
Ikiwa mambo ni hivyo, basi inakuwajibikieni
mjisalimishe na mnyenyekee kwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Rudi kwenye Sura
109. Wakito ujali wito wako, basi waambie: Nimekufunzeni yote aliyo
niamrisha Mola wangu Mlezi; na kwa hivyo tumekuwa sawa kwa kuyajua hayo.
Wala mimi sijui hayo ya kufufuliwa na kuhisabiwa mliyo ahidiwa, yatakuwa
karibu au mbali.
Rudi kwenye Sura
110. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua yote yasemwayo, mnayo yadhihirisha
na mnayo yaficha.
Rudi kwenye Sura
111. Na sijui pengine huko kupewa muhula na kuakhirishiwa adhabu
nyinyi ndio Mwenyezi Mungu anakufanyieni mtihani tu, na kukustarehesheni
kwa ladha za maisha mpaka alipo kadiria Mwenyezi Mungu kukuhisabieni kwa
hikima yake.
Rudi kwenye Sura
112. Ewe Nabii! Sema: Ewe Mola Mlezi! Tuhukumu baina yangu na hawa
nilio wafikishia Wahyi kwa uadilifu ili wasiwe sawa Waumini na makafiri.
Na Mola wetu Mlezi Mwenye kuneemesha kwa neema kubwa, Mwenye kustahiki
kuhimidiwa na kushukuriwa, ndiye wa kutakiwa msaada kuvunja uzushi mnao
zua, enyi makafiri.
Rudi kwenye Sura