1. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameanza Sura hii kwa harufi,
nazo ni T'a na Ha, ili kupingana na makafiri wanao kanya, na kuwa kama
ishara ya kwamba hii Qur'ani imeundwa kwa hizi hizi harufi mnazo zitumia
katika kusema kwenu. Na juu ya hivyo nyinyi mmeajizika (yaani mmeshindwa,
ndio likatokea hilo neno "Muujiza") kuleta Sura walau ndogo, au baadhi
ya Aya zilizo mfano wa Qur'ani.
Rudi kwenye Sura
2. Ewe Mtume! Sisi hatukukufunulia wewe Qur'ani hii iwe ni sababu
ya kukupa dhiki ya nafsi yako kwa kuwasikitikia hao wapuuzi kukupuuza wewe.
Rudi kwenye Sura
3. Lakini tumekuteremshia iwe ni kumbusho kwa mwenye kumkhofu Mwenyezi
Mungu apate kumt'ii.
Rudi kwenye Sura
4. Hii Qur'ani umeteremshiwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye uwezo,
Muumba ardhi na mbingu zilio nyanyuka juu.
Rudi kwenye Sura
5. Mtukufu wa rehema, ametawala sawa sawa juu ya Ufalme wake.
Rudi kwenye Sura
6. Ni wake Yeye tu, Subhanahu, ufalme wa mbinguni na viliomo humo,
na wa ardhi na viliomo juu yake, na ufalme wa vilio baina ya hivyo, na
maadeni na kheri nyenginezo zilizo fichikana chini ya ardhi.
Rudi kwenye Sura
7. Na kama uwezo wa Mwenyezi Mungu ulivyo kusanya kila kitu, kadhaalika
ujuzi wake pia umekusanya kila kitu. Na ewe mtu, ukinyanyua sauti kwa kusema,
basi Mwenyezi Mungu anajua. Kwani Yeye anajua unapo sema na mtu,
na anajua unapo zungumza na nafsi yako.
Rudi kwenye Sura
8. Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Mungu wa Pekee, Mwenye kustahiki kuabudiwa
peke yake. Kwani Yeye amesifika kwa sifa za ukamilifu, naye ndiye Mwenye
bora ya sifa.
Rudi kwenye Sura
9. Ewe Nabii! Unajua khabari za Musa na Firauni?
Rudi kwenye Sura
10. Pale Musa alipo uona moto katika safari yake ya usiku kutoka Madyana
kwendea Misri, akamwambia mkewe na walio kuwa naye: Ngojeni hapa! Mimi
nimeuona moto ule; natumai nitakupatieni kijinga cha moto kutoka
kule mpate kuashia moto, au huko nitapata mtu wa kuniongoza njia.
Rudi kwenye Sura
11. Alipo fika huko, akasikia sauti yenye kutoka juu inamwita: Ewe
Musa!
Rudi kwenye Sura
12. Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mola wako Mlezi! Basi vua viatu
vyako kwa hishima ya pahala hapa; kwani wewe upo katika bonde safi
lenye baraka, nalo ni T'uwa.
Rudi kwenye Sura
13. Na Mimi Mwenyezi Mungu nimekuteuwa wewe kwa kukupa Utume. Basi
sikiliza haya ninayo kufunulia uyajue na ukawafikishie watu wako.
Rudi kwenye Sura
14. Hakika Mimi ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa Pekee, hapana wa kuabudiwa
kwa haki isipo kuwa Mimi. Basi niamini Mimi, na niabudu Mimi, na dumu daima
katika kuishika Sala ili uwe daima unanikumbuka.
Rudi kwenye Sura
15. Hakika Saa ndiyo miadi ya kukutana nami; nami miadi hiyo nimeificha
kwa waja wangu, na nimewaonyesha ishara zake. Hiyo Saa itakuja bila ya
shaka yoyote, na kila nafsi itahisabiwa kwa iliyo tenda.
Rudi kwenye Sura
16. Ewe Musa! Asikuachishe kuiamini Saa na kujitayarisha kwa ajili
yake yule ambaye haisaidiki, na akafuata pumbao lake akahiliki.
Rudi kwenye Sura
17. Na nini hicho ulicho kamata kwa mkono wako wa kulia?
Rudi kwenye Sura
18. Musa akajibu: Hii ni fimbo yangu, najikongojea ninapo kwenda,
na ninachungia kondoo na mbuzi wangu, na inanifaa kwa manufaa mengine,
kama kuwatetea hayawani wangu.
Rudi kwenye Sura
19. Mwenyezi Mungu Subhanahu akamwambia Musa: Itupe hiyo fimbo
chini kwenye ardhi.
Rudi kwenye Sura
20. Musa akaitupa; akashtuka kuiona imegeuka nyoka anakwenda!
Rudi kwenye Sura
21. Akamwogopa. Mwenyezi Mungu akamtuza kwa kumwambia: Mwokote wala
usikhofu, kwani tutamrejesha hali yake kama ya kwanza.
Rudi kwenye Sura
22. Na ingiza mkono wako ndani ya mfuko wa nguo ukiambatisha na ubavu
wako, utatoka mweupe safi bila ya maradhi. Na huo tumekufanyia ni muujiza
wa pili wa Utume wako...
Rudi kwenye Sura
23. Ili tukuonyeshe baadhi ya miujiza yetu mikubwa iwe ni dalili
ya ukweli wa Utume.
Rudi kwenye Sura
24. Nenda kwa Firauni umtake amuamini Mwenyezi Mungu Mmoja wa Pekee.
Kwani yeye Firauni amepindukia mipaka kwa ukafiri wake na ujeuri wake.
Rudi kwenye Sura
25. Musa akamnyenyekea Mola wake Mlezi kwa kumwomba: Nikunjulie kifua
changu, iniondoke ghadhabu, nitimize ujumbe wa Mola wangu Mlezi.
Rudi kwenye Sura
26. Na unisahilishie kazi yangu ili nipate kutimiza waajibu wangu.
Rudi kwenye Sura
27. Na likate fundo la ulimi wangu, nibainishe maneno,
Rudi kwenye Sura
28. Ili watu wafahamu vyema niyasemayo.
Rudi kwenye Sura
29. Na nijaalie mtu wa kuniunga mkono katika watu wangu,
Rudi kwenye Sura
30. Naye ni ndugu yangu Harun.
Rudi kwenye Sura
31. Anizidishe nguvu zangu.
Rudi kwenye Sura
32. Na umshirikishe nami katika kubeba mizigo ya ujumbe na kuifikisha.
Rudi kwenye Sura
33. Ili tukithirishe kukutakasa na yasiyo kuwa laiki yako,
Rudi kwenye Sura
34. Na tuyakariri majina yako mazuri kwa wingi.
Rudi kwenye Sura
35. Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika
Wewe daima unatuangalia sisi, na unayashughulikia mambo
yetu...
Rudi kwenye Sura
36. Mwenyezi Mungu akamwita Mtume wake, Musa, kwa kusema: Nimekwisha
kukubalia uliyo yaomba, na hii ni zawadi tulio kutunukia wewe kwa hisani.
Rudi kwenye Sura
37. Na Sisi tumewahi zamani kukufadhili wewe kwa hisani bila ya kuomba.
Rudi kwenye Sura
38. Tulipo mwongoza mama yako kwa uwongozi wenye nafuu katika maisha
yako.
Rudi kwenye Sura
39. Tulimuamrisha akuweke, na hali wewe ni mtoto mchanga wa kunyonya,
katika kisanduku, na kisha hicho kisanduku akitie katika mto, ili usije
kuuliwa na Firauni, pale alipo kuwa anawauwa watoto wote wanaume wa
Banu Israili. Tukayafanya maji ya mto yachukue kisanduku kile mpaka ufukweni.
Kwa mujibu wa mipango yetu Firauni, adui yangu na wako, akakichukua kile
kisanduku. Nami nikakupa mapenzi ya rehema na ulinzi, ukapendwa na kila
aliye kuona. Ukapata malezi mazuri yaliyo bora chini ya ulinzi wangu.
Rudi kwenye Sura
40. Ewe Musa! Jua ya kwamba zamani Sisi tulikwisha kukufanyia hisani
pale dada yako alipo kuwa anakwenda akiangalia hali yako ulipo kuwa katika
jumba la Firauni, na akawaona wanakutafutia mtu wa kukunyonyesha. Ni yeye
aliye waongoza kwa mama yako, nasi tukakurejesha kwake apate kufurahi kukuona
uhai na umerejea kwake, na asite huzuni na kilio. Na ulipo kua, na ukamuuwa
mtu katika kaumu ya Firauni bila ya kukusudia, tukakuvua kutokana na dhiki
iliyo kupata, na tukakusalimisha na shari yao. Ukenda mpaka Madyana na
huko ukakaa miaka kadhaa wa kadhaa, kisha ukatoka Madyana ukarejea kwa
muda tulio kukadiria kwa ujumbe wako..
Rudi kwenye Sura
41. Na nikakuteua kukupa Wahyi (Ufunuo) na kubeba Utume wangu.
Rudi kwenye Sura
42. Nenda, wewe na nduguyo, nanyi mkisaidiwa na miujiza yangu yenye
kuashiria Unabii na Utume, wala msidhoofike katika kutimiza Ujumbe wangu,
wala msighafilike kunikumbuka na kuniomba msaada.
Rudi kwenye Sura
43. Nenda pamoja na duguyo Harun kwa Firauni. Hakika huyo amepindukia
mipaka katika ukafiri wake na jeuri zake.
Rudi kwenye Sura
44. Mtakeni kwa upole na ulaini aniamini Mimi kwa kutaraji
asaa akakumbuka Imani aliyo isahau, na akaogopa matokeo ya ukafiri wake
na ujeuri wake.
Rudi kwenye Sura
45. Musa na Harun wakanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, wakasema: Ewe
Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tunaogopa huyu Firauni asituvamie kwa madhara,
na akapindukia mpaka katika uovu.
Rudi kwenye Sura
46. Mwenyezi Mungu akawapoza kwa kusema: Msimkhofu Firauni; kwani
Mimi ni pamoja nanyi kukuangalieni na kukulindeni, nayasikia ayasemayo,
na nayaona ayatendayo. Sitomwachia kukudhuruni.
Rudi kwenye Sura
47. Nendeni kwa Firauni, na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume tulio
tumwa kwako na Mola wako Mlezi. Tumekuja kukutaka umuamini Yeye, na uwaache
Wana wa Israili watoke utumwani na adhabuni. Na sisi tumekuletea muujiza
kutokana na Mwenyezi Mungu kuwa ni ushahidi wa ukweli wa haya tunayo kuitia,
na mwenye kuufuata uwongofu atasalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu
na kughadhibika kwake.
Rudi kwenye Sura
48. Na hakika Mwenyezi Mungu ametufunulia sisi kuwa adhabu yake kali
itamshukia anaye tukadhibisha, na akapuuza wito wetu.
Rudi kwenye Sura
49. Firauni kwa ujeuri wake na ujabari wake akasema: Ewe Musa! Ni
nani huyo Mola wenu Mlezi?
Rudi kwenye Sura
50. Musa akamjibu: Mola wetu Mlezi ni yule aliye kipa neema ya umbo
kila kilicho umbwa, akakiumba kwa sura aliyo ipenda Yeye Subhanahu, na
akakielekeza kwa alivyo kiumbia.
"Akasema: Mola wetu Mlezi ni yule aliye kipa kila kitu umbo
lake, kisha akakiongoa." Mwenyezi Mungu Subhanahu amekijaalia kila kiumbe
kina sifa zake makhsusi za kutekeleza kazi yake kilicho umbiwa nacho katika
maisha, kama alivyo pewa hidaya mwanaadamu.
Rudi kwenye Sura
51. Firauni akasema: Je, nini hali ya karne za zamani, na yaliyo
pitikana huko?
Rudi kwenye Sura
52. Musa akasema: Ujuzi wa karne hizo uko kwa Mola wangu Mlezi peke
yake. Hayo yamedhibitiwa katika madaftari ya vitendo vyao. Hapana kitendo
kinacho mpotea asikijue, wala Yeye hasahau.
Rudi kwenye Sura
53. Yeye huyo ndiye Mungu Mwenye kuwafadhili waja wake kwa kuwaumba
na kuwalinda. Amekutengenezeeni ardhi, akaikunjua kwa uwezo wake, na akakupasulieni
njia mnazo pitia, na akakuteremshieni mvua zinazo leta mito, na Yeye Subhanahu
akatoa namna mbali mbali za mimea, inayo khitalifiana kwa rangi, na utamu,
na manufaa. Mingine myeupe, mingine myeusi, myengine mitamu na mingine
michungu..
Rudi kwenye Sura
54. Naye Subhanahu amewaelekeza waja wake wanufaike kwa mimea aliyo
watolea, kwa kula na kulishia mifugo yao na kama hayo. Na akataja kuwa
katika kuumba huku, na kuanzisha huku, na kutumia huku, ni dalili zilizo
wazi za kumwongoa mwenye akili afikie Imani ya kumuamini Mwenyezi Mungu
na kuamini Mitume wake.
Rudi kwenye Sura
55. Na kutokana na udongo wa ardhi hii ndio Mwenyezi Mungu amemuumba
Adam na dhuriya zake. Na humo ndio anawarudisha baada ya kufa kwa ajili
ya kusitiri miili yao. Na kutoka humo atawatoa tena kuwafufua na
kuwalipa kwa waliyo yatenda.
Rudi kwenye Sura
56. Na hakika Sisi kwa kupitia kwa Musa tulimwonyesha Firauni miujiza
ya dhahiri ya kuunga mkono Ujumbe wa Musa na ukweli wake kwa yote aliyo
simulia kutokana na Mwenyezi Mungu na athari ya uwezo wake. Juu ya hayo
Firauni alishikilia ukafiri wake, akayakadhibisha yote hayo, na akakataa
kuyaamini.
Rudi kwenye Sura
57. Firauni akamwambia Musa: Je, umetujia upate kututoa katika nchi
yetu ipate kuwa mikononi mwa watu wako kwa uchawi wako ulio ulia watu?
Rudi kwenye Sura
58. Basi sisi tutauvunja huo uchawi wako. Weka miadi baina yetu na
wewe, tukutane, wala tusikhitalifiane.
Rudi kwenye Sura
59. Musa akawajibu: Miadi yetu ni siku ya Idi yenu mnapo jipamba,
na watu wakusanyike kabla ya adhuhuri siku hiyo, waone yatayo kuwa baina
yetu na nyinyi.
Rudi kwenye Sura
60. Firauni akaondoka na akayashughulikia mambo mwenyewe. Akakusanya
mipango yake, na wakuu wa wachawi, na zana za uchawi. Kisha akahudhuria
na yote hayo kwa mujibu wa miadi.
Rudi kwenye Sura
61. Musa akawaambia kuwahadharisha maangamizo ya Mwenyezi Mungu na
adhabu yake, na akawakataza wasizue uwongo, kwa kumdaia ungu Firauni, na
kuwakadhibisha Mitume wa Mwenyezi Mungu, na kuikataa miujiza. Na akawatisha
kwamba Mwenyezi Mungu atawapatiliza kwa adhabu wakiendelea na hayo, na
akatilia mkazo sana khasara ya mwenye kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
62. Wakatishika na maonyo ya Musa, wakaingia kusemezana wao kwa kwao
wakivutana, na kila mmoja akitoa maoni yake juu ya aliyo yasema Musa.
Rudi kwenye Sura
63. Wakawafikiana kwamba Musa na Harun ni wachawi ambao wanafanya
hila kutaka kuwatoa katika nchi yao, kwa kuwapokonya madaraka, yatoke mikononi
mwao. Na hayo ni kwa uchawi, ili Wana wa Israili wapate ushindi. Na wawaharibie
watu wa Firauni imani yao wanayo iona kuwa ni nzuri!
Rudi kwenye Sura
64. Basi fanyeni njama zenu muwafikiane kitu kimoja cha kumfanyia
Musa, kisha mkusanye wateuliwa, ili watazamaji waingiwe na kitisho kwa
heba yao. Atakaye fuzu leo basi ndio kashinda kweli.
Rudi kwenye Sura
65. Wachawi walimkabili Musa kwa rai moja, na wakamkhiarisha kwa
majivuno na kiburi, waanze wao au aanze yeye kuonyesha ubingwa wake.
Rudi kwenye Sura
66. Musa akasema: Bali anzeni nyinyi! Basi wakazitupa kamba zao na
fimbo zao. Zikamdhihirikia Musa, kwa uchawi, kuwa zimegeuka nyoka zinakwenda.
Rudi kwenye Sura
67. Musa akaingiwa na khofu kwa aliyo yaona kwa kuzugwa na uchawi,
na kuona huenda watu wakadanganyika kwa uchawi wakadhani ni muujiza.
Rudi kwenye Sura
68. Mwenyezi Mungu akamdiriki kwa upole, akamwambia: Usiogope kitu.
Wewe utaushinda tu leo huu upotovu wao.
Rudi kwenye Sura
69. Itupe hiyo fimbo uliyo nayo mkononi mwako wa kulia ivimeze hivyo
walivyo vizua kwa uchawi. Kwani hayo waliyo yaunda ni mazonge tu ya uchawi,
na hakika mchawi popote alipo hawezi kufuzu.
Rudi kwenye Sura
70. Musa akaitupa fimbo yake, na hapo hakika ikageuka kwa uwezo wa
Mwenyezi Mungu ikawa joka kubwa la kutisha. Likavimeza vyote walivyo unda
wao. Wachawi walipo uona muujiza huu mbio mbio wakasujudu kwa kuyakinika
na ukweli wa Musa, huku wakisema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu Mmoja wa Pekee,
Mola Mlezi wa Harun na Musa, Mola Mlezi wa kila kitu.
Rudi kwenye Sura
71. Firauni akasema: Vipi mnamuamini huyu bila ya ruhusa yangu? Hakika
huyu ndiye mkubwa wenu aliye kufunzeni uchawi, wala kitendo chake hichi
si muujiza kama mnavyo dhani! Akawatishia kwa kusema: Kwa yakini nitaikata
mikono yenu na miguu yenu mbali mbali, mkono wa kulia kwa mguu wa kushoto
n.k. Na hakika nitakubandikeni misalabani kwenye vigogo vya mitende. Na
hapo mtajua ni mungu gani kati yetu aliye mkali zaidi na kudumu zaidi katika
mateso - mimi au mungu wa Musa?
Rudi kwenye Sura
72. Wachawi wakasimama imara juu ya Imani yao, na wakajibu vitisho
vya Firauni kwa kauli yao: Sisi hatuendelei na kubakia nawe katika ukafiri
baada ya kwisha tubainikia yaliyo ya kweli katika muujiza wa Musa. Wala
sisi hatutakukhiari wewe kuliko Mungu wa Musa ambaye ndiye aliye tuumba.
Basi wewe tenda utakayo yatenda! Madaraka yako hayapindukii maisha haya
mafupi.
Rudi kwenye Sura
73. Kwani hakika sisi ni wenye kusimama juu ya Imani kumuamini Mola
wetu Mlezi wa Haki, ili atufutie madhambi yetu yaliyo pita, na atusamehe
huku kushughulikia uchawi ulio tulazimisha tujifunze na tuufanye! Na Mola
wetu Mlezi ni Mbora wa malipo kuliko wewe, akit'iiwa; na ufalme wake na
uwezo wake kulipa unadumu zaidi kuliko wako.
Rudi kwenye Sura
74. Hakika anaye kufa katika ukafiri akakutana na Mwenyezi Mungu
hali naye ni mkhalifu basi malipo yake ni Jahannamu. Humo hafi, akapumzika
na adhabu; wala hawi hai wa maisha ya kustarehe na neema.
Rudi kwenye Sura
75. Na mwenye kukutana na Mola wake Mlezi naye yumo katika Imani
na a'mali njema, basi huyo atakuwa na vyeo vya juu.
Rudi kwenye Sura
76. Vyeo hivyo ni Bustani za Peponi za kudumu katika neema. Baina
ya miti yake inapita mito, na humo watadumu milele. Hayo ni malipo ya mwenye
kuitakasa nafsi yake na ukafiri kwa kuijaza Imani, na ut'iifu baada ya
ukafiri na maasi.
Rudi kwenye Sura
77. Tena vikapishana vituko baina ya Firauni na Musa. Mwenyezi Mungu
akampa Wahyi (ufunuo) Mtume wake, Musa, atoke Misri na Wana wa Israil,
wakati wa usiku. Na aipige bahari kwa fimbo yake, utatokea muujiza mwingine,
nao ni kufunguka njia kavu baharini. Naye akamtuliza asiingiwe na khofu
kuwa atakamatwa na Firauni, au kuwa atazama katika maji!
Rudi kwenye Sura
78. Musa akafanya kama alivyo muamrisha Mwenyezi Mungu. Akatoka Firauni
na askari wake nyuma yake, akawakuta kwenye bahari. Akenda nyuma yao kwenye
njia iliyo funguka baharini kwa ajili ya Musa na kaumu yake. Na hapo ukatokea
muujiza; nao ni maji kumfudikiza Firauni na kaumu yake, wakazama wote!
Rudi kwenye Sura
79. Hivi ndivyo Firauni alivyo potea yeye na watu wake wakaacha Haki,
wakateketea wote!
Rudi kwenye Sura
80. Enyi Wana wa Israili! Sisi tulikuokoeni na adui yenu, Firauni,
na tukakuahidini kuokoka kwa ulimi wa Musa kuwa mtafika salama mpaka kwenye
kando ya mlima. Na tulikuteremshieni Manna na Salwa, chakula kizuri, cha
tam-tam na nyama ya ndege nono.
Rudi kwenye Sura
81. Kuleni vitu hivi vizuri tulivyo kuruzukuni bila ya taabu yoyote
kwenu. Wala msidhulumu, wala msiingie kumuasi Mwenyezi Mungu katika maisha
haya ya starehe, isije kukuteremkieni ghadhabu yangu. Kwani anaye teremkiwa
na ghadhabu yangu huporomoka katika matabaka ya chini kabisa ya mateso
ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
82. Na hakika Mimi ni Mtukufu wa Kusamehe kwa anaye acha ukafiri
wake, na akatengeneza Imani, na akatenda yaliyo mema, na akadumu juu ya
hayo mpaka akakutana na Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
83. Musa aliwatangulia watu wake kwenda mlimani, apate kuzungumza
na Mola wake Mlezi. Mwenyezi Mungu akamuuliza sababu ya kufanya kwake haraka
kufika mbele kabla ya kaumu yake.
Rudi kwenye Sura
84. Musa akasema: Hakika watu wangu wapo karibu nami, watanikuta.
Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi nimewatangulia ili kutaka kukuridhisha Wewe.
Rudi kwenye Sura
85. Mwenyezi Mungu akamwambia: Sisi tumewafanyia mtihani watu wako
baada ya wewe kuwawacha. Wakaingia katika fitna; Msamaria amewapotoa!
Rudi kwenye Sura
86. Musa akawarejea watu wake naye kaghadhibika sana, na huzuni ya
uchungu. Akawasemeza watu wake kwa hamaki: Mola wenu Mlezi alikuahidini
kuwa atakuokoeni na atakuongoeni, kwa kuiteremsha Taurati na kupata ushindi
kwa kuingia nchi takatifu. Haujapita muda mrefu wa ahadi ila nyinyi mmekwisha
sahau ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Kwa kitendo chenu kiovu hichi
mnataka ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ikuteremkieni kwa maasi yenu aliyo kuhadharisheni
nayo? Mmesahau ahadi yenu mliyo nipa kuwa mtafuata mwendo wangu, na mtafuata
nyayo zangu?
Rudi kwenye Sura
87. Watu wa Musa wakasema kwa kutafuta udhuru: Hatukwenda kinyume
na ahadi yako kwa khiari yetu. Lakini tulipo toka Misri tulibebeshwa mizigo
ya mapambo ya watu. Kisha tukaona - kwa uzito wake kwetu - tuepukane nayo.
Msamaria akawasha moto katika shimo, tukaitupa hiyo mizigo. Na kadhaalika
Msamaria naye katupa vyombo alivyo kuwa navyo.
Rudi kwenye Sura
88. Basi Msamaria akawaundia ndama aliye na mwili wa dhahabu, ukipita
upepo ndani yake, hutoa sauti, husikilizana kama mlio wa ng'ombe, ili udanganyifu
utimie. Akawaita wamuabudu na wao wakamwitikia. Akasema yeye na wafwasi
wake: Huyu ndiye mungu wenu, na ndiye mungu wa Musa. Akasahau Msamaria
kuwa ni wepesi mtu, akizingatia na kutafuta dalili, kufahamu kuwa ndama
hawezi kuwa mungu.
Rudi kwenye Sura
89. Macho yaliingia upofu yalipo zingatia kuwa huyu ndama ni mungu!
Hawaoni kwani hawarejezei kauli yao? Wala hawezi kuwaondolea madhara yoyote?
Wala kuwaletea manufaa yoyote?
Rudi kwenye Sura
90. Na Harun alikuwa pamoja nao ilipo tokea fitna hii. Naye kabla
ya kurejea Musa a.s. alikwisha waambia: Enyi watu wangu! Nyinyi mmeingia
katika fitna ya Msamaria kwa upotovu huu! Hakika Mungu wenu wa Haki ni
Mwenyezi Mungu, Arrahman, Mwingi wa Rehema, wala hana mwenginewe.
Nifuateni mimi kwa haya ninayo kunasihini, na ishikeni rai yangu kwa kuachilia
mbali upotovu huu.
Rudi kwenye Sura
91. Wakasema: Sisi tutaendelea kumuabudu huyu ndama mpaka atakapo
rejea Musa kwetu!
Rudi kwenye Sura
92. Musa kwa kuathirika na aliyo yajua na kuyaona ya watu wake, alisema:
Ewe Harun! Sababu gani iliyo kukataza hata usiwazuie na upotovu ulipo kwisha
waona wameuingia?
Rudi kwenye Sura
93. Na usisimame msimamo wangu kwa kuwanasihi kama nilivyo chukua
ahadi kwako? Hukunifuata katika ahadi niliyo ahidiana nawe, au umevunja
amri yangu?
Rudi kwenye Sura
94. Harun akamwambia Musa: Ewe mwana wa mama yangu! Usinichukulie
papara kwa hasira zako, wala usizishike ndevu zangu na kichwa changu. Hakika
mimi nilikhofu lau ningeli wafanyia ukali, wakafarikiana makundi na mapande
usije ukaniambia: Umewagawanya Wana wa Israil, wala hukuyafuata niliyo
chukua ahadi kwako.
Rudi kwenye Sura
95. Musa a.s. akamwambia Msamaria: Jambo hili jambo gani la khatari
ambalo laonekana ni balaa ulilo lizua?
Rudi kwenye Sura
96. Msamaria akamwambia Musa: Nimejua ustadi wa ufundi na mbinu zake
wasizo zijua Wana wa Israil; nikawaundia sanamu la ndama lenye kutoa sauti,
na nikachukua sehemu ya Taurati nikaitia ndani ya ndama, kuwazuga watu.
Basi ndio hivyo, nafsi yangu imenizaini nifanye hayo niliyo yafanya.
Rudi kwenye Sura
97. Musa akamwambia Msamaria: Tokana nasi, na uwe mbali nasi. Na
jaza yako duniani uwe unatanga tanga ovyo, na watu wakikukimbia, mpaka
usiwe na makhusiano na yeyote, na asiwepo ndudu ya mtu kukukaribia, wala
wewe usimkaribie mtu. Na hakika adhabu yako kesho Akhera umewekewa kwa
ahadi huwezi kuikimbia! Musa tena akimbeua huyo
mungu wake kwa kusema: Tazama sasa nini tunalo mfanyia huyu mungu wako
ulio kaa wewe ukimuabudu, na kwa sababu yake ukawafitini watu! Tutamuunguza,
na kisha tutamtawanya baharini apotelee mbali!
Rudi kwenye Sura
98. Musa akaingia kutimiza aliyo yasema, na kisha baada ya mazingatio
hayo aliwaelekea Wana wa Israili kuwaambia: Hakika Mungu wenu ni Mmoja.
Yeye ndiye ambaye hapana anaye abudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye. Na ujuzi
wake umeenea kila kitu kilicho kuwa na kitakacho kuwa.
Rudi kwenye Sura
99. Ewe Mtume! Kama tulivyo kusimulia khabari za Musa, tunakupa khabari
za kweli za kaumu zilizo tangulia. Na Sisi tumekuteremshia wewe Kitabu
kutoka kwetu, ndani yake yamo mawaidha kwako na kwa umma wako, ya kukufaeni
katika Dini yenu na dunia yenu.
Rudi kwenye Sura
100. Mwenye kuacha kukiamini Kitabu hicho na kufuata uwongofu wake,
basi amepotea katika maisha yake, na Siku ya Kiyama atakuja naye amebeba
madhambi ya aliyo yatenda, na atalipwa kwa adhabu kali.
Rudi kwenye Sura
101. Na atadumu katika adhabu hii, na ni mzigo muovu kweli huo Siku
ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
102. Ewe Mtume! Watajie umma wako Siku ambayo tutawaamrisha Malaika
walipulize baragumu la kuwafufua watu kutoka makaburini, na kuwaita hapo
pa mkutano, na tutapo wachunga wakhalifu kwendea ufundoni na nyuso zao
rangi ya buluu kwa khofu na kitisho.
Rudi kwenye Sura
103. Wakinong'onezana wao kwa wao katika udhalili na kubabaika jinsi
walivyo ona maisha ya dunia ni mafupi, hata waone kama kwamba hawajapata
kustarehe nayo, na wala hawakukaa humo duniani ila siku kumi tu!
Rudi kwenye Sura
104. Wala si kama hiyo minong'ono yao ndiyo haisikilizani, kwani
Sisi tunajua vyema wao wananong'onezana nini, na tunayajua vyema wanayo
yasema wale walio kuwa mahodari zaidi kulinganisha hisiya zao kwa dunia,
kuwa hayo maisha ya duniani ni kama kwamba hayakutimia hata siku moja.
Rudi kwenye Sura
105. Ewe Mtume! Wanakuuliza hao wanao kanya kufufuliwa, nini hali
ya milima Siku ya Kiyama hiyo unayo itaja? Wajibu: Mwenyezi Mungu ataivuruga
kama mchanga, kisha ataipeperusha kwa upepo kama vumbi!
Rudi kwenye Sura
106. Na pahala pao baada ya kwisha vurugika milima patakuwa sawa
sawa laini.
Rudi kwenye Sura
107. Hutoona kwenye ardhi kudidimia wala kunyanyuka, kama kwamba
haikupata kukaliwa kabla yake.
Rudi kwenye Sura
108. Siku ya Kiyama watu wakisha toka makaburini, watamfuata mwenye
kuwaita mpaka pahala pa mkutano nao wamesalimu amri. Hawezi yeyote kati
yao kuelekea kulia wala kushoto. Sauti zote zimenyenyekea kwa utulivu na
kitisho kwa utukufu wake Arrahmani, Mwingi wa Rehema. Basi husikii ila
sauti ya chini kabisa ya mnong'ono.
Rudi kwenye Sura
109. Siku hiyo hapana uombezi unao faa kitu, ila wa aliye pata hishima
ya Mwenyezi Mungu kwa kuruhusiwa naye na kuridhiwa aseme. Na hapana uombezi
wa yeyote utao faa ila wa aliye pata ruhusa ya Mwenyezi Mungu kuombea,
na akawa ni Muumini, na Mwenyezi Mungu akaridhia kauli yake kwa Tawhidi
na Imani.
Rudi kwenye Sura
110. Na Mwenyezi Mungu, aliye tukuka shani yake, anayajua mambo yao
waliyo yakadimisha katika dunia yao na waliyo yaakhirisha. Yeye Subhanahu
anawapangia mambo yao kwa mujibu wa ujuzi wake. Na wao hawaijui mipango
yake na hikima zake.
Rudi kwenye Sura
111. Nyuso zitadhalilika Siku hii, na zitamnyenyekea Mwenyezi Mungu
Aliye Hai asiye kufa, Mwenye kusimamia kupanga mambo yote ya viumbe vyake.
Na amepoteza uwokofu na thawabu Siku ya Akhera mwenye kuidhulumu nafsi
yake duniani, na akamshirikisha Mola wake Mlezi.
Rudi kwenye Sura
112. Na mwenye kutenda mambo ya ut'iifu, naye akawa anayasaidiki
aliyo yaleta Muhammad, s.a.w. huyo hana khofu ya kuzidishiwa makosa yake
au kupunguziwa mema yake.
Rudi kwenye Sura
113. Na mfano wa maelezo haya ya haki yaliyo kwisha tangulia katika
Sura hii, ya kumtukuza Mwenyezi Mungu, na hadithi ya Musa na khabari za
Kiyama, Mwenyezi Mungu ameyateremsha katika Kitabu hichi cha Qur'ani
kwa lugha ya Kiarabu, na ameeleza mara kwa mara kwa njia za kuonya
ili watu waweze kutanabahi waache maasi, na Qur'ani iwazindue upya kwa
kuwapa mawaidha na mazingatio.
Rudi kwenye Sura
114. Basi ametukuka na dhana dhana, na amejitenga na kushabihiana
na viumbe, huyo Mfalme ambaye anahitajiwa na watawala na wanao tawaliwa,
Mwenye haki katika Uungu wake na Utukufu wake. Na wewe, ewe Muhammad, usiifanyie
haraka Qur'ani kabla Malaika hajakusomea. Na sema: Ewe Mola wangu Mlezi,
nizidishe ilimu kwa Qur'ani na maana zake.
Rudi kwenye Sura
115. Ewe Mtume! Sisi tulimuusia Adam tangu mwanzo, asende kinyume
na amri yetu, akasahau ahadi yetu akenda kinyume. Na hatukumwona tangu
mwanzo wake kuwa ana azma baraabara, na ukakamavu wa kutosha asiingiliwe
na Shetani akamtia wasiwasi katika nafsi yake.
Rudi kwenye Sura
116. Ewe Mtume! Na kumbuka pale Mwenyezi Mungu alipo waamrisha Malaika
wamtukuze Adam kwa njia aliyo itaka Yeye Subhanahu, na wakafuata. Lakini
Iblisi, naye alikuwa pamoja nao, alikuwa jini, akenda kinyume akakataa,
akatolewa akafukuzwa!
Rudi kwenye Sura
117. Mwenyezi Mungu akamsemeza Adam kwa kumwambia: Hakika huyu Shetani
aliye kwenda kinyume na amri yetu ya kukuadhimisha wewe ni adui yako wewe
na Hawa, mkeo. Basi tahadhari na uchochezi wake kukuingizeni katika maasi,
isije kuwa ndio sababu ya kutoka kwenu kwenye Bustani hii, ukaja pata taabu,
ewe Adam, katika maisha baada ya kutoka kwenye Bustani.
Rudi kwenye Sura
118. Sisi tunakudhaminia mahitaji ya maisha yako katika Bustani.
Humo hutopata njaa wala hutakuwa uchi.
Rudi kwenye Sura
119. Na wala hutopata kiu, wala hutopata joto la jua, kama wanavyo
pata wanao sumbuka nje ya Bustani.
Rudi kwenye Sura
120. Shetani akamfanyia hila akimnong'oneza katika roho yake, kumraghibisha
yeye na mkewe, waule ule mti walio katazwa, akiwaambia: Ewe Adam! Mimi
nitakuonyesha mti huo, ataye kula basi ataishi milele, na atapata ufalme
usio na mwisho.
Rudi kwenye Sura
121. Akamwonyesha mti ulio katazwa. Adam na mkewe wakakhadaika kwa
kudanganywa na Iblisi, na wakasahau makatazo ya Mwenyezi Mungu, na wakaula.
Utupu wao ukadhihiri, kuwa ni malipo ya tamaa yao, mpaka wakasahau wakaingia
katika ukhalifu. Wakawa wakikata majani ya miti ya Bustani ile ili wajisitiri
utupu wao. Ikawa Adam kamkhaalifu Mola wake Mlezi. Hayo yalikuwa
kabla hajapewa Unabii. Akayakosa maisha ya milele aliyo kuwa anayatamani,
na yakaharibika maisha yake.
Rudi kwenye Sura
122. Kisha Mwenyezi Mungu alimteuwa ampe Utume, na akaipokea toba
yake, na akamwongoa atake udhuru na aombe msamaha.
Rudi kwenye Sura
123. Mwenyezi Mungu aliwaamrisha Adam na mkewe watoke kwenye Bustani,
wateremke kwenye ardhi, naye Subhanahu akawaambia kwamba utakuwapo uadui
baina ya vizazi vyao, na kwamba Yeye Subhanahu atawaongoa kwa uwongofu
na uwongozi. Mwenye kufuata uwongofu wa Mwenyezi Mungu hatoingia katika
maasi duniani, wala hatoteseka kwa adhabu.
Rudi kwenye Sura
124. Na mwenye kujiepusha na uwongofu wa Mwenyezi Mungu na ut'iifu
wake, basi ataishi maisha yasiyo na starehe, hatokinai na chochote anacho
pewa na Mwenyezi Mungu, wala hatokuwa radhi na hukumu ya Mwenyezi Mungu
na kudra yake. Mpaka ikija Siku ya Kiyama atakuja kwenye mkutano wa hisabu
atashikwa kwa madhambi yake, naye hana hoja ya kutoa, kama alivyo kuwa
duniani ni kipofu hazioni ishara zote za Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
125. Na kwenye mkutano huo atamuuliza Mola wake Mlezi kwa fazaa:
Ewe Mola wangu Mlezi! Vipi umenisahaulisha hoja, hata nisiweze kujitolea
udhuru, na umenisimamisha kama kipofu, na hali mimi duniani nilikuwa naona
kila kitu, nikishindana na kutetea?
Rudi kwenye Sura
126. (Naye atajibiwa:) Mambo kwako ndivyo kama yalivyo. Zimekujilia
dalili zetu, na Mitume wetu duniani; yote hayo ukayasahau, na ukajitia
upofu, na hukuamini. Na leo basi kadhaalika unaachwa umesahauliwa umo katika
adhabu na fedheha.
Rudi kwenye Sura
127. Na mfano wa malipo haya mabaya tunamlipa duniani mwenye kutenda
maasi, na akamkadhibisha Mwenyezi Mungu na ishara zake. Na hakika adhabu
za Akhera zina uchungu mkali zaidi, na zinadumu zaidi kuliko za dunia.
Rudi kwenye Sura
128. Vipi wanajitia upofu na ishara za Mwenyezi Mungu, na wanajua
kuwa tumezihiliki kaumu nyingi zilizo tangulia kwa sababu ya ukafiri wao,
nao hawakuwaidhika kwao juu ya kuwa wao wanapita wanatembea kwenye
majumba yao na maskani zao, na wanayaona magofu yao na athari ya adhabu
zilizo wapata? Hakika mambo kama hayo peke yake ni mawaidha kwa watu wenye
akili za kufahamu.
Rudi kwenye Sura
129. Na lau kuwa haikutangulia hukumu ya Mola wako Mlezi ya kuwaakhirishia
adhabu mpaka siku ya miadi maalumu, nayo ni Siku ya Kiyama, basi adhabu
lazima ingeli wapata hapa hapa duniani kama ilivyo kwisha wapata makafiri
wa karne zilizo pita.
Rudi kwenye Sura
130. Ewe Mtume! Vumilia hayo wayasemayo ya kukukadhibisha na kuukejeli
Utume wako, na mtakase Mola wako Mlezi na yote yasiyo mfalia kwa kumsifu,
na kumuabudu Yeye pekee daima, na khasa kabla ya jua kuchomoza, na kabla
halijachwa. Na mtakase, umuabudu katika saa za usiku, na katika ncha za
mchana kwa kusali, ili yadumu mawasiliano yako na Mwenyezi Mungu, upate
kutua kwa hayo uliyo nayo, na uridhike kwa uliyo kadiriwa.
Rudi kwenye Sura
131. Wala usivuke mipaka kwa kuangalia yale mambo ya starehe ya namna
mbali mbali tuliyo waonjesha makafiri. Kwani starehe hizi ni uzuri na pambo
la duniani tu analo wafanyia mtihani kwayo Mwenyezi Mungu waja wake. Na
Mwenyezi Mungu anakuwekea wewe Akhera yaliyo bora zaidi na yenye kudumu
zaidi kuliko starehe hizi.
Rudi kwenye Sura
132. Na waelekeze ahli zako washike Sala kwa nyakati zake. Kwani
Sala ni kiungo chenye nguvu kabisa cha kuwaunganisha na Mwenyezi Mungu,
na kudumu kuishika Sala kwa nyakati zake ndio ukamilifu. Sisi hatukulazimishi
ujiruzuku nafsi yako, bali ni Sisi ndio kazi yetu kukuruzuku. Na hakika
mwisho wa kusifiwa duniani na Akhera ni wa watu wema na wenye kumcha Mungu.
Rudi kwenye Sura
133. Na makafiri katika inadi yao wanasema: Kwa nini Muhammad hatuletei
dalili inayo toka kwa Mola wake Mlezi inayo tulazimisha sisi kumuamini?
Na vipi wao wanaipinga Qur'ani, nayo imewajia hali imekusanya yaliyomo
katika Vitabu vilivyo tangulia katika khabari za watu walio pita, na maangamizo
yao kwa sababu ya kuwakadhibisha Mitume? Na Muhammad si wa kwanza katika
hayo!
Rudi kwenye Sura
134. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu ange wafanyia haraka kuwahiliki makafiri
hawa, kabla ya kumtuma Muhammad kwao, wange toa udhuru Siku ya Kiyama kwa
kusema: Ewe Mola wetu Mlezi! Kwa nini hukutuletea Mtume duniani mwenye
ishara tumfuate, kabla hujatuteremshia adhabu na hizaya Akhera? Lakini
sasa hawana udhuru wowote baada ya kutumiwa Mtume.
Rudi kwenye Sura
135. Ewe Mtume! Waambie hawa wenye inda: Hakika sisi sote tunangojea
yatavyo kwenda mambo yetu na yenu. Na mtajua kwa hakika nani katika makundi
mawili walio watu wa Dini ya Haki, na wenye kuongoka kwa uwongofu wa Mwenyezi
Mungu.
Rudi kwenye Sura