1. Alif Lam Ra (A.L.R.)...Hizi ni harufi zilizo anziwa
Sura hii kuwa ni ishara kuwa Qur'ani ni muujiza juu ya kuwa imeundwa kwa
hizi hizi harufi zinazo tamkwa, na pia ni kuwazindua watu wanapo isikiliza
inapo somwa Qur'ani Tukufu kuwa ni Kitabu chenye shani kuu. Zimeteremshwa
Aya zake zimeshikana, madhubuti, hazina ndani yake upotovu, wala ubabaishi,
na zimetungwa kwa njia isiyo na dosari, iwazi, na yenye kubainisha. Kisha
hukumu zake zikapambanuliwa. Na Kitabu hichi juu ya utukufu wake ulio nao
nafsi yake, kina utukufu zaidi kwa kuwa kimetokana na Mwenyezi Mungu ambaye
anajua kila kitu, na Yeye Subhanahu anapanga mambo yote kwa pahala pake.
Rudi kwenye Sura
2. Ewe Nabii! Waongoze watu kwa hii Qur'ani, na uwaambie: Msimuabudu
yeyote ila Mwenyezi Mungu tu. Na hakika mimi nimetumwa kutoka kwake ili
nikuonyeni msikufuru ikakupateni adhabu yake, na nikupeni bishara njema
kuwa mkiamini na mkat'ii, basi mtapata malipo yake..
Rudi kwenye Sura
3. Mnyenyekeeni Mwenyezi Mungu na huku mnamwomba akusameheni dhambi
zenu. Kisha rejeeni kwake kwa kumuabudu kwa ikhlasi na vitendo vyema, ili
apate kukustarehesheni starehe nzuri duniani mpaka utakapo kufikieni muda
wenu uliyo kadiriwa, na apewe Akhera kila mwenye vitendo vyema malipo
ya kazi yake na fadhila yake. Na pindi mkiyaacha haya ninayo kuitieni kwayo
itakuwa mtajiletea adhabu. Na mimi nakukhofieni adhabu hii katika Siku
Kubwa watakapo fufuliwa watu wote, na kutokea vitisho vikubwa kabisa!
Rudi kwenye Sura
4. Marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu peke yake hapa duniani na Siku
ya Kiyama, atakapo kufufueni kutoka makaburini mwenu, ili akulipeni kwa
vitendo vyenu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu. Kwani Yeye ndiye aliye kamilika
uwezo wake, na hashindwi na kitu chochote.
Rudi kwenye Sura
5. Watu wanafunika vifua vyao kujaribu kuficha yanayo wapitia humo.
Wanajitahidi kuficha, wakidai makusudio ya hayo ni kumficha Mwenyezi Mungu
asijue hisiya za nyoyo zao! Hebu nawajue watu hawa kuwa hata wanapo kwenda
kulala vitandani mwao, na wakavaa nguo zao za kulalia, na wakajisitiri
na kiza cha usiku na usingizi, na kujifunika vifua, basi hapana shaka yoyote
kuwa Mwenyezi Mungu anawajua, wakificha au wakitangaza. Kwani Yeye anayajua
yaliyomo vifuani, na yanayo funikwa ndani yake.
Rudi kwenye Sura
6. Na wajue watu hawa kuwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na neema zake,
na ujuzi wake, umeenea kila kitu. Basi hapana mnyama anaye furukuta katika
ardhi ila Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake kesha mtengenezea riziki yake
inayo wafikiana naye katika hali mbali mbali. Naye anajua anakaa wapi katika
hali ya uhai wake, na pahala atapo wekwa wakati wa kufa kwake! Kila
kitu katika hayo kimekwisha dhibitiwa kwake Subhanahu katika Kitabu chenye
kuweka wazi hali zote ziliomo.
Rudi kwenye Sura
7. Na Mwenyezi Mungu kaziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yake
katika siku sita. Na kabla ya hapo palikuwa hapana chochote zaidi kuliko
ulimwengu wa maji, na juu yake A'rshi, Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu ameumba ulimwengu wote huu ili adhihirishe kwa kukujaribuni
hali zenu, enyi watu, atokeze kati yenu anaye mkubali Mwenyezi Mungu kwa
ut'iifu na vitendo vyema, na nani anaye yaacha hayo...Na juu ya uwezo huu
wa kuumba, ukiwaambia kwa yakini: Nyinyi mtafufuliwa kutoka makaburini
kwenu, na kwamba wao wameumbwa ili wafe na wafufuliwe, wao mbio mbio wanakurudi
kwa mkazo kuwa haya mliyo kuja nayo hayana ukweli wowote! Wala hayo si
chochote ila ni kama uchawi ulio wazi wa kuchezea akili tu.
Rudi kwenye Sura
8. Ilivyo kuwa hikima yetu ni kuakhirisha adhabu ya ukafiri wao hapa
duniani mpaka wakati tuliyo uweka, nao ni Siku ya Kiyama, wao husema kwa
kejeli: Nini kinacho mzuia hivi sasa? Na ailete hiyo adhabu ikiwa
anasema kweli katika hiyo ahadi yake! Basi nawajue hao kwamba adhabu itakuja
tu bila ya muhali. Na itapo wajia hawatapata kuokoka, na itawazunguka kwa
sababu ya kejeli zao na kutaka kuvunja hishima.
Rudi kwenye Sura
9. Na katika tabia za binaadamu ni kujizamisha mwenyewe katika hali
aliyo nayo. Basi tukimpa baadhi ya neema na rehema, kama vile afya nzuri,
na ukunjufu wa riziki, kisha baadae tukamwondolea neema hizo, kwa mujibu
wa mipango yetu, yeye hupita mipaka katika kukata tamaa kuwa neema hiyo
haitorudi tena; na akapita mipaka katika kuzikufuru neema nyengine ambazo
bado angali anastarehe nazo.
Rudi kwenye Sura
10. Na tukimpa neema baada ya shida aliyo kuwa nayo yeye husema:
Shida zangu zote zimekwisha niondokea, wala hazitarudi tena! Na hayo humpelekea
upeo wa kufurahikia starehe za dunia, na kujifakhirisha bila ya kiasi.
Moyo wake huwa umeshughulika, usimshukuru Mola wake Mlezi! Hii ndiyo hali
ya binaadamu wengi, wanababaika baina ya kukata tamaa na kujitapa!
Rudi kwenye Sura
11. Na aibu hii hawaachi kuwa nayo ila wale wanao subiri wakati wa
dhiki, na wakatenda mema wakati wa faraji na shida. Hawa watasamehewa dhambi
zao, na watapata ujira mkubwa kwa vitendo vyao vyema.
Rudi kwenye Sura
12. Ewe Nabii! Usijaribu kutaka kuwaridhi washirikina, kwani hao
hawaamini. Na huenda ukijaribu kutaka kuwaridhi ukaacha kusoma baadhi ya
uliyo letewa Wahyi, katika yale wasiyo penda wao kuyasikia, kama vile kudharauliwa
baadhi ya miungu yao, kwa kukhofu kuwa wasije wakakejeli! Na huenda pengine
ukahisi dhiki unapo wasomea, kwa kuwa wao wanataka Mwenyezi Mungu akuteremshie
khazina ustarehe nayo kama wafalme, au waje nawe malaika watwambie ukweli
wake! Basi, ewe Nabii! Usizibali inadi zao. Kwani wewe si chochote ila
ni mwonyaji na mhadharishaji wa adhabu za Mwenyezi Mungu kwa anaye kwenda
kinyume na amri yake. Nawe hayo umefanya, basi jipumzishe nafsi yako nao.
Na jua kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuangalia na kulinda kila kitu. Naye
atawafanyia kama wanavyo stahiki.
Rudi kwenye Sura
13. Katika Qur'ani ipo Ishara inayo thibitisha ukweli wako. Basi
wao wakisema, kuwa hii umeitunga wewe na umemzulia Mwenyezi Mungu, wewe
waambie: Ikiwa Qur'ani hii imetokana na mwanaadamu, basi yamkinika mwanaadamu
mwengine kuleta mfano wake. Na nyinyi ni mafasihi kuliko wote. Basi leteni
Sura kumi kama hii mbali mbali, na mtakeni msaada yeyote mnaye weza kumtaka,
katika watu na majini, kama hakika mnasema kweli katika hayo madai yenu
kuwa haya ni maneno ya binaadamu.
Qur'ani si muujiza tu katika maandishi yake, bali ndani yake mna
hadithi za kweli, na ilimu mbali mbali za sayansi za uumbaji zilizo ashiriwa,
na hazikuwa zikijuulikana wakati wa kuteremka kwake, na pia katika hukumu
ziliomo ndani yake.
Rudi kwenye Sura
14. Mkishindwa, na wakashindwa mlio wataka msaada, kuleta mfano wake
hii wa kuzua, basi jueni kuwa Qur'ani haikuteremshwa ila kwa kuambatana
na ujuzi wake Mwenyezi Mungu. Ilimu yake haijui mtu ila Yeye. Na jueni
kuwa hapana mungu ila Allah, Mwenyezi Mungu tu. Hapana anaye tenda kazi
yake. Basi kuweni Waislamu baada ya kwisha thibiti hoja hizi juu yenu,
kama nyinyi mnataka Haki.
Rudi kwenye Sura
15. Wenye kutaka uhai wa duniani, na kustarehea ladha zake na pumbao
lake, tutawapa matunda ya vitendo vyao bila ya nuksani.
Rudi kwenye Sura
16. Hao ambao hima yao ni kushughulikia dunia tu, Akhera hawana lao
jambo ila adhabu ya Motoni, na kuharibikiwa na yote waliyo yafanya duniani,
kwa sababu hawakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hayo wayatendayo
pia yatakuwa yameharibika vile vile, kwani kitendo kisicho leta mafanikio
ya daima ni kama kwamba hakikupata kuweko.
Rudi kwenye Sura
17. Je, anaye kuwa anakwenda katika maisha yake kwa uangalifu na
uwongofu kutokana na Mola wake Mlezi, na anaitaka Haki kwa kuifanyia ikhlasi,
pamoja naye anaye shahidi anaye mshuhudia kuwa kweli katoka kwa Mwenyezi
Mungu, naye shahidi huyo ni Qur'ani, na shahidi wa kabla yake ni Kitabu
cha Musa alicho kiteremsha Mwenyezi Mungu kiwe ni uwongozi wa kufuatwa
kwa aliyo yaleta, na ni rehema kwa wenye kukifuata, je, huyo ni sawa sawa
na anaye kwenda katika maisha yake katika giza na upofu, hashughulikii
ila starehe za duniani tu na pumbao lake? Hao walio tajwa mwanzo ndio wale
ambao Mwenyezi Mungu ameyatia nuru macho yao. Wanamuamini Nabii huyu, na
Kitabu alicho teremshiwa. Na wenye kumkataa wakakusanyika na kujiunga dhidi
yake, basi Moto ndio pahali pa miadi yao Siku ya Kiyama. Ewe Nabii! Usiwe
na shaka na hii Qur'ani (1). Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi.
Haingii upotovu. Lakini watu wengi wanapotezwa na matamanio, basi hawaamini
kama iwapasavyo.
(1) Mwenyezi Mungu amemuamrisha Nabii s.a.w. asitie shaka, si kwa
kuwa yawezekana kuwa yeye awe na shaka, lakini ni kuashiria kuwa walio
kuwa duni yake Nabii wajilinde wasiache shaka ikaingia nyoyoni mwao.
Rudi kwenye Sura
18. Hapana walio zidi kujidhulumu nafsi zao na wakajitenga mbali
na Haki kuliko wale wanao tunga uwongo, na kisha wakamnasibishia Mwenyezi
Mungu. Hakika watu hawa Siku ya Kiyama watadhihirishwa mbele ya Mola wao
Mlezi awahisabie kwa yale maovu waliyo yatenda. Mashahidi miongoni mwa
Malaika, na Manabii, na wengineo, watasema: Hawa ndio walio tenda makosa
maovu kabisa na dhulma kwa mintarafu ya Muumba wao! Hapana shaka laana
ya Mwenyezi Mungu itawapata hao kwa kuwa ni wenye kudhulumu.
Rudi kwenye Sura
19. Hawa ndio wanawageuza watu wasiifuate Dini ya Mwenyezi Mungu,
na wanawazuia. Nayo hiyo ndiyo Njia yake Iliyo Nyooka. Na wanataka Njia
hii iwafikiane na matamanio yao na pumbao lao, kwa hivyo yende upogo. Hao
wanaikanya Akhera, na yaliyomo ndani ya kulipwa thawabu Muumini na kuadhibiwa
kafiri.
Rudi kwenye Sura
20. Hao makafiri hawana nguvu za kumshinda Mwenyezi Mungu asiwatie
nguvuni duniani akawaadhibu; na hawana wasaidizi wa kuweza kuwakinga na
adhabu yake pindi Mwenyezi Mungu akitaka kuwaletea hiyo katika Akhera,
hata ikiwa mardufu ya ile ambayo wangeli ipata duniani, ingeli kuwa Mwenyezi
Mungu anataka iwafikie. Kwa sababu hao wamechukia kuisikia Qur'ani, na
kuzingatia Ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu. Wamekuwa kama kwamba
hawakuwa wakiweza kusikia wala kuona.
Rudi kwenye Sura
21. Hao makafiri hawapati faida yoyote katika kumuabudu asiye kuwa
Mwenyezi Mungu! Bali wamejikhasiri nafsi zao, na huko Akhera huo uwongo
walio kuwa wakiuzua, na madai ya upotovu, na miungu ya uwongo waliyo kuwa
wakiiunda, na wakadai kuwa hiyo ati ikiwafaa au itawaombea - yote hayo
yatawapotea. Kwa sababu hakika Siku ya Kiyama ndiyo Siku ya hakika,
ambayo haina udanganyifu wala uzushi.
Rudi kwenye Sura
22. Kweli, hakika wao Siku ya Akhera ndio wenye kukhasiri kuliko
watu wote!
Rudi kwenye Sura
23. Bila ya shaka wale wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake,
na wakatenda a'mali njema, na nyoyo zao zikanyenyekea na zikatua kuikubali
hukumu ya Mola wao Mlezi, hao ndio wanao stahiki kuingia Peponi na kudumu
humo milele.
Rudi kwenye Sura
24. Mfano wa makundi mawili hayo, ya Waumini na makafiri, ni kama
kipofu anaye kwenda bila ya uwongofu na kiziwi asiye sikia uwongozi wa
kuokoka, na kundi la pili ni kama mwenye macho anaye iona njia ya kheri
na uokofu, na mwenye masikio makali anaye sikia kila lenye manufaa naye.
Makundi mawili hayo hayawezi kuwa sawa katika hali yao na kuishia kwao!
Basi, enyi watu, hamfikiri yaliyo baina yenu ya khitilafu ya utambuzi na
ukafiri, na khitilafu baina ya baat'ili na Haki, mkawa mbali na njia ya
upotovu, na mkaishika Njia Iliyo Nyooka?
Rudi kwenye Sura
25. Na kama tulivyo kutuma kwa watu wako uwaonye na uwabashirie kheri,
wakakukabili baadhi yao kwa inadi na upinzani, kadhaalika tulimtuma Nuhu
kwa watu wake, akawaambia: Mimi nakuhadharisheni na adhabu ya Mwenyezi
Mungu, na nakuonyesheni njia ya kuokoka.
Rudi kwenye Sura
26. Akawaambia: Mimi nilitakalo kwenu ni kuwa msimuabudu ila Mwenyezi
Mungu tu, kwa sababu nakukhofieni, mkimuabudu mwenginewe au mkimshirikisha
pamoja naye wenginewe katika kumuabudu, isije ikakufikieni siku ya adhabu
yake yenye machungu makali.
Rudi kwenye Sura
27. Wakuu wa kaumu yake wakasema: Sisi hatukuoni wewe ila kuwa ni
mtu kama sisi. Hapana lolote linalo kufanya uwe namna ya peke yako, au
uwe na ubora wa kutupelekea tukuamini kuwa wewe ni Mtume utokaye kwa Mwenyezi
Mungu! Na wala hatuwaoni hao walio kufuata ila ni watu wa t'abaka la chini
miongoni mwetu! Wala hatukuoneni nyinyi kuwa ni bora kuliko sisi! Bali
sisi tunaitakidi kuwa nyinyi ni waongo tu katika hayo mnayo dai.
Rudi kwenye Sura
28. Nuhu akasema: Enyi watu! Hebu nambieni, ikiwa mimi naungwa mkono
na hoja zilizo wazi kutokana na Mola wangu Mlezi, naye akanipa kwa rehema
yake Unabii na Utume, na nuru yake ikafichikana kwenu, na kughurika kwenu
kwa cheo na mali kukakutieni upofu msizione, basi je, itafaa tukulazimisheni
mziamini hoja kwa nguvu na karaha?
Rudi kwenye Sura
29. Enyi watu! Mimi sitaki mali kwa kufikisha Ujumbe wa Mola wangu
Mlezi, bali nataraji malipo yangu kwa Mwenyezi Mungu. Wala mimi siwafukuzi
kwenye baraza yangu na kuingiana nami walio muamini Mola wao Mlezi, kwa
sababu ya kuwa nyinyi mnawadharau tu! Kwani wao watakuja kukutana na Mola
wao Mlezi Siku ya Kiyama na watanishitaki kwake ikiwa nimewafukuza kwa
ajili ya ufakiri wao. Lakini mimi nakuoneni nyinyi ni watu msio jua nini
kinacho watukuza viumbe mbele ya Mwenyezi Mungu! Ni utajiri na cheo kama
mnavyo dai, au kufuata Haki na kufanya kheri?
Rudi kwenye Sura
30. Enyi watu! Hapana yeyote awezaye kunikinga na adhabu ya Mwenyezi
Mungu nikiwafukuza hao hali nao ni wenye kumuamini Yeye. Je, bado mngali
mnashikilia ujinga wenu? Hamkumbuki basi kuwa hawa watu wanaye Mola wao
Mlezi wa kuwalipia?
Rudi kwenye Sura
31. Wala sikwambiini kuwa kwa sababu mimi ni Mtume, basi ninazo khazina
za riziki ya Mwenyezi Mungu, nitumie nitakavyo, na kwa hivyo nimfanye anaye
nifuata tajiri! Wala sikwambiini kuwa mimi najua mambo ya ghaibu,
na kwa hivyo nikupeni khabari yale yaliyo mkhusu Mwenyezi Mungu tu kuyajua,
kwa kuwa hapana mja yeyote anaye yajua! Wala mimi sikwambiini kuwa mimi
ni Malaika, na kwa hivyo mnirudi kwa kauli yenu: Huyu si chochote ila mwanaadamu
tu! Wala siwasemi wale mnao wadharau kwamba Mwenyezi Mungu hatowapa kheri
yoyote kwa kutaka kuridhi myatakayo! Kwani Mwenyezi Mungu peke yake ndiye
anaye jua ikhlasi iliomo katika nafsi zao!..Mimi nikisema myatakayo nitakuwa
katika wenye kujidhulumu na kudhulumu wengineo.
Rudi kwenye Sura
32. Wakasema: Ewe Nuhu! Umebishana nasi ili tukuamini, na umezidisha
kutujadili mpaka tumechoka. Sasa hatuyastahamilii tena maneno yako. Basi,
hebu, tuletee hiyo adhabu unayo tutishia, kama wewe kweli unayo yasema
kwamba Mwenyezi Mungu atatuadhibu tukito kuamini!
Rudi kwenye Sura
33. Nuhu akasema: Mambo haya yamo mikononi mwa Mwenyezi Mungu pekee.
Yeye ndiye atakuleteeni alitakalo kwa hikima yake. Wala nyinyi hamwezi
kuikimbia adhabu yake itakapo kuja. Kwani Yeye, Subhanahu, haemewi na chochote
katika ardhi wala katika mbingu.
Rudi kwenye Sura
34. Wala nasaha yangu haitakufaeni kitu kwa kuwa tu nakutakieni kheri,
ikiwa Mwenyezi Mungu anakutakeni mpotee kwa mujibu wa ilimu yake na uwezo
wake kwa kuharibika nyoyo zenu, hata zimekuwa haziikubali Haki! Yeye Subhanahu
ndiye Mola wenu Mlezi, naye atakurejesheni kwake Siku ya Kiyama. Na atakulipeni
kwa mlivyo kuwa mkitenda.
Rudi kwenye Sura
35. Nini msimamo wa washirikina kukhusu hadithi hizi za kweli? Watasema
kazizua? Wakisema hivyo, basi waambie: Ikiwa nimezizua kama mnavyo dai,
basi hilo ni kosa kubwa; ni juu yangu mimi tu dhambi zake! Na ikiwa nimesema
kweli, basi nyinyi ndio wenye makosa, na mimi sikhusiki na matokeo ya makosa
yenu.
Rudi kwenye Sura
36. Mwenyezi Mungu akamletea wahyi Nuhu akamwambia: Hatakusadiki
wala hataifuata Haki yeyote katika kaumu yako baada ya sasa, isipo kuwa
wale walio kwisha tangulia kukuamini kabla ya hayo. Basi ewe Nuhu! Usihuzunike
kwa sababu ya waliyo kuwa wakikutendea, ya kukukadhibisha, na kukuudhi.
Kwani Sisi tutawalipiza karibu.
Rudi kwenye Sura
37. Tukamwambia: Tengeneza chombo chini ya uangalizi na ulinzi wetu,
wala usinisemeze kwa ajili (1) ya hawa madhaalimu, kwa sababu nilikwisha
itikia ombi lako, na nimekwisha amrisha wateketezwe kwa kuzamishwa.
(1) Tazama Aya 27 Surat Al Muuminun (23).
Rudi kwenye Sura
38. Nuhu akaingia kujenga chombo. Kila wakipita waongozi wa makafiri
katika kaumu yake wakimfanyia maskhara, kwa ujinga wao na kuwa hawajui
nini anacho kusudia! Nuhu akawaambia: Mkitufanyia maskhara sisi kwa kutojua
kwenu ukweli wa ahadi ya Mwenyezi Mungu, basi hakika sisi pia tutakufanyieni
maskhara, kama mnavyo tufanyia sisi.
Rudi kwenye Sura
39. Mtakuja jua nani kati yetu atakaye fikiwa na adhabu ya kumdhalilisha,
na atafikiwa na adhabu ya kudumu milele katika Akhera!
Rudi kwenye Sura
40. Hata ulipo wadia wakati wa amri yetu ya kuwahilikisha, yalikuja
maji kwa nguvu yakifoka na kutoa mapovu, kama maji yanavyo tokota juu ya
moto. Tukamwambia Nuhu: Wapakie nawe katika hiyo Safina kutoka kila namna
ya wanyama dume na jike. Na pia wapakie humo ahali zako, yaani watu wa
nyumbani kwako, isipokuwa ilio kwisha pita juu yake hukumu yetu ya kumteketeza.
Na pia kadhaalika wapakie humo katika watu wako walio amini. Na hao hawakuwa
ila idadi chache tu.
Rudi kwenye Sura
41. Na baada ya kwisha liweka tayari jahazi Nuhu aliwaambia watu
wake: Pandeni humo kwa kujipigia feli njema kwa kulitaja jina la Mwenyezi
Mungu Mtukufu (kupiga BISMILLAHI) wakati wa kwenda na wakati wa kusimama,
na wakati wa kuingia na wakati wa kutoka humo. Na muombeni Mwenyezi Mungu
akusameheni kwa madhambi mlio tenda, na akurehemuni. Kwani maghfira na
rehema ni katika shani yake Subhanahu wa Taa'la.
Rudi kwenye Sura
42. Wakaingia katika Safina, ikawa inakwenda katika mawimbi makubwa
makubwa kama milima! Na ilipo anza kwenda Nuhu alimkumbuka mwanawe kwa
huruma ya baba, naye alikuwa yuko mbali kajitenga na wito wa baba yake.
Akamwita: Ewe mwanangu! Panda nasi, wala usiwe katika wanao ikataa Dini
ya Mwenyezi Mungu Mtukufu!
Rudi kwenye Sura
43. Mtoto hakumt'ii baba yake mwenye kumwonea huruma! Akasema: Nitakwenda
pahala pa kunilinda na maji! Baba, mwenye kujua hukumu ya Mwenyezi Mungu
kwa wenye kuasi, alisema: Ewe mwanangu! Hakipatikani cha kuzuia hukumu
ya Mwenyezi Mungu ya kuwazamisha walio dhulumu! Basi yule kijana
akapotea kwenye macho ya baba yake anaye mnasihi nyuma ya wimbi lilio
panda juu; akawa pamoja na wakanushao, walio zama, walio teketea.
Rudi kwenye Sura
44. Walipo kwisha hiliki makafiri kwa kuzamishwa, ikaja amri ya Mwenyezi
Mungu ya maumbile. Ikasemwa kwa hukumu ya uumbaji: Ewe ardhi! Yameze maji
yako, na wewe mbingu! Sita na kuteremsha maji. Yakaondoka maji kwenye ardhi,
wala kisiongezeke chochote kutoka mbinguni. Hukumu ya Mwenyezi Mungu ya
kuhiliki ikamalizika. Jahazi likatua na likasimama juu ya mlima uitwao
Al Juudiy.(1) Na Mwenyezi Mungu akawahukumia walio dhulumu kwa kuwatenga
na rehema yake. Ikasemwa: Wateketee kaumu walio dhulumu kwa sababu ya dhulma
zao.
(1) Mlima huo uko Mosal (kaskazini mwa Iraq na kusini ya Turki)
Ulikuwa maarufu hapo kale.
Rudi kwenye Sura
45. Huruma ilimshika Nuhu moyoni mwake kwa ajili ya mwanawe. Akamwomba
Mola Mlezi wake kwa unyenyekevu na kuona huruma, akasema: Ewe Muumba
wangu, uliye nianzisha nami sijawa chochote! Hakika huyu mwanangu ni kipande
cha nafsi yangu, naye ni katika ahali zangu. Na Wewe umeahidi kuwa utawaokoa
ahali zangu, na ahadi yako ni ya kweli, madhubuti, lazima iwe. Na hapana
muadilifu kama Wewe! Kwani Wewe ndiye Mjuzi kushinda wote, na Wewe ni mwingi
wa hikima kuliko wote wenye kuhukumu!
Rudi kwenye Sura
46. Allah Subhanahu akasema: Hakika huyo mwanao si katika ahali zako.
Kwani yeye kwa ukafiri wake na mwendo wake pamoja na makafiri amekata makhusiano
baina yako na yeye. Naye ametenda vitendo visio vyema. Kwa hivyo amekuwa
si katika wewe. Nawe usitake jambo usilo lijua, kuwa ndilo au silo. Wala
usende kufuata huruma zako. Na mimi nakuongoza njia ya Haki ili usiwe katika
wajinga ukasahau kwa huruma zako Hakika iliyo thibiti!
Rudi kwenye Sura
47. Nuhu akasema: Ewe Muumba wangu, uliye tawala mambo yangu yote!
Mimi nakuangukia Wewe. Sitakuomba nisicho kijua hakika yake. Nawe nisamehe
kwa niliyo yasema kutokana na huruma zangu. Kama hukunipa fadhila ya msamaha
wako, na ukanirehemu kwa rehema yako, nitakuwa katika makundi ya walio
khasiri.
Rudi kwenye Sura
48. Akaambiwa kwa wahyi: Ewe Nuhu! Teremka nchi kavu kutokana na
hiyo Safina ya uwokovu, salama usalimina, kwa amani itokanayo kwa Mwenyezi
Mungu Mtukufu, na baraka nyingi zitokazo kwa Mwenyezi Mungu juu yako na
juu ya hao walio pamoja nawe, ambao watakuja kuwa mataifa mbali mbali baada
yako. Na baadhi yao watapata baraka ya Imani na ut'iifu, na baadhi yao
watakuwa watu wanao itaka starehe ya dunia, na watapata starehe yake bila
ya kuit'ii Haki. Kisha Siku ya Kiyama itawapata adhabu chungu na kali.
Rudi kwenye Sura
49. Hizo ni simulizi tulizo kusimulia wewe, ewe Nabii, juu ya Nuhu
na kaumu yake. Hizo ni khabari za ghaibu ambazo hazijui ila Mwenyezi Mungu.
Wewe wala watu wako hamkuwa mkizijua kwa namna hii, na kwa tafsili hii,
kabla ya wahyi huu. Basi wewe vumilia maudhi ya watu wako, kama walivyo
subiri Manabii wa kabla yako. Kwani mwisho wako ni kufuzu kama ulivyo kuwa
mwisho wao hao. Na Mwisho mwema daima ni wa wale wanao iogopa adhabu ya
Mwenyezi Mungu kwa kuamini na kutenda vitendo vyema.
Rudi kwenye Sura
50. Na Sisi tuliwapelekea Kaumu ya A'adi wa mwanzo ndugu yao katika
kabila yao, naye ni huyo Hud. Akawaambia: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi
Mungu pekee. Kwani hamna anaye stahiki kuabudiwa isipo kuwa Yeye. Na nyinyi
si cho chote ila mnazua uwongo tu kudai kuwa Mwenyezi Mungu ana washirika
wanao stahiki nao kuabudiwa ili wawe waombezi wenu kwa Mwenyezi Mungu!
Tazama maelezo ya ki-ilimu juu ya Aya 65 katika Sura Al-Aa'raaf.
(7).
Rudi kwenye Sura
51. Enyi watu! Kwa nasaha hii sitaki kwenu kulipwa kwa cheo,
au utawala, au mali. Kwani ujira wangu uko kwa Mwenyezi Mungu aliye niumba.
Wala haikufaliini nyinyi mkawa mmechotwa akili zenu kwa kughafilika msitambue
linalo kufaeni na linalo kudhuruni!
Rudi kwenye Sura
52. Enyi watu! Mtakeni aliye kuumbeni akusameheni madhambi yaliyo
kwisha tangulia. Kisha rejeeni kwake. Hapana shaka mkifanya hayo atakuleteeni
mvua nyingi mfululizo, basi zitaongezeka kheri zenu, na zitazidi nguvu
zenu juu ya nguvu mnazo jivunia sasa! Wala msiyawache haya ninayo kuiteni
muyafwate, mkashikilia maasi ambayo yatakuangamizeni kwenye hilaki.
Rudi kwenye Sura
53. Wakasema: Ewe Hud! Hukutuletea hoja yoyote iliyo wazi ya kuonyesha
ukweli wa hayo unayo tuitia. Wala sisi hatutoacha kuabudu miungu yetu kwa
kufuata kauli yako tu! Je, tuwawache hao, na hali sisi hatukusadiki wewe?
Rudi kwenye Sura
54. Na hatuna la kusema juu ya msimamo wako nasi ila kuwa mmojapo
katika miungu yetu imekupatiliza kwa shari, ndio maana ukawa unaropokwa
maneno haya! Naye akasema naye ameshikilia Imani yake na anawapinga: Ninasema,
na namshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa haya niyasemayo, na nakushuhudisheni
nyinyi, ya kwamba mimi najitenga mbali kabisa na maradhi ya ushirikina
mliyo nayo. Kwani nyinyi ni wagonjwa!
Rudi kwenye Sura
55. Wala mimi sikujalini, wala siwajali miungu yenu hiyo ambayo mnadai
kuwa imenipatiliza kwa uovu! Basi saidianeni, nyinyi na miungu yenu, kunifanyia
vitimbi. Kisha wala msiakhirishe hiyo adhabu yenu kwangu hata dakika moja,
kama mnaweza!
Rudi kwenye Sura
56. Mimi namtegemea Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye Mwenye mamlaka
juu ya mambo yangu na mambo yenu. Wala hashindwi na kitu chochote katika
kupinga vitimbi vyenu. Na Yeye ni Muweza wa kila kitu. Basi hapana kiumbe
yoyote ila yuko chini ya madaraka yake, na Yeye ndiye Mwenye kumsarifu
atakavyo. Basi Yeye hashindwi na kunilinda na maudhi yenu, wala hashindwi
kukuangamizeni! Hapana shaka vitendo vya Mola wangu Mlezi vinafuata njia
ya Haki na Uadilifu katika ufalme wake. Yeye huwanusuru Waumini watendao
mema, na huwahizi makafiri waharibifu.
Rudi kwenye Sura
57. Na mkiukataa wito wangu, basi kukataa kwenu hakunidhuru kitu.
Na mwisho mbaya utakuwa wenu. Kwani mimi nimekwisha kufikishieni ujumbe
aliyo nituma Mwenyezi Mungu kwenu. Na sina jukumu ila kufikisha tu. Na
Mwenyezi Mungu atakuangamizeni nyinyi, na awalete watu wengine wachukue
majumba yenu na mali yenu! Na nyinyi hamumdhuru kitu chochote Yeye kwa
kukataa kwenu kumuabudu! Hakika Mola wangu Mlezi ni Mlinzi wa kila kitu,
Mwenye kujua kila kitu. Basi hapana katika mtendalo linalo fichikana kwake,
wala haghafiliki kukutieni nguvuni.
Rudi kwenye Sura
58. Na ilipo kuja amri yetu ya kuwahiliki qaumu ya A'adi tulimwokoa
Hud, na walio amini pamoja naye, kutokana na adhabu ya upepo mkali ulio
wahiliki, na tukawaokoa na adhabu kubwa ya duniani na Akhera. Na hayo ni
kwa sababu ya rehema yetu juu yao, kwa kuwawezesha kushika Imani.
Rudi kwenye Sura
59. Hao, basi, ndio kina A'adi! Walizikataa hoja zote zilizo wazi,
na wakawaasi Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, kwa vile kumuasi yule Mtume
wao aliye tumwa kwao, na vile kumt'ii kila aliye kuwa jeuri na mwingi wa
inda katika maraisi wao na wakubwa wao!
Rudi kwenye Sura
60. Kwa hivyo wakastahiki kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na Malaika,
na watu wote kupata laana ya hapa duniani, na laana ya kuwafuatia Siku
ya Kiyama. Basi na atanabahi kila mwenye kuijua khabari ya A'adi kwamba
hao kina A'adi waliikataa neema ya Muumba wao kwao, wala hawakuishukuru
kwa kumuamini Yeye peke yake. Kwa hivyo ndio wakawa wanastahili wafukuzwe
kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu, na wateremshiwe maangamizo makali! Hebu
zingatieni maangamizo yao kwa kumkadhibisha Hud!
Rudi kwenye Sura
61. Na kwa kina Thamud tulimtuma mmoja wao ambaye amefungana
nao kwa nasaba na mapenzi, naye ni Saleh. Akawaambia: Enyi watu wangu!
Muabuduni Mwenyezi Mungu pekee. Nyinyi hamna anaye stahiki kuabudiwa isipo
kuwa Yeye. Yeye ndiye aliye kuumbeni kwenye ardhi, na akakuwekeni muiimarishe,
na muitoe mavuno ya kukufaeni kheri yake...Basi mwombeni Yeye apate kukusameheni
makosa yenu yaliyo kwisha tangulia. Kisha mrejee kwake na majuto kwa mlivyo
muasi, na mkubali kumtii, kila mnapo tumbukia katika madhambi. Hakika Mola
wangu Mlezi yupo karibu kwa rehema, na Mwenye kupokea maombi kwa mwenye
kutaka msamaha na kumwomba.
Tazama maelezo ya ki-ilimu juu ya Aya 73 katika Sura Al-Aa'raaf
(7).
Rudi kwenye Sura
62. Wakasema: Ewe Saleh! Hakika wewe ulikuwa kwetu mtu wa kutarajiwa
mema, na kupendwa, na kutukuzwa katika nyoyo zetu, kabla ya haya unayo
tuitia! Hivyo unatutaka tuache ibada waliyo kuwa wakiabudu baba zetu na
tuliyo izoea sisi na wao? Hakika sisi tuna shaka na huo wito wako wa kumuabudu
Mwenyezi Mungu Mmoja. Haya ni mambo ya kukutilia shaka na dhana mbovu wewe
na huo wito wako!
Rudi kwenye Sura
63. Akasema: Enyi watu wangu! Hebu nambieni: ikiwa mimi kwa haya
ninayo kukuitieni kwayo nina ujuzi nayo vilivyo, na nina hoja za kunitia
nguvu kutoka kwa Mola wangu Mlezi, na ikawa Mola wangu Mlezi kanipa mimi
na nyinyi rehema itokayo kwake, nayo ni Unabii na Utume, vipi basi nende
kinyume na amri yake, na nimuasi kwa kutofikisha ujumbe wake kwa sababu
ya kukusikilizeni nyinyi? Na nani wa kuninusuru na kunisaidia kuikinga
adhabu yake nikimuasi Yeye? Nyinyi hamwezi kuninusuru na kunikinga
na adhabu yake. Basi hamtonizidishia ila kupotea na kuingia khasarani ni
kikut'iini nyinyi, na nikamuasi Mola wangu na Mola wenu Mlezi.
Rudi kwenye Sura
64. Na enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu; amemfanya
awe ni alama kwenu ya kushuhudia ukweli wa haya ninayo kuleteeni. Kwani
huyu ni namna mbali na hao mlio wazoea. Basi mwachieni ale katika ardhi
ya Mwenyezi, kwani yeye ni ngamia wake, na ardhi ni yake. Wala msimfikishie
uovu wowote wa kumdhuru. Kwani mkifanya hivyo Mwenyezi Mungu atakuangamizeni
kwa adhabu iliyo karibu.
Rudi kwenye Sura
65. Na wao wasiisikie nasaha yake, wala wasimkubalie. Kiburi chao
na dharau yao iliwapelekea kumuuwa yule ngamia. Basi yeye akawaambia: Stareheni
na maisha yenu ya kilimwengu katika miji yenu muda wa siku tatu. Kisha
baadae itakujieni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ni ahadi ya kweli wala
haina kinyume, wala haina uwongo ndani yake.
Rudi kwenye Sura
66. Ilipo kuja adhabu yetu tulimwokoa Saleh na wale walio amini pamoja
naye kutokana na maangamizo kwa rehema iliyo toka kwetu khasa. Na tukawaokoa
na hizaya na fedheha ya siku ya maangamizo ya Thamud. Hakika Mola wako
Mlezi, ewe Nabii, ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda. Basi tuwa ukitegemea
nguvu zake, na ushindi wake, na msaada wake, na nusra yake.
Rudi kwenye Sura
67. Ukelele uliwatwaa kina Thamud kwa nguvu zake, na tetemeko lake,
na ngurumo lake, kwa kuwa hao walijidhulumu wenyewe kwa ukafiri wao na
uadui. Kulipo pambazuka wakawa katika majumba yao kimya, wamejinyoosha
kifudifudi, maiti, hawatweti!
Rudi kwenye Sura
68. Mambo yao yakawaishia, na alama zao zikaondoka katika majumba
yao. Wakawa kama kwamba hawajapata kuwamo humo. Hali yao ni ya kumzindua
kila mwenye akili azingatie, na ajue kuwa hao kaumu ya Thamud walizikanya
Ishara za aliye waumba!! Na kwa sababu ya hayo ndio wakaangamizwa na wakatengwa
mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
69. Na Sisi tuliwatuma Malaika kwa Ibrahim wampe bishara njema yeye
na mkewe kuwa watapata mwana. Waliwasalimu kwa kauli ya: Salama! Naye akarejesha
amkio lao kwa kusema: Salama! Upesi upesi akenda kuwatengezea ndama aliye
nona wa kuchoma ili wale.
Rudi kwenye Sura
70. Alipoona kuwa hawanyooshi mikono yao kama ada ya wageni akawatilia
shaka kuwa hawa si wageni wa kawaida, na akahisi kuwa hawa ni Malaika.
Ikamjia khofu kuwa isije kuwa kuja kwao ni kwa jambo ambalo halikumpendeza
Mwenyezi Mungu, au kuwaadhibu watu wake. Wakasema, nao walijua athari ya
ile khofu katika nafsi yake: Usiogope! Hakika sisi tumetumwa kuwahiliki
kaumu Lut'.
Rudi kwenye Sura
71. Na mkewe alikuwa kasimama karibu akisikia maneno yao. Akacheka
kwa furaha ya kuwa mwenyewe Lut', ambaye ni mtoto wa ndugu wa mumewe, atasalimika.
Basi Sisi tulimbashiria kwa ndimi za wale Malaika kuwa atamzalia mumewe
Ibrahimu mtoto mwanamume ataye itwa Is-haq, na huyo mtoto ataishi, na baadae
Is-haq atampata Yaaqub.
Rudi kwenye Sura
72. Mke wa Ibrahim alipiga ukelele kwa kustaajabu: Ajabu gani hii,
jamani! Nizae mimi kikongwe, na huyu mume wangu mnamuona kesha kuwa kizee
kabisa! Kama huyu hapati mwana tena. Hakika haya ninayo yasikia ni mambo
ya ajabu. Vipi vikongwe viwili kama mimi na mume wangu wazae tena?
Rudi kwenye Sura
73. Malaika wakamwambia: Unastaajabu nyinyi wawili kupata mwana kwa
ajili ya uzee wenu? Haya yanatokana na amri ya Mwenyezi Mungu asiye shindwa
na chochote. Hiyo ndiyo rehema ya Mwenyezi Mungu. Na neema zake ni nyingi
juu yenu wa ukoo wa Nabii. Basi hapana la ajabu nyinyi kupewa wasio pewa
wenginewe. Mwenye kutenda hayo hakika anastahiki kuhimidiwa, ni mwingi
wa hisani na ukarimu na upaji.
Rudi kwenye Sura
74. Zilipo mtoka khofu Ibrahim, na akaisikia bishara ya kumfurahisha
ya kupata mwana, ikamwingia huruma, akaanza kujadiliana na wale wajumbe
katika shauri la kuangamizwa kaumu Lut'.
Rudi kwenye Sura
75. Hakika Ibrahim ni mpole mno, hapendelei mapatilizo ya kwa haraka,
mwingi wa kuungulika na kuona uchungu kwa shida zinao wapata watu, tena
yeye ni mwenye kutubu na kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa yale ayapendayo
na kuyaridhi. Basi ule upole wake, na rehema zake, na huruma zake ndizo
zilizo mpelekea kubishana kule kwa kutaraji kuwa asaa Mwenyezi Mungu akawaondolea
adhabu watu wa Lut', na wao wapate kutubu na kurejea kwake.
Rudi kwenye Sura
76. Malaika wakasema: Ewe Ibrahim! Wachilia mbali haya majadiliano,
na kuwatakia rehema watu hawa. Kwani amri ya Mola wako Mlezi ya kuwaangamiza
imekwisha kuja! Hapana budi kuwa adhabu itawashukia, na wala haitarudishwa
kwa majadiliano au bila ya majadiliano.
Rudi kwenye Sura
77. Walipo kuja wajumbe wetu, hao Malaika, kwa Lut' kwa sura ya vijana
wazuri, Lut' aliungulika na akaudhika. Alihisi unyonge hana nguvu za kuwahami
na hao watu wake, akawaonea dhiki kwa kuwaogopea ufisadi wa kaumu yake!
Akasema: Hii leo ni siku ya karaha kubwa na machungu!
Rudi kwenye Sura
78. Watu wake wakajua kuwa wamekuja wale wageni, wakamwendea mbio
mbio. Na kabla ya hayo ilikuwa kazi yao kufanya huo uchafu wao na kutenda
maovu! Lut' akawaambia: Enyi watu wangu! Hawa binti zangu, waoeni. Hao
ni safi zaidi kwenu kuliko kwenda kufanya uchafu kwa wanaume! Mwogopeni
Mwenyezi Mungu, na jilindeni nafsi zenu na adhabu yake; na msinifedhehi
na mkanidharaulisha kwa kuwavamia wageni wangu! Basi hivyo hamna kati yenu
hata mtu mmoja mwenye rai iliyo sawa, mwenye akili iliyo ongoka, akakuzuieni
na maasi na akakukatazeni maovu?
Rudi kwenye Sura
79. Wakasema: Wajua vyema ewe Lut', kuwa sisi hatuna haki ya kuwaoa
binti zako, wala hatuwataki. Na wewe hapana shaka unajua tukitakacho tulipo
kujia kwa haraka.
Rudi kwenye Sura
80. Lut' akasema: Laiti ningeli kuwa nina nguvu au nina nguzo yenye
nguvu ya kutegemea, msimamo wangu juu yenu ungeli kuwa mwengine, na ningeli
weza kuwalinda wageni wangu nikakuzueni msiwafanye mambo mabaya.
Rudi kwenye Sura
81. Malaika wale wakamwambia, na wao ukweli wao ulikwisha dhihiri:
Ewe Lut'! Usikhofu wala usihuzunike! Sisi ni wajumbe wa Mola wako
Mlezi, wala si binaadamu kama tuonekanavyo kwako na kwa hawa kaumu yako.
Wala wao hawa hawatakufikishia shari yoyote ya kukuudhi au kukudhuru. Basi
toka wewe na ahali zako usiku ukisha zagaa. Mtoke mji huu, wala yeyote
katika nyinyi asigeuke kutazama nyuma, asije akaona vitisho vya adhabu
naye akasibiwa na shari yake! Lakini mkeo ambaye amekukhuni, yeye hatokuwa
pamoja na watao toka nawe. Yeye lazima yampate yatao wapata hawa watu.
Na miadi ya kuangamia kwao ni asubuhi, na miadi hiyo ni karibu. Basi usitie
khofu.
Rudi kwenye Sura
82. Ulipo fika wakati wa adhabu tuliyo ikadiria na tukaitolea hukumu,
tuliupindua mji ule walio kuwa wakiishi ndani kaumu Lut' juu chini. Na
tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo ulio okwa Motoni hata ukawa changarawe!
Rudi kwenye Sura
83. Wakawa wanaangukiwa na hayo mawe mfululizo kuwa ni adhabu inayo
toka kwa Mola wako Mlezi, ewe Nabii! Na hayo si mbali kumfikilia kila mwenye
kudhulumu katika kaumu yako.
Rudi kwenye Sura
84. Na kwa watu wa Madyana (1) tulimtuma ndugu yao kwa nasaba na
mapenzi na kuoneana huruma, Shua'ib. Aliwaambia: Enyi watu wangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu Mmoja peke yake. Nyinyi hamna anaye stahiki kuabudiwa isipo
kuwa Yeye. Wala msipunguze vipimo na mizani mnapo wauzia watu vitu vya
kupimwa kwa pishi au kwa mizani. Hakika mimi nakuoneni ni watu wa kutarajiwa
kheri kwa kumshukuru na kumt'ii Mwenyezi Mungu, na kuwapa watu haki zao
kaamili. Na mimi nakukhofieni ikiwa hamtaishukuru kheri ya Mwenyezi Mungu
na hamuitikii amri yake, isije ikakuteremkieni adhabu ya siku msio weza
kuvikimbia vitisho vyake, kwa kuwa hivyo huwazinga wanao adhibiwa wasipate
njia ya kusalimika.
(1) Hizi Aya mbili zinakataza kupunja kwa vipimo na mizani
kwa kuwa ni ukhalifu unao stahiki kupewa adhabu na kuaziriwa. Makosa haya
ya kupunja na udanganyifu pia yanahisabiwa ni ukhalifu hata katika kanuni
za kutungwa za dikrii. Na katika Qur'ani tukufu ni moja katika njia
ya kulinda mali. Nchi ya Madyana ipo baina ya kaskazi ya Hijazi na kusini
ya Sham. Na hii ilikuwa imejaa miti. Ikiitwa Al-aykah,(yaani Machakani).
Na Mwenyezi Mungu aliwapelekea adhabu kwa sababu ya uasi wao.
Rudi kwenye Sura
85. Enyi watu wangu! Toeni vipimo na mizani sawa na kwa uadilifu
pale mnapo uza, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye ujeuri na
fisadi katika nchi kwa kwiba mali ya watu na kupokonya, au kuvamia wapita
njia, mkifanya fisadi ndio chumo la maisha yenu
Rudi kwenye Sura
86. Kidogo kinacho kuzidieni katika mali ya halali aliyo kuruzukuni
Mwenyezi Mungu ni bora kwenu kuliko chungu ya mali mnayo yakusanya kwa
njia ya haramu, ikiwa nyinyi kweli mnamuamini Mwenyezi Mungu, na mnaepuka
aliyo kukatazeni. Basi jipimeni nafsi zenu, na mumuangalie Mola wenu Mlezi.
Mimi si mlinzi wenu wa kuchunga vitendo vyenu na kukupimieni.
Rudi kwenye Sura
87. Wakasema kwa maskhara na kukejeli: Ewe Shua'ibu! Hivyo ni hizo
sala zako ndizo zinazo kuamrisha kutushikilia tuache kuabudu masanamu waliyo
kuwa wakiyaabudu baba zetu, na tuache kustarehe kutumia mali zetu kama
tunavyoona wenyewe kuwa ni maslaha yetu? Hakika huo ndio mwisho wa upumbavu
na utovu wa akili, wala haulingani na akili na rai njema tunazo kujua unazo;
kwani wewe ni maarufu kwa ustahamilivu wako na uwongofu wako!
Rudi kwenye Sura
88. Yeye akasema: Enyi watu! Hebu nambieni, ikiwa mimi nina hoja
iliyo wazi na ya yakini kutokana na Mola Mlezi wangu, naye akaniruzuku
kwa fadhila yake riziki iliyo njema, je ingeli nifalia mimi nifiche aliyo
niamrisha kukufikishieni, nako ni kuacha kuabudu masanamu, na kukutakeni
mtimize vipimo na mizani, na muache kufanya uharibifu katika nchi? Na mimi
si kama ninapenda kwenda kutenda haya ninayo kukatazeni, wala sitaki kwa
mawaidha yangu, na nasaha zangu, na amri zangu, na makatazo yangu, ila
kutengeneza kwa kadri ya ukomo wa uwezo wangu, na juhudi yangu, kama nilivyo
jaaliwa. Wala sina uwezo wa kuifikilia haki ila kwa msaada wa Mwenyezi
Mungu na kuungwa mkono naye, na ninamtegemea Yeye peke yake. Na kwake Yeye
tu ndio ninarejea.
Rudi kwenye Sura
89. Na enyi watu! Hizi khitilafu ziliopo baina yangu na nyinyi zisikupelekeeni
kufanya inda na mkashikilia ukafiri, hata yakakupateni yaliyo wapata kaumu
ya Nuhu, na kaumu ya Hud, na kaumu ya Saleh. Na wala zama na pahala pa
kaumu Lut' na maangamizo yao si mbali nanyi! Basi zingatieni yasikusibuni
yaliyo wasibu hao.
Rudi kwenye Sura
90. Na mtakeni Mwenyezi Mungu akusameheni madhambi yenu, na rejeeni
kwake kwa majuto mkiomba maghfira kila mtendapo dhambi. Hakika Mola wangu
Mlezi ni mwingi wa rehema, ni mwenye mapenzi. Huwasamehe wenye kutubu,
na anawapenda wenye kurejea kwake.
Rudi kwenye Sura
91. Wakasema: Ewe Shua'ibu! Mengi unayo yasema sisi hatuyafahamu!
Na sisi tunakuhakikishia kuwa sisi tunakuona wewe dhaifu, huna nguvu zozote
za kujitetea, wala kutukinaisha tukitaka kukutenda unayo yachukia. Na lau
kuwa si kwa wema wetu kwa jamaa zako, kwani wao wanafuata dini yetu, tungeli
kuulia mbali kwa kukupiga mawe. Na wewe si mtukufu kati yetu hata tukutukuze,
na tukuhishimu, na tukukirimu na tuache kukuuwa kwa mawe! Ni wema tunao
wafanyia jamaa zako tu ndio unao tuzuia tusikuuwe.
Rudi kwenye Sura
92. Akasema Shua'ibu: Enyi watu wangu! Hivyo jamaa zangu ndio
wanastahiki kufanyiwa wema kuliko Mwenyezi Mungu. Wao mnawakumbuka, na
mkataka kunifanyia jamala mimi kwa ajili yao. Lakini Yeye mmemsahau
na mkamfanya kama kitu kilicho tupiliwa mbali nyuma ya migongo yenu!
Hakika Mola Mlezi wangu ni Mwenye kuyazunguka yote mnayo yafanya kwa kuyajua,
hapana linalo fichikana kwake katika vitendo vyenu, na atakuhisabieni kwavyo
hata ikiwa nyinyi mtasahau.
Rudi kwenye Sura
93. Enyi watu wangu! Tendeni mnayo weza nyinyi kuyatenda. Kama hamsikilizi
nasaha zangu, mimi naendelea kushikilia kutenda kinyume na vitendo vyenu.
Na hapo tutakuja jua ni nani kati yetu ataye fikiwa na adhabu ya kumfedhehi
na kumdhalilisha, na ni nani kati yetu ni mwongo - mimi ninaye kuonyeni
na adhabu, au nyinyi mnao nionya kunifukuza katika mji wenu? Ngojeeni nini
litatokea, na mimi nangojea pamoja nanyi.
Rudi kwenye Sura
94. Ilipo kuja amri yetu ya kuwaadhibu na kuwaangamiza, tulimwokoa
Shua'ibu na walio amini pamoja naye wasipate adhabu na maangamizo. Kuokoka
kwao kulikuwa kutokana na rehema iliyo tokana nasi. Ukelele uliwatwaa watu
wa Madyana, na tetemeko la kuteketeza, wakapambaukiwa wamekwisha jifia
katika majumba yao, wamelala kifudifudi, hawatukusiki hata kidogo!
Rudi kwenye Sura
95. Mambo yakawishia, na athari zao zikapotea. Wakawa kama kwamba
hawajapata kukaa katika majumba yao! Hali yao ikatamka ya kumzindua kila
mwenye akili apate kuzingatia! Zingatia basi maangamizo ya Madyana, na
vipi walivyo baidika na rehema ya Mwenyezi Mungu kama walivyo baidika watu
wa Thamud kabla yao!
Rudi kwenye Sura
96. Na hakika tulimtuma Musa na tukamuunga mkono kwa miujiza yenye
kuonyesha ukweli wake, na uthibitisho ulio wazi wenye nguvu juu ya nafsi.
Rudi kwenye Sura
97. Tulimtuma ende kwa Firauni na wakuu katika watu wake. Firauni
akamkanya Musa na akawaamrisha watu wake wamfuate yeye Firauni katika ukafiri
wake. Wakenda kinyume na amri ya Musa! Wala amri ya Firauni haikuwa ni
nyoofu yenye matokea mema hata istahiki kufuatwa.
Rudi kwenye Sura
98. Siku ya Kiyama Firauni atawatangulia kaumu yake kama alivyo watangulia
hapa duniani, na atawaingiza Motoni wakipenda wasipende, wataingia humo
wakizigugumia adhabu zake! Na uovu ulioje wa maji
yanayo tokota watayo kunywa humo kutafuta kuondoa kiu; maji
hayo yatakatakata matumbo yao!
Rudi kwenye Sura
99. Na wao katika dunia hii iliwafuata laana ya Mwenyezi Mungu, na
ya Malaika, na ya watu. Na Siku ya Kiyama kadhaalika itawafuata laana hiyo
vile vile, kwani hiyo ndiyo zawadi yao. Zawadi hiyo ni ovu ya kuonyesha
dhambi. Itasemwa : Ovu mno zawadi hii wapewao watu hawa!
Rudi kwenye Sura
100. Hadithi hio, ewe Nabii, ni baadhi ya khabari za miji tuliyo iteketeza.
Tunakusimulia wewe upate kuwatolea mawaidha kwa khabari hizo watu wako,
na utumaini kuwa Mwenyezi Mungu atakunusuru. Baadhi ya miji hiyo imekuwa
kama mimea iliyo simama juu ya mashina yake ili waone yaliyo tokea, na
baadhi yao imefutika athari yake kama mazao yaliyo kwisha vunwa.
Rudi kwenye Sura
101. Wala Sisi hatukuwadhulumu kwa vile tulivyo wateketeza; lakini
wamejidhulumu wenyewe kwa kufuru zao, na kuacha kumuabudu Mwenyezi Mungu,
na kuleta uharibifu katika nchi. Kwa hivyo miungu yao waliyo kuwa wakiiabudu
badala ya Mwenyezi Mungu haikuweza kuwakinga na hilaki, wala haikuwafaa
kitu ilipo kuja amri ya Mola wako Mlezi, ewe Nabii! Na kushikilia kwao
kuabudu masanamu hakukuwazidishia ila hilaki na upotovu!
Rudi kwenye Sura
102. Na kuwateketeza kwa ukali kama huu, ewe Nabii, alivyo wateketeza
Mola wako Mlezi kaumu ya Nuhu, na ya A'adi, na ya Thamud, na wengineo,
ndivyo anavyo itwaa kwa nguvu miji inapo kuwa watu wake wanaingia katika
dhulma kwa ukafiri na uharibifu! Hakika kuangamiza kwake Mwenyezi Mungu
kuna nguvu, na kuna uchungu, na ukali kwa wenye kudhulumu.
Rudi kwenye Sura
103. Hakika katika hadithi hizi yapo mawaidha yanayo faa kuzingatiwa
na wenye kuyakinika kuwa kupo kufufuliwa, na kwa wenye kukhofu adhabu ya
Siku ya Mwisho! Siku hiyo ndiyo Siku ya kukusanywa watu kwa ajili ya hisabu,
na Siku hiyo itashuhudiwa na Malaika na watu pia.
Rudi kwenye Sura
104. Wala Sisi hatuiakhirishi ila kwa muda mfupi tuliyo kwisha uwekea
kiwango. Na ingawa kwa nadhari ya watu itaonekana iko mbali, kwa Mwenyezi
Mungu ni muda mchache tu.
Rudi kwenye Sura
105. Kikija kitisho chake mwanaadamu hatoweza kusema ila kwa ruhusa
ya Mwenyezi Mungu. Kwani miongoni mwa watu wapo wenye mashaka, dhiki, wasio
na bahati kwa kila namna ya shida watazo pata. Hao ndio makafiri. Na wengine
wenye furaha, walio bahatika, kwa neema zinazo wangojea Akhera. Hao ndio
Waumini.
Rudi kwenye Sura
106. Ama wale wenye mashaka mwisho wao ni Motoni. Kuvuta pumzi kwao
kutakuwa ni kwa machungu makubwa, na mikoromo na kuyayatika, wanapo vuta
pumzi na kutoa.
Rudi kwenye Sura
107. Watadumu Motoni muda wa kudumu mbingu na ardhi. Hawatotoka humo
mpaka apendapo Mwenyezi Mungu, awaadhibu kwa adhabu namna nyengine! Ewe
Nabii, Mwenyezi Mungu hutenda atakalo; hapana yeyote wa kumzuia.
Rudi kwenye Sura
108. Ama wale ambao Mwenyezi Mungu amewajaalia kuwa na bahati njema
wataingia Peponi wadumu humo tangu mwanzo, mara baada ya kwisha hisabiwa.
Huko hakuna mwisho. Isipo kuwa kikundi ambacho Mwenyezi Mungu anataka kukiakhirisha
kisiingie pamoja na wale wa mwanzo - na hao ni wale Waumini walio fanya
maasi. Hao watacheleweshwa Motoni kwa kadiri ya kupata adabu ya kuwasafisha
wapate kuingia Peponi. Na Mwenyezi Mungu atawalipa hawa walio bahatika
malipo bora kabisa ya kudumu, yasio na kasoro, wala yasio katika.
Rudi kwenye Sura
109. Ilivyo kuwa hali ya watu washirikina walio dhulumu katika dunia
na akhera ni hiyo tuliyo kusimulia, ewe Nabii, basi usiwe na shaka yoyote
juu ya mwisho wa hao katika kaumu yako wanao abudu masanamu pindi wakiendelea
katika upotovu wao. Kwani hali yao ni hali ya baba zao walio watangulia,
ambao khabari zao tumekusimulia. Wote hao ni washirikina. Na Sisi tutawatimizia
kwa ukafiri wao adhabu kaamili kwa kadiri ya makosa yao. Hawatapunguziwa
hata chembe.
Rudi kwenye Sura
110. Na Sisi tunakuhakikishia, ewe Nabii, kwamba tulimpa Musa Taurati.
Na watu wake baada yake wakakhitalifiana katika tafsiri yake na maana yake,
kwa kufuata pumbao lao na matamanio yao. Kila mmoja wao anataka kuielekeza
ifuate matamanio yake. Wakafarikiana makundi mbali mbali. Wengi wao wakajitenga
na Haki iliyo wajia. Na lau kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu haikutangulia
kuwa itaakhirishwa adhabu yao mpaka Siku ya Kiyama, ingeli wateremkia katika
hii dunia yao hukumu ya Mwenyezi Mungu wakateketezwa wapotovu na wakaokoka
walio na haki, kama yalivyo washukia wengineo, walio jiwa na ujumbe wakakhitalifiana
katika kuufahamu baadae, na wakaugeuza, hata ikawa ni uzito kuifahamu kweli.
Na hawa walio irithi Taurati wanababaika hawaijui kweli iko wapi!
Rudi kwenye Sura
111. Hapana shaka yoyote kila kikundi katika hawa Mola wako Mlezi
atawalipa jaza ya vitendo vyao. Hakika Yeye Subhanahu ni Mjuzi wa ukamilifu
wa kubwa na dogo wanayo yatenda, ikiwa kheri na ikiwa shari. Na atamlipa
kila mmoja wapo kwa mujibu alivyo tenda.
Rudi kwenye Sura
112. Ikiwa hii ndiyo hali ya kaumu zilio jiwa na Kitabu kutoka kwa
Mwenyezi Mungu, nao wakakhitalifiana kwacho na wakakitupa, basi jilazimishe
kusimama sawa sawa wewe na Waumini walio pamoja nawe kuifuata Njia Iliyo
Nyooka kama alivyo kuamrisha Mwenyezi Mungu. Wala msipindukie mipaka ya
uadilifu kwa kupunguza, na kupuuza, na kuzidisha, kwa kuzikalifisha nafsi
zenu kwa msilo liweza. Hakika Yeye Subhanahu ameyazunguka kwa ujuzi wake
yote mnayo yatenda, na atakulipeni kwayo.
Rudi kwenye Sura
113. Wala msiwapende hata kidogo maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui
zenu walio zidhulumu nafsi zao na wakapindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu.
Wala msiwategemee, au mkapendezewa na mwendo wao, na kwa kumili huko mkastahiki
adhabu ya Moto, na msimpate yeyote wa kuwatetea. Mwisho wenu mtakuwa hamtanusuriwa
kwa maadui zenu kwa kuwa Mwenyezi Mungu atakutupeni na kwa kuwa nyinyi
mnamtegemea adui yake!
Rudi kwenye Sura
114. Ewe Nabii! Timiza Sala kwa ukamilifu katika ncha mbili za mchana,
na nyakati mbali mbali za usiku. Kwani Sala husafisha nafsi na hushinda
katika kung'oa shari, na hufuta athari ya maovu ambayo mwanaadamu shida
kuepukana nayo! Hayo uliyo amrishwa, ewe Nabii, katika uwongofu wa kheri
ni mawaidha ya kuwanufaisha wale ambao walio tayari kuyakubali, ambao kwamba
wanamkumbuka Mola wao Mlezi, wala hawamsahau.
Rudi kwenye Sura
115. Ewe Nabii! Vumilia mashaka ya haya tunayo kuamrisha, na yatimize
vilivyo. Mwenyezi Mungu atakulipa malipo makubwa. Kwani kwake Yeye hayapotei
malipo ya watendao mema kwa mujibu wa vitendo vyao.
Rudi kwenye Sura
116. Ilikuwa inapasa katika kaumu zilizo tangulia na tukaziteketeza
kwa dhulma zao, wawepo jamaa kati yao wenye kusikilizwa kauli yao, na wenye
vyeo katika dini na akili, wawakanye wenzi wao waache uharibifu katika
nchi, ili wasalimike na adhabu iliyo wateremkia. Lakini hayakuwa hayo.
Yaliyo tokea ni kuwa walikuwapo Waumini wachache wasio sikilizwa rai zao
wala uwongozi wao. Hao Mwenyezi Mungu aliwaokoa pamoja na Mitume wao wakati
ule walipo shikilia wenye kudhulumu wenye inda kung'ang'anilia yale maisha
ya anasa na fisadi waliyo yazoea. Hayo yakawa ni pingamizi wasiweze kunafiika
na wito wa Haki na kheri, na kwa kukhiari kwao njia hiyo wakazama katika
madhambi na vitendo viovu. Basi Mwenyezi Mungu akawahiliki kwa mujibu wa
mwendo wake wa maumbile.
Rudi kwenye Sura
117. Wala sio mwendo wake Mwenyezi Mungu, wala sio uadilifu wake
wa maumbile, kuudhulumu umma wowote akauteketeza nao unashikamana na Haki,
unafuata mwendo bora, unatenda yanao wafaa wao na wenginewe.
Rudi kwenye Sura
118. Ewe Nabii! Lau kuwa Mola wako Mlezi angeli penda angeli wafanya
watu wote wafuate dini moja, wakimt'ii Mwenyezi Mungu kwa ut'iifu wa maumbile,
kama Malaika. Na ulimwengu ungeli kuwa sio ulimwengu huu. Lakini Yeye Subhanahu
hakutaka hayo, bali amewaacha waweze kuchagua wenyewe. Basi hawaachi kukhitalifiana
katika kila kitu, hata katika misingi ya imani, kama kumuamini Mwenyezi
Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho
- mambo ambayo haifai kukhitalifiana kwayo. Wao hufuata nyoyo zao, na matamanio
yao, na fikra zao, kila kikundi kimeshikilia kwa nguvu rai ile ile walio
kutana nayo kwa baba zao!
Rudi kwenye Sura
119. Lakini wale Mwenyezi Mungu alio warehemu kwa kusalimika kwao
kwa walivyo jaaliwa, hao wameridhia hukumu ya Mwenyezi Mungu juu yao, wakawaamini
Mitume wake wote, na Vitabu vyake vyote, na Siku ya Mwisho. Na kwa namna
hivi ilivyo pita hukumu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mpango wa huu
ulimwengu ndivyo alivyo waumbia Subhanahu kwa kuwaweka tayari kuwateua
na kuwavusha na hizo khitilafu, ili aweke tayari panapo stahiki thawabu
na adhabu. Kwa hivyo ahadi ya Mola wako Mlezi itatimia ya kwamba hapana
budi kuwa ataijaza Jahannamu kwa wafuasi wa Iblis miongoni mwa majini na
watu.
Rudi kwenye Sura
120. Ewe Nabii! Tunakusimulia kila namna ya khabari ya Mitume walio
pita pamoja na kaumu zao kwa ajili ya kukupa nguvu wewe uweze kubeba mashaka
ya Utume. Na katika khabari hizi yamekujia maelezo ya haki unayo ilingania
mfano walivyo lingania Mitume walio kutangulia, nayo ni Tawhidi ya kuwa
Mwenyezi Mungu ni Mpweke, na kuepuka yale ambayo yanamkasirisha, kama yalivyo
wajia mawaidha na mazingatio yanayo wanufaisha Waumini, ili wazidi imani
yao, na wanao jitayarisha kwa imani ili waifanyie haraka hiyo imani.
Rudi kwenye Sura
121. Ewe Nabii! Waambie hao wanao shikilia inadi na ukafiri: Tendeni
kama mnavyo weza kuupiga vita Uislamu na kuwaudhi Waumini. Sisi tunaendelea
na njia yetu, na tumethibiti katika a'mali yetu.
Rudi kwenye Sura
122. Na yangojeni hayo mnayo yangojea, na sisi kadhaalika tunangojea
ahadi ya Mwenyezi Mungu, kuwa wito wetu utashinda na tutawashinda maadui
zake.
Rudi kwenye Sura
123. Ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kujua yaliyo ya ghaibu
katika mbingu na ardhi. Anayajua yatakayo kufikieni, na yatakayo tufikia
sisi. Ni kwake Yeye tu yanarejea mambo yote kuendeshwa. Ilivyo kuwa mambo
ni hivyo, basi muabudu Mola wako Mlezi peke yake, na mtegemee Yeye, wala
usimwogope yeyote isipo kuwa Yeye. Na Mola wako Mlezi haghafiliki kabisa
na yote myatendayo, enyi Waumini na makafiri. Na kila mmoja atalipwa hapa
duniani na Akhera kwa mujibu anavyo stahiki.
Rudi kwenye Sura