1. Harufi hizi - Alif Lam Raa - ni sawa na A.L.R. Mwenyezi
Mungu Mtukufu ameanzia Sura hii. Na Yeye ndiye anajua muradi wake. Na juu
ya hivyo zinaashiria kuwa Qur'ani imeundwa kwa harufi hizi hizi za Alifbete,
na nyinyi mmeshindwa kuleta mfano wake! Na kwa harufi hizi za kutamkwa
zinawazindua washirikina, wakawa wanasikiliza, ijapo kuwa wanawafikiana
kuwa wasizisikilize Aya Tukufu hizi na mfano wake ambazo ni Aya za Qur'ani
yenye hikima katika mpango wake na maana zake, na ambayo imekusanya hikima
na kila linalo wanafuisha watu katika Dini yao na dunia yao.
Rudi kwenye Sura
2. Haiwafalii watu kustaajabu wakakanusha wahyi wetu tunao
mfunulia mtu mmoja wao, naye ni Nabii Muhammad s.a.w., ili awahadharishe
watu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na awape bishara njema wale miongoni
mwao walio amini, ya kwamba hapana shaka yoyote wana cheo kitukufu cha
juu kwa Mola wao Mlezi. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu haigeuki. Wala haiwafalii
hao watu wakanushi kumsema Muhammad, Mtume wetu, kuwa yeye ni mchawi maarufu.
Rudi kwenye Sura
3. Enyi watu! Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu aliye umba
mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake katika siku sita (1) ambazo kipimo
chake hakijui ila Mwenyezi Mungu. Akatandaza utukufu wa utawala wake, peke
yake, na akayapanga mambo yote ya viumbe vyake. Basi hapana yeyote mwenye
chochote pamoja na utawala wa Mwenyezi Mungu. Wala hawezi yeyote katika
viumbe vyake hata kumwombea mtu isipo kuwa kwa ruhusa yake. Huyo, basi,
ndiye Mwenyezi Mungu Muumba, huyo ndiye Mola wenu Mlezi, na ndiye Mlinzi
wa neema zenu. Basi muabuduni Yeye peke yake, na msadikini Mtume wake,
na kiaminini Kitabu chake. Juu yenu kukumbuka neema za Mwenyezi Mungu,
na zingatieni Ishara zake zinazo thibitisha Upweke wake.
(1) Mwenyezi Mungu ameumba viumbe vyote kwa vipindi sita, na vipindi
hivi ni viwango vya mamilioni ya makarne na makarne. Na hivyo ndivyo vinavyo
itwa Siku Sita. Na katika kila nguzo za ulimwengu zipo Ishara wazi zilizo
zagaa za kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Miongoni mwa hizi,
ni hivi kufanywa jua na mwezi na nyota kunyenyekea kwa faida ya binaadamu.
Na kadhaalika kupishana zamu usiku na mchana, na kuwa mchana unaingilia
kiza cha mbingu. Na umetajwa usiku mbele kwa kuwa kiza ndio asli. Ama mchana
umezuka kwa kuathirika kwa mwangaza wa jua katika anga la ardhi, ambayo
hiyo ardhi inazunguka wenyewe kwa wenyewe kama pia ili ipate mwangaza wa
jua, mara upande huu na mara upande huu.
Rudi kwenye Sura
4. Kama Mwenyezi Mungu alivyo anzisha uumbaji wa viumbe peke yake,
basi marejeo yenu, na marejeo ya viumbe vyote ni kwake Yeye. Na Mwenyezi
Mungu ameahidi hivyo kwa ahadi ya kweli isiyo na khitilafu. Na hakika Yeye
Subhanahu ameanzisha kuumba viumbe kwa kudra yake, na vitapo teketea atavirejesha
kwa kudra yake, ili awalipe Waumini wenye kumt'ii thawabu kwa uadilifu
ulio timia. Ama makafiri, wao huko katika Jahannamu watapewa
vinywaji vinavyo tokota kweli kweli, na watapata adhabu yenye kutia machungu
kuwa ni malipo ya ukafiri wao.
Rudi kwenye Sura
5. Na Mola wenu Mlezi ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akalifanya
jua litoe mwanga, na mwezi utoe nuru. Na akajaalia mwezi uwe na vituo ili
vikusaidieni kuweza kupima nyakati zenu, na mjue idadi ya miaka na hisabu
(1). Na wala Mwenyezi Mungu hakuumba hayo ila kwa hikima. Na Yeye Subhanahu
katika Kitabu chake anazikunjua Ishara zenye kuonyesha Ungu wake na ukamilifu
wa uwezo wake, ili mpate kuzingatia kwa akili zenu, na mkubali kwa yanayo
hitajia ujuzi.
(1) Aya hii ya 5 inahakikisha ukweli wa kisayansi ambao haukujuulikana
na hiyo sayansi ila hivi mwishoni. Hapo kwanza haukujuulikana, nao ni kuwa
jua ni umbo lenye kuwaka moto, na ndio chanzo cha nguvu za kufanyia
kazi zote, kwa Kiarabu huitwa T'aaqa, na kwa Kiingereza Energy, na kwa
Kiswahili cha sasa Nishati. Katika nguvu hizo ni huo Mwangaza na Joto.
Ama mwezi hauwaki moto, bali unarudisha mwangaza wa jua, kama kioo, kwa
hivyo huonekana una nuru. Kwa hivyo Subhanahu ameeleza kuwa jua lina mwangaza
wa asli, na mwezi unatoa nuru tu. Na Aya hii imeashiria hakika ya nyendo
za falaki, nayo ni kuwa mwezi unaizunguka ardhi, na kila siku unakuwa katika
mahala fulani kwa mintarafu ya dunia. Ukimaliza mzunguko wake ndio unatimia
mwezi, huu wa siku 30 au 29. Kwa hivyo tunaweza kujua kiasi cha mwaka,
na kwa hivyo twaweza kujua hisabu za miaka, miezi na siku.
Rudi kwenye Sura
6. Hakika katika kufuatana usiku na mchana na kukhitalifiana kwao,
kwa kuzidi na kupungua, na katika uumbaji wa mbingu na ardhi na vitu vyote
viliomo humo, zipo dalili zilizo wazi na hoja zilizo dhaahiri zenye kuhakikisha
Ungu wa Mwenye kuumba, na uwezo wake. Hayo ni kwa wenye kutaka kuiepuka
ghadhabu yake na wakaiogopa adhabu yake.
Aya hii ya 6 inaashiria hakika inayo onekana, nayo kukhitalifiana
urefu wa usiku na mchana kwa mwaka mzima katika pahala popote duniani.
Na kadhaalika kufuatana mchana na usiku, na kuwa mchana ni wa kuangaza
na kuonana, na usiku ni giza. Na maana ya hayo ni kuwa msingi wake ni kuwa
dunia inazunguka wenyewe kwa wenyewe kama pia juu ya msumari wake, na vile
vile inalizunguka jua. Na yote hayo ni dalili ya uwezo wa Mwenye kuumba
katika kuanzisha uumbaji. Ujuzi wa mambo hayo wakati wa Mtume s.a.w. haukuwepo.
Na hii ni dalili nyengine ya kwamba haya hayakuwa ila ni wahyi, ufunuo,
ulio toka kwa Mwenyezi Mungu kumpa Mtume s.a.w.
Rudi kwenye Sura
7. Hakika wale wasio amini kufufuliwa na kukutana na Mwenyezi Mungu
Siku ya Mwisho, na wakaamini - kwa kudhani tu - kuwa uhai wa duniani ndio
mwisho wao na hapana baada yake uhai mwingine, na wakatulia nyoyo zao
kwa hayo, na wala wasijue nini kitakuwa baada yake, na wakaghafilika na
Ishara za Mwenyezi Mungu juu ya kufufuliwa na kuhisabiwa,
Rudi kwenye Sura
8. Watu hao, makaazi yao watakapo
dumu ni Motoni. Hayo ni malipo kwa waliyo yachuma ya ukafiri na vitendo
viovu.
Rudi kwenye Sura
9. Hakika walio amini Imani ya kweli kweli, na wakatenda mema katika
dunia yao, Mola wao Mlezi atawathibitisha kwenye Uwongofu kwa sababu ya
Imani yao, na Siku ya Kiyama atawatia katika Bustani zipitazo mito
kati yake, na wataneemeka kwa neema za milele.
Rudi kwenye Sura
10. Dua za Waumini katika Bustani hizo ni kumsabihi na kumtakasa
Mwenyezi Mungu na kila waliyo kuwa wakiyasema makafiri duniani, na kusalimiwa
na Mwenyezi Mungu, na kusalimiana wao kwa wao ili kuthibitisha amani na
utulivu. Na kukhitimishia dua yao ni kumhimidi Mwenyezi Mungu kwa tawfiqi
yake, kuwawezesha, kufikia Imani na kufuzu kwao kuipata radhi yake.
Rudi kwenye Sura
11. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli waitikia watu wanapo jiapizia
shari kama vile wanavyo jihimizia kuitaka kheri, angeli waangamiza akawateketeza
wote. Lakini Yeye anawachukulia kwa upole basi anaakhirisha kuwateketeza,
ili kungojea wadhihirishe walio nayo kwa mujibu wa anavyo wajuulia,
upate kuonekana wazi uadilifu wake kwa atavyo walipa. Wanaachwa na ushahidi
wa kutosha umesimama dhidi yao, nao makusudi wanakengeuka na kuelekea njia
ya upotovu na udhalimu.
Rudi kwenye Sura
12. Na mtu akisibiwa na madhara katika nafsi yake au mali yake au
mfano wa hayo, huhisi unyonge wake, na humwomba Mola wake Mlezi kwa
hali yoyote - akiwa kajinyoosha, au kakaa kitako, au kasimama - amwondolee
dhiki zake! Mwenyezi Mungu akisha mwitikia, na akamwondolea hizo shida
zake, humuacha kando Mwenyezi Mungu na akaendelea na maasi yake, na akasahau
fadhila za Mwenyezi Mungu juu yake, kama kwamba hakupatikana na madhara
yoyote, wala hajapata kumwomba amwondolee! Na mfano wa mtindo huu
Shetani ndio huwazaini Makafiri, akawapambia vitendo vyao viovu, na uzushi
wao mpotovu, wakaona yote hayo ni mazuri.
Rudi kwenye Sura
13. Na Sisi tulikwisha ziangamiza kaumu zilizo kutangulieni kwa sababu
ya kufuru zao walipo wajia Mitume na Ishara zilizo wazi za kusadikisha
wito wao wa kuitia Imani. Na Mwenyezi Mungu akijua, kwa ajili ya kung'ang'ania
kwao ukafiri na uasi, kuwa haitopatikana Imani kwao! Basi enyi makafiri
wa Kikureshi! Zingatieni! Kama tulivyo waangamiza walio kuwa kabla yenu,
kadhaalika tutawalipa wakosefu kwa maangamizo.
Rudi kwenye Sura
14. Enyi Umma wa Muhammad! Tumekujaalieni muwe makhalifa wa ardhi,
mshike pahala pa walio kutangulieni, ili tukujaribuni tudhihirishe mtacho
kikhiari, ut'iifu au uasi, baada ya mlivyo kwisha jua yaliyo wapata walio
kutangulieni.
Rudi kwenye Sura
15. Zilipo dhihiri Aya (Ishara) za Qur'ani kutokana na Mtume wetu
Muhammad juu ya washirikina, walisema makafiri wasio ikhofu adhabu ya Mwenyezi
Mungu wala hawataraji thawabu zake: Tuletee kitabu kinginecho kisicho kuwa
hii Qur'ani. Au badilisha yaliyomo humu, yale yasiyo tupendeza. Waambie
ewe Mtume: Hayumkini wala haijuzu mimi kugeuza au kubadilisha kwa nafsi
yangu. Mimi si chochote ila ni mwenye kufuata na mwenye kufikisha kile
kinacho funuliwa kwangu kutokana na Mola wangu Mlezi. Mimi naogopa, nikienda
kinyume na Wahyi, Ufunuo, wa Mola wangu Mlezi, adhabu ya Siku ambayo khatari
yake ni kuu, na kitisho chake ni kikubwa!
Rudi kwenye Sura
16. Waambie ewe Mtume! Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa asiniteremshie
Qur'ani kutoka kwake, wala mimi nisikufikishieni, asingeli teremsha, wala
mimi nisingeli kusomeeni, na wala Mwenyezi Mungu asingeli kufundisheni.
Lakini Yeye kateremsha, na kanituma mimi kwayo, na mimi nimekusomeeni kama
alivyo niamrisha. Na mimi nilikwisha kaa nanyi wakati mrefu kabla ya kupewa
Utume, na mimi sikudai Utume wakati huo, wala sikukusomeeni kitu chochote.
Na nyinyi mmeshuhudia kuwa mimi ni mkweli na muaminifu. Lakini umekuja
Ufunuo na nimeamrishwa niusome. Basi hebu yatieni akilini haya mambo, na
myazingatie, na yakutanisheni yaliyo pita ya zamani na ya yaliopo sasa.
Rudi kwenye Sura
17. Hapana mtu aliye jidhulumu nafsi zaidi kuliko anaye kufuru na
akamzulia uwongo Mwenyezi Mungu, au akazikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu
alizo kuja nazo Mtume wake. Hakika hafuzu kafiri katika vitendo vyake.
Naye amekhasiri khasara iliyo wazi kwa ukafiri wake na amemghadhibisha
Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
18. Na hawa washirikina wanao mzulia Mwenyezi Mungu kuwa ana washirika,
wanaabudu masanamu ya upotovu. Hayawadhuru wala hayawanufaishi. Na wanasema:
Masanamu haya yatatuombea kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Akhera! Ewe Mtume!
Waambie: Hivyo nyinyi mnamwambia Mwenyezi Mungu kuwa ana washirika ambao
hawajui, la katika mbingu wala katika ardhi? Mwenyezi Mungu ametakasika
na kuwa na washirika, na yote mnayo zua kwa kuwaabudu hao washirika.
Rudi kwenye Sura
19. Watu kwa maumbile yao hawakuwa ila ni Umma mmoja tu. Kisha tukawapelekea
Mitume wawaongoze na wawaongoe kwa mujibu wa Ufunuo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ikawa tabia ya kibinaadamu iliyo pelekea kheri na shari ndiyo sababu ya
kuwa na nguvu zaidi shari katika baadhi yao. Juu yao hao matamanio na nyendo
za Shetani zikatawala, na kwa hivyo wakakhitalifiana. Na lau kuwa hukumu
ya Mola wako Mlezi haikutangulia ya kuwapa muhula makafiri kwa ajili yako,
Ewe Nabii, na kuakhirisha maangamizo yao mpaka siku maalumu iliyo ahidiwa,
Mwenyezi Mungu angeli wapelekea upesi maangamizo na adhabu, kwa sababu
ya mfarakano waliyo uingia, kama zilivyo ingia kaumu zilizo kwisha pita.
Rudi kwenye Sura
20. Na hawa washirikina wanasema: Hivyo Muhammad hateremshiwi muujiza
usio kuwa hii Qur'ani, wa kutuyakinisha Utume wake? Waambie Ewe Mtume!
Kuteremshwa Ishara ni jambo la ghaibu, hapana alijuaye ila Mwenyezi Mungu.
Kama Qur'ani haikufaini basi ngojeni hukumu ya Mwenyezi Mungu baina yangu
na nyinyi katika hayo mnayo yabisha. Na mimi ni pamoja nanyi katika wanao
ngojea.
Rudi kwenye Sura
21. Katika mitindo ya watu ni kuwa pale tunapo waneemesha baada ya
kwisha patwa na shida katika nafsi zao, au ahli zao (watu wao), au mali
zao, hawamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema anazo waneemesha na kuwaondolea
madhara. Bali huyakaabili hayo kwa kukakamia katika kuzikadhibisha na kuzikataa
Ishara za Mwenyezi Mungu! Ewe Mtume! Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza
wa kukuhilikini na kukuadhibuni upesi upesi, lau kuwa si hukumu yake tangu
hapo kukupeni muhula mpaka siku ya miadi aliyo iweka mwenyewe kwa ilimu
yake peke yake. Hakika Wajumbe wetu, Malaika waliyo wakilishwa juu yenu
wanaviandika vitimbi mnavyo vipanga, na Yeye Mwenyezi Mungu atakuhisabieni
na atakulipeni.
Rudi kwenye Sura
22. Mwenyezi Mungu mnaye ikufuru neema yake, na mnakanusha Ishara
zake, ndiye Yeye anaye kuezesheni kwenda na kutembea nchi kavu kwa miguu
au kwa vipando, na baharini kwa vyombo alivyo fanya vikutumikieni, vinavyo
kwenda juu ya maji, kama anavyo visahilishia Mwenyezi Mungu kwa upepo mzuri
unao puliza kwa amani mpaka kufikilia huko vyendako. Hata mkisha tumaini
na mkafurahia huvuma tena upepo mkali ukatibua mawimbi kutoka kila upande,
na mkayakinika kuwa hapana ila kuhiliki tu! Katika shida kama hii hamna
tegemeo ila Mwenyezi Mungu. Hapo basi mnamwomba madua kwa usafi wa niya,
kwa kuyakinika kuwa hapana mwokozi isipo kuwa Yeye, na mnampa ahadi kuwa
pindi akikuvueni na balaa hiyo mtamuamini, na mtakuwa wenye kushukuru.
Rudi kwenye Sura
23. Na akisha waokoa kutokana na khatari ya kuteketea, wanavunja
ahadi yao, na mara wanarejea kwenye fisadi walizo kuwa nazo kabla! Enyi
watu mvunjao ahadi! Hakika matokeo ya kupindukia mipaka ya starehe na kudhulumu
kwenu yatarejea juu yenu peke yenu. Na hakika hizo starehe mnazo zistarehea
katika dunia yenu ni starehe za kidunia zenye mwisho. Kisha
marejeo yenu ya mwisho ni kwa Mwenyezi Mungu, na Yeye atakulipeni kwa vitendo
vyenu mlivyo vitanguliza duniani.
Rudi kwenye Sura
24. Hakika hali ya uhai wa dunia kwa uzuri wake na starehe zake,
na kisha baada ya hayo kutoweka, si chochote ila ni kama hali ya maji yanayo
teremka mbinguni, yakachanganyika na mimea ya ardhi inayo liwa na watu
na wanyama. Mimea hiyo ikastawi na ikatoa matunda, na ardhi ikapambika
kwa kunawiri. Uzuri huo ukisha fika ukomo wake, na wenyewe wakayakinika
kuwa kweli ni mali yao, na kuwa watanafiika kwa matunda yake na neema zake,
amri yetu ya kuondoa yote hayo ikaja. Tukaifanya kama kwamba iliyo fyekwa,
na kama kwamba haijapata kukaliwa wala haikupata kuwa na uzuri kabla yake!
Na hali zote mbili za kustawi na kunawiri ya kufurahia watu na kinyume
cha hayo, ni mambo ya kuondoka na kutoweka! Na kama alivyo bainisha
Mwenyezi Mungu kwa mifano iliyo wazi, anabainisha Aya zake na anafafanua
hukumu zake na Ishara kwa watu wanao fikiri na wanapima kwa akili.
Aya hii inaashiria ukweli ulio anza kuchomoza, nao ni kuwa mwanaadamu
kwa kuifanya ilimu imtumikie ameweza kuyamiliki anayo yataka. Hata inapo
kuwa karibu ya kufikilia ukweli huu kukamilika, na akaona huyo mwanaadamu
amekwisha fikilia kilele cha ujuzi, hapo basi amri ya Mwenyezi Mungu hutokea.
Rudi kwenye Sura
25. Na Mwenyezi Mungu anawaitia waja wake kwa Imani na vitendo vyema
wendee Peponi, makao ya amani na utulivu. Na Yeye Subhanahu humwongoa amtakaye
- kwa kuwa kesha jitayarisha vyema na kaelekea kheri - kwenye Njia ya Haki,
nayo ni ya Salama.
Rudi kwenye Sura
26. Wanao tenda mema kwa kuitikia Wito wa Mwenyezi Mungu, wakaamini
na wakafanya kheri kwa Dini yao na dunia yao, hao watapata wema katika
Akhera, na wema huo ni Pepo. Na tena watapata yaliyo zidi hayo kwa fadhila
na ukarimu wa Mwenyezi Mungu. Wala nyuso zao hazitafunikwa na huzuni na
hamu na fedheha. Hawa ndio watu wa Peponi watakao neemeka humo daima milele.
Rudi kwenye Sura
27. Na wale ambao hawakuitikia Wito wa Mwenyezi Mungu, wakakufuru,
wakatenda maasi, watalipwa kwa mujibu ya uovu walio utenda. Na hawana
mlinzi wa kuwakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na nyuso zao zitasawajika
kwa ghamu na huzuni kama kwamba zimefunikwa na weusi wa kiza cha usiku!
Na hao ndio watu wa Motoni, watasononeka humo milele.
Rudi kwenye Sura
28. Ewe Mtume! Kumbuka kitisho cha siku watapo kusanywa viumbe vyote,
kisha tuwaambie walio mshirikisha Mwenyezi Mungu katika ibada zao: Simameni
pahala penu nyinyi na hao mlio wafanya washirika wa Mwenyezi Mungu, muangalie
mtafanywa nini? Patatokea mfarakano baina ya washirikina na hao miungu
yao ya uwongo walio washirikisha na Mwenyezi Mungu. Hao miungu watajitenga
na wale wafwasi wao, kwa kusema: Sisi hatukukutakeni mtuabudu. Wala nyinyi
hamkuwa mkituabudu sisi! Hakika mlikuwa mkiyaabudu matamanio yenu tu!
Rudi kwenye Sura
29. Mwenyezi Mungu anatutosheleza kwa ilimu yake na hukumu yake kuwa
ni Shahidi wa kutupambanua baina yetu na nyinyi. Sisi tulikuwa mbali nanyi,
wala hatukuwa tunafaidika vyovyote kwa huko kutuabudu kwenu.
Rudi kwenye Sura
30. Katika msimamo huo kila mtu atajua kheri gani au shari gani aliyo
ifanya, na atalipwa malipo yake. Na hapo hao washirikina watayakinika kuwa
kweli Mwenyezi Mungu ni Mmoja na wa pekee, Mwenye Haki. Na yote waliyo
kuwa wakimzulia Mwenyezi Mungu yatavunjika.
Rudi kwenye Sura
31. Ewe Mtume! Lingania kwenye Tawhidi safi, na useme: Nani anaye
kuleteeni riziki kutoka mbinguni inapo teremka mvua, na katika ardhi inapo
mea mimea na kuzaa? Na nani aliye kupeni kusikia na kuona? Na nani anaye
toa vilio hai kutokana na vilio maiti, kama mimea, nayo ni hai kutokana
na ardhi maiti? Nani anaye mtoa maiti kutokana na hai, kama mtu anavyo
kufa? Na nani anaye panga na kuendesha mambo yote ya ulimwengu kwa kudra
yake na hikima yake? Wataungama: Hapana pa kukimbilia! Kwa hakika
ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mtenda yote. Ewe Mtume! Waambie watapo
ungama: Si waajibu mkubwa kuit'ii Haki, na kumkhofu Mwenyezi Mungu, Mmiliki
Ufalme wote?
Rudi kwenye Sura
32. Huyo basi ndiye Mwenyezi Mungu mliye mkiri, na Yeye tu peke yake
ndiye Mola wenu Mlezi aliye thibiti kuwa ni Mola na Mlezi, na akapasa kuabudiwa
pekee, wala hapana mwenginewe. Na hapana baada ya Haki ya Umoja wa Mwenyezi
Mungu na kumuabudu Yeye tu, ila kutumbukia katika upotovu, nao ni kumshirikisha
Mwenyezi Mungu na kumuabudu mwenginewe. Basi vipi mnaiacha Haki mkauendea
upotovu?
Rudi kwenye Sura
33. Kama ulivyo thibiti Ungu wa Mwenyezi Mungu na kumuabudu Yeye,
vile vile imethibiti hukumu juu ya walio tokana na amri ya Mwenyezi Mungu
wakimuasi kwa kuwa hawaifuati Haki. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu
hawaongoi kwenye Haki ila wanao ishika njia yake, sio wanao mfanyia uasi.
Rudi kwenye Sura
34. Ewe Mtume! Waambie hao washirikina: Yupo yeyote katika hao mlio
wafanya washirika wa Mwenyezi Mungu mkawaabudu, awezaye kuanzisha kuumba
tangu mwanzo, na tena akarejea tena baada ya kwisha toweka? Hapana shaka
watashindwa kujibu! Basi hapo tena waambie: Allah, Mwenyezi Mungu, tu peke
yake, ndiye anaye anzisha kuumba kutokana na kuto kuwepo, na tena viumbe
vikitoweka huvirejesha. Vipi basi nyinyi mnaiacha Imani?
Rudi kwenye Sura
35. Ewe Mtume! Waambie hao washirikina: Yupo yeyote katika hao mlio
wafanya washirika wa Mwenyezi Mungu mkawaabudu, awezaye kupambanua baina
ya uwongofu na upotovu, akawaongoza watu kwenye Njia ya Haki? Wataemewa!
Basi, je! Yupi bora kufuatwa - Mwenye kuweza kuongoa kwendea Haki au asiye
weza hata kujiongoa nafsi yake? Naye huyo hawezi kumwongoa mtu, ila yeye
anahitaji mtu wa kumwongoa. Hao ndio kama wakuu wa makafiri, mapadri na
mamonaki ambao ndio mmewafanya ni waola mkamuacha Mwenyezi Mungu!! Nini
basi kilicho kupelekeeni kukengeuka hata mkawashirikisha hawa na Mwenyezi
Mungu? Na nini hali ya ajabu iliyo kusukumeni kwenye hizo hukumu na sharia
za kigeni?
Rudi kwenye Sura
36. Wengi wa washirikina hawafuati katika itikadi zao ila dhana potovu
zisio kuwa na dalili zozote! Na kwa jumla, dhana haifidi kitu, wala haiwezi
kuwa ni badala ya kuijua Haki, na khasa ikiwa dhana yenyewe ni ya kuzua
tu, kama hizi dhana za washirikina. Na hakika Mwenyezi Mungu anayajua vyema
wayafanyayo wakuu wa ukafiri na wafuasi wao, naye atawalipa kwa hayo.
Rudi kwenye Sura
37. Haiwezi kutokea kuwa hii Qur'ani aizue mtu yeyote, kwani katika
kuwa haiwezi kuigwa, na katika uwongofu wake, na hukumu zake, hayumkini
kuwa itoke kwa yeyote isipo kuwa kwa Mwenyezi Mungu tu. Nayo inasadikisha
Vitabu vya mbinguni vilivyo tangulia katika mambo ya Haki yaliyo tajwa
humo, na inaweka wazi yaliyo kwisha andikwa na kuthibitishwa katika mambo
ya hakika na sharia. Hapana shaka kuwa Qur'ani hii ina cheo maalumu kwa
Mwenyezi Mungu, nayo ni muujiza ambao hapana mtu anaye weza kuleta mfano
wake.
Rudi kwenye Sura
38. Bali hawa washirikina wanasema: Muhammad kaizua hii Qur'ani mwenyewe!
Ewe Mtume! Waambie: Ikiwa hii Qur'ani ni kazi ya mwanaadamu, basi nyinyi
leteni Sura moja tu mfano wake, na muwatake muwatakao, isipo kuwa
Mwenyezi Mungu, waje kukusaidieni; ikiwa nyinyi ni wasema kweli katika
madai yenu kuwa hii Qur'ani nimeitunga mimi.
Rudi kwenye Sura
39. Bali hawa washirikina wamekimbilia kuikadhibisha Qur'ani bila
ya kuzingatia, wakajua yaliomo ndani yake! Wao wenyewe hawakutazama mna
nini, wala hawakusita kuitafuta tafsiri yake, na kutaka kuelewa hukumu
zake kwa kuwauliza wenginewe! Na kukadhibisha namna hii bila ya ujuzi,
ndivyo walivyo wakanusha makafiri wa kaumu za zamani Mitume wao na Vitabu
vyao! Basi, ewe mwanaadamu! Angalia yaliishiaje mambo ya walio kadhibisha
walio tangulia. Waliachiliwa mbali na wakateketezwa kwa adhabu! Na huu
ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa mfano wa hao.
Rudi kwenye Sura
40. Na miongoni mwa hawa wakanushao wapo ambao watakuja iamini Qur'ani
baada ya kuyafahamu yaliyomo ndani yake, na wakayaelewa maana yake. Na
kipo miongoni mwao kikundi ambacho hakiamini wala hakiachi upotovu wake!
Na Allah Subhanahu wa Taa'la anawajua vyema wakanushao mafisadi, na atawalipa
kwa vitendo vyao.
Rudi kwenye Sura
41. Na ewe Mtume! Wakishikilia kuendelea na kukukadhibisha baada
ya kuwadhihirikia wazi dalili za Unabii wako, basi wewe waambie: Hakika
mimi nitalipwa kwa a'mali yangu,(vitendo vyangu); na nyinyi mtalipwa kwa
a'mali yenu kama itakavyo kuwa. Na mimi naendelea na Wito wangu, na nyinyi
hamtahisabiwa kwa a'mali yangu, wala mimi sitahisabiwa kwa a'mali yenu.
Basi nyinyi fanyeni mpendavyo. Na Mwenyezi Mungu atamlipa kila mtu kwa
aliyo yachuma.
Rudi kwenye Sura
42. Na katika hawa makafiri wapo wanao kusikiliza wewe, Mtume, pale
unapo waita wafuate Dini ya Mwenyezi Mungu, na hali nyoyo zao zimefungwa
hazikubali Wito wako. Basi wewe huwezi kuwafanya hawa viziwi wakusikie
na waongoke. Na khasa ilivyo kuwa juu ya uziwi wao, hawafahamu uyasemayo.
Rudi kwenye Sura
43. Na wengine wapo wanao kutazama na wanalifikiria jambo lako, na
wanaona dalili zilizo wazi za Unabii wako. Lakini bado hawaongoki wakafuata.
Mfano wa hayo ni mfano wa kipofu, nawe huwezi kuwaongoa hao vipofu. Upofu
wa macho ni kama upofu wa moyo. Wote hawana uwongofu! Kipofu haioni njia
kwa kuhisi, na mpotovu haongoki kwa maana.
Rudi kwenye Sura
44. Hakika Mwenyezi Mungu Subhanahu atawalipa watu kwa vitendo vyao
kwa uadilifu na haki, wala hatamdhulumu hata mmoja wapo kwa kitu chochote.
Lakini watu wanajidhulumu nafsi zao kwa kukhiari kwao ukafiri kuliko Imani.
Rudi kwenye Sura
45. Ewe Mtume! Wahadharishe na Siku tutayo wakusanya kwa ajili ya
Hisabu, wawe na hakika kuwa Siku ya Akhera itakuja, baada ya kuwa walikuwa
wakiikanusha na wakikumbuka maisha yao ya duniani tu. Waone ni kama saa
moja tu ya mchana, hapana wasaa wa kufanya kitendo chochote cha kheri,
na wajuane wao kwa wao wakilaumiana kwa kufuru na upotovu walio kuwa nao!
Wamekhasiri wakanushao Siku ya Akhera na wasitangulize vitendo vyema katika
dunia yao, na wakakosa neema za Akhera kwa kufuru zao.
Rudi kwenye Sura
46. Ewe Mtume! Tukikuonyesha baadhi ya tunayo waahidi, nayo kuwa
utawashinda na wao watapata adhabu, au tukakufisha kabla ya kuyaona yote
hayo, vyovyote vile hawawezi kuepuka kurejea kwetu tuwahisabie na kuwalipa.
Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Mwenye kuwachungua na Mwenye kujua kila
walitendalo, naye atawalipa.
Rudi kwenye Sura
47. Na kila umma ulijiwa na Mtume akafikisha wito wa Mwenyezi Mungu,
akaamini aliye amini, na akakanusha aliye kanusha. Ikifika Siku ya kufufuliwa,
Mtume wao atakuja na kuwatolea ushahidi wale walio mkadhibisha kuwa hao
ni makafiri, na walio amini kuwa ni Waumini. Basi Mwenyezi Mungu atawahukumu
kwa uadilifu ulio timia. Hatomdhulumu yeyote katika malipo anayo stahiki.
Rudi kwenye Sura
48. Na makafiri wanakusudia kuikanusha Siku ya Akhera, basi wanaihimiza
kwa kejeli na kusema: Itakuwa lini hiyo adhabu unayo tuahidi, kama wewe,
ewe Mtume, na hao walio pamoja nawe, ni wakweli katika hayo mnayo yaamini
na mnatuitia sisi tuyakubali?
Rudi kwenye Sura
49. Ewe Mtume! Waambie: Mimi sina uwezo wa kujitendea mwenyewe kheri
wala shari, ila kwa aliyo niwezesha Mwenyezi Mungu. Basi vipi niweze kuihimiza
ije upesi hiyo adhabu? Hakika kila umma una ukomo wake aliyo uwekea Mwenyezi
Mungu tangu na tangu. Ukiwadia ukomo huo basi hawatoweza kuuchelewesha
hata kidogo, kama wasivyo weza kuutanguliza!
Rudi kwenye Sura
50. Waambie wanao himiza ifike adhabu: Hebu niambieni, ikikufikieni
adhabu ya Mwenyezi Mungu usiku au mchana, pana faida gani watayo ipata
wakosefu wenye madhambi kutaka ije kwa haraka? Na hali adhabu yote ni mbaya!
Rudi kwenye Sura
51. Sasa mnaikanusha adhabu? Tena itapo kufikieni mtaambiwa kwa kubeuliwa:
Je! Sasa mnaamini kwa kuwa mnaiona, na nyinyi huko duniani mlikuwa mkiihimiza
kwa dharau na kukanusha!
Rudi kwenye Sura
52. Tena Siku ya Kiama wataambiwa walio jidhulumu nafsi zao kwa kukufuru
na kukanusha: Onjeni adhabu ya milele..sasa hamlipwi ila kwa a'mali zenu
mlizo zitenda duniani.
Rudi kwenye Sura
53. Na makafiri, kwa njia ya kejeli na kukataa, wanakutaka wewe,
Mtume, uwaambie hivyo ni kweli hayo uliyo yaleta katika Qur'ani na khabari
za kufufuliwa, na adhabu? Waambie: Naam! Kwa haki ya Muumba wangu aliye
niumba, hakika hayo yatakuwa bila ya shaka yoyote. Wala nyinyi hamtoshinda
wala hamwezi kuzuia adhabu aitakayo Mwenyezi Mungu kukuleteeni.
Rudi kwenye Sura
54. Na lau kuwa vitu vyote viliomo duniani ni mali ya kila nafsi
iliyo dhulumu kwa ushirikina na kukanusha, ingeli vitoa fidia kwa adhabu
itayo wakabili Siku ya Kiyama, na ambayo wataviona vitisho vyake. Na hapo
basi majuto na masikitiko yatawajaa nyoyoni mwao kwa kutoweza kuyatamka,
na kwa fazaa itayo wapata kwa kuiona adhabu! Na hukumu ya Mwenyezi Mungu
itapita juu yao kwa uadilifu, na wala hawatodhulumiwa katika malipo hayo,
kwani hayo ni matokeo ya waliyo yatenda duniani!
Rudi kwenye Sura
55. Watu nawajue kuwa hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kumiliki
na Mwenye madaraka makuu juu ya vyote viliomo mbinguni na duniani. Na pia
wajue kuwa ahadi yake ni ya kweli. Basi Yeye hashindwi na kitu, na hapana
yeyote ataye epuka malipwa yake. Lakini wao wamedanganyika na maisha ya
dunia, hawajui hayo kwa ujuzi wa yakini!
Rudi kwenye Sura
56. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu anavihuisha vitu baada ya kuwa havipo,
na anaviondoa baada ya kuwapo. Na kwake Yeye tu ndio marejeo katika Akhera.
Na mwenye kuwa hivyo hapana kuu la kumshinda.
Rudi kwenye Sura
57. Enyi watu! Kimekujieni kwa ulimi wa Mtume Muhammad Kitabu kilicho
toka kwa Mwenyezi Mungu. Ndani yake mna makumbusho ya Imani, na ut'iifu,
na mawaidha ya kuhimiza kheri, na kukataza vitendo viovu, na kueleza mzingatie
khabari za walio kutangulieni, na kukutakeni muangalie utukufu wa uumbaji
ili mpate kuuelewa utukufu wa Muumba. Na ndani ya Kitabu hicho mna dawa
ya maradhi ya nyoyo zenu, maradhi ya shirki na unaafiki; na mna uwongofu
wa kuendea Njia Iliyo Nyooka. Na yote hayo ni rehema kwa Waumini wanao
itikia wito.
Rudi kwenye Sura
58. Ewe Mtume! Waambie: Furahieni fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema
yake juu yenu kwa kuiteremsha Qur'ani, na kubainisha Sharia ya Islamu.
Na hii ni bora kuliko starehe zote anazo zikusanya mtu duniani, kwa sababu
hichi ni chakula cha nyoyo na dawa ya maradhi yake.
Rudi kwenye Sura
59. Ewe Mtume! Waambie makafiri walio pewa baadhi ya starehe za duniani:
Niambieni khabari ya vyakula vizuri vya halali alivyo kuruzukuni Mwenyezi
Mungu, mkajifanya wenyewe ni watungaji sharia, mkahalalisha vingine na
mkaharimisha vingine, bila ya kufuata Sharia ya Mwenyezi Mungu! Hakika
Mwenyezi Mungu hakukupeni ruhusa mfanye hayo, bali nyinyi mnamzulia uwongo
Mwenyezi Mungu.
Rudi kwenye Sura
60. Na watadhani nini Siku ya Kiyama hao walio mzulia uwongo Mwenyezi
Mungu, wakajipa kuhalalisha na kuharimisha bila ya kuwa nayo dalili yoyote?
Hakika Mwenyezi Mungu amewaneemesha neema nyingi na amezihalalisha kwao
kwa fadhila yake, na amewawekea Sharia yenye kheri kwao. Lakini hawamshukuru
Mwenyezi Mungu kwa hayo, bali wanamzulia Mwenyezi Mungu uwongo!
Rudi kwenye Sura
61. Ewe Mtume! Hakika wewe umefikisha ujumbe wako, na hayo Mwenyezi
Mungu anayajua. Na hapana jambo lolote katika mambo yako, na huwasomei
Qur'ani, na wewe na umma wako hamtendi kitu, ila Sisi tunayashuhudia na
tunayaangalia mnapo yaingia kwa juhudi. Na Mola wako Mlezi haachi kujua
chochote hata kikiwa kina uzito wa chembe hichi, ikiwa katika mbingu au
katika ardhi, kidogo na kikubwa. Vyote hivyo vinadhibitiwa katika Kitabu
kilichoko kwa Mwenyezi Mungu, nacho ni chenye kubainisha wazi.
Rudi kwenye Sura
62. Enyi watu! Tanabahini na mjue ya kuwa wenye kumuelekea Mwenyezi
Mungu kwa Imani na ut'iifu Yeye anawapenda, na wao wanampenda. Hawana khofu
ya kuhizika duniani, wala kupata adhabu ya Akhera. Wala wao hawahuzuniki
kwa kukosa starehe za duniani, kwa kuwa watapata kwa Mwenyezi Mungu yaliyo
makubwa na mengi kuliko hayo.
Rudi kwenye Sura
63. Na hao ndio walio yasadiki yote yaliyo toka kwa Mwenyezi Mungu,
na wakaifuata Haki, na wakayaepuka maasi, na wakamkhofu Mwenyezi Mungu
katika kila walitendalo.
Rudi kwenye Sura
64. Kwa wapenzi hawa wa Mwenyezi Mungu pana bishara ya kheri hapa
duniani, kwa vile Mwenyezi Mungu amewaahidi kuwapa ushindi na utukufu,
na Akhera itatimia ahadi ya Mwenyezi Mungu. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu
haigeuki. Na haya ndiyo waliyo bashiriwa kwayo duniani, na watayapata Akhera.
Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
Rudi kwenye Sura
65. Ewe Mtume! Usihuzunuke kwa wayasemayo washirikina ya kejeli,
na matusi, na kukadhibisha. Wala usidhani kuwa hali yao hii itadumu. Bali
ushindi ni wako, na Uislamu utatukuka, kwani utukufu wote ni wa Mwenyezi
Mungu Mtukufu, na ushindi upo mkononi mwake, na Yeye atakunusuru uwashinde
hao makafiri. Na Yeye Subhanahu ni Mwenye kuyasikia wanayo kuzulia, na
Mwenye kuyajua wanayo dhamiria. Na Yeye atawalipa kwa hayo.
Rudi kwenye Sura
66. Enyi watu! Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu peke yake vyote viliomo
mbinguni na duniani, kwa kuviumba, na kuvimiliki, na kuviendesha. Na hao
wanao mshirikisha Mwenyezi Mungu kwa hakika hawawafuati hao miungu ya ushirikina.
Hao si chochote ila wanafuata mawazo tu, wanadhani kuwa uwezo umo katika
vitu ambavyo havijifai wenyewe, la kwa manufaa wala madhara.
Rudi kwenye Sura
67. Hakika huyo Mwenye kumiliki viliomo katika mbingu na ardhi, ndiye
aliye kuumbieni usiku mpate kupumzika na mahangaiko ya mchana. Na amekuumbieni
mchana wenye kuangaza mpate kufanya kazi na mshughulikie maslaha yenu.
Hakika katika kuumbwa usiku na mchana zipo dalili zilizo wazi kwa wenye
kusikia na wakapima.
Rudi kwenye Sura
68. Na ikiwa wanao abudu masanamu wamefanya ushirikina wa kuabudu
mawe, na hawakumtakasa Mwenyezi Mungu kwa haki ya kumtakasa, na wakasema
kuwa Allah, Mwenyezi Mungu, ana mwana, basi Mwenyezi Mungu ametakasika
na hayo. Yeye hana haja ya kuwa na mwana; kwani kuwa na mwana kunaonyesha
wazi kutaka kubakia ukoo wako baada ya kufa kwako. Na Mwenyezi Mungu hafi.
Yeye ni Mwenye kubakia milele. Na vyote viliomo katika mbingu na viliomo
katika ardhi ni vyake, vimeumbwa na vinaendeshwa na Yeye. Na nyinyi wazushi,
hamna hoja yoyote wala dalili ya hayo mnayo zua! Basi msikhitalifiane juu
ya Mwenyezi Mungu kwa mambo yasiyo na msingi wa hakika.
Rudi kwenye Sura
69. Ewe Mtume! Waambie: Hao wanao
mtungia Mwenyezi Mungu uwongo, na wanadai kuwa ana mwana, hawatafanikiwa
milele.
Rudi kwenye Sura
70. Wao wana starehe hapa duniani ya kudanganyika nayo. Nayo ni chache,
ikiwa itachukua muda mrefu au mfupi, ukilinganisha na hayo yanayo wangojea!
Kisha marejeo yao ni kwetu, Sisi. Tutawahisabia na tutawaonjesha adhabu
ya kutia uchungu kwa sababu ya ukafiri wao.
Rudi kwenye Sura
71. Yanayo kupata kutoka kwa watu wako, yaliwapata Manabii walio
kutangulia. Basi wasomee hawa watu, Ewe Mtume, aliyo kuteremshia Mola wako
Mlezi katika Qur'ani kisa cha Nuhu, Mtume wa Mwenyezi Mungu. Alipo iona
chuki na uadui wa watu wake kwa ujumbe wake, aliwaambia: Enyi watu wangu!
Ikiwa kuwa pamoja nanyi kwa ajili ya kufikisha ujumbe kumekuwa ni shida
juu yenu, basi mimi ni mwenye kuendelea na wito wangu, na ni mwenye kushikilia
hapo hapo, na ni mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu katika hili jambo langu.
Basi nyinyi na washirika wenu jifungeni madhubuti katika shauri yenu, wala
msiufiche uadui wenu kwangu kabisa, wala msinipe muhula wowote kwa maovu
mnayo nipangia kunitendea, kama kweli mnaweza kuniletea madhara. Kwani
Mola wangu Mlezi ananilinda.
Rudi kwenye Sura
72. Na ikiwa mtabaki kukataa wito wangu, basi hayo hayatanidhuru
mimi kitu. Kwani mimi sikufanya hivyo kwa kutaraji kupokea ujira kwenu
ambao naogopa nitaukosa, kwa sababu ya kukataa kwenu! Ujira wangu mimi
nautaka kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na Yeye ameniamrisha niwe Muislamu,
nimsalimishie Yeye mambo yangu yote.
Rudi kwenye Sura
73. Na juu ya juhudi hizo, na kukakamia huko aliko kakamia Nuhu kwa
ajili ya kutaka kuwaongoa hao watu wake, bado walishikilia kuendelea na
kumkanusha na kumfanyia uadui. Basi Mwenyezi Mungu alimwokoa yeye pamoja
na wenye kumuamini, wakapanda marikebu. Na akawajaalia hao ndio walio iamirisha
nchi baada ya kuteketea makafiri, walio gharikishwa na tofani. Hebu angalia,
ewe Muhammad! Vipi walio puuza onyo ulivyo malizikia mwisho wao mbaya.
Rudi kwenye Sura
74. Baada ya Nuhu tuliwatuma Mitume wengine wakilingania Tawhid,
Upweke wa Mwenyezi Mungu, wakibashiria kheri na wakionya, na wakiungwa
mkono na miujiza yenye kuonyesha ukweli wao. Watu wao wakawakanya kama
walivyo kanya kaumu ya Nuhu. Haukuwa mwendo wa wapinzani kuwa wat'iifu,
kwa sababu kule kukadhbisha kwao kulikuwa ni mbele kuliko kuzingatia
na kupima. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu alipiga muhuri wa upotovu juu ya nyoyo
za wale ambao mtindo wao ni kuzifanyia uadui hakika na Ishara zilizo wazi!
Rudi kwenye Sura
75. Kisha baada yao tulimtuma Musa na ndugu yake Haruni wende kwa
Firauni, mfalme wa Misri na watu wake wakuu makhsusi, kuwaita wamuabudu
Mwenyezi Mungu peke yake. Nao waliungwa mkono na hoja zenye nguvu. Firauni
na kaumu yake walitakabari wakakataa kuitikia wito wa Musa na Haruni. Kwa
kukataa kwao huko wakawa wamefanya makosa makubwa na dhambi.
Rudi kwenye Sura
76. Ilipo dhihiri Haki yetu kwa mkono wa Musa, ule muujiza wa Musa
- nao ni fimbo kugeuka nyoka mbele ya macho yao - wao walisema: Hakika
huu ni uchawi ulio dhaahiri!
Rudi kwenye Sura
77. Musa akawaambia kukanya uzushi wao: Nyinyi mnaita Haki iliyo
toka kwa Mwenyezi Mungu kuwa ni uchawi? Hivyo hii kweli mliyo iona kwa
macho yenu ni uchawi? Basi hivi hapa mimi nakutakeni mthibitishe kwamba
huu ni uchawi. Waleteni wachawi wathibitishe hayo mnayo yadai. Na wachawi
hawafanikiwi abadan!
Rudi kwenye Sura
78. Firauni na watu wake walimwambia Musa: Hapana shaka wewe umekuja
kwa makusudi ya kutuachisha dini ya baba zetu, na mila za kaumu yetu, ili
nyinyi wawili mpate kuwa na wafuasi; wewe na nduguyo mpate ufalme na utukufu
na urais wa kutawala na kuhukumu! Kwa hivyo basi sisi hatutakuaminini nyinyi
wala huo utume wenu!
Rudi kwenye Sura
79. Firauni na kaumu yake wakadai kuwa Musa na nduguye ni wachawi,
wala si Mitume! Akawataka watu wake wamhudhurishe kila aliye hodari katika
fani za uchawi katika mamlaka yake.
Rudi kwenye Sura
80. Walipo hudhuria wachawi, na wakasimama mbele ya Musa kupambana
naye kwa uchawi wao mbele ya watu, Musa aliwaambia: Leteni huo uchawi mlio
nao!
Rudi kwenye Sura
81. Walipo tupa kamba zao na fimbo zao, Musa aliwaambia: Huo mlio
fanya ni uchawi kweli, na Mwenyezi Mungu Subhanahu atauvunja kwa mkono
wangu! Hakika Mwenyezi Mungu hawasahilishii mafisadi vitendo vyao vikawa
vizuri na vyenye nafuu.
Rudi kwenye Sura
82. Ama Haki hapana shaka Mwenyezi Mungu atainusuru na ataiunga mkono
kwa uwezo wake na hikima yake hata makafiri wakisaidiana katika kuichukia
na kuipiga vita.
Rudi kwenye Sura
83. Na juu ya kudhihiri Ishara zote za kusadikisha Ujumbe, wale walio
muamini Musa hawakuwa ila ni kikundi cha watu wachache tu katika kaumu
ya Firauni. Waliamini juu ya kuwa wakiogopa asije Firauni na walio pamoja
naye wakawaachisha waliyo yaamini. Jeuri za Firauni zilikuwa kubwa mno
katika Misri! Hakika yeye ni katika walio pita upeo katika kutakabari na
kujivuna.
Rudi kwenye Sura
84. Ama Musa aliwaambia Waumini kwa kuwawasa na kuwashajiisha: Enyi
watu wangu! Ikiwa Imani imekwisha ingia nyoyoni mwenu kwa kumsafishia niya
Mwenyezi Mungu, basi msimwogope yeyote mwenginewe. Nanyi msalimishie Yeye
mambo yenu yote, na mtegemeeni Yeye, na muwe na yakini mwishoe atakunusuruni,
ikiwa nyinyi mmethibiti katika Uislamu.
Rudi kwenye Sura
85. Waumini wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi Mungu peke yake. Kisha
wakamwomba Mola wao Mlezi asiwatie katika mitihani na mateso ya makafiri.
Rudi kwenye Sura
86. Wakamwomba Mola wao Mlezi wakisema: Kwa vile ulivyo tumiminia
neema na rehema, na kwa wingi wa rehema yako unayo sifika nayo, tuokoe
na hawa watu wanao kataa, wenye kudhulumu.
Rudi kwenye Sura
87. Tukawafunulia Musa na nduguye Haruni kuwapa amri wafanye nyumba
za kukaa watu wao katika nchi ya Misri, na watu wa Imani wenye kufuata
wito wa Mwenyezi Mungu wazielekee nyumba hizo, na wawe wanashika Sala kwa
sura ya ukamilifu. Na Waumini wanabashiriwa kheri!
Rudi kwenye Sura
88. Walivyo shikilia makafiri katika kumfanyia inda Musa, alimwomba
Mwenyezi Mungu kwa kusema: Ewe Mola Mlezi wangu! Hakika Wewe umempa Firauni
na watukufu wake starehe za duniani, na mali, na wana, na utawala. Na matokeo
ya neema hizi ni kupita kwao mipaka katika kupotea na kupoteza watu waache
Njia ya Haki! Ewe Mwenyezi Mungu! Yafutilie mbali mali yao, na uwaache
katika kiza cha nyoyo zao, wasijaaliwe kuipata Imani mpaka waione kwa macho
adhabu iliyo chungu, ambayo ndiyo mwisho unao wangojea, ili wawe ni onyo
kwa wengineo.
Rudi kwenye Sura
89. Mwenyezi Mungu akasema: Dua zenu zimeitikiwa. Basi endeleeni
katika Njia Iliyo Nyooka, na iwacheni njia ya wale wasio jua mambo yalivyo,
wala hawaifuati Haki iliyo wazi.
Rudi kwenye Sura
90. Tulipo wavusha bahari Wana wa Israili, Firauni na askari wake
waliwafuatia nyuma yao, tukawafunika kwa bahari! Alipo kuwa anazama, Firauni
alisema: Nimemsadiki Allah, Mwenyezi Mungu, walio msadiki Wana wa Israili,
na wakamfuata. Na mimi ni katika wenye kut'ii walio wanyenyekevu!
Rudi kwenye Sura
91. Mwenyezi Mungu hakukupokea kuamini huko kwa Firauni ambako alikuwa
hana budi nako. Toba hiyo ilikuwa pale mauti yamekwisha mkabili, naye aliishi
maisha yake yote katika kumuasi Mwenyezi Mungu, akifisidi nchi, naye akafa
kafiri wa kutupwa!
Rudi kwenye Sura
92. Na leo siku ulipo angamia tutautoa mwili wako baharini, na tutauweka
uwe ni onyo na funzo kwa hao walio kuwa wakikuabudu, na hawakuwa wakikutarajia
utapata mwisho huu wa hizaya wa machungu.(1) Lakini watu wengi wanaghafilika
na Ishara zilizo wazi na zilizo zagaa katika ulimwengu, na ambazo zinathibitisha
uwezo wetu.
(1) Inaonyesha Aya hii tukufu kuwa mwili wa Firauni utabaki umehifadhiwa
ili watu wauone, na wapime kwa macho yao hali ya ule mzoga wa yule aliye
kuwa akijiona ni mungu, na akiwaambia watu wake wanao mnyenyekea: Hamna
mungu ila mimi!
Kadhaalika tujue kuwa kutoka Wana wa Israili katika nchi ya Misri
kulikuwa mwishoni mwa karne ya kumi na tatu kabla ya kuzaliwa Nabii Isa
a.s., katika enzi ya mmoja wa Mafirauni wa Ukoo wa kumi na tisa, naye ni
Minfitah mwana wa Ramsis wa Pili, ambaye ndiye aliye wakandamiza Wana wa
Israili akawalazimisha wamjengee Jiji la ufalme wake.
Uvumbuzi wa machimbo ya vitu vya kale wa hivi karibuni umedhihirisha
kuwa jina la mji huo ulio funikika chini ya ardhi, ni "Bur'amsis". Kulikuwa
kutoka kwa Wana wa Israili pamoja na Musa ni kwa ajili ya wito wa Tawhidi,
Umoja wa Mwenyezi Mungu, na kuikata shemere ya Firauni iliyo wadhalilisha,
na ikawakutisha adhabu ya mwisho.
Na ilikuwa haijuulikani na Waarabu ambao hawajui kusoma na kuandika,
wala kwa wengineo, kwamba mwili wa Firauni huyu ungalipo mpaka hii leo.
Lakini Qur'ani imeyataja hayo, na ukweli wake umethibiti mwaka 1900 B.K.,
yaani karne kumi na tatu baada ya kuteremka Qur'ani. Je, hii si dalili
ya kuwa imetoka kwa Mungu?
Rudi kwenye Sura
93. Na tuliwaweka vyema Wana wa Israili wakaishi katika nchi nzuri
na huku wakiihifadhi Dini yao, nao wako mbali na dhulma iliyo kuwa ikiwapata;
riziki na neema zimewajalia. Lakini mara baada ya kuonja neema ya
utukufu baada ya unyonge, yaliwasibu maradhi ya kufarikiana. Wakakhitalifiana
juu ya kuwa imekwisha bainika kweli na uwongo! Mwenyezi Mungu atahukumu
baina yao Siku ya Kiyama, na atamlipa kila mmoja kwa alilo tenda.
Rudi kwenye Sura
94. Ikikuingia shaka wewe au mwengineo katika huu wahyi tuliyo kuteremshia,
basi waulize watu wa Vitabu vilivyo tangulia walivyo teremshiwa Manabii
wao. Kwao utapata jawabu ya kukata, yenye kuwafikiana na haya tuliyo kuteremshia
wewe. Na hayo ni kutilia mkazo ukweli wa uwazi wa dalili pindi ikitokea
shaka yoyote. Basi hapana njia ya kutia shaka. Sisi tumekuteremshia Haki
isiyo na shaka yoyote. Basi usishindane na yeyote mwenginewe katika kutia
shaka na kutaradadi.
Rudi kwenye Sura
95. Wala usiwe wewe, wala yeyote katika wanao kufuata, miongoni mwa
wanao kadhibisha hoja na Ishara zilio wazi, msije mkaingia khasarani na
ghadhabuni, kama hali ya makafiri wasio amini. Na akisemezwa Nabii basi
ndio wanasemezwa wote wanao mfuata.
Rudi kwenye Sura
96. Hakika wale iliyo kwisha pita juu yao hukumu ya kuwa wao ni makafiri,
kwa kujuulikana inadi yao na chuki zao, hawatoamini hata ukijihangaisha
vipi nafsi yako kuwakinaisha.
Rudi kwenye Sura
97. Na ukiwajia na kila hoja, na iwe wazi vipi, hawakinaiki. Wataendelea
tu na upotovu wao mpaka wamalizikie kupata adhabu chungu.
Rudi kwenye Sura
98. Lau kila mji ungeli amini ingeli wafaa Imani yao. Lakini hawaamini,
na kwa hivyo hayapatikani manufaa. Ila kaumu ya Yunus. Kwani wao waliamini,
na wakapata manufaa yao. Tuliwaondolea hizaya na machungu, na tukawapa
starehe ya dunia inayo pita, mpaka ifike Siku ya Kiyama.
Rudi kwenye Sura
99. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka watu wote katika ardhi
waamini, wangeli amini. Basi wewe usihuzunike kwa ukafiri wa washirikina.
Wala haiwi Imani ila kwa khiari. Basi wewe huwezi kuwalazimisha watu kwa
nguvu ili wafuate Haki na waitikie. Haikupasii kutaka kuwalazimisha waamini,
wala hutoweza, hata ukijitahidi vipi.
Rudi kwenye Sura
100. Hawezi mtu kuamini ila akiielekeza nafsi yake kwa hayo, na Mwenyezi
Mungu akamsahilishia sababu na njia za hayo. Ama yule asiye ielekea Imani
huyo basi amestahiki kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu, na kupata adhabu
yake. Na mwendo wa Mwenyezi Mungu ni kuwapa adhabu na ghadhabu wale wanao
zipuuza na kuzikataa hoja zilio wazi, na wala hawazizingatii.
Rudi kwenye Sura
101. Ewe Nabii! Waambie hawa wenye inda: Tazameni Ishara zilizo wazi
zinazo onyesha Ungu na Upweke wa Mwenyezi Mungu zilio enea katika mbingu
na ardhi. Lakini Ishara, juu ya wingi wake, na maonyo na yangawa na nguvu,
hayawafai kitu watu wanao kataa na wala hawatumii akili zao. Hawa wanao
kanya kama hawaamini, basi hawatoangalia.
Aya hii na Aya nyingi nyenginezo zinaita watu wajifunze kwa kuangalia
na kuzingatia (Observation). Na inaita watu wajifunze ilimu ya ulimwengu
na viliomo ndani yake, kwani huo ulimwengu umedhalilishwa kwa ajili ya
mwanaadamu. Kisha hizo Aya zinataka watu waingie katika ilimu za kujaribu
(Experimental Science). Kwani hiyo ni njia ya kujua kwa kuona vinavyo onekana.
Rudi kwenye Sura
102. Basi hao wakanyao wanangojea lolote ila kufikiwa na siku za
shida kama zilizo wapata kaumu ya Nuhu, na kaumu ya Musa, na wengineo?
Ewe Nabii! Waambie: Ikiwa mnangojea mfano wa hayo, basi ngojeni! Nami pia
nangojea pamoja nanyi. Na karibu hivi mtasibiwa na kushindwa, na Siku ya
Kiyama mtapata adhabu.
Rudi kwenye Sura
103. Kisha Sisi huwaokoa Mitume wetu na Waumini kutokana na adhabu
hiyo. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewaahidi kuwaokoa, na ahadi yake ni ya
kweli, wala hayendi kinyume.
Rudi kwenye Sura
104. Ewe Mtume! Waambie: Ikiwa mna shaka na ukweli wa Dini niliyo
tumwa kuileta kwenu, basi jueni kuwa kama mtavyo tia shaka mimi kabisa
sitoabudu hayo masanamu mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Lakini
mimi namuabudu Mwenyezi Mungu ambaye mambo yenu yote yapo mikononi mwake.
Yeye ndiye anaye kutoeni roho. Na Yeye ameniamrisha niwe katika wanao muamini
Yeye.
Rudi kwenye Sura
105. Ewe Nabii! Simama sawasawa, umuelekee Mwenyezi Mungu vilivyo.
Wala usijitie katika miongoni mwa walio mshirikisha Mwenyezi Mungu. Epukana
nao, na uwe mbali nao, wewe na Waumini wanao kufuata.
Rudi kwenye Sura
106. Wala usimkimbilie kwa kumwomba na kumuabudu yeyote asiye kuwa
Mwenyezi Mungu. Hao hawakuletei manufaa wala madhara. Ukifanya hayo inakuwa
umekwisha ingia miongoni mwa washirikina walio dhulumu. Na anayo katazwa
Nabii, ndio wanakatazwa umma wake wote. Na hivyo ndio ukomo wa kukanya.
Kwani kumkanya ambaye hayumkiniki kutenda anacho kanywa, ndio hadi ya kukanya.
Rudi kwenye Sura
107. Ewe Nabii! Yakikusibu madhara kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hapana
wa kuyaondoa ila Yeye. Na akikujaalia kheri hapana anaye weza kukunyima
yeyote. Kwani yeye anagawa kheri kuwapa waja wake kwa fadhila yake. Na
Yeye Subhanahu ni Mkunjufu wa maghfira, Mkuu wa rehema.
Rudi kwenye Sura
108. Ewe Mtume! Fikisha wito wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote! Na
waambie: Enyi watu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteremshieni Sharia ya Haki
kutokana naye. Anaye taka kuongoka basi afanye haraka. Kwani faida ya uwongofu
wake utamrejea mwenyewe. Na mwenye kushikilia upotovu utamuangukia mwenyewe.
Na mimi sikuwakilishwa nikulazimisheni muamini, wala kukutawalini.
Rudi kwenye Sura
109. Ewe Mtume! Thibiti juu ya Dini ya Haki. Na fuata wahyi ulio
teremshiwa, nawe uwe na subira kwa maudhi yanayo kufika kwa ajili ya Njia
ya Da'wa (Wito), mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yako na wao, kwa vile
alivyo kuahidi kuwa atawapa ushindi Waumini, na watahizika makafiri.
Na Yeye ndiye mbora wa mahakimu.
> Rudi kwenye Sura