Sifa
njema zote anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote, na rehema na
amani zimshukie aliye khitimisha Mitume
wote, Bwana wetu Muhammad, na Aali zake, na Masahaba wake, na walio wafuata.
Ama
baada:
Qur'ani
ni maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyo mteremkia Muhammad s.a.w. kwa ajili ya
kupambana na kushinda kuwa ni muujiza wa kiibada kwa kusomewa sisi kwa
kupokewa, yaliyo kusanywa baina jalada mbili tangu Sura ya Al-Fatiha (Al-
hamdu) mpaka Sura ya Annas (Qul Audhubi Rabbi nnas). Mwenyezi Mungu
ameiteremsha kwa Mtume wake wa mwisho ili iwe ni Kitabu cha mwisho kuwateremkia
watu wote, chenye kukusanya yaliyo na kheri kwa wanaadamu na maslaha ya hali
zao za sasa na za baadaye, za dunia yao na Akhera yao, ikiteremka kwa mapande
mbali mbali, kwa Aya na Sura kwa mujibu wa haja ya mambo yanavyo tokea katika
muda wa miaka ishirini na tatu katika maisha ya Mtume s.a.w. Baadhi yake hii
Qur'ani iliteremka kabla ya kuhama kwake kutoka Makka kwenda Madina, na baadhi
yake nyengine ni baada ya kuhama kwake. Na Aya na Sura za Makka zilizo shuka
Makka aghlabu yake zinakusanya misingi ya itikadi za Imani ya Mwenyezi Mungu,
na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Mwisho. Kisha
zikateremka Aya na Sura za Madina. Na hizo zinakusanya mambo ya ibada, na mambo
ya matawi, na hukumu za Sharia.
Ndani
yake zimo khabari za kabla yetu na khabari za baada yetu, na hukumu za baina
yetu sisi.
Zimo
khabari za umma walio kuwepo kabla yetu na karne zilizo kwisha pita, ndani yake
zimo hadithi za Manabii na Mitume, na mataifa na makundi na watu, na vituko, na
mambo, na nyendo za taarikhi (historia) za jamii za kibinaadamu zenye
mazingatio kwa mwenye kuzingatia, na mawaidha kwa mwenye moyo au mwenye kutega
sikio naye anaona, na zinatamka kwa mtindo wake Mwenyezi Mungu ambao hawendi
kinyume katika kuwateketeza wapotovu walio dhulumu, na kuwaokoa waongofu walio
kwenda sawa. Na kwamba dunia ya watu, na hata ikipitiwa na miaka mingi na
dahari haiwezi kusilihi bila ya Dini ya Mwenyezi Mungu. Na kwamba kwa hakika
wanaadamu, vyo vyote vile walivyo, hawawezi kufikilia mafanikio wanayo yatafuta
ila wakiongozwa na uwongofu wa Mwenyezi Mungu na Ujumbe wake.
Na
katika hiyo Qur'ani zipo hukumu za kutatua matatizo yaliyo baina yetu, na
masuala ambayo yanahitajia kubainishwa na kuwekwa sawa katika mambo ya itikadi
na mambo ya fikra, na masuala ya akhlaki, na mwenendo, na maingiliano katika
yaliyo khusu fedha, na mambo ya ibada, na hukumu za baina ya watu binafsi na
zisio kuwa binafsi. "Enyi watu!
Hakika umekufikieni uthibitisho kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na
tumekuteremshieni nuru iliyo dhaahiri." Annisa 4.174
"Na tumekuteremshia Kitabu hiki
kinacho eleza kila kitu, na ambacho ni uwongofu na rehema, na bishara kwa
Waislamu." Annah'l 16.89
Hapana hukumu ya Sharia ya Dini au hukumu au tatizo
lolote lilio gusana na dunia ya watu na maisha yao, au linazama katika maisha
hayo ila utayakuta yote hayo katika Qur'ani kama mshipa unao pwita, au chemchem
isiyo kauka. Na utakuta humo uwongofu, na ufafanuzi na uwongozi ama moja kwa
moja kwa uwazi, au kwa makisio."Bila
ya shaka imekwisha kujieni nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Kitabu kinacho
bainisha, ambacho kwacho Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake
katika njia za salama, na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri
yake, na huwaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka." Al-Maaidah 5.15
Naam, hakika bila ya shaka yoyote hii Qur'ani tukufu ni mwenge wa uwongofu ulioko njiani kuwaongoza wanaadamu wote, na kuwatoa kwenye giza kuwapeleka kwenye nuru, na kuwashika mkono kuwasogeza kwenye Haki na kwenye Njia Iliyo Nyooka. Na hapo ndipo pahala pa kuondokea katika taarikhi yake ndefu, kubadilika katika uhai wake wa madhambi na uharibifu na upotovu kuendea maisha ya kheri na Haki na uwongofu, na ndio yakatokea katika ulimwengu wote ya vipimo na kufahamu vyema na mazingatio yaliyo mnyanyua mwanaadamu kutoka kiwango cha chini kabisa na kumfikisha katika cheo cha juu cha kuzagaa na kukamilika.
Uwongofu
na maana ziliomo ndani ya Qur'ani ambazo zilizo tangulia kuashiriwa haziwezi
kujuulikana ila kwa kufasiriwa, yaani
kuelezwa ile matini ya Qur'ani yenyewe na Aya zake. Na Tafsiri ni kuweka wazi makusudio ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na
ujuzi wa makusudio haya kwa maneno yake katika hii Qur'ani ni kwa kiasi ya
uwezo wa kibinaadamu. Na ilimu ya Tafsiri
ilianza kidogo kidogo, na ikakua kidogo kidogo mpaka ukakamilika muda wake, na
ikafikilia kiwango cha kukua kwake. Ikawa hiyo Ilimu ya Tafsiri katika sura ya
kushangaza tuijuavyo hii leo. Kwani katika zama za Mtume s.a.w. haikuwapo haja
kubwa ya kuipanga Tafsiri, wala kuitunga Ilimu ya Tafsiri, kwa sababu Qur'ani
kwa jumla yake ilikuwa iwazi na ikifahamika kwa Mtume s.a.w. na Masahaba zake.
Na juu ya hivyo mwenyewe Nabii s.a.w. alikuwa akitoa tafsiri za baadhi ya
Aya na maneno ambayo huenda yalikuwa
yakifichikana makusudio yake. Na Masahaba nao na Taabii'na, walio wafuata, na
walio wafuatia baada yao kadhaalika walikuwa pia na Tafsiri zao zilizo kuwa
zinakhitalifiana maoni yake, na ambazo zikileta majadiliano kwa sababu kadhaa
au kadhaa ambazo haziachi kutokea katika umma mchanga mwanzoni unapo chipuka
kukomboka, na ukaingia katika misukosuko ya taarikhi, na majadiliano ya
kimadhehebu, na khitilafu za fiqhi na siyasa.
Qur'ani,
basi, haikuacha kuwa, na mpaka sasa ingali kuwa ndiyo ya kati katika utamaduni
wa Kiislamu, na harakati za fikra na mambo yote ya kiakili, na hizo Aya zake
zimehimiza watu waziangalie na wazizingatie. Kwani amesema Mwenyezi Mungu
Mtukufu: "Na hiki Kitabu,
tumekiteremsha kwako kimebarikiwa, ili wapate kuzizingatia Aya zake, na wenye
akili wawaidhike." S'ad 38.29
Na
akasema: "Hawaizingatii Qur'ani? Na
lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani
yake khitilafu nyingi." Annisa 4.82
Na
pia akasema: "Je! Hawaizingatii hii Qur,ani? Au kwenye nyoyo zao pana
kufuli?" Muhammad 47.24
Na
Tafsiri ya haya haiwezi kuwa natija yake ila ni kuwaza na kuzingatia, na maoni
ya wenye kufasiri bila ya shaka yamekhitalifiana, na kadhalika njia zao na
mbinu zao katika tafsiri.
Miongoni mwao wapo
walio pendelea makindano ya fikra za itikadi wakajitawanya
vikubwa mno katika kuzichambua Aya zilizo khusikana na hayo, na tafsiri zao
zikaonyesha kumili upande huo zaidi. Na wapo wengine walio vutika na migogoro
ya lugha na ufasihi. Basi wakajitawanya vikubwa mno katika uwanja huo. Bado na
wengine walio vutika na mizozano ya Fiqhi na Sharia, na wao wakajitawanya pia
katika midani hiyo, na hali kadhaalika walio jitawanya katika masimulizi ya
hadithi na khabari na walio jitawanya katika mambo ya akhlaki na tasawwufu na
mawaidha na Ishara za Mwenyezi Mungu katika nafsi na katika viumbe na mfano wa
hayo. Kadhaalika wapo wafasiri walio endelea kueleza kwa urefu mpaka
wakachosha, na walio fupisha mpaka ikawa hawakueleza kitu. Na wapo walio kuwa
wakati na kati, baina ya hawa na hao. Na wapo ambao walio mili kufuata tafsiri
za kizamani zilizo pokewa, na wapo ambao wanao tumia maoni yao wenyewe. Wapo
wenye mtindo wa kufasiri kwa njia za kubania bania zisio kuwa nyepesi kufahamika,
na wako wanao andika kwa njia ya uwazi. Na wote, wa pande zote, wametuachia
utajiri mkubwa wa ilimu, na mawazo ya akili yanayo pelekea mastaajabu na
kuyathamini, na yapasa sifa kwa umma ulio tumikiwa Kitabu cha Mola wao Mlezi
kwa mfano usio pata kutokea kwa kitabu chochote duniani, kwa kuhifadhiwa, na
kudhibitiwa, na kuchambuliwa, na kuchujwa, na kutukuzwa, na kutakaswa kwa muda
wa karne kumi na nne, zikifuatiwa na karne na karne nyengine mpaka Mwenyezi
Mungu atapo irithi ardhi na vilio juu yake. "Hakika
Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutakao
ulinda." Al-H'ijr 15.9
"Na bila ya shaka hayo ni Kitabu
chenye nguvu. Haitakikifia baat'ili mbele yake wala nyuma yake; kimeteremshwa
na Mwenye hikima, Msifiwa." Fuss'ilat 41.41
Fikra
zinazuka mpya, na tamaduni mbali mbali zinatiana mimba, na maisha yanageuka, na
kila siku mpya yanazuka mawazo mapya ya mwanaadamu. Kila zama zikiendelea mbele
wanaadamu wanazidi kukaribiana na kuchanganyika, na njia za kuwasiliana na
maendeleo zinasaidia hayo, kana kwamba wanataka kufasiri kwa kitendo kauli ya
Qur'ani isemayo: "Enyi watu! Hakika
Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanmke. Na tumekujaalieni kuwa ni
mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa
Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kujua Mwenye khabari." Al-H'ujurat 49.13
Na kuyashikilia waliyo yasema watu wa mwanzo, bila ya kuleta lolote jipya au kuanzisha ni kuacha kuwa na maendeleo na kubakia nyuma. Na kuwa na uwezo juu ya mageuzo na kutafautisha baina ya kavu na nono, na mzozano wa kubakia, na kubakia linalo faa, ni alama ya uhai, na ndio akili ya maisha, na ndio mwenendo wa Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake. Na Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni bahari isiyo kuwa na ufukwe, wala kina chake hakitambulikani, wala ukubwa wake hauweleweki.
Huchoki kukichungua na
kukizingatia,
wala hukomi kukifikiri
kwa kuendelea.
Kwa kila kipindi
ukikyangaza
Uzuri jadidi wa
kushangaza
Haya
ndiyo yaliyo fungua fursa kwa kila yanayo patikana katika Tafsiri na wenye
kufasiri.
Na
haya ndiyo yaliyo ikabili Baraza Kuu ya Mambo ya Kiislamu (ya Misri) hata
ikaunda halmashauri za ilimu za mabingwa wanazuoni wakubwa wakubwa, na
wachunguzi wataalamu na watu wa fikra, ili washughulikie kutunga Tafsiri kwa
njia za kisasa, nyepesi, iliyo kunjuka, yenye ibara wazi, mukhtasari, si tupu
wala haichoshi, haina khitilafu za kimadhehebu, wala maneno maneno ya kifundi
fundi ya kutatanisha, na kujaza jaza itikadi za maneno, ili iwe katika hali ya
kusilihi kutarjumiwa katika lugha nyengine za kigeni, ambazo inatarajiwa
wasemao lugha hizo wasome yaliomo katika Qur'ani hii na wafahamu itikadi na
misingi, na mafunzo ya kuwaongoza, kutimiza waajibu ulio juu ya shingo zetu, sisi
tunao sema lugha ya Kiarabu, nao ni kutarjumu maana ya Qur'ani kwa wasio kuwa
Waarabu ili ipate kuwa sahali Ujumbe wa Muhammad kuwafikilia watu wote na
wangakhitalifiana ndimi zao na rangi zao. Kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
"Na hatukumpeleka Mtume yeyote isipo kuwa kwa lugha ya watu
wake ili apate kuwabainishia." Ibrahim 14.4
Ilivyo kuwa Ujumbe wa Mtume s.a.w. ni kwa watu wote, na yeye ni Mwaarabu mwenye kusema lugha ya Kiarabu basi hapana shaka Ujumbe wake lazima ufike kwa wasio kuwa Waarabu kwa njia ya tarjama itakayo chukua pahala pa asli, na kwa hii tarjama iliyo sawa na sahihi yenye kufuata uaminifu, iliyo simama juu ya kufahamu na kuelewa kwa huyo mwenye kutarjimu. Na huyo mtarjimu tunamfungia njia asiziendee tarjuma chungu nzima zilizo potolewa makusudi kwa kujazwa uharibifu na upotovu.
Na
tafsiri fupi itakuja fuatwa karibu na tafsiri nyengine ya ukunjufu zaidi
kidogo, yaani yenye kuzidi uchunguzi na uangalizi, na kuchambua ibara na
ufasihi na mafunzo, na uwongozi wa kuwashika mkono Waislamu ili wazindukane na
waendeshe maisha yao kwa mujibu kama waadhi huu wenye hikima unavyo wataka
washike njia za kuwaletea nguvu, na utukufu na hishima. Na humo mnaashiriwa
mambo yanayo ongozwa na Aya zake kwenye sharia za maisha, na siri za ulimwengu,
na mambo yake ya ki-ilimu ambayo yalikuwa hayakuwa yakijuulikana ila katika
zama hizi za mwisho kwa kuvumbuliwa na sayansi. Na hayumkini kuwa Qur'ani
kuyaashiria mambo hayo hapo zamani ila kwa kuwa hayo si maneno ya mwanaadamu
bali ni maneno ya Mwenyezi Mungu Muumbaji Mwenye Nguvu na Uweza, ambaye
ameahidi kwa uwazi katika Kitabu hichi hichi: "Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi
zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwa Mola
wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?" Fussilat 41.53
Na
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuwezesha.
HALMASHAURI YA QUR'ANI NA SUNNA.