Ukitaka hakika ni kweli kuwa mtu ye yote anayesoma hizi hizi
Injili ziliomo katika Biblia kwa uangalifu ataona ushahidi wa nguvu kuwa huyo
aliyetundikwa msalabani hakufa hapo msalabani, bali alionekana tu
Ni wazi kuwa Yesu wakati ule hakuwa mtu maarufu katika mji wa Yerusalemu.
Alikuwa ni mgeni kwa wale waliokuwa wakimsaka. Yeye alikuwa mshamba,
ametoka huko Galilaya. Tangu kuanza kuhubiri ni kiasi ya miaka miwili
mitatu tu, naye akitanga tanga huku na huku bila ya kutulia, hata hakuwa na
pahala pa kuweka kichwa chini. (Mathayo 8.20). Mnamo wakati huo hakupata kwenda Yerusalemu
isipokuwa mara chache tu. Marko anasema alikwenda mara moja, na Yohana anasema
mara nne. Jinsi ya kuwa hajuulikani vyema hata ikalazimu Yuda amtambulishe
kwa kumbusu; alisema: "Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni."
(Mathayo 26.48). The Interpreter's Bible kutafuta kijisibabu kwa
huko kumuashiria kwa kumbusa inasema: "Yesu angejuulikana bila ya
ishara, lakini wale waliokuja kumkamata hawakutaka kubahatisha kwa sababu
makosa yaweza kutendeka kwa wepesi wakati wa usiku, na khasa pangetokea
pata-shika." Vyo vyote vile iwavyo, ikiwa ni kwa ugeni, ikiwa ni
kwa giza la usiku, au ikiwa kwa ghasia na fujo lililokuwapo, ni jambo
lilioelekea sana kumkosea Yesu akakamatwa mtu mwingine. Wafuasi wake wote
walimkataa, hata Petro naye ambaye alikuwa karibu mno na Yesu katika wanafunzi
wake wote, naye pia alisema: "Simjui mtu huyu". (Mathayo
26.74). Basi je, tuukatae na kuutenga kando ushahidi wa wanafunzi wake wote
wanaoitwa Watakatifu tuukubali wa khaini, msaliti mmoja, Yuda? Tena hata
yeye hakuutoa ushahidi wake mahkamani, baada ya kuapishwa, bali huko huko
kwenye vurugu kizani, tena ni kwa ishara tu ya kumbusu, ambayo tunaambiwa na
waandikaji kwamba walikubaliana baina yake Yuda na askari wa Kirumi faraghani,
ambako bila ya shaka yo yote hao waandikaji au waliowasimulia hawakuwapo. Hayo
ni mambo ya dhana tu. Kuambiwa tena kuwa hayo nayo yalikuwa ni kutimiza bishara
za Agano la Kale, au zake mwenyewe Yesu, ni hadi ya kuilazimisha imani ikubali
lisilokubaliwa na akili.
Tena hebu tuzichungue jawabu alizozitoa mshtakiwa huko mahkamani. Hadi yake
tunaweza kusema kuwa hizo jawabu ni za ubabaishi. Injili tatu za mwanzo,
nazo ndizo zenye kueleza maisha ya Yesu, zimeshindwa kutoa ushahidi hata mmoja
kuthibitisha kuwa ni nani khasa huyo mshtakiwa. Injili ya Luka inasimulia
kuwa alipoulizwa barazani: "Kama wewe ndiwe Kristo, tuambie."
Akawaambia: "Nijapowaambia, hamtasadiki kabisa."
Na alipoambiwa: "Basi wewe ndiwe Mwana wa Mungu?"
Akawaambia: "Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye."
Maana ya kauli hiyo sio maana yake kukubali yasemwayo, bali ni kukanya na
kumsukumia jukumu yule amuulizae na kumtuhumu kwa hayo - yeye hakimu
pamoja na wote waliozua hayo mashtaka. Na vyo vyote alisemalo hasadikiwi, kwani
waliomkamata wamesha kata shauri kuwa yeye ndiye Yesu Kristo, na hali siye.
Basi hapana haja ya kusema lo lote.
Katika Injili ya Marko tunasoma: Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe Mfalme wa
Wayahudi?
Akajibu, akamwambia: "Wewe wasema." Nao wakuu wa makuhani
walikuwa wakimshitaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena akisema:
"Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki!"
Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu.
Kama alivyojibu kuwa yeye si Mfalme wa Wayahudi, hali kadhaalika si Mwana wa
Mungu, wala si Kristo. Kwa suala zote tatu hizo mshtakiwa anasema kuwa
hayo wanayasema wale wanaomshtaki, si yeye.
Kadhaalika Injili ya Mathayo inatwambia: Naye Yesu akasimama mbele ya
liwali; liwali akamwuliza, akasema,"Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?"
Yesu akamwambia: "Wewe wasema."
Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno.
Ndipo Pilato akamwambia: "Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?"
asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana. Na sote lazima
tustaajabu. Ikiwa yeye ni Yesu, Kristo, Mwana wa Mungu, kama ilivyodaiwa kuwa
anadai, kwa nini hakubali? Hapo mahkamani sipo khasa pa kueneza ujumbe wake?
Zingatia vyema kuwa hadithi hizi ziliandikwa miaka mingi baada ya kutokea hayo
mambo, tena zimeandikwa na watu wenye kuamini kabisa kuwa huyo aliyekamatwa na
kusalibiwa ni kweli Yesu Kristo, mwana wa Maryam. Juu ya hivyo hata wao
hawakuweza kuleta ushahidi wo wote wa kweli au wa kubuni usipokuwa ule wa Yuda,
msaliti. Huyo mshtakiwa hakukiri hata mara moja kuwa yeye ndiye Yesu
anayetuhumiwa. Na wanafunzi wake nao hawakumtambua wala hawakukiri kuwa wao
wanamjua, bali walikataa kwa nguvu, na wakamkimbia.
Tukizingatia haya kwa usafi wa nia na kwa kutumia akili zetu bila ya kugubikwa
na mawazo na imani tulizozoeshwa tangu utotoni, na pia tukatia maanani yale
tuliyokwisha yasimulia yaliyomo katika Injili nyenginezo zisiokubaliwa na
Kanisa, pamoja na nyaraka za kale zilizogundulikana karibuni zinazotufahamisha
nini ilikuwa imani ya Wakristo wa asli ya kwamba Yesu hakufa msalabani, ukweli
wa Qur'ani unathibiti kwa uwazi kabisa:
(Qur'ani) An Nisaa 4.157
Wataalamu
wa Biblia wa nchi za magharibi wa sasa baada ya uchunguzi wanakubali ukweli huu
wa Qur'ani. Na Qur'ani iliteremshwa kwa mtu asiyejua kusoma wala kuandika
miaka elfu moja na mia nne iliyopita.