Wacha Biblia Iseme

Imetungwa na Sheikh Ali Muhsin

Bismillahi Arrahmani Arrahim
Kwa Jina La Mwenyezi Mungu Mwingi Wa Rehema Mwenye Kurehemu

SHUKRANI

Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniongoza Njia iliyonyooka.
Pia nampa ahsante Bw. Kingsley Green, Mwalimu wa biology wa asli ya Kiaustralia aliyekuwa akisomesha Mazengo Secondary School, Dodoma, Tanzania, ambaye kwa kuwa ni mhubiri alikuwa akija kutuzuru gerezani tulipokuwa tumewekwa kizuizini baada ya kupinduliwa serikali yetu ya Zanzibar.  Kwake yeye nilijifunza kuisoma Biblia kwa nidhamu.
Hali kadhaalika nawapa ahsante wahubiri wengi wa Kikristo waliokuwa wakituhubiria nilipokuwako Chuo Kikuu Makerere, na nilipokuwako kizuizini. Kwa wanafunzi wenzangu na wafungwa wenzangu ambao nikijadiliana nao kirafiki katika mambo ya dini nina  deni kubwa la shukrani.
Ni waajibu wangu kushukuru Shirika la Kimataifa la Msamaha (Amnesty International) kwa kuniletea vitabu nilipokuwa kizuizini, ambavyo vitabu hivyo vimenisaidia sana kunizidishia  maarifa juu ya mawazo ya Kikristo ya hivi sasa.
Sina fadhila ya kumlipa Baba yangu mzazi, Sheikh Muhsin bin Ali Barwani (ambaye kwake ndio nimesoma sana ilimu za dini ya Kiislamu), na kaka yangu Sheikh Muhammad Muhsin, na mashekhe na walimu kadhaa wa kadhaa wengineo niliosoma kwao.  Miongoni mwa hao ni Sheikh Abubakar Baakathir, Sheikh Muhammad bin Omar Al Khatib, Sheikh Suleiman Al Alawy, Sheikh Burhan Mkelle, Sheikh Abdulrahman Muhammad Al Kindy, Sheikh Said bin Abdulla Lindi, na Sheikh Abdulla Saleh Al Farsy. Pia nawashukuru kwa kuniongoza kwa nasaha na mifano Habib Omar bin Sumeit, Sayyid Ahmed bin Husein, Sheikh Abdulla Muhammad Al-Hadhramy, Sheikh Muhammad Abubakar, Sheikh Muhammad Salim Barwani (Jinja), Sayyid Hamid Mansab na Sheikh Abdulla bin Suleiman Al Harthy. Sina la kuwalipa ila kuwaombea Mwenyezi Mungu awarehemu, na kama itapatikana faida yo yote kwa walionifundisha basi thawabu zake zirejee kwao mashekhe na walimu wangu niliowataja na nisiowataja.
Mwishoni siwezi ila kumshukuru mwenzangu wa maisha, mzazi mwenzangu, Azza bint Muhammad bin Seif, ambaye kwa subira yake na ushujaa wake na imani yake iliyo kubwa, ndio nikaweza kubeba taabu za kizuizi zaidi ya miaka kumi, huku yeye peke yake akijitazama mwenyewe na watoto wetu, naye yupo uhamishoni kama ni mkimbizi katika nchi ya ugeni Misri.  Ingelikuwa si yeye na wema wa wahisani wetu wa Kimisri, na khasa  katika wao Dr. Abdoh Sallam, Bw. Fathi Sabri, Dr. Mustafa Momen, Dr. Farid Abul Ezz, Bw. Hilmy Shaarawy, Bw. Bahgat Disouqy na Dr. Muhammad Abdul-Aziz Is'haq, mimi nisingekuwa na tamakuni ya moyo hata nikaweza kusoma nilikosoma, kuchungua nilikochungua, na kuandika nilikoandika nami nimo katika utumwa wa kifungoni.
Taarikh 2 Ramadhani mwaka 1409 A.H. iliyo wafikiana na 7 Aprili 1989, mwenzangu wa miaka 45, Mama Azza, aliniacha mkono, Mwenyezi Mungu akamkhitari. Shida na taabu zilizo mpata kwa yaliyo tokea kwetu, na kifungo changu, na maisha ya ukimbizi kwa robo karne, yalimuathiri afya yake sana na mwisho ndio akanitoka katika umri wa miaka 63.
Fadhila ya uchapishaji kitabu hichi kwa Kiswahili na kabla yake kwa Kiingereza inarejea kwa Muislamu mtenda wema, Dr. Moawiyah Shunnar wa Dubai, Mwenyezi Mungu amjaze kila kheri.