Mt Paulo alikuwa Myahudi aliyezaliwa katika mji wa
Alipokuwa yuko njiani anakwenda Dameski (Dimishqi) miaka kadhaa wa kadhaa baada
ya Yesu kwisha ondoka duniani, yasemekana kuwa Paulo alijiwa na Yesu ambaye
alimwambia maneno fulani. Tangu hapo akaingiwa na hamu kubwa ya kutaka kuwaita watu
waingie katika dini ya Kikristo. Juu ya hivyo huo Ukristo wa Mt Paulo
aliodai kuwa umefunuliwa kwake na Yesu mwenyewe, ni namna mbali kabisa na
Ukristo waliokuwa wamefunzwa wanafunzi wake Yesu, alioweteuwa mwenyewe na
akawafunza katika uhai wake. Kwa hivyo pakatokea mzozano mkubwa baina ya
Paulo na wanafunzi wa Yesu wa asili, ambao walikuwa wanashikilia kufuata sharia
ya Musa, kama alivyokuwa akiifuata mwenyewe Yesu.
Kwa kuwa alielewa vyema ilimu na ustaarabu wa Kirumi na Kiyunani (Kigiriki), na
kuwa alikuwa ni mtu mwenye akili, Paulo aliweza upesi kuwa ni kiongozi katika
wale wanafunzi wa Yesu, ijapokuwa yeye hakika hakupata kumwona Yesu ila katika
hiyo ndoto iliyomjia alipoanguka njiani kwa kupigwa jua kali. Kwa uhodari wake
aliweza kuathiri sana mawazo na fikra za dini ya Kikristo kama inavyojuulikana
hii leo. Jinsi mawazo yake yalivyotawala na kuenea hata baadhi wanamwona
kuwa ni yeye ndiye muanzishaji wa Ukristo. Mafunzo ya imani ya Paulo
hayakutegemea sana juu ya maneno na vitendo vya Yesu kama yalivyotegemea juu ya
falsafa za Kigiriki, itikadi za Kiyahudi, na itikadi za kipagani (kishirikina)
zilizokuwa zimeenea katika eneo lile la dunia wakati ule. Kwa hivyo utaona kuna
mkorogo na migongano katika imani ya Mungu mmoja kama alivyokuwa akiamini Yesu
pamoja na Mayahudi wote, na imani ya miungu kadhaa kama walivyokuwa wakiamini
mapagani wa Kirumi, Kigiriki, Kimisri na Kiajemi katika zama zile. Utaona
mgongano baina ya imani ya wanafunzi wake Yesu kuwa Yesu hakuuliwa msalabani,
na imani ya Mayahudi kuwa wamemwua kwa kumtundika msalabani na kwa hivyo kafa
kifo cha laana, kama isemavyo Taurati kuwa anayekufa kwa kutundikwa huyo ni
mlaanifu. Kwa uhodari mkubwa Paulo alikusanya ya huku akachanganya na ya huku
akaunda hii ijuulikanayo kuwa ni Thiolojia (ilimu ya Ungu) ya Kikristo. Yeye
alikuwa ni mhubiri mwenye hima na hamasa kubwa, na alikuwa tayari, kama
anavyojisifu mwenyewe, afanye lo lote ili makusudio yake yatimie, yaani apate
wafwasi wengi kama inavyowezekana.
Barua zake alizokuwa akiwapelekea Wakristo mbali mbali zimo katika Biblia na
zinahisabika kuwa ni sehemu ya Agano Jipya. Muhimu katika mafunzo yake ni kuwa
mtu anapata haki kwa imani si kwa vitendo, na imani ya kwamba kila mwanaadamu
kazaliwa na dhambi ya asili ambayo haifutiki ila aamini kuwa Bwana Mungu
kamleta mwanawe wa pekee kuja duniani ili ateseke na auliwe msalabani kuwa kama
ni kafara ya hiyo dhambi ya tokea Adam. Hayo yanatosha. Kufuata sharia sio
muhimu. Ni yeye Paulo ndiye aliyeondoa na kubatilisha sharia ya tangu
Ibrahim ya kuingia tohara, na kuwa nyama wasiochinjwa, na nguruwe ni
haramu. Sharia zote ambazo Yesu na wanafunzi wake wote walikuwa
wakizifuata Paulo alifunza kuwa hazina maana. Haya yalikuwa na maana kabla Yesu
hajajitoa mhanga msalabani. Baada ya hapo litakikanalo ni Imani tu ya
uwokozi wa watu kwa kifo cha Yesu msalabani.
Jengine lililoleta ugomvi baina yake Paulo na wanafunzi wa asili wa Yesu ni
kuwa mafunzo ya Yesu kwenda kufunzwa kabila nyengine zisiokuwa Wana wa Israili,
ndio hao waitwao "Mataifa" katika Biblia. Wanafunzi wa Yesu kwa
kufuata amri zake mwenyewe alizohimiza mara kadhaa wa kadhaa walipinga shauri
ya Paulo kutaka kuwahubiria dini watu wasiokuwa Bani Israili. Paulo kwa ukaidi
wake, na werevu wake mwingi aliwashinda nguvu wanafunzi wa Yesu waliopewa jukumu
kuitangaza dini katika taifa la Israili tu.
Paulo aliuliwa kwa kukatwa kichwa karibu na Roma baina ya mwaka 61 B.K. na 68
B.K.