16- MWILI NA DAMU YA YESU

Yesu alipobashiri kuja kwa huyo "Msaidizi" ambaye atauhakikisha ulimwengu kwa khabari ya dhambi kwa sababu watu walikuwa hawamuamini yeye, alikuwa anasema kweli tupu.  Kwani yeye alikuwa kawajia Waisraili ambao walikuwa wakishikilia sana kufuata madhaahiri ya sharia na wakapuuza undani wake.  Wakiitenda sharia ila imani yao ilikuwa chache, na uchamngu wao ulikuwa dhaifu. Jitahada yake ilikuwa bure kuwahimiza kuwa yapasa vitendo vyao vinavyoonekana vichanganyike na imani ya roho.   Alijaribu kuwafanya wafahamu khitilafu iliopo baina ya mikazo inayoletwa na wanaadamu na sharia za milele za Mwenyezi Mungu. Aliwaambia:

Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu.

Marko 7.9

Yesu hakuanzisha sharia yo yote mpya.  Kazi yake ilikuwa kuitimiza sharia ya Musa kwa uchamngu.  Lakini baada yake ulizuka mzozano juu ya tafsiri ya sharia. Kikundi kimoja miongoni mwa wafuasi wake kiliona kuwa maadamu yeye ni Muisraili aliyefuata sharia na hataki kutengua sharia hata nukta moja, basi ni waajibu kwa wafuasi wake wote wafuate sharia kwa kila neno, kama yeye, hata katika mambo ya kutahiri, na kuacha kula nyama za haramu kama nguruwe na visivyochinjwa kisharia na damu, na kuitukuza Jumaamosi kuwa ni siku ya Sabato. Hawa ndio wanaitwa Wakristo wa Kiyahudi.  Kikundi kingine, na mkubwa wao ni Paulo, kilichoathirika na upagani wa Kizungu, kiliona uzito kujifunga na sharia za Musa. Kilitoa hoja kuwa maadamu Yesu hakutoa sharia mwenyewe basi wao ni huru, kwani Yesu kwa kufa msalabani damu yake imekwisha wakomboa wanaomuamini na mikazo ya sharia. Sharia ni laana, na Yesu kwa kufa kifo cha laana msalabani amechukua yeye dhambi za watu, na vile vile ameondoa laana ya sharia. Liliokuwa la lazima si matendo ya sharia bali kuamini tu kuwa Yesu amekufa msalabani kwa ajili yao. Huo ni uokofu wa kutosha. Ili imani hii iingie na isaki katika akili na nyoyo za waumini ikazuliwa hiyo ibada iitwayo Ekaristi, au Chakula cha Bwana, Ushiriki au Misa takatifu. Katika ibada hii ya kuonyesha neema ya dhaahiri na ya ndani, au ya kiroho, huliwa kidogo mkate uliobarikiwa, na hunywewa mvinyo kidogo iliyobarikiwa, kwa kuwa ni mwili na damu ya Yesu. Injiili inasema:

Nao walipokuwa wakila, Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle;  huu ndio mwili wangu.  Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.

Mathayo 26.26-28

Upton Sinclair katika kitabu chake A Personal Jesus anatoa maoni yake juu ya maneno hayo ya Injili tuliyoyanukulu:

"Kutokana na hayo umetokea mtindo uitwao Ekaristi, Ushiriki, Misa:  ibada ya taadhima isiyokadirika.  Badala ya kumtoa mhanga mwana kondoo asiyejifaa kitu, ni mwili wa Yesu uliotolewa mhanga msalabani, na damu yake iliyomwagwa, na kwa mageuzo ya ajabu mkate na mvinyo ikawa ni mwili wake na damu yake, na wewe unakaa kwa unyenyekevu ukila na ukinywa au unamuacha padri akulie na akunywie.  Mamilioni na mamilioni ya maneno yametumiwa katika kuhojiana, na maelfu ya vitabu vimepigwa chapa juu ya suala hili; vipi mageuzo hayo yanatokea...Wakatoliki wanaamini hayo wanayoyaita Mahudhurio ya Hakika (Real Presence); yaani, wanasema kuwa ule mkate na ile mvinyo hakika inakuwa ni mwili na damu, ijapokuwa sura yao inabaki vile vile kama mkate na mvinyo.  Wote Wakatoliki wachamngu huenda kila wiki waone kitendo hichi kikitendwa na padri, na tena hapo ndio wanajua kuwa roho zimesalimika na moto wa jahannam.  Mimi sitaki kumuudhi mtu ye yote, na kwa hivyo najitosheleza nafsi yangu kwa kusema kuwa mimi siamini kuwa Yesu alikuwa akishughulikia mtindo huu."


Marcello Craveri anasema juu ya jambo hili hili katika kitabu chake The Life of Jesus (Maisha ya Yesu):

"Ikiwa tunaamini kuwa Yesu ni mwanaadamu, basi hichi Chakula cha Bwana (Misa au Ekaristi) kinakuwa na sifa ya ibada ya wala-watu; ikiwa tumfanye kuwa ni Mwana wa Mungu, ile fikra safi na tukufu ya Mwenyezi Mungu ambayo mwenyewe Yesu akiishika, inaporomoka chini na kuwa ni itikadi ya mungu dhaalimu asiye na huruma anayetaka daima dawamu Mwanawe mteule atolewe kikoa."


Mtaalamu huyo wa Kitaliana ameendelea kueleza katika kitabu chake kuwa mtindo huu kwa hakika ameuzua Paulo kufuata mitindo ya kikafiri (kipagani) iliyokuwa imeenea wakati ule katika pande zile.  Anaendelea kusema:

"Maandishi ya Injili yakajazwa kwa kuongezwa na Paulo, ambaye alibatilisha ukweli wote wa historia (taarikh) kwa ajili ya kufuata maelekeo ya imani yake, na huku akitangaza bila ya kuona haya wala aibu kuwa kila kitu amekipata moja kwa moja kutokana na Yesu mwenyewe.  Ni yeye ndiye aliyemfanya Yesu aseme baada ya kukata mkate: Chukueni, kuleni;  huu ni mwili wangu, uliovunjwa kwa ajili yenu. Na huku akiibariki mvinyo: 'Kikombe hichi ndio agano jipya katika damu yangu.'"


Ushahidi wa kuwa hadithi hiyo, yaani kuwa Yesu kawataka wanafunzi wake wale mkate na mvinyo kuwa ndio mwili wake na damu yake, imezuliwa na kubuniwa na Paulo, umo katika barua yake mwenyewe Paulo aliyowaandikia Wakorintho:

Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliyotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu;  fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.  Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu;  fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.  Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

1 Wakorintho 11.23-26

Marcello Craveri anatwambia:

"Paulo, kwa kuwa aliathirika na dini za mazingaombwe zilizoenea katika jamii za Kigiriki na Kiasia alimoishi yeye, alimchanganya Yesu pamoja na vile vijiungu vya bandia viokozi kama Orfia, Dionisa, Attis n.k. - vilivyokuwa vikiabudiwa na mila hizo.Vijiungu hivi pia viliteseka na vikafa ili viwape watu fursa ya roho zao kufikilia rehema ya kiungu. Waumini waliingizwa katika dini hizo kwa kupitia katakismu (yaani kufahamishwa maana ya tambiko), kufunga, na kusafishwa.  Hapo tena hukubaliwa kuwa ni wanachama wa kaumu ya dini na hupata hifadhi ya mungu. Huweza kuungana au kushirikiana kiroho na huyo mungu mwenyewe kwa kula nyama ya mnyama mtakatifu ambaye ndiye ishara yake.  Nyama na damu ya mnyama yule huingiza sifa na khulka ya mungu katika roho ya mwenye kula nyama na kunywa damu. Kadhaalika Paulo aliwaza mawazo yale ya nguvu za uchawi zinazotokana na ule mkate wa Ekaristi kama wale mapagani makafiri walivyokuwa wakiwaza katika wale wanyama wao wa muhanga."


Yapasa tukumbuke kuwa Mt Paulo hakuwa mwanafunzi wa Yesu wakati wa uhai wake, wala hakuweza kudai kuwa waliwahi kukutana ila  katika hiyo "njozi" aliyodai kaiona alipokuwa njiani kwenda Dameski, na Yesu hayupo tena. Madai yake yote anayategemeza juu ya "ufunuo" huo alioupata.  Kisa hicho kinasimuliwa mara tatu katika kitabu cha Matendo ya Mitume kiliomo katika Biblia, na kila mara hadithi hiyo inakhtialifiana na nyengine, kama tulivyokwisha ona.