17- MAONI YALIYOKAA SAWA
Alipokuja Nabii Muhammad s.a.w. mambo yote yaliwekwa sawa.
Mafunzo safi ya
Musa yalirejeshwa pahala pake, na dini ya Yesu ilisafishwa na kutolewa takataka
za Upaulo. Zote dini hizo mbili, Uyahudi na Ukristo, bali dini zote zilizogeuka
zilirejeshwa kwenye umbo lao la asli lisiloharibika, umbo la Uislamu.
Muhammad s.a.w. alifunza kwa uwazi kabisa juu ya dhambi, na akalegeza mikazo
iliyokuwa imewabana Mayahudi. Alifahamisha kuwa baadhi ya mikazo hiyo ni
matokeo ya inda yao
wenyewe na uasi wao, na mingine ilizuliwa na makuhani wao tu ili wazidi
kuwakandamiza na kuwaendesha watakavyo wafuasi wao. Upande mwingine
hakuwaacha watu wakitangatanga gizani bila ya uwongozi, wala hakuwaacha watu
watende horera watakavyo au kuwaambia watazame maandishi ya kale ambayo jinsi
yalivyo chafuliwa kwa maongezo na mabadiliko hata mtu hawezi kutambua lipi la
kweli na lipi la uwongo, lipi la Mungu na lipi la matamanio ya binaadamu.
Kuachia mambo hivyo huzidisha zogo penye fujo. La! Muhammad alikuja na
Qur'ani, kitabu cha kusomwa, au kwa jina jingine, Furqan, yaani Kitabu
cha kufarikisha, yaani kupambanua, baina ya haki na baatili, baina ya kweli na
uwongo. Alileta Sharia, Sharia ya Kweli ya Mwenyezi Mungu, iliyomkomboa
binaadamu kutokana na minyororo iliyowatatiza Mayahudi, lakini haikuacha mambo
ovyo kila mtu atende atakavyo kama alivyofanya
Paulo kuivunja sharia kabisa. Huo ni utumwa mwingine ambao ni mbaya zaidi, kwa
kuwa ni utumwa wa ubongo na roho, kuuwachilia mwili utende upendalo na
kuifunga akili isifikiri na roho isinawirike. Sharia ya Qur'ani ni sharia ya kati na kati.
Dini ya Kiislamu ni ya kati na kati. Si ya kulia wala kushoto lakini ya kuongoza
mbele moja kwa moja kumfikilia Mwenyezi Mungu. Anasema Mola Mlezi katika
Qur'ani:
Adhabu yangu
nitamfikishia nimtakaye, na rehema yangu imekienea kila kitu. Lakini
nitawaandikia wale wanaomcha Mungu, na wanaotoa Zaka na wanaoziamini Aya zetu,
ambao wanamfuata Mtume, Nabii asiyejua kusoma na kuandika, ambaye wanamkuta
ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, ambaye anawaamrisha mema na
anawakataza maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaondolea mizigo yao na
minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale waliomuamini yeye, na
wakamhishimu, na wakamsaidia, na wakaifuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye -
hao ndio wenye kufanikiwa.
(Qur'ani) Al Aaraf 7.156-57
Huyu
ndiye Roho wa Kweli aliyetolewa bishara yake na Yesu kama ilivyo katika Injili
ya Yohana sura ya 16. Ni yeye ambaye amesimuliwa kuwa "akisha kuja,
huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu...huyo
roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote." Ni huyu
Muhammad s.a.w. ndiye aliyeambiwa Nabii Musa a.s. na Mwenyezi Mungu katika
Kumbukumbu la torati sura ya 18:
Mimi
nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe.
Kumbukumbu 18.18
Mafunzo
ya Nabii Muhammad ndiyo yale ya Nabii Isa na ndio yale ya Nabii Musa na Nabii
Ibrahim na kila Nabii aliyetokana na Mwenyezi Mungu. Msingi wao ni
mmoja. Sharia zaweza kukhitilafiana kwa mujibu wa zama na hali, ama Imani
na mambo ya kiroho na wema na ubaya hayo ni mamoja. Qur'ani imetilia
nguvu sana juu ya Imani, Imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mwingi wa Rehema,
Mwenye kurehemu, Imani kamili ya fadhila na neema ya Mwenyezi Mungu.
Na lau kuwa si
fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu asingelitakasika miongoni
mwenu kabisa hata mmoja.
(Qur'ani) An Nur 24.21
Lakini
kumuamini Mwenyezi Mungu ni kutenda yale ayapendayo. Kama asemavyo Jalaludin
Rumi, mshairi sufi mkubwa: "Ukimuamini Mwenyezi Mungu muamini kwa
vitendo vyako! Atika mbegu, tena ndio mtegemee Mwenyezi Mungu!"
Mswahili akichukua jembe kwenda kondeni husema: "Nenda omba Mungu."
Alikuwapo mtu mmoja akamuuliza Mtume s.a.w. amwachilie ngamia wake naye
akimtegemea Mwenyezi Mungu? Mtume alimjibu: "Mfunge ngamia wako,
ukisha ndio mtegemee Mwenyezi Mungu."
Qur'ani imejaa maneno kama haya: "Wanaoamini wakatenda mema".
Na Yesu naye amefunza haya haya kama yaliyomo katika maneno yake mwenyewe, sio
ya Paulo. Na waraka wa Yakobo, nduguye Yesu, unasema hivyo hivyo.
