Mtume
Muhammad ndiye aliyekuja kumtukuza Yesu. Aliyapinga madai ya Mayahudi
kumshutumu Maryam na kumshutumu Yesu, na akauhakikisha ulimwengu kuwa Yesu ni
mwana wa halali, ni Nabii mtukufu aliyetumwa kwa Wana wa Israili, wala si
maluuni kama walivyodai Mayahudi, na wala si mungu wa bandia wa kishirikina,
kama walivyomfanya Wakristo bila ya wenyewe kutambua nini walitendalo. Kwa watu
wanaoamini kuwa Adam alikuwa hana baba wala mama kwa nini ikawa ni vigumu
kuamini kuwa Yesu alikuwa hana baba? Yohana Mbatizaji anasema:
Mathayo 3.9
Je,
Mungu awezaye kuinua watoto katika mawe, kama alivyomuumba Adam kutokana
na udongo, atashindwa kumzalisha mwanamke bila ya mume? Mtume Muhammad
aliwahakikishia maadui wa Kiyahudi kuwa Yesu ndiye Kristo, ndiye Masihi
ambaye amebashiriwa katika maandiko yao wenyewe. Aliwakanya
Mayahudi walipodai kuwa Yesu amelaanika kwa sababu wao waliweza kumuua kwa
kumbandika msalabani. Qur'ani imesema:
(Qur'ani) An Nisaa 4.157
Utafiti
wa ilimu za kisasa katika masomo ya Biblia unathibitisha huu ukweli wa Qur'ani.
Yajuulikana kuwa zipo Injili nyengine zenye maelezo mbali juu ya mateso ya Masihi
yanayokhitalifiana na ya hizi Injili nne zilizokubaliwa na Kanisa. Katika miaka
ya karibuni mwangaza mpya umepatikana kutufahmisha nini khasa zilikuwa
imani za wale Wakristo wa mwanzo. Zimepatikana nyaraka za zamani sana ambazo
ziko katika jumba la kuhifadhi nyaraka huko Istambul, Uturuki. Aliyegundua ni
Dr. Samuel Stern wa Chuo Kikuu cha Oxford. Wale Wakristo wa kwanza, ambao
wakiitwa Wanasoria au Wanazaria (ambayo yanaelekana na jina litumiwalo katika
Qur'ani kuwaita Wakristo "Wanasara") hapo awali ndio waliokuwa
wengi na wenye nguvu. Hao Wanasara wakidai kuwa wao wamezalikana na
wanafunzi wake Yesu wa kwanza kabisa. Wakaja wakapambana na Wakristo
wamfuatao Mt Paulo. Hao Wanasara wakimuamini Yesu kuwa ni Nabii mtukufu
na mwanaadamu mwema mwenye haki. Wakamshutumu Paulo kuwa amezua kwa
kutumbukiza mila za Kirumi badala ya mafunzo ya asli ya Yesu, na kumsingizia
Yesu kuwa ni Mungu. Walikataa kusherehekea Krismasi kwa kuwa waliona hiyo
ni sikukuu ya kikafiri ya kipagani.
Hadithi ya mateso ya Yesu iliyomo katika hizo nyaraka za kale ni kuwa Yuda
aliwakhadaa Mayahudi kwa kuwaletea mtu mwingine badala ya Yesu. Huyu mtu
mwingine alikataa kata-kata mbele ya Hirodi (Mfalme wa Mayahudi) na Pilato
(Liwali wa Kirumi) hayo mashtaka kuwa yeye anadai Umasihi. Kwa mujibu wa
hadithi hii ilikuwa Hirodi, wala si Pilato (kama isemavyo Biblia) ndiye
aliyechukua maji akanawa mikono kuikosha na dhambi ya damu yake, kudhihirisha
kuwa yeye hakumwona na kosa. Tena Hirodi akamfungia ndani huyo
aliyedhaniwa kuwa ni Yesu usiku kucha; lakini asubuhi yake alishikwa na
Mayahudi wakamtesa na mwishoe wakamsalibu.
Hadithi hii ya kusalibiwa walau inatupa sura njema kuliko ile iliomo katika
Biblia inayomueleza Yesu kuwa aliyayatika kama asiye na imani ya kutosha, pale
alipokuwa msalabani. Kwani katika Injili ziliomo katika Biblia, yaani
zile walizozikubali wakuu wa Kanisa, yasimuliwa kuwa Yesu alilia: "Mungu
wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?" Kwa mtu wa hivi hivi,
mchache wa imani, aweza kusamehewa akifanya hivyo, lakini hayamuelekei hayo
mwenye kuongoza watu, seuze Nabii, seuze Mwana wa Mungu, kama
tunavyoambiwa. Tena Mwana Mungu wenyewe ambaye amekuja makusudi huku
duniani kwa kazi hiyo ya kutundikwa msalabani ili waokoke viumbe vyake.
Ikiwa aliyesalibiwa ni Yesu, na Yesu ni Mungu, hadithi hiyo haingii
akilini. Upton Sinclair anaandika katika kitabu chake A
Personal Jesus (Yesu Mtu):
Kitandawili kinacho watatanisha wasomaji wenye akili zao kama Upton Sinclair
kinatatuliwa na vile wale Wanasara wa kale wanavyoeleza kile kisa cha
kusalibiwa. Kwa maelezo yao Yesu anatakasika na tuhuma ya woga na ukosefu
wa imani ya rehema ya Mwenyezi Mung, kama alivyoonyesha yule mtu
aliyesalibiwa. Hali kadhaalika tunaweza kuelewa kwa nini wanafunzi wa
Yesu aliowateuwa mwenyewe walivyomkana na sote
tukaona wamefanya kitendo cha woga na
ukhaini. Wakati ule wa shida vipi
wafuasi wake wote wamkatae? Wangapi waliokhiari kufa kwa ajili ya
waja wa kawaida kama sisi tuliojaa dhambi, itakuwa wanafunzi aliowateuwa
mwenyewe Yesu kuwa ndio watakao eneza mafunzo yake wamtupilie mbali kama
tambara bovu mara baada ya kuingia matesoni? Na miongoni mwa watu hao awemo
Petro ambaye Yesu alimwita mwamba ambaye juu yake atajenga Kanisa lake?
Kudai kuwa yote hayo ni kutimiza bishara ziliomo katika Agano la Kale ni
kutumwagia mchanga wa macho. Lakini walivyoeleza wale Manasara wa mwanzo
yanaingia sana akilini. Ni kweli yule aliyekamatwa na kubandikwa msalabani
akayayatika kama mtu asiye na imani si Yesu, siye Bwana wao, siye mwongozi wao,
siye Mwalimu wao. Ni kweli hawamjui mtu yule. Yule mtu
waliyemsaliti, waliyemkataa, waliyemwacha ateseke na auliwe bila ya kunyanyua
kidole kumtetea, wala kutoa kauli kumsemea wala dua kumwombea, ni kweli
hawamjui.
Injili ya Barnaba ambayo Kanisa limeikataa inaeleza kuwa yule aliyesalibiwa ni
Yuda; na madhehebu ya Kikristo ya kale iitwayo Basilidoni ikiamini kuwa ni
Simoni Mkirene ndiye aliyesalibiwa, si Yesu. Kwa mujibu wa Injili tatu za
mwanzo, yaani Mathayo, Marko na Luka, ni huyo Simoni ndiye aliyebeba msalaba.
Ni Injili ya Yohana tu ndiyo inayotwambia kwamba ni Yesu mwenyewe aliyebeba
msalaba wake. Jambo hili lafaa kuzingatiwa na kutiwa maanani.
Wataalamu wengine, wanaotegemeza utafiti wao juu ya hizi hizi Injili nne
zilizokubaliwa na Kanisa na kutiwa katika Biblia, wana mawazo mengine juu ya
hichi kisa cha kusalibiwa. Mmoja wao
Mathayo 27.45-50
Hayo ni
maelezo ya Injili ya Mathayo. Lakini Schonfield anadai ya kuwa hiyo ilikuwa ni
hila tu kumwokoa Yesu asife msalabani. Alipewa hiyo dawa ili aonekane
kama aliyekufa. Kwa mujibu wa Injili Yesu alibakia hapo msalabani kwa
muda wa saa tatu tu, ilhali ilikuwa ni ada mtu kubaki ananing'inia msalabani
kwa siku kadhaa wa kadhaa yupo baina ya uhai na mauti akisononeka. Tena kwa
kufuata mpango maalumu uliopangwa, alitokea mfuasi wake Yesu, tajiri mmoja
aitwaye Yusufu wa Arimathaya akamwendea Liwali wa Kirumi, Pilato, akamwomba
ampe yeye maiti akamzike. Akapewa.
Mtaalamu wa ilimu ya binaadamu (Anthropology) Michael J. Harner wa Chuo
Kikuu cha California katika kuthibitisha hayo alisema kuwa ni kweli ilikuwa
ikifanywa mvinyo kutokana na mmea wa tunguje mwitu ambayo ikitumiwa kumfanya
mtu kuzimia na kuonekana kama kafa ili kumwokoa na kifo cha kusononeka
msalabani. Huyo Yusufu tena alimpeleka huyo aliyeonekana kama maiti kwenye
pango alilolichonga kama chumba kwenye bustani yake liwe ati ni kaburi. Na jiwe
kubwa likawekwa mlangoni. Hakuzikwa katika kaburi liliochimbwa chini kwenye
ardhi na kufukiwa kwa udongo.