Kuzozana sio makusudio ya kuandika Risala hii. Makusudio ya
hakika ni kutaka kuwapa mwangaza Wakristo na Waislamu ambao katika sehemu
nyingi za ulimwengu inawapasa waishi kama ni wananchi wamoja na jirani.
Inatumainiwa pindi wakinawirika, na kila mmoja akaifahamu vyema misingi ya
imani ya mwenziwe, wote watakuja thamini ule msingi mmoja unaowaunga wote
kwenye Imani ya asli, nayo ndiyo Dini ya Ulimwengu mzima inayofunza kila
mwanaadamu ajisalimu kwa ukamilifu wake kwenye mapenzi ya Mwenyezi Mungu Mmoja
wa kweli, kwani hapo ndipo unapotegemea mwendo mwema wa binaadamu.
Kwa bahati mbaya Yesu Kristo (Isa Masihi) hakutuachia mafunzo yake kwa
maandishi ya kutegemewa kama alivyofanya Nabii Muhammad. Katika Qur'ani utakuta
mafunzo ya Kiislamu yaliyo safi kabisa, yasiyo na chembe ya ila au
wasiwasi. Hatukutii katika Injili mfano wa hayo. Hizo ziitwazo Injili
zaweza kulinganishwa na Hadithi za Mtume, bali khasa ni kama Sira Nabawiya,
yaani Hadithi za Maisha ya Mtume, ni kama vitabu vya Maulidi.
Inakubaliwa na Wakristo wenyewe kuwa katika maneno na vitendo vya Yesu, kama
inavyoelezwa katika Biblia, yamo mengi ambayo si ya kweli, na si ya kutegemewa,
kama yalivyokuwepo katika Hadithi za Mtume kabla ya kuchujwa na kun'golewa
hadithi na khabari zilizo dhaifu na kuthibitishwa zenye nguvu, Sahihi.
Haikataliki kuwa kwa sababu za kimadhehebu na sababu nyenginezo za mfarakano
hadithi nyingi ziliwahi kubuniwa na kusingiziwa kuwa ni za Mtume, hali Mtume
hakukhusika nazo kabisa.
Wachunguzi wa haki lazima wakiri kuwa katika kuzichambua na kuzikusanya Hadithi
za Mtume Muhammad kulikuwepo mwendo bora zaidi wa kitaalamu kuliko uliokuwapo
zilipoteuliwa hizi Injili ziliomo katika Biblia. Hao wanazuoni wakubwa -
Maimamu - waliotumia maisha yao yote katika kukusanya Hadithi, yaani semi na
vitendo vya Mtume Muhammad, walifanya kila juhudi waliyokuwa nayo (yaani
Ijtihad) wakitumia vipimo vya ilimu (scientific methodology)
kuhakikisha ukweli na umadhubuti wa kila kauli na kila kitendo cha Mtume.
Kila Hadithi waisikiayo waliichungua na kuipekua kwa nani imepokelewa, na huyo
naye kaipokea kwa nani, na tena kwa nani, mpaka kwa aliyeipata kwa mwenyewe
Mtume. Kila kiungo katika mnyororo wa wapokeaji uwe madhubuti sawa sawa
kwa kila njia. Maisha ya kila mmoja ya wapokeaji yalilazimu kusomwa na
yadurusiwe, na yachunguzwe kwa uangalifu kamili, mpaka uthibiti bila ya shaka
yo yote uaminifu wake wa kupokea na kusimulia khabari kwa kweli bila ya
kuzidisha wala kupunguza. Hiyo peke yake ni ilimu iliyotungiwa vitabu kwa
vitabu. Tena huchunguzwa lugha - jee, ni ndio lugha namna hiyo na mbinu
zake kama ilivyokuwa ikitumika Makka na Madina katika zama za Mtume? Ni
kweli ndiyo namna ya lugha alivyokuwa mwenyewe Mtume akijuulikana
kutumia? Pia huchunguzwa kuwa hayo maneno anayoambiwa Mtume kayasema, au
vitendo kavitenda, havigongani kwa namna yo yote na mafunzo yaliomo katika
Qur'ani? Kwani Qur'ani ndicho kipimo madhubuti kabisa. Hayagongani na
hakika ya mambo yanavyojuulikana kikweli bila ya khitilafu? Kwa njia hizi na
nyenginezo ndio hao Maimamu waliokusanya Hadithi za Mtume wakizichuja, na zenye
shaka wakizitenga kando, na kuziita Dhaifu, au Ziliobuniwa. Ziliopasi ndio
wakaziita Sahihi na nzuri.
Lakini juu ya jitahada kuu waliyoifanya hao wanazuoni wa Hadithi bado juhudi
yao ni juhudi ya kibinaadamu, na huenda ikakosea. Kwa bahati njema ipo Qur'ani,
amabayo ukweli wake haujapata kutolewa kombo na rafiki wala adui. Kila
mtu ameangusha shingo yake mbele ya ukweli wa Qur'ani kuwa hapana mfano wake
kitabu cho chote duniani ambacho kimebakia karne nenda karne rudi bila ya
mabadiliko yo yote au machafuzi yo yote. Hapana neno moja lililoongezwa,
wala neno moja lililopunguzwa. Hii Qur'ani iliopo sasa kwa lugha ya
Kiarabu (sio tafsiri za maana yake katika lugha mbali mbali) ndio ile ile
Qur'ani ambayo Mtume Muhammad aliyowakariria wafwasi wake miaka 1400 iliyopita,
na wao wakaihifadhi kwa moyo na kuiandika, na khalafu yake miaka michache tu
baada ya kufa kwa Mtume ikakusanywa pamoja kuwa ni Msahafu kama huu tuuonavyo
sisi hii leo. Huu basi ndio msingi usiolegalega, uliojengewa juu yake
mafunzo ya Imani ya Kiislamu. Hichi ndicho kipimo cha kupimia usahihi wa
Hadithi au Khabari yo yote ya Mtume, na ndio mwamba ambao juu yake limejengwa
jengo la Uislamu.
Katika sahifa zifwatazo itaonekana kuwa nimependelea mno kunukulu maneno
kutokana na vitabu mbali mbali. Huu ndio mtindo wangu ninapoandika juu ya
jambo muhimu, na khasa jambo lilio muhimu kupita kiasi kama hili la dini.
Sipendelei kuwa miongoni mwa wale "ambao wanaojadili mambo yaliyomkhusu
Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, wala uwongofu wala kitabu chenye kutoa
mwangaza", kama isemavyo Qur'ani.
Nilipokuwa nikiidurusu Biblia katika upweke wa kizuizini katika magereza ya
Tanzania nalijaribu kuyatafuta mafunzo ya kweli ya Yesu na Manabii wa Wana wa
Israili waliomtangulia. Miaka kumi na miezi mitano ya kizuizi ikawa ni miaka
kumi na miezi mitano ya mafunzo ya kweli kweli ya Biblia. Kwa juhudi na
taabu nikawa nabandua, bandu bandu, kidogo kidogo, magamba yaliyoifunika hiyo
niliyokuwa nina yakini nayo - Lulu in'gaayo iliyozikwa chini ya magamba.
Nikaigundua.
Basi sasa nawaomba ndugu zangu wa Kiislamu ambao kuujua kwao Ukristo ni juu juu
tu, na rafiki zangu wa Kikristo ambao takriban hawajui lo lote la kweli katika
Uislamu (na kwa hakika hata Ukristo wa kweli) waje nami, na katika sahifa hizi
zifwatazo tuutafute Ukweli. Tutauona, kwani Ukweli ni Nyumba iliyojengwa
juu ya Mwamba, na mvua itaanguka, na pepo zitavuma, lakini Nyumba
haitaanguka. Huko katika Yerusalemu Takatifu walipopaa wote wawili,
Muhammad na Yesu, kwa uvuto wa kiroho mpaka wakafikilia Utukufu wake Mola
Mlezi, kuna ishara ya dhaahiri inayotoa mwanga wa kuenea kote kote, ishara ya
Ukweli unaomuamrisha Mwislamu na Mkristo kumsujudia Mwenyezi Mungu yule yule
ambaye anaabudiwa kwa hamu na unyenyekevu sawasawa katika Msikiti ulio juu ya
Mwamba na katika Kanisa la Kaburi Takatifu. Ukweli huu unatuamrisha
tuache mila za binaadamu na tufuate amri za Mwenyezi Mungu. Ukweli huu
unatuamrisha tuache mtindo wa kuigawa Dini katika vikundi vikundi vya
madhehebu na tuushikilie Umoja wa Mungu (Tawhid) unaotuunga sote
pamoja. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani:
Tusitangetange ovyo katika vichochoro vya makosa na hali Njia safi Iliyonyooka
iko wazi machoni mwetu. Tujifunze ukweli kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu.
Tufahamiane na tukubaliane kuwa kila mmoja wetu kwa dhati ya nafsi yake
atafanya juhudi kuutafuta Ukweli, kwani Ukweli ndio utaotupa uzima.
Ali Muhsin Al Barwani