13- BIBLIA NA QUR'ANI
Yesu aliungama kuwa hakuyasema yote aliyoyataka kuyasema,
lakini huyo atakaye kuja yeye ndiye ataitimiza kazi. Mafunzo ya Muhammad
juu ya dhambi, juu ya kuhisabiwa haki, na juu ya hukumu yamo katika Qur'ani,
kitabu cha namna ya pekee ulimwenguni kwa usafi wake, kutokuwa na migongano yo
yote na kuwa hakiwezekani kuigwa mfano wake. Tangu kilipoteremka kwa Mtume
s.a.w. miaka 1400 iliyokwisha pita hakikubadilika hata kwa neno moja, na kwa
uwezo wa Mwenyezi Mungu, hakitobadilika mpaka Siku ya Kiyama. Sir William
Muir, mtoa kombo maarufu wa Uislamu, akiandika katika kitabu chake The life
of Mohamet (Maisha ya Muhammad) amesema:
"Labda hapana kitabu cho chote kinginecho duniani ambacho kwa
muda wa karne kumi na mbili kilichobaki na maandiko yake safi namna hii."
Tangu Sir William alipoandika hayo karne mbili nyenginezo zimekwisha biringita
na Qur'ani imebaki vile vile safi kama siku alipoipokea Mtume Muhammad s.a.w. kwa Mwenyezi
Mungu.
Kwa mintaraf ya Biblia lakini hatuwezi kuona msimamo mmoja, kwa
sababu kwanza kuwa Biblia si kitabu kimoja, bali ni mkusanyiko wa vitabu vingi
vilivyoandikwa na watu mbali mbali, katika zama mbali mbali. Makanisa
yanazozana hata kuwa vitabu vipi vikubaliwe kuwa ndio Biblia, na vipi sivyo,
vipi vimeandikwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu na vipi sivyo. Mara nyingi
inatokea katika kitabu kimojawapo hicho hicho kinapingana wenyewe kwa wenyewe, kama tulivyokwisha ona mfano wake katika hadithi ya
kutanasari Paulo iliomo katika kitabu cha Matendo ya Mitume.
Hugh Schonfield akiandika katika kitabu chake Those Incredible Christians,
anasema:
"Ndani ya jalada za Biblia twaweza kukuta udanganyifu, mageuzo,
na uzushi wa kukusudia kama unavyokuta katika
vitabu vyenginevyo nje. Wataalamu wanajua vyema haya; lakini
inapokuwa andiko la ndani ya Biblia si la huyo anayedai kuwa ndiye muandishi
kila juhudi inafanywa lisitumiwe neno udanganyifu. Hali ni hiyo hiyo kwa maneno anayoambiwa Yesu
kayasema na yanajuulikana kuwa si kweli. Tunaviita vitabu kama hivyo kuwa ni
vya kikundi cha mawazo ya Kipaulo au Kipetro, na maneno yaliyogeuzwa au
yaliyozuliwa tunayaita kuwa ni "ya pili"(Secondary). Kama hatukutumia
hila itaonekana kuwa Roho Mtakatifu alishirikiana katika udanganyifu.
Ni jambo
lililoandikwa na kujuulikana kuwa mpaka ilipokatwa shauri mwishoe vitabu gani
vihisabiwe kuwa ni Maandiko Matakatifu baadhi ya vitabu viliomo katika Biblia
vilipingwa. Ilitolewa hoja na Wakristo wa kweli kwamba vitabu fulani havikuwa
hakika vimeandikwa na hao wanaodaiwa kuwa ni waandishi wake. Pengine jina la
mwenye kufanya udanganyifu lilidhukuriwa. Paulo anataja wakati wa uhai wake
zilikuwepo barua za uwongo zikienezwa kwa jina lake yeye. Liliokuwa
laonekana lafaa ni maslaha ya Kanisa tu. Mawazo yasiyokhusiana hata
chembe na ukweli yakitumika kuelekeza maandishi na fikra kinyume na hakika ya
walivyosema wenyewe watu kadhaa wa kadhaa wenye maana. Mtindo kama huu
ulikuwa ni jambo la kawaida katika kazi ya uenezi hapo kale, na yafaa tuelewe
kuwa ilikuwa ni kawaida vile vile miongoni mwa Wakristo wa zamani. Hivi
ndivyo mchezo wa kueneza na kupendekeza ulivyokuwa ukichezwa. Na kwa wale wasio
na dhamiri wala haya, wanaoamini kuwa muhimu ni lengo sio njia uitumiayo,
mchezo huo unachezwa hata hivi sasa."
Asli ya vitabu vya Biblia haipo na haijuulikani, kwa hivyo ndio tunapata nakala
nyingi sana. Inakubaliwa kuwa vitabu hivyo kama vilivyo sasa vimeandikwa na
waandishi wanaadamu. Juu ya hivyo waweza kugundua baadhi ya maneno ambayo
yametokana na Mungu asli yake. Lakini jinsi maandishi yalivyochanganyika, na
yalivyoongezwa na kupunguzwa hata inakaribia kuwa ni muhali kulitambua lipi la
Mungu na lipi la mwanaadamu ambaye alikuwa anawania madhehebu yake fulani au
wazo lake maalumu. Qur'ani ni kinyume cha hayo. Kila neno lake ni la
mwenyewe Mwenyezi Mungu. Yote ni maneno yake Mola Mlezi kama alivyofunuliwa kwa
ufunuo (Wahyi) Mtume s.a.w., neno kwa neno, na yeye Mtume akiyatamka na
wenye kuhifadhi kwa moyo wakihifadhi, na waandishi waaminifu wakiandika. Mkristo,
Dr. John B. Taylor, Mwalimu wa Masomo ya Kiislamu katika Selly Oak Colleges, Birmingham anaandika
katika kitabu chake Thinking About Islam:
"Tumekwisha hakikisha kwamba Waislamu hawasemi kuwa Muhammad
kaandika Qur'ani, lakini kuwa kaipokea na akaisoma. Kama alivyokuwa
Muhammad mwenyewe alivyoishughulikia matini ya Qur'ani, vile vile Waislamu wa
baada yake walichukua kila taabu kuuhifadhi kwa ukamilifu usafi wa vipande
vyote vya Qur'ani. Miaka miwili tu baada ya kufa Muhammad, na kuwa baadhi
ya wale waliokuwa wameihifadhi Qur'ani kwa moyo, wakifa vitani, vipande mbali
mbali vilikusanywa...
Miaka michache baadaye, katika enzi ya Uthman, Khalifa wa tatu
kuwatawala Waislamu baada ya kifo cha Muhammad, matini ilipitiwa tena
kusahihishwa. Twaweza kusema vipi wale Waislamu wa kwanza
walivyoshughulikia na kuwa na hamu kwa kuwa hata khitilafu za matamshi ya pande
mbali mbali za ulimwengu wa Kiislamu hazikuruhusiwa katika kuisoma Qur'ani; na
kwa hivyo matini rasmi ikahakikishwa inayofuata lafdhi ya Makka, na nakala
nyenginezo zote ziliteketezwa kwa amri ya Khalifa. Kwa hivyo tunaweza
kuwa na imani ya yakini kuwa hii Quran tuliyo nayo hii leo kama
inavyomkinika kibinaadamu ndio ile ile iliyohakikishwa mnamo miaka michache tu
baada ya kufa Mtume."
Hayo ni maoni ya mtoa kombo wa Kikristo. Qur'ani ni neno la Mwenyezi Mungu
lisio na toa. Hiyo ndiyo maana ya maneno ya Yesu aliponena: "Hatanena
kwa shauri lake mwenyewe lakini yote atayoyasikia atanena."
