Ikiwa
Yesu hakutuachia uongozi wa kutosha katika mambo ya dhambi na kuhisabiwa haki,
na hukumu, basi ni kwa sababu madhubuti, ambazo yeye mwenyewe amezitaja.
(Tazama Injili ya Yohana 16.5-14 kama tulivyokwisha nukulu.) Tena,
lakini alimuelezea hivi huyo ambaye atakuja: "Naye akiisha kuja,
huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na
hukumu...atawaongoza awatie kwenye kweli yote."Yesu alisema kuwa huyo
ajaye ataufundisha ulimwengu khabari ya hukumu. Yeye mwenyewe hakuweza
kuweka mfano wa uhakimu kwa kuwa maisha yake alikuwa mkimbizi anakimbia
kuhukumiwa. Historia haitwambii kuwa alikuwapo mwongozi ye yote wa dini baada
ya Masihi aliyeshika uhakimu isipokuwa Muhammad. Muhammad amepitia kila
namna ya maisha. Alikuwa mchunga kondoo, mwananchi wa kawaida, mume,
baba, mpigania uhuru, mtawala, mtunga sharia, mwana siasa, hakimu, walii na
Mtume wa Mwenyezi Mungu, tena ndiye wa mwisho wa wote. Amebeba ujumbe
uliotoka moja kwa moja kutokana na Mwenyezi Mungu. Muhammad akihukumu,
lakini hukumu yake ilikuwa imelainishwa na rehema, kama inavyoelekea kwa mtu
anayehukumu kwa nguvu na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Maisha yake ya kila
namna ni ruwaza ya kutosha kwetu sisi sote, kuiga kama tulivyojaaliwa katika
maisha yetu. Yeye alifunza kwa maneno na vitendo. Hakuwa mtu aliyejitenga
na ulimwengu akasema maneno matamu lakini maneno yenyewe hayatendeki.
Alikuwa mtu wa vitendo, mtu wa kidunia, na wakati huo huo kwa upande wa kiroho
alikuwa na khulka bora kabisa hata mwenyewe Aliyemuumba hakuweza ila kumsifu
kwa kumwambia:
(Qur'ani) Al Qalam 68.4
Mara
moja Bibi Aisha, mkewe, aliulizwa (na nani amjuaye mtu kuliko mkewe?) nini
tabia ya Mtume, alijibu kwa mkato: "Khulka yake ni Qur'ani!"
Hapana sifa kubwa kuliko hii. Mtu huyu aliishi ile dini yake. Maadui zake
wanakubali kuwa hapana kitabu kinachokubaliana na mtu, kuliko Qur'ani
inavyokubaliana na maisha ya Mtume Muhammad s.a.w. Amri
zilizotokana na Mungu wake, ndio maisha yake. Si ajabu basi Yesu kusema
kuwa Muhammad atauhakikisha ulimwengu kwa khabari ya haki.
Huyo mtu aliyebashiriwa na Yesu kuwa atakuja ni kuwa atakuwa Mtume wa ulimwengu
mzima, kwani zama za Mitume ya kabila fulani na kondoo fulani waliopotea
umekwisha. Huyo ajaye ni Mtume wa watu wote, wa kabila zote, na wa mambo
yote. Huyo ni wa kuuhakikisha ulimwengu, na wa kufunua kweli yote. Hali
kadhaalika Mwenyezi Mungu anamwambia Muhammad:
(Qur'ani) Saba 34.28
(Qur'ani) Al Anbiyaa 21.107
Yesu
alisema ana mengi ya kusema, lakini watu wake hawakuwa na uwezo wa kuyachukua
wakati ule. Wataongozwa kwenye kweli yote na huyo ajaye, Roho wa Kweli,
ambaye itakuwa fakhari yake kuutangazia ulimwengu baada ya kutimiza ujumbe
wake: "Hapana Nabii baada yangu." Ni yeye huyo ambaye
ameitwa na Mwenyezi Mungu: "Khaatamun Nabiyyiina, Mwisho wa Manabii,
Muhuri wa Manabii. Waraka ukisha tiwa muhuri hapana ruhusa kuongeza kitu juu
yake. Chupa ikitiwa Khaatam, (Seal), ndio imezibwa, huwezi kuongeza kitu
tena. Ukiongeza unaghishi, unafanya khadaa. Qur'ani na mwenendo wa Mtume
Muhammad upo kutuongoza sisi katika mambo yetu yote mpaka Siku ya Mwisho.
Hakujuidai ila lilio haki yake. Alikataa katakata kufanywa mungu wa
bandia. Daima akisema: "Mimi ni mwanaadamu tu."
Mwenyezi Mungu alimuamuru aseme:
(Qur'ani) Al Kahf 18.110
Kazi
yake, kama ilivyokuwa kazi ya Yesu, ilikuwa kufanya apendavyo Yeye Mwenyezi
Mungu aliyemtuma. Muhammad hakudai kuwa yeye ni muanzishi wa dini
mpya. Bali aliendeleza na akatimiza dini aliyokuja nayo Ibrahim, Musa,
Isa (Yesu), na Manaabii wote waliotoka kwa Mwenyezi Mungu. Wote hao
wakitenda mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Na huo ndio Uislamu. Neno
"Islam" lina maana ya Usalama, na maana ya kujisalimu kwa Mwenyezi
Mungu, utende lile limpendezalo Mwenyezi Mungu, yaani kutenda mapenzi ya Mungu,
kama asemavyo Yesu. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani kuwa hapana
kaumu ila walipelekewa Nabii. Lakini Mtume Muhammad kwa kuwa ni wa
ulimwengu mzima, kama alivyobashiri Yesu, na kwa kuwa ni wa mwisho, basi ni mwenye
kuthibitisha ukweli wa ujumbe wote uliotoka kwa Mwenyezi Mungu, na mwenye
kuondoa makosa yaliyopachikwa na wanaadamu katika dini ya Mwenyezi Mungu.
Kwa kuwa wakati umefika wa kukusanya ulimwengu mzima uwe na Imani moja, na
kuelekea kumoja, ndio akaja Mtume Muhammad, kama ni Mtume wa Mwisho wa
ulimwengu mzima. Myahudi mwenye kumkubali kumfuata Mtume Muhammad ndio
basi ametimiza maamrisho ya Musa na Ibrahim na Manabii wake wote
anaowaamini. Mkristo anayemkubali Muhammad na akamfuata ndio ametimiza
Ukristo wake, na amekubali kweli mafunzo yaliyomo katika Taurati na Injili na
khasa ameyafuata maamrisho ya Yesu. Qur'ani inasema:
(Qur'ani) Al Baqara 2.62
Dunia
wakati wa Yesu ilikuwa bado haijawa tayari kuweza kupokea fikra ya dini ya
kukusanya ulimwengu mzima, dini isiyokuwa ya kabila fulani, au rangi
fulani. Sisi leo tunaona jambo hilo ni la kawaida tu, lakini zama zile
kila kikabila kilikuwa na lake. Ndio maana hata Manabii wa kweli waliotokana na
Waisraili walimwita Mwenyezi Mungu kwa jina la Mungu wa Israili. Na kweli kila
taifa lilikuwa na mungu wake, na ibada zake. Ni khatua kubwa hiyo aliyochukua
Yesu kuwaambia wanafunzi wake wende kwa kabila kumi na mbili za Israili. Yesu
hakutangaza dini yake ila kwa "kondoo waliopotea wa nyumba ya Israili."
Ndio maana akasema kuwa yeye hawaombei walimwengu, bali wale tu aliopewa na
Mungu, Wana wa Israili. Yesu aliogopa kuwa mafunzo yake yakipelekwa kwa
mataifa mengine wasio Waisraili yatavurugwa mafunzo hayo kama nguruwe
waliotupiwa lulu wangeziponda hizo lulu na kuwararua watu kwa kutojua thamani ya
lulu. Lakini Yesu alisema katika Karamu ya Mwisho kuwambia wanafunzi wake kuwa
wakati ukifika atakuja atayetimiza kweli yote, atafunza ulimwengu mzima juu ya
dhambi, haki na hukumu.
Na kweli tumeiona. Historia iwazi kuwa hapana mtu aliyefunza udugu wa walimwengu
kama alivyofunza Mtume Muhammad. Hapana mtu aliyevunja ubaguzi kama
alivyouvunja Muhammad. Hapana mtu aliyepiga marfuku khitilafu za rangi na
kabila na taifa kama Muhammad. Ndio maana tangu mwanzo wake waliomfuata
wakawa pamoja naye kufa kupona, hawakuwa watu wa kabila lake tu la Kikureshi,
au taifa lake tu la Kiarabu, bali walikuwamo pia Wazungu, Waafrika na
Waasia. Ni yeye Muhammad ndiye aliyesema: "Majivuno kwa
uungwana wa kikale nayakanyaga chini ya miguu yangu. Mwaarabu si bora
kuliko asiyekuwa Mwaarabu, wala asiyekuwa Mwaarabu si bora kuliko
Mwaarabu. Mwekundu si bora kuliko mweusi wala mweusi si bora kuliko
mwekundu, ila kwa uchamngu. Watu wote ni sawa kama meno ya kitana.
Wote ni wana wa Adam, na Adam ametokana na mchanga."
Hayo ni machache katika maneno yake aliyoyasema juu ya ubaguzi wa rangi na
taifa, jambo ambalo mpaka hii leo linawahangaisha wasiomfuata Muhammad.
Tena Mtume Muhammad hakusema tu bali alitenda.
Katika Uislamu hapana waajibu wenye fadhila kama sala za jamaa. Na katika hizo,
nyadhifa mbili ndio tukufu: Imamu na Muadhini. Mtume mwenyewe
alikuwa ndiye Imamu, na akamteua Bilal kuwa Muadhini wa kwanza katika
Uislamu. Bilal alikuwa Muafrika mweusi, aliyekombolewa na Abubakar kutoka
utumwani. Mtume hakuona junaha kumwoza Zaid binti wa shangazi lake yeye Mtume,
na ilhali huyo Zaid alikuwa kwanza ni mtumwa wa Kiarabu, wake yeye mwenyewe
Muhammad, na akamuachia huru. Wala hakuona kiroja kumteua Usama, chotara wa
mama wa Kiafrika mweusi, awe Jemadari wa jeshi kuu la Kiislamu kupambana na
Warumi, na chini yake walikuwa Masahaba wakubwa wakubwa wa Kikureshi.
Yeye huyo kijana chotara, Usama, alikuwa umri wake miaka 18.
Safari moja walikuja baadhi ya Waarabu wakamtaka Mtume awapatie mume wa Kiarabu
wa ukoo mzuri kumwoza binti yao. Mtume akawaambia: Mwamuonaje
Bilal? Wale jamaa wakenda zao. Siku ya pili wakaja tena, na Mtume
akawauliza suala lile lile la jana; wakenda zao. Siku ya tatu wakaja
tena, na Mtume akawauliza suala lile lile la jana na juzi, lakini akaongeza:
"Mwamuonaje mwanamume katika watu wa Peponi?" Wakamwoza.
Watu wote wakajua kuwa Muhammad habagui baina ya watu ila kwa uchamngu wao
tu. Masahaba walimtukuza Bilal kama alivyokuwa akitukuzwa na mwenyewe
Mtume.
Mwenyezi Mungu wa watu wote, dini ya watu wote, Udugu wa watu wote - hayo
yasingeweza kufunzwa ila na mtu kama yule, na kukubaliwa na watu kama wale, kwa
zama kama zile. Si ajabu basi vile Uislamu ulivyotanda kama kwamba ni
moto wa nyikani. Thomas Carlyle, muandishi na mtu mwenye mawazo madhubuti,
maarufu wa Kiingereza alisema katika khutba yake kumsifu Mtume Muhammad
aliyoitoa London yapata miaka mia mbili iliyopita:
Si imani tu ndio iliyofanya muujiza, lakini namna ya imani yenyewe, imani
ya udugu wa binaadamu wote, na dini ya ulimwengu mzima. Kutoka Kaskazini
mpaka Kusini mwa dunia, kutoka Mashariki mpaka Magharibi, wote wakaifuata imani
moja. Wote wakaelekea Makka. Wote wakawa ndugu, wote wakachanganya damu
na tamaduni. Wakawa Umma mmoja, Taifa moja, Taifa la Kiislamu, wafuasi wa
Muhammad na Isa na Musa na Ibrahim, na kila Nabii aliyetumwa na Mwenyezi Mungu.
Wote walimuamini Mungu Mmoja, asiyezaa wala kuzaliwa, wala hana mfano wake.
Wote waliwaamini Manabii walioletwa na Mwenyezi Mungu, na wakaamini ukweli wa
asli ya dini zote zilizitoka mbinguni.