2- BIBLIA

Hili neno Biblia ni neno la Kigiriki, na maana yake ni "vitabu". Basi Biblia ni mkusanyiko wa vitabu vingi ambavyo ndio vinafanya msingi wa imani ya Kikristo.  Inakubaliwa kuwa vitabu hivi vimeandikwa na watu wengi mbali mbali, wajuulikanao na wasiojuulikana.  Lakini hao waandishi wanaaminiwa kuwa walipata ufunuo kutokana na Mwenyezi Mungu, na wameandika walivyoandika chini ya uangalizi na uwongozi wa Mwenyezi Mungu;  kwa hivyo Biblia inaambiwa kuwa ni Neno la Mungu.  Biblia ya Wakatoliki, lakini, kidogo inakhitalifiana na ya Waprotestani.  Ya Wakatoliki ina vitabu 73, na ya Waprotestani ina vitabu 66.
Kwa jumla Biblia imegawika sehemu mbili kubwa, Agano la Kale na Agano Jipya.  Agano la Kale ni vitabu vyote vilivyoandikwa kabla ya kutokea Yesu Kristo.  Vitabu hivi vinaeleza tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, na Adamu na Hawa, historia (taarikh) ya wanaadamu na khasa ya Wana wa Israili, sharia alizopewa Musa na Mwenyezi Mungu, vita vya Mayahudi na jirani zao, mafunzo ya manabii kadhaa wa kadhaa katika Bani Israili yaliyotokana na Mwenyezi Mungu. Isipokuwa kwa baadhi ya vitabu ambavyo hawavikubali hili liitwalo Agano la Kale, kwa jumla, ndio liliokuwa Biblia na mpaka hivi sasa ndio Biblia ya Mayahudi. Mayahudi hawaikubali kabisa sehemu ya pili iitwayo Agano Jipya inayokubaliwa na Wakristo.
  Agano Jipya ni ile sehemu ya Biblia iliyoandikwa baada ya Yesu Kristo.  Sehemu hiyo inakusanya Injili nne. Hizi ziitwazo Injili ziliomo katika Biblia ni vitabu vinavyosimulia maisha ya Yesu Kristo na mafunzo yake. Katika Agano Jipya kipo kitabu
kinachoitwa Matendo ya Mitume, kinachoeleza khabari za wanafunzi wake Yesu aliowatuma kwenda tangaza dini. Pia kipo kitabu kinacho itwa "Ufunuo" chenye kueleza mambo ya ajabu ajabu ambayo yasimuliwa kuwa Yohana alifunuliwa akayaona. Hali kadhaalika zimo barua kadhaa wa kadhaa, nyingi zao ni za Paulo, walizopelekewa watu fulani fulani kuwafunza mambo ya dini. Hizi barua za Paulo, Myahudi aliyetanasari, zinategemewa sana na Wakristo, na ndio msingi wa imani na itikadi zao, hata wengi wapo wanaosema kuwa huu Ukristo tuuonao sasa kwa hakika uliasisiwa na Paulo.
Vitabu viliomo katika Agano la Kale kama vilivyo hivi sasa labda viliandikwa baada ya kurejea Mayahudi kutoka utumwani Babilionia, yaani baada ya mwaka 536 kabla ya Kristo.  Na vitabu vya Agano Jipya vilikusanywa na kukubaliwa na wakuu wa Kanisa katika karne ya nne baada ya Kristo (kiasi 367 A.D.) Injili nne ziliomo katika Agano Jipya, yaani ya Mathayo, ya Marko, ya Luka na ya Yohana, ndizo zilizoteuliwa na kukubaliwa na wakuu wa Kanisa kutokana na Injili nyingi sana ambazo zimekataliwa. Neno "Injili" ni neno la Kigiriki, na maana yake ni "Khabari Njema", kwa kuwa Yesu alikuwa akisema kuwa analeta Khabari Njema, yaani Bishara. Vitabu ambavyo vingeweza kuwa ni sehemu ya Biblia, na kwa hakika vikawa vinakubaliwa kwanza na pengine mpaka sasa na baadhi ya madhehebu za Kikristo, vinaitwa "Apokrifa", yaani "vilivyofichwa".
Sisi tunaposema Biblia tunakusudia vitabu vinavyotambuliwa na madhehebu kuu za Kikristo kuwa ndivyo Neno la Mungu tu.